6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَا يَبْعَثُ اللَّـهُ مَن يَمُوتُ بَلَىٰ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu (kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu. Ndio! Ni ahadi iliyo lazima kwake, lakini watu wengi hawajui
لِيُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي يَخْتَلِفُونَ فِيهِ وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّهُمْ كَانُوا كَاذِبِينَ ﴿٣٩﴾
39. Ili awabainishie yale walioyokhitalifiana na ili wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.
إِنَّمَا قَوْلُنَا لِشَيْءٍ إِذَا أَرَدْنَاهُ أَن نَّقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٤٠﴾
40. Kauli yetu kwa kitu tunachokitaka kiwe, ni kukiambia: Kuwa tu! Basi kinakuwa.
وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي اللَّـهِ مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا لَنُبَوِّئَنَّهُمْ فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَلَأَجْرُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾
41. Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, hakika tutawaweka katika dunia kwa wema. Na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi, lau wangelikuwa wanajua.
الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٤٢﴾
42. Wale wanosubiri na wakamtegemea Mola wao.
WANAAPA KWA MWENYEZI MUNGU
Aya 38 – 42
MAANA
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu.
Katika Aya ya 20 ya Sura hii, Mwenyezi Mungu aliwaambia washirikina kuwa nyinyi mnaabudu aliyeumbwa badala ya kumwabudu muumbaji, Katika Aya ya 24, amewasimulia kuwa wameibandaka jina Qur’an kuwa ni ngano za watu wa kale. Katika Aya ya 35 ametaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa wao wanategemeza shirki yao na shirki ya mababa zao kwa Mwenyezi Mungu.
Katika Aya hii tuliyonayo Mwenyezi Mungu anasema kuwa wao wanapinga ufufuo, wakiapa viapo vya nguvu na kufanya juhudi kueleza kuwa mwenye kufa yake yamekwisha, kwa sababu kitu kikitawanyika hakiwezi kujirudia mara ya pili.
Hayo tumeyazungumzia katika Juz, 13 (13:5).
(Kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu, Ndio! Ni ahadi iliyo lazima kwake, lakini watu wengi hawajui.
Washirikina walikuwa wakiaamini kuweko Mwenyezi Mungu na kuweko washirika wake na walikuwa wakipinga ufufuo. Kwa vile wao wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu, ndio likaja jibu kuwa ufufuo uko tu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu wanayemwamini kuwa yuko, ndiye aliyetoa ahadi ya ufufuo na ahadi yake ni kweli. Ama kuvikusanya viungo baada ya kutawanyika kwake, hilo ni jepesi zaidi kuliko kuviumba. Kwa sababu ambaye amefanya kitu kilichokuwa hakipo basi ni rahisi zaidi kwake kuki kusanya baada ya kutawanyika.
Ili awabainishie yale walioyokhitalifiana na ili wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.
Ufufuo una hekima nyingi sana; mingoni mwazo ni hizi zifuatazo:- Kujulikana mzuri na mbaya, mwema na muovu na malipo wanayostahiki. Hekima nyingine ni Mwenyezi Mungu kuwabainishia viumbe haki waliyokuwa wakihitalifiana; kama vile Tawhid, utume, halali na haramu.
Wale walioapa kuwa hakuna ufufuo wajue na wahakikishe kuwa wao walikuwa waongo katika viapo vyao.
Kauli yetu kwa kitu tunachokitaka kiwe, ni kukukiambia: Kuwa tu! Basi kinakuwa.
Mwenyezi Mungu alianza kuumba kwa neno ‘kuwa’ na atarudisha kwa neno hilohilo, “Na hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi na Yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.
Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhu- lumiwa, hakika tutawaweka katika dunia kwa wema.
Aya hii inawahusu moja kwa moja waliohama (wahajiri) katika maswahaba wa mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
ambao walipata mtihani mwema kwa kumsaidia Mtume; wakacha dunia, watu wao na mali zao kwa kukimbia na dini yao na kumfuata Mtume wao kwa ajili ya kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ama wema ambao Mwenyezi Mungu amewapa duniani kabla ya Akhera ni majumba yao na milki zao mpya hapo Madina, kwani zilikuwa ni bora kuliko zile za Makka.
Na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi kuliko dunia na vilivyomo lau wangelikuwa wanajua!
Maneno hapa, wanaambiwa washirikina ambao walipinga ufufuo, Ama waumini, hasa maswahaba, wao wanajua kwa yakini kuwa thawabu za Akhera ni kubwa na adhimu zaidi. Tumezungumzia kuhusu Hijra na wahajiri katika Juz. 5 (4: 97 – 100) na kuhusu Wahajiri na Answari katika Juz. 10 (72 – 75).
Wale wanosubiri na wakamtegemea Mola wao.
Hakika Mumini wa kweli ana sifa na alama. Zilizo muhimu zaidi ni hizi zifuatazo:-Kuacha ubinafsi, kujitoa mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuvumilia maudhi na mashaka kwa ajili ya kuihakikisha haki na kuibatilisha batili na kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake, sio mali wala cheo au ukoo; sawa na walivyokuwa maswahaba wa Mtume mtukufu(s.a.w.w)
.
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٤٣﴾
43. Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi, Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.
بِالْبَيِّنَاتِ وَالزُّبُرِ وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٤٤﴾
44. Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu. Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.
أَفَأَمِنَ الَّذِينَ مَكَرُوا السَّيِّئَاتِ أَن يَخْسِفَ اللَّـهُ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ يَأْتِيَهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٤٥﴾
45. Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua?
أَوْ يَأْخُذَهُمْ فِي تَقَلُّبِهِمْ فَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٤٦﴾
46. Au Awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka?
أَوْ يَأْخُذَهُمْ عَلَىٰ تَخَوُّفٍ فَإِنَّ رَبَّكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٤٧﴾
47. Au awakamate kidogo kidogo? Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.
أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ يَتَفَيَّأُ ظِلَالُهُ عَنِ الْيَمِينِ وَالشَّمَائِلِ سُجَّدًا لِّلَّـهِ وَهُمْ دَاخِرُونَ ﴿٤٨﴾
48. Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea?
وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مِن دَابَّةٍ وَالْمَلَائِكَةُ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika, nao hawatakabari.
يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٥٠﴾
50. Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.
WAULIZENI WENYE UKUMBUSHO
Aya 43 – 50
MAANA
Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi.
Washirikina waliukana utume wa Muhammad na wakasema kuwa Mwenyezi Mungu hakutuma mtu kuwa mjumbe. Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao kwamba mitume na Manabii wote waliotangulia walikuwa ni watu wanaume wakiletewa wahyi; kama vile: Nuh, Ismail, Musa na wengineo. Kwa sababu lengo la kutumwa Mtume haliwezi kutimia ila ikiwa aliyetumwa ni jinsi ya wale waliotumiwa:
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ﴿٤﴾
“Na hatukumtumma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia.” Juz. 13 (14:4)
قُل لَّوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَّسُولًا ﴿٩٥﴾
“Sema: Ingelikuwa katika Ardhi kuna malaika wanotembea katika ardhi kwa utulivu, basi hakika tungeliwateremshia Malaika kuwa ni mitume wao” (17:95).
Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.
Makusudio ya wenye ukumbusho hapa ni wenye elimu wanaochunga haki; ni sawa wawe ni katika Watu wa kitab au wengineo. Maana ni kuwa enyi washirikina! Mkiwa na shaka na maneno yetu, basi waulizeni wajuzi wawambie kuwa mitume wote walikuwa ni watu.
Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu.
Yaani Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume wakiwa na hoja zilizowazi ambazo ni dalili na ishara. Na kwa vitabu ambavyo vina ubainifu wa dini, itikadi na sharia.
Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.
Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w)
, Makusudio ya ukumbusho hapa ni Qur’an. Ilivyo hasa ni kuwa lengo la kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni kuwaongoza watu kwenye haki na uadilifu na maisha ya amani na raha.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wapate kufikiri’ ni kuwa wapate kuizingatia vizuri Qur’an na kugundua siri zake na malengo yake wapate kujua kuwa imeteremshwa kwa maslahi yao.
Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu.
Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya waliofanya vitimbi hapa ni washirikina wa kiquraish, kwa vile wao ndio waliomfanyia uovu Mtume(s.a.w.w)
na wakamfanyia njama. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewahofisha na aina nne za adhabu:
1.Kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi;
kama alivyomfanyia Qarun:
فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الْأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِن فِئَةٍ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُنتَصِرِينَ ﴿٨١﴾
“Na tukamadidimiza yeye na nyumba yake, wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia zaidi ya Mwenyezi Mungu” (28:81)
2.Au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua
, awaangamize ghafla, kama alivyofanya kwa watu wa Lut.
3.Au awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka
, Yaani awaangamize wakiwa wanashughulika kutafuta riziki.
4.Au awakamate kidogo kidogo.
Neno kidogo kidogo, limefasiriwa kutokana na neno takhawwuf; kama walivyosema wafasiri wengi wakiongozwa na Tabrasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatawaangamiza mara moja bali atawapa balaa ya kupungukiwa na watu na mali kidogo kidogo mpaka wa mwisho wao.
Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.
Miongoni mwa huruma zake ni kutowaharakishia adhabu wanayostahiki waasi, kwa kutumai kuwa watatubia na kuongoka.
Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea.
Wanaoambiwa hapa ni wale waliofanya vitimbi vya uovu, waliotajwa katika Aya iliyotangulia na pia inawezekana wanaambiwa watu wote. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema kwa kuwatahayariza wapinzani wenye inadi.
Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Vivuli vinaelekea’ ni kuwa kila kitu kina kivuli; kama vile milima, miti, wanyama, majengo n.k. Na kauli yake: ‘kuliani na kushotoni’ ni ishara ya upande wa kitu kilicho na kivuli. Kwa sababu kivuli cha kitu kinakuwa upande mmoja kuanzia mawiyo hadi Adhuhuri na kinageuka upande wa pili kuanzia adhuhri hadi machweo.
Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaleta ibara ya kulia kwa upande mmoja na ibara ya kushoto kwa upande wa pili. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu: “ Na vivuli vyao asubuhi na jioni” Juz. 13 (13: 15) Ama kauli yake vikimsujudia Mwenyezi Mungu ni fumbo la utiifu. Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu alipotaja kulia ametaja kwa tamko la umoja na alipotaja kushoto akatumia tamko la wingi (yamin wa shamail)
?
Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu ambayo la karibu zaidi ni kuwa mfumo wa fasihi ya kiarabu wakitaja vitu viwili vyenye maana mbili tofauti kimoja kinatajwa kwa umoja na kingine kwa wingi; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu: “Amejaalia viza na mwanga.”
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kuwahadharisha washirikina na wenye inadi, anasema katika Aya hii, kwamba kila kilicho ulimwenguni – isipokuwa washirikina na wenye inadi – vinamnyenyekea na kufuata amri yake.
Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika nao hawatakabari.
Viumbe vyote vya juu na chini vinafahamisha waziwazi kuweko aliyevifanya na kufahamisha uweza wake, elimu yake na hekima yake na dalili hii ndio tasbihi, tahmid, sujudi na rukui kwa muumbaji.
Pia haya ndio makusudio ya kusujudi kwa viumbe visivyo na akili; kama ambavyo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na hakuna kitu chochote ila kinamtakasa kwa sifa zake” (17: 44). Lengo la kutaja wanyama na Malaika, baada ya kutaja vilivyo katika mbingu na ardhi, ni ubainifu wa kuchanganya aina zote za viumbe, Yametangulia maelezo yake katika Juz, 13 (13:13-25).
Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.
Aya hii inafahamisha waziwazi kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu humhofia na hutii amri yake na makatazo yake, na inafahamisha katika madhumuni yake kwamba mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu kisha akadai kuwa anamwamini na anamhofia, basi huyo ni mwongo katika madai yake.
وَقَالَ اللَّـهُ لَا تَتَّخِذُوا إِلَـٰهَيْنِ اثْنَيْنِ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ ﴿٥١﴾
51. Na amesema Mwenyezi Mungu: Msiabudu miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu. Basi niogopeni mimi tu.
وَلَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَهُ الدِّينُ وَاصِبًا أَفَغَيْرَ اللَّـهِ تَتَّقُونَ ﴿٥٢﴾
52. Ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, na dini ni yake Yeye daima, Je, mtamcha mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu?
وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu, Kisha ikiwagusa dhara mnamlilia yeye.
ثُمَّ إِذَا كَشَفَ الضُّرَّ عَنكُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنكُم بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ ﴿٥٤﴾
54. Kisha anapowaondolea dhara, kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.
لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ فَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٥٥﴾
55. Ili wakufuru tuliyowapa, Basi stareheni mtakujajua.
HAKIKA YEYE NI MUNGU MMOJA TU
Aya 51 – 55
MAANA
Na amesema Mwenyezi Mungu: Msiabudu miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu. Basi niogopeni mimi tu.
Kuna desturi maarufu kwa wanafiqhi isemayo: Hakika dharura hupimwa kwa kiasi chake na kwamba kinachozidi haja na dharura basi ni upuzi.
Desturi hii tunaweza kuitumia kwa yule anayemshirikisha Muumba, kwamba kuchukulia kuwa kuna Muumba mwenye kupanga vizuri mambo na mwenye hekima ni jambo la lazima halikimbiliki katika mtazamo wa kiakili, ambapo haiwezekani kuufasiri ulimwengu na vilivyomo ndani yake kuanzia nidhamu na mfumo isipokuwa lazima awepo mpangaji wa hayo Mwenye hekima.
Kwa hiyo baada ya kuchukulia huku haiwezekani kubakia madai yoyote ya kuchukulia kuwa kuna Mungu mwingine, katika mtazamo wa kiakili; bali akili inalikataa hilo, Angalia katika Juz. 5 (4:48-50) kifungu ‘Dalili ya umoja na utatu’.
Kisha umoja wa Mwenyezi Mungu una athari na mambo yanayolazimiana nao, ameyadokeza Mwenyezi Mungu kwa kauli yake kama yafuatavyo:-
1.Ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini.
Hilo halina upinzani wala ubishi, kwa sababu yeye ndiye aliyeiumba mbin- gu na ardhi na viliyvomo ndani yake.
2.Na dini ni yake Yeye daima.
Makusudio ya dini hapa ni kufuatwa na utiifu. Ikiwa Mwenyezi Mungu ni muumba na mmiliki wa kila kitu basi imethibitika kuendelea kutiiwa Yeye tu si mwenginewe.
3.Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu,
Kwa sababu Yeye ni Muumba wa kila kitu moja kwa moja kwa neno ‘kuwa na kikawa’ au kupitia kitu kingine.
Kisha ikiwagusa dhara mnamlilia Yeye; kisha anapowaondolea dhara, kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.
Muumin wa kweli anamtegemea Mwenyezi Mungu katika hali zote, lakini mfanyabiashara humkimbilia Mwenyezi Mungu wakati wa dhiki na anajipurukusha naye wakati wa raha. Umepita mfano wa Aya hii katika Juz, 11 (10: 12).
Ili wakufuru tuliyowapa.
Makusudio ya kukufuru hapa ni kukufuru neema; zikiwemo kuondolewa madhara. Maana ya ‘ili’ ni natija; kama kusema amejitia kwenye hatari ili afe.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha lakini natija ya neema yake ikawa ni kukufuriwa neema zake.
Basi stareheni mtakujajua
mwisho wenu mbaya na mtajuta, ambapo hakutafaa chochote kujuta kwenu.
وَيَجْعَلُونَ لِمَا لَا يَعْلَمُونَ نَصِيبًا مِّمَّا رَزَقْنَاهُمْ تَاللَّـهِ لَتُسْأَلُنَّ عَمَّا كُنتُمْ تَفْتَرُونَ ﴿٥٦﴾
56. Na ambao hawajui wanawawekea sehemu ya tunavyowaruzuku. Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua.
وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ الْبَنَاتِ سُبْحَانَهُ وَلَهُم مَّا يَشْتَهُونَ ﴿٥٧﴾
57. Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti. Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani.
وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِالْأُنثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٥٨﴾
58. Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.
يَتَوَارَىٰ مِنَ الْقَوْمِ مِن سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ أَيُمْسِكُهُ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿٥٩﴾
59. Anajificha na watu kwa ubaya wa aliyobashiriwa. Je, akae naye juu ya fedheha au amfukie mchangani, Ehe! Yamekuwa maovu wanayoyahukumu.
لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ مَثَلُ السَّوْءِ وَلِلَّـهِ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٦٠﴾
60. Sifa ya wale wasioamini Akhera ni uovu na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.
WANAMFANYIA MWENYEZI MUNGU MABINTI
Aya 56 – 60
MAANA
Na ambao hawajui wanawawekea sehemu ya tunavyowaruzuku, Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua.
Wanaoweka ni washirikina na wanaowawekea ni masanamu. Imesemwa ‘hawajui’ kwa masanamu badala ya ‘hayajui’ kwa vile wao wameyaweka daraja ya wenye akili; kama vile ilivyosemwa katika Aya ya 20 ya Sura hii: “Na wale ambao wanawaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.” Kwa hiyo Qur’an imelitumia neno hilo kulingana na itikadi ya washirikina.
Maana ni kuwa washirikina waliyawekea, fungu katika mali zao, masana- mu ambayo yameganda hayana chochote yajualo wala hisia zozote.
Inawezekana kuwa ‘ambao hawajui’ ni washirikina. Kwa maana ya kuwa washirikina waliyawekea fungu masanamu wakiwa hawajui kuwa masanamu hayana fungu lolote katika mali zao wala katika zisizokuwa mali zao. Lakini kufasiri kwa maana haya kunakalifisha kukadiria maneno yasiyokuwepo. Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6: 136).
Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti, Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani
Waliposikia kuwa Mwenyezi Mungu ana Malaika wakafikiria ni wanawake tena ati ni mabinti wa Mungu. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanayomsifu. Wakamabandikiza yale wanayoyachukia wao, huku wenyewe wakiwa na wavulana wanaowapenda. Mwenyezi Mungu anasema: “Je, Mola wenu amewachagulia wavulana na Yeye akawafanya Malaika ni wanawake? Kwa hakika nyinyi mnasema kauli kubwa (17: 40).
Baadhi ya tafsiri zinasema kuwa walioitakidi hivi ni Bani Khuza’a na Kinana.
Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.
Qur’an hutumia neno ‘bishara’ kwa habari njema na mbaya; kwa mfano:
وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ﴿٢٥﴾
“Na wabashirie walioamini na wakafanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani”
Juz,1 (2:25).
وَبَشِّرِ الَّذِينَ كَفَرُوا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣﴾
Na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo, Juz, 10 (9:3).
Kusawijika uso ni fumbo la kuhuzunika sana. Waarabu hulitumia neno hilo kwa mtu aliyepatwa na mambo ya kuchukiza.
Ingawaje hii ni desturi ya kijahili na Qur’an ikaikemia na kuwasafihi watu wake, lakini kuna Waislamu wengi wanachukia kupata watoto wasichana, na wanasawijika nyuso wakipewa habari za kuzaliwa msichana.
Anajificha na watu kwa ubaya wa aliyobashiriwa.
Wakati wa jahiliya, mtu akiwa mkewe anaanza uchungu wa kuzaa anajificha mpaka ajuea atakayezaliwa, akiwa ni mwanamume anajitokeza na kufurahi na akiwa ni mwanamke huhuzunika na kufikiria afanye nini.
Je, akae naye juu ya fedheha
abakie na udhaliliau amfukie mchangani
akiwa hai? Imesimuliwa kuwa baadhi ya waarabu walikuwa wakiwazika hai watoto wao wa kike, wengine wakiwatupa, wengine wakiwachinja na hata wengine walikuwa wakiwatosa.
Walikuwa wakifanya hivyo ama kwa hasira au kwa kuogopa ukata; kama alivyodokeza Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao.” Juz. 8 (6:151).
Imesimuliwa kuwa mtu mmoja alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: mimi sina raha tangu nisilimu. Kwani nilikuwa na binti wakati wa ujahili, nikamwaamrisha mke wangu ampambe kisha nikatoka naye hadi kwenye bonde lenye kina nikamtupa huko, akaniambia: ‘Baba yangu unaniua! Kila ninapokumbuka kauli yake hiyo sioni kitu chochote kinachonifaa.
Inaweza kudhania kuwa ukatili huu unatokana na ujinga na kutoendela, lakini sisi hivi sasa tuko kwenye zama za kutembea angani, bado wakoloni na wazayuni wanatupa makombora kwa vikongwe, wanawake na watoto huko Vietnam na Palestina.
Wanayatupa sio kwa hasira za kijinga wala kuhofia ukata; isipokuwa ni kwa sababu ya kuzidisha faida na kurundika utajiri. Sasa ni nani kati ya makundi mawili haya ndio walio waovu zaidi. Je, watu wa jahilia au ni wakoloni na wazayuni walio katika wakati wa elimu na mwanga?
Ehe! Yamekuwa maovu wanayoyahukumu na wanayoyazua na kuyafanya, Sisi tuna hakika kabisa kuwa kila mwenye kuzama kwenye uovu mwisho utamrudia mwenyewe.
Sifa ya wale wasioamini Akhera ni uovu na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Mataghuti wana sifa mbaya ambayo ni dhulma, unyang’anyi, ufisadi na kuua watoto na wasio na hatia. Na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu ambazo ni umoja, uadilifu, utukufu na sifa zote nzuri za ukamilifu.
Ilivyo ni kuwa lengo la kutaja sifa za Mwenyezi Mungu pamoja na kuwataja wao ni kujibu kauli yao kuwa Mungu ana wasichana na wao wana wavulana.