2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ ﴿٢٦﴾
26. Na hakika tulimuumba mtu kutokana udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾
27. Na majini tumewaumba kwa moto wenye joto kali.
وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ ﴿٢٨﴾
28. Na Mola wako alipowaambia Malaika: “Hakika mimi nitamuumba mtu kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ ﴿٢٩﴾
29. Basi nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi muangukieni kumsujudia.
فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ ﴿٣٠﴾
30. Wakasujudu Malaika wote pamoja.
إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ أَن يَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ ﴿٣١﴾
31. Isipokuwa Ibilisi alikataa kuwa pamoja na waliosujudi.
MTU KUTOKANA NA UDONGO
Aya 26 – 31
MAANA
Na hakika tulimuumba mtu kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
Watu wamezungumza mengi sana kuhusu asili ya mtu. Darwin amesema kuwa asili ya mtu ni nyani. Tumefafanua kuhusu dhana ya Darwin na asili ya mtu katika Juz. 8. (7: 11). Hapa tunayarudia maudhui hayo kwa mfumo mwingine:
Maarifa ya kujua mambo yanakuwa tu katika hali zifuatazo:- Majaribio, kushuhudia, akili na wahyi. Ni wazi kwamba, kutokana na utafiti, tunaweza kumjua mtu alivyo. Ama kujua alipatikana vipi na alikuwa katika hali gani, swali hili haliwezi kujibiwa na majaribio.
Tukija kwenye kushuhudia, hakuna mtu aliyeshuhudia uumbwaji wa mtu, wala hakuna kitu, katika vinavyofukuliwa, kinachofahamisha asili ya mtu, Hilo tumelifafanua katika Juz. 8: (7:11–18). Ama tukiuliza akili kuhusu asili ya mtu, ni sawa na kuiuliza hiyo akili, ni nani baba yake fulani, je alikuwa ni mrefu au mfupi? Kwa hiyo basi hakuna kilichobakia katika kuja asili ya kuumbwa mtu isipokuwa ni kwa wahyi tu.
Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an yenye hekima, atakuta baadhi ya Aya zinaasema:
وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ مِنَ الْمَاءِ بَشَرًا ﴿٥٤﴾
Yeye ndiye aliyemuumba binadamu kutokana na maji (25:54).
Nyingine inasema:
كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٥٩﴾
“...ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.” Juz.3 (3:59)
Pia kuna ile isemayo: “Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo.” Juz, 7 (6:2) udongo uliokusudiwa hapa, kutokanana neno la kiarabu twin ni udongo mbichi – machanganyiko wa mchanga na maji.
Aya tuliyo nayo inasema kuwa mtu ameumbwa kutokana na udongo mkavu kwa tope nyeusi zinazoweza kufinyangwa, bila shaka hapo itakuwa ni mchanganyiko wa udongo na maji.
Kwa hiyo basi asili ya mtu ni maji na mchanga alioumbia Mwenyezi Mungu baba wa watu.
Na majini tumewaumba kwa moto wenye joto kali.
Jamaa wamekanusha kuweko majini, Baadhi ya waumini wamefasri majini waliotajwa katika Qur’an kuwa ni viini (microbe) visivyoonekana kwa macho. Wamechukulia neno Jinn kilugha, lenye maana ya kitu kililichofichikana na macho.
Wengine wakasema kuwa majini wapo, Wakatunga vitabu kuhusu idadi yao, miji yao, desturi zao, nembo zao na hata viongozi wao. Pia wakaelezea uwezekano wa jini kumuoa mtu au mtu kumuoa jini.
Sisi tunaamini kuweko majini, si kwa jingine isipokuwa tu wahyi umethibitisha hilo na inakubalika kiakili, Hatumwamini yeyote anayedai kuwa ana mawasiliano au kumuona jini. Hatukubali masimulizi yoyote yanayohusiana nao isipokuwa kwa kutamkwa wazi na wahyi.
Aya hii tuliyonayo imeweka wazi kuwa jini ameumbwa kutokana na moto na pia ile isemayo:
وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾
Na akawaumba majini kwa ulimi wa moto (55:15).
Kwa hiyo sisi tunaamini kuwa asili ya majini ni moto. Lakini ni aina gani ya moto na je, umbile lenyewe lilikuwaje, Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi.
Katika baadhi ya niliyoyasoma ni kuwa wataalamu wamegundua aina ya vidudu ambavyo haviwezi kupata uhai isipokuwa kwenye hewa ya sumu na vingine uhai wake uko kwenye visima vya mafuta na kwenye mwako.
Kwa hiyo kuna uwezekano kuwa kwenye sayari ya Jua kuna viumbe hai vinavyoafikiana na joto la Jua; kama samaki anavyoishi kwenye maji na kipepeo anavyopata rangi ya waridi na kobe kuwa na rangi ya jangwani.
Na Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitamuumba mtu kutokana udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
Mwenyezi Mungu aliwaambia hivi Malaika, lakini Malaika nao wakamawambia Mungu:
Je utaweka humo watakaofanya ufisadi humo na kumwaga damu? Juz,1 (2:30).
Tumeeleza huko kuhusu Malaika kujibizana na Mungu na kwamba aliwa- pa nafasi ya maswali na majibizano yaliyofanana na kupinga; kisha akawafahamisha uhakika kwa njia ya upole. Pengine anaweza kupata funzo yule anayejiona ni zaidi ya wote.
Basi nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu.
Yaani nitakapompa uhai, Angalia Juz, 6 (4: 171 – 173), huko tumefafanua zaidi kuhusu neno roho
Basi muangukieni kumsujudia, Wakasujudu Malaika wote pamoja isipokuwa Ibilisi alikataa kuwa pamoja na waliosujudu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:34).
قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا لَكَ أَلَّا تَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ ﴿٣٢﴾
32. Akasema (Mwenyezi Mungu): Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?
قَالَ لَمْ أَكُن لِّأَسْجُدَ لِبَشَرٍ خَلَقْتَهُ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ ﴿٣٣﴾
33. Akasema (Iblis): “Haiwi mimi kumsujudia uliyemuumba kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.”
قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ ﴿٣٤﴾
34. Akasema (Mwenyezi Mungu): Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa.
وَإِنَّ عَلَيْكَ اللَّعْنَةَ إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٣٥﴾
35. Na hakika itakuwa juu yako laana mpaka siku ya malipo.
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿٣٦﴾
36. Akasema (Iblisi): “Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴿٣٧﴾
37. (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda.
إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ ﴿٣٨﴾
38. Mpaka siku ya wakati maalum.
قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٣٩﴾
39. Akasema (Iblisi): Kwa ulivyonipoteza, basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote.
إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ ﴿٤٠﴾
40. Isipokuwa waja wako waliosafishwa.
قَالَ هَـٰذَا صِرَاطٌ عَلَيَّ مُسْتَقِيمٌ ﴿٤١﴾
41. Akasema (Mwenyezi Mungu): Hii ni njia juu yangu mimi iliyonyooka.
إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ ﴿٤٢﴾
42. Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, isipokuwa wale wapotofu waliokufuata.
وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٣﴾
43. Na hakika Jahannam ndipo mahali pao walipoahidiwa wote.
لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَابٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ ﴿٤٤﴾
44. Ina milango saba, kila mlango una sehemu waliyotengewa.
MUNGU ANAULIZA NA IBLISI ANAJIBU
Aya 32 – 44
MAANA
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamuru Malaika kumsujudia Adam kwa sijda ya kimaamkuzi sio ya kiibada, Wakatii wote, lakini Ibilisi akaasi. Maulamaa wamehitilafiana kuhusu jinsia ya Iblisi, kuwa je, alikuwa Malaika kisha akafukuzwa au alikuwa shetani tangu mwanzo?
Mzozo huu ni tasa. Maadam Ibilisi kwa hali yoyote ni mwenye kulaumiwa na mwenye kufurushwa. Alpojizuia kusujudu Mola Mtukufu alimuuliza:
Akasema (Mwenyezi Mungu): Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?
Je, wewe una cheo zaidi au ni mtukufu sana kuliko waliomsujudia Adam?
Akasema (Iblis): Haiwi mimi kumsujudia uliyemuumba kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
Iblisi aliasi na kufanya jeuri, sio kwa kitu kingine isipokuwa ni ubaguzi wa rangi tu. Na kila mwenye kufanya ubaguzi kwa sababu ya asili yake na jinsia yake, basi ni mwenye kulaaniwa, kufukuzwa na kulaumiwa; sawa na Iblisi.
Akasema (Mwenyezi Mungu): Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa na hakika itakuwa juu yako laana mpaka siku ya malipo.
Humo, ni humo mwenye daraja ya juu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alimfukuza Iblisi kutoka kwenye rehema yake hadi kwenye adhabu yake na akamfanya ni maluuni kwa ndimi zote mpaka siku ya Kiyama, ikiwa ni malipo ya kiburi chake na kuacha kwake kumtii Mwenyezi Mungu.
Akasema (Iblisi): “Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
Alitaka muda huu kwa haja yake aliyoikusudia, tutakayoifafanua mbele(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda mpaka siku ya wakati maalum.
Hiyo ni siku ya kupuliziwa parapanda ambayo inafahamishwa na Aya isemayo:
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ ﴿٦٨﴾
“Na itakapopuziwa parapanda wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini” (39:68)
Akasema (Iblisi): Kwa ulivyonipoteza,
Yaani kwa sababu ya kunitia mtihani wa amri ya kumsujudia Adam ambayo imeniingiza katika upotevu na uasi,basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote, isipokuwa waja wako waliosafishwa.
Iblisi alichukua ahadi ya kuchukua kisasi cha maafa yake kwa kiumbe hiki kilichokuwa ni sababu ya kufukuzwa kwake kutoka rehema ya Mola wake hadi kwenye laana yake.
Akasema (Mwenyezi Mungu): Hii ni njia juu yangu mimi iliyonyooka.
Hii ni ishara ya kujichunga wale wenye ikhlasi kutokana na shetani na upotevu wake.
Juu yangu mimi, yaani ni yenye kuthibiti kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu; mfano kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mola wenu amejilazimisha rehema, Juz, 7 (6:54).
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amejilazimishia kwamba ikhlasi ndiyo njia ya kunyooka. Mwenye kuifuata ataokoka na mwenye kukengeuka nayo ameangamia.
Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, isipokuwa wale wapotofu waliokufuata.
Wale wanaoabudu pesa wakiuza dini na nchi kwa kila atakayetoa pesa. Ama wale wema wenye ikhlasi, hawawezi hata kusogelewa na Iblisi, sikwambii kuwa na mamlaka nao. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz, 8 (7:11- 18).
Na hakika Jahannam ndipo mahali pao walipoahidiwa wote.
Huko kwenye shimo la Jahannam watakutana wote, Iblisi na wafuasi wake. Kila mmoja atamlaani mwenzake na kumkana; mfuaswa atamkana mfuasi, Kwa maelezo zaidi angalia kifungu cha ‘Hotuba ya shetani’ katika Juz. 13 (14:22)
Ina milango saba, kila mlango una sehemu waliyotengewa.
Imesemekana kuwa makusudio ya milango ni milango hasa kwa maana ya tamko lenyewe. Wengine wakasema makusudio ni tabaka na kwamba baadhi ya moto uko juu ya baadhi ya mwingine; na kuwa kila tabaka ina jina lake inalolihusu; kama vile Jahnnam, Jahim, Ladhaa, Saqar, Hutama n.k.
Vyovyote yatakavyokuwa makusudio, hali halisi inajulikana; kwamba maovu yana daraja; kuna yaliyo makubwa ya hatari, yaliyo madogo yasiyo na hatari na yale ya katikati, Kila ovu lina adhabu yake inayolistahili bila ya kuzidi, Tumefafanua katika Juz, 13 (46 – 52), Kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi.
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٤٥﴾
45. Hakika wenye takua watakuwa katika Bustani (Pepo) na chemchemi.
ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ آمِنِينَ ﴿٤٦﴾
46. (Wataambiwa): Ingieni kwa salama mkiwa na amani.
وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na tutaondoa chuki iliyokuwamo vifuani mwao wawe ndugu, juu ya viti wakielekeana.
لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ ﴿٤٨﴾
48. Humo hayatawagusa machovu wala hawatatolewa humo.
نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٤٩﴾
49. Watanabahishe waja wangu ya kwamba mimi ndiye Mwenye kughufiria, mwenye kurehemu.
وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ ﴿٥٠﴾
50. Na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu.
WENYE TAKUA PEPONI
Aya 45 – 50
MAANA
Bada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja adhabu ya wakosefu na wale waliopotea, na kwamba wao watafufuliwa kesho huku nyuso zao zikiwa zimegubikwa na moto tena wakiwa na nguo za moto, amefuatishia kwa kutaja malipo ya wenye takua, wacha Mungu. Kwamba wao watalipwa raha starehe amani na usafi wa kila aina, kwa ufafanuzi ufuatao:
1.Hakika wenye takua watakuwa katika Bustani (Pepo) na chemchemi.
Maisha ni mazuri katika kila kitu, kuanzia vyakula hadi vinywaji na mandhari hadi Hurulaini.
وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ﴿٧١﴾
Kuna vinavyopendwa na nafsi na kufurahiwa na macho (43:71).
2.(Wataambiwa): Ingieni kwa salama mkiwa na amani.
Maisha mazuri ya amani yasiyokuwa na hofu wala huzuni
Na tutaondoa chuki iliyokuwamo vifuani mwao wawe ndugu, juu ya viti wakielekeana.
Hata starehe pia ni safi, hakuna chuki zinazochemka nyoyoni; kama ilivyo kwa watu wa motoni, alipowasifu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: “Kila utakapoingia umma utalaani ndugu zake. Juz.8 (7:38).
3.Humo hayatawagusa machovu wala hawatatolewa humo.
Hakuna ufukara, maradhi, hofu wala chuki, Pia hakuna tabu wala kuchoka, Sifa zote hizi ni za kudumu, haziondoki wala kupungua.
Watanabahishe waja wangu ya kwamba mimi ndiye Mwenye kughufiria, mwenye kurehemu, na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekutanisha, katika Aya mbili hizi, bishara na hadhari, ili muasi asikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu na maghufira yake, bali arejee na atubie kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu na ili awe na hadhari mtiifu kutokana na makosa na ufisadi, na awe mnyenyekevu; wala asijitie majivuno na ghururi. Razi anasema: “Mwenyezi Mungu alipotaja maghufira na rehema alilisisitiza sana kwa matamshi matatu: ‘Hakika mimi, mimi na kuingiza alif na lam katika neno la kiarabu al-ghafur (mwenye kughufiria). Lakini alipotaja adhabu hakusema hakika mimi wala mimi; bali amesema: hakika adhabu yangu.