TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 12139
Pakua: 3306


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12139 / Pakua: 3306
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا مُفْتَرُونَ ﴿٥٠﴾

50. Na kwa A’ad (tulimpeleka) ndugu yao Hud, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye tu. Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni wazushi.

يَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى الَّذِي فَطَرَنِي أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٥١﴾

51. Enyi watu wangu! Siwaombi ujira juu ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa yule aliyeniumba, basi hamtumii akili?

وَيَا قَوْمِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ وَلَا تَتَوَلَّوْا مُجْرِمِينَ ﴿٥٢﴾

52. Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake, atawaletea mbingu zenye mvua tele na atawazidishia nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke kuwa waovu.

قَالُوا يَا هُودُ مَا جِئْتَنَا بِبَيِّنَةٍ وَمَا نَحْنُ بِتَارِكِي آلِهَتِنَا عَن قَوْلِكَ وَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٥٣﴾

53. Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi, wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kauli yako na wala sisi hatukuamini wewe.

إِن نَّقُولُ إِلَّا اعْتَرَاكَ بَعْضُ آلِهَتِنَا بِسُوءٍ قَالَ إِنِّي أُشْهِدُ اللَّـهَ وَاشْهَدُوا أَنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٥٤﴾

54. Hatuna la kusema ila baadhi ya miungu yetu imekutia balaa. Akasema: Hakika mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu na nyinyi shuhudieni kwamba niko mbali na hao mnaowashirikisha.

مِن دُونِهِ فَكِيدُونِي جَمِيعًا ثُمَّ لَا تُنظِرُونِ ﴿٥٥﴾

55. Mkamwacha Yeye. Basi nyote nifanyieni vitimbi tena msinipe muda.

إِنِّي تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّـهِ رَبِّي وَرَبِّكُم مَّا مِن دَابَّةٍ إِلَّا هُوَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهَا إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٦﴾

56. Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu Mola wangu na Mola wenu. Hakuna mnyama yeyote isipokuwa Yeye amemshika utosi wake. Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka.

NA KWA A’AD NDUGU YAO HUD

Aya 50-56

MAANA

Na kwa A’ad (tulimpeleka) ndugu yao Hud, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye tu. Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni wazushi mnaozusha ibada ya masanamu.

Hud anatokana na kabila la A’ad kinasaba na kinchi, ndio maana Mwenyezi Mungu akamsifu kuwa ni ndugu yao. Ujumbe wake huu ni ujumbe wa mitume wote.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika kisa cha Nuh katika Aya 26 ya sura hii, na kisa cha Hud katika Juz.8 (7:65).Na tumetaja ilipo kaburi yake na kwamba yeye ndiye wa kwanza kuzungumza kiarabu; naye ndiye baba wa ya Yaman na Mudhar. Rudia huko.

Enyi watu wangu! Siwaombi ujira juu ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa yule aliyeniumba, basi hamtumii akili?

Anayefanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hataki riziki kutoka kwa mwengine na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayedhuru na kunufaisha. Tafsiri hii imepita katika Aya 29 ya sura hii.

Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.

Tofauti kati ya kuomba maghufira na kutubia ni: Kuomba maghufira ni kutaka msamaha wa yaliyopita bila ya kuangalia yajayo. Na kutubia ni kuomba msamaha kwa yaliyopita na kuahidi kutofanya tena

Atawaletea mbingu zenye mvua tele na atawazidishi nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke kuwa waovu.

Inaonyesha kuwa wao walikuwa ni watu wa kilimo na mifugo ndio maanaMwenyezi Mungu akawavutia kwenye mvua nyingi; kama ambavyo kauli yake: ‘Atawazidishia nguvu juuu ya nguvu zenu,’ inafahamisha kuwa walikuwa ni watu wenye nguvu za Kiundani na dhahiri (kimaana na kimaada) Hilo linaonyeshwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ ﴿٦﴾ إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ ﴿٧﴾ الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ ﴿٨﴾

” Je, hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya Aa’d Wairam wenye maguzo marefu. Ambao mfano wao haukuumbwa katika miji” (89:6-8).

Unaweza kuuliza kuwa : Mwenyezi Mungu ameunganisha baina ya imani na kuteremshwa mvua. Utasemaji wewe ulipofasiri Juz. 9 (8:2) ukasema kuwa dini haioteshi ngano na kwamba Mwenyezi Mungu hupitisha mambo kwa desturi ya kimaumbile?

Jibu : Ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu anapitisha mambo kulingana na desturi ya kimaumbile, hilo halina shaka. Lakini hilo halizuwii kupatikana muujiza, au kuacha desturi kwa hekima fulani. Ukomo wa desturi zote na maumbile unaishilia kwenye matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Yeye pekee ndiye msababishaji wa sababu zote. Na matakwa haya matakatifu yanaweza kufungamana na kupatikana kitu moja kwa moja bila ya kupitia sababu yoyote iliyozoeleka; kama Tufani ya Nuh n.k. Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka kutoidhihirisha miujiza hii inayohalifu kawaida, isipokuwa kwa kupatikana mtume, ili kuthibitisha utume wake, kuitikiwa mwito wake au kuwaadhibu maadui zake.

Kwa maneno mengine ni kuwa kupita mambo kwa desturi ni kitu kingine na muujiza ambao unategemea matakwa ya Mwenyezi Mungu ni kitu kingine.

Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi.

Huu ni uongo na uzushi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatumi mjumbe ila humsheheni na hoja za kutosha juu ya utume wake. Watu wa Hud walikataa mwito wake na hoja zake kwa vile zinapingana na hawaa zao; kama ilivyokuwa kwa kaumu nyingine za mitume. Mwenyezi Mungu anasema:

كُلَّمَا جَاءَهُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنفُسُهُمْ فَرِيقًا كَذَّبُوا وَفَرِيقًا يَقْتُلُونَ ﴿٧٠﴾

“Kila alipowafikia Mtume kwa yale zisiyoyapenda nafsi zao kundi moja wakalikadhibisha na kundi jengine wakaliua.”Juz.6 (5:70)

Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kauli yako.

Mwenye Kitabu Al-Mughni anasema kuwa herufi a’n hapa ni ya sababu; yaani hatuwezi kuacha miungu kwa sababu tu ya kusema kwako iacheni, bila kutuonyesha dalili wala ubainifu

Na wala sisi hatukuamini wewe.

Huu ni ufafanuzi wa kauli yao ya kutoacha miungu yao. Amesema kweli yule aliyesema: Mtu ndiye aliyeumba Miungu wala sio miungu iliyoumba mtu.

Hatuna la kusema ila baadhi ya miungu yetu imekutia balaa.

Kauli yao hii inaonyesha upeo wa ujinga wao na imani yao iliyo kombo ya vigano. Mawe yaliyotulia wanayaamini kuwa yanamdhuru anayesema yasiabudiwe! Mtu akifikia kiwango hiki cha ujinga basi ni wa kuachana naye tu. Ndio maana Mwenyezi Mungu akawasifu kwa uziwi na upofu.

Akasema: Hakika mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu na nyinyi shuhudieni kwamba niko mbali na hao mnaowashirikisha. Mkamwacha Yeye basi nyote nifanyieni vitimbi tena msinipe muda.

Walipomwambia kuwa miungu yao imemdhuru, aliwapinga na kuwapa ushindani kuwa wajikusanye wao na waungu wao na wajaribu kila wawezavyo wamdhuru na yeye yuko tayari. Hii maana yake ni kwamba wao wako kwenye mghafala na ni wenye kudanganyika.

Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu Mola wangu na Mola wenu.

Hii ndio sababu ya kushinda kwao kumdhuru na kuwabeza wao na masanamu yao.

Hakuna mnyama yeyote isipokuwa Yeye amemshika utosi wake.

Yaani hakuna kiumbe chochote ila Mwenyezi Mungu hukiendesha vile atakavyo. Hakuna chochote kinachoweza kujikinga au kujinufahisha hicho chenyewe tu, sikwambii kunufaisha au kudhuru kingine.

Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka.

Yeye ndiye anayenusuru na kutweza na anatoa thawabu na kuadhibu kwa msingi wa njia hii iliyonyooka, njia ya haki na uadilifu.

Unaweza kuuliza : Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyeshika hatamu ya mja na utosi wake, kwa maana ya kumpeleka vile atakavyo; na ikiwa Yeye Mwenyezi Mungu yuko juu ya njia iliyonyooka, hapo patakuwa na mambo mawili:

1. Kuwa mja ni mwenye kuendeshwa hana hiyari; kwa sababu anakokotwa.

2. Kuwa kila mtu yuko juu ya njia iliyonyooka katika vitendo vyake vyote na kauli zake; kwa vile anamfuata; Mungu sawa na mnyama aliyefungwa hatamu anavyomfuata yule mwenye kushika hatamu akiwa kwenye njia nzuri na mnyama naye atakuwa kwenye njia nzuri?

Jibu: Makusudio ya kushika utosi sio kuwa mja hana hiyari katika cho- chote; isipokuwa ni fumbo la uweza wa Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu na kwamba Yeye pekee ndiye mwenye kunufaisha. Hiyo ni kuwajibu washirikina ambao wameyapa masanamu uwezo wa kudhuru na kunufaisha.

فَإِن تَوَلَّوْا فَقَدْ أَبْلَغْتُكُم مَّا أُرْسِلْتُ بِهِ إِلَيْكُمْ وَيَسْتَخْلِفُ رَبِّي قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّونَهُ شَيْئًا إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ ﴿٥٧﴾

57. Wakirudi nyuma, basi mimi nimekwishawafikishia niliyotumwa kwenu. Na Mola wangu atawaleta watu wengine badala ya nyinyi. Wala hamumdhuru kitu. Hakika Mola wangu ni mwenye kuhifadhi kila kitu.

وَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا هُودًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَنَجَّيْنَاهُم مِّنْ عَذَابٍ غَلِيظٍ ﴿٥٨﴾

58. Ilipofika amri yetu tulimwokoa Hud na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu na tukawaokoa na adhabu ngumu.

وَتِلْكَ عَادٌ جَحَدُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَعَصَوْا رُسُلَهُ وَاتَّبَعُوا أَمْرَ كُلِّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ ﴿٥٩﴾

59. Na hao ndio Aa’d, walikanusha Ishara za Mola wao na wakawaasi mitume wake na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inadi.

وَأُتْبِعُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ أَلَا إِنَّ عَادًا كَفَرُوا رَبَّهُمْ أَلَا بُعْدًا لِّعَادٍ قَوْمِ هُودٍ ﴿٦٠﴾

60. Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na siku ya kiyama. Ehee! Hakika Aa’d walimkufuru Mola wao. Ehee! Wamepotelea mbali watu wa Hud.

WAKIRUDI NYUMA

Aya 57-60

MAANA

Wakirudi nyuma, basi mimi nimekwishawafikishia niliyotumwa kwenu bila ya kuchoka wala kuzembea.

Na Mola wangu atawaleta watu wengine badala ya nyinyi baada ya kuwaletea adhabu ya dunia kabla ya Akhera.

Wala hamumdhuru kitu kwa kuacha kwenu imani

Hakika Mola wangu ni mwenye kuhifadhi kila kitu anachunga kila kitu na kukiangalia kwa ujuzi wake na hekima yake. Anasema ibn Arabi katika Futahatul Makkiyya: “Kama ambavyo Mola wako ni mwenye kuhifadhi kila kitu, basi naye ni mwenye kuhifadhika na kila kitu.” Anaashiria kauli ya aliyesema: “Kila kitu kina Aya”

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Hud na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu na tukawaokoa na adhabu ngumu.

Makusudio ya amri yetu ni adhabu yetu, kuokoka kwa kwanza ni kutokana na adhabu ya dunia na kuokoka kwa pili ni kutokana na adhabu ya Akhera.

Imesemekana kuwa kuokoka kwa kwanza ni kubainisha kuokoka na adhabu bila ya kuangalia aina yake na kuokoka kwa pili ni kubainisha aina ya adhabu iliyowashukia watu wa Hud ambayo ilikuwa ni ngumu. Maana zote mbili zinakubali. Yametangulia maelezo ya kuokoka Hud na waliokuwa pamoja naye katika Juz. 8 (7:72).

Na hao ndio Aa’d, walikanusha Ishara za Mola wao na wakawaasi mitume yake na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inadi.

Baada ya kuelza kwa ufupi kisa cha Aa’d aliashiria Mwenyezi Mungu, sababu ya kuangamia kwao kwamba ni kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu na Ishara zake, kuasi kwao mitume, kuacha kuitetea haki, kuikinga batili na kufuata kwao upotevu na utaghuti.

Mwenyezi Mungu amesema: ‘na wakawaasi mitume’ na wala hakusema na wakamuasi mtume. Kwa sabau mwenye kumwasi mtume mmoja basi ni kama amewaasi wote kwa kuangalia kuwa ujumbe ni mmoja tu, nao ni mwito wa imani ya umoja wa Mungu na ufufuo

Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na siku ya kiyama.

Yaani walifanya yanayowajibisha laana duniani na Akhera. Maana ya laana ni kuwa mbali na kheri. Ndio maana Mwenyezi Mungu akasema:

Ehee! Hakika Aa’d walimkufuru Mola wao. Ehee! Wamepotelea mbali watu wa Hud.

Limekaririka neno ‘Ehe!’ kwa kutilia mkazo na kusisitiza kukanya.

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ ﴿٦١﴾

61. Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye. Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na ardhi na akaifanya iwe koloni lenu. Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake. Hakika Mola wangu yuko karibu mwenye kuitikia maombi.

قَالُوا يَا صَالِحُ قَدْ كُنتَ فِينَا مَرْجُوًّا قَبْلَ هَـٰذَا أَتَنْهَانَا أَن نَّعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ ﴿٦٢﴾

62. Wakasema: Ewe Swaleh! Ulikuwa ukitarajiwa kwetu kabla ya haya. Hivi unatukataza kuabudu waliyokuwa wakiyaabudu mababa zetu? Na sisi tuna shaka na wasiwasi kwa haya unayotuitia.

قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَآتَانِي مِنْهُ رَحْمَةً فَمَن يَنصُرُنِي مِنَ اللَّـهِ إِنْ عَصَيْتُهُ فَمَا تَزِيدُونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ ﴿٦٣﴾

63. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na akanipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu kama nikimwasi? Basi hapo hamtanizidishia isipokuwa hasara tu.

SWALEH

Aya 61-63

MAANA

Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye.

Imetangulia Aya hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (7:73).

Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na ardhi.

Hakuna kitu chochte chenye uhai, kiwe binadamu, mnyama au mmea, ila kitakuwa kimetokana na Ardhi moja kwa moja au kupitia kingine.

Na akaifanya iwe koloni lenu.

Qur’ani Tukufu imelitumia neno hili ukoloni (istimari) kwa maana ya kuamirisha na kuendeleza. Na hii ndiyo maana yake nzuri. Ama hivi leo neno hili linatumika katika dhulma, unyang’anyi na kuwakandamiza wanyonge; na hiyo ndiyo maana mbaya sana. Angalia kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu ameitengeneza ardhi na binadamu akaiharibu’ katika Juz. 8 (7:56)

Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.

Hud aliwaambia watu namna hii hii katika Aya 52 ya sura hii. Huko tumeeleza tofauti kati ya kuomba maghufira na kutubia.

Hakika Mola wangu yuko karibu mwenye kuitikia maombi.

Yuko karibu na mwenye kumfanyia ikhlas na mwenye kumwitikia anayeitikia mwito wake.

Wakasema: Ewe Swaleh! Ulikuwa ukitarajiwa kwetu kabla ya haya ya kutukataza kuabudu masanamu. Lakini hivi sasa, baada ya kutukataza hatukuamini tena.

Hivi unatukataza kuabudu waliyokuwa wakiyaabudu mababa zetu?

Vizazi na vizazi wameyaabudu na wakayapelekea madhabihu na hakuna yeyote aliyewahi kuwakataza, je yeye watamkubalia kweli?

Na sisi tuna shaka na wasiwasi kwa haya unayotuitia.

Hii ndiyo mantiki ya kijinga kila mahali na kila wakati. Kila kitu ni desturi yetu na kufuata wazee wetu tu.

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na akanipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu kama nikimwasi?

Walimwambia Swaleh kuwa wanashaka naye, naye akawaambia, hebu niambieni nifanyeje ikiwa nina uhakika kwamba Mwenyezi Mungu amenituma kwenu na akaniamrisha niwalinganie kwenye Tawhid; tena akanipa dalili za kutosha juu ya ujumbe huu, je, nimuasi kwa ajili ya kuwaridhisha nyinyi? Na ni nani atakayenikinga na adhabu yake kama nikimwasi?

Basi hapo hamtanizidishia isipokuwa hasara tu.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa maana yake ni, nikiwatii mtanifanya nipate hasara. Na wengine wakasema kuwa ni, upinzani wenu haunizidishii chochote isipokuwa ni hasara yenu.

Tuonavyo sisi ni kuwa Swaleh alitaka kuwaambia watu wake lau atawakubalia, basi watamwamini, lakini yeye hatapata radhi ya Mwenyezi Mungu.

وَيَا قَوْمِ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ ﴿٦٤﴾

64. Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu, ni ishara kwenu, basi mwacheni ale katia ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikawaangamiza adhabu iliyo karibu.

فَعَقَرُوهَا فَقَالَ تَمَتَّعُوا فِي دَارِكُمْ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ ذَٰلِكَ وَعْدٌ غَيْرُ مَكْذُوبٍ ﴿٦٥﴾

65. Wakamchinja. Basi (Swaleh) akasema: Stareheni katika mji wenu kwa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokadhibishwa.

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا صَالِحًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَمِنْ خِزْيِ يَوْمِئِذٍ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ ﴿٦٦﴾

66. Ilipofika amri yetu tulimwokoa Swaleh na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu kutokana na hizaya ya siku hiyo. Hakika Mola wako ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.

وَأَخَذَ الَّذِينَ ظَلَمُوا الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٦٧﴾

67. Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.

كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا فِيهَا أَلَا إِنَّ ثَمُودَ كَفَرُوا رَبَّهُمْ أَلَا بُعْدًا لِّثَمُودَ ﴿٦٨﴾

68. Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! Hakika Thamud walimkufuru Mola wao. Ehee! Thamud wamepotelea mbali.

NGAMIA WA MWENYEZI MUNGU

Aya 64-68

MAANA

Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu, ni ishara kwenu, basi mwacheni ale katia ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikawaangamiza adhabu iliyo karibu.

Imekwishatangulia tafsiri yake katika Juz.8 (7:73).

Wakamchinja. Basi Swaleh akasema: Stareheni katika mji wenu kwa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokadhibishwa.

Swaleh(a.s) aliwaamrisha waachane naye ngamia, lakini wakamchinja, basi akawaonya kushukiwa na ahabu kwa muda wa siku tatu.

Ibn Abbas anasema kuwa Mungu aliwapa muda huu kuwahimiza imani na kutubia, lakini wao waling’ang’ania ukafiri wao, kwa sababu hawakumwamini Swaleh na ahadi yake.

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Swaleh na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu kutokana na hizaya ya siku hiyo. Hakika Mola wako ni mwenye nguvu mwenye kushinda.

Baada ya siku tatu, ilishuka adhabu, wakaokoka wauminii na wakaangamia makafiri, baada ya kuwasimamia hoja. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kuzama katika upotevu na ufisadi.

Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.

Hapa amesema ukulele ukawaangamiza na katika Juz.8 (7:78) amesema na mtetemeko ukawaangamiza. Maana ni kuwa ukelele ulileta mtetemeko na hofu katika nyoyo zao.

Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! Hakika Thamud walimkufuru Mola wao. Ehee! Thamud wamepotelea mbali.

Yani jinsi walivyoondoka haraka ni kama kwamba hawakukaa majumbani mwao, na wala hawakuzifaidi mali zao na watoto wao.

Hawakuicheka dunia bali imewacheka wao. Mwenye akili ni yule anayepata somo kutokana na mwengine.

وَلَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا سَلَامًا قَالَ سَلَامٌ فَمَا لَبِثَ أَن جَاءَ بِعِجْلٍ حَنِيذٍ ﴿٦٩﴾

69. Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim na bishara, wakasema: Salaam! Naye akasema: Salaam! Hakukaa ila akaleta ndama aliyeokwa.

فَلَمَّا رَأَىٰ أَيْدِيَهُمْ لَا تَصِلُ إِلَيْهِ نَكِرَهُمْ وَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً قَالُوا لَا تَخَفْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمِ لُوطٍ ﴿٧٠﴾

70. Alipoona mikono yao hamfikii, aliwatilia shaka na akawahofia. Wakasem: usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut.

وَامْرَأَتُهُ قَائِمَةٌ فَضَحِكَتْ فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ ﴿٧١﴾

71. Na mkewe kasimama wima akacheka. Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.

قَالَتْ يَا وَيْلَتَىٰ أَأَلِدُ وَأَنَا عَجُوزٌ وَهَـٰذَا بَعْلِي شَيْخًا إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عَجِيبٌ ﴿٧٢﴾

72. Akasema: Miye! Hivi nitazaa na hali mimi ni kikongwe na huyu mume wangu ni mzee? Hakika hili ni jambo la ajabu!

قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ ﴿٧٣﴾

73. Wakasema: Unastajabu amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake iko juu yenu enyi watu wa nyumba hii Hakika yeye ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.

MALAIKA WANAMBASHIRIA IBRAHIM

Aya 69-73

MAANA

Na wajumbe wetu walimjia ibrahim na bishara, wakasema: Salaam! Naye akasema: Salaam!

Wajumbe walikuwa ni Mlaika waliomjia Ibrahim(a.s) kwa sura za kibinadamu, ili wampe habari njema ya kumzaa Ish-haq (a.s). Walianza kwa maakuzi, naye akawarudishia mfano wake au zaidi. Mwenyezi Mungu ameashiria ugeni huu pale aliposema:

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ ﴿٢٤﴾

Je, imekufikia hadithi ya wageni waheshimiwa wa Ibrahim?” (51:24)

Hakukaa ila akaleta ndama aliyeokwa.

Ibrahim(a.s) alikuwa maarufu kwa ukarimu na kuwapenda wageni. Kwa hiyo aliharakisha kutayarisha ndama aliyechomwa kwa moto wa mbali, kwa kuangalia hali ya wageni. Ndama alikuwa amenona, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ ﴿٢٦﴾

“Mara akaenda kwa watu wake akaleta ndama aliyenona” (51:26)

Alipoona mikono yao hamfikii, aliwatilia shaka na akawahofia.

Hawakuweza kula kwa sababu wao si watu. Kwahiyo Ibrahim akawahofia kwa sababu yeye aliwachukulia ni watu kumbe sivyo; na hajui wanataka nini. Mtu yeyote, awe Maasum (aliyehifadhiwa na dhambi) au la, akijiwa na jambao la ghafla asilolijua mwisho wake, lazima ahofie.

Malaika walipomuona hali yakeWakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut, wala hatuna ubaya na wewe wala kaumu yako. Mahali pengine hofu imeelezwa:

Akasema:

إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿٥٢﴾

“Hakika sisi tunawaogopa.” (15:52).

Na mkewe kasimama wima akacheka.

Kusimama ni kusikiliza mazungumzo yanayoendelea baina ya mumewe na Malaika. Ama kicheko, Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye. Kila mazungumzo kwa wanawake ni bashasha. Wafasiri wamegawanyika kuhusu hilo.

Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.

Yaani tukampa habari njema ya kumzaa Is-haq na Is-haq atamzaa Ya’qub. Hiyo inafahamisha kuwa mtoto wa mtoto ni mtoto.

Akasema: Miye! Hivi nitazaa na hali mimi ni kikongwe na huyu mume wangu ni mzee? Hakika hili ni jambo la ajabu!

Alistaajabu kwa vile si desturi mwanamke aliye katika umri wake kuweza kuzaa au mwanamume aliye katika umri wa mumewe kuweza kuzaa. Katika Kitabu cha kikiristo, Kutoka, imeelezwa kuwa Ibrahim wakati huo alikuwa na umri wa Miaka mia na mkewe, Sarah alikuwa na miaka tisini. Sisi hatukikubali Kitabu hicho. Tunalolifahamu ni kuwa wote wawili walikuwa wazee sana. Ama idadi ya miaka yao anayeijua ni Mungu.

Wakasema: Unastajabu amri ya Mwenyezi Mungu?

Vipi isiwezekane na yeye amri yake ni kukiambia kitu kuwa kikawa.

Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake iko juu yenu enyi watu wa nyumba hii.

Na amewahusu na neema nyingi. Na hii ni mojawapo. Kuna ajabu zaidi ya kuufanya moto uwe baridi na salama kwa Ibrahim?

Hakika yeye ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.

Ni mwenye kusifiwa kwa sababu ana sifa njema ni mwenye kutukuzwa kwa sabubu ana ukarimu. Kwa hiyo siajabu kumpa anayemuomba na asiyemuomba na mwenye kutazamia na asiyetazamia.