5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
Sura Ya Kumi Na Tatu: Surat Ar-Ra’d
Imeshuka Madina, ina Aya 43
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
المر تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ وَالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
1. Alif Laam Raa. Hizo ni Aya za Kitabu. Na uliyoteremshiwa kutoka Mola wako ni haki lakini watu wengi hawaamini.
HIZO NI AYA ZA KITAB
Aya 1
MAANA
Alif Laam Raa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 mwanzo wa Sura Baqara.
Hizo ni Aya za Kitabu.
Yaani Aya za Sura hii ni katika Qur’an Tukufu. Lengo la kutoa habari hii ni kubainisha kuwa sura hii ni haki kwa sababu ni katika Qur’an. Kwa vile Qur’an ni haki basi nayo ni haki. Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ni haki.
Hapa linakuja swali
: Kuna dalili gani kuwa Qur’an ni haki?
Jibu
: utalipata Juz. 1 (2:23-25) Imam Ali
anasema:“Hakika Qur’an dhahiri yake ni safi na undani wake ni wa kina, maajabu yake hayaishi wala giza haliondoki ila kwayo.”
Lakini watu wengi hawaamini
Qur’an wala kauli nyingine ya haki na uadilifu ila yule anayeona heri yake ni heri ya watu na shari yake ni shari yao pia.
Mtu mmoja katika watu wa Mungu aliambiwa kuwa soko limeungua lakini duka lako halikuungua, akasema: Alhamdullilah. Kisha akatanabahi kuwa ameasi kwa kujitakia yeye binafsi heri kuliko watu wengine, akatubia dhambi yake na akaomba msamaha.
Mfano wa watu hawa ni wachache ambao wanawafikiria wengine, ndio aliowakudia Mwenyezi Mungu kwa kusema: ‘Lakini watu wengi hawaamini”.
اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى يُدَبِّرُ الْأَمْرَ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُم بِلِقَاءِ رَبِّكُمْ تُوقِنُونَ ﴿٢﴾
2. Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona; kisha akatawala kwenye Arshi na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliotajwa. Anayapanga mambo Anazipambanua ishara, ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Mola wenu.
وَهُوَ الَّذِي مَدَّ الْأَرْضَ وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنْهَارًا وَمِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ جَعَلَ فِيهَا زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٣﴾
3. Na yeye ndiye aliyeitandaza ardhi. Na akaweka humo milima na mito. Na katika kila matunda akafanya humo viwili viwilidume na jike. Huufunika usiku kwa mchana. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaofikiri.
وَفِي الْأَرْضِ قِطَعٌ مُّتَجَاوِرَاتٌ وَجَنَّاتٌ مِّنْ أَعْنَابٍ وَزَرْعٌ وَنَخِيلٌ صِنْوَانٌ وَغَيْرُ صِنْوَانٍ يُسْقَىٰ بِمَاءٍ وَاحِدٍ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الْأُكُلِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٤﴾
4. Na katika ardhi mna vipande vilivyokaribiana. na zipo bustani za mizabibu na mimea mingine na mitende ichipuayo kwenye shina na isiyochipua kwenye shina moja inayonyweshwelezwa maji yale yale Na tunaifanya bora baadhi yake kuliko mingine katika kula. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanotia akilini (mambo).
AMEINUA MBINGU BILA YA NGUZO
Aya 2-4
MAANA
Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona.
Yaani mnaziona hizo mbingu, Maana ni kuwa hakika Mwenyezi Mungu ameziinua mbingu kwa amri yake nazo zimeinuliwa hasa kama mnavyoziona bila ya nguzo.
Katika Mustadrak Nahjul-balagha imeelezwa kuwa Imam Ali
alizisifu mbingu kwa kusema:“Ameinua mbingu bila ya nguzo – yaani kihalisi na kidhahiri – na akaitandika ardhi hewani bila ya nguzo”.
Kisha akatawala kwenye arshi.
Hili ni fumbo kuwa yeye anamiliki ulimwengu na kupangilia mambo yake kwa elimu yake na hekima yake, kama alivyosema: ‘Anayepanga mambo.’ Jumla hii imekwishapita katika Juz. 8 (7:54) na katika Juz. 11 (10:3).
Na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliotajwa.
Kwa nidhamu, kama yaonavyo macho yetu na kwa lengo maalum kama zinavyotambua akili zetu.
Jua linapita kwenye falaki yake katika mwaka, na mwezi nao unapita kwenye falaki yake kwa muda wa mwezi mmoja. Vilikuwa hivyo tangu mamilioni ya miaka iliyopita na vitaendelea hivyo mpaka atakapotaka Mwenyezi Mungu.
Hakuna mwaka unaotofautiana na mwingine wala muda unaotofautiana na muda mwingine. Hii ni dalili mkataa ya kuweko mjuzi mwenye hekima. Ama sadfa inabatilishwa na nidhamu na kukaririka mambo.
Anayapanga mambo yote
bila ya kubakisha, yakiwemo kulitiisha jua na mwezi, kutuma mitume kuteremsha vitabu n.k.
Anazipambanua ishara,
Anabainisha dalili za kupatikana kwake, Kwa nini anafanya hivyo?
Ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Mola wenu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimwengu na akaupanga kwa ukamilifu katika njia zote. Akili iliyosalama inatambua mipangilio hii na kupata dalili kwayo ya kupatikana mzingatiaji mwenye hekima na uweza wake wa kurudisha viumbe.
Kwa sababu mwenye kuweza kuuleta ulimwengu uliokuwa hauko na akaupangilia pamoja na vilivyomo ndani yake, zikiwemo nyota na sayari nk, kwa mpangilio wa kiuhakika, basi bila shaka atakuwa na uwezo zaidi wa kuukusanya pamoja baada ya kutawanyika.
Ukithibiti kwa akili uwezo wa kuurudisha, na mkweli mwaminifu akautolea habari kwa wahyi, basi kutokea kwake ni kwa lazima.
Baada Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja mbingu ametaja ardhi na lengo ni moja - kuwatanabaisha walioghafilika kwenye dalili za kiulimwengu za kupatikana Mwenyezi Mungu na utukufu wake.
Na kwamba mwenye kuumba ulimwengu huu mkubwa pamoja na ardhi yake na mbingu yake anaweza kutuma mitume na kuteremsha vitabu, kufufua wafu.
Dalili hizo miongoni mwake ziko za mbinguni; kama vile kuinua mbingu bila ya nguzo, kulitiisha jua na mwezi n.k. Na nyingine ni za ardhini; kama zile alizoziashiria Mwenyezi Mungu kwa kauli zifuatazo:
1.Na yeye ndiye aliyeitandaza ardhi yaani aliyeitandika.
Mahali pengine Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ بِسَاطًا ﴿١٩﴾
“Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye wafanyia ardhi kuwa busati” (71:19)
وَالْأَرْضَ بَعْدَ ذَٰلِكَ دَحَاهَا ﴿٣٠﴾
“Na ardhi baada ya hayo akaitandika” (79:30)
Inavyoonyesha ni kwamba kutandazwa ardhi na kutandikwa pamoja na upana wake, hakuna uhusiano wowote na kuwa ardhi ni mviringo au ni bapa. Kwa sababu kitu kikiwa kikubwa sana, kama ardhi, kila upande wake unakuwa umeenea kwa upana na urefu, hata kama kiko mviringo.
Kwa hiyo basi Aya haizuii kuwa ardhi ni mviringo, jambo ambalo halina shaka. Razi anasema katika kufasiri Aya hii: “Hakika imethibiti, kwa dalili kwamba, ardhi ni tufe na ardhi ni kitu kikubwa na tufe likiwa ni kubwa sana basi kila sehemu yake inaonekana kama bapa.”
Wataalamu wa Kiyunani (kigiriki) katika enzi za Aristatle, waliafikiana kuwa ardhi ni mduara, lakini wakasema kuwa imetulia.
2.Na akaweka humo milima.
Neno milima limefasiriwa kutoka na neno Rawasi lenye maana ya kila kitu kilichothibiti mahali, lakini neno hili limetumika zaidi kwa milima, kiasi ambacho likitajwa tu bila ya nyongeza, inafahamika kuwa ni milima.
Hekima ya kupatikana hiyo milima ni utulivu wa ardhi na uthabiti wake, Mwenyezi Mungu anasema: “Je, hatukuifanya ardhi kuwa ni tandiko na milima kuwa ni vigingi?” (78:7).
3.Na mito.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekutanisha kutaja milima na mito kwa sababu mito inachimbuka kutoka humo milimani. Anasema:
وَجَعَلْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ شَامِخَاتٍ وَأَسْقَيْنَاكُم مَّاءً فُرَاتًا ﴿٢٧﴾
“Na tukaweka humo milima mirefu na tukawanywesha maji tamu” (77:27)
4.Na katika kila matunda akafanya humo viwili viwili–dume na jike.
Kila aina ya matunda ina dume na jike katika aina zake kwa dhahiri, kama vile mtende dume mtende jike, au kwa undani, kama mimea mingine.
Sheikh Al-Maraghi, katika tafsiri yake, anasema: “Imethibitisha elimu hivi sasa kwamba mti na mmea wowote hauzai matunda isipokuwa kwa ushirikiano baina ya wa kike na wa kiume. Aghlabu mbegu zinakuwa katika mti mmoja kama ilivyo miti mingi, au katika miti miwili tofauti, kama ilivyo kwa mtende.”
Katika jarida la Al-ulum la Lebanon toleo la Juni 1967 kwenye kichwa cha maneno “Vipi uhai unakuwa katika vitu”, imeelezwa kuwa vidudu vinachukua mbegu za uzazi kwenye mwili wake kupeleka kwenye makole ya maua bila ya kukosea, na kwamba ndege wanachukua mbegu za uzazi za yungi yungi kwenye midomo yao. Hakika ni muujiza.
Katika vita kuu vya ulimwengu vya pili walifika wapiganaji huko Corse, zaituni ikapata magonjwa na matunda yakapungua. Amerika ikataka kusaidia kutatua tatizo hilo, Kwa hiyo wakanyunyizia miti dawa ya DDT. Vidudu vya maradhi vikafa, lakini vikafa na vidudu vingine. Katika mwaka uliofuatia natija ikawa ni kutopatikana chochote! Si zaituni si limao wala lozi.
Kwa hiyo inatubainikia kuwa mimea haiwezi kuzaa matunda isipokuwa kwa kukutana mbengu za kike na za kiume.
5.Huufunika usiku kwa mchana.
Imepita tafsiri yake katika Juz. 8 (7:54).
Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaofikiri.
Katika ulimwengu huu ambao unakwenda kulingana na kanuni thabiti zisizotetereka kwa hali yoyote ile. Lau si uthabiti wake, isingeliwezekana kwa wataalamu kuuchunguza na kuuelewa. Ilivyo ni kwamba linalodumu linapinga sadfa. Na kwa ajili hii wataalamu wengi wa maumbile wameamini kuweko Mungu.
Na katika ardhi mna vipande vilivyokaribiana.
Ardhi imeungana, lakini kuna sehemu kadhaa zinazotofautiana, kuna tambarare, milima na mabonde. Pia kuna udongo mgumu na mchangatifu, changarawe na utelezi, weusi na weupe n.k. Siri ya hilo ni amri ya Mwenyezi Mungu na upangiliaji wake katika kuumba.
Na zipo bustani za mizabibu na mimea mingine na mitende ichipuayo kwenye shina,
Ni mitende ya aina moja.
Na isiyochipua kwenye shina moja
ni ile mitende inayotokana na mashina tofauti. Amehusisha kutaja mizabibu na mitende kwa sababu ndiyo matunda yanayopatikana sehemu nyingi au ndio yenye chumo na pengine ndiyo iliyokuwa muhimu wakati huo. Hilo linafahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا رَّجُلَيْنِ جَعَلْنَا لِأَحَدِهِمَا جَنَّتَيْنِ مِنْ أَعْنَابٍ وَحَفَفْنَاهُمَا بِنَخْلٍ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمَا زَرْعًا ﴿٣٢﴾
“Na wapigie mfano wa watu wawili: Mmoja wao tulimjalia vitalu viwili vya mizabibu na tukavizungushia mitende na kati yake tukatia mimea ya nafaka” (18:32)
Inanyweshwelezwa maji yale yale
; kama vile mvua, kisima au mto. Pia sehemu ni moja kwa kukarubiana, lakini matunda yanatofautiana kirangi, ukubwa, harufu na hata ladhaa. Siri ya hilo ni upangiliaji wake Mwenyezi Mungu na hekima yake.
Na tunaifanya bora baadhi yake kuliko mingine
katika kula pamoja na kuwa nyezo za kumea kwake ni aina moja.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotia akilini (mambo).
Yaani tofauti hii inayopatikana katika nyezo za aina moja, yakiwemo maji na hewa, ni dalili wazi ya kuweko mpangiliaji mambo vizuri, kwa yule ambaye haamini kitu ila baada ya kufikiri na kutia akilini.
Miongoni mwa kauli ya Imam Ali
:“Hakuna elimu kama kufikiri wala hakuna fahari kuliko kunyeyekea”
.
SAYYID AFGHANI NA WANAOMKANA MUNGU
Ufafanuzi mzuri wa Aya hii kwa ujumla ni majibu ya Sayyid, Jamaluddin Al-Afghani, kwa wale wanaokana kuweko Mwenyezi Mungu anasema: “Akiulizwa Darwin kuhusu miti iliyoko katika misitu wa India na mimea inayozaliana humo tangu zama za kale sana ambazo historia haijui muda wake, isipokuwa kudhania tu.
Mashina yake yote yako katika uwanja mmoja matawi yake yote yanakwenda kwenye anga moja, Sasa ni kitu gani kinachofanyika mpaka mmoja ukatofautiana na mwingine katika umbile lake, majani yake, kimo chake na ukubwa.
Vile vile maua yake, matunda yake na hata ladha yake? Ni, kitu gani cha nje kilichoathiri mpaka ikapatikana tofauti katika makuzi ya aina moja, maji na hewa ya aina moja? Nadhani hawezi kupata jibu la hayo
Akiulizwa kuhusu hawa samaki wa mto Oural na wa bahari ya Qazwini (Caspian sea) wanashirikiana katika vyakula, lakini wanatofautiana kabisa kimaumbile, je kuna sababu gani ya kutofautiana huku? Sioni kama ataweza kuwa na majibu isipokuwa kushindwa”
Unaweza kuuliza kuwa
: Darwin anaweza kumjibu Sayyid Afghani kwamba wataalamu wa mimea wanajua sababu ya kutofautiana huku na wanaweza kuifichua kwa kila anayetaka na kupendelea; Kwa hiyo basi, hakuna dharura, katika hali hii, kulazimika kuweko mpangiliaji?
Jibu
: Tuchukulie kuwa wataalamu wa mimea wanajua sababu ya hilo, lakini ujuzi wao utakuwa na kiwango cha kujua sababu ya karibu ya hilo.
Na kama wakiulizwa sababu ya mbali iliyosababisha hii ya karibu hawatapata isipokuwa moja ya sababu mbili: Ama sadfa au kuweko mpangiliaji mwenye hekima. Sababu ya kwanza itakuwa batili kwa sababuu sadfa haikaririki wala kudumu, Kwa hiyo itabaki sababu ya pili.
Mara kadhaa tumebainisha kuwa ni desturi ya Qur’an kutegemeza matukio yote ya kimaumbile kwenye sababu yake ya kilimwengu.
Hilo ni katika kukitegemeza kitu kwa mtendaji wake wa kwanza, kwa lengo la kukumbusha kuweko Mwenyezi Mungu na kwamba yeye ndiye muumba wa ulimwengu wote pamoja na ardhi yote na mbingu yake.
Unaweza kusema tena
: Wakana Mungu nao wanaweza kuuliza: Kuna sababu gani ya kuweko mpangiliaji mambo?
Jibu
: Hakika swali hili sio la msingi kwa sababu kuweko mpangiliaji hakuna sababu na kwamba yeye ndiye msabibishaji sababu. Kuuliza sababu ya kuweko msababishaji ni sawa na kuuliza: Nina ni aliye muumba Mungu baada ya kufaradhia kuwa yeye ni muumba sio muumbwa.
Au kuuliza sababu ya kusadikisha jicho lilichokiona na sikio lilichokisikia na huku tunaamini kuwa hiyo ni hoja mkataa ya kila shaka na kila shubha.
وَإِن تَعْجَبْ فَعَجَبٌ قَوْلُهُمْ أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ وَأُولَـٰئِكَ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٥﴾
5. Na kama ukistaajabu basi cha ajabu ni usemi wao: ‘Ati tutakapokuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya?’ Hao ndio waliomkufuru Mola wao na hao ndio watakokuwa na minyororo shingoni mwao na hao ndio watu wa motoni, Humo watadumu.
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ وَقَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِمُ الْمَثُلَاتُ وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ لِّلنَّاسِ عَلَىٰ ظُلْمِهِمْ وَإِنَّ رَبَّكَ لَشَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٦﴾
6. Wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa imepita kabla yao mifano. Na hakika Mola wako ni mwenye maghufira kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako ni mkali wa kuadhibu.
وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ إِنَّمَا أَنتَ مُنذِرٌ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ ﴿٧﴾
7. Na husema wale ambao wamekufuru: ‘Mbona hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake.’ Hakika wewe ni mwunyaji tu. Na kila kaumu ina wa kuwaongoza.
KWELI TUTAKUA KATIKA UMBO JIPYA?
Aya 5-7
MAANA
Na kama ukistaajabu basi cha ajabu ni usemi wao: ‘Ati tutakapokuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya?’
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
wasemaji ni washirikina waliokana utume wake. Maana ni kuwa ikiwa ewe Muhammad utashangazwa na ibada ya masanamu ya washirikina na kukanusha kwao utume wako, basi la kushangaza zaidi ni kukadhibisha kwao ufufuo.
Kwa sababu wao wanakubali kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Muumba wa ulimwengu, na mwenye kuweza hilo si anakuwa na uwezo zaidi wa kumrudisha mtu baada ya kufa kwake?
Hao ndio waliomkufuru Mola wao na hao ndio watakokuwa na minyororo shingoni mwao na hao ndio watu wa motoni, Humo watadumu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja neo ‘hao’ mara tatu kuelezea kwa ufasaha zaidi hasira zake na kuchukia kwake. Kauli yake: Hao ndio waliomkufuru Mola wao, inafahamisha kuwa Mwenye kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni muumba wa ulimwengu inamlazimu yeye, kwa hali yoyote, kuamini kuwa yeye ni muweza wa kuwafufua walio makaburini. Atakayepinga hilo atakuwa moja kwa moja amemkufuru Mwenyezi Mungu atake asitake.
Mwenye kuchanganya imani ya Mungu na kushindwa kufufua watu, atakuwa amechanganya mambo mawili yanayopingana. Washirikina wamepinga ufufuo, kwa vile, kulingana na madai yao, Mwenyezi Mungu hawezi; kama inavyojulisha kauli yao “Ati tutakapokuwa…” Kwa hiyo, ilivyo hasa, ni kuwa wao wanampinga Mwenyezi Mungu kwa ndimi zao.
WANAOAMINI MAADA NA MAISHA BAADA YA MAUTI
Wanaoamini maada wanakana kuweko Mwenyezi Mungu, sana sana wanapinga maisha baada ya mauti. Dalili yao ni moja tu haibadiliki wala haigeuki. Nayo ni kuwa kila linaloweza kuhisiwa na kushuhudiwa inapasa kuliamini na kila lisiloweza kuhisiwa inapasa kulikana na kulipinga.
Kwa hiyo, kwao, hisia ya dhahiri peke yake ndiyo dhahiri na ndiyo batini, ndiyo ya mwanzo na ya mwisho; kama wanavyosema. Vipi wataamini Bustani (Pepo) nao hawajala matunda yake, vipi wakubali kuwa kuna Jahannam na moto wake haujawafikia?
Sisi nasi, kwa upande wetu, tunauliza hivi: Mmepata wapi elimu au imani ya kuwa hisia za dhahiri pekee ndiyo njia ya haki na hali halisi, na kwamba mengineyo ni upuuzi? Mkisema hayo mmeyajua kupitia hisia, tutasema:
Sisi pia tunazo hisia na hatujamuona mwingine zaidi yenu akisema kuwa msiamini isipokuwa hisia. Ikiwa mtasema mmejua hilo kwa njia nyingine isiyokuwa hisia, basi mtakuwa mmejipinga wenye kwa kuamini kisichoshuhudiwa na hisia.
Mnamo mwaka 1962 nilitunga kitabu kuwajibu wanaoamini maada, kwa jina Falsafatul-Mabda’ (falsafa ya misingi), Kisha baadae nikasoma mambo mengi kuhusu wanavyoamini wa maada na majibu yao; miongoni mwayo ni:
1. Kwa mujibu wa wanaoamini maada ni lazima kutokuweko tofauti yoyote baina ya mtu aliye na miujiza na vidudu duni vinavyotokana na uchafu kwa vile wote hao ni watoto wa sharia ya sadfa na maumbile pofu yasiyokuwa na mipangilio yoyote
2. Wataalamu wamepata katika ubongo wa binadamu nyuzi milioni elfu 14 zimefumwa na kupangiliwa vizuri sana kwa namna ambayo wahandisi wakuu wote hawawezi; kiasi ambacho unyuzi mmoja tu ukienda kombo basi mtu hatakuwa na utambuzi au atachanganyikiwa, sawa na umeme ukiharibika moja ya nyaya zake. Hakuna tafsiri ya hayo, kwa mwenye akili, isipokuwa kuweko mpangiliaji mwenye hekima asiyeweza kuonwa kwa jicho, kusikiwa na sikio, kuguswa kwa mkono, kunuswa na pua au kuonjwa kwa ulimi.
Kwa namna yoyote itakavyokuwa sadfa na muujiza, lakini haiwezi kufanya umeme; sikwambii kuunganisha nyuzi milioni elfu 14 zilizopangiliwa, kiufundi na kuwekwa kwenye chombo kimoja kwa idadi ya vichwa na bongo za binadamu wote; tena waweze kuhisi na kutambua.
3. Waamini maada wanasema kuwa ubongo wa binadamu ni sawa na akili ya mashine. Zote mbili zimetokana na vitu vilivyosukwa na kupangwa kuweza kuleta athari.
Mtaalamu wa kifaransa, aitwaye Caussine, aliwajibu kwa kusema: Iwapo gari yangu ya zamani ikianza kutoa sauti mbovu kama mtu aliyepatwa na ugonjwa wa baridi yabisi, inawezekana niseme kuwa gari yangu ina baridi yabisi? Na kabureta inapotatarika wakati ninapokanyaga mafuta, je, itafaa niseme kuwa gari yangu imepatwa na pumu?
Nasi tunaongezea juu ya kauli ya mtaalamu huyu kwa kusema: mpangilio na utaratibu kwenye akili ya mashine umetokana na kitendo cha mtu, hilo halina shaka. Lakini ni nani aliyepangilia na akaweka mfumo kwenye ubongo wa binadamu?
Ikiwa binadamu amevumbua akili ya mashine, je akili hii ya mashine inaweza kuvumbua akili nyingine mfano wake au kitu duni kama pini? Katika kitabu Al-amal wal – Mukh (kazi na ubongo), kilichofasiriwa na Shakri Azir cha Mtaalamu wa Kirusi Yuri Bakhlov, anasema: Wale wanaodhani kuwa kuna uwezekano wa mashine kuchukua nafasi ya akili ya binadamu wamekosea kosa kubwa sana… ubongo wa binadamu unatofautiana kabisa na chombo chochote katika utendaji kazi wake, uwelekevu na ustadi wake usio na kikomo. Ama akili ya mashine ina kikomo - kile alicho kiweka binadamu.
4. Kuna ugunduzi mkubwa wa nyuki kuhusu vifaa vya kupunguza joto (viyoyozi), Kwamba nyuki aligundua kifaa hiki kabla ya binadamu. Joto linapozidi kwenye Masega ya nyuki kundi moja linaondoka kuleta maji kwa kutumia visiku vyao na kuyaweka kwenye tanki. Kikipatikana kiasi cha kutosha husimama kundi jengine kunyunyiza maji na kundi jingine la tatu linatengeneza tiyara ya hewa na maji yanayayuka kwa haraka; kwa myeyuko huo kiwango cha joto kinashuka.
Ni nani aliyempa nyuki akili hii? Ni sadfa? Au kuna nguvu ya hakika inayojitokeza kwenye maumbile na nidhamu yake? Nyuki na sisimizi wana masimulizi ambayo hayana tafsiri wala picha yoyote isipokuwa kuweko mpangiliaji mwenye hekima.
Turudie kauli ya Voltare ambaye huko nyuma tumewahi kumdokeza mara kwa mara, anasema: Mbele ya fikra ya kuweko Mwenyezi Mungu kuna vikwazo lakini katika fikra ya kupinga kuna upumbavu …Namna hii binadamu anahama kutoka kwenye shaka hadi shaka nyingine mpaka anafikia kusadikisha kuwa kuweko Mwenyezi Mungu ndio jambo la karibu zaidi na kwaye zinafungamana kanuni za dharura ya ulimwengu.
Wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa imepita kabla yao mifano.
Makusudio ya maovu hapa ni adhabu na mema ni thawabu na mifano ni mifano ya adhabu.
Mtume(s.a.w.w)
aliwalingania washirikina kwenye Tawhid, na akawaahidi thawabu wakiitikia mwito na kuwapa kiaga cha adhabu wakitoitikia.
Wao badala ya kuitikia mwito na kutubia shirk, waliendelea kuasi na wakajifanya jeuri, huku wakisema: Harakisha unayotuahidi ukiwa ni mkweli waliyasema haya bila ya kuzingatia umma zilizopita ziliyoyapata baada ya kuwaasi Mitume wao.
Kwa hakika mghafala huu wa kutopata funzo, hauhusiki na washirikina peke yao, Watu wengi hawazingatii yaliyowapata wenzao wala hawapati funzo; hata wenyewe wanaotoa mawaidha. Siri ya hilo ni kuwa wengi wanashindwa na tamaa na masilahi sio kwa akili wala dini.
Kuna mfano maarufu wa kimagharibi unaosema: Mwanamke kumwongoza mwana- mume kwa tumbo si kwa akili.
Na hakika Mola wako ni mwenye maghufira kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako ni mkali wa kuadhibu.
Makusudio ya maghufira hapa ni kupuuza na kutoharakisha adhabu kwa dhambi. Hilo linafahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na hakika Mola wako ni mkali wa kuadhibu. Kwa sababu maghufira hayawi pamoja na adhabu ya akhera sikwambii iliyo kali.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hamwadhibu mja mara tu anapo- fanya dhambi isipokuwa anamngojea na kumfungulia mlango wa toba ili aweze kurejea kutokana na upotevu wake, aweze kupata thawabu kwenye uwongofu wake.
Kuna tafsiri nyingine isemayo kuwa Mwenyezi Mungu husamehe dhambi za walioasi katika waislamu na anakuwa mkali wa kuadhibu kwa makafiri. Lakini tafsiri hii iko kinyume na dhahiri, tena inahimiza uasi. Usawa hasa ni yale tuliyoyasema kuongezea Aya nyingine isemayo:
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِم مَّا تَرَكَ عَلَيْهَا مِن دَابَّةٍ ﴿٦١﴾
“Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa sababu ya dhulma yao, asingelimwacha hata mnyama mmoja juu yake” (16:61).
Na husema wale ambao wamekufuru: ‘Mbona hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake?’ Hakika wewe ni mwonyaji tu. Na kila kaumu ina wa kuwaongoza.
Imepita mifano yake katika Juz.7 (6:37), Na tumefafanua kuhusu muujiza wa Mtume Muhammad(s.a.w.w)
na matakwa ya wenye kiburi katika Juz 1 (2:118).