2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ ﴿١٥﴾
15. Wanaotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُوا فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٦﴾
16. Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu ispokuwa moto. Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.
أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِ وَيَتْلُوهُ شَاهِدٌ مِّنْهُ وَمِن قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ مِنَ الْأَحْزَابِ فَالنَّارُ مَوْعِدُهُ فَلَا تَكُ فِي مِرْيَةٍ مِّنْهُ إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٧﴾
17. Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake na anaifuata na shahidi atokaye kwake na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?) Hao wanamwamini yeye. Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake. Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako. Lakini watu wengi hawaamini.
WANAOTAKA MAPAMBO YA DUNIA
YA 15-17
MAANA
Wanotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.
Atakayepanda atavuna, mwenye kufanya biashara vizuri, atapata faida, mwenye kusoma kwa bidii, atafaulu, mwenye kujenga viwanda, kuchimba visima vya mafuta na madini bila shaka hazina yake itajaa mali na kila mwenye kulifanyia bidii jambo lolote, atapata matunda yake, awe mumin au kafiri.
Riziki huja ikiwa ni natija ya kazi; haipunguzwi na ulafi wala kuzidishwa na imani. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.” Hata hivyo ufisadi nao una athari zake; kama tulivyoieleza katika Juz. 6 (5:64).
Neema za maisha ya Akhera zinashikiliwa na kazi ya hapa duniani; sawa na mapambo katika maisha haya. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu na hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:
أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾
“Je, mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu haja wajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?” Juz.4 (3:142).
Amesema tena Mwenyezi Mnungu:
وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾
“Na anayeitaka Akhera na akaihangaikia inavyotakikana, naye ni mumin, basi hao mahangaiko yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa” (17:19)
Mwenye kuhangaikia riziki yake nzuri ya halali, basi atakuwa amehangaikia dunia na Akhera.
Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu isipokuwa moto.
Hao ni ishara ya wale waliozama katika dunia wakawa hawajishughulishi na lolote isipokuwa dunia tu. Hawatakuwa na malipo yoyote isipokuwa adhabu.
Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.
Humo ni duniani. Maana ni kuwa matendo yao si kitu mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama watu watanufaika nayo, maadamu lengo halikuwa la heri ya kiutu. Kwa ufupi, mwenye kutafuta heri yoyote itamfikisha pale anapopataka; mwenye akili hujichagulia njia ya uokovu bila ya kudanganyika na chochote.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumtaja yule anayejishighulisha na dunia tu, amemtaja anayetenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kumlin- gania yeye tu, akiwa na dalili itokayo kwa Mola wake. Ufafanuzi ni kama ufuatao:
Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake.
Makusudio ya aliye na dalili wazi ni Muhammad(s.a.w.w)
na dalili wazi ni Qur’ani.
Na anaifuata na shahidi atokaye kwake.
Tabari, Razi, Abu Hayan Alaandalusi na wengineo katika wafasiri, wamesema kuwa kuna kutofautiana kuhusu shahidi huyu anayemshuhudia Muhammad na utume wake. Wengine wamesema ni Jibril, wengine ni ulimi wa Muhammad na wengine wakasema ni Ali bin Abutwalib.
Waliosema kuwa ni Ali wametoa dalili kwa Hadith aliyoipokea Bukhari katika Sahih yake, inayosema: “Alisema Mtume(s.a.w.w)
kumwambia Ali:Wewe ni katika mimi na mimi ni katika wewe.”
Na Umar akasema: Mtume(s.a.w.w)
alikufa akiwa yuko radhi naye (Ali).
Na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?).
Tawrat ilimbashiria Muhammad na utume wake kabla ya kushuhudiwa na Qur’ani. Tawrat ni Kitab cha Mwenyezi Mungu alichomteremshia Musa na ni kiongozi kinachofuatwa katika mambo ya kidini na rehema kwa anayekitumia kabla ya kupotolewa.
Hao wanamwamini yeye.
Yaani yeye Muhammad(s.a.w.w)
na hao ni wale wanaofuata dalili za haki na ubainifu wake; kama vile Qur’ani na Kitabu cha Musa jinsi kilivyoteremshwa. Na hao, wanaoashiriwa, hawakutajwa katika Qur’ani, isipokuwa wametajwa kwa sifa zao.
Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake.
Makusudio ya makundi ni yaliyompiga vita Mtume(s.a.w.
w
)
. Mwenye Tafsir Al-manar na sheikh Al-maraghi, wamesema: “Amesema Muqatil: Hao ni ni ukoo wa Ummayya, ukoo wa Mughira bin Abdallah Al-makhzumi na jamii ya Twalha bin Abdallah na mfano wao katika Mayahudi na manaswara”
Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako.
Dhamir katika usiwe na shaka naye na hakika yeye, inaweza kuwa ni ya Muhammad au ya Qur’ani na msemo wa usiwe, unaelekezwa kwa kila aliyesikia ujumbe wa Muhammad. Maana ni kuwa haitakikani kwa mwenye akili kutia shaka kuwa Muhammad ni mtume na kwamba Qur’ani ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, baada ya kuweko na dalili zilizowazi juu ya hilo.
Ikiwa mtu anaweza kutia shaka kuwa Tawrat na Injil zimetoa bishara ya utume wa Muhammad, je anaweza kutia shaka kwamba Muhammad amewapatia watu njia za maisha na kwamba yeye ameleta ambayo hakuwahi kuwaletea nabii au kiongozi yeyote.
Lakini watu wengi hawaamini
haki, kwa sababu hiyo ni adui wa dhulma yao na ufisadi wao katika nchi au kwa kuwa wao hawatilii umuhimu dini ya haki au batil madamu maisha yao hayategemei dini. Sisi tutaachana nao hawa na yale waliyojichagulia; na wao wawaache wengine na yale waliyojichagulia na wasiingilie dini wasiyoijua isipokuwa jina tu.
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أُولَـٰئِكَ يُعْرَضُونَ عَلَىٰ رَبِّهِمْ وَيَقُولُ الْأَشْهَادُ هَـٰؤُلَاءِ الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَىٰ رَبِّهِمْ أَلَا لَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ ﴿١٨﴾
18. Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo. Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao. Na watasema mashahidi: Hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.
الَّذِينَ يَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ ﴿١٩﴾
19. Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.
أُولَـٰئِكَ لَمْ يَكُونُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كَانَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ يُضَاعَفُ لَهُمُ الْعَذَابُ مَا كَانُوا يَسْتَطِيعُونَ السَّمْعَ وَمَا كَانُوا يُبْصِرُونَ ﴿٢٠﴾
20. Hao hawataweza kuponyoka katika nchi na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu maradufu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٢١﴾
21. Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao. Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.
لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْأَخْسَرُونَ ﴿٢٢﴾
22. Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَخْبَتُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٣﴾
23. Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kunyenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.
مَثَلُ الْفَرِيقَيْنِ كَالْأَعْمَىٰ وَالْأَصَمِّ وَالْبَصِيرِ وَالسَّمِيعِ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٢٤﴾
24. Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia. Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Je, hamfikiri?
WATAHUDHURISHWA MBELE YA MOLA WAO
Aya 18-24
MAANA
Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo.
Ikiwa kumzulia uongo kiumbe ni kauli mbaya, itakuwaje kwa muumba? Kumzulia uongo Mwenyezi Mungu kuko aina nyingi; kama vile kumfanyia washirika, kuhalalisha na kuharamisha bila ya hoja kutoka Qur’ani au Hadith, wizi na unyang’anyi kwa kisingizio cha demokrasia n.k.
Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao.
Hao ni ishara ya wale wazushi, na kwamba wao kesho watasimama kuhisabiwa; kaulizao na vitendo vyao vitahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na watasema mashahidi: hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hahitajii mashahidi, kwa sababu yeye anajua na ni muweza wa kila kitu; anahukumu kwa ujuzi wake na uadilifu wake na kutekeleza kwa neno ‘kuwa.’
Ama ushuhuda wa Malaika na mitume na ushuhuda wa ndimi za waongo waliopotea na mikono yao na miguu yao, lengo lake ni kuzidisha majuto na kwamba wawe na yakini kuwa hawana hoja wala udhuru watakaoukimbilia; hakuna kuepuka laana ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.
Aya hii ni ubainifu na tafsiri ya madhalimu ambao Mwenyezi Mungu amewalaani; kwamba wao wanawazuia watu na tawhid na imani ya ufufuo. Vile vile wanawadanganya kwa shirki na kuikataa siku ya mwisho.
Hao hawataweza kuponyoka katika nchi.
Vipi waweze kufanya hivyo na hali lau Mwenyezi Mungu angelitaka asingeliacha yeyote kwenye ardhi
Na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu.
Hata masanamu waliyokuwa wakiyafanya mungu na kuyaabudu na pia watawa na wakuu wao waliowafanya waungu hawawezi kufaa kitu.
Watazidishiwa adhabu maradufu.
Hili ni jawabu la swali la kukadiriwa; kama kwamba muulizaji ameuliza wale waliozulia Mwenyezi Mungu uwongo wana hukumu gani? Basi Mwenyezi Mungu akajibu, watazidishiwa adhabu mara mbili.
Kuwa maradufu adhabu hapa ni fumbo la ukali wa adhabu. Wengine wamesema maana yake ni kuwa kila kosa lina adhabu yake: Watadhibiwa kwa uzushi na watadhibiwa kwa kuzuia njia na kupinga ufufuo.
Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.
Hii ni sababu ya kufanyiwa adhabu maradufu kwamba Mwenyezi Mungu akiwapa adhabu hii kwa vile walikuwa hawawezi kuisikiliza haki wala kuichunguza, kwa sababu ya kuzama kwao kwenye kufru na inadi.
Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao.
Mwenye hasara zaidi katia watu ni yule aliyejihasiri mwenyewe na adhabu isiyokwisha wala kupunguzwa.
Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.
Ambayo ni kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika na watetezi, kuhalalisha na kuharamisha kwa uwongo na uzushi.
Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa wao wamezitia hasara nafsi zao, amesisitiza kuwa hasara hii itatokea tu, haina kizuizi wala kuikimbia.
Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kun- yenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.
Baada ya Mwenyezi Mungu(s.w.t) kuwataja makafiri, amefuatilia kwa kuwataja wauminii na malipo yao; kama ilivyo desturi ya Qur’ani – kutaja vitu na vinyume vyake.
Neno kunyenyekea hapa limetumika kutokana na neno ‘khibt’ lenye maana ya kunyenyekea na utulivu. Tabrasi anasema: Asili ya neno khibt ni usawa wenye kuenea yaani ardhi iliyo sambamba.
Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia.
Makundi mawili ni makafiri na waumini. Moja halinufaiki na hisia zake, ambapo kipofu hanufaiki na macho yake na kiziwi hanufaiki na masikio yake; na jingine linanufaika na hisia hizo mbili. Imama Ali (a.s.) anasema: “Mwenye kuzingatia huwa na busara na mwenye busara hufahamu na mwenye kufahamu huwa na elimu.” Ni hivyo hivyo mwenye kusikia.
Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa?
Kwa sifa na hali.Je, hamfikiri?
Hiyo tofauti?
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ إِنِّي لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٢٥﴾
25. Hakika tulimpeleka Nuh kwa watu wake. Hakika: mimi kwenu ni muonyaji abainishaye.
أَن لَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ أَلِيمٍ ﴿٢٦﴾
26. Ya kwamba msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iumizayo.
UJUMBE WA NUH
Aya 25-26
MAANA
Aya mbili hizi zinaelezea kwa ufupi kwamba watu wa Nuh walikuwa wakiabudu masanamu. Inasemekana wao ndio wa kwanza kufanya shirki na kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika.
Ndipo Mwenyezi Mungu akawapelekea mtume awape bishara na maonyo.
Basi Nabii Nuh
akatekeleza risala yake kwa maneno haya mafupi: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake wala msimshirikishe na kitu.
Akadhihirisha hurumma yake kwao kwa kuwahofia kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama wataendelea na shirk. Huu ndio msingi wa kwanza wa risala ya mitume wote.
فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا نَرَاكَ إِلَّا بَشَرًا مِّثْلَنَا وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ وَمَا نَرَىٰ لَكُمْ عَلَيْنَا مِن فَضْلٍ بَلْ نَظُنُّكُمْ كَاذِبِينَ ﴿٢٧﴾
27. Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake: Hatukuoni ila ni mtu sawa na sisi. Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu; bali tunawaona kuwa mu waongo.
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَآتَانِي رَحْمَةً مِّنْ عِندِهِ فَعُمِّيَتْ عَلَيْكُمْ أَنُلْزِمُكُمُوهَا وَأَنتُمْ لَهَا كَارِهُونَ ﴿٢٨﴾
28. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake, ikafichikana kwenu, Je, tuwalazimishe na hali nyinyi mnaichukia?
وَيَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مَالًا إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّهُم مُّلَاقُو رَبِّهِمْ وَلَـٰكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ ﴿٢٩﴾
29. Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakika wao watakutana na Mola wao. Lakini mimi nawaona nyinyi ni watu wajinga.
وَيَا قَوْمِ مَن يَنصُرُنِي مِنَ اللَّـهِ إِن طَرَدتُّهُمْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٣٠﴾
30. Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza? Basi je, hamfikiri?
وَلَا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ إِنِّي مَلَكٌ وَلَا أَقُولُ لِلَّذِينَ تَزْدَرِي أَعْيُنُكُمْ لَن يُؤْتِيَهُمُ اللَّـهُ خَيْرًا اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا فِي أَنفُسِهِمْ إِنِّي إِذًا لَّمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٣١﴾
31. Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa mimi ni Malaika. Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao. Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.
NUH NA WATU WAKE
Aya 27-31
MAANA
Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake, hatukuoni ilia ni mtu sawa na sisi.
Nuh alipowalingania watu wake kwenye tawhid walikataa mwito wake, kabla ya kuchunguza uhakika wake. Wakaleta sababu mbili: Ya kwanza, kwamba vipi watamfuata na hali yeye ni mmoja wao? Wao waliangalia msemaji, hawakuangalia yanayosemwa; wakapima haki na watu badala ya kuwapima watu na haki.
Unaweza kuuliza
: Hili halihusiki na watu wa Nuh tu, tumewaona watu wengi wamewatukuza wageni kuliko wenyeji; na kuna usemi mashuhuri usemao: ‘msichana wa nyumbani ana sura mbaya,’ sasa kuna ubaya gani?
Jibu
: ni kweli kwamba hayo hayahusiki na watu wa Nuh tu na wala Aya haipingi hilo; isipokuwa inawashutumu kwa jambo hilo na hii haiwabakishi watu wengine, wote wanashutumiwa.
Sababu ya pili waliyoisema wapinzaini ni:
Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu.
Yaani walimwambia Nuh na waumini kuwa vipi tuwafuate na nyinyi hamtuzidi na chochote kihali na kimali; sawa na walivyosema washirikina wa kiqurayash kumwambia Muhammad(s.a.w.w)
:
لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ ﴿١٢﴾
“Mbona hakuteremshiwa hazina” (11:12).
Na wakasema tena:
لَوْلَا نُزِّلَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ ﴿٣١﴾
“Mbona hii Qur’ani haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili.” (43:31)
Bali tunawaona kuwa mu waongo
, kwa vile nyinyi ni mafukara mlio maskini. Haya ndiyo matamshi ya wenye utajiri kung’ang’nia mali tu, lakini maneno ya kheri na matendo mema kwao ni maneno matupu yasiyokuwa na faida.
Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake.
Hili ni jawabu la kauli yao, kuwa vipi tukuamini na wewe ni kama sisi. Maana ya jawabu ni kuwa nifanye nini ikiwa Mwenyezi Mungu amenichagua kutekeleza ujumbe wake na amenihusu mimi na rehema yake? Tena akanipa ubainifu kutoka kwake wa risla hii.
Je, nikatae; nimwambie Mwenyezi Mungu sitaki kutumwa na wewe wala sitafikisha ujumbe wako kwa waja wako. Je, yote hayo niyakatae?
Kwa vile nyinyi hamna akili ndioikafichikana kwenu
risala na mmeshindwa kuifahamu.
Je, tuwalazimishe?
Yaani tuwalazimishe na ujumbe wangu,na hali nyinyi mnaichukia?
Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili
la kuwaonya.
Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa sababu mwenye kuzungumzia jina la Mwenyezi Mungu, akiwa ni mkweli katika maneno yake, basi hataki malipo kutoka kwa mwenginewe. Na wanaotafuta riziki kwa jina la dini ndio waombao watu mali na sadaka; na ndio wengi siku hizi.
Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakiaka wao watakutana na Mola wao.
Kwa nini niwafukuze? Kwani ufukara ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu anajua imani yao kwa vile wao wanamwelekea yeye.
Lakini mimi nawaona ni watu wajinga
. Na watu ni maadui wa wasichokijua.
Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza?
Je, mnaweza nyinyi au wengine kunikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Basi je, hamfikiri?
Vipi atafikiri ambaye haogopi mwisho?
Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa ni Malaika.
Kauli hii ni ya Nuh
ikiwa ni ufafanuzi na tafsiri ya kauli yake: “Hakika mimi kwenu ni muonyaji abainishaye” Si lazima muonyaji amiliki mali, ili fukara aonekane mwongo; wala si lazima ajue ghaibu, ili aonekane mwongo yule asiyejua ghaibu; wala pia si lazima awe Malaika ili asiyekuwa Malaika ambiwe wewe si lolote isipokuwa ni mtu.
Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao.
Kuna mazoweya ya wenye mali kuona utajiri ndio kipimo cha haki na heri; bali hata wajinga na wapumbavu huona hivyo. Ama mbele ya Mwenyezi Mungu na watu wa Mwenyezi Mungu kipimo ni takua na amali njema na Nuh
anapima kwa vipimo vya Mwenyezi Mungu. Vipi awaambie waumini kuwa hamtapata heri ya Mwenyezi Mungu; kama walivyoambiwa na mataghut? Ila ikiwa yeye naye ni taghuti kama wao.
Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.
Kama wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, wakavikataa vitabu vyake na mitume yake.