TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10001
Pakua: 3647


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10001 / Pakua: 3647
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

Mwandishi:
Swahili

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

وَلَا تَتَّخِذُوا أَيْمَانَكُمْ دَخَلًا بَيْنَكُمْ فَتَزِلَّ قَدَمٌ بَعْدَ ثُبُوتِهَا وَتَذُوقُوا السُّوءَ بِمَا صَدَدتُّمْ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَكُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٩٤﴾

94. Wala msivifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu. Na mkaonja maovu kwa sababu ya kuzuilia kwenu njia ya Mwenyezi Mungu na mkapata adhabu kubwa.

وَلَا تَشْتَرُوا بِعَهْدِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا إِنَّمَا عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٩٥﴾

95. Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilicho kwa Mwenyezi Mungu ndio bora kwenu ikiwa mnajua.

مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٦﴾

96. Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobaki. Na kwa hakika tutawalipa waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٧﴾

97. Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.

فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴿٩٨﴾

98. Unaposoma Qur’an muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani mwenye kufukuzwa.

إِنَّهُ لَيْسَ لَهُ سُلْطَانٌ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٩٩﴾

99. Hakika yeye hana madaraka juu ya walioamnini na wakamtegemea Mola wao.

إِنَّمَا سُلْطَانُهُ عَلَى الَّذِينَ يَتَوَلَّوْنَهُ وَالَّذِينَ هُم بِهِ مُشْرِكُونَ ﴿١٠٠﴾

100. Hakika madaraka yake yako juu ya wale tu wanaomtawalisha na wale ambao kwaye wanashirikisha.

KILICHO KWA MUNGU NI BORA

Aya 94 – 100

Katika Aya ya 91, ya sura hii, Mwenyezi Mungu amesema: “Wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha,” katika Aya 92 akasema: Wala msiwe kama mwanamke ambaye ameufumua uzi wake baada ya kuusokota na kuwa mgumu Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa kundi moja lina nguvu zaidi kuliko jengine?” na katika Aya hii tunayoifasiri anasema:

MAANA

Wala msivifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu , Je, nini lengo la kukaririka huku?

Razi, akiwanukuu wafasiri, anasema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwanza amewakataza watu wote kutovunja viapo na ahadi, kisha akawahusu watu maalum ambao ni wale waliombai Muhammad(s.a.w.w) kwa Uislamu.

Ufafanuzi huu uko mbali na ufahamisho wa Aya. Kwa sababu kukataza kuvunja ahadi na kiapo kumekuja kiujumla bila ya kufungwa na baia au jambo jenginelo.

Jawabu bora ni kuwa kukaririka kukataza hapa kumekuja kwa sababu zake ambazo zinatajwa, akasema Mwenyezi Mungu baada ya katazo la kwan- za:” Ilhali mmekwishamfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu.´ Hapo anawakumbusha kuwa wao wamekwishamfanya Mwenyezi Mungu ni mdhamini, kwa hiyo ni lazima watekeleze; vinginevyo watakuwa wamemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu hasa.

Baada ya kutaja katazo la pili akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwayo.” Hii ni kuwakumbusha walioapa kwamba Mwenyezi Mungu anawapa mtihani ili wastahiki kile watakacholipwa.

Baada ya katazo la tatu akasema:Usije mguu ukateleza baada ya kuimarika kwake. Hili ni kemeo na kiaga kwa yule mwenye kuiacha haki akafuata batili na uwongofu kwa upotevu.

Na mkaonja maovu kwa sababu ya kuzuilia kwenu njia ya Mwenyezi Mungu na mkapata adhabu kubwa.

Kila mwenye kuizuilia njia ya Mwenyezi Mungu na haki ni wajibu kumzuia kwa mawaidha na mwongozo. Akitubia na kurejea nyuma, ndio sawa. Vinginevyo itakuwa ni wajibu kumpiga jihadi na inafaa kumchukua mateka au kumuua. Hii ni katika dunia. Ama huko Akhera atakuwa na adhabu kuu.

Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo.

Ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kulazimiana na haki na kuitumia; ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi na kiapo. Makusudio ya thamani ndogo ni manufaa ya kidunia hata kama yatakuwa mengi. Maana ni kuwa manufaa yenu ya kibinafsi yasiathiri haki mkaiuza kwa mali na cheo au kwa starehe yoyote katika dunia hii. Kwani hakika dunia na vilivyomo si chochote kulinganisha na yale ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia watiifu na wahisani.

Hakika kilicho kwa Mwenyezi Mungu ndio bora kwenu kuliko manufaa ya dunia, kwa vyovyote yakavyofikia na yatakavyokuwa,ikiwa mnajua.

Tofauti ni kubwa baina ya manufaa ya Akhera na ya kidunia; kisha Mwenyezi Mungu akabainisha wajihi wa tofauti hiyo kwa kusema:

Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobaki.

Hakuna mwenye shaka kwamba vinavyodumu ni bora kuliko vinavyokwisha. Zaidi ya hayo ni kuwa manufaa ya dunia yanaambatana na tabu na shida. Yakiwa matamu upande fulani yanakuwa machungu kwa upande mwengine. Lakini manufaa ya Akhera ni safi kabisa hayambatani na chochote.

Na kwa hakika tutawalipa waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.

Ilivyo ni kuwa mwito wa haki na uimara wake unaleta maudhi kutoka kwa wapinzani. Kwa hiyo mwenye kuvumilia misukosuko atakayoipata katika njia ya haki na akawa imara katika jihadi na maadui wa haki mpaka mwisho, basi Mwenyezi Mungu atamlipa malipo ya wavumilivu walio na juhudi.

Unaweza kuuliza : kauli yake hii Mwenyezi Mungu inaashiria kwamba Mwenyezi Mungu atawalipa kwa yale mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya, ama yale mazuri ya kawaida hayatalipwa kitu. Je, maana haya ndiyo yaliyokusudiwa na Aya?

Jibu : Hakika matendo ya mtu yanagawanyika kwenye utiifu, wajibu na sunna. Vile vile kwenye maasi na halali. Hakuna mwenye shaka kwamba yaliyo mazuri zaidi ni utiifu na yaliyo mabaya zaidi ni uasi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawalipa thawabu wale wenye kuwa na subira kutokana na yote ya utiifu waliyoyafanya, ikiwemo subira na uvumilivu katika kumtii Mwenyezi Mungu ambako ndiko bora na kutukufu zaidi, Ama mwenye kutenda yaliyo halali hastahiki adhabu wala thawabu.

Kwa hiyo makusudio ya mazuri zaidi waliyoyafanya ni yale ya utiifu waliyoyafanya kwa namna zake zote na sio makusudio kuwa ni subira tu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameweka wazi kwambaYeye atawalipa waliosubiri kutoka na mema yao, na akanyamazia maovu yao. Katika unyamazo huu kuna ahadi au mfano wa ahadi kwamba Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawasamehe kwa rehema yake na fadhila zake.

Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.

Katika Aya hii kuna njia zifuatazo:-

Aya imefahamisha kwamba kila mmoja kati ya mwanamume na mwanamke anapimwa kwa vitendo vyake mbele ya Mwenyezi Mungu; na kwamba hakuna mbora zaidi kati yao isipokuwa kwa takua. Ikiwa mwan- mke atakuwa mcha Mungu zaidi ya mwanamume basi atakuwa ni bora na mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko mwanamume na ikiwa mwanamume atakuwa anamcha Mungu zaidi ya mwanamke basi atakuwa ni bora na mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko mwanamke.

Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 2 (2:228) kifungu cha ‘Mwanamume na mwanamke katika sharia ya Kiislamu.

Aya imefahamisha vilevile kuwa imani na matendo mema ndio sababu ya malipo na thawabu za akhera, Ama moja pekee haitoshelezi. Lakini tukichanganya Aya hii na ile isemayo: Atakayefanya wema uzani wa chembe atauona, (99:7), inakuwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anambadilishia kafiri mwenye kufanya wema kwa siha, mali, jaha au kurefuka umri katika maisha ya dunia, au kupunguziwa adhabu huko akhera, Yametangulia maelezo haya katika, Juz. 7 (3:178) kwa anuani ya Kafiri na amali ya kheri.

Wametofautiana katika uhai mwema uliotajwa katika Aya hii, kuwa je, utapatikana duniani au Akhera?

Ni jambo la kushangaza kwa wafasiri kutofautiana katika hilo, na wao wenyewe wanashuhudia kwa hisia na macho kwamba dunia ni pepo ya makafiri na jela ya muumini! Pia wanasoma na kuifafanua Aya isemayo:

وَلَوْلَا أَن يَكُونَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً لَّجَعَلْنَا لِمَن يَكْفُرُ بِالرَّحْمَـٰنِ لِبُيُوتِهِمْ سُقُفًا مِّن فِضَّةٍ وَمَعَارِجَ عَلَيْهَا يَظْهَرُونَ ﴿٣٣﴾وَلِبُيُوتِهِمْ أَبْوَابًا وَسُرُرًا عَلَيْهَا يَتَّكِئُونَ ﴿٣٤﴾ وَزُخْرُفًا وَإِن كُلُّ ذَٰلِكَ لَمَّا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةُ عِندَ رَبِّكَ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٣٥﴾

“Na lau isingekuwa watu watakuwa umma mmoja, bila shaka tungelifanya nyumba za wanaomkufuru Mwingi wa rehema zina dari ya fedha na ngazi wanazopandia na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyoviegemea na mapambo, lakini yote si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia. Na Akhera iliyoko kwa Mola wako ni ya wenye takua” (43:33 – 35).

Kwa hiyo basi tunaipa nguvu kauli ya kuwa makusudio ya Aya ni maisha mema Peponi na kwamba kaulia yake Mwenyezi Mungu: ‘tutawapa ujira wao...’ inaungana kitafisiri na kuli hii:”tutamhuisha maisha mema” Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu, katika Aya ya 105 ya sura hii: “. Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu, na hao ndio waongo “ (16:105).

Unaposoma Qur’an muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani mwenye kufukuzwa.

Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) na hukumu inawaenea wote. Maana ni kuwa mwenye kutaka kusoma Qur’an aseme kabla ya kusoma “Audhu billahi minashhaytwnir-rajim” (Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na shetani mwenye kufukuzwa).

Katika tafsir ya Razi kuna maelezo kwamba Malik na Daud Dhahiri wanasema kuwa kusoma Audhu ni baada ya kusoma Qur’an sio kabla yake. Wamesema hivyo kwa kuganda kwenye dhahiri ya tamko. Vyovyote iwavyo, kusoma Audhu ni sunna wala sio wajib kwa maafikiano ya wote.

Hakika yeye hana madaraka juu ya walioamnini na wakamtegemea Mola wao mlezi. Hakika madaraka yake yako juu ya wale tu wanaomtawalisha na wale ambao kwaye wanashirikisha.

Neno ‘yeye’ linamrudia shetani na neno ‘kwaye’ inawezekana kuwa linamrudia Mwenyezi Mungu, kwa maana ya kuwa wanamshrikisha Mungu au likamarudia shetani kwa maana ya kuwa wanamshirikisha Mungu kwa sababu ya kumtii shetani.

Maana ni kuwa shetani hana njia yoyote ya kumfanya binadamu afanye haramu isipokuwa kwa wasiwasi na hadaa, na hawamuitikii kwa hilo isipokuwa wenye nyoyo na imani dhaifu. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 13 (14:22) na Juz, 14 (15: 39 – 42).

وَإِذَا بَدَّلْنَا آيَةً مَّكَانَ آيَةٍ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يُنَزِّلُ قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مُفْتَرٍ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٠١﴾

101. Na tunapoibadilisha Aya mahali pa Aya nyingine, na Mwenyezi Mungu anajua anayoteremsha, wao husema: Hakika wewe ni mzushi, Bali wengi wao hawajui.

قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ لِيُثَبِّتَ الَّذِينَ آمَنُوا وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Sema, ameiteremsha Roho takatifu kutoka kwa Mola wako, ili awathibitishe wale walioamini na kuwa ni uwongofu na bishara kwa Waislamu.

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ لِّسَانُ الَّذِي يُلْحِدُونَ إِلَيْهِ أَعْجَمِيٌّ وَهَـٰذَا لِسَانٌ عَرَبِيٌّ مُّبِينٌ ﴿١٠٣﴾

103. Na hakika tunajua kwamba wao wanasema yuko mtu anayemfundisha, Lugha ya huyo wanayemuelekezea sio fasaha na hii ni lugha ya kiarabu bayana.

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ لَا يَهْدِيهِمُ اللَّـهُ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٠٤﴾

104. Hakika wale ambao hawaziamini Aya za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao watapata adhabu chungu.

إِنَّمَا يَفْتَرِي الْكَذِبَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٠٥﴾

105. Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu, na hao ndio waongo.

AYA MAHALI PA AYA NYINGINE

Aya 101 – 105

LUGHA

Tofauti kati ya neno Aa’jamiyy na A’jamiyy ni kuwa la kwanza lina maana ya mtu asiyekuwa fasaha katika Kiarabu, hata kama ni mwarabu, Na lapili lina maana ya lugha nyingine isiyokuwa Kiarabu.

MAANA

Na tunapobadilisha Aya mahali pa Aya nyingine, na Mwenyezi Mungu anajua anayoteremsha. Wao husema: “Hakika wewe ni mzushi, Bali wengi wao hawajui.

Wanaosema hapa ni washirikina waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaumba viumbe na Yeye ni mwenye hekima, Mjuzi wa kujua masilahi yao na uharibifu wao. Mara nyingine hekima inaona kuwa ni masilahi kuweka kwa waja wake sharia ya hukumu kwa muda fulani, wakafanya.

Kisha ukiisha ule muda, sharia ile inaondolewa na Yule ambaye imetukuka hekima yake huweka hukumu nyingine mahali pa ile hukumu ya kwanza kulingana na masilahi vilevile.

Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Tunapobadilisha Aya mahali pa Aya nyingine’

Washirikina walipokuwa wakiona hivi humwambia Muhammad(s.a.w.w) kuwa wewe unajifanyia mwenyewe tu haya kisha unayanasibisha kwa Mwenyezi Mungu kwa uwongo na uzushi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua kuwa Yeye ndiye aliyeteremsha mabadiliko haya kwa Mtume wake mkweli, mwaminifu na anajua kuwa wao ndio wazushi kwa kusema kwao kuwa Mtume ni mzushi.

Tafsiri wazi zaidi niliyosoma kuhusu Aya hii ni ile iliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba inapoteremshwa Aya ya ugumu kisha ikateremshwa Aya ya laini, maquraishi husema kuwa Muhammad anawachezea maswahaba zake; leo anawaamrisha hivi na kesho anawakataza na kwamba yeye hayasemi haya ila yeye mwenyewe tu, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii, tumezungumzia kuhusu kufuta hukumu katika Juz. 1 (2:106).

Sema ameiteremsha Roho takatifu kutoka kwa Mola wako, ili awathibitishe wale walioamini na kuwa ni uwongofu na bishara kwa Waislamu.

Roho takatifu ni Jibril. Ameitwa hivyo kwa sababu ameteremsha Qur’an ambayo ni takatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu hadi kwa Muhammad(s.a.w.w) . Umetangulia mfano wa Aya hii katika Aya ya 89 ya sura hii.

Hapa imetajwa kwa kuwarudi washirikina walionasibisha kubadilisha kwa Mtume. Kule imetajwa kwa mnasaba wa kuwa Mwenyezi Mungu amesema atamleta shahidi kwa kila umma na Muhammad atakuwa shahidi wa umma wake kwamba yeye amiefikisha Qur’an ambayo ni ubainifu wa kila kitu.

Na hakika tunajua kwamba wao wanasema yuko mtu anayemfundisha.

Washirikina walimtuhumu Muhammad(s.a.w.w) kwamba yeye anafundishwa Qur’an na mtu mwingine. Hakuna mwenye shaka kwamba hii ni aina ya vita vya propaganda za uwongo wanazozitangaza wafisadi duniani kwa masilahi yao. Leo watu wameendelea na mfumo wa aina yake katika propaganda dhidi ya wenye ikhlasi na viongozi wema. Wamekuwa na ufundi ambao unawahadaa watu wema wengi walio wasafi.

Lugha ya huyo wanayemuelekezea sio fasaha na hii ni lugha ya kiarabu bayana.

Yaani lugha ya huyo mtu wanayemsema ni kiarabu cha mtaani.

Hii ni kuwarudi washirikina na kauli yao kuhusu Muhammad(s.a.w.w) kwamba anafundiswa na mtu mwingine. Hapa inaonyesha kwamba huyo mtu waliyemsema kuwa anamfundisha, lugha yake ni ya mtaani na lugha ya Qur’an ni kiarabu fasihi, Sasa itawezekana vipi asiyejua fasihi amfundishe mwengine fasihi.

Walirudiarudia uzushi huu maadui wa Uislamu baadae na mpaka leo wahubiri wengi wa Kikiristo wanathubutu kusema, kwa kutojua au kujitia kutojua, kwamba kwenye Qur’an kuna fani na hekima ambazo wakati huo hazikuwa na athari yoyote.

Kama tukichukulia kuwa zilikuweko, basi isingewezekana yeyote kuzikusanya na kuzijua na kama angelizijua basi umashuhuri wake ungelizidi ule wa Aristatle ambaye Waarabu wanamwita mwalimu wa kwanza. Licha ya wao kujua kwamba hakuwa na yeyote aliyekuwa wakati wa Mtume aliyedaiwa kujua hizo elimu zilizomo ndani ya Qur’an.

Hakika wale ambao hawaziamini Aya za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao watapata adhabu chungu.

Makusudio ya Aya za Mwenyezi Mungu ni dalili zinazosema kuhusu kuweko kwake, miujiza inayoshuhudia utume wa Mitume na hukumu zilizoteremshwa kwao. Ama makusudo ya uongofu hapa ni thawabu; yaani Mwenyezi Mungu hatampa thawabu, bali atamwadhibu kwa aina za adhabu

MWONGO KAFIRI

Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu wala ufufuo, hisabu na malipo; kama washirikina waliomwambia Muhammad(s.a.w.w) yale waliyomwambia.

Na hao ndio waongo.

Wanajasiri kusema uwongo na kufanya ufisadi na dhambi kwa vile wao hawaogopi adhabu ya uwongo na wala hawatarajii thawabu.

Unaweza kuuliza : Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu’ si inatosha, sasa kuna haja gani tena ya kusema: Na hao ndio waongo? Je, kuna makusudio gani ya kukaririka huku?

Wafasiri wamejibu kuwa : lengo ni kutanabahisha kuwa sifa ya uwongo kwao imethibiti; sawa na kumwambia mtu: ‘Wewe ni mwongo tena mwongo sana’ yaani hali yako na mazoweya yako ni uwongo tu.

Swali la pili ni : Mwenyezi Mungu anasema “Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu” Hii si ni kuwafanya makafiri kuwa ndio waongo tu; na inajulikana kuwa kuna makafiri walio wakweli sana na wakutegemewa zaidi, katika mazungumzo yao, kuliko wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho?

Jibu : Hakika Mwislamu muongo anamwamini Mwenyezi Mungu kinad- hariya na ni kafiri kimatendo. Kwa hiyo yeye kwa wasifu wake ni muumini kinadhariya na kifikra, atachukuliwa duniani kuwa ni Mwislamu. Na kafiri kwa wasifu wake atachukuliwa kuwa ni kafiri kulingana na Aya hii na yaliyopokewa kutoka kwa Mtume, alipoulizwa: Je, Mumin anasema uwongo? Akajibu: La; kisha akasoma Aya hii.

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٠٦﴾

106. Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake, Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿١٠٧﴾

107. Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya akhera, Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَسَمْعِهِمْ وَأَبْصَارِهِمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٠٨﴾

108. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.

لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٠٩﴾

109. Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.

ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ هَاجَرُوا مِن بَعْدِ مَا فُتِنُوا ثُمَّ جَاهَدُوا وَصَبَرُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٠﴾

110. Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

يَوْمَ تَأْتِي كُلُّ نَفْسٍ تُجَادِلُ عَن نَّفْسِهَا وَتُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١١١﴾

111. Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.

MOYO WAKE UMETUA JUU YA IMANI

Aya 106 –111

MAANA

Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake.

Tabari ametaja njia nne za irab ya jumla hii. Razi ametaja njia nne na akachagua moja kuwa iko mahali pa maf ’ul; kwa maana ya kukadiriwa kuwa, ninamkusudia kumtaja anayemkufuru...

Ama sisi tumechagua kuwa iko mahali pa mubdata (jumla ya kuanzia maneno) na Khabar yake (ukamailisho wake) ni jumla inayokadirwa kuwa, anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yake. Jumla hii inafahamika kutokana na jumla iliyo mwishoni mwa Aya hiyo hiyo: ‘Basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao.

Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani.

Hii inafahamisha kuwa iko ruhusa ya kutamka neno la kufuru kwa ajili ya kujiokoa na kuuuliwa ikiwa mwenye kutamka ni muumini wa kweli.

Imeelezwa katika tafsiri ya Razi: Watu walilazimishwa neno la kufuru. Miongoni mwao ni Ammar na wazazi wake Yasir na Summayya. Vilevile Suhayb, Bilal, Khabbab na Salim, Wote hao waliaadhibiwa.

Summayya alifungwa baina ya ngamia wawili na akachomwa mkuki moyoni mwake na Yasir naye pia akauawa, lakini Ammar aliwapatia kile walichotaka kwa ulimi wake, akiwa amelazimika kufanya hivyo. Baadhi ya watu wakasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika Ammar amekufuru.

Mtume(s.a.w.w) akasema: Hapana! Hakika Ammar imani imemmjaa kuanzia utosini mwake hadi nyayoni mwake.

Ammar akamajia Mtume huku akilia, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akawa anampangusa machozi na kumwambia: Kwani una nini? Wakikurudia, rudia uliyosema, Yametangulia maelezo ya Taqiya katika Juz, 3 (3:28).

Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumtaja muumini halisi aliyedhihirisha kufu- ru, kuwa yeye anakubaliwa udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu; sasa anamtaja yule kafiri wa kweli asiyekuwa na jengine zaidi ya kupendelea ukafiri. Hakuna malipo kwa huyu isipokuwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake kali.

Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya Akhera.

Hiyo ni ishara ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Wamestahabu, yaani wameathirika zaidi, Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaondolea makafiri rehema yake na atawaadhibu kwa moto wake, kwa sababu wao wameathirika zaidi na maisha ya dunia na starehe zake.

Maana ya yote haya ni kuwa kila mwenye kuathirika na matamanio kuliko haki na mambo ya sasa kuliko yajayo, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama kafiri na mshirikina katika kustahiki ghadhabu na adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.

Kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu hawazingatii kuwa ni wenye kuongoka baada ya kustahabu ukafiri kuliko imani. Vilevile hawaongozi kwa maana ya kuwa hawalipi thawabu. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu amewaongoa kwa maana ya kuwa amewawekea dalili za kutosha juu ya kuweko kwake Mwenyezi Mungu na utume wa mitume yake. Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ ﴿١٧﴾

Na ama Thamud tuliwaongoa, wakastahabu upofu kuliko uongofu” (41:17).

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.

Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz. 1 (2:2).

Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.

Wala hapana hasara kubwa zaidi kuliko ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja waumini halisi na makafiri dhahiri, hapa sasa anataja wale waliokuwa wamemwamini Mtume, lakini wakabakia Makka na wasihame naye kwenye Hijra, Wakawapa washirikina baadhi ya waliyoyataka. Kisha wakatubia, wakahama kwa Mtume na wakasubiri kwa kupigania jihadi dhidi ya washirikina na wafisadi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha hukumu ya ya hawa kwa kusema: “Bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.”

Makusudio ya baada ya hayo ni hayo waliyoyatenda; kama unavyofahamisha mfumo wa maneno. Inawezekana pia ni kwa maana ya baada ya kutubia kwao pamoja na kuhama, jihadi na subira.

Katika tafsiri nyingi imeeelezwa kuwa Aya hii ilishuka kwa sababu ya jamaa fulani katika maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) waliokuwa wamebaki nyuma Makka na wasihame pamoja na Mtume. Washirikina wakawapa shida sana mpaka baadhi yao wakafitinishwa na dini yao; kisha wakajuta, lakini wakahofia kuwa toba yao haitatakabaliwa; ndipo ikashuka Aya hii.

Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea.

Yaani kila mtu siku ya Kiyama atajitetea mwenyewe, wala hatajishuguhulisha na mwingine:

لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾

Kila mtu siku hiyo atakuwa na jambo linalomshughulisha, (80:37).

Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.

Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٢﴾

“Na ili ilipwe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa” (45:22)

na pia kauli yake:

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا تَسْعَىٰ ﴿١٥﴾

Ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyahangaikia, (20:15).

Yamekaririka maana ya Aya hii katika Aya nyingi.

وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا قَرْيَةً كَانَتْ آمِنَةً مُّطْمَئِنَّةً يَأْتِيهَا رِزْقُهَا رَغَدًا مِّن كُلِّ مَكَانٍ فَكَفَرَتْ بِأَنْعُمِ اللَّـهِ فَأَذَاقَهَا اللَّـهُ لِبَاسَ الْجُوعِ وَالْخَوْفِ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ ﴿١١٢﴾

112. Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hiyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.

وَلَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مِّنْهُمْ فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ وَهُمْ ظَالِمُونَ ﴿١١٣﴾

113. Na alikwishawajia Mtume kutoka miongoni mwao, lakini wakamkadhibisha, basi ikawafikia adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.

MJI ULIOKUWA NA AMANI

Aya 112 – 113

MAANA

Wafasiri wametofautiana kuhusu mji uliotajwa kuwa, je, ni mji hasa au ni kiasi cha kukadiria tu kwa ajili ya kupigia mfano? Razi amenukuu kutoka kwa wafasiri wengi kuwa makusidio ya mji huo ni Makka.

Vyovyote iwavyo, sifa hizi zinafanana na Makka na watu wake. Kwa sababu watu walikuwa na amani ya nafsi na mali zao; hawakuwa na hofu ya vita wala ujambazi; kama ilivyokuwa kwa miji mingine ya waarabu.

Pia wakazi wa hapo hawakuwa na haja ya kuhemea chakula, kwa sababu riziki ilkuwa ikiwajia kutoka kila mahali, kutokana na kuitikiwa dua ya Ibrahim(a.s) :

رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ ﴿٣٧﴾

Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda. Juz; 13: (14:37).

Lakini watu wa Makka walizikufuru neema za Mwenyezi Mungu kwa kumkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) na wakaazimia kumuua mpaka akalazimika kuuhama mji wake.

Watu wa Makka walipatwa na njaa kwa dua ya Mtume(s.a.w.w) , pale aliposema: “Ewe Mola wangu! Wadhikishe kwa madhara na uajaalie miaka (ya shida) kama miaka ya Yusuf, Basi Mwenyezi Mungu akaitikia maombi yake. Wakapatwa na shida mpaka wakawa wanakula mizoga, majibwa, mifupa iliyochomwa, manyani na ngozi iliyochanganywa na damu.

Mtu alikuwa akiangalia mbinguni na kuona moshi kutokana na njaa. Ama hofu iliyowapata ni pale nchi ilipowatingisha wakaanguka ni mateka wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

فَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاشْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ {114 }

114. Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu.

إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٥﴾

115. Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.

وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَـٰذَا حَلَالٌ وَهَـٰذَا حَرَامٌ لِّتَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ ﴿١١٦﴾

116. Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu, mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu, Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu.

مَتَاعٌ قَلِيلٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١١٧﴾

117. Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.

وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا مَا قَصَصْنَا عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١١٨﴾

118. Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla, Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.

ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٩﴾

119. Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

KULENI NA MSHUKURU

Aya 114 – 119

MAANA

Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu. Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.

Umetangulia mfano wa Aya hizi na tafsiri zake katika Juz. 2 (2:173) na katika Juz. 6 (5: 3)

Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu.

Watu wa jahilia walikuwa wakijihalalalishia na kujiharamishia wao wenyewe tu; kisha wananasibisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; kama kuhalalisha nyamafu, damu, nyama ya nguruwe na mnyama aliyechinjwa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Vilevile kusema kuwa aliye tumboni mwa mnyama huyu ni wa wanaume tu na ni haramu kwa wanawake na mengineyo yaliyotajwa katika Juz, 8 (6: 139 – 139).

Ndipo Mwenyezi Mungu akawakataza hayo na kusema kuwa ni uwongo na uzushi:Mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu.

Kila mwenye kumtegemezea Mwenyezi Mungu hukumu, kauli au jambo lolote bila dalili mkataa basi atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo.

Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu. Vipi watafaulu na Mwenyezi Mungu amewakasirikia na amewaandalia adhabu chungu?

Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.

Manufaa yoyote katika dunia hayalingani hata na ile adhabu ndogo ya akhera, sikwambi tena ikiwa ni ahabu kubwa:

نُمَتِّعُهُمْ قَلِيلًا ثُمَّ نَضْطَرُّهُمْ إِلَىٰ عَذَابٍ غَلِيظٍ ﴿٢٤﴾

Tunawastarehesha kidogo kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu. (31:24).

Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla.

Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu anamkumbusha yale aliyomwambia hapo nyuma: “Na kwa wale walio mayahudi tuliharamisha kila mwenye kucha. Na katika ng’ombe na mbuzi na kondoo tukawaharamishia mafuta yao; isipokuwa yale iliyobeba migongo yao, au matumbo, au iliyochanganyika na mifupa, Juz. 8 (6:146).

Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.

Kwa sababu wao walimwasi Mwenyezi Mungu na wakapetuka mipaka, ndipo akawaadhibu kwa uharamisho huu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

فَبِظُلْمٍ مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ ﴿١٦٠﴾

“Basi kwa dhuluma ya ambao ni mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa,” Juz.6 (4:160).

Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Umepita mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz.7 (6: 54).