5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
فَلَمَّا ذَهَبَ عَنْ إِبْرَاهِيمَ الرَّوْعُ وَجَاءَتْهُ الْبُشْرَىٰ يُجَادِلُنَا فِي قَوْمِ لُوطٍ ﴿٧٤﴾
74. Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.
إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَحَلِيمٌ أَوَّاهٌ مُّنِيبٌ ﴿٧٥﴾
75. Hakika Ibrahim alikuwa mpole, mwenye huruma, mwepesi wa kurejea (kwa Mungu).
يَا إِبْرَاهِيمُ أَعْرِضْ عَنْ هَـٰذَا إِنَّهُ قَدْ جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ وَإِنَّهُمْ آتِيهِمْ عَذَابٌ غَيْرُ مَرْدُودٍ ﴿٧٦﴾
76. Ewe Ibrahim! Achana nayo haya. Hakika amri ya Mola wako imekwishakuja, na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.
IBRAHIM ANAJADILI KUHUSU WATU WA NUH
Aya 74-76
MAANA
Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.
Baada ya kujua Ibrahim hali halisi ya wageni wake na madhumuni yao alitulia, na akajawa na furaha yeye na mkewe, Sarah, kwa habari ya kupata mtoto na mjukuu. Lakini hakufurahishwa na habari ya adhabu ya watu wa Lut. Akawa anajadiliana naao.
Kundi kubwa la wafasiri, akiwemo Arrazi na mwenye Tafsir Al-Manar, wamesema kuwa Ibrahim hakujadili kuhusu watu wa Lut; isipokuwa alijadili kuhusu Lut akihofia kupatwa na adhabu. Wafasiri hao wametoa dalili kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:
قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٢﴾
Akasema: Humo yumo Lut. Wakasema: Sisi twajua zaidi aliyemo humo, kwa hakika tutamuokoa yeye na watu wake ila mkewe aliye miongoni mwa watakaobaki nyuma. (29:32).
Lakini ilivyo, Aya hii waliyoitolea ushahidi, haina uhusiano wowote na mjadala wa wa Ibrahim; isipokuwa ni kutolea habari tu kwamba humo yumo Lut; na ndio maana wakasema tunajua sana.
Ayah hii tunayoifasiri inazungumzia mjadala kuhusu watu wa Lut sio kwa Lut peke yake. Kuongezea kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.
Dhamir katika hakika wao na itawajia inawarudia watu wa Lut ambao ibrahim amewajadili. Lakini wafasiri wakasema kuwa kuwajadili watu wa Lut ni kumkosea Adabu Mwenyezi Mungu, na Ibrahim ni Maasum, kwa hiyo hapana budi iwe ni kujadili Lut pekee.
Nasi tunasema:
Kwanza
: hakuna tofauti katika kumjadili Lut peke yake au kaumu yake. Kujadili ni kujadili tu.
Pili
: Mjadala ulikuwa unahusiana na kuondolewa adhabu waja wa Mungu au kuchelweshwa. Kwa hiyo hilo si dhambi; bali ni kinyume cha hivyo. Kwa sababu mjadala huu hauna kupingana wala kuzozana; isipokuwa ni kutaka hurumma kutoka kwa mwenye nguvu kwenda kwa mnyonge. Ombi hili linafahamisha upole na hurumma.
Ndio maana Mwenyezi Mungu akamsifu kuwa niMpole, mwenye hurumma mwepesi wa kurejea (kwa Mungu)
baada ya kuwahurumia watu wa Lut
Tatu
: Ibrahim alijadili kuhusu watu wa Lut ili awe na yakini kwamba wao wameasi kiasi ambacho hakuna tamaa ya kuongoka kwao; sawa na alivyosema:
قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ﴿٢٦٠﴾
Akasema: Huamini? Akasema: Kwa nini! (naamini) Lakini upate kutulia moyo wangu. (2:260).
Hili linasisitizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Ewe Ibrahim! Achana nayo haya. Hakika amri ya Mola wako imekwishakuja, na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.
Yaani usiniulize ewe ibrahim katika mambo yanayohusu watu wa Lut, kwa vile wao wataangamia tu, kwa sababu ya kuendelea kwao na shirk na ufisadi na kutokuwepo tama ya kutubia.
وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَصِيبٌ ﴿٧٧﴾
77. Na wajumbe wetu walipomfikia lut, aliwahuzunikia na akawaonea dhiki. Na akasema: Hii ni siku ngumu.
وَجَاءَهُ قَوْمُهُ يُهْرَعُونَ إِلَيْهِ وَمِن قَبْلُ كَانُوا يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ قَالَ يَا قَوْمِ هَـٰؤُلَاءِ بَنَاتِي هُنَّ أَطْهَرُ لَكُمْ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَلَا تُخْزُونِ فِي ضَيْفِي أَلَيْسَ مِنكُمْ رَجُلٌ رَّشِيدٌ ﴿٧٨﴾
78. Na wakamjia kaumu yake mbiombio na kabla ya haya walikuwa wakifanya maovu. Akasema: Enyi kaumu yangu! Hawa binti zangu wao wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu. Wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu. Hivi hakuna mtu muongofu miongoni mwenu.
قَالُوا لَقَدْ عَلِمْتَ مَا لَنَا فِي بَنَاتِكَ مِنْ حَقٍّ وَإِنَّكَ لَتَعْلَمُ مَا نُرِيدُ ﴿٧٩﴾
79. Wakasema: Umekwishajua hatuna haki juu ya binti zako, na hakika unajua tunayoyataka.
قَالَ لَوْ أَنَّ لِي بِكُمْ قُوَّةً أَوْ آوِي إِلَىٰ رُكْنٍ شَدِيدٍ ﴿٨٠﴾
80. Akasema: Lau ningelikuwa na nguvu kwenu au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!
HUZUNI YA LUT
Aya 77- 80
MAANA
Na wajumbe wetu walipomfikia Lut, aliwahuzunikia na akawaonea dhiki.
Ujumbe uliondoka kwa Ibrahim
kuelekea kwa Lut
.
Katika Juz.8 (7:80) tulitaja kuwa Lut ni mtoto wa ndugu yake Ibrahim na kwamba yeye alikuwa mashariki mwa Jordan na kaumu yake ndio watu wa kwanza kuwaingilia kimwili wanaume badala ya wanawake. Na hili walikuwa wakilifanya dhahiri bila ya uficho wowote. Mwenye kukataa walikuwa wakimshika kwa nguvu; hata kama ni mgeni mheshimiwa.
Kwa hiyo walipokuja wajumbe wa Mwenyezi Mungu kwa Lut, kwa sura za kibinadamu, alihofia watu wake wasiwakosee heshima, huku akiwa hawezi kuwazuia.
Basi akawa anaona uchunguNa akasema: Hii ni siku ngumu.
Na wakamjia kaumu yake mbiombio.
Yaani walikuja nyumbani kwa Nuh haraka wakidhani kuwa siku hii ni kama nyinginena kabla ya haya walikuwa wakifanya maovu
hawakufkiria mwisho wake.
Akasema: Enyi kaumu yangu! Hawa binti zangu wao wametakasika zaidi kwenu.
Makusudi ya binti zake ni binti wa umma wake; kwa sababu mtume ni kama mzazi kwa umma wake. Maana ni kuwa oweni wanawake na mstarehe kwa halali na wema na muache ulawiti kwa sababu hiyo ni kazi ya shetani.Basi mcheni Mwenyezi Mungu.
Anawahofisha na Mungu, na hilo wanalipuuza watu wa ufuska na uovu.
Wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu.
Ikiwa hamumuogopi Mwenyezi Mungu basi angalau muone haya, msinifedheheshe mbele ya wageni.Hivi hakuna mtu muongofu miongoni mwenu?
mwenye akili atakayewazuia hayo mnayotaka?
Wakasema: Umekwishajua hatuna haki juu ya binti zako
Yaani hatuwataki.Na hakika unajua tunayoyataka.
Yaani unajua kuwa sisi hatupendelei mabinti, tunataka wanaume na unajua kuwa sisi hatutishwi na huyo Mungu wako. Binadamu anafikia kiwango hiki cha kiburi akiwa amejiachia, akipinga misimamo na kukosa majukumu.
Kuna watu leo walio mfano wa kaumu Lut katika ushenzi na kiburi tena ni wengi. Miongoni mwao wamo walezi na waalimu wa mashule na vyuo vikuu.
Na sisi hatuna shaka kwamba kuna watu wa dini ambao ni waovu mara elfu kuliko hao. Lakini la kusisitiza ni kuwa lau kusingelikuweko na watu wanaolingania kwenye dini na misimamo, basi ulimwengu ungelikuwa mbaya kuliko ulivyo hivi sasa.
Akasema: Lau ningelikuwa na nguvu kwenu au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!
Baada ya Lut kukata tamaa na watu wake, alitamani lau angelikuwa na nguvu za kuwazuia au kupata msadizi. Alitamani hivi akiwa hajui kwamba nusura ya Mwenyezi Mungu iko nyumbani kwake na kwamba umebakia wakati mchache sana wa kuangamia wafisadi.
قَالُوا يَا لُوطُ إِنَّا رُسُلُ رَبِّكَ لَن يَصِلُوا إِلَيْكَ فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ إِلَّا امْرَأَتَكَ إِنَّهُ مُصِيبُهَا مَا أَصَابَهُمْ إِنَّ مَوْعِدَهُمُ الصُّبْحُ أَلَيْسَ الصُّبْحُ بِقَرِيبٍ ﴿٨١﴾
81. Wakasema: Ewe Lut! Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako. (Hawa) hawatakufikia. Basi ondoka pamoja na watu wako wa nyumbani katika sehemu ya usiku. Wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma, isipokuwa mke wako, kwani yeye yatamsibu yatakayowasibu. Hakika miadi yao ni asubuhi, je asubuhi si karibu?
فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ ﴿٨٢﴾
82. Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini. Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana.
مُّسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ وَمَا هِيَ مِنَ الظَّالِمِينَ بِبَعِيدٍ ﴿٨٣﴾
83. Yaliyotiwa alama kwa Mola wako. Na hayo hayako mbali na wenye kudhulumu.
HAWATAKUFIKIA
Aya 81-83
MAANA
Wakasema: Ewe Lut! Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako. Hawa hawatakufikia.
Arrazi anasema: Malaika walipoona wasiwasi na huzuni ya Lut walimpa bishara zifuatazo:
1. Kwamba wao ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu.
2. Makafiri hwatafikia lile walilolikusudia.
3. Mwenyezi Mungu atawaangamiza.
4. Mwenyezi Mungu atamwokoa yeye na watu wake kutokana na adhabu.
5. Kwamba yeye Lut yuko kwenye Nguzo yenye nguvu, kwa sababu Mungu atamwokoa na watu madhalimu.
Basi ondoka pamoja na watu wako wa nyumbani katika sehemu ya usiku. Wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma, isipokuwa mke wako, kwani yeye yatamsibu yatakayowasibu.
Malaika walimtaka Lut atoke na watu wake wa nyumbani na kutoangalia nyuma yeyote. Huenda hekima ya hilo ilikuwa ni kutoona muangaliaji jinsi mji wake unavyoangamia asishikwe na hurumma akahuzunika.
Ama mkewe alimwacha, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, pamoja na makafiri kwa sababu yeye ni miongoni mwao. Kwa hiyo naye alikuwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu zake.
Hakika miadi yao ni asubuhi, je asubuhi si karibu?
Haya ni katika maneno ya kuashiria jibu la anayeharakisha adhabu.
Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini.
Dhamiri ya tuliiegeuza ni ya ardhi ya vijiji vya kaumu ya Lut. Baadhi ya tafsiri zinasema kuwa umbali wake na Baytul maqdis ni mwendo wa siku tatu
Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana, yaliyotiwa alama kwa Mola wako.
Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:
لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ ﴿٣٣﴾
“Tuwatupie mawe ya udongo” (51:33).
Yaliyopandana inaweza kuwa ni kupandana hayo yenyewe au kupandana kwa mfululizo wa kushuka. Alama ni alama maalumu ya kumfikia yule anayestahiki. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliteremsha adhabu mbili kwa kaumu ya Lut: Mvua ya mawe na kuzama ardhini.
Na hayo hayako mbali na wenye kudhulumu.
Wafasiri wanasema kuwa wenye kudhulumu hapa ni makafiri wa Makka, kwamba Mwenyezi Mungu aliwaahidi kuwa wao, yatawapata yaliyowapata watu wa Lut, kama wataendelea kumkadhibisha Muhammad(s.a.w.w)
.
Maana haya hayako mbali, pamoja na kujua kuwa kila dhalimu aliyeko mashariki au magharibi anaweza kushukiwa na adhabu kutoka mbinguni au kuadhibiwa ardhini. Kwani mapinduzi yoyote yanayotokea au yatakayotokea, basi matokeo yake ni adhabu kwa dhulma na watu wake na kwa ufisadi na wasaidizi wake.
وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ وَلَا تَنقُصُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ إِنِّي أَرَاكُم بِخَيْرٍ وَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ مُّحِيطٍ ﴿٨٤﴾
84. Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Wala msipunguze kipimo na mizani. Mimi ninawaona mko katika kheri; na mimi nawahofia na adhabu ya siku izungukayo.
وَيَا قَوْمِ أَوْفُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٨٥﴾
85. Enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.
بَقِيَّتُ اللَّـهِ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ وَمَا أَنَا عَلَيْكُم بِحَفِيظٍ ﴿٨٦﴾
86. Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ni bora kwa ajili yenu ikiwa nyinyi ni waumini. Wala mimi si mlinzi wenu.
SHUAIB
Aya 84-86
MAANA
Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake.
Imepita tafsiri ya Aya hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (7:85).
Wala msipunguze kipimo na mizani.
Hili ni katazo la kupunja; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾ الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾
“Ole wao wanopunja. Ambao wanapojipimia kwa watu hutaka watimiziwe. Na wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.” (83:1-2)
Mimi ninawaona mko katika kheri.
Makusudio ya kheri hapa ni riziki nyingi.
Na mimi nawahofia na adhabu ya siku izungukayo.
Hii ni kuwaonya na adhabu, kama wataendelea na maasi
Enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu.
Baada ya kuwakataza kupunguza sasa anawaamrisha kutimiza vipimo. Maana zote mbili ni sawa. Hatufahamu lengo lake zaidi ya kuwa ni kusisitiza tu.
Wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao.
Vitu ni kila kitu; kama vile haki ya kimaada (yakuonekana) na ya kimaana (isyoonekana). Kwa hiyo ni haramu kumpunguzia mtu kitu au jambo lolote; kama ilimu yake na hulka yake.
Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.
Katika Aya hii kuna maneo mawili (ta’thaw na Mufsidin) yenye maana moja, ya ufisadi. Kwa hiyo ikawa ni lazima kufanya T’awil (tafsir inayowakilisha). Ama kutafsir Ta’athaw kwa maana ya juhudi; yaani msifanye juhudi ya kuleta ufisadi; au kutafsir Mufisidin kwa maana ya kuleta vurugu; kama vile vita na umwagaji damu, bila ya sababu inayowajibisha. Lakini vita vyenyewe vikiwa ni vya kuondoa ufisadi, basi itakuwa kuacha kupigana ndio ufisadi. Hapo Ndipo jihadi inakuwa ndio twaa bora. Taawili hii ni bora kuliko ile ya kwanza.
Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ni bora kwa ajili yenu ikiwa nyinyi ni waumini.
Halali ni njema na yenye kubaki hata ikiwa chache na haramu ni uovu, ni shari na inakwisha hata ikiwa nyingi. Tukichunguza sababu ya vita leo, tutaona ni kujilundikia mali wachache na kunyimwa wengi.
Imetokea sadfa kusoma magazeti ya leo 24-12-1968, kwamba jamaa huko London walifanya maandamano kuelekea makao ya mfalme, Birmingham (Birmingham Palace) wakimtaka malkia aiache ikulu yake, inayoweza kukaliwa na watu elfu, ambapo London pekee ina watu elfu sita wasio na makazi.
Wala mimi si mlinzi wenu wa kuwazuia na maasi kwa nguvu.
Umuhimu wangu ni kuwanasihi na kufikisha tu, na nimekwishatekeleza kwa ukamilifu na nimeondokana na majukumu. Shuaib (a.s.) ndiye anayesema hivyo.
قَالُوا يَا شُعَيْبُ أَصَلَاتُكَ تَأْمُرُكَ أَن نَّتْرُكَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا أَوْ أَن نَّفْعَلَ فِي أَمْوَالِنَا مَا نَشَاءُ إِنَّكَ لَأَنتَ الْحَلِيمُ الرَّشِيدُ ﴿٨٧﴾
87. Wakasema: Ewe Shuaib! Je, Swala yako inakuamuru tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au kufanya tupendavyo katika mali zetu? Hakika wewe ndiwe mpole, mwongofu!
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَرَزَقَنِي مِنْهُ رِزْقًا حَسَنًا وَمَا أُرِيدُ أَنْ أُخَالِفَكُمْ إِلَىٰ مَا أَنْهَاكُمْ عَنْهُ إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ مَا اسْتَطَعْتُ وَمَا تَوْفِيقِي إِلَّا بِاللَّـهِ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ ﴿٨٨﴾
88. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na ameniruzuku riziki njema itokayo kwake? Wala sipendi kuwakhalifu nikafanya yale ninayowakataza. Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyoweza. Na taufiki yangu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu. Kwake ninategemea na kwake naelekea.
وَيَا قَوْمِ لَا يَجْرِمَنَّكُمْ شِقَاقِي أَن يُصِيبَكُم مِّثْلُ مَا أَصَابَ قَوْمَ نُوحٍ أَوْ قَوْمَ هُودٍ أَوْ قَوْمَ صَالِحٍ وَمَا قَوْمُ لُوطٍ مِّنكُم بِبَعِيدٍ ﴿٨٩﴾
89. Na enyi watu wangu! Kupingana nami kusije kukawapelekea yakawasibu kama yaliyowasibu kaumu ya Nuh au kaumu ya Hud au kaumu ya Swaleh, na kaumu ya Lut si mbali nanyi.
وَاسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ ﴿٩٠﴾
90. Na muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake. Hakika Mola wangu ni Mwenye kurehemu, Mwenye upendo.
HISTORIA YA UKOMUNISTI NA UBEPARI
Aya 87-90
MAANA
Wakasema: Ewe Shuaib! Je, Swala yako inakuamuru, tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au kufanya tupendavyo katika mali zetu?
Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, huifanya swala ni ya kudharau na kuifanyia stizai pamoja na hao wanaoswali. Bila shaka yoyote Shuaib alikuwa ni katika wanaoswali.
Alipowaamuru watu wake kutupilia mbali masanamu, na kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuwakataza chumo la haramu, ndio wakaanza kumdharau na kusema: Hivi swala yako ya kipuuzi unayoiswali ndiyo inakufanya utuamrishe tuache ada zetu tulizowakuta nazo mababa zetu na mababu zetu jadi na jadi; tena unatukataza tuache kuchumma mali vile tupendavyo?
Hakika wewe ndiwe mpole, mwongofu!
Yaani, kweli wewe una akili kwa haya uyasemayo?
Aya hii inakusanya mambo yafuatayo:-
1. Risala ya mitume haiko kwenye nembo peke yake, bali inakusanya maisha ya kijamii na kumpangia binadamu uhuru wake na matumizi yake na kumwekea mipaka ya kutomwingilia mwingine, vilevile kumzuia kufanya tendo lolote baya litakaloleta madhara kwa mtu binafsi na kwa jamii. Dalili wazi juu ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya 85 ya sura hii: “wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu”
2. Aya imefahamisha kuwa maadui wakubwa wa mitume na wenye kuswali ni wale wanaotafuta mali kwa hadaa na utapeli na kutumia vipato vya watu vile wanavyotaka; kama yanavyofanya mashirika mengi ya ulanguzi na unyonyaji.
3. Vilevile Aya inafahamisha kwamba ubepari una mizizi ya kihistoria.
Ushahidi wa hilo ni mwingi sana. Kwa mfano huu ubepari unaotaka kila mtu awe na uhuru wa kupata utajiri vile atakavyo, iwe ni kwa uporaji au kwa lolote lile. Hilo linafafanuliwa na kauli ya waliomdodosa Shuaib: “Au kufanya tupendavyo katika mali zetu” Makusudio sio kula na kuvaa watakavyo; isipokuwa ni kuwatumia watu katika kupata mali vile wapendavyo.
Kama ambavo historia imeonyesha kuwa siasa za Ubepari zilianza zamani, vilevile inafahimisha historia kuwa Ukomonisti nao ulianza zamani. Imeelezwa katika uchunguzi wa mwanahistoria W.L. Dewarnet kwamba watafiti walipata ubao wa Sumeria ambao tarehe yake inarudi kwenye mwaka 2100, kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, ukisema kuwa Serikali ndiyo inayopanga mwelekeo wa kiuchumi.
Katika Babilon, mnamo mwaka wa 1750, kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, Sheria ya Hamurabi ndiyo iliyokuwa ikipanga bei za kila kitu. Na katika zama za Batholomeo, serikali ndiyo iliyokuwa ikimiliki ardhi na kuongoza kilimo na mengimeyo.
Uislamu haukubaliani na siasa za ubepari wala za ukomonisti kwa maana yake yaliyo mashuhuri; isipokuwa unakubaliana na kila linalotatua matati- zo ya maisha bila ya kuwapunguzia watu vitu vyao. Angalia kifungu, ‘Tajiri ni wakili sio mweneyewe’ katika kufasiri Juz. 4 (3:182)
Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ni dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu?
Imetangulia Aya kama hii katika Aya 28 ya sura hii.
Na ameniruzuku riziki njema itokayo kwake?
Baada ya Shuaib kuwaamrisha watu wake wachume kihalali na kuwakataza haramu, aliwapa hoja ya riziki aliyoruzukiwa na Mwenyezi Mungu, inayotosheleza mahitaji yake yote, pamoja nakuwa yeye yuko mbali na haramu.
Kwa hiyo basi sababu za riziki nzuri sio haramu. Ni jambo lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu afungue mlango wa riziki kisha awanyime waja wake. Kauli yake: Na ameniruzuku riziki njema, inaonyesha alikuwa na maisha mazuri.
Wala sipendi kuwakhalifu nikafanya yale ninayowakataza.
Lau angelifanya hivyo wao wangelikuwa na hoja juu yake. Na katika sharti za mtume ni kuwa sifa zake zote ziwe ni za kuvutia sio za kufukuza. Na ilivyo ni kuwa anayesema asiyoyafanya basi atakimbiwa.
Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyoweza.
Na mtengenezaji huwaonya watu kwa vitendo vyake kabla ya maneno yake. Na kuendeleza mwito wake huku akivumlia adha na mashaka. Ndio maana Shuaib na mitume wengineo walikuwa wakila kutokana na kazi ya mikono yao na walikuwa wakivumilia adha kutoka kwa makafiri na wapinzani.
Na taufiki yangu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu. Kwake ninategemea na kwake naelekea.
Yaani kwamba yeye ataendelea kutekeleza risala yake kwa hali yoyote itakavyokuwa, akiwa anamtegemea Mwenyezi Mungu, kutaka msaada wake na kumrejea yeye katika mambo yake.
Na enyi watu wangu! Kupingana nami kusije kukawapelekea yakawasibu kama yaliyowasibu kaumu ya Nuh au kaumu ya Hud au kaumu ya Swaleh, na kaumu ya Lut si mbali nanyi.
Yaani uadui wenu kwangu usije ukawasababishia adhabu. Kwani hakuna watu waliomfanyia uadui mtume wao ila huwashukia wao adhabu. Ushahidi wa hayo ni mitume waliotajwa. Ni kama mfano wa anayeambiwa: Usimuudhi baba yako usije ukapatwa na hasira za Mwenyezi Mungu.
Na muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.
Umepita mfano wake pamoja na tafsir yake katika Aya ya 52 na 61 ya Sura hii.
Hakika Mola wangu ni Mwenye kurehemu Mwenye upendo.
Mwenye kurehemu anayemtaka maghufira na Mwenye upendo kwa kuwaneemesha waja wake, kuwapa nasaha na kuapa muda ili wapate kurejea.