10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
Sura Ya Kumi Na Nne: Surat Ibrahim
Imeshuka Makka. Ina Aya 52, Imesemekana kuwa Aya mbili katika hizo zimeshuka Madina.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
الر كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِ رَبِّهِمْ إِلَىٰ صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿١﴾
1. Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu gizani uwapeleke kwenye nuru, kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe kwenye njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.
اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَوَيْلٌ لِّلْكَافِرِينَ مِنْ عَذَابٍ شَدِيدٍ ﴿٢﴾
2. Ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali.
الَّذِينَ يَسْتَحِبُّونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا أُولَـٰئِكَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ ﴿٣﴾
3. Wale ambao wamestahabu maisha ya dunia kuliko Akhera na wakawazuilia watu na njia ya Menyezi Mungu na wanataka kuipotosha, hao wamepotelea mbali.
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ فَيُضِلُّ اللَّـهُ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٤﴾
4. Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia. Basi humpoteza amtakaye na humwongoza amtakaye na Yeye ni Mwenye nguvu mwenye hekima.
DINI NI NURU
Aya 1-4
MAANA
Alif Laam Raa
Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:1).
Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu gizani uwapeleke kwenye nuru, kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe kwenye njia ya Mwenye nguvu Mwenye kusifiwa.
Makusudo ya Kitabu hapa ni Qur’an. Msemo wa tumekuteremshia unaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
. Na makusudio ya idhini ni amri.
Aya inafahamisha kwa uwazi kuwa lengo la msingi la kutumwa Muhammad(s.a.w.w)
na kuteremshwa Qura’n ni kuziweka pamoja nguvu zote za watu na kuwa na mshikamano kwa ajili ya ubinadamu na heri yake na utulivu wake. Kwa sababu kuwatoa watu kwenye giza hakuwezi kukamilika kwa miito na Swala; isipokuwa ni kwa juhudi za pamoja, sio za mtu pekee, dhidi ya ukandamizaji, ujinga, ufisadi na uigizaji wa kipumbavu.
Na kweli Muhammad aliunganisha udugu baina ya maswahaba zake, na akawaingiza roho ya kusafiana nia, mahaba na kujitolea na akawafanya miongoni mwao - wakiwa ni washamba na wajinga-wajumbe wa heri wenye kuelimika na maendeleo.
Kwa mnasaba huu tunagundua kuwa wale matapeli wanaohimiza upotofu kwa kuupa jina la dini, kuwa ni maadui wakubwa wa Mwenyezi Mungu na mtume wake. Kwa sabu dini ni nuru na upotofu ni giza, dini ni njia ya Mwenyezi Mungu mwenye kusifiwa na giza ni njia ya shetani mwenye kulaaniwa. Unaweza kuuliza, kuna Aya isemayo:
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾
Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia. Juz. 10 (9:33)
Unaweza kuuliza
: Dahiri ya Aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu amemtuma Muhammad kwa lengo la kuwa dini yake iwe juu ya dini zote. Sasa kuna wajihi gani wa kuunganisha baina ya Aya hizi mbili (kushinda dini na kutoa gizani)?.
Jibu
:kwanza
: makusudio ya dini katika kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘ili ipate kushinda dini zote,’ ni ushirikina. Hilo linafahamika kutokana na kauli yake: ijapokuwa washirikina wamechukia.
Pili
: kwamba dini zote katika zama za Muhammad zilikuwa ni giza, hata zile dini za mbinguni zilikuwa zimechezewa na mikono ya wapotofu.
Tatu
: Kuwa juu dini ya Muhammad ndio kuwa juu haki ambayo, siku zote iko juu wala haikaliwi. Vyovyote iwavyo ni kwamba misingi yoyote wanayonufaika nayo watu kwa namna yoyote ile, inakutana katika upande huu na dini ya Mwenyezi Mungu na mwito wa Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
.
Ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini
Kauli hii imekaririka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu mara kumi, Na lengo ni kukumbusha kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu na ni mtawala wa vilivyo humo.
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) anataja malipo ya makafiri na sifa zao:
1.Na ole wao makafiri kwa adhabu kali.
Hiki ni kiaga cha Mwenyezi Mungu kwa makafiri kutokana na ukafiri wao, kwamba malipo yao ni maangamizi na adhabu. Razi anasema: “Hakika amewahusu kwa ole wao, kwa sababu watakuwa katika adhabu kali wakisema ole wetu.”
2.Wale ambao wamestahabu maisha ya dunia kuliko Akhera.
Huu ndio wasifu wa kwanza wa makafiri; kwamba wao wameathirika na batili kuliko haki, dhulma kuliko uadilifu na ufisadi kuliko wema. Kila anayekuwa hivyo basi yeye ni kafiri au anakutanishwa na makafiri katika vitendo vyake, naye anastahiki laana na adhabu, kama wanavyostahiki makafiri; ajapo swali, akufunga na akahiji.
3.Na wakawazulia watu na njia ya Mwenyezi Mungu.
Wanawazulia watu na njia ya haki na uongofu, wakawa kwa hilo ni wenye kupotea na wenye kupoteza, wafisadi na wenye kufisidisha.
4.Na wanataka kuipotosha, hao wamepotelea mbali.
Neno upotofu linaashiria kuwa wao wanafikia malengo yao kwa njia kombokombo na za haramu; kama vile uwongo, utapeli, njama na kusaidiana na mataghuti. Wasifu huu hauhusiki na washirikina na makafiri peke yao; kwani Waislamu wengi wanasema uwongo, wanafanya hiyana na kupanga njama pamoja na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa wananchi dhidi ya viumbe wa Mwenyezi Mungu na nyenzo zao. Hawa ni wapotevu zaidi na waliopotea njia.
Makusudio ya upotevu uliombali, ni kuwa wao wamezama kwenye upote- vu mpaka wakafikia mwisho wake.
Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia waweze kumfahamu na litimie lengo la risala yake.
Lau kungelikuwa na Lugha inayoweza kufahamika na watu wote, basi angelitumwa nayo Muhammad(s.a.w.w)
, kwa sababu yeye ni Mtume wa watu wote sehemu zote na wakati wote.
Hata hivyo ni lazima ifahamike kuwa kuna tofauti baina ya kusema Tumemtuma kwa lugha ya watu na kusema Tumemtuma kwa watu wa lugha yake. Tamko la kwanza halizuiwii kuwa mjumbe wa wote na tamko la pili linahusika na watu wake tu. Angalia Juz. 12 (12:2).
Mwenyezi Mungu aliwatuma wajumbe wake kwa waja wake ili awaokoe kutokana na ujinga na upotevu. Basi mwenye kuwasikiliza na akatii, ameongoka na mwenye kuachana nao akaasi basi ni mpotevu. Kwa hiyo uon- gofu unapimwa kwa kumtii Mwenyezi Mungu na upotevu kwa kumwasi.
Na lau kama Mwenyezi Mungu hakuweka sharia wala kuwatuma mitume basi kusingelikuwa na twaa na maasi wala uongofu na upotevu, Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ameweka sharia akatuma mitume. Kwa hiyo natija ya hayo ni twaa na maasi, uongovu na upotevu.
Kwa kuzingatia hivi ndipo ikafaa kunasibisha upotevu na uongofu kwake Yeye Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka utukufu wake Angalia Juz.1 (2:26) na Juz. 5 (4: 88).
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا أَنْ أَخْرِجْ قَوْمَكَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَذَكِّرْهُم بِأَيَّامِ اللَّـهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ ﴿٥﴾
5. Hakika tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu kuwa watoe watu wako kutoka gizani kwenda kwenye nuru, Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.
وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ أَنجَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ وَيُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ ﴿٦﴾
6. Na Musa alipowaambia watu wake: “Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, alipowaokoa na watu wa Firauni walipowapa adhabu mbaya na wakiwachinja watoto wenu wa kiume na wakiacha hai watoto wenu wa kike, Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa kutoka kwa Mola wenu.”
وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ ﴿٧﴾
7. Na alipotangaza Mola wenu: Mkishukuru nitawazidishia na mkikufuru basi adhabu yangu ni kali.
وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿٨﴾
8. Na alisema Musa: mkikufuru nyinyi na waliomo duniani wote, hakika Mwenyezi Mungu ni mkwasi mwenye kusifiwa.
TULIMTUMA MUSA
Aya 5-8
MAANA
Hakika tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu kuwa watoe watu wako kutoka gizani kwenda kwenye nuru.
Maneno yamerudi tena kwa Musa
na Waisrail ambao walimtoa roho. Mazungumzo yamewarudia wao na yamekaririka mara kadhaa. Mimi sijui siri ya kukaririka mazungumzo yanayowahusu wao kuliko wengine isipokuwa ni kwamba wao wamevuka mipaka ya kiutu kitabia na kivitendo; kama nilivyodokeza mwanzoni. Mimi sifichi kuwa ninaona uzito sana nikifasiri Aya zilizo na jina la Waisrail.
Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu.
Siku zilizo dhahiri zaidi na zenye neema juu yao ni zile walizookolewa na adhabu ya Firauni na kukombolewa kutoka utumwani.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa kila mwenye kusubiri mwenye kushukuru.
“Vumilia mitihani yako kwa kutumaini nusura yako”
Makusudio ya hayo ni hayo ya ukumbusho. Na makusudio ya ishara hapa ni mazingatio na mawaidha. Ilivyo ni kuwa mwenye kuzingatia na akawaidhika ndiye mumin wa kweli anayeshukuru wakati wa raha na kuvumilia wakati wa balaa pamoja na kujitahidi kufanya ikhlas.
Na Musa alipowaambia watu wake: “Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, alipowaokoa na watu wa Firauni, walipowapa adhabu mbaya na wakiwachinja watoto wenu wa kiume na wakiacha hai watoto wenu wa kike. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa kutoka kwa Mola wenu.
Musa
aliwakumbusha wana wa Israil aliyowafanyia Firauni-kuwachinja watoto wao wa kiume na utumwa. Na akawakumbusha neema ya kuepukana na hayo na akawaamrisha wamkumbuke Mwenyezi Mungu na wamshukuru. Lakini wao hawakumshukuru wala kumkumbuka; bali walimkufuru Mwenyezi Mungu na wakaikana neema yake wakamuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wao Musa kwa kumwambia: Tuonyeshe Mungu waziwazi, Nenda wewe na Mola wako mkapigane.
Walipowapitia watu wakiabudu masanamu wakamwambia Musa tufanyie Mungu kama huyu wao; kisha wakaabudu ndama.
Hayo ndiyo malipo ya kumlipa Mungu aliyewaokoa na adhabu ya Firauni. Musa alipokata tamaa nao na kuona dhiki kubwa alimwelekea Mwenyezi Mungu na kusema:
قَالَ رَبِّ إِنِّي لَا أَمْلِكُ إِلَّا نَفْسِي وَأَخِي فَافْرُقْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ ﴿٢٥﴾
Ewe Mola wangu! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu; basi tutenge na watu hawa mafasiki Juz.6 (5:25)
Kuna maajabu gani baada ya hayo ikiwa Mayahudi wataikana neema ya waislamu kwao siku walipokataliwa na ulimwengu, ambapo hakukuwa na Amerika wala Uingereza au Ujerummani ya magharibi kuwafanya wao ni madalali na mbwa wa kulinda ukoloni na u-Nazi, Umepita mfano wake katika Juz.1 (2:49).
Na alipotangaza Mola wenu: Mkishukuru nitawazidishia na mkikufuru basi adhabu yangu ni kali.
Makusudio ya kukufuru hapa ni kumuudhi yule mneemeshaji na kuzikana neema zake, kwa sababu mazungumzo yanahusiana na waisrail kukana neema za Mwnyezi Mungu. Wamesema wafasiri wengi kuwa Mwenyezi Mungu akimneemesha mja wake na akashukuru na akamkiri Mwenyezi Mungu kwazo, basi Mwenyezi Mungu atamdumisha nayo na kumzidishia. Wamesema hivi kwa kuchukulia kauli mashuhuri: “Shukrani zinadumisha neema.”
Tuonavyo sisi ni kwamba makusudio ya kuzidi neema ni kuzidi hiyo neema Akhera si duniani, kwa sabubu ni uhakika kuwa makusudio ya adhabu kali ya kukufuru neema ni adhabu ya Akhera, kwa hiyo malipo ya kushukuru vilevile yatakuwa ni Akhera. Imethibiti kutoka kwa Mtume kwamba yeye alifanya sawa kumpa mwema na muovu. Imam Ali amesema: “Mali ingelikuwa yangu ningelifanya sawa; vipi isiwe hivyo na mali yote ni ya Mwenyezi Mungu”
Zaidi ya hayo tunashuhudia mali nyingi inarundikana kwa mataghuti kadiri wanvyozidi uasi na kupetuka mipaka. Ndio! Kama ingelikuwa makusudio ya kushukuru ni kuichunga mali, kuipangia vizuri na kuizalisha, basi wafasiri wangelikuwa na njia ya kusemea, lakini hiyo ni kinyume na dhahiri ya Aya ilivyo na wala hakuna aliyewahi kusema hivyo, hata hao wafasiri wenyewe.
Na alisema Musa: “Mkikufuru nyinyi na waliomo duniani wote, hakika wenyezi Mungu ni mkwasi mwenye kusifiwa.”
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu si mwingine, na kujitosheleza ni kwake Yeye si mwingine. Musa alisema kauli hii kutokana na kukata kwake tamaa ya kuongoka Waisrail.
أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَبَأُ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَالَّذِينَ مِن بَعْدِهِمْ لَا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا اللَّـهُ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرَدُّوا أَيْدِيَهُمْ فِي أَفْوَاهِهِمْ وَقَالُوا إِنَّا كَفَرْنَا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ وَإِنَّا لَفِي شَكٍّ مِّمَّا تَدْعُونَنَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ ﴿٩﴾
9. Je haziukuwafikia habari za walio kabla yenu: Kaumu ya Nuh na A’d na Thamud na walio baada yao? Hakuna awajuaye illa Mwenyezi Mungu, Waliwajia mitume wao kwa hoja zilizo wazi. Wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao. Na wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyotumwa na hakika sisi tuna shaka kubwa ya mnayotuitia.
قَالَتْ رُسُلُهُمْ أَفِي اللَّـهِ شَكٌّ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَدْعُوكُمْ لِيَغْفِرَ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُؤَخِّرَكُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى قَالُوا إِنْ أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا تُرِيدُونَ أَن تَصُدُّونَا عَمَّا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا فَأْتُونَا بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿١٠﴾
10. Mitume wao wakasema: “Je kuna shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi? Anawaita ili apate kuwaghufiria dhambi zenu na anawapa muhula mpaka muda uliowekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Mnataka kutuzuwia na waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu, Basi tuleteeni hoja iliyo wazi.
قَالَتْ لَهُمْ رُسُلُهُمْ إِن نَّحْنُ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَمُنُّ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَمَا كَانَ لَنَا أَن نَّأْتِيَكُم بِسُلْطَانٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١١﴾
11. Mitume wao wakawaambia: “Sisi si chochote ila ni wanadamu kama nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu humneemesha amtakaye katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kuwaletea dalili isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.
وَمَا لَنَا أَلَّا نَتَوَكَّلَ عَلَى اللَّـهِ وَقَدْ هَدَانَا سُبُلَنَا وَلَنَصْبِرَنَّ عَلَىٰ مَا آذَيْتُمُونَا وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُتَوَكِّلُونَ ﴿١٢﴾
12. Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu na hali yeye ametuongoza kwenye njia yetu na hakika sisi tutavumilia mnayotuudhi, na kwa Mwenyezi Mungu nawategemee wenye kutegemea.
JE HAZIKUWAFIKIA HABARI
Aya 9-12
MAANA
Je haziukuwafikia habari za walio kabla yenu: Kaumu ya Nuh na A’d na Thamud na walio baada yao? Hakuna awajuaye illa Mwenyezi Mungu.
Mfumo wa maneno unaonyesha kuwa haya ni maneno kutoka kwa Nabii Musa
kwenda kwa wana wa Israil, sio kutoka kwa Muhammad(s.a.w.w)
kwenda kwa washirikina wa kiarabu au wengineo, kama ilivyosemekana.
Maana ni kuwa Nabii Musa anawaambia Waisrail kuwapa mawaidha na kuwahadharisha kuwa mumesikia tufani ya Nuh na majanga yaliyowapitia watu wa A’d na Thamud na mengineyo zaidi ya hayo ambayo hajui idadi yake isipokuwa Mwenyezi Mungu? Aliwafanyia hayo Mwenyezi Mungu kwa sababu wao waliasi Mitume na wakafanya ukaidi. Je, hamzingatii na kupata mawaidha kwa umma zilizotangulia? Musa aliwaambia haya na zaidi watu wake, lakini Israil ni ileile ya mwanzo na ya mwisho.
Waliwajia mitume wao kwa hoja zilizo wazi.
Kila mtume anayetoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa waja wake hana budi kuwa amepewa hoja mkataa zinazofahamisha utume wake; kama vile balozi anavyoleta makaratasi ya kumjulisha kutoka kwenye serikali yake iliyomchagua kuwa balozi wake. Kwa hiyo basi inafahamisha kuwa makusudio ya hoja zilizowazi ni miujiza inayofahamisha juu ya unabii na utume wao.
Wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao.
Waliorudisha ni watu wa Nuh na waliokuwa baada yao. Kurudisha mikono vinywani mwao ni fumbo la kukataa sana; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
عَضُّوا عَلَيْكُمُ الْأَنَامِلَ مِنَ الْغَيْظِ ﴿١١٩﴾
“Huwaumia vidole kwa hasira” Juz.4 (3:119)
Na wakasema: “Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyotumwa na hakika sisi tuna shaka kubwa ya mnayotuitia.
Washirikina walitia shaka au walidhihirisha shaka katika ukweli wa mitume wao na hapo mwanzo walikuwa wakiwakubali kuwa ni wakweli na wenye ikhlasi. Kwanini? Si kwa lolote ila ni kuwa manabii waliwataka walazimiane na haki na uadilifu na kuacha dhulma na batili. Haya hasa ndio mantiki ya wale wanaoangalia masilahi yao tu; leo wanayakana yale waliyoyakubali jana na kinyume chake. Siri ya hilo inakuwa katika faida na chumo; wao wako pamoja nayo popote ilipo na itakapokuwa.
Mitume wao wakasema: “Je kuna shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi?
Ni ajabu ya maajabu kutia shaka mahali pa imani na kuamini mahali pa shaka. Walimpinga Muumba wao wakaamini mawe, yanayokojolewa na mambwa, na kuyaabudu.
Anawaita ili apate kuwaghufiria dhambi zenu.
Mwenyezi Mungu ametukuka! Angalia ukarimu wake na upole wake, anawaita waja wake kwenye msamaha wake na rehema yake na anawatakia yale yanayowanufaisha.
Na anawapa muhula mpaka muda uliowekwa,
wala hana haraka ya kuwaadhibu, bali anawapa muda ili warejee kwenye uongofu.
Wakasema: “Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi.
Kauli hii inafahamisha fikra yao kwamba watu wa kawaida hawafai kushika uongozi wa juu, hata kama watakuwa na ikhlasi, ukweli, na kujitolea kwa kiwango cha juu.
Mnataka kutuzuwia na waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu.
Kwa hiyo baba zao ni watukufu zaidi ya Mwenyezi Mungu na kufuata kwao upotevu ni haki zaidi ya twaa ya Mwenyezi Mungu; hata kama baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawaongoki.
Basi tuleteeni hoja iliyo wazi.
Mitume waliwajia na hoja wazi na muujiza unaofahamisha kuhusu ukweli, lakini washirikina walitaka miujiza maalum ambayo Mwenyezi Mungu aliashiria kwa kusema:
لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ أَوْ جَاءَ مَعَهُ مَلَكٌ ﴿١٢﴾
Mbona hakuteremshiwa hazina au wakaja naye Malaika? Juz, 12 (11:12)
وَقَالُوا لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ تَفْجُرَ لَنَا مِنَ الْأَرْضِ يَنبُوعًا ﴿٩٠﴾
Na wakasema: hatutakuamuini mpaka utuchimbulie chemchem katika ardhi hii au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu na utupitishie mito kati yake ikimiminika (17:90)
wao wanataka miujiza, lakini kupitia tumboni sio akilini.
Mitume wao wakawaambia: “Sisi si chochote ila ni wanadamu kama nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu humneemesha amatakaye katika waja wake.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima na kwa vile yeye ni mwenye hekima na mjuzi, basi hamneemeshi kwa risala yake ila yule aliye kufu nayo mwenye sifa za kuichukua na kutekeleza:
اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ﴿١٢٤﴾
Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake” Juz.8 (6:124)
Wala sisi hatuwezi kuwaletea dalili isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.
Angalia katika Juzuu hii (13: 38), Juz.7 (6:37) na Juz.1 (2:118).
Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu na hali yeye ametuongoa kwenye njia yetu na hakika sisi tutavumlia mnayotuudhi; na kwa Mwenyezi Mungu nawategemee wenye kutegemea.
Tunayafupiliza maana, ingawaje yako wazi, kuwa Mitume waliwaambia washirikina: sisi tunafikisha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na tunamlingania Yeye; hatujali yule atakayekataa wala maudhi yatakayotupata katika njia hii. Kwa sababu sisi tunamtegemea Mola wetu na ubainifu wa jambo letu. Swali hili la: ‘Tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu.’ linafahamisha kwamba mitume hawaoni kitu isipokuwa Mwenyezi Mungu.