8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا عَبْدًا مَّمْلُوكًا لَّا يَقْدِرُ عَلَىٰ شَيْءٍ وَمَن رَّزَقْنَاهُ مِنَّا رِزْقًا حَسَنًا فَهُوَ يُنفِقُ مِنْهُ سِرًّا وَجَهْرًا هَلْ يَسْتَوُونَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٧٥﴾
75. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtumwa mwenye kumilikiwa asiyeweza kitu, na mwengine tuliyemruzuku riziki njema inayotoka kwetu, naye anatoa katika riziki hiyo kwa siri na kwa dhahiri, Je, wanalingana sawa? Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu; bali wengi wao hawajui.
وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلَيْنِ أَحَدُهُمَا أَبْكَمُ لَا يَقْدِرُ عَلَىٰ شَيْءٍ وَهُوَ كَلٌّ عَلَىٰ مَوْلَاهُ أَيْنَمَا يُوَجِّههُّ لَا يَأْتِ بِخَيْرٍ هَلْ يَسْتَوِي هُوَ وَمَن يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَهُوَ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٧٦﴾
76. Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake, Popote anapomuelekeza haleti kheri. Je, huyo anaweza kuwa sawa na yule anayeamrisha uadilifu, naye yuko juu ya njia iliyonyooka?
وَلِلَّـهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا أَمْرُ السَّاعَةِ إِلَّا كَلَمْحِ الْبَصَرِ أَوْ هُوَ أَقْرَبُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٧٧﴾
77. Mwenyezi Mungu ana siri zote za mbingu na ardhi. Wala halikuwa jambo la saa (ya kiyama) ila kama kupepesa kwa jicho au karibu zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
MWENYE UWEZA NA MWENYE KUSHINDWA
Aya 75 – 77
MAANA
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtumwa mwenye kumilikiwa asiyeweza kitu, na mwengine tuliyemruzuku riziki njema inayotoka kwetu, naye anatoa katika riziki hiyo kwa siri na kwa dhahiri, Je, wanalingana sawa?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja, katika Aya iliyotangulia, kwamba washirikina wamemfanyia Mungu mfano, hapa anataja mifano miwili ya kuwafahamisha washirikina kwamba Mwenyezi Mungu hana wa kufanana naye.
Kwa ufupi mfano wa kwanza unaoelezwa na Aya hii, ni kuwa mfano wenu enyi washirikina katika kumfanya Mungu kuwa ni sawa na masanamu unafanana na anayemfanya mtumwa asiyemiliki chochote na kushindwa kufanya chochote kuwa ni sawa na aliye huru ambaye ni tajiri tena mkarimu anatoa kwa siri na kwa dhahiri bila ya kumwogopa yeyote.
Ikiwa akili na maumbile zinaakataa usawa huu, basi imekuwaje nyinyi kumfanya sawa Mwenyezi Mungu Mwenye uweza wa kila kitu na masana- mu yasiyioweza chochote?
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.
Hii ni jumla iliyoingia kati, ikiwa na maana kuwa hakuna yeyote anayestahiki sifa, shukrani na kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Bali wengi wao hawajui
kuwa sifa njema zinaamstahiki Mungu tu sio mwengine.
Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake, Popote anapomuelekeza haleti kheri. Je, huyo anaweza kuwa sawa na yule anayeamrisha uadilifu, naye yuko juu ya njia iliyonyooka?
Huu ni mfano wa pili. Kwa ufupi ni kuwa bubu anayeshindwa na kila kitu hawezi kuwa sawa na anayetamka. Kwa hiyo vipi nyinyi washirikina mnafanya ni sawa katika ibada baina ya mwenye kuwa na sifa zote za ukamailifu na ambaye si chochote?
Mwenyezi Mungu ana siri zote za mbingu na rdhi.
Kila siri mbele ya Mwenyezi Mungu inajulikana na kila ghaibu kwake inaonekana. Punde tu imetangulia Aya ya 73 ya sura hii isemayo: ‘Hakika Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.’
Wala halikuwa jambo la saa (ya kiyama) ila ni kama kupepesa kwa jicho au karibu zaidi.
Hii ni ibara nyingine ya: “Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia kuwa na kikawa”. Ndani yake mna makemeo na kumuhofisha yule anayehalifu na akawa na inadi.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Wala hakuna yeyote anayeweza kumzuia akitaka kuwaangamiza washirikina na viumbe wote
وَاللَّـهُ أَخْرَجَكُم مِّن بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ لَا تَعْلَمُونَ شَيْئًا وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾
Na Mwenyezi Mungu amewatoa matumboni mwa mama zenu hamjui kitu, na amewajaalia usikizi na uoni na nyoyo ili mpate kushukuru.
أَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ مُسَخَّرَاتٍ فِي جَوِّ السَّمَاءِ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا اللَّـهُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٧٩﴾
79. Je, hawaoni ndege waliowezeshwa katika anga ya mbingu? Hawazuii isipokuwa Mwenyezi Mungu, Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaoamini.
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّن بُيُوتِكُمْ سَكَنًا وَجَعَلَ لَكُم مِّن جُلُودِ الْأَنْعَامِ بُيُوتًا تَسْتَخِفُّونَهَا يَوْمَ ظَعْنِكُمْ وَيَوْمَ إِقَامَتِكُمْ وَمِنْ أَصْوَافِهَا وَأَوْبَارِهَا وَأَشْعَارِهَا أَثَاثًا وَمَتَاعًا إِلَىٰ حِينٍ ﴿٨٠﴾
80. Na Mwenyezi Mungu amewafanyia majumba yenu yawe ni maskani. Na akawafanyia kutokana na ngozi za wanyama wenu nyumba mnazoziona nyepesi siku ya kusafiri kwenu na siku ya kutulia kwenu. Na katika sufu zao na manyoya yao na nywele zao mnatengeneza vyombo na vifaa vya kutumia kwa muda.
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّمَّا خَلَقَ ظِلَالًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنَ الْجِبَالِ أَكْنَانًا وَجَعَلَ لَكُمْ سَرَابِيلَ تَقِيكُمُ الْحَرَّ وَسَرَابِيلَ تَقِيكُم بَأْسَكُمْ كَذَٰلِكَ يُتِمُّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْلِمُونَ ﴿٨١﴾
81. Mwenyezi Mungu amewafanyia vivuli katika alivyoviumba na amewafanyia makazi katika milima na amewafanyia nguo za kuwakinga na joto na nguo za kuwakinga na vita vyenu. Ndio hivyo anatimiza neema zake kwenu ili mpate kusilimu.
فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٨٢﴾
82. Na kama wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha tu ujumbe ulio wazi.
يَعْرِفُونَ نِعْمَتَ اللَّـهِ ثُمَّ يُنكِرُونَهَا وَأَكْثَرُهُمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٣﴾
Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha, Na wengi wao ni makafiri.
MWENYEZI MUNGU AMEWATOA MATUMBONI MWA MAMA ZENU HAMJUI KITU
Aya 78 – 83
MAANA
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya hizi baadhi ya dalili za kuweko Muumbaji mwenye kupangilia mambo vizuri, Wakati huo huo dalili hizo ni katika neema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Dalili hizo ni hizi zifuatazo:
PAMOJA NA WENYE MAADA
Na Mwenyezi Mungu amewatoa matumboni mwa mama zenu hamjui kitu na amewajaalia usikizi na uoni na nyoyo ili mpate kushukuru.
Mtu anatoka tumboni mwa mama yake hajui chochote, lakini Mwenyezi Mungu ana zana za maarifa za hisia ambazo ni usikizi na uoni na zana za maarifa ya kiakili ambazo ni akili na maumbile.
Wanaoamini maada wanasema kuwa maada pofu na kiziwi imejianzishia hiyo yenyewe usikizi, uoni na akili. Sisi tunawajibu hivi: Kwanza, asiye nacho hawezi kutoa kitu. Pili, ikiwa maisha na utambuzi unahusika na maada tu basi itabidi usikizi, uoni na moyo uwe ni maada; Kwa sababu kuenea sababu kunapeleka kuenea msababishaji.
Wakisema kuwa kwenye maada kuna aina maalum inayohusika nayo; Kwa namna ambayo inakuwa ni lazima mwili usikie uone na utambue, nasi tutawaambia: ama mseme kwamba maada hiyo yenyewe ndiyo iliyoleta uhai na utambuzi au mseme hapana. Mkisema ndio, itakuwa ni lazima maada iwe na uhai na utambuzi. Mkisema hapana, itakuwa ni lazima maada yote isiwe na uhai kabisa.
Yote mawili hayawezekani; Kwa sababu imeshuhudiwa waziwazi kwamba baadhi ya maada zimeganda na nyingine ziko hai na utambuzi. Na mgawanyiko huu unajulisha kuwa nyuma ya maada kuna nguvu yenye ujuzi na hekima; ndiyo ambayo imeleta uhai, na utambuzi kwenye baadhi ya maada na kuleta kutofautiana kwenye hizo maada.
ULIMWENGU NI MKUBWA KULIKO MAROKETI
Je, hawaoni ndege waliowezeshwa katika anga ya mbingu? Hawazuii isipokuwa Mwenyezi Mungu, Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaoamini.
Makusudio ya kuwezeshwa hapa ni kuwezeshwa kuruka angani; na kuzuwiya ni kuzuiwa wasianguke; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ فَوْقَهُمْ صَافَّاتٍ وَيَقْبِضْنَ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا الرَّحْمَـٰنُ ﴿١٩﴾
“Kwani hawaoni ndege walioko juu yao wanavyozikunjua mbawa na kuzikunja, hawazuii isipokuwa Mwingi wa rehema” (67:19).
Ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu anapitisha mambo kwenye sababu zake, Inaeleweka kwamba Mwenyezi Mungu akilitaka jambo huliandalia sababu.
Kwa hiyo maana ya kauli yake Mungu: ‘Hawazuii isipokuwa Mwingi wa rehema’ ni kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumbia ndege mbawa mbili na akaziwekea vitu vinavyowezesha kuruka angani baina ya mbingu na ardhi:
فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا ﴿٢﴾
“Na ameumba kila kitu akakikadiria kwa kipimo (chake)”, (25:2).
إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾
“Hakika sisi kila kitu tumekiumba kwa kipimo,” (54:49).
Kwa hiyo kuumba, kukadiria na mpangilio ni dalili wazi kuwa kuna Muumbaji mwenye kupangilia vizuri.
Kuna wanouliza, kuwa
: binadamu amevumbua ndege inayokwenda kwa kasi zaidi ya sauti, akatengeneza roketi inayokata maelfu ya maili kwa muda wa saa, ikaweza kufika hadi mwezini. Tena binadamu huyo akatengeneza satelaiti inazozunguuka ardhini na mwezini na kuzungumza na wataalamu kwa lugha zao kutoka huko iliko. Sasa ndege wanoruka angani ni kitu gani mbele ya uvumbuzi huu?
Jibu
: Ajabu ya mtu na akili zake kuuliza swali kama hili. Anashangazwa na ugunduzi huu akisahau yule aliyeifanya akili iliyoweza kugundua vitu hivyo? Lau mtu atafanya insafu akajiangalia yeye mwenyewe na akili yake, ataiona ni kubwa zaidi kuliko kuvumbua maroketi, madege n.k.
Bali lau atafanya insafu akaangalia ulimwengu, atauona ni mkubwa kuliko kuumbwa binadamu aliyevumbua maroketi na masatalaiti. Mwenyezi Mungu anasema:
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٧﴾
“Hakika kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu, lakini watu wengi hawajui” (40:57)
na kuumba mtu ni kukubwa mara nyingi zaidi kuliko kutengeneza maroketi.
Zaidi ya hayo mazungumzo tangu mwanzo yalikuwa juu ya mnyama ndege aliye hai. Ama ndege za kutengeneza, roketi na satalaiti ni katika vitu visivyo na uhai. Kwa hiyo kuvilinganisha na vyenye uhai si mahali pake. Ni wazi kuwa wataalamu wa maroketi wakichanganyika na wataalamu wa kijini hawawezi kuumba nzi hata ubawa wake:
لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ﴿٧٣﴾
“Hawataumba hata nzi ijapokuwa watajumuika kwa hilo, Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake” (22:73).
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ametegemeza kuzuiya ndege angani kwake moja kwa moja kwa vile yeye ndiye sababu ya kwanza na akamapa viungo vya kurukia.
Ashaira wamekana kuweko sababu za kimaumbile kwa aina zote na wakasema, kila vitendo vinategemezwa kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya kuingia kati kitu chochote kwa namna yoyote ile; ni sawa vitendo hivyo vijitokeze kwenye ndege au wadudu, wanyama au binadamu, au hata kwenye maumbile mengine.
Kwa hiyo, kwa upande wao, hakuna uhusiano wowote baina ya kuungua na moto, au kuondoka kiu na kunywa maji, wala baina ya kushiba na kula. Mwenyezi Mungu ndiye anayeunguza wakati wa kugusa moto, ndiye anayeondoa kiu wakati wa kunywa maji na pia ndiye anayeshibisha wakati wa kula, sio kuwa moto wenyewe ndio uliounguza, au maji kuondoa kiu au kuwa chakula ndio kilichoondoa njaa.
Kujibu hoja hiyo inatosha tu kusema kuwa hilo linapingana na hisia na dhamira. Na kwamba linapelekea kuwa mtu ni sawa na mnyama na vitu visiyo na harakati; hawezi kusifika kwa wema wala ubaya na kuwa ni mwenye hatia au asiye na hatia.
Kwa hiyo hatastahiki sifa wala lawama au thawabu wala adhabu; Kwa sababu Mungu ndiye mtendaji na mtu ni chombo tu; sawa na chombo cha kuwekea maji
Na Mwenyezi Mungu amewafanyia majumba yenu yawe ni maskani.
Makusudio ya maskani hapa ni utulivu kutokana na neno la kiarabu sakan; yaani kutulia majumbani, majumba haya ni yale yanayojengwa kwa miti, mawe simiti n.k.
Na akawafanyia kutokana na ngozi za wanyama wenu nyumba mnazoziona nyepesi siku ya kusafiri kwenu na siku ya kutulia kwenu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja majumba yaliyojengwa, sasa anataja majumba ya kutembea nayo; kama vile mahema. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja ngozi na wala hakuaja katani n.k., kwa sababu ngozi ndiyo iliyokuwa ikitumika zaidi katika nchi za uarabuni. Vyovyote itakavyokuwa nyumba, itakuwa inafahamisha kupatikana aliyeiumba na kuitengeneza.
Imenipendeza ibara ya mwanafasihi mmoja na fasaihi yake, ninamnukuu: “kila kilicho juu yako kikakufunika basi ni paa, kila kilicho chini yako basi ni sakafu na kila kinachokusitiri katika pembe nne basi ni kuta, Vyote hivyo ukivipangilia na ukavishikanisha basi hiyo ni nyumba.”
HESHIMA YA NYUMBA KATIKA SHARIA
Aina zote za nyumba ni katika neema za Mwenyezi Mungu. Haijui thamani yake ila yule asiyekuwa nayo. Nyumba ina heshima zake katika sharia ya kiislamu; miongoni mwazo ni kutoingia mtu bila ya hodi na kukaribishwa. Mwenyezi Mungu anasema:
فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا ﴿٢٨﴾
“Basi msiyaingie mpaka mpewe idhini na mkiambiwa rudini basi rudini” (24:28).
Wanafiqh wanasema kuwa mwenye kuchungulia nyumba ya mtu kutoka tunduni au kwenye mwanya wa mlango n.k., mwenye nyumba anayo haki ya kumkemea, akiendela anayo haki ya kumpiga au kumrushia jiwe n.k., akipata madhara mchunguliaji basi ni shauri yake, mwenye nyumba hana lawama yoyote.
Kuna Hadith ya Mtume(s.a.w.w)
isemayo:“Mwenye kukuchungulia ukimtupia jiwe na jicho lake likapofuka basi huna lawama.”
Imam Jafar As- swadiq
amesema:“Tupu ya muumini ni haramu kwa muumini Mwenye kumchungulia muumini katika nyumba yake, basi macho yake ni halali yake katika hali hiyo.”
Na katika sufu zao na manyoya yao na nywele zao mnatengeneza vyombo na vifaa vya kutumia kwa muda.
Makusudio ya vyombo hapa ni mahitaji ya mtu, kama vile matandiko, mavazi n.k. Vifaa ni kila kinachomnufaisha mtu katika mahitaji yake. Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kwa muda’ ni ishara ya kuwa vitu vyote vya maisha ya hapa duniani ni vya muda sio vya kudumu.
VIPI NEEMA YA DHAHABU NYEUSI
Mwenyezi Mungu amewafanyia vivuli katika alivyoviumba.
Kivuli ni kile anachojikinga mtu na joto la Jua.
Na amewafanyia makazi katika milima.
Chochote anachokihitajia mtu ni katika neema akikipata; hata wingu litakalomkinga na jua, bali hata pango katika milima.
Na amewafanyia nguo za kuwakinga na joto.
Vilevle za kuwakinga na baridi. Hazikutajwa kwa sababu ya kujulikana kwa kutajwa moja.
Na nguo za kuwakinga na vita vyenu
. Hizi ni deraya n.k.
Ndio hivyo anatimiza neema zake kwenu ili mpate kusilimu.
Makusudio ya kusilimu hapa ni kutii na kuinyenyekea haki kwa kuifuata na kuitumia.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa watu neema ya majumba, vifaa, mavazi ya kawaida, mavazi ya vita, vivuli na mapango, ili waweze kumshukuru na kumcha Yeye na wasilete ufisadi katika nchi.
Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa waarabu wa wakati wa giza, vivuli, miti, mawingu na mapango ya milima na akazingatia kuwa hizo zote ni katika kutimiza neema zake, na akawataka washukuru kwa hayo na wainyenyekee haki tena akawahadharisha wale watakaoasi.
Ikiwa ni hivyo, itakuwaje kwa neema hii ya dhahabu nyeusi inayotiririka katika miji ya Waarabu? Itakuwaje majumba yanayopasua mawingu wanayoyajenga kwayo? Vipi vifaa wanavyomiliki, zikiwemo ndege gari n.k.?
Mwenyezi Mungu aliwaneemesha waliopita kwa wanyama; kama ngamia, nyumbu baghala na punda. Vilevile kwa majumba ya mawe, ngozi, vifaa vya sufu na manyoya ya wanyama na nguo za kuwakinga na joto na baridi; bali hata mapango. Pia naye amewataka washukuru na wakumbuke.
Je, vipi wale wenye kustarehe hivi leo wakikaa kwenye majumba ya ghorofa wakiibadilisha hewa vile watakavyo – baridi au joto na pembeni mwao kuna mahema ya wakimbizi na huku wanadai kuwa wao wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho?
Na kama wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha tu ujumbe ulio wazi
na hisabu ni juu yetu sisi. Wewe umekwishamaliza kazi yako kwa ukamilifu na sisi tutawalipa hisabu yao na malipo yao.
Imetangulia Aya hii katika Juz.3 (3:20) na Juz.13 (13:40),Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha
. Makusudio ya kuzijua ni kwamba wao wanazitumia. Na kuzikanusha ni kwamba wao wanazitegemeza neema hizo kwa asiyestahiki. Yaani wanakula riziki ya Mwenyezi Mungu na wanamwabudu mwingine.
Na wengi wao ni makafiri.
Inafaa kulitumia neno wengi kwa maana yake ya dhahiri na inafaa pia kulitumia kwa maana ya wote. Makusudio hapa ni kila ambaye imemfikia risala ya Muhammad(s.a.w.w)
na akaikanusha kwa inadi.