2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
وَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَخَاهُ قَالَ إِنِّي أَنَا أَخُوكَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٦٩﴾
69. Walipoingia kwa Yusuf alimkumbatia ndugu yake akasema: Hakika mimi ni nduguyo, Basi usihuzunike kwa waliyokuwa wakiyafanya.
فَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ جَعَلَ السِّقَايَةَ فِي رَحْلِ أَخِيهِ ثُمَّ أَذَّنَ مُؤَذِّنٌ أَيَّتُهَا الْعِيرُ إِنَّكُمْ لَسَارِقُونَ ﴿٧٠﴾
70. Alipokwisha watengenezea mahitaji yao akaweka kopo katika mzigo wa ndugu yake. Kisha mnadi akanadi: “Enyi wasafiri! Hakika nyinyi ni wezi.”
قَالُوا وَأَقْبَلُوا عَلَيْهِم مَّاذَا تَفْقِدُونَ ﴿٧١﴾
71. Wakasema na hali wamewaelekea: “Mmepoteza nini?”
قَالُوا نَفْقِدُ صُوَاعَ الْمَلِكِ وَلِمَن جَاءَ بِهِ حِمْلُ بَعِيرٍ وَأَنَا بِهِ زَعِيمٌ ﴿٧٢﴾
72. Wakasema: “Tumepoteza kopo la mfalme na atakayelileta atapata shehena nzima ya ngamia na mimi ni mdhamini.
قَالُوا تَاللَّـهِ لَقَدْ عَلِمْتُم مَّا جِئْنَا لِنُفْسِدَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كُنَّا سَارِقِينَ ﴿٧٣﴾
73. Wakasema: “Wallahi mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya ufisadi katika nchi hii wala sisi si wezi.”
قَالُوا فَمَا جَزَاؤُهُ إِن كُنتُمْ كَاذِبِينَ ﴿٧٤﴾
74. Wakasema: “Malipo yake yatakuwa ni nini ikiwa nyinyi ni waongo?”
قَالُوا جَزَاؤُهُ مَن وُجِدَ فِي رَحْلِهِ فَهُوَ جَزَاؤُهُ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ ﴿٧٥﴾
75. Wakasema: “Malipo yake ni yule ambaye litaonekana katika mzigo wake, basi huyo ndiye malipo yake, Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.”
فَبَدَأَ بِأَوْعِيَتِهِمْ قَبْلَ وِعَاءِ أَخِيهِ ثُمَّ اسْتَخْرَجَهَا مِن وِعَاءِ أَخِيهِ كَذَٰلِكَ كِدْنَا لِيُوسُفَ مَا كَانَ لِيَأْخُذَ أَخَاهُ فِي دِينِ الْمَلِكِ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَّن نَّشَاءُ وَفَوْقَ كُلِّ ذِي عِلْمٍ عَلِيمٌ ﴿٧٦﴾
76. Basi akaanza na mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake; kisha akalitoa katika mzigo wa ndugu yake, Hivyo ndivyo tulivyomfanyia hila Yusuf hakuweza kumchukua ndugu yake katika sharia ya mfalme, isipokuwa alivyotaka Mwenyezi Mungu, Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao, Na juu ya kila mwenye elimu yuko ajuaye zaidi.
MIMI NI NDUGUYO, USIHUZUNIKE
Aya 69-76
Maana
Walipoingia kwa Yusuf, alimkumbatia ndugu yake akasema: “Hakika mimi ni nduguyo, Basi usihuzunike kwa waliyokuwa wakiyafanya.”
Watu wa tafsiri akiwemo Tabari, Razi, Tabrasi na Abu Hayani al-andalusi, wametaja ufafanuzi wa Aya hii ambao hauna dalili katika Qur’an, lakini unaoana nayo na kunasibiana nayo. Kwa ajili hii tutafupiliza kauli zao, kama ifuatavyo:
Ndugu wa Yusuf walipofika Misr aliwaalika kwenye chakula na akawaweka wawili wawili, kwa lengo la kuwa yeye abakie na ndugu yake Bin-yamin akae naye kwenye meza yake ya chakula; sawa na alivyofanya Muhammad(s.a.w.w)
baina ya maswahaba zake wawili wawili kuwa ndugu na akambakisha Ali awe wake yeye.
Baada ya chakula, Yusuf aliwapangia vyumba vya kulala wawili wawili na ndugu yake Bin-yamini akalala naye chumba kimoja. Walipokuwa peke yao akamwambia: “Je, unapenda mimi niwe ndugu yako?” Akamjibu ni nani anaweza kuwa na ndugu mfano wako? Lakini wewe hukuzaliwa na Ya’qub wala Rahel. Basi akamkumbatia na kumwambia: “Mimi nimezaliwa na Ya’qub na Rahel. Basi mimi ni ndugu yako, Wala usuhuzunike na waliyotufanyia ndugu zetu.” Bin-Yamin akafurahi sana na akamshukuru Mwenyezi Mungu.
Alipokwisha watengenezea mahitaji yao akaweka kopo katika mzigo wa ndugu yake. Kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hakika nyinyi ni wezi.
Yusuf alitaka kumtenga Bin-yamin na ndugu zake na kubaki naye, lakini hakuwa na njia ila kufanya ujanja. Katika sharia ya watu wa Ya’qub ni mwizi kufanywa mtumwa. Ndio watumishi wakaweka chombo cha kupimia kwenye mzigo wa Bin-yamin, kwa amri ya Yusuf. Akanadi mnadi kuwa nyinyi wana wa Ya’qub! Ni wezi, kwa hiyo msiendelee na msafara hadi tuangalie mambo yenu.
Wakashangaa watoto wa Ya’qub kwa mshtukizo huu.
Wakasema na hali wamewaelekea: Mmepoteza nini?
Walisema hivi wakiwa na yakini kuwa hawana hatia yoyote. Na hii ni mara yao ya kwanza kusikia tuhuma hii.
Wakasema
watumishi wa Yusuf:
Tumepoteza kopo la mfalme na atakayelileta atapata shehena nzima ya ngamia na mimi ni mdhamini.
Mdhamini huyu ndiye aliyewaambia nyinyi ni wezi, kama walivyosema wafasiri, na akadhamini kwa sharti ya kuwa mtu aliye na hicho chombo akirudishe yeye mwenyewe.
Aya hii inaingia kwenye milango miwili ya Fiqh: Jaala, ambayo ni kutangaza zawadi kwa atakayeleta kilichopotea na Dhamana ambayo ni kutekeleza ahadi; kama vile kauli ya alisema: ‘Na mimi ni mdhamini.’ Yaani nadhamini kutekeleza ahadi ya shehena ya ngamia, Kuna hadithi isemayo: “Mdhamini ni mwenye kugharimika.”
Wakasema
watoto wa Ya’qub:Wallahi mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya ufisadi katika nchi hii wala sisi sio wezi.
Walibishana wakajadiliana na kuleta hoja za kutokuwa na hatia na usafi wao; miongoni mwa waliyoyasema ni: Vipi mnatutuhumu na mnajua nasabu yetu na sera yetu katika safari yetu ya kwanza na hii ya pili kwamba hatukuja kufanya ufisadi au hiyana; isipokuwa tumekuja kuwanunulia chakula watu wetu.
Kwenye tafsiri nyingi imeelezwa kuwa watoto wa Ya’qub, kwenye safari yao ya kwanza, walipokuta bidha zao zimerudishwa walidhani kuwa zimesahaulika, kwa hiyo hawakuzitumia, bali walizirudisha Misr. Kwa hiyo wakawa mashuhuri kwa wema na uamnifu wao.
Kauli hii ya wafasiri haiku mbali; bali inaashiria kauli ya watoto wa Ya’qub: Wallah mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii
Unaweza kuuliza
: Imekuwaje kwa Yusuf kufanya njama hizi za kuwaelekezea tuhuma ndugu zake na hali anajua kuwa hawana hatia?
Jibu
: Kwanza, tukio hili ni maalum, lina sababu zake, haifai kulipima na matukio mengine. Pili, aliyelengwa na tuhuma za wizi ni Bin-yamin, ndugu wa Yusuf kwa baba na mama, na hilo lilikuwa kwa makubaliano yao na kuridhika kwake, kwa hekima iliyotaka hivyo; wakati huohuo hilo halipingi msingi wowote katika misingi ya sharia; kama vile kuhalalisha haramu au kuharamisha halali.
Zaidi ya hayo, tendo la watoto wa Ya’qub la kumtoa Yusuf kwa baba yake na kumtupa kisimani kwa lengo la kumuua ni zaidi ya wizi.
Swali la pili
: Vipi Yusuf kumtenganisha nduguye na baba yake na kumzidishia baba yake majonzi juu ya majonzi?
Jibu
: Kila alilolifanya Yusuf lilikuwa kwa maslahi ya ndugu yake na baba yake; akiwa na uhakika kuwa baba yake atamkubalia na hata kumshukuru atakapojua uhakika wake. Na lilifanyika hilo. Kimsingi ni kuwa mambo hupimwa kwa matokeo yake sio kwa mfumo wake. Katika hali nyingine mitume hawatuhumiwi katika upande wa haki.
Wakasema: “Malipo yake yatakuwa ni nini ikiwa nyinyi ni waongo?”
Watumishi waliwaambia watoto wa Ya’qub ili waseme wenyewe kwamba mwizi atachukuliwa mateka au mtumwa, kama malipo ya tendo lake hilo. Ili iwe ni hoja juu yao pale Yusuf atakapomchukua ndugu yake.
Wakasema: “Malipo yake ni yule ambaye litaonekana katika mzigo wake, basi huyo ndiye malipo yake, Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.
Kusema ‘basi huyo ndiye malipo yake’ ni kuzidisha ufafanuzi; sawa na kusema: malipo ya muuaji ni kuuliwa, hayo ndiyo malipo yake.
Ndugu wa Yusuf walisema hiyo ndiyo sharia yetu, ambaye mtamkuta nalo mtamchukua mtumwa au mateka. Walisema hivyo wakiwa na uhakika kuwa wao hawana hatia
Basi akaanza na mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake; kisha akalitoa katika mzigo wa ndugu yake.
Mtafutaji alianza na mizigo yao kabla ya ndugu yao madogo, ili kuificha hila. Mpaka alipoishia kwenye mzigo wa Bin-yamin akalitoa na akawaonyesha; wakapigwa na butwa na wakawa na wakati mgumu, lakini ni wapi haya na waliyomfanyia Yusuf katika giza la shimo akiwa peke yake?
Hivyo ndivyo tulivyomfanyia hila Yusuf.
Yaani tulimpa wahyi wa mpango huu, ili ndugu zake waseme wenyewe, kuwa waziri amchukue nyara au mtumwa. Imeitwa hila kwa sababu dhahiri yake sio hali halisi; na ilijuzu kisharia, kwa sababu haikuhalalisha haramu wala kuharamisha halali.
Hakuweza kumchukua ndugu yake katika sharia ya mfalme.
Yaani sharia na hukumu ya mfalme. Maana ni kuwa lau si mipango hii ingelikuwa uzito kwa Yusuf kumchukua ndugu yake, kwa sababu sharia ya mfalme wa Misr sio kuchukua mateka, bali ni kumfunga au kupigwa, na Yusuf hakutaka kumdhuru ndugu yake. Hayo ndio makusudio ya kauli yake:
Isipokuwa alivyotaka Mwenyezi Mungu.
Kwa ufupi ni kuwa hekima ilikuwa ni kutosema Yusuf kuwa yule ni ndugu yake na wakati huo huo asipatwe na sharia ya mfalme ya kufungwa au kupigwa; bali apatwe na hukumu ya watu wa Ya’qub.
Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao Kwa elimu na utume kama tulivyomfanyia Yusuf juu ya ndugu zake.
Na juu ya kila mwenye elimu yuko ajuaye zaidi
mpaka ishie kwa aliye juu zaidi.
Hiyo ni ishara kuwa ndugu wa Yusuf walikuwa ni maulama, lakini Yusuf alikuwa na elimu zaidi na mkamilifu zaidi.
قَالُوا إِن يَسْرِقْ فَقَدْ سَرَقَ أَخٌ لَّهُ مِن قَبْلُ فَأَسَرَّهَا يُوسُفُ فِي نَفْسِهِ وَلَمْ يُبْدِهَا لَهُمْ قَالَ أَنتُمْ شَرٌّ مَّكَانًا وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا تَصِفُونَ ﴿٧٧﴾
77. Wakasema: Kama ameiba, basi ndugu yake pia ameiba zamani.” Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwadhihirishia; akasema: “Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi; na Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayoyasema.
قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ إِنَّ لَهُ أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا فَخُذْ أَحَدَنَا مَكَانَهُ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٧٨﴾
78. Wakasema: “Ewe mheshimiwa! Hakika anaye baba mzee sana, Kwa hiyo mchukue mmoja wetu badala yake, Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
قَالَ مَعَاذَ اللَّـهِ أَن نَّأْخُذَ إِلَّا مَن وَجَدْنَا مَتَاعَنَا عِندَهُ إِنَّا إِذًا لَّظَالِمُونَ ﴿٧٩﴾
79. Akasema: “Mwenyezi Mungu apishe mbali kumchukua ila yule tuliyekuta mali yetu iko kwake, Hivyo basi tutakuwa ni wenye kudhulumu.”
فَلَمَّا اسْتَيْأَسُوا مِنْهُ خَلَصُوا نَجِيًّا قَالَ كَبِيرُهُمْ أَلَمْ تَعْلَمُوا أَنَّ أَبَاكُمْ قَدْ أَخَذَ عَلَيْكُم مَّوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ وَمِن قَبْلُ مَا فَرَّطتُمْ فِي يُوسُفَ فَلَنْ أَبْرَحَ الْأَرْضَ حَتَّىٰ يَأْذَنَ لِي أَبِي أَوْ يَحْكُمَ اللَّـهُ لِي وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ ﴿٨٠﴾
80. Walipokata tamaa naye walikwenda kando kunong’ona. Akasema mkubwa wao: “Je, hamjui kuwa baba yenu amechukua ahadi kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Na hapo zamani mlikosea katika Yusuf? Basi sitaondoka nchi hii mpaka baba yangu aniruhusu au Mwenyezi Mungu anihukumie; naye ni mbora wa mahakimu.
KAMA AMEIBA BASI NDUGUYE PIA ALIIBA ZAMANI
Aya 77-80
MAANA
Wakasema: Kama ameiba, basi ndugu yake pia ameiba zamani.
Ndugu zake Yusuf ndio waliosema hivyo, wakimkusudia Bin-yamin na Yusuf. Hizo ni tuhuma walizombadika nazo Yusuf. Hakuna ishara yoyote katika Aya yoyote kwamba Yusuf kuanzia utotoni aliwahi kuiba yai au kuku au kuiba sanamu ya babu yake mzaa mama yake, au mkanda wa shangazi yake n.k.
Lakini Qur’an imesajili waziwazi uwongo wa ndugu zake Yusuf, pale waliposema kuwa ameliwa na mbwa mwitu. Kuongezea hasadi na chuki yao iliyowapelekea kufanya waliyoyafanya. Kwa hiyo basi wao ni waongo katika kumnasibishia kwao Yusuf wizi alipokuwa mtoto.
Kusema hivi, ingawaje ni natija ya uchambuzi, lakini ndio mantiki ya sawa, au angalau ndio kauli ya karibu na maana.
Wafasiri wameichukulia kauli ya nduguze Yusuf kuwa ni ya kweli, kama kwamba uwongo unastahili. Wakawa wanafanya utafiti wa hicho alichokiiba Yusuf. Kuna aliyesema kuwa aliiba yai akampa mwenye njaa; mweingine akasema ni kuku.
Wa tatu akasema aliiba sanamu la babu yake mzaa mama yake na akalivunja. Wa nne akasema kuwa alikuwa akilelewa na shangazi yake, bint wa Is-haq, alipokuwa na baba yake, akataka kumchukua, kwa hiyo akamtuhumu kuiba mkanda wa mume wa shangazi yake ili abaki naye kama mtumwa; kwa vile adhabu ya mwizi ilikuwa ni kufanywa mtumwa.
Wafasiri wengi wako juu ya kauli hii ya mwisho, Lakini jambo la ajabu ni kuwa hakuna hata mmoja wao aliyezinduka kuwa hukumu ya watoto sio ya wakubwa katika sharia zote, Ajabu zaidi ni kauli ya baadhi ya Masufi kwamba ndugu zake Yusuf walimtuhumu na wizi wa kuiba roho ya baba yake!
Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwadhihirishia.
Aliapuuza maneno yao kwa upole na ukarimu; kama asemavyo mshairi: Nampitia mlaumu akinitusi Namsamehe nasema hanihusi
Akasema: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi.
Haya aliyasema kisirisiri, kwa dalili ya kauli yake: “Wala hakuwadhihirishia.”
Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayoyasema ya kuninasibishia wizi mimi na ndugu yangu, kwamba ni uwongo na uzushi.
Wakasema: Ewe mheshimiwa! Hakika anaye baba mzee sana, Kwa hiyo mchukue mmoja wetu badala yake, Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
Baada ya mambo kudhihirika na kwamba hukumu ni kuchukuliwa mtumwa ndugu yao Bin-yamin, walielekea kutaka kuhurumiwa kwa kusamehewa au kuchukuliwa fidia ya mmoja wao badala yake. Walibembeleza sana kwa kutumia wema wa Yusuf na uzee wa baba yao na cheo chake na jinsi anavyompenda sana mwanawe Bin-yamin.
Walifanya hivyo sio kwa kumpenda ndugu yao, bali ni kujitoa kwenye lawama kutokana na ahadi waliyoichukua kwa baba yao.
Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumchukua ila yule tuliyekuta mali yetu iko kwake, Hivyo basi tutakuwa ni wenye kudhulumu.
Yusuf alikataa ombi lao na matarajio yao na akashikilia kumchukua ndugu yake, kwa jambo ambalo Mwenyezi Mungu alitaka kulitimiza baada ya kupita mtihani na balaa.
Yusuf alitumia ibara ya ndani sana na yenye hekima ya kumwepusha ndugu yake na wizi, alposema: Yule tuliyekuta mali yetu iko kwake, ambapo ndugu zake walifahamu: ‘aliyeiba mali yetu.’ Na tofauti hapo ni kubwa sana.
Walipokata tamaa naye walikwenda kando kunong’ona.
Baada ya kukata tamaa watoto wa Ya’qub ya kumpata ndugu yao walijitenga ili washauriane jinsi watakavyomwambia baba yao.
Akasema mkubwa wao: Je, hamjui kuwa baba yenu amechukua ahadi kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa makusudio ya mkubwa wao ni mkubwa kiakili si kimiaka. Wengine wakasema ni kiakili na kimiaka.
Kauli hii ndiyo inayokuja haraka akilini, Vyovyote iwavyo ni kwamba mkubwa huyo aliwaambia ndugu zake mtafanyaje mtakapofika kwa baba yenu bila ya Bin-yamin nanyi mliapa kuwa mtamrudisha?
Na hapo zamani mlikosea katika Yusuf?
Anaashiria walivyomtupa shimoni na baba yao alivyokuwa mkali.
Basi sitaondoka nchi hii mpaka baba yangu aniruhusu au Mwenyezi Mungu anihukumie; naye ni mbora wa mahakimu.
Mkubwa wao aliamua abakie karibu na ndugu yake kwa kumwonea haya baba yake na kwamba hataondoka kwenye nchi aliyo Bin-yamin mpaka apewe idhini na baba yake au apate faraja yoyote, kutoka kwa Mwenyezi Mungui hata kama ni mauti. Muda haukuwa mrefu ikaja faraja kwa wote; kama yatakavyokuja maelezo.
ارْجِعُوا إِلَىٰ أَبِيكُمْ فَقُولُوا يَا أَبَانَا إِنَّ ابْنَكَ سَرَقَ وَمَا شَهِدْنَا إِلَّا بِمَا عَلِمْنَا وَمَا كُنَّا لِلْغَيْبِ حَافِظِينَ ﴿٨١﴾
81. Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ewe baba yetu! Hakika mwanao ameiba, na hatutoi ushahidi ila tunayoyajua; wala hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibuu.
وَاسْأَلِ الْقَرْيَةَ الَّتِي كُنَّا فِيهَا وَالْعِيرَ الَّتِي أَقْبَلْنَا فِيهَا وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٨٢﴾
82. Na waulize watu wa mji tuliokuwako na msafara tuliokuja nao, Na hakika sisi tunasema kweli.
قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًا فَصَبْرٌ جَمِيلٌ عَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٨٣﴾
83. Akasema: “Bali nafsi zenu zimewashawishi jambo fulani. Basi subira ni njema. Huenda Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja, Hakika Yeye ni Mjuzi, Mwenye hekima.
وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٨٤﴾
84. Na akajitenga nao, na akasema: Oh! Masikitiko yangu juu ya Yusuf! Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni naye akawa anaizuia.
قَالُوا تَاللَّـهِ تَفْتَأُ تَذْكُرُ يُوسُفَ حَتَّىٰ تَكُونَ حَرَضًا أَوْ تَكُونَ مِنَ الْهَالِكِينَ ﴿٨٥﴾
85. Wakasema: “Wallahi huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika wenye kuaangamia.”
قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٨٦﴾
86. Akasema: “Majonzi yangu na huzuni yangu ninamshtakia Mwenyezi Mungu Na ninajua kwa Mwenyezi yale msiyoyajua.
يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِن يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾
87. Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye wala msikate tamaaa na faraja ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri.
HATUTOI USHAHIDI ILA TUNAYOYAJUA
Aya 81-87
MAANA
Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ewe baba yetu! Hakika mwanao ameiba na hatutoi ushahidi ila tunayoyajua; wala hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu.
Hii ni kauli ya mkubwa wao akiwausia ndugu zake kuwa waseme ukweli kwa baba yao. Wampe habari kuwa wamewaona watumishi wa waziri wakitoa chombo cha kupimia cha mfalme katika mzigo wa Binyamin, Na kwamba waziri aling’ang’ania kumchukua, Hayo ndiyo tuliyoyashuhudia.
Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyo nyuma ya hayo, Na lau tungelijua ghaibuu, basi tusingemchukua wala kukupa ahadi ya kurudi naye, Tumefanya bidii sana. Tunaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na kwako.
Na waulize watu wa mji tuliokuwako.
Yaani waulize watu wa Misr, jambo hili la wizi limeenea kwao.
Na msafara tuliokuja nao.
Yaani vile vile uliza msafara tuliokuja nao kutoka Misr ambao uko jirani yako katika nchi ya Kanaan.
Na hakika sisi tunasema kweli
kwa haya tunayokusimulia. Mara hii walikuwa wakisema kwa kujiamini kwa sababu walikuwa na uhakika wa wanayoyasema kinyume na mara ya kwanza walipokuja na damu ya uwongo kwenye kanzu ya Yusuf.
Akasema: Bali nafsi zenu zimewashawishi jambo fulani.
Walipomweleza baba yao aliwaambia mmefanyia vitimbi kama mlivyomfanyia ndugu yake, Yusuf.
Wafasiri wamejiuliza kuwa vipi Ya’qub aliwatuhumu wanawe kwa vitimbi kabla ya kuthibitisha na yeye ni mtume ma’asum?
Kisha wakajbu kwa njia nyingi zisizotegemea msingi wowote. Njia nzuri zaidi waliyoitaja ni ile kuwa makusudio ya Ya’qub ni kuwa nafsi zenu zimewapa picha ya kuwa Bin-yamin ni mwizi na hali yeye si mwizi.
Tuonavyo sisi ni kuwa Ya’qub aliwatuhumu na vitimbi kwa kuchukulia walivyomfanyia Yusuf, lakini yeye hakuchukulia moja kwa moja, kwa kukosa dalili ya uwongo wao. Vile vile hakuwachukulia hatua yoyote kwa dhana, Kwa sababu dhana haitoshelezi kitu.
Hiyo haipingani na cheo cha utume. Kwa sababu mtume hajui ghaibu, naye ni kama mtu mwingine anadhania na kuchukulia uwezekano. Tofauti ni kuwa kwake yeye dhana haina athari yoyote, kama afanyavyo asiyekuwa ma’sum.
Subira ni njema.
Yaani ‘subira yavuta heri, Haya aliwahi kuyasema zamani alipopotea Yusuf na sasa anayasema kwa Bin-yamin.
Huenda Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja.
Yaani Yusuf, Bin-yamin na kaka yao aliyebakia Misr karibu na ndugu yake. Neno ‘huenda‘ ni mwangaza wa matumaini; hasa likiwa linatoka kwa anayeamini ghaibu kikwelikweli; kama mitume na wasadikishao. Katika Nahjulbalagha imeelezwa: “Haiwi kweli imani ya mja mpaka yawe yaliyo kwa Mwenyezi Mungu ni ya kutegemewa zaidi kuliko yaliyo mikononi mwake” Kuna Hadith nyingi zenye maana haya.
Hakika yeye ni Mjuzi Mwenye hekima.
Anajua huzuni yangu na machungu yangu na anapanga mambo kwa hekima yake.
Na akajitenga nao, na akasema: Oh! Masikitiko yangu juu ya Yusuf!
Alijitenga na watu ili aomboleze peke yake, ambapo huzuni na kilio kilizidi kwa kumkosa mwanawe, Bin-yamin (Benjamin)na macho yake yakawa meupe kwa huzuni.
Yaliathirika kwa sababu ya kulia.
Naye akawa anaizuia.
Yaani anameza uchungu kwa mwili na mishipa yake.
Wakasema: Wallahi huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika wenye kuaangamia.
Yaani wanawe walimwambia bado unamkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au ufe bure, kwa sababu Yusuf amekwenda harudi tena.
Akasema: Majonzi yangu na huzuni yangu ninamshtakia Mwenyezi Mungu,
sio kwenu kwa sababu ni udhalili na usafihi kumshtakia ambaye haondoi dhara. Imam Ali
anasema:“Allah Allah! Na kumshatakia ambaye hawezi kuondoa mashaka yenu, wala hawezi kupunguza kwa rai yake yale mliyokwishayapitisha”
Na ninajua kwa Mwenyezi yale msiyoyajua.
Yaa’qub ameteseka kwa kumkosa Yusuf, lakini wakati huo huo bado anamtegemea Mwenyezi Mungu na kumwekea dhana nzuri wala hakati tamaaa na rehema yake huku akiamini kuwa mwisho wa subra ni faraja (baada ya dhiki faraja); kama ilivyofahamisha kauli yake kuwaambia wanawe “Wala msikate tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu.”
Tukiunganisha kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu katika ndoto ya Yusuf udogoni mwake natija ni kuwa Yaa’qub ana matumaini ya uhai wa Yusuf hadi atakapokuwa mkubwa, lakini hajui yuko wapi na ana hali gani, Yuko utumwani au kwenye uhuru, Huo ndio ulikuwa wasiwasi wake.
HAKUNA KUNGOJA MEMA YAJE YENYEWE WALA MABAYA
Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye wala msikate tamaaa na faraja ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri.
Nendeni mkatafute wala msikate tama, Amekutanisha matumaini na kutenda. Maana yake ni kuwa. Ikiwa hakutakuwa na matendo basi Aya itakwenda kinyume; na uvivu utaambatana na kukata tamaa na yatakuwa matarajio bila ya kufanya kitu ni ujinga na upumbavu. Neno tafuteni linawajibisha kutenda kwa hisia zote dhahiri na batini.
Ndivyo alivyo mwenye akili akitokewa na janga lolote anajitahidi kuondoa visababishi vyake, ni sawa viwe ni ufisadi au uzembe.
Na anapopatwa na mazuri huhofia asijisahau akapetuka mpaka kwa utajiri au cheo kikamletea kiburi. Kwa hiyo hujikinga kwa takua:
فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٩٩﴾
“Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.” Juz. 9 (7:99).
Kwa ufupi ni kuwa mwenye kutaraji mabaya ni yule asemaye hakuna faida ya kujisumbua, na mvivu ni yule mwenye kutaraji mazuri yaje yenyewe.