TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10006
Pakua: 3647


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10006 / Pakua: 3647
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

Sura Ya Kumi na Sita: Surat An Nahl.

Sura Annahl (Nyuki) Ina Aya 128.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

أَتَىٰ أَمْرُ اللَّـهِ فَلَا تَسْتَعْجِلُوهُ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿١﴾

1. Imefika amri ya Mwenyezi Mungu msiifanyie haraka. Ametakata na kutukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.

يُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ بِالرُّوحِ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ أَنْ أَنذِرُوا أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاتَّقُونِ ﴿٢﴾

2. Huwateremsha Malaika na roho kwa amri yake juu ya anayemtaka katika waja wake; kwamba onyeni kuwa hakuna Mola aabudiwaye isipokuwa mimi tu, basi niogopeni.

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ تَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣﴾

3. Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, ametukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.

خَلَقَ الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ ﴿٤﴾

4. Amemuumba mtu kwa tone la manii, mara amekuwa hasimu aliye dhahiri.

IMEFIKA AMRI YA MWENYEZI MUNGU

Aya 1 – 4

Badhi ya Aya za sura hii zimeshuka Makka na nyingine zimeshuka Madina. Wametofautiana katika idadi ya Aya za Makka na zile za Madina. Ikasemekana kuwa kuanzia ya kwanza hadi ya arobaini ni za Makka na zilizobaki ni za Madina, Pia ikasemekana kuwa zote zilishuka Makka isipokuwa tatu za mwisho.

MAANA

Imefika amri ya Mwenyezi Mungu msiifanyie haraka, Ametakata na kutukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.

Mtume alikuwa akiwaonya washirikina na kuwahofisha na adhabu kali, lakini wao walikuwa wakimjibu kwa dharau huku wakisema:

فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٢﴾

“Basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo, ” Juzl 9 (8:32).

Basi Mwenyezi Mungu akawajibu kuwa adhabu itakuja na kila lijalo liko karibu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya kitendo kilichopita ‘imefika’ kwa maana ya kuwa itafika, kwa kufahamisha kuwa hakuna budi kutokea kwake. Kila ambalo linawajibika kutokea basi ibara yoyote itakayoelezewa iwe ya kupita ya sasa au ya muda ujao itakuwa sawa tu. Kesho wataambiwa:

هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ ﴿١٤﴾

“Haya ndiyo yale mliyokuwa mkiyaharakishia” (51:14).

Hawatakuwa na jibu isipokuwa kusema:

يَا وَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا بَلْ كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٩٧﴾

“Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika na haya; bali tulikuwa wenye kudhulumu.” (21:97).

Huwateremsha Malaika na roho kwa amri yake juu ya anayemtaka katika waja wake; kwamba onyeni kuwa hakuna Mola aabudiwaye isipokuwa mimi tu, basi niogopeni.

Makusudio ya roho hapa ni wahyi, kwa sababu wenyewe ni kwa ajili ya nafsi, sawa na roho kwa ajili ya mwili. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anachagua anayestahiki risala yake.

Na risala yenyewe kwa ufupi ni Tawhid kiitikadi na msimamo kimatendo. Kwa sababu kila mwenye kumcha Mwenyezi Mungu basi yuko katika njia ya amani iliyo na msimamo na kila mwenye kumwasi yuko katika njia ya maangamivu na upotevu.

Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, ametukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja, katika Aya iliyotangulia, kuwa hakuna mola isipokuwa Yeye, katika Aya hii, ameishiria dalili ya hilo; kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi na akazipangilia bila ya kuwa na msaidizi yeyote. Kuumba bila ya kutumia nyenzo yoyote ni dalili ya uungu; kama ambavyo kuwa Peke Yake katika kuumba ni dalili ya umoja. Tazama Juz. 5 (4:48) kifungu cha ‘Dalili ya umoja na utatu’

Amemuumba mtu kwa tone la manii, mara amekuwa hasimu aliye dhahiri.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria dalili ya umoja anasema, lakini binadamu huyu dhaifu tuliyemuumba kwa tone anakufuru neema ya aliyemneemesha na anapinga kuweko aliyemleta; huku akiabudu yale yasiyodhuru wala kunufaisha.

Yametangulia maelezo mara nyingi sana kwamba mtu hawi kombo ila kwa ujinga na ugizaji au kwa manufaa binafsi. Tazama Juz, 13 (14: 34) Kifungu ‘je mtu ana maumbile ya hatia?.

وَالْأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٥﴾

5. Na wanyama amewaumba, katika hao mnapata joto na manufaa na wengine mnakula.

وَلَكُمْ فِيهَا جَمَالٌ حِينَ تُرِيحُونَ وَحِينَ تَسْرَحُونَ ﴿٦﴾

6. Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka asubuhi.

وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ إِلَىٰ بَلَدٍ لَّمْ تَكُونُوا بَالِغِيهِ إِلَّا بِشِقِّ الْأَنفُسِ إِنَّ رَبَّكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٧﴾

7. Na hubeba mizigo kupeleka kwenye mji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu ni Mpole sana, Mwenye kurehemu.

وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٨﴾

8. Na farasi na nyumbu na punda ili muwapande na pambo, Na anaumba msivyovijua.

وَعَلَى اللَّـهِ قَصْدُ السَّبِيلِ وَمِنْهَا جَائِرٌ وَلَوْ شَاءَ لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩﴾

9. Na nijuu ya Mwenyezi Mungu njia iliyo sawa. Na nyingine ni kombo, Lau angelitaka angeliwaongoza nyote.

WANYAMA, FARASI, NYUMBU NA PUNDA

Aya 5-9

MAANA

Na wanyama amewaumba, katika hao mnapata joto na manufaa na wengine mnakula.

Wanyama waliokusudiwa ni wale wa kufugwa amabo ni ngamia, ngombe, mbuzi na kondoo.

Qur’an ilishuka wakati ambao maisha ya kilimo na mengineyo yalikuwa hayapangiki bila wanyama. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja aina mbalimbali za wanyama na faida zake katika Aya kadhaa, kwa makusudio ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu na neema zake kwa waja wake ili waweze kumcha Yeye katika matendo yao na kauli zao. Miongoni mwa Aya hizo ni: Juz, 8 (6: 143-144).

Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu ametaja faida tatu za wanyama; Joto kwa maana ya mavazi ya kuzuia baridi yanayotokana na ngozi za wanyama, sufu, manyoya yake n.k. Ametaja manufaa, yakiwa ni pamoja na maziwa, samli na kulima. Ama kauli yake ‘mnakula’ ni nyama pamoja na bidhaa za maziwa ambazo pia ni miongoni mwa manufaa.

Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka asubuhi.

Makusudio ya kuona raha hapa ni kuona raha ya mandhari ya wanyama hasa wakiwa wamenona. Makusudio ya kuwarudisha jioni ni kuwarudisha zizini kutoka malishoni na kuwapeleka asubuhi ni kuwatoa zizini kwenda malishoni. Mandhari haya kwa hakika ni mazuri yanayoleta raha kwenye nafsi.

Na hubeba mizigo kupeleka kwenye mji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja faida ya wanyama kwa chakula na kivazi, hapa anataja kuwa pia wanyama ni nyenzo ya mawasiliano na uchukuzi kutoka mji mmoja hadi mwengine; na lau si hao basi binadamu angelipata tabu.

Hakika Mola wenu ni Mpole sana Mwenye kurehemu.

Miongoni mwa huruma zake ni kuwatumikisha wanyama kwa masilahi ya watu ilikuweza kurahisisha mambo na kupunguza tabu

Na farasi na nyumbu na punda ili muwapande na pambo.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja manufaa matatu ya wanyama, sasa anataja manufaa ya farasi, nyumbu na punda, ambayo muhimu zaidi ni kupanda na vipambo, katika wakati huo.

Na anaumba msivyovijua.

Kila mwanachuoni ameifasiri jumla hii kulingana na wakati wake na maisha yake. Baadhi ya wakale wamesema kuwa makusudio ni kuwa Mwenyezi Mungu anaumba aina ya wanyama, mimea na vitu vingine vingi sana ambavyo watu hawavijui.

Tabari anasema: Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu atawaumbia watu wa Peponi aina kadha za neema na atawaumbia watu wa motoni aina kadhaa za adhabu ambazo hakuna jicho lililoziona wala sikio lililozisikia au moyo ulioziwazia. Baadhi ya wafasiri wapya, akiwemo Sheikh Al-maraghi, wamesema:

“Hii ni ishara ya ndege, magari n.k.”

Maana yanayonasibiana na mfumo wa maneno – tuonavyo sisi – ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kutaja manufaa kwa waja wake, anasema kuwa haya ni machache miongoni mwa manufaa mengi msiyoyajua wala kujua idadi yake.

Kwa maneno mengine jumla hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 18 ya Sura hii: “Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti.

Sha’rani amenukuu katika kitabu chake Al-mizani kutoka kwa Abu Hanifa, uharamu wa nyama ya farasi. Na kutoka kwa Shafii, Malik, na Ibn Hambal wamesema ni halali.

Ama nyama ya nyumbu na punda, amenukuu kutoka kwa Shafi, Abu Hanifa na Ibn Hambal kuwa ni haramu. Shia Imamiya wamesema kuwa nyama ya farasi, nyumbu na punda ni halali, lakini ni makruh.

Na ni juu ya Mwenyezi Mungu njia iliyo sawa.

Juu hapa, ni kwa maana ya wajibu. Aya hii inafanana na ile isemayo: “Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu” (92:12). Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amejilazimisha kuwabainishia watu, kupitia Mitume, njia ya haki na ya uongofu.

Na nyingine ni kombo.

Yaani kuna njia zilizo sawa, kama vile Uislamu, na nyingine ziko kombo kombo, kama dini nyinginezo.

Lau angelipenda angeliwaongoza nyote.

Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwaelekeza watu wote kwenye imani kwa nguvu na asingelikufuru yeyote.

Lakini Yeye Mwenyezi Mungu amemwachia mtu hiyari, baada ya kumbainishia njia mbili, kwa kuchukulia utu wake. Angalia Juz. 12 (12: 118).

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً لَّكُم مِّنْهُ شَرَابٌ وَمِنْهُ شَجَرٌ فِيهِ تُسِيمُونَ ﴿١٠﴾

10. Yeye ndiye aliyewateremshia maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa na miti ya kulishia.

يُنبِتُ لَكُم بِهِ الزَّرْعَ وَالزَّيْتُونَ وَالنَّخِيلَ وَالْأَعْنَابَ وَمِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿١١﴾

11. Kwayo anazalisha mimea kwa ajili yenu na mizaituni na mitende na mizabibu na kila matunda. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wanaofikiri.

وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومُ مُسَخَّرَاتٌ بِأَمْرِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿١٢﴾

12. Na amefanya uwatumikie usiku na mchana na jua na mwezi na nyota ziwatumikie kwa amri yake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu walio na akili.

وَمَا ذَرَأَ لَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٣﴾

13. Na alivyovieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaowaidhikia.

وَهُوَ الَّذِي سَخَّرَ الْبَحْرَ لِتَأْكُلُوا مِنْهُ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُوا مِنْهُ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا وَتَرَى الْفُلْكَ مَوَاخِرَ فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٤﴾

14. Yeye ndiye aliyeifanya bahari iwatumikie ili kutoka humo mpate kula nyama freshi na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.

وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَأَنْهَارًا وَسُبُلًا لَّعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٥﴾

15. Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi. Na mito na njia ili mpate kuon- goka.

وَعَلَامَاتٍ وَبِالنَّجْمِ هُمْ يَهْتَدُونَ ﴿١٦﴾

16. Na alama nyingine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.

أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لَّا يَخْلُقُ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿١٧﴾

17. Je, anayeumba ni kama asiyeumba? Hivi hamkumbuki?

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا إِنَّ اللَّـهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٨﴾

17. Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ﴿١٩﴾

19. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya siri na mnaoyoyatangaza.

KUKUMBUSHA NEEMA ZA MWENYEZI MUNGU

Aya 10 – 19

MAANA

Yeye ndiye aliyewateremshia maji kutoka mbinguni, Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa na miti ya kulishia.

Kila kinachomea katika ardhi ni mti. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha waja wake kwa maji akayafanya kinywaji chao na akaotesha mimea ambayo wanalishia wanyama wao.

Kwayo anazalisha mimea kwa ajili yenu na mizaituni na mitende na mizabibu na kila matunda. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wanaofikiri.

Vilevile Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa maji haya ameotesha vitu kwa masilahi yetu na manufaa yetu. Basi na tufikiri na kuzingatia kwa makini uweza wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake na tumshukuru kwa kumtii na kutenda kulingana na radhi yake. Huko nyuma tumewahi kudokeza kuwa maji yanatokana na sababu za kimaumbile alizoziweka Mwenyezi Mungu katika ulimwengu huu; na kwamba inategemezwa kwake moja kwa moja kwa kuwa Yeye ndiye msababishi wa kwanza.

Mfano wa Aya hii umetangulia katika Juz. 13 (14:32) na katika Juz. hii tuliyo nayo (15:22).

Na amefanya uwatumikie usiku na mchana na Jua na Mwezi na nyota ziwatumikie kwa amri yake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu walio na akili.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:2) na (14: 33). Kusema ‘kwa amri yake’ kunaishiria majibu ya wamaada wanaodai kuwa matukio yote ya ulimwengu yanatokana na sababu zake za kimaumbile tu.

Unaweza kuuliza : Kwani haitoshi kutaja usiku mpaka utajwe mwezi na mchana mpaka litajwe jua?

Jibu : Hapana! Usiku unaweza kuweko bila ya mwezi, Na mchana ni baadhi tu ya athari na faida za Jua, lakini kuna athari na faida nyinginezo zinazoletwa na Jua.

Na alivyovieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali, Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaowaidhikia.

Makusudio ya kueneza ni kuumba, na rangi ni aina. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametupatia vitu alivyoviumba duniani, vikiwemo vitu vikavu kama madini na vya majimaji, tuvitumie, ili aweze kuwaid- hika mwenye kuwaidhika na ashukuru mwenye kushukuru.

Yeye ndiye aliyeifanya bahari iwatumikie ili kutoka humo mpate kula nyama freshi[3] na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.

Ametaja Mwenyezi Mungu faida tatu za bahari:

1. Samaki

2. Vipambo; kama vile lulu na marijani. Mwenyezi Mungu anasema: “Hutoka humo lulu na marijani” (55: 22). Al-Maraghi katika kufasiri Aya hii anasema: “Yanapatikana mashamba ya lulu na marijani ndani ya bahari ya kati (Mediterranean sea) baina ya Tunisia na Algeria. Serikali ya Ufaransa ndiyo inayovuna mashamba haya kisha huwauzia wenyewe; kama kwamba wao hawakusoma Qur’an, kama kwamba wao hawakuumbiwa dunia hii na kama kwamba wao hawakuamrishwa kufanya kazi na kuitoa.”

3. Safari ya baharini kibiashara na mengineyo.

Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi.

Ameweka mlima katika ardhi ili iwe imara kusipatikane mgongano. Umepita mafano wake katika Juz. hii (15:19).

Na mito na njia ili mpate kuongoka.

Amepitisha mito pia amefanya njia ili muweze kufika kule mnakotaka kwa njia hizo.

Na alama nyingine.

Makusudio ya alama hapa ni dalili zinaazomsadia msafiri kufuata njia; mfano mlima, mabonde n.k.

Na kwa nyota wao wanjiongoza wanaposafiri bara na baharini.

Umepita mfano wake katika Juz. 7 (6:97).

Je, anayeumba ni kama asiyeumba? Hivi hamkumbuki?

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa Yeye ndiye muumbaji wa mbingu na ardhi, binadamu, wanyama, maji, miti, Jua, Mwezi n.k. Sasa anasema kuwa je, aliyeumba vyote hivi anakuwa sawa na jiwe na sanamu?

Swali hili liko pamoja na jawabu lake.

Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti.

Umepita mfano wake katika Juz, 13 (14:34).

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Anamsamehe mwenye kuzembea kumshukuru bila ya kumnyang’anya neema, kwa sababu ya kumuonea huruma.

Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya siri na mnaoyoyatangaza.

Ikiwa anayajua mnayoyafanya siri na mnayoyafanya dhahiri ni wajibu kumtii Yeye kwa kuhofia hasira zake na adhabu yake.

وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ ﴿٢٠﴾

20. Na wale wanaowaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.

أَمْوَاتٌ غَيْرُ أَحْيَاءٍ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ ﴿٢١﴾

Ni wafu si hai. Na wala hawatambui watafufuliwa lini.

إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ قُلُوبُهُم مُّنكِرَةٌ وَهُم مُّسْتَكْبِرُونَ ﴿٢٢﴾

22. Mungu wenu ni Mungu mmoja, Lakini wasioamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wana kiburi.

لَا جَرَمَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْتَكْبِرِينَ ﴿٢٣﴾

23. Hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya siri na wanayoyatangaza, Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi.

WANAOOMBA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU

Aya 20 – 23

MAANA

Na wale wanaowaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.

Yametangulia mazungumzo kuhsu ushirikina na mjadala pamoja na washirikina, katika Aya kadhaa. Sasa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuelezea aina kadhaa za neema zake kwa waja wake, anadokeza, kwenye Aya hizi na zinaazofuatia, kuhusu wale wanaomkufuru Mwenyezi Mungu na wanaomfanyia washirika katika kuumba kwake.

Akawaambia wazi na kwa hoja fasaha, kwamba Mungu anayefaa kuabudiwa ni yule anayekuwa muumbaji sio aliyeumbwa, Na nyinyi washirikina mnaabudu aliyeumbwa sio aliyeumba.

Ni wafu si hai.

Vile vile miongoni mwa masharti ya mwenye kuabudiwa ni kuwa hai; na mnayemwabudu ameganda tu hana uhai.

Na wala hawatambui watafufuliwa lini.

Jumla hii maana yake yatafahamika kutokana na maswali mawili yafutayo pamoja na majibu yake:

Swali la kwanza : Neno hawatambui linatumika kwa wenye akili na washirikina wanaabudu masanamu, sasa imekuwaje kutumia dhamiri ya wenye akili kwa visivyo na akili?

Jibu : matumizi haya yamekuja kulingana na wanavyoitakidi washirikina kwamba masanamu yanaakili na utambuzi. Kwani kuna ubaya gani wa matumizi haya na mfano wake maadamu ni masuala ya tamko tumko tu na ibara?

Swali a pili : Masanamu hayatafufuliwa, vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) akasema: ‘Na wala hawatambui watafufuliwa lini’

Jibu : baadhi ya wafasiri wamejibu kwamba dhamir katika ‘hawatambui’ ni ya masanamu na ‘watafuliwa’ ni ya washirikina; Kwa hiyo maana yanakuwa masanamu hayatambui lini watafufuliwa washirikina kutoka makubirini mwao, Ikiwa masanamu hayatambui hayo, basi inakuwaje kuwa yanastahiki kuabudiwa?

Mungu wenu ni Mungu mmoja, Lakini wasioamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wana kiburi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya hii, ametaja sifa mbili za wanaopinga Akhera:

Sifa ya kwanza: kwamba nyoyo zao zimepinga na kuikana Akhera. Kwa hiyo wao hawafanyi chochote kwa kutummai thawabu au kuhofia adhabu; isipokuwa wanafanya kwa misingi ya faida na manufaa ya maisha haya ya dunia. Sifa ya pili: kwamba wao wanaikimbia haki na wala hawaifuati kwa sababu ya kujiona wakubwa na kuwa na kiburi.

Hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya siri na wanyoyatangaza, Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi.

Hakika Yeye Mwenyezi Mungu anajua kupinga kwao kulikuwa ni kwa kujipa uluwa na kiburi, naye anawachukia wanaoinyenyekea haki na atawaadhibu yale wanayostahiki.

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

وَإِذَا قِيلَ لَهُم مَّاذَا أَنزَلَ رَبُّكُمْ قَالُوا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾

24. Wanapoambiwa: Ameteremsha nini Mola wenu? Husema: ngano za watu wa kale.

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ ﴿٢٥﴾

25. Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu siku ya Kiyama na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Ehe! Ni maovu hayo wanayoyabeba.

قَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَأَتَى اللَّـهُ بُنْيَانَهُم مِّنَ الْقَوَاعِدِ فَخَرَّ عَلَيْهِمُ السَّقْفُ مِن فَوْقِهِمْ وَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٢٦﴾

26. Walipanga vitimbi waliokuwa kabla yao. Mwenyezi Mungu akazifikia nyumba zao kwenye misingi akayasekua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao na adhabu ikawajia kutoka wasipotambua.

ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يُخْزِيهِمْ وَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تُشَاقُّونَ فِيهِمْ قَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ إِنَّ الْخِزْيَ الْيَوْمَ وَالسُّوءَ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٢٧﴾

27. Kisha siku ya Kiyama atawahizi. Na atasema: Wako wapi hapo hao washirika wangu ambao kwao mlikuwa mkipatisha mashaka. Watasema waliopewa: Hakika leo hizaya na uovu utawashukia makafiri.

الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ فَأَلْقَوُا السَّلَمَ مَا كُنَّا نَعْمَلُ مِن سُوءٍ بَلَىٰ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٢٨﴾

28. Wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamejidhulumu. Basi watasalimu amri (waseme): Hatukuwa tukifanya uovu: Ndiyo! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyokuwa mkiyatenda.

فَادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا فَلَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ ﴿٢٩﴾

29. Basi ingieni milango ya Jahannam, humo mdumu, Ni maovu mno makazi ya wafanyao kiburi.

HUSEMA NGANO ZA WATU WA KALE

Aya 24 – 29

MAANA

Wanapoambiwa: Ameteremsha nini Mola wenu? Husema: ngano za watu wa kale.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja kuwa wanaopinga Akhera wamefanya hivyo kwa kujifanya wakubwa na kiburi cha kutoinyenyekea haki. Katika Aya hii anawasimulia kuwa wao wanaipa Qur’an sifa ya kuwa ni uzushi na ni vigano.

Katika Aya nyingine Muhammad(s.a.w.w) wamembandika uwendawazimu na mara ningine wanasema ni mshairi au kuhani. Pia wanadiriki kusema kuwa ni mchawi.

Lengo lao la kwanza ni kuwapoteza watu wasiijue haki ambayo inafichua aibu zao na hakika yao. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja hawa wanowazuia watu na na haki katika Aya nyingi. Mara nyingine amewapa sifa ya wanaotaka kupotosha na pia akawataja kuwa wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu akawahadharisha kwa kusema: Na kwa hakika watabeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa siku ya kiyama yale waliyokuwa wakiyazua (29:13). Maana ya Aya hii yanafanana na Aya ifuatayo:

Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu siku ya Kiyama na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Ehe! Ni maovu hayo wanayoyabeba.

Hakika wamepotea na wakapoteza wengine. Kwa sababu ya upotevu wao basi wao watabeba madhambi yao kwa ukamailifu; yaani Mwenyezi Mungu hatawasamehe kitu. Na kwa sababu ya kuwapoteza wengine basi watabeba dhambi nyingine za wale waliowapoteza na kuwaharibu. Kuna hadithi isemayo: “Yeyote atakayetoa mwito wa upotevu na wakafuata- yaani wakifuata watubasi atakuwa na malipo sawa na yale ya waliomfu- ata bila ya kupungua kitu katika madhambi yao.”

Walipanga vitimbi waliokuwa kabla yao. Mwenyezi Mungu akazifikia nyumba zao kwenye misingi akayasekua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao na adhabu ikawajia kutoka wasipotambua.

Makusudio ya majengo, misingi na dari ni kufananisha matendo yao na hayo majengo. Maana ni kuwa washirikina wa mwanzo walipanga njama na hila dhidi ya mitume na manabii wa Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu akazitibua zote na ikawa ndiyo sababu ya kuangamia kwao; sawa na aliyejenga nyumba akaipangilia vizuri pamoja na msingi wake; na alipoanza kufanya maskani hapo na kutulia ikaporomoka kuanzia msingi, ikawa chini juu. Huu hasa ndio mwisho wa kila mwenye kuipinga haki na akaeneza uzushi na propaganda. Ni sawa haki ije kupitia kwa Muhammad(s.a.w.w) au mwenginewe.

Kisha siku ya kiyama atawahizi.

Makusudio ya kuhizi hapa ni adhabu ya moto: “Mola wetu! Hakika wewe, ambaye utamwingiza motoni utakuwa umemuhizi, Juz, 4 (3:192).

Na atasema: Wako wapi hapo hao washirika wangu ambao kwao mlikuwa mkipatisha mashaka.

Anayesema ni Mwenyezi Mungu, wanaoambiwa ni washirikina na maana ya kupatisha mashaka ni kule kugombana nao kuhusu masanamu. Kwa sababu washirikina walikuwa wakiyaabudu na kuyatetea na kugombana na kila mwenye kuyashutumu na kuyasema kwa ubaya. Walikuwa wakisema: haya yanatuombea na kutuweka karibu na Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo watakaposimama kesho mbele ya Mwenyezi Mungu atauliza kuhusu hayo kwa kuwatahayariza: wakowapi hao washirika wangu mliokuwa mkidai? Hata ikiwa hakuna adhabu basi swali hili peke yake, kutoka kwa Mwenye nguvu, linatosha.

Watasema waliopewa elimu ya haki na wakaitumia:Hakika leo hizaya na uovu utawashukia makafiri.

Makusudio ya makafiri hapa ni kila wanaopinga haki na wakaacha kuinyenyekea, wawe walahidi au la. Kwa sababu wote hao wataingia Jahannam na ni mahali pabaya.

Wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamejidhulumu.

Wamejidhulumu kwa vile wamekufa wakiwa ni makafiri na wapotevu.

Basi watasalimu amri.

Wanasalimu amri siku ambayo hakufai kitu kusalimu kwao wala kunyenyekea(waseme): Hatukuwa tukifanya uovu na hapo Mwenyezi Mungu atajibu kwa kusema:

Ndiyo! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyokuwa mkiyatenda. Miongoni mwa dhulma na madhambi, na leo mtalipwa adhabu kwa yale mliyokuwa mkiyazua

Basi ingieni milango ya Jahannam, humo mdumu. Ni maovu mno makazi ya wafanyao kiburi.

Kila mwenye kuikataa haki basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni mwenye kiburi, ni sawa awe amenasibika na Uislamu au kunasibika na dini nyingine. Mwisho wake ni kudumu katika Jahannam, Ama kuhusu milango yake, yametangulia maelezo katika Juz hii (15: 44).

وَقِيلَ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا مَاذَا أَنزَلَ رَبُّكُمْ قَالُوا خَيْرًا لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ وَلَنِعْمَ دَارُ الْمُتَّقِينَ ﴿٣٠﴾

30. Na wataambiwa wale waliofanya takua: Mola wenu ameteremsha nini? Watasema: Kheri, Waliofanya wema katika dunia hii watapata wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi. Na ni bora mno nyumba ya wenye takua.

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ لَهُمْ فِيهَا مَا يَشَاءُونَ كَذَٰلِكَ يَجْزِي اللَّـهُ الْمُتَّقِينَ ﴿٣١﴾

31. Bustani za milele wataziingia, hupita chini yake mito, Humo watapata watakacho, Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye takua.

الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ طَيِّبِينَ يَقُولُونَ سَلَامٌ عَلَيْكُمُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٣٢﴾

Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema. Wanawaambia, amani iwe juu yenu (Salamun alaykum) kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ أَمْرُ رَبِّكَ كَذَٰلِكَ فَعَلَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٣٣﴾

33. Je, wanangojea jengine isipokuwa Malaika wawafikie au iwafikie amri ya Mola wako? Kama hivyo walitenda waliokuwa kabla yao, Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, Lakini wamejidhulumu wenyewe.

فَأَصَابَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا عَمِلُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٣٤﴾

34. Basi ukawasibu uovu wa waliyoyatenda na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia stihzai.

WATASEMA KHERI

Aya 30 – 34

MAANA

Na watambiwa wale waliofanya takua: Mola wenu ameteremsha nini? Watasema: kheri.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja washirikina ambao waliitaja Qur’an kuwa ni potofu na ni ngano za watu wa kale, sasa anawataja waumini katika Aya hii, na kwamba wao watakapo ulizwa kuhusu Qur’an wataitaja kwa utukufu na taadhima na kuisifu kama alivyoisifu Imam Aliy(a.s) katika Nahjul- balagha:“Dhahiri yake ni safi na undani wake ni wakina. maajabu yake hayatoweki na mshangazo wake hauishi, wala giza halitanzuki ila kwayo”

Waliofanya wema katika dunia hii watapata wema.

Hii ni jumla inayoanza upya, haina uhusiano na maneno yaliyo kabla yake. Imesemekana kuwa ni katika maneno ya wenye takua. Hata hivyo maana ni moja tu katika makadirio yote mawili, nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawalipa heri watenda mema hapa duniani ijapokuwa ni kwa kutajwa vizuri

Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi kuliko neema ya duniani iliyojaa ghasia na wasiwasi na iliyo na kipimo na kiasi.Na ni bora mno nyumba ya wenye takua, kwa sababu ni nyumba ya raha ya daima ambayo haina tashwishi yoyote ya wasiwasi wala kutaabika.

Bustani za milele wataziingia, hupita chini yake mito, Humo watapata watakacho, Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye takua.

Hawaaingii Pepo hii adhimu isipokuwa wenye takua, nao ni wale waliofanya juhudi ya kuinusuru haki, wakavumilia adha kwa ajili yake. Qur’an imenukuu wazi aina hii ya wenye takua watakaoingia peponi, pale iliposema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾

Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira? Juz, 4 (3:142).

Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema kwenye makusudio yao na kwenye vitendo na kauli zao. Mtu hupimwa kwa mwisho wake na mwema ni yule mwenye kuiacha dunia hii na Mungu yuko radhi naye na kumshuhudia kuwa yeye ni katika watu wema.

Wanawaambia amani iwe juu yenu (Salamun alaykum) kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

Yaani Malaika wanawasalimu watu wema wakati wa kufa kwa rehema, huku wakiwabashiria Pepo, ili zitulie nyoyo zao na wapate furaha ya karama na vyeo walivyoahidiwa na Mwenyezi Mungu.

Je, wanangojea jengine isipokuwa Malaika wawafikie au iwafikie amri ya Mola wako?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6: 159).

Kama hivyo walitenda waliokuwa kabla yao.

Huu ni ukumbusho na onyo kwa wale ambao wamemkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) kwamba yatawapata yaliyowapata waliotangulia.

Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu.

Vipi iwe hivyo na hali Yeye mwenyewe ameikataza dhulma na kuiita kuwa ni upotofu tena akawalaani madhalimu?

بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾

“Bali madhalimu wako katika upotovu ulio wazi” (31:11)

“Basi mtangazaji atatangaza kati yao kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu”

Juz. 8 (7:44)

Lakini wamejidhulumu wenyewe.

Maana haya yamekaririka katika Aya kadha, Iliyo wazi zaidi ni ile isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu watu chochote, lakini watu wanajidhulumu wenyewe.” Juz,11 (10:44).

Mwenyezi Mungu amekariri neno watu ili kuondoa tashwishi. Lau si Ashaira (Sunni) kusema kuwa mtu hana hiyari bali ni mwenye kuendeshwa, basi tusingelikuwa na haja ya kurefusha maneno au misisitizo hii ambayo inafanana na kufafanua ufafanuzi.

Basi ukawasibu uovu wa waliyoyatenda na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia stihzai.

Washirikina walipinga risala ya Muhammad(s.a.w.w) , wakaidharau na wakawazuia watu nayo, basi nao watapata matunda ya matendo yao, wala hawatadhulumiwa, Bali wengi katika wao watapata malipo yaohapa duniani kabla ya akhera.

وَقَالَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ نَّحْنُ وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ كَذَٰلِكَ فَعَلَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَهَلْ عَلَى الرُّسُلِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٣٥﴾

35. Na wale ambao wameshirikisha wanasema: “Lau Mwenyezi Mungu angelitaka, tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya Yeye. Kama hivyo walifanya waliokuwa kabla yao. Basi kuna lolote juu ya mitume isipokuwa kufikisha kwa uwazi?

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ فَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ ﴿٣٦﴾

36. Na kwa hakika tulimtuma Mtume kwa kila umma kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu na mumwepuke taghuti. Basi miongoni mwao wapo aliowaongoa Mwenyezi Mungu na miongoni mwao wapo ambao uliwathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.

إِن تَحْرِصْ عَلَىٰ هُدَاهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَن يُضِلُّ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٣٧﴾

37. Hata ukipupia kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu hamuongoi yule aliyempoteza, wala hawatapata wa kuwanusuru.

WAKASEMA WALIOSHIRIKISHA

Aya 35 – 37

MAANA

Na wale ambao wameshirikisha wanasema: Lau Mwenyezi Mungu angelitaka tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya Yeye.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (6:149).

Kama hivyo walifanya waliokuwa kabla yao.

Huu ndio msingi wa mataghuti kila wakati na kila mahali. Wanaipinga haki na kuwapiga vita wenye haki, kisha wanalibadilisha hilo kwenye matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Basi kuna lolote juu ya mitume isipokuwa kufikisha kwa uwazi?

Huu ndio umuhimu wa kufikisha amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ama kuyatenda wanayoyafikisha hiyo si kazi yao kidogo wala sana, Maana ya Aya hii yametangulia katika Aya nyingi.

Na kwa hakika tulimtuma Mtume kwa kila umma kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu na mumwepuke taghuti.

Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ametuma Mtume, kwa kila umma katika kila karne na kila mahali, awaamrishe ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake na kuwakataza ibada ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu; iwe ni sanamu, nyota, binadamu au kitu chochote. Si lazima Mtume huyu awe ni mtu, inaweza kuwa akili. Kwani akili ni mtume wa ndani na Nabii ni mtume wa nje, Angalia kifungu ‘Mwenyezi Mungu na maumbile’ katika Juz, 7 (6: 41).

Basi miongoni mwao wapo aliowaongoa Mwenyezi Mungu na miongoni mwao wapo ambao uliwathibitikia upotovu.

Makusudio ya upotovu hapa ni adhabu; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَرِيقًا هَدَىٰ وَفَرِيقًا حَقَّ عَلَيْهِمُ الضَّلَالَةُ ﴿٣٠﴾

“Kundi moja ameliongoa na kundi jingine limethibitikiwa na upotofu” Juz, 8 (7: 30)

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alituma Mitume kuleta bishara na kuonya. Wakaamini baadhi ya watu, wakawa ni katika walioongoka wenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu. Na wengine wakakufuru, wakawa ni wenye kuwekwa mbali wenye kuadhibiwa.

Basi tembeeni katika ardhi muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.

Yamekaririka maana ya Aya hii katika Aya nyingi, ikiwemo ile iliyo katika Juz, 4 (93:137)

Hata ukipupia kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu hamuongoi yule aliyempoteza, wala hawatapata wa kuwanusuru.

Hakuna mwenye shaka kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anapupia watu wote waongoke; hasa watu wake Maquraishi, lakini kupupia tu kwa mtume sio sababu ya kupatikana uongofu; isipokuwa sababu ni matakwa ya mtu kuongoka kama ambavyo sababu ya kupotea ni matakwa ya mtu mwenyewe.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezithibitisha sababu zote hizi mbili; kwa maana ya kuwa Yeye ambaye hekima yake imetukuka, amejaalia matakwa ya mtu katika uongofu ndiyo natija ya uongofu wake na matakwa ya mtu katika upotevu ndio natija ya upotevu wake; sawa na mwenye kunywa sumu itakayomuua na yule mwenye kujiepusha na hatari atakavyookoka.

Haya ndio makusudio ya kunasibisha uongofu na upotevu kwa Mwenyezi Mungu, katika Aya hii na mfano wake. Mwenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayeungiza uongofu au upotevu ndani ya binadamu, huyo atakuwa ni katika washirikina ambao Mwenyezi Mungu amewasimulia katika Aya iliyotangulia: “Lau Mwenyezi Mungu angelitaka tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya Yeye.”

Mwenyezi Mungu ametakata na wayasemayo madhalimu kabisa.