6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
اللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَىٰ وَمَا تَغِيضُ الْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾
8. Mwenyezi Mungu anajua mimba aibebayo kila mwanamke na kinachopungua na kuzidi matumboni. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.
عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾
9. Ni mjuzi wa ghaibu na yanayoshuhudiwa, mkubwa aliyetukuka.
سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ ﴿١٠﴾
10. Ni sawa anayeficha kauli kati yenu na anayeidhihirisha na anayejibanza usiku na anayetembea mchana.
لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾
11. Ana yanayomfuatilia mbele yake na nyuma yake yanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao, Mwenyezi Mungu akiwatakia watu uovu hakuna cha kumzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.
MWENYEZI MUNGU ALIJUA
Aya 8-11
MAANA
Mwenyezi Mungu anajua mimba aibebayo kila mwanamke na kinachopungua na kuzidi matumboni.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya iliyotangulia ametaja kuwa washirikina walimtaka Muhammad(s.a.w.w)
muujiza zaidi unao fahamisha kuhusu utume wake.
Katika Aya hii anasema kuwa Yeye anajua kilicho katika matumbo ya uzazi awe ni mtoto wa kiume au wa kike mmoja au zaidi upungufu au ukamilifu. Basi mwenye kujua yote hayo, anajua kwamba kutaka muujiza zaidi ni inadi na kiburi tu, si kutaka kuongoka.
Wameafikiana Waislamu wote kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua viumbe vyote vikubwa kwa vidogo; Kwa sababu kila kiumbe kinajulikana mbele yake. Kwa ibara ya Muhyiddin bin Al-arabi:
“Hakika hakuna chochote kilichopo ulimwenguni ila kina wajihi maalum kwa yule aliyekifanya kiweko”
Kisha wanafalsafa wakatofautiana na ulamaa wa elimu ya Mwenyezi Mungu ambao wanasema kuwa Mwenyezi Mungu anajua mafungu yote; kama vile aina ya wanyama, mimea na vitu vingine kwa ujuzi wa moja kwa moja bila ya kuweko kitu chochote kati yake. Wanafalsafa nao wanasema anajua kupitia sababu zake na kinachozalikana nacho.
Sisi hatuoni faida yoyote ya tofauti hii; Kwa sababu ni juu ya Mwislamu kuamini kuwa elimu ya Mwenyezi Mungu imeenea kwenye kila kitu, kiujumla na kimafungu; hata mapigo ya moyo na pepesi za akilini. Ama kuamini elimu yake kwa namna hii au ile si chochote katika dini.
Kuna hadithi zinazokataa kuifikiria dhati ya Mwenyezi Mungu na kuamuru kufikiria kuumba kwake na utengenezaji wake.
Na kila kitu kwake ni kwa kipimo
haumbi kimchezomchezo na bila ya misingi; bali kila kitu kina kiwango chake na nidhamu yake katika kipimo cha mafungu, mihimili athari na mahusiano yake. Vile vile kinamna kitakavyokuwa na sura, mahali, wakati, sababu na desturi yake. Yote hayo ni kulingana hekima na masilaha.
Analoweza binadamu ni kuona, kuchunguza, kupima na kukisia; Kwa hivyo anaweza akapatia au kukosea. Kwa sababu elimu ya mtu inatokana na kutafuta, kwa hiyo inahitaji msababishaji.
Mara nyingi sana kuna yanayodhaniwa kuwa ni sababu ya jambo fulani, kumbe sivyo kabisa. Ama elimu Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ya kidhati na hali halisi.
Ni mjuzi wa ghaibu na yanayoshuhudiwa, Mkubwa aliyetukuka.
Makusudio ya ukubwa sio ukubwa wa umbo na utukufu sio mahali panapohisiwa, bali hayo ni mafumbo ya utukufu wa dhati Yake na sifa Zake. Mjuzi wa ghaibuu ni kujua yale tusiyoyajua, yaliyo ughaibuuni kutokana na elimu yetu na yanayoshuhudiwa ni yale tunayoyaona na kuyashuhudia.
Hakika ulimwengu umejaa viumbe jinsi na aina mbali mbali za hali ya juu na za chini. Kuanzia vidudu hadi binadamu na Malaika, madini hadi mimea na wanyama, mpaka kufikia maji na hewa na mengineyo yasiyokuwa na ukomo.
Mtume anaweza kujua upande moja tu wa baadhi ya vitu vya ulimwengu lakini ujuzi wake, kadiri utakavyokuwa si chochote kulinganisha na asiyoyajua, Mengi yanayofichuka yanaficha siri nyingi.
Wala hajui yaliyoko ulimwenguni isipokuwa muumba wa ulimwengu huo tu. Yeye peke yake ndiye ambaye, kwake, siri na dhahiri ni sawa tu.
وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾
“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” (17:85)
Ni sawa anayeficha kauli kati yenu na anayeidhihirisha na anayejibanza usiku na anayetembea mchana.
Umepita mfano wake katika Juz. 7(6:3) na Juz.10 (9:78).
Ana yanayomfuatilia mbele yake na nyuma yake yanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Anayefuatiliwa ni binadamu na yanayomfuatilia ni fumbo la hisia na silika zake ambazo zina athari katika kuwa kwake na kuhifadhi utu wake. Hayo yametokana na riwaya iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq (a.s.).
Wafasiri wamesema kuwa makusudio yayanayomfuatilia
ni Malaika, na tafsiri nyingine zinasema kuwa Mwenyezi Mungu hupeleka Malaika kumi mchana kumlinda binadamu na jua linapozama wanaondoka hao na kuja wengine kumi wa zamu ya usiku; na kwamba kila mtu anakuwa hivyo. Iblisi naye zamu yake ya kuwapoteza watu ni mchana na usiku ni zamu ya watoto wake.
Mbali ya kuwa maelezo hayo yako mbali na tamko linavyofahamisha, lakini akili pia inayakataa. Tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ya yanayofuatilia ni hisia zinazomhifadhi mtu; kama tulivyotangulia kueleza. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuumba mtu, akampa masikio, macho, utambuzi na mengineyo, ili yamlinde na kumchunga.
Maana haya, ingawaje yako mbali na tamko la Aya, lakini yanaafikiana na hali halisi wala hayapingani na mfumo wa Aya. Ni kwa utambuzi, mtu ana mapambano kati ya manufaa na madhara, ni kwa macho anaweza kufuata njia iliyosalama na ni kwa kupenda dhati ndio atajihifadhi na maangamizi.
HABADILISHI MPAKA WAJIBADILISHE
Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao.
Wafasiri wamesema: Aya hii inafahamisha kuwa watu wanaoishi katika neema ya mali, amani na jaha, Mwenyezi Mungu hawezi kuwaondolea madamu wanaswali na kutoa Zaka, lakini wakiasi basi anawaondolea neema hii.
Ama sisi tutafasiri Aya hii katika mwelekeo wa mafunzo ya kiislamu na maana yanayochukuliwa na tamko la Aya.
Katika mafunzo ya Uislamu, yaliyo muhimu ni wajibu wa jihadi ya nafsi ikiwa inapondokea kwenye haramu na maangamizi au kuridhia udhalili na ufukara. Vile vile jihadi ya nafsi na mali katika njia ya uadilifu na kujikomboa kutokana na dhulma na utumwa.
Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kupinga udhalili, akapuuza uhai na kukataa kila kitu isipokuwa heshima yake au mauti, basi Mwenyezi Mungu atamshika mkono kumpeleka kwenye matakwa na malengo anayoyakusudia.
Na mwenye kubweteka kwenye raha na uvivu, vyovyote itakavyokuwa Mwenyezi Mungu atamdhalilisha na kumwachia udhaifu wake wala hatamwangalia au kumsikiliza; hata kama ataijaza dunia kwa unyenyekevu, vilio, na dua.
Kwa hivyo basi inatufunukia kuwa maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “ Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao,” ni kuwa Yeye ambaye imetukuka heshima yake, atambakisha mtu kwenye udhalili ikiwa amekaa tu bila ya kujikwamua na kuipinga batili.
Ndio! Mwenyezi Mungu hawezi kutuondolea ufukara mpaka tuamini kuwa ufukara umetoka ardhini sio mbinguni, na mpaka tupigane jihadi dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji na mpaka tujenge viwanda na tulime mashamba.
Mwenyezi Mungu hatubadilishii ujinga mpaka tujenge mashule na vyuo vikuu, Mwenyezi Mungu hatubadilishii utumwa mpaka tulete mapinduzi dhidi ya dhulma. Na Mwenyezi Mungu hatatubadilishia matatizo mbalimbali mpaka tuzisafishe nyoyo zetu na tuondoe pingamizi na vikwazo vilivyo baina yetu.
Mwenyezi Mungu akiwatakia watu uovu hakuna cha kumzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.
Makusudio ya uovu hapa ni adhabu. Wakati wowote Mwenyezi Mungu anapomtakia mtu au kundi jambo lolote, basi hakuna wa kuzuwiya, na Yeye ni mwadilifu, hamtakii isipokuwa analostahiki. Ulinzi ni katika sifa za Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye analinda mambo na huyasimamia kwa mipangilio iliyo kamili.
هُوَ الَّذِي يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنشِئُ السَّحَابَ الثِّقَالَ ﴿١٢﴾
12. Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito.
وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلَائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَن يَشَاءُ وَهُمْ يُجَادِلُونَ فِي اللَّـهِ وَهُوَ شَدِيدُ الْمِحَالِ ﴿١٣﴾
13. Na radi inamtakasa kwa kumsifu na Malaika pia kwa kumhofia. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye, Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu; na yeye ni mkali wa hila.
لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ إِلَّا كَبَاسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى الْمَاءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَالِغِهِ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ ﴿١٤﴾
14. Kwake ndio maombi ya haki, Na hao wanaoomba badala yake hawajibiwi chochote isipokuwa kama yule anyooshaye viganja vyake kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotevu.
وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ﴿١٥﴾
15. Na vilivyomo mbinguni na ardhini vinamsujudia Mwenyezi Mungu vitake visitake na vivuli vyao asubuhi na jioni.
ANAYEWAONYESHA UMEME
Aya 12-15
MAANA
Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na tamaa na huyaleta mawingu mazito.
Umeme unaokusudiwa hapa ni ule wa radi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimengu; ulimwengu nao una mambo yake na desturi zenye athari; ukiwemo umeme radi mawingu, vimondo na mengineyo anayoweza kuyashuhudia mtaalamu na mtu wa kawaida na pia muumin na mlahidi. Wala hajui hakika yake na umbile lake isipokuwa wataalamu wahusika.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyategemeza kwake moja kwa moja, wala hakuyategemeza kwenye sababu za ulimwengu, kwa upande wa kutegemeza kitu kwenye sababu yake ya kwanza.
Lengo ni kukumbusha kwamba Yeye ndiye sababu ya sababu zote, na kwake Yeye pekee yanarejea mambo yote.
Kauli yake kwa hofu na tamaa ni kuashiria umeme, mara nyingine unakua ni kutoa onyo la kupiga radi ya kimondo na mara nyingine ni dalili njema ya mvua. Kwa hiyo mtu anapata hofu na furaha kwenye kitu hicho hicho kimoja.
Na radi inamtakasa kwa kumsifu na Malaika pia kwa kumhofia.
Makusudio ya kumtakasa (tasbih) ya radi ni kufahamisha uweza na cheo chake Mwenyezi Mungu; sawa na maandishi yanavyomfahamisha mwandishi na jengo na mjengaji wake.
Hapa ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ ﴿٤٤﴾
Na hapana kitu chochote ila kinamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsifu” (17:44).
Yaani kinamfahamisha, Kwa maneno mengine kila kitendo kizuri kilichofanywa kwa mpangilio mzuri kinamfahamisha aliyekifanya jinsi alivyo na kumsifia, kwa lugha ya hali.
Hakuna mwenye shaka kwamba kila kilichomo ulimwenguni kimefanywa kwa mpangilio mzuri usio na kikomo. Kwa hivyo kinafahamisha jinsi alivyo muumba wake na kumsifia.
Kauli ya kushangaza ni ile ya baadhi ya masufi wanaosema kuwa radi ni kukoroma kwa Malaika na umeme ni mapigo ya nyoyo zao.
Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye.
Unaweza kuuliza
: mapigo ya radi mitetemeko ni mambo ya kidhahiri ya kimaumbile na desturi yake. Ni wazi kwamba maumbile ni pofu hayachagui baina ya mwema na muovu, shari yake na heri yake inawaenea wote bila kutofautisha, lakini kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ‘yakampata amtakaye’ inatambulisha kutofautisha?
Jibu
: Makusudio ya mapigo ya radi hapa ni adhabu ya radi aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa wale waliong’ang’ania shirki wakawafanyia inadi Mitume wao; kama vile kaumu ya A’d na Thamud, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ ﴿١٣﴾
“Kama wakikataa waambie nawahadharisha na pigo la radi mfano wa pigo la radi la A’d na Thamud.” (41:13).
فَقَالُوا أَرِنَا اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ بِظُلْمِهِمْ ﴿١٥٣﴾
“Walisema: ‘Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi.’Wakapigwa na radi kwa sababu ya dhulma yao.” Juz.6 (4:153).
Imetangulia mara nyingi kuelezwa kwamba Qur’an inajitamkia yenyewe kwa yenyewe na baadhi yake ina shuhudia baadhi nyingine.
Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu.
Wanaobishana ni washirikina. Maana ni kuwa hawa wanabishana katika uweza wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake, Mtume Muhammad(s.a.w.w)
na Utume wake na pia ufufuo na uwezekano wake, pamoja na kudhihiri dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, Muujiza wazi wa Utume wa Muhammad(s.a.w.w)
na kushuka adhabu kwa wapinzani wa ufufuo na hisabu.
Na yeye ni mkali wa hila.
Yaani ni mwenye nguvu sana za kuwakamata maadui zake na maadui wa mawalii wake. Kwa ufupi ni kuwa washirikina wanabishana kwa maneno na Mwenyezi Mungu anakamata kwa vitendo.
إِنَّ بَطْشَ رَبِّكَ لَشَدِيدٌ ﴿١٢﴾
“Hakika mashiko ya Mola wako ni makali.” (85:12).
Kwake ndio maombi ya haki, Na hao wanaoomba badala yake hawajibiwi chochote isipokuwa kama yule anyooshaye viganja vyake kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotevu.
Mwenyezi Mungu ndiye haki, Mwenye kutenda kwa ajili yake na akamtegemea yeye, basi atamlipa thawabu na mwenye kuasi na akafanya jeuri atastahiki adhabu; mwenye kuomba mwenginewe, kama masanamu ,atakuwa ameomba batili isiyodhuru wala kunufaisha.
Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotovu.
Sawa na mwenye kiu akidhani moshi ni mawingu na mangati kuwa ni maji. Ananyoosha viganja vyake ili avijaze maji na anafungua kinywa chake ili aburudike, mara hamna kitu.
Na vilivyomo mbingu ni na ardhini vinamsujudia Mwenyezi Mungu vitake visitake.
Umepita mfano wake katika Juz.3(3:83).
Na vivuli vyao asubuhi na jioni.
Kivuli ni akisi ya mwili ambao unakuwa nacho, ukitingishika nacho hutingishika; sawa na sura ya kitu kwenye kioo. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja asubuhi na jioni, kwa sababu kivuli kinarefuka katika nyakati mbili hizi.
Maana ni kuwa vilivyomo mbinguni na ardhini na pia vivuli vyao vinamsujudia. Unaweza kuuliza: Kivuli si chochote isipokuwa kinafuata na kinapigiwa mfano wa kutokuwepo kitu. Vipi Mwenyezi Mungu amejaalia ni kitu na akaunganisha na mwenye kivuli hicho?
Sufi wamejibu kuwa vilivyomo mbinguni na ardhini ni viwiliwili na vivuli ni roho.
Tunavyofahamu ni kuwa kivuli ni fumbo la kuenea kwenye kila kitu na kwamba kila kilichoko ulimwenguni kinamsujudia Mwenyezi Mungu; yaani kinakubali kuweko kwake, hata kivuli kingelimsujudia kama kingelikuwa ni kitu.
قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾
16. Sema: Ni nani Mola wa mbingu na ardhi? Sema, ni Mwenyezi Mungu. Sema: Je, mnawafanya wengine badala yake kuwa ni walinzi na hawajifai wenyewe kwa nafuu wala dhara? Sema: Je, anaweza kuwa sawa kipofu na aonaye? Au je, huwa sawa giza na nuru? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika, walioumba kama kuumba kwake kwa hiyo kuumba kukashabihiana kwao? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu na yeye ni mmoja, Mwenye kushinda.
KIPOFU NA MWENYE KUONA
Aya 16
MAANA
Sema: Ni nani Mola wa mbingu na ardhi?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa kila kilichomo ulimwenguni kinanyenyekea uweza wake, anawarudia washirikina na kuwauliza kupitia mdomoni mwa Mtume wake Mtukufu, kuwa ni nani aliyeumba ulimwengu ikiwemo ardhi yake na mbingu yake?
Kwa kuwa swali liko pamoja na jawabu lake; na wala aliyeulizwa hawezi kupinga, alimwamrisha Mtume wake awajibu:Sema: ni Mwenyezi Mungu.
Sema: Je, mnawafanya wengine badala yake kuwa ni walinzi na hawajifai wenyewe kwa nafuu wala dhara?
Mara nyingine, tena kwa kusisitiza hoja, Mwenyezi Mungu anamwamrisha Muhammad awaambie washirikina kuwa nyinyi mnaabudu mawe ambayo yenyewe hayajiwezi kujikinga na madhara wala kuleta manufaaa, je yataweza kumfaa mwingine?
Aya hii si majibu ya washirikina pekee, bali pia ni majibu ya wale wasemao kuwa akili za watu zinajitosha, hazihitajii kupelekewa mitume na kuteremshwa vitabu kutoka mbinguni. Waabudu mawe walikuwa na wanaendelea kuwa wanajiona ni wenye akili na pia watu wangine wanawaona hivyo.
Sema: Je, anaweza kuwa sawa kipofu na aonaye?
Makusudio ya kipofu ni kafiri. Kwa sababu hakuweza kutofautisha baina ya yule asiyejiweza, na mwenye kumiliki dhara na manufaa? Makusudio ya mwenye kuona ni mumin ambaye anatofautisha kati ya wawili hao (asiyejiweza na mwenye uwezo).
Au je, huwa sawa giza na nuru?
Giza ni fumbo la kufuru na nuru ni fumbo la imani. Mwenyezi Mungu anasema:
الر كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ﴿١﴾
“Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu gizani uwapeleke kwenye nuru” (14:1).
Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika, walioumba kama kuumba kwake kwa hiyo kuumba kukashabihiana kwao?
Hii ni kuwarudi washirikina. Ufupisho wake ni kuwa mawe ambayo wanayaabudu hayaumbi chochote; kama aumbavyo Mwenyezi Mungu. Sasa wamethubutu vipi kusema kuwa Mungu anaumba na masanamu yanaumba.
Ikiwa Mwenyezi Mungu anastahiki Uumbaji, basi vile vile atastahiki Uungu na ibada. Ufafanuzi ni kama ifuatavyo:
AKILI ZA WATU HAZIWATOSHELEZI
Maarifa ya mtu yanagawanyika kwenye mafungu mawili: Maarifa ya kiumbile ya kidhati na maarifa ya kinadharia ya kutafuta. Ya kimaumbile hayahitaji bidii wala juhudi, bali yanapatikana kiasi cha kuleta picha tu kichwani; kama kujua kwamba nuru sio giza, kuona si upofu, urefu sio ufupi, jiwe limeumbwa na haliwezi kuumba. Katika maarifa haya anashiri kimjuzi na asiyekuwa mjuzi, na mwenye kukosea hana udhuru wowote [2]
.
Ama maarifa ya kinadharia ya kutafuta hayapatikani kwa kuleta picha, bali inahitajika kuyafanyia kazi, juhudi na bidii; kama vile kujua kuwa maji yameshikana au yameachana? Na kujua mardhi haya yanaambukiza au la.
Kadhia hii huitwa ‘nadharia’ ambayo inatofautiana kulingana na maarifa na vipawa vya wenye nadharia hizo. kukosea katika nadharia kunasame- hewa kukiwa kumetokea baada ya bidii na juhudi. Kwa sababu kupatia katika kila kitu ni jambo zito.
Masanamu waliyoyaabudu washirikina hayana mshabaha wowote na uungu kwa njia yoyote ile ya mbali au ya karibu, kuweza kumfanya mtu aingie shaka au aone uwezekano wa kuwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake.
Itakuwaje yakiwa hayo yenyewe yanakojolewa na mbwa na vicheche? Kuyaabudu ni upumbavu zaidi kuliko kusema kuwa giza ni nuru au kipofu anaona.
Unaweza kuuliza
: Ni kweli kwamba kuna aina ya maarifa ambayo ni maumbile na kwamba kuukana uungu wa mawe ni mambo ya kimsingi yaliyo wazi yasiyohitaji nadharia, lakini washirikina pamoja na akili yao ya kimaumbile wameweza kuyaabudu, wakiwa ni wenye akili timamu. Je, ni kwa nini?
Jibu
: Baadhi yao waliabudu kijujuu tu kwa sababu ya chumo na masilahi fulani, wengine waliabudu kwa kuiga na kurithi. Ilivyo ni kuwa akili inadhoofika na kurudi nyuma katika kuigiza au mazoweya, hasa muda ukiwa mrefu na kurithiwa na vizazi baada ya vizazi vingine.
Ndio maana ikawa dini iliyo salimika ni dharura na lazima kwa binadamu kadiri atakavyokuwa na akili na elimu. Kuna wengi sana waliozowea mifu- mo ya elimu na njia zake za undani, hivi sasa, wanaamini mambo mengi ya upotevu. Gustave Labon, anasema katika kitabu Al-arau wal-mutaqada (Rai na itikadi).
“Hakika wataalamu wanatokewa na mambo ya kijinga sawa na wanavyotokewa wasiojua chochote. Ni mara chache sana mtaalamu kusalimika na ujinga katika mambo yasiyokuwa fani yake.
Kwa maelezo haya ndio tunapata sababu ya wataalamu bora zaidi kuaamini mambo ya kipumbavu sana!! Kisha akatoa mifano mingi sana ya hilo; miongoni mwa mifano hiyo ni: kulikuwa na mtaalamu mmoja mkubwa katika zama zake alikuwa hawezi kutoka nyumbani kwake mpaka afunge kamba shingoni ya kumkinga na dege na uchawi.
Sema: Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu na yeye ni mmoja, Mwenye kushinda.
Ni mmoja katika dhati yake, sifa zake, na kuumba kwake. Mwenye kumshinda kila mwenye inadi na mwenye kuasi hukumu miongoni mwa hukumu zake.
Katika Juz.5 (4:48) Tumetaja dalili za umoja wa muumba. Hapa tutaunganisha na maelezo yaliyo katika Kitab Difau anil- Islam (kuutetea uislam) kilichoandikwa na Laura Fisheva Gallery na kutarjumiwa na Ustadh Munir Baalbaki.
Anasema: Mtume mwarabu alitoa mwito wa itikadi ya umoja wa Mungu (Tawhid) akapata upinzani wa wasio na mtazamo ambao ulimuongoza mtu kwenye shirk. Muhammad alitoa mwito wa kusoma kitabu cha maisha na kufikiria kwenye ulimwengu na desturi yake akiwa anaamini kuwa kila mwenye akili hana budi mwisho kuamini Mungu mmoja.