TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16094
Pakua: 3335


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 19 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16094 / Pakua: 3335
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Sura Ya Kumi Na Saba: Al –Israi.

Ina Aya 111, Imeshuka Makka, Isipokuwa Aya tano, na imesemekana ni nane.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu.

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

1. Ametakasika aliyempeleka usiku mja wake kutoka Msikiti Mtakatifu mpaka msikiti wa mbali ambao tumevibariki vilivyo kandoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

ISRAI

Aya 1

MAANA

Ametakasika aliyempeleka usiku mja wake kutoka Msikiti Mtakatifu mpaka msikiti wa mbali ambao tumevibariki vilivyo kandoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

MAANA YA NEON ISRAI

Maana ya neno Israi katika lugha ya kiarabu ni kutembea usiku. Makusudio ya neno ‘mja wake’ hapa ni Muhammad(s.a.w.w) . Msikiti mtakatifu ni ule ulioko Makka kwenye Al-ka’ba.

Anasema mwenye Rawhul-lbayan na wengineo: “Riwaya iliyo sahihi zaidi ni kuwa safari ya Israi ilianzia kwenye nyumba ya Ummu Hani, dada yake Ali bin Abu Twalib.”

Msikiti wa mbali (Masjidul-Aqswa) ni hekalu la Nabii Suleiman. Umeitwa msikiti kwa sababu ni mahali pa kusujudu, kutokana na neno la Kiarabu masjid (msikiti) lenye maana ya mahali pa kusujudu. Na umeitwa Masjidul Aqswa (msikiti wa mbali), kwa sababu ya kuwa mbali na Makka. Msikiti huo umebarikiwa kandoni mwake kwa baraka za kidini, kwa vile ni nchi ya mitume na kwa baraka za kidunia kwa mito na miti.

Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

Inawezekana ‘Yeye’ kuwa ni Mwenyezi Mungu kwa maana ya kuwa anamjua Mwenye kuamini na mwenye kukanusha tukio la Israi. Pia inawezekana kuwa ‘yeye’ hapa ni Muhammad(s.a.w.w) kwa maana ya kuwa anajua ukuu na utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Imesemekana kuwa Israi ilikuwa usiku wa kuamkia tarehe 27 Rajab (mfunguo kumi), Na pia imesemekana ilikuwa 17 Rabiul-awwal (mfunguo sita).

ISRAI KWA ROHO NA MWILI

Ulama wengi wanalitumia neno israi kwa safari ya Mtume(s.a.w.w) kutoka Masjidul-haram (Msikiti Mtukufu) ulioko Makka, hadi Masjidul-aqswa (Msikiti wa mbali) ulioko Baytul- muqaddas (Nyumba yenye kutakaswa).

Na wanalitumia neno Mi’raj (miraji) kwa safari ya kutoka Baytul-muqad- das hadi juu mbinguni. Wengine hawatofautishi baina ya maneno hayo mawili; wanatumia Miraji kwa kupanda mbinguni na Israi kwa kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas[1] .

Wote wameafikiana kutokea tukio hili kutokana na nukuu za Qur’an na Hadith za Mtume. Lakini wametofautiana kuwa je, lilikuwa kwa roho tu bila ya mwili au kwa mwili na roho? Sisi tuko pamoja na wale wasemao lilikuwa kwa mwili na roho. Hapa tutazungumzia Israi – safari ya kutoka Msikiti Mtakatifu hadi Msikiti wa mbali, Ama miraji - kupanda juu mbinguni, mazungumzo yake yatakuja katika Juz; 27 Sura 53.

Wale wanaosema kuwa ilikuwa ni kwa mwili na roho wametoa dalili zifuatazo:

1. Israi ni jambo linaloingia akilini na dhahiri ya wahyi umelitolea dalili; pale aliposema Mwenyezi Mungu: “Aliempeleka usiku mja wake” na hakusema roho ya mja wake. Neno mja linatumika kwa roho na mwili; kama alivyosema Mwenye Mungu:

Je, unamuona yule ambaye anamkataza mja anaposwali? (92: 10). Misingi (usul) ya Uislamu iliyothibitishwa ni kuwa kila lililoelezwa na dhahiri ya wahyi na lisipingane na akili, basi ni lazima kuliamini.

Kama Israi ingelikuwa ni kwa roho tu, kusingelikuwa na mshangao wowote, wala washirikina wasingeliharakisha kumfanya mwongo Muhammad. Kuna Hadith isemayo kuwa Ummu Hani alimwambia Mtume mtukufu(s.a.w.w) : “Usiwaambie watu wako hilo, nahofia watakufanya muongo,” lakini hakutilia maanani hofu ya Ummu Hani kwa kuona kuwa maadamu ni haki basi haina neno. Kwa hiyo akawatangazia watu wake aliyoyaona. Wakashangaa na wakampinga. Kama ingelikuwa ni kwa usingizi wasingelikuwa na mshangao huu.

2. Kwenda Israi kimwili na kiroho ni nembo ya kuwa kila mtu ni lazima ayafanyie kazi maisha yake ya kimwili na kiroho, sio upande mmoja tu.

3. Ni mashuhuri kuwa Mtume amesema:“Nilipelekwa usiku kwenye mnyama anayeitwa Buraq.” Ni wazi kwamba Israi ya kiroho peke yake haihitajii kupanda mnyama wala chombo chochote.

Kwa mnasaba wa Buraq tutaashiria makala iliyo kwenye gazeti la Al-Jumhuriya la Misr, iliyoandikwa na Muhammad Fathi Ahmad, yenye kichwa cha maneno ‘Madhumuni ya kisayansi ya Israi na Miraji,’ Ninamnukuu:

Alipanda Mtume mtukufu mnyama anayeitwa Buraq. Kulingana na Hadith ni mnyama anayemzidi punda kwa kimo na yuko chini kidogo ya baghala. Hapo kuna somo kutoka kwa Mwenyezi Mungu tunapaswa tulitafutie maelezo Mwenyezi Mungu hashindwi kumchukua Mtume wake kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas bila ya nyenzo yoyote ambapo Mtume angeweza kujikuta tu yuko kwenye mlango wa Masjidul-aqswa. Lakini Mwenyezi ambaye imetukuka hekima yake alipitisha kuwa kila kitu kiende kwa kanuni yake, bila ya mabadiliko wala mageuko.

Safari hii iliyokata masafa marefu katika kasi ya kushangaza, inahimiza akili ianzishe nyenzo mpya ya kwenda masafa marefu katika muda mdogo. Kisha tujiulize, ni kitu gani katika ulimwengu kinakwenda kasi zaidi kulin- gana na utafiti wa elimu? Bila shaka jibu litakuja bila ya kusita kuwa ni mwangaza ambao unakwenda kwa kasi ya 300,000 km. kwa sekunde moja.

Buraq aliyemtumia Mtume alitembea kwa kasi ya mwanga kwa sababu neno Buraq ni mnyambuliko wa neno Barq lenye maana ya mwako kama wa umeme (flush).

Kupitia majaribio ya kiakili katika uchunguzi wa anga za juu, binadamu ameweza kugundua siri nyingi na ameweza kwa nguvu ya elimu kupenya kutoka ardhini hadi kwenye ufalme wa mbingu. Lakini elimu ya maada pekee inamsahaulisha binadamu na muumba wake.

Tukio la Israi na Miraji linatupa somo kwamba maada na roho ziko sambamba. Kwa hiyo kwenda kwake kwenye utukufu wa juu kulikuwa ni kwa umbile la kibinadamu kutokana na maada na kuendeshwa kulikotokana na roho ya Muumba Mtukufu, Jibril akawa anachukua nafasi ya muelekezaji njia. Nasi hatuna kizuizi cha kumfanya ni nembo, kwa madaraka ya elimu, ambayo itatuongoza kwenye safari yetu katika maisha haya kuelekea kwa muumba wa ulimwengu”.

Ya kushangaza niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kauli ya anayesema kuwa Israi ya Mtume(s.a.w.w) ilikuwa kwa roho sio kwa mwili wake mtukufu kwa kutoa dalili ya hadith iliyopokewa kutoka kwa Aisha, kwamba mwili wa Mtume haukumwacha usiku ule. Na inajulikana kuwa wakati wa Israi, Aisha alikuwa mdogo, wala hakuwa ameolewa na Mtume(s.a.w.w) ; Kwa hiyo Hadithi hiyo inajipinga yenyewe.

MASJIDUL-HARAM NA MASJIDUL-AQSWA

Masjidul-Aqswa unafanana na Masjidul-Haram katika mambo haya yafutayo:-

1. Yote iko upande wa mashariki.

2. Historia ya yote ni ya zamani; isipokuwa Masjidul-haram ni wa zamani zaidi na pia ni mtukufu zaidi. Kwa sababu ndiyo nyumba ya kwanza kujengwa kwa ajili ya ibada duniani: “Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ni ile iliyoko Makka yenye kubarikiwa na mwongozo kwa viumbe. Mna humo ishara zilizo wazi: Mahali aliposimama Ibrahim. Na mwenye kuingia humo huwa katika amani; na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea. Juz; 4 (3:96–97).

3. Miji yote miwili, Makka ulio na Masjidul-haram na mji wa Quds ulio na Msjidul–Aqswa ilianzishwa na Waarabu au walishiriki kuianzisha. Makka ilijengwa na Ibrahim na mwanawe Ismail waliojenga Al-ka’aba: “Na tuliagana na Ibrahim na Ismail kuwa: Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga huko kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu… Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile Nyumba (Al-Kaaba) na Ismail (wakaomba): Ewe mola wetu! Tutakabalie; hakika wewe ndiye Msikizi, Mjuzi, Juz; 1(2:125,127).

Inajulikana kuwa Ismail ndiye Mtume wa kwanza kuzungumza lugha ya Kiarabu ambayo haikuwa lugha ya baba yake. Maquraysh na waarabu wengineo wanatokana naye. Qur’an ilishuka kwa lugha yake.

Quds nayo waliishi hapo wayabusi, kabila la waarabu wa Kanani. Walifika kwenye mlima maarufu unaojulikana kwa jina la Zayuni, mnamo mwaka wa 2500 (B.C.) kabla ya kuzaliwa Nabii Isa wakiongozwa na mzee wao aliyeitwa Salim Al-yabusi. Watu wa kabila hili ndio wa kwanza kuweka jiwe la kwanza la kujenga mji wa Quds ambao baadae ulikuwa ndio Qibla cha ulimwengu.[2]

Baada ya Waislamu kuuteka mji wa Quds walijenga msikiti ulioitwa Masjid Umar, uliasisiwa na Umar bin A-khattwab na Masjid Qubbatusswakhra (msikiti wa kuba la mwamba) ulioasisiwa na Abdulmalik bin Marwana, Yote hiyo ilikuwa ndani ya haramu ya Quds, Waislamu walikuwa hawaruhusu asiyekuwa Mwislamu kukanyaga hapo.

4. Waislamu wanaitukuza misikiti yote miwili, ambapo mwanzo walikuwa wakiswali kwa kuelekea Masjiul-Aqswa kwa muda wa miaka 13 wakiwa Makka na miezi kadhaa Madina. Kuongezea safari ya Israi, inakuwa si jambo la ajabu kwa Waislamu kupafanya mahali hapo ni pa takatifu na ni pa pili baada ya Makka na Madina kwa utukufu, heshima na ulinzi.

Mpokezi mengi yanaeleza kuwa Mtume alimfunga Buraq hapo Baytul-Muqaddas, Mpaka sasa ukuta wa magharibi ya haram, mahali alipomfunga, unaitwa ukuta wa Buraq, pia mapokezi yanaeleza kuwa Mtume aliswali kwenye sehemu ya mwinuko katika hekalu la Nabii Suleiman, pamoja na Nabii Ibrahim, Musa na Isa akiwa yeye ndiye Imam. Na kwamba yeye alitumia mwamba wa Ya’qub kuwa ndio kituo chake cha kupanda mbinguni.

Ndio maana uharibifu wa Quds mnamo mwaka 1967 uliyotekelezwa na wazayuni na wakoloni wa kimarekani na waingereza, ni maafa ya waislamu na wakiristo.

Mkono mchafu ulichafua na kudharau sehemu takatifu za dini ya kiislamu na ya kikiristo. Usiku huo wa damu walikesha na ufuska; wakafanya sherehe za dansi na ulevi.

Ajabu ya maajabu ni kwa Marekani na Uingereza kudai kuwa wao ni wahami wa dini na ni maadui wa ulahidi, wakati huo huo wakiwasaidia wazayuni amabo hawaamini misimamo yoyote, hawaheshimu maadili, hawaheshimu dini za wengine wala hawatambui haki yoyote katika haki za binadamu.

Amerika na Uingerza zimeisaidia Israili, zikaipa mali na silaha na zikaiunga mkono kweneye Baraza la usalama na Umoja wa mataifa. Zikaipongeza kwa kuingila sehemu takatifu za waislamu na wakiristo. Wameendelea na misimamo hii ulimwenguni pote.

Sisi hatuna shaka kwamba iko siku itawafikia wakoloni na marafiki zao wazayuni kupitia mikononi mwa wanamapinduzi wapigania uhuru; kama ilivyowafikia hivi sasa wamarekani kutoka kwa wavietnam na kabla yake iliwafikia wazayuni kutoka kwa Nebuchadnezzar, Waroma, Mtume(s.a.w.w) na Khalifa wa pili Umar bin Al-khattwab.

Hivi sasa kila siku vyombo vya habari haviachi kutangaza habari za upinzani wa Palestina na kujitoa mhanga ambako kumeifanya Israil yote iishi kwenye jinamizi la hofu na woga[3] .

SOMO KATIKA ISRAI

Qur’an hii ambayo tunaisoma ni masomo aliyompatia Muumbaji Mtume wake ili ayafikishe kwa watu wote, Masomo haya yako aina nyingi. Miongoni mwayo ni hukumu ya maarifa ya halali na haramu, jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, ikhlasi na subira kwa ajili ya haki.

Lililo muhimu zaidi katika yote ni kumwamini Mwenyezi Mungu na utukufu wake kwa imani sahihi inayobainishwa na maarifa ya kujua; sio kwa kuigiza, kasema fulani au kwa kuwazia tu.

Mwenyezi Mungu ameongoza njia za elimu na yakini ambazo ni kufikiri katika maumbile ya ulimwengu pamoja na ardhi na mbingu yake. Pia mipangilio, hekima na mfumo sahihi katika vyote vilivyo baina ya mbingu na ardhi, vikiwa mbalimbali na pamoja:

أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِم مَّا خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُّسَمًّى ﴿٨﴾

Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi ila kwa haki na kwa muda maalum. (30:8).

Baada ya Mwenyezi Mungu kumpa wahyi mja wake kwa somo la ukuu wa ulimwengu na kuumba mbingu na ardhi, alimuhusisha yeye tu kwa safari ya ardhini, kutoka Masjidul-haram hadi Masjidul-aqswa na safari ya mbinguni, kutoka Masjidul-aqswa hadi kwenye wingu wa juu.

Lengo la safari hizi mbili ni kuwa Mtume apate somo la kimatendo baada ya kupata la kinadharia kuhusu ulimwengu, aone mwenyewe, kwa macho yake, maajabu ambayo akili haiwezi kuyawazia. Njia hii, siku hizi, watu wanaifuata, ambapo waalimu wanawaandalia wanafunzi wao safari za kimasomo ili wakajionee wenyewe yale waliyojifunza.

Kwa hiyo basi somo kubwa katika safari mbili za Mtume ni kuhimiza akili kuangalia vizuri katika uumbaji wa mbingu na ardhi:

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ ﴿١٨٥﴾

Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu, Juz. 9 (7:185).

Imam Ali(a.s) anasema:“Nashangaa na anyemtilia shaka Mungu na anaona alivyoviumba Mungu!”

وَآتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ أَلَّا تَتَّخِذُوا مِن دُونِي وَكِيلًا ﴿٢﴾

2. Na tukampa Musa Kitabu na tukakifanya ni uongofu kwa Wana wa Israil, kwamba msi- fanye mtegemewa asiyekuwa Mimi.

ذُرِّيَّةَ مَنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ إِنَّهُ كَانَ عَبْدًا شَكُورًا ﴿٣﴾

3. Enyi kizazi tulichokichukua pamoja na Nuh! Hakika yeye alikuwa ni mja mwenye shukrani.

NA TUKAMPA MUSA KITABU

Aya 2-3

MAANA

Na tukampa Musa Kitabu na tukakifanya ni uongofu kwa Wana wa Israil, kwamba msimfanye mtegemewa asiyekuwa Mimi.

Makusudio ya kitabu hapa ni Tawrat na Israil ni Ya’qub bin Is-haq bin Ibrahim(a.s) . Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameitermsha Tawrat kwa Musa ili Wana wa Israil waongoke nayo kwenye njia ya haki na ukweli na wamtegemee Mungu peke yake wala wasimfanye mwengine kuwa ni msimamizi au msaidizi wao.

Lakini wao waliyapotosha maneno ya Mwenyezi Mungu, wakaabudu ndama, wakaua mitume, na wakaijaza dunia shari na ufisadi kwa kila nyenzo waliyo nayo.

Enyi kizazi tulichokichukua pamoja na Nuh!

Nuh alichukuwa watoto wake watatu pamoja na wake zao katika Safina. Wao walikuwa ni Ham, Sam, na Yafith. (Hamu Shemu na Yafeti). Kutokana na wao kizazi kiliendelea baada ya tufani; miongoni mwa hicho kizazi ni Wana wa Israil waliokuwa katika zama za Nabii Musa. Hapa ni kuwakumbusha Wana wa Israil neema za Mwenyezi Mungu ambazo wao wanazikufuru na kuzikana.

Hakika yeye alikuwa ni mja mwenye shukrani.

Yeye ni Nuh(a.s) ; yaani enyi mayahudi! Kuweni na shukrani na kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu; kama alivyokuwa Nuh, lakini hashukuru neema ila mkweli aliye mwaminifu. Na haikujulikana kwa waisraili, tangu walipopatikana, isipokuwa uongo udanganyifu na hiyana.

Imepokewa Hadith kutoka kwa Imam Ja’far Asswadiq(a.s) kwamba: Nuh(a.s) anapopambaukiwa alikuwa akisema hivi:“Ewe mola wangu! Hakika ninashuhudia kwamba neema ya dini au dunia iliyonipambaukia inatokana na wewe; huna mshirika; wakusifiwa na kushukuriwa kwa neema hizo kwangu ni wewe mpaka uridhie.”

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَقَضَيْنَا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ فِي الْكِتَابِ لَتُفْسِدُنَّ فِي الْأَرْضِ مَرَّتَيْنِ وَلَتَعْلُنَّ عُلُوًّا كَبِيرًا ﴿٤﴾

4. Na tukawaambiwa wana wa Israili katika kitabu, hakika mtafanya ufisadi katika ardhi mara mbili, Na hakika mtajitia uluwa, uluwa mkubwa.

فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ أُولَاهُمَا بَعَثْنَا عَلَيْكُمْ عِبَادًا لَّنَا أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ فَجَاسُوا خِلَالَ الدِّيَارِ وَكَانَ وَعْدًا مَّفْعُولًا ﴿٥﴾

5. Basi itakapofika ahadi ya kwanza yake, tutawapelekea waja wetu wenye nguvu wakali na wakawasaka majumbani. Na ilikuwa ni ahadi iliyotimizwa.

ثُمَّ رَدَدْنَا لَكُمُ الْكَرَّةَ عَلَيْهِمْ وَأَمْدَدْنَاكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَجَعَلْنَاكُمْ أَكْثَرَ نَفِيرًا ﴿٦﴾

6. Kisha tukawarudishia nguvu dhidi yao na tukawasaidia kwa mali na watoto na tukawajaalia mkawa watu wengi zaidi.

إِنْ أَحْسَنتُمْ أَحْسَنتُمْ لِأَنفُسِكُمْ وَإِنْ أَسَأْتُمْ فَلَهَا فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ لِيَسُوءُوا وُجُوهَكُمْ وَلِيَدْخُلُوا الْمَسْجِدَ كَمَا دَخَلُوهُ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَلِيُتَبِّرُوا مَا عَلَوْا تَتْبِيرًا ﴿٧﴾

7. Mkifanya uzuri mnajifanyia wenyewe na mkifanya ubaya mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho, ili waziharibu nyuso zenu. Na waingie msikiti kama walivyoingia mara ya kwanza na waharibu kila walichokiteka kwa uharibifu mkubwa.

عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يَرْحَمَكُمْ وَإِنْ عُدتُّمْ عُدْنَا وَجَعَلْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ حَصِيرًا ﴿٨﴾

8. Huenda Mola wenu akawarehemu, Na mkirudia, na sisi tutarudia. Na tukaifanya jahannam ni gereza kwa ajili ya makafiri.

WAISRAILI NA UFISADI MARA MBILI

Aya 4 – 8

LUGHA

Neno Qadha lina maana nyingi; miongoni mwazo ni kuhukumu. Maana nyingine ni kuumba; kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu aliposema: “Na akaziumba mbingu saba kwa siku mbili” (41:12). Maana nyingine ni kupitisha jambo; kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu katika Sura hii tuliyo nayo Aya 23, aliposema: “Na Mola wako amepitisha kuwa msimwabudu yoyote ila Yeye tu na kuwatendea wema wazazi wawili.” Pia lina maana ya kutoa habari kama lilivyotumika katika Aya hii tuliyo nayo.

MAANA

Maana ya kijumla ya Aya hizi ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwapa habari wana wa Israil kwamba wao watafanya ufisadi katika ardhi kisha Mungu atawaletea watakaowadhalilisha kwa kuuliwa kutekwa na kuporwa. Baadae Mungu atawarudishia nguvu zao, lakini watarudia ufisadi mara ya pili na Mungu atawaletea tena watakaowapa pigo mara ya pili.

Ufafanuzi wa hayo ni kama ifuatavyo:

1.Na tukawaambiwa wana wa Israili katika kitabu.

Makusudio ya neno Qadhayna hapa ni kutoa habari na kuweka wazi, sio kupitisha, kwa sababu Mwenyezi Mungu hapitishi ufisadi: “Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi machafu.” Juz,8 (7:28).

Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat iliyoteremshwa kwa Nabii Musa(a.s) kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya iliyopita: “Na tukampa Musa Kitabu.” Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwapa habari Waisraili kuwa watakaowafuatia watafanya ufisadi katika nchi mara mbili.

2.Hakika mtafanya ufisadi katika ardhi mara mbili.

Makusudio ya ufisadi hapa sio ufisadi kwa maana yake ya kiujumla ambayo yanachanganya ukafiri, uongo, kula riba, kupanga njama n.k; kwani hayo yote ndio dini yao na mazowea yao wakati wowote na katika kila kizazi chao, ambapo Mwenyezi Mungu alikwisha wasimulia pale aliposema: “Walisema Mayahudi: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba.

Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa waliyoyasema… Kila mara wanapowasha moto wa vita Mwenyezi Mungu huuzima, Na wanajitahidi kuleta ufisadi katika ardhi, Na Mwenyezi Mungu hawapendi wafisadi, Juz; 6 (5: 64).

Makusudio hasa ya ufisadi hapa ni kwa maana maalum ambayo ni kutawala na kwamba utawala wao wenyewe utakuwa ni ufisadi, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwaambia Wana wa Israil:

3.Na hakika mtajitia uluwa, uluwa mkubwa.

Qur’an inalitumia neno uluwa kwa maana ya kupetuka mipaka na ufisadi. Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّ فِرْعَوْنَ عَلَا فِي الْأَرْضِ ﴿٤﴾

“Hakika Fira’un alijitia uluwa katika ardhi,” (28:4).

Amesema tena:

تِلْكَ الدَّارُ الْآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لَا يُرِيدُونَ عُلُوًّا فِي الْأَرْضِ وَلَا فَسَادًا وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٨٣﴾

“Hiyo nyumba ya Akhera tumewafanyia wale wasiotaka kujitia uluwa katika ardhi wala ufisadi na mwisho ni wa wenye takua.” (28:83).

Maana ni kuwa nyinyi Wana wa Israil, mtatawala mara mbili na utawala wenu mtaufanya ni nyenzo ya ufisadi mkubwa na wa hatari ambao hauna mfano wake; mtachafua sehemu takatifu, mtavunja miko ya Mwenyezi Mungu na mtadharau misimamo mizuri, maadili na kila haki ya Mungu na ya watu.

Qur’an haikueleza mahali wala wakati wa ufisadi wao huo mara mbili, lakini wanahistoria na jamaa katika wafasiri wamesema kuwa Wana wa Israil waliivamia Palestina baada ya kuhangaika, kwa uongozi wa Yusha bi Nun, (Yoshua) khalifa wa Musa bin Imran, wakaikalia kwa mabavu na wakapora mali yote baada ya kuwafyeka wenyeji wa hapo wengi ambao walikuwa ni Wakan’ani (wakanani) na waliobakia wakawafanya watumwa. Sera yao kwa Yusha ilikuwa kama ilivyokuwa kwa Musa – uasi na inadi. Hiyo ndiyo iliyokuwa mara yao ya kwanza, kama wanavyosema wafasiri na wanahistoria.

Ama mara ya pili, kuna wanaosema kuwa bado haijatokea na kwamba itatokea baadae kwa Waarabu na Waislamu katika Palestina. Wengine wanasema kuwa imekwishatokea na kuisha, Kauli hii ndiyo yenye nguvu. Kwa hali yoyote ni kwamba Qur’an inaeleza waziwazi kuwa Wana wa Israil wakitawala hufanya ufisadi katika ardhi na kupanda kiburi kikubwa.

Kwa hiyo si uzushi kwa dola ya kizayuni kupasua matumbo ya wanawake wa kipalestina wenye mimba, kuwazika wazima vijana, kuwamiminia risasi wafungwa, kuwapiga mabomu ya sumu walio majumbani, kuvunja majumba ya wenyeji na kuwaziba midomo kwa mali na kwa vikwazo. Kisha inajitia kulia kuwa eti inachokozwa na kudhulumiwa.

Tunasema hivi tukijua kuwa Qur’an haikukiashiria kikundi hiki ambacho kimejiuza kwa kila mwenye kuongoza shari, lakini imekuja ishara yake kwa sababu kina jina la Israil na kunasibika kwenye kizazi kilichogeuzwa manyani na nguruwe.

Basi itakapofika ahadi ya kwanza yake.

Yaani ya kwanza katika hizo mara mbili za kufanya ufisadi, Ahadi hapa ni kwa maana ya wakati walioahidiwa Wana wa Israil kufanya ufisadi.

Tutawapelekea waja wetu wenye nguvu wakali.

Wanaambiwa Wana wa Israil. Waja sio lazima wawe wema, kama wanavyodai wengine, wanaweza pia kuwa waovu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

يَا حَسْرَةً عَلَى الْعِبَادِ مَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٣٠﴾

Ni sikitiko kwa waja, hakuwafikia Mtume yeyote ila walikuwa wakimfanyia stihzai, (36:30).

Wenye nguvu na wakali, ni ukali wa vita. Hao walikuwa ni wababilon wakiongozwa na Nebuchadnezzar au baba yake Nabopolassar ambao waliwaua mayahudi, wakachoma Tawrat na wakawachukua mateka watu wengi, wake kwa waume na watoto, Hayo yalikuwa mnamo mwaka 586 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (586 B.C.). Imesemekana kuwa ni mwaka 596.

Na wakawasaka majumbani.

Neno kuwasaka hapa tumelifasiri kutoka neno la Kiarabu Jasu ambalo maana yake hasa ni kutafuta sana na kurudiarudia. Qur’an haikulitumia neno hili isipokuwa hapa tu.

Maana ni kuwa hao jamaa walikuwa waki- watafuta Mayahudi majumbani mwao na wakirudi tena kuwatafuta ili wawaue.

Na ilikuwa ni ahadi iliyotimizwa bila ya kuhalifu au kuachwa Muhtasari wa Aya hizi ni kuwa Wana wa Israil walipofanya ufisadi mara ya kwanza Mwenyezi Mungu aliwapelekea watu wenye nguvu waliowaua, wakuwafurusha wanaume na kuchukua wanawake, wakapora mali zao na kuharibu majumba yao. Ufisadi huo wa kwanza na pigo lake ulikuwa kabla ya Uislamu.

Kisha tukawarudishia nguvu dhidi yao na tukawasaidia kwa mali na watoto na tukawajaalia mkawa watu wengi zaidi.

Waliorudishiwa nguvu ni Wana wa Israil dhidi ya Wababiloni; yaani Wana wa Israil walijikomboa kwa Wababilon. Inajulikana kuwa Wana wa Israil hawakupigana na Wababiloni katika miji yao wala hawakuwahi kuwashinda.

Lakini mnamo mwaka 538 Bc, mfalme wa Fursi (Iran ya sasa) aliishinda miji ya Wababiloni na akawakomboa mateka wa Kiisrail waliokuwa humo. Kwa hiyo nguvu za Wana wa Israil dhidi ya Wababiloni ni kupitia mfalme wa Fursi.

Abu Hayan Al-andalusi anasema katika Tafsir yake Albahrul-Muhit: “Mfalme alipigana vita na Wababilon. Nebuchadnezzar alikuwa ameua wana wa Israil elfu arubaini, waliobaki wakawa ndani ya Babilon wakidhalilishwa. Basi mfalme alipopigana nao na akawashinda alioa mwanamke wa Kiisrail. Huyo mke akamtaka mumewe awarudishe watu wake Baytul–Muqaddas, naye akafanya hivyo.”[4]

Waliporejea wana wa Israil Palestina, Mwenyezi Mungu aliwasaidia kwa mali na watoto na akaifanya idadi yao zaidi ya ilivyokuwa mwanzo. Lakini mara tu iliporudi nguvu yao, walirudia uovu na kupotoka na dini kuliko mwanzo. Wakamuua Zakariya na wakaazimia kumuua Bwana Masih(a.s) .

Mkifanya uzuri mnajifanyia wenyewe, na mkifanya ubaya mnajifanyia wenyewe.

Katika maana haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

ل هَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ﴿٢٨٦﴾

“Faida ya yale iliyoyachuma ni yake na hasara iliyochuma ni yake.” Juz, 3 (2:286)

مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ﴿٤٦﴾

“Mwenye kutenda wema basi ni kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe na mwenye kutenda uovu basi ni juu yake” (41:46).

Na ikifika ahadi ya mwisho.

Baada ya kupita ufisadi wa kwanza wa wana wa Israil na ikapita misukuosuko yake, ulikuja ufisadi wa pili na misuko suko ya pili nayo ikachukua nafasi yake, basi Mwenyezi Mungu aliwapelekea watuili waziharibu nyuso zenu.

Hapo wanaambiwa wana wa Israil. Kuharibika nyuso ni fumbo la misukosuko na kudhalilika kwao. Kwa sababu uso unadhihirisha furaha au huzuni iliyo moyoni. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

سِيئَتْ وُجُوهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ﴿٢٧﴾

“Nyuso za waliokufuru zitaharibika” (67:27).

Na waingie msikiti kama walivyoingia mara ya kwanza na waharibu kila walichokiteka kwa uharibifu mkubwa.

Makusudio ya msikiti hapa ni mji wa Quds, kwa sababu ndani yake mna hekalu la Nabii Suleiman. Limeitwa msikiti (masjid) kwa vile ni mahali pa kusujudu.

Maana ni kuwa wana wa Israil walipofanya ufisadi mara ya pili, Mwenyezi Mungu aliwapelekea watu waliowapa adhabu mbaya na hali yao ikawa kama ya kwanza – kuuliwa, kufukuzwa na kuharibiwa majumba.

Mara zote mbili za ufisadi na kuadhibiwa zilikwishapita kabla ya Uislamu.

Katika Majmau-bayan imeelezwa kuwa aliyewashambulia wana wa Israil mara ya kwanza ni Nebuchadnezzar na aliyewashambulia mara ya pil ni mfalme wa Roma, akaharibu Baytul-Muqaddas na akawateka wenyeji wake.

Haya yanaafikiana na aliyoyanukuu Al-Maraghi kutoka Tawarikhl-Yahud, akasema kuwa muda baina ya mashambulizi mawili ulikuwa miaka mia tano.

Huenda Mola wenu akawarehemu.

Kwa sharti la kutubia na kuwa na huruma. Kwa sababu asiyekuwa na huruma hahurumiwi; kama ilivyoelezwa katika Hadith tukufu.

Na mkirudia ufisadi kujitia uluwa na kiburi,na sisi tutarudia kuwaadhibu na kuwadhalilisha.

Walirudia na wakafanya ufisadi; wakataka kumuua Masih(a.s) na wakamkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu akawapelekea Waislamu, wakawaua Bani Quraydha, wakawatawala Bani Nadhir, wakaichukua Khaybar na wakafukuzwa Mayahudi Bara Arabu.

Na tukaifanya Jahannam ni gereza kwa ajili ya makafiri.

Wengine wamefasiri neno hasir kwa maana ya busati. Yaani tumeifanya Jahannam ni busati.

Vyovyote iwavyo, makusudio yake hapa ni kuwa Jahannam itawazunguka wala hakuna matarajio ya kuepukana nayo; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

أُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَلَا يَجِدُونَ عَنْهَا مَحِيصًا ﴿١٢١﴾

“Hao makazi yao ni moto wa Jahannam wala hawatapata pa kuukimbia” Juz. 5 (4:121).

KUELEZEA MWENYEZI MUNGU NA DOLA YA ISRAIL

Mnamo mwezi Januari mwaka hu 1969, kulitokea mjadala motomoto kwenye magazeti ya Misr kuhusu Aya inayoeleza ufisadi wa wana wa Israil. Walishiriki kwenye mjadala huu wataalamu wengi wenye ghera ya haki, Uliendelea mjadala na malumbano kwa muda kiasi, Gazeti liliuchapisha kwenye matoleo mane ya kila Ijumaa ya mwezi huo tulioutaja.

Washiriki waligawanyika makundi mawili:

Kundi la kwanza linasema kuwa pigo la kwanza la wana wa Israil lilitokea kutoka kwa Umar bin Al-khttab alipoishinda Quds. Yeye na waislamu wakasaka nyumba za wapalestina. Na ufisadi wa pili wakasema kuwa ni Walivyofanya wazayuni mnamo mwaka 1967 na wanavyoendelea kufanya leo.

Kundi hili limefasiri kuwa pigo la pili la Mayahudi litatoka kwa warabu ambao watashinda hivi karibuni na warudishe ardhi zao zilizoporwa na na wakoloni hao.

Na wakasema kuwa hiyo ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na waingie msikiti kama walivyoingia mara ya kwan- za.” Yaani waarabu wataukomboa Msikiti wa Aqswa kutoka kwa Waisrail kama walivyoukomboa kwanza.

Hakuna rejea ya tafsir hii isipokuwa matamanio na utabiri ambao ni wajibu kuuepusha na Qur’an. Kwa sababu hiyo ni Kitabu na nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayofichua kawaida na desturi ya maumbile ambayo hayageuki wala kubadilika na inaangalia kila kilichomo ulimwenguni, kuanzia chembechembe hadi vitu vikubwa; wakati huo Qur’an inambebesha kila mtu majukumu ya kufanya mambo kwa juhudi na kuchukuliwa hisabu yake mbele ya Mwenyezi Mungu, ya dhamira na ya watu wote. Kundi la pili linasema mara zote mbili za ufisadi pamoja na mapigo yake yamekwisha pita kabla ya Uislamu.

• Pigo la kwanza lilitangulia Uislamu kwa kiasi cha miaka elfu moja na lilitekelezwa na Nebuchadnezzer au baba yake, ambaye aliiharibu Quds, kuchoma Hekalu, kuua wayahudi wengi na waliobaki wakawateka nyara hadi Babiloni.

• Pigo la pili, linasema kundi hili, kuwa lilitokea mnamo mwaka wa 70.

Baada ya kuzaliwa Nabii Isa (70A.D.) lilitekelezwa na Titus (Tito) wa Roma ambaye aliuzingira mji wao na akauponda ukuta wake, akaingilia kuharibu majumba kubomoa hekalu na kuua kiasi cha watu milioni moja mbali na waliochukuliwa watumwa na kuuzwa sokoni; kama anavyosema Flavius ambaye aliishuhudia tukio lenyewe, Waliobaki wakasambaa ulimwenguni[5] .

Vilevile, kundi hili la pili, limesema kuwa Qur’an haishirii kwa mbali wala karibu kuhusu kikundi kilichoko katika ardhi ya Palestina kinachojiita Israil. Kwani hicho si kikundi cha kidini wala chama cha kisiasa au serikali ya kiuhakika; isipokuwa ni adui mpya wa waarabu na Waislam, nacho ni ukoloni wa kizayuni au uzayuni wa kikoloni ambacho kimevaa nguo ya Daud kikiwa kimechukua ramani ya ulafi iliyosajiliwa kwenye Tawrat ya kupangwa iliyopotolewa ‘kuanzia Nail hadi Furat’ na kunyakua mali ya taifa chini ya nembo ya uyahudi. Lengo la kwanza na lamwisho ni kuleta ukoloni mamboleo kwa waarabu na waislamu kikiongozwa na Marekani.

Kwa ufupi ni kuwa Qur’an haikuashiria kabisa Israil ya sasa na kwamba Aya zinazozungumzia Wana wa Israil zimewakusudia koo kumi na mbili katika kizazi cha Ya’qub bin Is-haq bin Ibrahim ambao walikuwa katika zama za Nabii Musa na Harun. Na hawa ambao wamenyakua ardhi yetu kwa silaha za ukoloni na mali ya kizayuni si katika kizazi cha Israil bin Is-haq wala hawako kwenye dini yake wala dini ya Musa; isipokuwa wao ni viumbe wapya wa kushangaza wasiokuwa na mfano.

Kwa sababu wamepatikana kutokana na vizazi mbali visivyokuwa na mfungamano baina yao wala kujumuika kwa mkusanyiko wa kiinchi au lugha wala hawana msingi wowote isipokuwa msingi wa kibaraka wa nguvu ya shari.

Zaidi ya hayo ni kwamba tukitafsiri kuwa Mwenyezi Mungu amek- wishaeleza kuwa tutauingia msikiti, tutabweteteka tu na kuzitupilia mbali sababu za ushindi za kawaida alizozibainisha Mwenyezi Mungu katika Kitabu chake na kupitia kwa Mtume wake.

Ambapo mara anatuhimiza jihadi na mara nyingine anatuhiza kusaidiana, huku tukiwaandaa wengine, kutokata tamaa kuwa na subira na mara ningine kung’ang’ania jambo, kujitolea mali na kulifanya rahisi kila lililo ghali kwa ajili ya dini na uzal- endo; sawa na alivyofanya Muhammad, swahaba wa Muhammad(s.a.w.w) na waliowafuatilia wao kwa wema na kama vile wanavyofanya wanaoji- tolea mhanga hivi sasa.

Baada ya yote hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu hapigani wala hatapigana na Israil na ukoloni wa kizayuni kwa niaba yetu; hata kama tukiswali na kumtarajia Yeye tu. Kwa sababu ibada bora zadi kwake ni kujitolea mhanga kwa nyenzo na nguvu zote dhidi ya dhulma, ukandamizaji, ufisadi na uchokozi.

Nasi tunamiliki uwezo wa kutosha wa kumtoa adui kwenye ardhi yetu. Tunamiliki uwezo huo kwa idadi yetu, dini yetu, turathi zetu na mali zetu. Lililobaki ni kuzitumia tu na hapana budi, lazima tuzitumie. Kwa sababu kupenda kubakia kunalazimisha hilo. Ukoloni na uzayuni umetuweka kwenye mambo mawili hakuna la tatu: Ama kufa au kuishi, Hakuna anayependa kufa kuliko kuishi au kuwa mtumwa kuliko kuwa huru au udhalili kuliko heshima.