12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU
وَقَالَ الشَّيْطَانُ لَمَّا قُضِيَ الْأَمْرُ إِنَّ اللَّـهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ الْحَقِّ وَوَعَدتُّكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيْكُم مِّن سُلْطَانٍ إِلَّا أَن دَعَوْتُكُمْ فَاسْتَجَبْتُمْ لِي فَلَا تَلُومُونِي وَلُومُوا أَنفُسَكُم مَّا أَنَا بِمُصْرِخِكُمْ وَمَا أَنتُم بِمُصْرِخِيَّ إِنِّي كَفَرْتُ بِمَا أَشْرَكْتُمُونِ مِن قَبْلُ إِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٢﴾
22. Na shetani atasema itakapokatwa hukumu: “Hakika Mwenyezi Mungu aliwaahidi ahadi ya kweli nami nikawaahidi sikuwatimizia. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipokuwa niliwaita mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe, Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu wala nyinyi hamuwezi kuwa watetezi wangu, Mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha, Hakika madhalimu wana adhabu chungu.
وَأُدْخِلَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِمْ تَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ ﴿٢٣﴾
23. Na wale ambao wameamini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani (Pepo) ambayo hupita mito chini yake.
MIADI YA MWENYEZI MUNGU
Aya 22-23
HOTUBA YA SHETANI
Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu fikra ya Iblisi na Shetani, mwan- zoni mwa Juzuu ya kwanza na katika Juz.5 (4:38) na katika Aya nyingine zinazozungumzia shetani tumezungumzia kwa ujumla.
Hapa tunarudia kwa upana zaidi; kwa sababu Aya tuliyo nayo ndiyo iliyowazi zaidi kuonyesha dalili za kuweko shetani na kwamba ni hakika yenye kuthibiti; ingawaje haikueleza vile alivyo. Tutaeleza njia zinazoambatana na Aya hii, kama ifuatavyo:
1- Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemtaja shetani, katika Kitabu chake Kitakatifu, kwa ibara mbali mbali. Mara nyingine anasema, Mtukufu, kuwa shetani ni katika aina ya watu na majini; kama pale aliposema:
شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ﴿١١٢﴾
“Mashetani watu na majini Baadhi yao wanawapa wenzao maneno ya kupambapamba kuwahadaa.” Juz.8 (6:112).
Aya hii inaashira kwamba kila kauli ambayo dhahiri yake ni rehema na undani wake ni adhabu, basi hiyo ni kazi ya shetani, hata ikiwa imesemwa na nani.
Mara nyingine anasema Mwenyezi Mungu kuwa shetani ana askari na ana kabila; kama ilivyo katika Aya hizi:
وَجُنُودُ إِبْلِيسَ أَجْمَعُونَ ﴿٩٥﴾
“Na majeshi ya ibilisi yote” (26:95)
يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ يَنزِعُ عَنْهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوْآتِهِمَا إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ ﴿٢٧﴾
“Enyi wanaadamu! shetani asiwatie katika fitina, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo) akiwavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni, Juz.8 (7:27).
Aya hizi zinafahamisha kuwa mashetani hawana idadi kwa wingi na kwamba wao hawaonekani kwa macho wala kuguswa kwa mkono.
Mara ya tatu Mwenyezi Mungu anasema mashetani wana marafiki na wasimamizi; kama ilivyo katika Aya hizi:
وَمَن يَكُنِ الشَّيْطَانُ لَهُ قَرِينًا فَسَاءَ قَرِينًا ﴿٣٨﴾
“Na ambaye shetani amekuwa ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya, Juz,5 (4:38).
فَقَاتِلُوا أَوْلِيَاءَ الشَّيْطَانِ ﴿٧٦﴾
“Basi piganeni na marafiki wa shetani” Juz.5 (4:76)
Tamko hili peke yake linafahamisha kuwa kupigana jihadi na wapotufu ni lazima na wajib, wajapokuwa ni waislamu. Mara ya nne, Mwenyezi Mungu, ambaye imetukuka hekima yake na maneno yake, anasema:
هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَىٰ مَن تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ ﴿٢٢١﴾ تَنَزَّلُ عَلَىٰ كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ ﴿٢٢٢﴾
“Je, niwaambie nani wanawashukia Mashetani? Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi (26: 221-222).
Inafahamisha Aya hii kuwa Mashetani ni wale waongo wazushi.
Ama wadhifa wa shetani na askari wake, kama ulivyoelezwa, ni kupoteza na kudanganya ili kuzuia njia ya haki na kheri, kwa nguvu na kulazimisha; isipokuwa ni kwa wasiwasi, kupambapamba na kudanganya.
Kwa ajili hii, tunasema na tunaendelea kusema kwamba jambo lolote linalompambia mtu kufanya uovu na kumuhimiza shari na ufisadi kwa njia ya hadaa na shauku, basi hilo ni shetani aliyefukuzwa na ibilisi mlaanifu ni sawa iwe ni mtu, mali, jaha, kitabu, gazeti, wasiwasi, mazungumzo ya ndani ya nafsi au kitu chochote kingine kinachoonekana au kisichoonekana.
Hii ndio picha ya shetani iliyoakisi katika akili zetu, tukiwa tunafuatilia na kuzifikiria Aya za Mwenyezi Mungu katika Kitabu chake, tukiziamini pamoja na mitume wa Mwenyezi Mungu.
Mengineyo yasiyokuwa hayo, katika aina na ufafanuzi, tunaiachia elimu ya Mwenyezi Mungu; wala sisi hatukalifiwi nayo au kuulizwa nayo. La wajibu kwetu ni kutohadaika, kutojiingiza katika matamanio na kuacha kuwasikiliza wadanganyifu na wapotevu. Kikitutokea kitu katika hayo, basi tumkumbuke Mwenyezi Mungu kwa ahadi na miadi yake: “Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye, Hakika wale wanye takua zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka, Juz.9 (7:200-201), Rudia huko.
2- Katika nafsi ya binadamu kuna matamanio na silika, navyo ni vitenda- kazi vinavyopelekea kumuasi Mwenyezi Mungu na kuhalifu amri zake, kwa sababu vinakuja kutoka ndani sio nje na kutoka batini sio dhahiri. Kwa hiyo ikiwa ndani mwa mtu hamna nguvu kubwa na ngumu itakayomzuia kupondokea kwa ashetani na kudhibiti ukaidi wake, basi mtu bila shaka atakuwa amepigwa mwereka na matamanio.
3-Na shetani atasema itakapokatwa hukumu.
Kila kitu, isipokuwa Mwenyezi Mungu, kina mwanzo na mwisho. Inawezekana mwanzo wenyewe ukaonekana, kwa dhahiri, ni heri na mwisho ukaonekana, kiuhakika, ni shari na kinyume chake. Kwa ajili hii haifai kukihukumu kitu kwa dhahiri yake na mwanzo wake, maadamu mwisho wake uko kwenye elimu ya ghaibu.
Watu walimfurahia Qarun alipowatokea na kipambo chake na wakasema: Hakika yeye ni mwema na mtu adhimu. Ardhi ilipommeza yeye na nyumba yake, walisema ni mtu mbaya na muovu.
Dunia ni mwanzo na Akhera ni mwisho. Huko zitafunuka pazia na vifuniko; atajulikana kila mtu mwishilio wake, ambapo hakutakuwa na kombokombo wala kufungwafungwa. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Itakapokatwa hukumu’
4-Hakika Mwenyezi Mungu aliwaahidi ahadi ya kweli nami nikaawahidi sikuwatimizia.
Ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ufufuo, hisabu na malipo:
فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾
Kwa haki ya Mola wako! Tutawauliza wote yale waliyokuwa wakiyatenda (15:92-93).
Ama ahadi ya shetani ni kupinga ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa haku- na hisabu wala ufuo wala Pepo na moto. “Hakuna kingine ila maisha yetu ya dunia, wala sisi hatutafufuliwa, Jz.7 (7:29).
Haya ndiyo anayoyasema shetani kuwaambia marafiki zake hapa duniani, palipo na kupindisha pindisha mambo na kudanganya, lakini huko Akhera hakuna kitu isipokuwa haki na uadilifu; hata shetani mwenyewe ataji- tokeza wazi na uongo wake, akiri mwenyewe kwa kauli yake kuwa mwanzo alikuwa akiwafundisha watu uongo na uzushi.
5-Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipokuwa niliwaita mkaniitikia.
Kabisa! Shetani anakubali mwenyewe kuwa hana uwezo wala nguvu yoy- ote isipokuwa vitimbi na hadaa. Wala hawamwitikii isipokuwa wale wad- haifu wa akili, nafsi na imani. Kauli yake hiyo shetani ni ile aliyoambiwa na Mwenyezi Mungu:
إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ ﴿٤٢﴾
Hakika waja wangu wewe hutakuwa na mamlaka nao, isipokuwa wale wapotofu waliokufuata (15:42).
6-Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe.
Ikiwa ni ole wake yule aliyekufurishwa na Namrudi, itakuwaje kwa yule aliyekufurishwa na Iblisi? Ikiwa watu wanajilinda na shetani itakuwaje yule anyemtaka huyo shetani amlinde.
Huu ndio mwisho wa yule anayeidharau haki na watu wema kusaidia ufisadi na wafisadi na mwenye kufuata mlio. Tumewaona wengi katika mashetani watu wakiwahadaa walio wadhaifu, wanawaghuri kwa kueneza vurugu. Hata yakiwapata yale waliyoyafanya wenyewe, mashetani wao huwaambia yale yale atakayowaambia Ibilisi wafuasi wake siku ya hisabu na malipo.
7-Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu wala nyinyi hamuwezi kuwa watetezi wangu
Yaani shetani kesho atawaambia wafuasi wake: mimi siwatoshelezi na kitu chochte, wala nyinyi pia hamnitoshelezi. Mimi na nyinyi hatuna mawasiliano yoyote.
Mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha.
Ibilisi anawaambia wale wale waliotikia mwito wake: mlinitii katika yale niliyowalingalia, mkanifanya ni mshirika wa Mwenyezi Mungu katika wajibu wa twaa, na mimi ninajiepusha na shirki na yale mliyoyashirikisha; hata kama mtanifanya ni mshirika wa Mwenyezi Mungu.
Hakika madhalimu wana adhabu chungu.
Hii ni jumla nyingine inayoanza, si katika maneno ya Ibilisi, ikiwa na maana ya kutoa miadi. Inawezekana kuwa ni mwishilio wa hotuba ya Ibilisi.
Ajabu ni yaliyoelezwa na baadhi ya wafasiri kwamba Ibilisi atatoa hotuba yake hii kwa watu wa motoni kwenye mimbari atakyowekewa huko! Kama ni hivyo basi, itabidi awekewe spika kubwa, kwa sababu wasikilizaji, ambao ni jeshi lake, ni wengi kuliko idadi ya mchanga.
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani (Pepo) ambayo hupita mito chini yake.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja wapotevu na adhabu yao, sasa anataja waongofu wenye msimamo na malipo yao; kama iilvyo kawaida ya Qur’an. Umepita mfano wake katika Juz. 11 (10:9).
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ﴿٢٤﴾
24. Je, hukuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri; kama mti mzuri, mizizi yake ni imara na matawi yake yako mbinguni.
تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٥﴾
25. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الْأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٍ ﴿٢٦﴾
26. Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu uliong’olewa juu ya ardhi, hauna uimara.
يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ ﴿٢٧﴾
27. Mwenyezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera, na anawapoteza madhalimu; na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
NENO JEMA NA NENO OVU
AYA 24-27
MAANA
Je, hukuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri, kama mti mzuri.
Imesemekana kuwa maana ya neno zuri hapa ni tamko la Tawhidi: La ilaa-ha illa llah ‘Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hapana mwenye shaka kuwa Tawhid ndio msingi wa haki na chimbuko lake.
Ni kutokana na Tawhid na ikhlasi ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio tunaweza kulifasiri neno zuri kwa kila neno linalowanufaisha watu na kuwapatia kheri na utengeneo kwa namna moja au nyingine; ni sawa liwe ni neno la dini au sharia, elimu au falsafa na hata fasihi na fani. Mtu yeyote ambaye watu watanufaika na kauli yake au kitendo chake atakuwa, kwa upande huu, anakutana na misingi ya Uislamu na dini, kwa namana yoyote atakavyokuwa.
Kauli na neno bora zaidi ni neno la mapinduzi na kelele za hasira mbele ya mtawala jeuri na wale wanaomsaidia, miongoni mwa vibaraka na wanoji- weka nyuma. Kwa sababu wao ndio asili ya ugonjwa na chimbuko la balaa.
Amesema Imam Ali
:“Haikuwa kazi yoyote nzuri na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu katika kuamrisha mema na kukataza mabaya ila ni kama upumuo katika lindi la bahari na kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu hakukurubiwi na ajali wala hakupungukiwi na riziki na bora yake kabisa ni tamko la usawa mbele ya kiongozi jeuri.”
Kwa sababu kiongozi huyo ndio chimbuko la kila uovu; Kwa hiyo mwenye kumkabili na akampinga atakuwa ameupiga vita uovu wote.
Kuna Hadith kadha za Mtume Mtukufu(s.a.w.w)
zenye maana ya kauli hii ya Imam Ali, Kila kitokacho kwa Ali Amirul-muminin ni miali ya jua la Muhammad bwana wa viumbe wote.
Hakuna kitu kinachofahamisha kuwa makusudio ya neno zuri ni neno lenye faida na manufaa kuliko kufananishwa kwake na mti mzuri ambaomizizi yake ni imara
haungolewi na kimbungana matawi yake yako mbinguni
uko mbali na mabalaa ya dunia na uchafu wake.
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake
sio kuwa mara nyingine unakuwa mkarimu na mara nyingine unakuwa bakhili; kama mfanya biashara wa nipe nikupe, Huu unatoa tu wakati wote.
Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
Hufananisha maana ya ndani kwa maana ya dhahiri ili watu wafahamu njia ya uongofu wapate kuifuata na njia ya uongofu wapate kuiepuka.
Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu.
Kila neno linalodhuru watu wala lisiwanufaishe; hilo ni lenye kulaaniwa; ni sawa liwe linatokana na Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu; awe wa hali ya juu au mlalahoi. Bali kunyamazia batili kunahisabika ni katika madhambi makubwa. Kuna hadithi inayosema: “Mwenye kunyamazia haki ni shetani bubu.”
Ghandi alimwandikia Taghore “Hakika wewe ni mshairi adhimu lakini unacheza na nyumba inaungua nyimbo nzuri nzuri hazimshibishi mwenye njaa wala kumponyesha mgonjwa”
Ulion’golewa juu ya ardhi, hauna uimara.
Huu ni mfano sahii kabisa wa batili na watu wake wanojifanya wakubwa na wajinga wakidhaniwa kuwa wao ni watu wazito kumbe ni kama mti tu uliosimama bila ya mizizi, mara moja unaweza ukalala chini unapopigwa na upepo.
Mwenyezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera.
Makusudio ya wale walioamini sio waliosema tumemwamini Mungu na siku ya mwisho tu, kisha wasiisimamishe haki na kuipinga batili; isipokuwa makusudio ya wale walioamini ni wale aliowakusudia Mwenyezi Mungu katika kauli yake: “Hakika waumini ni wale tu walio mwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho; kisha wasiwe na sahaka na wakapigania njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao” (49:15)
Lakini wakidai tu kumwamini Mwenyezi Mungu kisha wasiizuie dhulma na ufisadi kwa ushujaa, basi hao ni wenye shaka sio waumini.
Maana ya kuwaimarisha kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa habari katika Kitabu chake kupitia Mtume wake kuwa wao wako katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye ndiye mlezi wao na msimamizi wao, mwenye kuwahifadhi na kuwanusuru; kama alivyo washujaisha na kuwasifu kwa ukweli na ikhlasi na mengineyo katika fadhila. Ama kuwaimarisha katika maisha ya akhera kwa kauli thabiti ni kauli YakeMwenyezi Mungu:
يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ ﴿٦٨﴾
Enyi waja wangu! Hamna hofu leo wala nyinyi si wenye kuhuzunika” (43:68).
Na anawapoteza madhalimu
kwa kufuru yao na utwaghuti wao.
Mara nyingi Qur’an hutumia neno dhulma kwa maana ya kufuru na shirki, lakini makusudio ya dhulma hapa ni kuidhulumu mtu nafsi yake kwa kufuru na kumdhulumu mwingine kwa uadui na uzushi; kama ambavyo makusudio ya upotevu hapa ni adhabu; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّـهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُّرْتَابٌ ﴿٣٤﴾
Hivyo ndivyo humpoteza Mwenyezi Mungu yule aliyepita kiasi mwenye shaka (40:34).
Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo
katika kumpa thawabu mtiifu na kumwadhibu mfisadi, wala hakuna mwenye kuzuia matakwa yake.
Nikiwa kwenye tafsiri ya Aya hii, nimesoma makala katika gazeti la Al-Ahram la Misr la tarehe 2, February 1969, yenye kichwa cha maneno: “Je ubinadamu utashuhudia kummalizika vita vya Atomic na kuanza vita vya sumu?” Miongoni mwa yaliyomo katika makala hiyo ni: “Imejitokeza silaha mpya hatari zaidi na yenye nguvu kulio silaha za nyuklia.
Silaha hiyo ni ya sumu na kwamba athari yake ni mtu anapoigusa chembe tu, basi viungo vyake vinanywea, macho yanamtoka na kufa papo hapo. Na kwamba Amerika na Uingereza tayari ina viwanda vya kutengeneza silaha hizi na kuzihifadhi mpaka pale zitakapohitajika. Wakati mataifa yakitafuta muafaka wa kummaliza silaha za nyuklia, huku mataifa mawili haya yanatafuta silaha hatari zaidi, kama badili ya mabomu ya Atomic na Haidrojeni.”
Je, imani inaweza kuwa pamoja na nia na maazimio ya kutumia silaha hizi? Je swala za wale wanaowaunga mkono wenye nia hizo na maazimio hayo zitawafaa mbele ya Mwenyezi Mungu?
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ بَدَّلُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ كُفْرًا وَأَحَلُّوا قَوْمَهُمْ دَارَ الْبَوَارِ ﴿٢٨﴾
28. Je, hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru? Na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamivu?
جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا وَبِئْسَ الْقَرَارُ ﴿٢٩﴾
29. Nayo ni Jahannam watakayoiingia, Ni mahala pabaya pa kukaa.
وَجَعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا لِّيُضِلُّوا عَن سَبِيلِهِ قُلْ تَمَتَّعُوا فَإِنَّ مَصِيرَكُمْ إِلَى النَّارِ ﴿٣٠﴾
30. Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze katika njia yake, Sema: Stareheni! Kwani hakika marejeo yenu ni motoni.
قُل لِّعِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا يُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خِلَالٌ ﴿٣١﴾
31. Waambie waja wangu walioamini wasimamishe Swala na watoe katika tulivyowaruzuku kwa siri na kwa dhahiri, kabla ya kuwajia siku isiyokuwa na biashara wala urafiki.
WALIBADILISHA NEEMA YA MUNGU KWA KUFURU
Aya 28 -31
MAANA
Je, hukuwaona wale waliboadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru? Na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamivu? Nayo ni Jahnnam watakayoiingia ni mahala pabaya pa kukaa.
Dhamiri ya wakawafikisha inawarudia viongozi wa kufuru na upotevu. Makusudio ya neema ya Mwenyezi Mungu ni imani na uwongofu. Maana ni kuwa, je, hustajabu ewe Muhammad au ewe msikilizaji na msomaji, hali ya viongozi wa kufuru na upotevu ambao wamehiyari upotevu kuliko uon- gofu na moto kuliko neema, wakiingia humo wao na wafuasi wao, wakawa ndio kuni zake.
Mfano wa Aya hii ni kama kauli yake Mwenyezi Mungu:
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ اشْتَرَوُا الضَّلَالَةَ بِالْهُدَىٰ فَمَا رَبِحَت تِّجَارَتُهُمْ وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ ﴿١٦﴾
“Hao ndio walionunua upotofu kwa uongofu, lakini biashara yao haikupa- ta faida wala hawakuwa ni wenye kuongoka.” Juz.1 (2:16)
Tabariy amenukuu, katika kufasiri Aya hii, kwamba Umar bin Al-Khatab alisema: “Wale ambao wamebadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru ni koo mbili ovu katika maqurayshi: Bani Mughira na Bani Umayya. Ama Bani Mughira mliwatosha siku ya Badr na Bani Umayya watajifurahisha muda mchache tu.”
Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze katika njia yake.
Walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika, wakiwapenda kama kumpenda Mungu na kuwaabudu kama kumwabudu Mungu.
Ilivyo hasa ni kuwa wao walifanya hivyo kwa kukusudia kuongoka si kwa kukusudia kupoteza njia. Kwa hiyo neno kwa ‘ili’ hapa halina maana ya kuwa ndio lengo bali ni matokeo. Maana yanakuwa kwamba washirikina waliabudu masanamu kwa kukusudia kuongoka nayo na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, lakini natija ikawa ni kupotea, kuangamia na kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu. Neno ‘ili’ hapa liko sawa na mfano wa kusema: Amekuja mwenyewe ili afe.
Sema: Stareheni! Kwani hakika marejeo yenu ni motoni.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha mtume wake kuwahadharisha washirikina na mwisho mbaya na kuwaambia kuwa starehe za dunia ni chache hata kama zinawapendeza na Akhera ni ya mwenye takua. Lakini lugha ya haki inafaa kitu kwa wale ambao hawatingishwi na lolote zaidi ya faida na chumo?
Waambie waja wangu walioamini wasimamishe Swala
ambayo mwenye kuiswali inamkumbusha Mungu na kumhadharisha na adhabu na mateso na kumkataza dhambi na makosa
Na watoe katika tulivyowaruzuku kwa siri na kwa dhahiri.
Zaka ni ndugu yake swala. Swala inamkumbusha Mungu na zaka inamkurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Umepita mafano wake katika Juz 3 (2:74).
Kabla ya kuwajia siku isiyokuwa na biashara wala urafiki.
Biashara hapa ni fumbo la fidia. Maana ni kuwa mwenye kutoa mali yake katika njia ya Mwenyezi Mungu atanufaika nayo huko akhera na mwenye kuifanyia ubakhili atakuwa na hasara na adhabu wala haitamfaa siku hiyo ambapo hakutakuwa na fidia wala urafiki, Umepita mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (13:18).