9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ أُكُلُهَا دَائِمٌ وَظِلُّهَا تِلْكَ عُقْبَى الَّذِينَ اتَّقَوا وَّعُقْبَى الْكَافِرِينَ النَّارُ ﴿٣٥﴾
35. Mfano wa Bustani (Pepo) waliyoahidiwa wenye takua inapita mito chini yake, matunda yake ni ya daima na pia kivuli chake. Hiyo ndio mwisho wa wale wenye takua. Na mwisho wa makafiri ni moto.
وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَفْرَحُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمِنَ الْأَحْزَابِ مَن يُنكِرُ بَعْضَهُ قُلْ إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ وَلَا أُشْرِكَ بِهِ إِلَيْهِ أَدْعُو وَإِلَيْهِ مَآبِ ﴿٣٦﴾
36. Na wale ambao tumewapa Kitabu wanafurahia uliyoteremshiwa, Na katika makundi mengine wapo wanayoyakataa baadhi yake. Sema: Nimeamrishwa nimwabudu Mwenyezi Mungu wala nisimshirikishe. Ninalingania kwake Yeye, na marejeo ni kwake.
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ حُكْمًا عَرَبِيًّا وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُم بَعْدَ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا وَاقٍ ﴿٣٧﴾
Na ndio kama hivyo tumeiteremsha Qur’an kuwa ni hukumu kwa Kiarabu. Na kama ukifuata hawaa zao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na msimamizi wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ ﴿٣٨﴾
38. Na hakika tulikwishawatumma mitume kabla yako na tukawajalia wawe na wake na kizazi. Na haiwi kwa Mtume kuleta muujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, Kila muda una kitabu.
MFANO WA BUSTANI
Aya 35-38
MAANA
Mfano wa Bustani (Pepo) waliyoahidiwa wenye takua inapita mito chini yake, matunda yake ni ya daima na pia kivuli chake.
Mwenyezi Mungu alipomaliza kutaja malipo ya makafiri, sasa anataja malipo za wenye takua, kama kawaida yake ya kutaja kitu na kinyume chake. Malipo ya wenye takua ni Bustani (Pepo) pamoja na nema yake ya kudumu – mito, matunda na vivuli.
Hiyo ndio mwisho wa wale wenye takua.
Hiyo ni ishara ya Pepo. Wenye kumcha Mungu ni wale wanoilinda haki na watu wake na kupambana na batili na watu wake. Kuna Hadith isemayo: “Hakika imani iko juu ya Uislamu na kumcha Mungu kuko juu ya Imani na yakini iko juu ya kumcha Mungu” Makusudio ya yakini ni kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye.
Na mwisho wa makafiri ni moto.
Makusudio ya makafiri hapa sio tu wale wanaomkana Mwenyezi Mungu au kumshirikisha; isipokuwa makusudio ni kila anayeipinga haki, huku akiwa anajua. Zimeleza Hadith nyingi kuwa unafiki ni ukafiri n ria ni shirk. Mwenyezi Mungu amewasifu na ukafiri madhalimu, aliposema:
فَأَبَى الظَّالِمُونَ إِلَّا كُفُورًا ﴿٩٩﴾
“Lakini madhalimu hawataki ila ukafiri” (17:99);
kama ambavyo amewasifu makafiri na washirikiana kwa dhulma katika Aya kadhaa.
SHIA IMAMIYA NA SWAHABA
Wamezowea baadhi ya wanaolipwa walio wajinga kuleta fitna na ghasia baina ya Waislamu ili kuuchafua umoja wao na kuwagombanisha. Wamezoya sana hilo kwa njia ya kutia doa na kuleta uzushi kwa Shia kwa kuwazulia kuwatukana maswahaba; kumfanya Mungu Ali, kuwa Qur’an imepotolewa, jambo ambalo linaitingisha Arsh, na mengineyo miongoni mwa uwongo na uzushi.
Nimeandika makala ndefu katika kuwajibu vibaraka na wafanya propaganda hizi. Kisha nikayaweka kwenye vitabu: Ma’shia al-imamiyya, Ashia wal-hakimun, Al-ithnaashariya wa Ahlulbayt, na Ashia wat tashayyu’ ambacho ni kikubwa kuliko vyote.
Lengo langu la kwanza la makala na tungo hizi ni kuuweka wazi uhakika kwa yule anayetaka kuujua na kuubatilisha uongo na uzushi uliosemwa na unaosemwa juu ya taifa hili.
Hapa nimedokeza niliyoyaandika na kuyatunga kuhusiana na maudhui haya kwa mnasaba wa Aya hii tuliyo nayo, kama ifuatavyo:
Na wale ambao tumewapa Kitabu wanafurahia uliyotermshiwa.
Amesema Abu Hayan Al-andalusi, Zamakhshari, Sheikh Al-maraghi, Al-baydhawi na wengineo katika maulama wa kisunni kuwa makusudio ya wale ambao wamepewa Kitabu ni Myahudi na Manaswara wale waliomwamini Muhammad(s.a.w.w)
.
Na akasema Tabrasiy, katika Tafsir Majmau’lbayan, ninamnukuu: “Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakusudia maswahaba wa mtume(s.a.w.w)
ambao walimwamini na kumsadikisha, wakapewa Qur’an na kuifurahia kushuka kwake” Tabrasiy ni miongoni mwa maulama wakubwa wa kishia (alikufa mwaka 548 AH).
Kwa hiyo basi wanchuoni wengi wa kisunni wamefasiri Aya hii kuwa ni waliosilimu katika Mayahudi na manaswara; na wa kishia wamefasiri kuwa ni Mswahaba wa Mtume mtukufu(s.a.w.w)
. Ikiwa wao wanawatukana maswahaba angelielekea Sheikh wao Tabrasiy, katika kufasiri Aya hii kwenye njia ya maswahaba, Hapa unatubainikia uzushi uliowekwa kwenye kundi hili.
Aban bin Taghlab ni mmoja katika wanafunzi wakubwa wa Imam Jafar As- Sadiq
, kiasi ambacho Imam alikuwa akiwaamuru Shia kuchukua dini kutoka kwake. Siku moja aliulizwa na mtu mmoja anayeitwa Abul-bilad kuhusu Shia, akamwambia: ni wale ambao wakitofautiana watu kuhusu riwaya iliyopokewa kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
basi huchukua riwaya ya Ali aliyoipokea kutoka kwa Mtume na wanapotofautiana watu katika riwaya ya Ali huchukua kauli ya Jafar As-Sadiq aliyoipokea kutoka kwa Ali.
Kwa hiyo basi, kwa Shia, kadhia ni mategemezi ya riwaya kutoka kwa Muhammad(s.a.w.w)
sio kadhia ya kutukana na kushutumu maswahaba wa Muhammad. Siri ya mategemezi yao Shia kwa Ahlu bayt (watu wa nyum- ba ya Mtume) ni Hadith kadhaa zilizothibiti, zinazohimiza hilo. Miongoni mwazo ni ile allyoipokea Muslim katika Sahihi yake kutoka kwa Mtume, kwenye mlango wa Fadhail Ali bin Abi Twalib (Ubora wa Ali bin Abi Twalib), kwamba mtume amesema:
Mimi ni mtu, mjumbe wa Mwenyezi Mungu anakurubia kunijia nimwitikie; nami ninacha kwenu vizito viwili, cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu ndani yake mna uongofu na nuru, basi kichukueni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na shikamaneni nacho.
Akahimiza kuhusu Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukipen- dekeza, kisha akasema: Na Ahl bayt yangu (watu wa nyumba yangu) ninawakumbusha kwa Mwenyezi Mungu kuhusu Ahl bayt wangu, Alilikariri hilo mara tatu.
Na katika makundi mengine wapo wanayoyakataa baadhi yake.
Makusudio ya makundi mengine ni watu wa mila na dini nyingine; kama vile mayahudi, manaswara na wengineo wanaoyakataa yale yanayokhalifiana na mapenzi yao na wakayakubali yanayoafikiana na mapenzi yao katika Qur’an.
Ilivyo ni kuwa kupinga kwao hawa na kukubali kwao ni sawa tu, kwa sababu kukubali ni kwa kuafikiana na hawaa zao sio kwa sababu ya Qur’an.
Sema: Nimeamrishwa nimwabudu Mwenyezi Mungu wala nisimshirikishe. Ninalingania kwake Yeye, na marejeo ni kwake.
Huu ndio Uislamu: Hakuna Mola mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu ni wake ufalme na mwito wa kuabudiwa ni kwake Yeye tu, na mwisho marejeo ni kwake yeye.
Na ndio kama hivyo tumeiteremsha Qur’an kuwa ni hukumu kwa Kiarabu.
Makusudio ya hukumu ni Qur’an, kwa sababu ndio hukumu ya Mwenyezi Mungu, isiyokuwa hiyo ni hukumu ya kijahili; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ ﴿٥٠﴾
“Je wanataka hukumu za Kijahiliya, Na ni nani aliye mwema zaidi kwa hukumu kuliko Mwenyezi Mungu, kwa watu wenye yakini” Juz, 6 (5:50)
Kama ambavyo Mwenyezi Mungu, alimtuma kila mtume kwa lugha ya watu wake, vilevile alimtuma Muhammad. Mwenyezi Mungu anasema:
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ﴿٤﴾
“Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia (14:4)
Tumefafanua sababu za kushuka Qur’an kwa kiarabu, pamoja na kuwa Muhammad ametumwa kwa watu wote, katika Juz. 12 (12:2).
Na kama ukifuata hawaa zao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na msimamizi wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wanaokusudiwa katika neno hawaa zao ni watu wa mila nyingine isiyokuwa Uislamu. Mwenyezi Mungu anajua kuwa Nabii hafuati wala hatafuata hawaa na matamanio yao. Lengo la ukatazo huu ni uthabiti na kuendelea kuilingania haki, wala asiogope lawama ya mwenye kulaumu. Tumeelza mara kwa mara kuwa amri ikitoka kwa mkubwa hakiangaliwi cheo cha mdogo vyovyote kilivyo
Na hakika tulikwishawatuma mitume kabla yako na tukawajalia wawe na wake na kizazi.
Asiye na haki akishindwa huanza kuzungusha maneno na kupima mambo kwa mawazo na njozi zake. Na hivyo hasa ndivyo ilivyokuwa kwa washirikina na Muhammad(s.a.w.w)
. Aliwaletea hoja na dalili, wali- poshindwa kuzijibu wakanza kusema: itakuwaje ni nabii naye ana mke na watoto.
Mantiki hii inafanana kabisa na mantiki ya wanaoamini utawa. Mwenyezi Mungu amewajibu kwa kuwambia kuwa Muhammad ni kama Nuh, Ibrahim, Ismail na wengineo katika mitume ambao wana wake na watoto, sasa kuna ajabu gani katika hilo?
Kuna hadith iliyopokewa kutoka kwa mtume, amesema: Ama mimi ninafunga, ninafungua, ninalala, ninaamka, ninakula nyama na ninaoa. Mwenye kujiepusha na desturi yangu basi yeye si katika mimi.
Na haiwi kwa Mtume kuleta muujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Haya vilevile ni majibu kwa washirikina ambao walimpendekezea mtume miujiza ile waitakayo. Njia ya majibu ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu swt) amemsheheneza mtume wake kwa dalili zinazotosheleza kujulisha juu ya utume wake, kwa yule mwenye kuzingatia na kuitafuta haki kwa njia ya haki. Ama kuitikia mapenzi ya mwenye inadi na kiburi hakukubaliwi na akili wala desturi. Anaachiwa Mwenyezi Mungu na hekima yake.
Kila muda una kitabu.
Yaani kila kitu kina muda wake, kiwe ni muujiza, adhabu, au chochote kile, Na muda umeandikwa hautangulizwi wala kucheleweshwa nao umefichwa, haujui isipokuwa Mwenyezi Mungu
يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ ﴿٣٩﴾
39. Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo na kwake kuna mama wa Kitab.
وَإِن مَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾
40. Na ikiwa tutakuonyesha baadhi ya tuliyowaahidi au tukakufisha, basi ni juu yako kufikisha na juu yetu ni hisabu.
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا وَاللَّـهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٤١﴾
41. Je hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza janibu zake. Na Mwenyezi Mungu huhukumu, hapana wa kupinga hukumu yake; na Yeye ni mwepesi wa kuhisabu.
قَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلِلَّـهِ الْمَكْرُ جَمِيعًا يَعْلَمُ مَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ وَسَيَعْلَمُ الْكُفَّارُ لِمَنْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٤٢﴾
42. Na wamekwisha fanya vitimbi waliokuwa kabla yao na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye vitimbi vyote, Anajua inayoyachumma kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho.
وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَسْتَ مُرْسَلًا قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَمَنْ عِندَهُ عِلْمُ الْكِتَابِ ﴿٤٣﴾
43. Na wale ambao wamekufuru wanasema wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi na yule mwenye elimu ya Kitabu.
MWENYEZI MUNGU HUFUTA NA HUTHIBITISHA AYATAKAYO
Aya 39-43
MAANA
Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo na kwake kuna mama wa Kitab.
Mama wa kitabu ni fumbo la ujuzi wake Mwenyezi Mungu wa yaliyokuwa na yatakayokuwa.
Lau ingekuwa inafaa kufasiri matamshi kwa muonjo na kupendeza, basi tungelifasiri kitabu ni ulimwengu na mama ni siri zake; kwa sababu Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: kimoja kinatamka kwa lugha ya hali nacho ni ulimwengu na kingine kinatamka kwa lugha ya maneno nacho ni Qur’an.
Ama kufuta na kuthibitisha, Tabrasi amenukuu katika maana yake kauli nane, iliyokaribu zaidi na maana ni kuwa makusudio ya kufuta ni kufuta sharia za zamani au kufuta baadhi ya hukumu zake; kama vile kufuta hukumu ya kuelekea Baytil-maqds. Ama kuthibitisha, makusudio yake ni kuthibitisha hukumu mpaka siku ya Kiyama.
Kwa hiyo maana ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anafuta au kuthibitisha sharia zote au baadhi, vile masilahi na hekima yake inavyotaka. Na Yeye ambaye umetukuka utufu wake anajua yaliyo na maslahi kwa waja na yaliyo na uharibifu. Kwa hiyo anawamrisha hili na kuwakataza lile, daima au kwa muda, kulingana na vile elimu yake inavyojua muda wa madhara na manufaa, Tumezungumzia kuhusu kufuta hukumu katika Juz.1 (2:106).
Na ikiwa tutakuonyesha baadhi ya tuliyowaahidi au tukakufisha, basi ni juu yako kufikisha na juu yetu ni hisabu.
Aya hii ianungana na Aya 31 ya Sura hii. Njia ya kuungana ni dhahiri: Kule amemwambia mtume wake kuwa Yeye kwa vyovyote atamteremshia adhabu yule anayemkadhibisha; hapa anasema kama tutakuonyesha adhabu yao au tutakufisha kabla ya hiyo adhabu, basi umuhimu wako wa kwanza na wa mwisho ni kufikisha tu, mengine tuachie sisi.
Je hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza janibu zake.
Ardhi ni tufe, lisilokuwa na ncha, lakini ni pana linaloweza kukaliwa na mamilioni ya aina mbali mbali ya viumbe, Nayo hubadilika daima. Binadamu anaweza kuona au kusikia kuwa ardhi hii ni nzuri kukaliwa na watu itakuwa na maendeleo na ardhi ile haifai ni njangwa. Mara ile iliyoonekana inafaa inakuwa haifai na ile iliyokuwa jangwa isiyofaa inakuwa bustani yenye mito.
Watu wa ardhi pia ni hivyo hivyo, maendeleo yanakuwa hai na mengine yanakufa; ufalme unasimama na mwingine unaanguka, Hivi ndivyo ilivyo dunia ‘kigeugeu’ Hakuna ubaya wala neema inayoweza kudumu hapa ardhini.
Imam Ali (a.s) anasema:“Tahadharini na dunia ina ghururi na inahadaa, inatoa na kuzuia, inavika na kuvua. Haidumu raha yake wala tabu yake haiishi.”
Kauli yake Mwenyezi Mungu: Tukiipunguza janibu zake, inaashiria maana hii na kwamba mwenye akili anapata funzo kwa mageuko haya:
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ﴿١٠٩﴾
“Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? (12:109).
Na Mwenyezi Mungu huhukumu, hapana wa kupinga hukumu yake.
Na amekwisha hukumu kuwaangamiza wenye makosa na amekwishaipitisha hukumu hiyo.
Na wamekwisha fanya vitimbi waliokuwa kabla yao na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye vitimbi vyote.
Makusudio ya vitimbi vya Mwenyezi Mungu ni kupangua vitimbi, Angalia Juz.3 (3:53).
Anajua inayoyachuma kila nafsi;
Kwa sababu yeye ni mwenye wasaa aliye mjuzi.
Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho. Siku ile watakaporudi kwa Mola wao na kusema leo ni siku nzito.
Na wale ambao wamekufuru wanasema wewe hukutumwa.
Waliukana utume wa Muhammad pamoja na dalili zote, kwa vile huo ni vita dhidi ya dhulma na utaghuti na jambo lolote linalozuia uhuru wa mtu, amani yake na wema wake
RAHA YA DHAMIRI NA MAWAZO
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi na yule mwenye elimu ya Kitabu.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anamwamrisha mtume wake awaambie: ikiwa mnakanusha utume wangu, basi Mwenyezi Mungu anshuhudia kuwa mimi ni mtume kutoka kwake, vile vile wenye kuchunga haki katika maulama wa Tawrat na Injil wanashuhudia hilo.
Haya ndio maana ya dhahiri na ndio makusudio yake na ndiyo waliyoeleza wafasiri na sisi tuko pamoja nao, lakini zaidi ya hiyo tunagusia maana kubwa zaidi inayofungamana na kila mwenye kuiamini haki akaitumia na akapingwa na wenye kufanya ufisadi katika ardhi na yakampata yaliyowapata.
Muhtasari wa maana haya makubwa na matukufu ambayo yanaashiriwa na Aya ni kuwa kila ambaye dhamiri yake inalionea raha jambo na kushuhudi- wa na mawazo yaliyo salama, basi Mwenyezi Mungu, Malaika wake na wenye kuchunga haki pia wanalishuhudia kuwa ni haki, awe ni Mtume au sio Mtume.
Unaweza kuuliza
: Ni wakati gani mtu anakuwa na raha ya dhamiri na kushuhudiwa na mawazo salama?
Jibu
: Hakika binadamu hawezi kuwa ni katika mwenye dhamiri hai na mawazo salama ila ikiwa anaamini msimamo wa kibinadamu; kama vile uadilifu, uhuru, ukweli, uaminifu na mengineyo ambayo heri yake inawarudia wote. Pale tu, mtu atakapoamini msimamo huu na ukaoana na vitendo vyake, basi atakuwa amestarehe dhamiri, na kushudiwa na mawazo yake.
Na wakati wowote, vitendo vyake na imani yake vitakapotengana, atakuwa ameitia utumwani dhamiri yake na itamsuta yeye mwenyewe.
Watu wa dhamiri na mawazo hawatilii umuhimu isipokuwa misimamo yao mbele ya dhamiri zao na mbele ya watu wema mfano wao ambao wanashirikiana nao kwa kuonyesha mfano na msimamo wa kibinadamu.
Lakini msimamo wao unakuwa hauna thamani mbele ya asiyekuwa na dhamiri ambaye haoni isipokuwa nafsi yake na masilahi yake tu.
Mimi nina yakini kwamba watu wema zaidi ni wale wenye misimsmo ya haki ambao hawajui starehe yoyote isipokuwa ile inayotuliza dhamiri zao.
Unaweza kuuliza
: kuwa watu wengi wanaona raha wanapo pata yale wanayoyataka, ingawaje wao hawamini misingi wala misimamo yoyote; je, hiyo si inamaana wema na raha ni kupata mtu atakacho na ubaya ni kukosa atakacho?
Jibu
:kwanza
: mazungumzo yetu tangu mwanzo ni juu ya watu wenye dhamiri, na hawa unaowasema hawana dhamiri yoyote.
Pili
: watu wengi wanaojionyesha kuwa wanapinga misimamo, huwa kiundani, wanaikubali ndani ya nafsi yao; lakini uovu ulipowashinda walijaribu kuficha kwa kukana yale wanayoyaamini, huku wakijidanganya kwa kusema:
Lau kungelikuwa na msimamo wowote tungelilazimiana nao; sawa na mwenye makosa kukana makosa yake, huku anajua kuwa yeye ni mwenye hatia.
MWISHO WA SURA YA KUMI NA TATU