1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
Mwendelezo Wa Sura Ya Kumi na Mbili: Surat Yusuf
وَمَا أُبَرِّئُ نَفْسِي إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلَّا مَا رَحِمَ رَبِّي إِنَّ رَبِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٣﴾
53. Nami sijitakasi nafsi yangu; hakika nafsi ndiyo iamrishayo mno uovu, isipokuwa ile ambayo Mola wangu ameirehemu. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
NAFSI
Aya 53
Mwanadamu ni mnyama mwenye akili na dini. Yeye kwa unyama wake au kwa nafsi yake anapondokea sana kwenye matamanio na starehe, hajali akili wala dini. Lakini kwa dini yake na akili yake anaizuia nafsi yake na akili yake isipetuke mipaka ya sharia.
Kwa hiyo mwenye kuiachia nafsi yake ifanye vile itakavyo, basi yeye ni mnyama katika sura ya binadamu, bali ni afadhali mnyama, kwa vile binadamu ana majukumu na ataulizwa, lakini mnyama hana majukumu yoyote. Ndio maana Mwenyez Mungu akasema:
إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٤٤﴾
“Hawakuwa wao ila ni kama wanyama, bali wao wamepotea zaidi njia” (25:44).
Ni kweli kwamba wakati mwingine mtu anaweza kuwa dhaifu mbele ya matamanio, lakini muumin mwenye akili anarudi kwenye uongofu wake na kutubia; Mwenyezi Mungu naye humsamehe, kwa sababu ni Mwingi wa Maghufira, Mwenye kurehemu.
Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Ispokuwa ile ambayo Mola wangu ameirehemu.” Maana yake ni kuwa nafsi yoyote haiwezi kusalimika na kasoro isipokuwa ile aliyoihifadhi Mwenyezi Mungu kutokan na makosa na madhambi (isma) kama nafsi za mitume na maimamu. Muhimu ni kutong’ang’ania mkosaji na kuachana kabisa na Mola wake. Imam Ali
anasema:“Dhambi kubwa ni ile ambayo mwenyewe ameipuuza”
yaani ameing’ang’ania na wala asiombe msamaha.
وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ أَسْتَخْلِصْهُ لِنَفْسِي فَلَمَّا كَلَّمَهُ قَالَ إِنَّكَ الْيَوْمَ لَدَيْنَا مَكِينٌ أَمِينٌ ﴿٥٤﴾
54. Akasema mfalme: Mleteni awe wangu mwenyewe. Basi alipozungumza naye alisema: Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima, mwenye kuaminika.
قَالَ اجْعَلْنِي عَلَىٰ خَزَائِنِ الْأَرْضِ إِنِّي حَفِيظٌ عَلِيمٌ ﴿٥٥﴾
55. Akasema (Yusuf): Nifanye mweka hazina wa nchi, hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.
وَكَذَٰلِكَ مَكَّنَّا لِيُوسُفَ فِي الْأَرْضِ يَتَبَوَّأُ مِنْهَا حَيْثُ يَشَاءُ نُصِيبُ بِرَحْمَتِنَا مَن نَّشَاءُ وَلَا نُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾
56. Na hivyo ndivyo tulivyompa cheo Yusuf katika nchi akae humo popote apendapo. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupotezi ujira wa wafanyao mema.
وَلَأَجْرُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٥٧﴾
57. Na ujira wa akhera ni bora kwa wale walioamini na wakawa wanamcha (Mungu).
YUSUF NI MUHESHIMIWA MISR
Aya 54-57
MAANA
Akasema mfalme: “Mleteni awe wangu mwenyewe.” Basi alipozungumza naye alisema: “Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima, mwenye kuaminika.”
Baada ya mke wa waziri na wale wanawake wengine kukiri na watu wote kujua kuwa Yusuf hana hatia, Yusuf alikubali kutoka gerezani na mfalme alipokutana naye na kumsikiza, alimpenda na akamtaka awe kiongozi katika serikali yake aweze kumsaidia kuendesha serikali, akamwambia: “Wewe ni mwenye heshima na mtu mwenye kuaminiwa kwenye kila kitu katika serikali.“
Mfalme hakuyasema haya ila baada ya kuwa na uhakika wa uwezo wake, ujuzi wake na hekima yake. Inasemekana umri wa Yusuf wakati huo ulikuwa ni miaka 30. Katika Majmaul bayan imeelezwa kuwa Yusuf alimsalimia mfalme kwa lugha ya kiarabu.
Mfalme alipomuuliza umeipata wapi lugha hii, alisema ni lugha ya ami yangu Ismail. Katika tafsir Al-manar imeelezwa kwamba mfalme aliyekuweko wakati wa Yusuf alikuwa ni katika wafalme wa kiarabu walio maarufu kwa jina la Hyksos.
Tabari anasema alikuwa akiitwa Walid bin Rayyan.
Akasema (Yusuf): “Nifanye mweka hazina wa nchi, hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.”
Baada ya mfalme kumwachia Yusuf afanye atakavyo na achague cheo, basi alichagua cheo cha wizara ya hazina na uchumi.
Alichagua cheo baada ya kuhiyarishwa na wala hakuanza yeye, isije ikaonekana kuwa anataka cheo. Hata kama tukisema ameanza yeye, basi itakuwa sio kwa maslahi yake bali ni kwa maslahi ya umma na kulinda haki za wanyonge; hasa kwenye mwaka wa kahati na njaa.
Yusuf alijua kuwa nchi inakabiliwa na janga; ikiwa mweka hazina si mjuzi na asiyekuwa mlinzi imara, basi watu hawatapata haki yao; hasa mafukara na maskini.
Zaidi ya hayo ni kuwa wizara hiyo ni nyeti sana; ikishikwa na watu wasio na ujuzi na uamnifu, umma utaangamia tu; hata ikiwa sio wakati wa shida. Lakini ikiwa mikononi mwa wajuzi na walio na uaminifu, umma utaongoka kidunia na kiakhera.
Wengi wamenukuu kuwa Yusuf aliposhikilia hazina, na watu kuona uamnifu wake na kumpa kila mtu haki yake, waliamini utume wake; hata mfalme pia alishahadia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Yusuf ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.
Ismail Haqqiy, anasema katik Rawhul bayan:
“Amesema Mujahid: Mfalme alisilimu kupitia kwa Yusuf, pamoja na watu wengi.” Mwenye Tafsir al-bayan, aliongezea juu ya kauli hii ya Mujahid kwa kusema: Ikiwa hisani na ukarimu wa Yusuf ni sababu ya imani, basi unaonaje yule aliyemsaidia mtume(s.a.w.w)
na akamkinga na kumhami muda wa uhai wake. Ambaye ni ami yake, Abu Twalib? Kwa hiyo ukweli hasa, yeye ni katika wale ambao Mwenyezi Mungu amewahuyisha kwa imani, kama ilivyotangulia kuelezwa.”
Yametangulia maelezo ya kusilimu Abu Twalib katika Juz. 11 (9:113).
Hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.
Nitailinda mali isipotee bure na kufanyiwa israf, na ninajua wale wanaostahiki kupewa na kila kitu nitakiweka mahali pake panapostahiki.
Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq, amesema: “Inajuzu kwa mtu kujisifu ikibidi kufanya hivyo, kwani Yusuf alisema: “Nifanye mweka haz- ina wa nchi; hakika mimi ni mlinzi, mjuzi.”
Katika baadhi ya Tafsiri imeelezwa kuwa Yusuf hakuwahi kumnyenyekea Mfalme kwa kumwambia: uishi ewe mfalme! Mimi ni mtumwa wako mnyenyekevu; kama wafanyavyo leo wale wanaojipendekeza kwa wakubwa; isipokuwa alitaka yale ambayo anaamini kuwa anayamudu; kama maandalizi ya kukabiliana na majanga na kulinda nchi kutokana na uharibifu. Laiti wale wanaojipendekeza kwa wakubwa wangelisoma Qur’an wakajua kuwa heshima haiji kwa kujipendekeza
Razi anasema: Yamepokewa masimulizi kuwa Mfalme alimwambia Yusuf: “Napenda kukushirikisha kwenye kila kitu isipokuwa katika watu wangu wa nyumbani na kula na mimi.” Yusuf akamwambia: “Siwezi kula pamoja nawe na mimi ni Yusuf bin Ya’qub bin Is-haq bin Ibrahim kipenzi cha Mungu!”
Na hivyo ndivyo tulivyompa cheo Yusuf katika nchi akae humo popote apendapo. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupotezi ujira wa wafanyao mema.
Yusuf alivumilia kutupwa kisimani, kuuzwa utumwani, kutumikia nyumba ya waziri, kutuhumiwa na kufungwa gerezani. Aliyavumilia yote hayo na mengine kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutosheka naye. Je, natija yake ilikuwa ni nini? Alitoka gerezani kishujaa akiwa ni mshindi wa vita vya uvumilivu; ni mtu huru na akawa mmoja wa viongozi wa nchi. Hivi ndivyo wanavyolipwa wavumilivu ujira wao katika dunia.
Na ujira wa akhera ni bora kwa wale walioamini na wakawa ni wenye kumcha (Mungu).
Malipo ya akhera ni Pepo ambayo “Haikatiki neema yake, haondoki mkazi wake, hazeeki anayedumu, wala kukata tamaaa anayekaa humo” kama alivyosema Imam Ali.
Sasa iko wapi neema hii na ile ambayo mfalme anazeeka kwa taabu na maumivu. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa mke wa mheshimiwa alimjia Yusuf siku za kahati akitafuta chakula, mumewe akiwa amekufa na yeye dunia imemwinamia, yakawa yamempata yaliyompata.
Yusuf alipomuona alimwambia imekuwaje kuwa katika hali hii, naye akasema:
Ametakataka na maovu ambaye anawafanya wafalme kuwa watumwa kwa kwa sababu ya kumwasi na anayewafanya watumwa kuwa wafalme kwa sababu ya kumtii.
وَجَاءَ إِخْوَةُ يُوسُفَ فَدَخَلُوا عَلَيْهِ فَعَرَفَهُمْ وَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ ﴿٥٨﴾
58. Wakaja ndugu zake Yusuf wakaingia kwake. Yeye akawajua na wao hawakumjua.
وَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ قَالَ ائْتُونِي بِأَخٍ لَّكُم مِّنْ أَبِيكُمْ أَلَا تَرَوْنَ أَنِّي أُوفِي الْكَيْلَ وَأَنَا خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٥٩﴾
59. Alipowatengenezea mahitaji yao aliwaambia: “Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je hamuoni kuwa mimi ninatimiza kipimo na kwamba mimi ni mbora wa wakaribishao?
فَإِن لَّمْ تَأْتُونِي بِهِ فَلَا كَيْلَ لَكُمْ عِندِي وَلَا تَقْرَبُونِ ﴿٦٠﴾
60. Msiponiletea basi hampati kipimo chochote kwangu wala msinikurubie.
قَالُوا سَنُرَاوِدُ عَنْهُ أَبَاهُ وَإِنَّا لَفَاعِلُونَ ﴿٦١﴾
61. Wakasema: “Tutamrairai baba yake, na hakika sisi tutafanya.”
وَقَالَ لِفِتْيَانِهِ اجْعَلُوا بِضَاعَتَهُمْ فِي رِحَالِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَعْرِفُونَهَا إِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٦٢﴾
62. Akawaambia watumishi wake: “Tieni bidhaa zao katika mizigo yao ili wazione watakaporudi kwa watu wao ili wapate kurejea.”
WAKAJA NDUGUZE YUSUF
Aya 58-62
MAANA
Wakaja ndugu zake Yusuf wakaingia kwake, Yeye akawajua na wao hawakumjua.
Kahati ilienea mpaka miji ya jirani, ikiwemo Palestina na Kanani aishipo Nabii wa Mungu, Ya’qub. Ikawa imeenea habari kwamba waziri wa Misr amejiandaa vizuri kuikabili njaa na kwamba yeye anagawanya chakula kwa uadilifu bila ya kumbagua yeyote.
Nyumbani kwa Ya’qub kukawa na shida, kama iliyoko katika majumba mengine, Hivyo akawaamrisha wanawe waende Misr kuhemera chakula.
Basi wakaondoka kuelekea Misr wakiwa ni watu kumi. Walipofika huko waliingia makao ya waziri wakamkuta Yusuf, kwa sababu alikuwa akisimamia kazi yeye mwenyewe, Yusuf akawatambua, lakini wao hawakumatambua.
Alipowatengenezea mahitaji yao
Baada ya kuwaandalia mahitaji yao yote pamoja na yale ya safari,aliwaambia: “Nileteeni ndugu yenu kwa baba.”
Wafasiri wanasema kuwa Yusuf aliwakirimu sana ndugu zake mpaka wakawa hawana wasiwasi naye; wakazungumza naye kuhusu maisha yao na ya baba yao na kwamba wao wana ndugu yao mdogo wa baba mmoja, Ndipo Yusuf akawaambia basi nileteeni huyo ndugu yenu mdogo.
Katika Aya hakuna linalofahamisha kuwa walizungumza naye, lakini kuhusu kuwakirimu kunafahamishwa na kauli:
Je hamuoni kuwa mimi ninatimiza kipimo na kwamba mimi ni mbora wa wakaribishao? Msiponiletea basi hampati kipimo chochote kwangu wala msinikurubie
Maana yako wazi, Kwa mnasaba wa Aya hii, wamekongamana mafakihi kwamba inafaa kwa muuzaji na mnunuzi kuweka sharti lolote apendalo katika biashara, maadam haliharamishi halali wala kuahalalisha haramu. Na sharti la Yusuf ni katika aina hii.
Wakasema: Tutamrairai baba yake; na hakika sisi tutafanya.
Wao walikuwa wanajua kuwa baba yao si rahisi kumtoa, ndio maana wakasema kuwa watamrairai; yaani watajitahidi na kumbembeleza baba yao; pamoja na ugumu wa jambo lenyewe.
Akawaambia watumishi wake: “Tieni bidhaa zao katika mizigo yao.
Yusuf aliwaamrisha watumishi wake warudishe vile vitu walivyonunulia chakula kwenye mizigo yao, bila ya wao kutambua.
Ili wazione watakaporudi kwa watu wao wapate kurejea
tena kwa kuwa na tamaa ya ukarimu wa Yusuf. Sio mbali kuwa lengo la Yusuf ni kumtuliza baba yake ili asione uzito kumwachia ndugu yake aje kwake.
فَلَمَّا رَجَعُوا إِلَىٰ أَبِيهِمْ قَالُوا يَا أَبَانَا مُنِعَ مِنَّا الْكَيْلُ فَأَرْسِلْ مَعَنَا أَخَانَا نَكْتَلْ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٦٣﴾
63. Basi waliporudi kwa baba yao, walisema: “Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula, basi mtume ndugu yetu pamoja nasi ili tupate kupimiwa na kwa hakika sisi tutamlinda.
قَالَ هَلْ آمَنُكُمْ عَلَيْهِ إِلَّا كَمَا أَمِنتُكُمْ عَلَىٰ أَخِيهِ مِن قَبْلُ فَاللَّـهُ خَيْرٌ حَافِظًا وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٦٤﴾
64. Akasema: Je nikuaminini kwa huyu kama nilivyokuaminini kwa nduguye zamani? Basi Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kulinda, na ndiye anayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu.
وَلَمَّا فَتَحُوا مَتَاعَهُمْ وَجَدُوا بِضَاعَتَهُمْ رُدَّتْ إِلَيْهِمْ قَالُوا يَا أَبَانَا مَا نَبْغِي هَـٰذِهِ بِضَاعَتُنَا رُدَّتْ إِلَيْنَا وَنَمِيرُ أَهْلَنَا وَنَحْفَظُ أَخَانَا وَنَزْدَادُ كَيْلَ بَعِيرٍ ذَٰلِكَ كَيْلٌ يَسِيرٌ ﴿٦٥﴾
65. Wailpofungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. (Wakasema): Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Na tutaleta chakula kwa ajili ya watu wetu na tutamlinda ndugu yetu na tutapata ziada ya kipimo cha ngamia mmoja. Hicho ni kipimo kidogo.
قَالَ لَنْ أُرْسِلَهُ مَعَكُمْ حَتَّىٰ تُؤْتُونِ مَوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ لَتَأْتُنَّنِي بِهِ إِلَّا أَن يُحَاطَ بِكُمْ فَلَمَّا آتَوْهُ مَوْثِقَهُمْ قَالَ اللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٦٦﴾
66. Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtamleta kwangu ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipompa ahadi yao, alisema: Mwenyezi Mungu ndiye mtegemewa kwa tuyasemayo.
MTUME NDUGU YETU PAMOJA NASI
Aya 63-66
MAANA
Basi waliporudi kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula.
Wakiashiria kauli ya Yusuf Msiponiletea basi hampati kipimo chochote kwangu, Kisha wakamwambia baba yao:
Basi mtume ndugu yetu pamoja nasi ili tupate kupimiwa na kwa hakika sisi tutamlinda.
Walitoa ahadi ya kumlinda na kumhifadhi ili baba yao asiwanyime.
Je nikuaminini kwa huyu kama nilivyokuaminini kwa nduguye zamani?
Mlivyomfanyia?
Kisha akaelekea kwa Mwenyezi Mungu na akasema:
Basi Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kulinda na ndiye anayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu.
Mimi namtegemea Mwenyezi Mungu katika uhifadhi na ulinzi wa mwanagu sio hifadhi yenu. Na yeye Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuhurumia unyonge wangu na uzee wangu. Inasemekana kuwa jina la huyo mtoto wake mdogo lilikuwa ni Bin-yamin (Benjamin).
Wailpofungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa.
Wakamkimbilia baba yao wakiwa na furaha na wakasema:
Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi?
Yaani tutatoa sababu gani kwake kama hatukwenda na ndugu yetu na ametukirimu namna hii kama uonavyo ameturudishia mali yetu.
Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa.
Inasemekana mali yenyewe ilikuwa ni viatu na ngozi.
Baadhi ya wafasiri wa kisasa wanasema kuwa walikuta mali yao tu, sio chakula na kwamba Yusuf alifanya hivyo ili walazimike kurudi na ndugu yao. Lakini hayo ni makosa kwa sababu yanapingana na dhahiri ya Qur’an amabayo ni: “Je hamuoni kuwa mimi ninatimiza kipimo na kwamba mimi ni mbora wa wakaribishao?”
Zaidi ya hayo kuwanyima ndugu chakula wakati wanakihitajia ni roho mbaya na ngumu sana, jambo ambalo liko mbali sana na Yusuf. Ama kauli yao “Tumenyimwa chakula” ni kunyimwa mara ya pili watakaporudi.
Na tutaleta chakula kwa ajili ya watu wetu na tutamlinda ndugu yetu
na kila jambo baya.
Na tutapata ziada ya kipimo cha ngamia mmoja.
Kwa sabbu Yusuf alikuwa akimpa kila mtu kipimo cha ngamia mmoja tu, ili watu wote wapate chakula. Kwa hiyo wakienda na ndugu yao watazidisha mzigo wao.
Hicho ni kipimo kidogo.
Yaani ziada itapatikana kwa kuweko ndugu yetu; vinginevyo, hatupati. Yaqub akaona haja ya chakula imezidi na kile walichokuja nacho
kinakaribia kwisha. Hivyo akakubali kwa sababu ya haja si kwa sababu ya shinikizo la wanawe, kuongezea kumwamini waziri kutokana na sifa nzuri alizozisikia na jinsi alivyowafanyia wanawe.
Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtamleta kwangu ila ikiwa mmezungukwa.
Aliwaruhusu kuondoka na Bin-yamin kwa sharti la kutoa ahadi madhubuti kuwa watamrudisha salama isipokuwa wakitokewa na sababu zisizoweza kuzuilika.
Basi walipompa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye mtegemewa kwa tuyasemayo.
Yaani walipompa ahadi aliyoitaka, kwamba watamfidia kwa roho zao, alisema Mungu peke yake ndiye shahidi wa haya tuyasemayo. Mkitekeleza, Mungu atawalipa mema na mkihalifu atawalipa adhabu kubwa.
وَقَالَ يَا بَنِيَّ لَا تَدْخُلُوا مِن بَابٍ وَاحِدٍ وَادْخُلُوا مِنْ أَبْوَابٍ مُّتَفَرِّقَةٍ وَمَا أُغْنِي عَنكُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَعَلَيْهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُتَوَكِّلُونَ ﴿٦٧﴾
67. Akasema: “Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbalimbali. Wala mimi siwafai na chochote mbele ya Mwenyezi Mungu; hukumu haiko ila kwa Mwnyezi Mungu tu, juu yake yeye ninategemea na juu yake yeye wategemee wanaotegemea.”
وَلَمَّا دَخَلُوا مِنْ حَيْثُ أَمَرَهُمْ أَبُوهُم مَّا كَانَ يُغْنِي عَنْهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ إِلَّا حَاجَةً فِي نَفْسِ يَعْقُوبَ قَضَاهَا وَإِنَّهُ لَذُو عِلْمٍ لِّمَا عَلَّمْنَاهُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٦٨﴾
68. Walipoingia kama alivyowaamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu; isipokuwa ni haja tu iliyo katika nafsi ya Ya’qub aliitimiza. Na hakika yeye ana elimu kwa tulivyomfundisha, lakini watu wengi hawajui.
MSIINGIE MLANGO MMOJA
Aya 67-68
MAANA
Akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbalimbali.
Baada ya kusisitiza ahadi yao kwa baba yao, aliwaruhusu kuondoka na ndugu yao mdogo na akawapa wasia huu. Inaonekana kuwa huo mji ulikuwa na milango mingi ya kuingilia, Baadhi ya tafsiri zinasema ilikuwa milango mine.
Wametofautiana wafasiri kuhusu lengo la Ya’qub kwenye wasia huu, Hakuna maelezo ya kutegemewa, Pengine inawezekana kuwa kama wataingia pamoja nao ni genge la watu 11, watu wanaweza kuanza kujiuliza uliza.
Au pengine ni kwa lengo la kuujua mji na kuchunguza habari za Yusuf. Kwa vyovyote iwavyo, sisi hatukalifiwi kutafiti lengo la wasia huo, maadamu Aya haikulidokeza.
Katika tafsir Bahrul Muhit, imeelezwa kuwa Ya’qub aliwatuma wanawe wamplekee salaam waziri kwamba baba yetu anakuombea rehema na anakushukuru ulivyotufanyia. Yusuf aliposikia ujumbe huu alilia. Hayo hayako mbali na maudhui haya.
Wala mimi siwafai na chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwnyezi Mungu tu.
Katika kufasiri Juz.12 (12:40) kifungu ‘Hakuna hukumu sipokuwa ya Mwenyezi Mungu’ tulibainisha kwamba hukumu yake Mwenyezi Mungu inaweza kuwa ni halali na haramu, inayoitwa hukumu ya sharia.
Vile vile inaweza kuwa ni kadha yake na kadari ambayo haiepukiki. Mfumo wa Aya unafahamisha kuwa hayo ndio makusudio yake hapa. Na maana yake ni kuwa mimi ninawapa nasaha na kuwatakia mema, lakini yote hayo hayawezi kuzuia kadari na hukumu ya Mwenyezi Mungu.
Lengo lake katika hilo ni kuwabainishia wanawe kwamba mtu asitegemee vitendo peke yake wala imani peke yake; bali afanye vitendo na kujitahidi huku akimtegemea Mwenyezi Mungu na kuitakidi kuwa yeye ndiye msaidizi wake. Ndio maana akasema:
Juu yake Yeye ninategemea na juu yake Yeye wategemee wanaotegemea.
Yaani mimi ninamwamini Mwenyezi Mungu na ninamtegemea Yeye na kila anayemwamini mwenyezi Mungu anatakikana kuwa hivyo.
Walipoingia kama alivyowaamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu.
Yaani watoto wa Ya’qub waliingia mjini Misr kwa kupitia milango mbalimbali, kwa kufuata amri ya mzazi wao, lakini hilo halikuwafaa kitu wala kuzuia balaa, kama alivyotangulia kusema baba yao: “Wala mimi siwafai na chochote mbele ya Mwenyezi Mungu” amabapo walituhumiwa wizi na kuchukuliwa Bin-yamin wakarudi kwa baba wakiwa hoi; kama itakavyoelezwa.
Ispokuwa ni haja tu iliyo katika nafsi ya Ya’qub aliitimiza.
Wamatofautiana wafasiri kuhusu haja ya Ya’qub iliyotimizwa na Mwenyezi Mungu. Kuna aliyesema kuwa ni kuwa watoto wa Ya’qub wasipatwe na jicho watakapoingia Misr. Mwingine akasema kuwa ni waziri asiwapate na jambo baya.
Tuanavyo sisi, kulingana na hali ilivyo, na kulingana na Aya inayoonyesha kuhangaika kwa Ya’qub juu ya Yusuf na nduguye, ni kwamba haja ya kwanza na ya mwisho ya Ya’qub, katika maisha haya, ni usalama wa Yusuf na nduguye na kuwa pamoja nao ni kitulizo cha moyo wake. Na mwenyezi Mungu alimtimizia aliyoyataka kwa uzuri.
Na hakika yeye ana elimu kwa tulivyomfundisha.
Yeye ni mtume na kila mtume anafundishwa na kupata elimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwa mafunzo hayo kwa Ya’qub ni uvumilivu wake wa misukosuko na kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu na kuacha kukata tamaa na rehema ya mwenyezi Mungu. Na miongoni mwa elimu yake ni kuwa mambo yote ya waja yako kwa Mwenyezi Mungu.
Lakini watu wengi hawajui
kwamba hukumu ni ya Mwenyezi Mungu na kwamba mipango yote ya waja bila ya msaada wa Mwenyezi Mungu haina manufaa yoyote.