TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 9745
Pakua: 3144


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9745 / Pakua: 3144
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ ﴿٥١﴾

51. Na watanabahishe kuhusu wageni wa Ibrahim.

إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿٥٢﴾

52. Walipoingia kwake wakasema: “Salaam.” Akasema: “Hakika sisi tunawaogopa.”

قَالُوا لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ ﴿٥٣﴾

53. Wakasema: Usiogope, Sisi tunakubashiria (kupata) kijana mwenye ujuzi.

قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَىٰ أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ ﴿٥٤﴾

54. Akasema: “Mnanibashira na uzee umenishika! Basi mnanibashiria kwa lipi?

قَالُوا بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ ﴿٥٥﴾

55. Wakasema: “Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.”

قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ ﴿٥٦﴾

56. Akasema: “Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.”

قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿٥٧﴾

57. Akasema: “Nini kusudio lenu enyi wajumbe?”

قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿٥٨﴾

58. Wakasema: “Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu.

إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥٩﴾

59. Isipokuwa familia ya Lut, hakika tutawaokoa wote.

إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٦٠﴾

60. Isipokuwa mkewe tumekadiria kuwa miongoni mwa watakaobakia nyuma.

WAGENI WA IBRAHIM

Aya 51 – 60

MAANA

Na watanabahishe kuhusu wageni wa Ibrahim.

Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) na wanotanabahishwa ni waja wa Mwenyezi Mungu waliotajwa katika Aya iliyotangulia. Wageni wa Ibrahim ni Malaika waliokuja kwake.

Walipoingia kwake wakasema: Salaam.

Waliingia kwake wakamsalimia naye akawarudishia salaam; kama ilivy- oelezwa katika Juz. 12: (11:69).

Akasema: Hakika sisi tunawaogopa.

Kwa sababu aliwaletea chakula wakakikataa.

Wakasema: “Usiogope. Sisi tunakubashiria (kupata) kijana mwenye ujuzi, ambaye atakuwa na shani.

وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَاقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١١٢﴾

Na tukamabashiria Is-haq, nabii miongoni mwa watu wema, (37:112).

Akasema: “Mnanibashira na uzee umenishika! Basi mnanibashiria kwa lipi?

Ibrahim hakuyasema haya kwa kutilia mashaka uwezo wa Mwenyezi Mungu wala kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; bali ni kwa kusisitiza ili atulie.

Wakasema: Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.

Malaika walidhani kuwa Ibrahim ni katika wanokata tamaa kutokana na swali lake. Ilifaa wadhanie hivyo, lakini Nabii Ibrahim aliikana dhana yao hiyo Akasema:

Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.

Kauli yake hii ni dalili mkataa kuwa yeye hakuuliza kwa kutilia shaka wala kukata tamaa; bali ni kusisitiza na kuthibitisha. Mahali pengine alisema: “Lakini upate kutulia moyo wangu. Juz.3 (2:260).

Akasema: Nini kusudio lenu enyi wajumbe?

Yaani ni jambo gani muhimu mlilotumiwa zaidi ya bishara mliyonipa.

Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu ambayo ni watu wa Lutisipokuwa familia ya Lut hakika tutawaokoa wote ambao ni watu wake wanomuhusu na wafuasi wake waumini.

Isipokuwa mkewe tumekadiria kuwa miononi mwa watakaobakia nyuma.

Mwenyezi Mungu alimwangamiza pamoja na walioangamia, kwa sababu alikuwa mnafiki akimpangia njama mumewe Lut pamoja na maadui zake washirikina. Umetangulia mfano wa Aya hizi katika Juz .12 (11: 69 – 74)

فَلَمَّا جَاءَ آلَ لُوطٍ الْمُرْسَلُونَ ﴿٦١﴾

61. Basi wajumbe walipokuja kwa familia ya Lut.

قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ ﴿٦٢﴾

62. Alisema: Nyinyi ni watu msiojulikana.

قَالُوا بَلْ جِئْنَاكَ بِمَا كَانُوا فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٦٣﴾

63. Wakasema: “Bali tumekuletea yale waliyokuwa wakiyafanyia shaka.

وَأَتَيْنَاكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٦٤﴾

64. Na tumefika kwako kwa haki na hakika tunasema kweli.

فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَاتَّبِعْ أَدْبَارَهُمْ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ وَامْضُوا حَيْثُ تُؤْمَرُونَ ﴿٦٥﴾

65. Ondoka na Ahali zako na usiku ungalipo nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma, Na mwende mnapoamrishwa.

وَقَضَيْنَا إِلَيْهِ ذَٰلِكَ الْأَمْرَ أَنَّ دَابِرَ هَـٰؤُلَاءِ مَقْطُوعٌ مُّصْبِحِينَ ﴿٦٦﴾

66. Na tukampa wahyi hukumu hiyo, ya kwamba wa mwisho wao ikifika asubuhi atakuwa amekatiliwa mbali.

وَجَاءَ أَهْلُ الْمَدِينَةِ يَسْتَبْشِرُونَ ﴿٦٧﴾

67. Wakaja watu wa mji huo wakifurahi.

قَالَ إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ ضَيْفِي فَلَا تَفْضَحُونِ ﴿٦٨﴾

68. Akasema: “Hakika hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe.

وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَلَا تُخْزُونِ ﴿٦٩﴾

Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.

قَالُوا أَوَلَمْ نَنْهَكَ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٧٠﴾

70. Wakasema: Je hatukukataza na watu.

قَالَ هَـٰؤُلَاءِ بَنَاتِي إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿٧١﴾

71. Akasema: “Hawa binti zangu ikiwa nyinyi ni watendaji.”

لَعَمْرُكَ إِنَّهُمْ لَفِي سَكْرَتِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٢﴾

72. Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao wakimangamanga.

KAUMU YA LUT

Aya 61 – 72

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hukariri visa vya mitume na upinzani uliowa- tokea na jinsi walivyoweza kusimama imara na ujumbe wao, ili watu wapate funzo na mawaidha kutokana na mwisho wa wakadhibishaji ulivyokuwa. Kila lililoelezwa katika Aya hizi tulizo nazo litakuwa limeelezwa kwa ufafanuzi katika sura ya Hud iliyoko katika Juz. 12. Vilevile maelezo ya Nabii Ibrahim(a.s) yaliyopita punde tu. Kwa ajili hii tutafupiliza kufasiri Aya hizi; kama tulivyofupiliza Aya zilizotangulia.

Basi wajumbe walipokuja kwa familia ya Lut.

Malaika walitoka kwa Ibrahim na wakaelekea kwa Lut. Walipofika kwake kwa kuwafikiria kuwa ni wageni, aliona dhiki sana kutokana na uovu wa kaumu yake.

Alisema: “Nyinyi ni watu msiojulikana siwajui wala sijui mnataka nini. Mmeingiaje mjii huu na wenyeji wake wanajulikana wanayoyafanya?

Wakasema: Bali tumekuletea yale waliyokuwa wakiyafanyia shaka na tumefika kwako kwa haki na hakika tunasema kweli.

Malaika walimfichulia Lut hakika yao na umuhimu waliokuja nao ambo ni kuwaangamiza kaumu ya Lut.Walikuwa wakiwaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake. Mtume wao Lut alikuwa akiwahadharisha na kuwaonya na adhabu itakayotokea mbinguni.

Malaika wakamwambia Lut: Tumekuja na adhabu uliyokuwa ukiwahadharisha nayo na kukukadhibisha na kwamba hiyo adhabu itatokea tu.

Ondoka na watu wako na usiku ungalipo nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma, Na mwende mnapoamrishwa.

Baada ya kumpa habari ya kutokea adhabu, alimwamrisha kujiokoa yeye na watu wake. Kwa kutoka usiku kabla ya asubuhi na yeye awe nyuma yao akiwaangalia na kuwatunza na kwamba asigeuke nyuma yeyote asije akaona adhabu akafazaika.

Na tukampa wahyi hukumu hiyo, ya kwamba wa mwisho wao ikifika asubuhi atakuwa amekatiliwa mbali.

Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Lut kwamba kufkia asubuhi atakuwa amewafyeka makafiri hadi wa mwisho wao, hakutabakia hata chembe.

Wakaja watu wa mji huo wakifurahi.

Wale mafasiki walikuja kwa wageni wa Lut wakipeana habari ya furaha kuwa wamepata nyara mpya. Uso wa Lut ukasawijika kwa kuwa hajawajua hasa wageni wake. Akawakabili kwa upole,Akasema: Hakika hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe na mumche Mwenyezi Mungu wala msinihizi.

Aliwahofisha na Mwenyezi Mungu ingawaje kwao si chochote na akawataka wawe na murua kwa kutomfedhehesha na wageni wake ingawaje walikuwa ni watu wasiokuwa na murua wala utu kabisa.

Wakasema: Je hatukukukataza na watu?

Yaani hatukukukataza kukaribisha watu wa nje? Angalia upuzi na ushenzi huu. Eti wao ndio wasiokuwa na kosa na Lut ndiye mwenye kosa, kwa vile wao walimkataza asikaribishe wageni na hakukoma! Je hatukukukataza!

Mantiki haya ya watu wa Lut ndio mantiki ya kila wachokozi. Sikuzote, hawana kipimo isipokuwa matakwa yao na manufaa yao. Wavietnam wamegeuka kuwa ndio wamwaga damu na wavunja amani kwa Wamarikani kwa vile tu wamekataa kutawaliwa na USA.

Waarabu wamekuwa magaidi na wanyama kwa Marekani na Uingereza kwa vile tu wanasema Palestina ni ya Wapalestina sio ya Wazayuni. Dola za kikoloni zinadai usalama na amani wakati zikiwapiga makombora na mabomu ya sumu wanyonge kwenye nchi zao.

Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.

Alileta ibara ya binti zangu, akiwakusudia wanawake wa kaumu yake, kwa sababu Mtume wa umma ni kama baba kwa wanachi wote waume kwa wake.

Lut aliwaambia watu wake waache kuwaendea wanaume na waoe wanawake walio halali, lakini nafsi zao hazioni raha isipokuwa kwa haramu na kupendelea dhambi na uchafu.

Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao wakimangamanga.

Wafasiri wengi wamesema kuwa msemo wa ‘naapa kwa umri wako’ unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekea kwa Muhammad(s.a.w.w) . Wengine wakasema unatoka kwa Malaika kuelekea kwa Lut(a.s) . Huenda hii iko karibu zaidi na dhahiri ya mfumo wa maneno. Maana yoyote yatakayokuwa ni kuwa kaumu Lut walizama kwenye upotevu wala hawakuwa na mwelekeo wa kuongoka kwa namna yoyote atakayokuwa muongozaji.

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُشْرِقِينَ ﴿٧٣﴾

73. Ukelele ukawanyakuwa wakipambaukiwa.

فَجَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ ﴿٧٤﴾

74. Tukaugeuza (mji) juu chini na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْمُتَوَسِّمِينَ ﴿٧٥﴾

75. Hakika katika hayo kuna ishara kwa waaguzi.

وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٍ مُّقِيمٍ ﴿٧٦﴾

76. Na hakika mji huo uko kwenye njia, bado iko.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾

77. Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.

وَإِن كَانَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ لَظَالِمِينَ ﴿٧٨﴾

78. Na hakika watu wa kichakani walikuwa madhalimu.

فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ وَإِنَّهُمَا لَبِإِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿٧٩﴾

79. Kwa hiyo tukawaadhibu, Na miwili hiyo iko katika njia iliyo wazi.

وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ ﴿٨٠﴾

80. Na hakika watu wa Hijr waliwakadhibisha Mitume.

وَآتَيْنَاهُمْ آيَاتِنَا فَكَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ ﴿٨١﴾

81. Na tuliwapa ishaa zetu nao wakazipuuza.

وَكَانُوا يَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا آمِنِينَ ﴿٨٢﴾

82. Na walikuwa wakichonga majumba katika majabali kwa amani.

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُصْبِحِينَ ﴿٨٣﴾

83. Ukelele ukawanyakuwa asubuhi.

فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨٤﴾

84. Hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَإِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ ﴿٨٥﴾

85. Na hatukuiumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki, Na hakika saa itafika, Basi samehe msamaha mzuri.

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ ﴿٨٦﴾

86. Hakika Mola wako ndiye Muumbaji, Mjuzi.

UKELELE UKAWANYAKUA

Aya 73 – 86

MAANA

Ukelele ukawanyakuwa wakipambaukiwa.

Yaani adhabu iliwashukia wakati wa mapambazuko. (mawiyo).

Tukaugeuza (mji) juu chini na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo.

Aya hii imetangulia kwa herufi zake hizi hizi katika Juz. 12. (11:92).

Hakika katika hayo kuna ishara kwa waaguzi.

Makusudio ya waaguzi hapa ni wenye akili ambao wanazingatia na kupata mawaidha.

Na hakika mji huo uko kwenye njia, bado iko.

Yaani athari za mji huo zilikuwako mpaka wakati wa Muhammad(s.a.w.w) na njia ya kwenda huko ilikuwako na kuweza kupitika kwa kila mwenye kutaka kwenda na kushuhudia athari za maangamizi. Wafasiri wanasema mji huo unajulikana kwa jina la Sodom[2] .

Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.

Yaani wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, wanaitakidi kwamba adhabu waliyoipata kaumu ya Lut ni malipo ya kufuru yao na upotevu wao.

Lakini walahidi wanasema ni matukio ya kawaida tu ya maumbile.

Na hakika watu wa kichakani walikuwa madhalimu.

Makusudio ya watu wa kichakani ni watu wa Shua’yb(a.s) . Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja maangamizi ya kaumu ya Lut, anadokeza kuhusu kaumu ya Shua’yb; kwamba Yeye pia aliwaangamiza kwa sababu ya kufru yao na kuipinga kwao haki, Yametangulia maneno kuhusu Shua’yb katika Juz, 8 (7:85), Vile vile yatakuja maelezo katika Juz 16 kwenye Sura ya Shua’rau.

Kwa hiyo tukawaadhibu. Na miwili hiyo iko katika njia iliyo wazi.

Yaani waliadhibiwa wote kaumu ya Lut na ya Shua’yb na miwili hiyo ni miji ya kaumu ya Lut na Shua’yb. Kwa maana ya kuwa dalili na athari za kuangamia miji miwili hiyo bado ziko na hata njia ya kuendea huko kujionea pia iko tena wazi wazi.

Na hakika watu wa Hijr waliwakadhibisha Mitume.

Watu wa Hijr ni watu wa Nabii Swaleh, mwenye ngamia, Hijr ni jina la mji waliokuwa wakikaa. Mtume waliyemkadhibisha ni mmoja tu, Mtume wao, lakini limekuja neno la wengi, Mitume, kwa vile mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja ni kama amekadhibisha Mitume yote.

Na tuliwapa ishara zetu nao wakazipuuza ingawaje zilikuwa na dalili za kutosha kuhusu haki, lakini kwa vile zilikuwa haziafikiani na hawa zao na kuigiza kwao ufisadi.

Na walikuwa wakichonga majumba katika majabali kwa amani.

Walikuwa wakikaa katika majumba ya mawe wakiwa na amani ya vita, kuonyesha kuwa walikuwa kwenye maendeleo wakati huo. Miongoni mwa ishara alizowaletea Mwenyezi Mungu mikononi mwa Mtume ni ngamia waliyemchinja huku wakijigamba kwa kusema:

يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧٧﴾

“Ee Swaleh! Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume. Jz. 8 (7:77).

Ukelele ukawanyakuwa asubuhi Yaani adhabu iliwafikia wakati wa asubuhi.

Hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.

Adhabu iliwafikia, lakini utajiri wao, majengo na makasri waliyoyajenga kwa mawe hayakuweza kuizuia. Umetangulia ufafanuzi wa Swaleh(a.s) na kaumu yake katika Juz.8 (7: 73).

Na hatukuiumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki.

Hakuna kitu chochote kilichopo ila kina hekima yake; kukiwemo kuangamia kwa makafiri katika umma uliotangulia. Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ﴿٢٧﴾

Hatukuiumba mbingu na ardhi na vilvyomo baina yake bure (38: 27).

Na hakika saa itafika.

Makusudio ya saa hapa ni Kiyama, wakati huo atalipwa kila mmoja stahiki yake.

Basi samehe msamaha mzuri.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad, akiamrishwa kuachana na washirikina na wajinga na kutojishughulisha nao. Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t): “Na vumilia na wayasemayo na jitenge nao kwa uzuri” (73: 10).

وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ ﴿٨٧﴾

87. Na hakika tumekupa Aya saba zinaazorudiwa rudiwa na Qur’an Tukufu.

لَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

88. Usikodolee macho yako yale tuliyowastareheshea makundi mbalimbali, Wala usiwahuzunikie. Na inamisha bawa lako kwa Waumini.

وَقُلْ إِنِّي أَنَا النَّذِيرُ الْمُبِينُ ﴿٨٩﴾

89. Na sema: Hakika mimi ni muonyaji niliye dhahiri.

كَمَا أَنزَلْنَا عَلَى الْمُقْتَسِمِينَ ﴿٩٠﴾

90. Kama tulivyowateremshia waliojigawanya.

الَّذِينَ جَعَلُوا الْقُرْآنَ عِضِينَ ﴿٩١﴾

91. Ambao wameipiga pande Qur’an.

فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾

92. Naapa kwa Mola wako wataulizwa wote.

عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾

93. Yale waliyokuwa wakiyatenda.

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ ﴿٩٤﴾

94. Basi yatangaze uliyoamrishwa na achana na washirikina.

إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ ﴿٩٥﴾

95. Hakika sisi tunakutosha na wafanyao isthizai.

الَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٩٦﴾

96. Wale wanaofanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yuko Mungu mwingine, basi watajua.

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ ﴿٩٧﴾

97. Na kwa hakika sisi tunajua kuwa kifua chako kinadhikika na yale wanayoyasema.

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ ﴿٩٨﴾

98. Basi msabihi Mola wako kwa sifa njema na uwe miongoni mwa wanaosujudi.

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ ﴿٩٩﴾

99. Na mwabudu Mola wako mpaka ikufikie yakini.

SABA ZINAZORUDIWA

Aya 87 – 99

LUGHA

Saba zinazorudiwa, ni Sura ya Fatiha, kwa vile ina Aya saba na inarudiwa kusomwa katika Swala. Imesemekana kuwa imeitwa saba kwa vile inazianzia Sura saba ndefu za mwanzo katika Qur’an ambazo ni: Al-baqara, Al-imran, An-nisaa, Al-maidah, Al-an’am, Al-a’raf na Yunus (2, 3, 4, 5, 6, 7, 8); kama ilivyoelezwa katika Tafsir At-tabari. Au Al-anfal pamoja na At-tawba; kama ilivyoelezwa katika tafsiri nyingine.

MAANA

Na hakika tumekupa Aya saba zinaazorudiwa rudiwa na Qur’an Tukufu.

Wametofautiana katika makusudio ya saba zinaazorudiwa. Wafasiri wametaja kauli tano, lakini yenye nguvu zaidi ni ile inayosema kuwa ni Sura ya Fatiha. Kwani ina Aya saba na kwenye swala inarudiwa na imeku- sanya mambo mawili ya Mungu na Ibada.

Usikodolee macho yako yale tuliyowastareheshea makundi mbalimbali.

Makusudio ya makundi mbalimbali hapa ni makafiri, washirikina na watu wa kitabu. Kwa maneno mengine ni aina zote za makafiri. Maana ni kuwa usiangalie au usishughulike na starehe wanazokuwa nazo makafiri katika washirikina na watu wa kitabu.

Wala usiwahuzunikie.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa akihuzunika na kuona uchungu sana kutokana na washirikina kukosa kuamini. Ndipo Mola Mtukufu akamwamrisha Mtume, lisimshghulishe hilo wala kumpa majonzi:

فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٨﴾

“Basi roho yako isitoke kwa majonzi juu yao; hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.” (35:8).

Na inamisha bawa lako kwa waumini.

Wanyenyekee waumini, kwani kuwanyenyekea hao ni kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Na kuwafanyia kiburi wahaini waliowafisadi ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu:

أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٥٤﴾

“Wanyenyekevu kwa waumini, wenye nguvu juu ya makafiri” Juz. 6: (5:54).

Na sema: Hakika mimi ni muonyaji niliye dhahiri.

Muhammad(s.a.w.w) aliwalingania watu kwa hoja na ubainifu, na bado mwito wake pamoja na hoja na dalili zake ziko mpaka leo na mpaka siku ya mwisho. Kwa hiyo kila mwenye akili anapaswa kuziangalia na kuzichunguza.

Akiziamini atakuwa ameziamini kwa hoja na akizikataa atakuwa ameziakataa kwa hoja, Ama yule mwenye kuzikimbia bila ya kuziangalia basi huyo ana lawama.

Kama tulivyowateremshia waliojigawanya ambao wameipiga pande Qur’an.

Makusudio ya waliojigawanya ni Mayahudi, kwani hao ndio walioigawa Qur’an vipande kwa kuamini baadhi na kupinga baadhi. Wanapinga yale yanayogongana na masilahi yao na maigizo yao na wakaamini yasiyokuwa hayo.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur’an kwa Muhammad(s.a.w.w) , kama alivyoiteremsha Tawrat kwa Mayahudi na Injili kwa manaswara ambao waliamini sehemu ya Qur’an na wakaipinga sehemu nyingine. Basi kuna ajabu gani kwa Muhammad kuteremshiwa kitabu kutoka kwa Mola wake ambaye alikwishateremsha vitabu kabla yake?

Naapa kwa Mola wako wataulizwa wote yale waliyokuwa wakiyatenda.

Qur’an hapa imethibitisha majukumu ya mtu kwenye matendo yake; kama ambavyo katika Aya nyingine imethibitisha majukumu katika kauli na nyingine ikathibitisha majukumu katika makusudio na maazimio:

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ ﴿١٨﴾

Hatamki kauli yoyote isipokuwa karibu yake yuko mngojeaji aliye tayari (50:18).

يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ ﴿١٩﴾

“Anajua hiyana ya macho na yanayoficha vifua” (40:19).

Kwa hiyo mtu atakapojua kuwa kuna anayemfuatilia, aliye na uwezo na mwadilifu, basi ataogopa na kuwa na takua. Ni vigumu kuweko nidhamu ya kibinadamu bila ya mtu kutambua majukumu na uwajibikaji wake.

Basi yatangaze uliyoamrishwa na achana na washirikina.

Lingania Mola wako kwa hoja na dalili wala usimjali anayekupinga na akakupa mgongo.

Hakika sisi tunakutosha na wafanyao isthizai, wale wanaofanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yuko Mungu mwingine, basi watajua.

Wafasiri, akiwemo Tabari, Razi na Tabrasi, wamesema kuwa jamaa wa kiqurayshi waliokuwa na nguvu walikuwa wakimdharau na kumcheza shere Mtume(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu akawaangamiza kwa sababu ndogo na nyepesi. Miongoni mwao ni Walid bin Al-mughira, Asi bin Wail, Uday bin Qays na As-wad bin Abd yaghuth.

Na kwa hakika sisi tunajua kuwa kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema. Basi msabihi Mola wako kwa sifa njema na uwe miongoni mwa wanaosujudi.

Ni kawaida Mtume kuhuzunika na kuona uchungu pale Washirikina wanapomdharau na kumwambia ni mwendawazimu au anamzulia Mungu. Vile vile ni kawaida kifua chake kidhikike na yale wayasemayo makafiri kwa sababu yeye ni binadamu kwa nyama na damu. Anafurahi kwa yale wanayoyafurahia watu na anahuzunika kwa yale wayahuzinikiayo watu.

Lakini kuna uhusiano gani baina ya huzuni na ibada ambayo Mwenyezi Mungu amemwamrisha kuikimbilia anapohuzunika na kudhikika kifua chake?

Jibu : Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakumwamrisha Mtume wake ibada hapa ili ambainishie kuwa kudhikika kifua ndio sababu ya amri ya ibada, hapana! Hakika amri ya ibada ya Mwenyezi Mungu haifungamani na furaha wala huzuni; isipokuwa amri ya ibada hapa ni fumbo la kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake, pale anapopata machungu na kuhuzunika; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾

Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu, Hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye. Juz; 9 (7:200).

Angalia huko utapata ufafanuzi zaidi.

Na mwabudu Mola wako mpaka ikufkie yakini.

Makusudio ya yakini hapa ni mauti kwa sababu hayana budi kutokea. Kwa maana ya kuwa mtu aendelee na ibada ya Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi maisha yake yote:

وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾

Na ameniusia Swala na Zaka maadamu ningali hai (19:31).

MWISHO WA SURA YA KUMI NA TANO