3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ وَيُبَشِّرُ الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا كَبِيرًا ﴿٩﴾
9. Hakika hii Qur’an inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa na inawabashiria waumini ambao wanatenda mema kwamba watapata malipo makubwa.
وَأَنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٠﴾
10. Na kwamba wale wasioamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu.
وَيَدْعُ الْإِنسَانُ بِالشَّرِّ دُعَاءَهُ بِالْخَيْرِ وَكَانَ الْإِنسَانُ عَجُولًا ﴿١١﴾
11. Na mtu huomba shari kama vile aombavyo kheri. Na mtu amekuwa ni mwenye pupa.
وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِّتَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ وَلِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ وَكُلَّ شَيْءٍ فَصَّلْنَاهُ تَفْصِيلًا ﴿١٢﴾
12. Na tumeufanya usiku na mchana kuwa ni ishara mbili, Tena tukaifuta ishara ya usiku. Na tukaifanya ishara ya mchana ni ya kuangazia ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu, Na kila kitu tumekifafanua wazi wazi.
QUR’ANI INAONGOZA KWENYE YALIYONYOOKA
Aya 9 -12
MAANA
Hakik hii Qur’an inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa na inawabashiria waumini ambao wanatenda mema kwamba watapata malipo makubwa.
Yaliyonyooka kabisa ni mila au njia ambayo imenyooka. Neno hili lina maana ya kuenea masilahi zaidi kwenye kila kitu, wakati wowote, mahali popote na kwa mtu yeyote.
Aya hii ni madai yaliowazi yaliyosajiliwa na Qur’an anayoyaamini kila Mwislamu - kwamba Uislamu ndio dini bora zaidi ya dini zote. Dalili ya usahihi wa madai haya na ukweli wake ni Qur’an kutokana na itikadi yake, sharia yake na mafunzo yake mengine kuongezea sera ya mwenye ujumbe huo, Muhammad Bin Abdillah(s.a.w.w)
ambaye ameijaza ardhi elimu, imani, wema na uadilifu baada ya kuwa na ujahili, kufuru na ufisadi.
Maulama wamethibitisha hakika hii na wakatunga mamia ya vitabu katika kufasiri maneno ya Mwenyezi Mungu na hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu na sera yake, itikadi sharia na maadili ya kiislamu ambayo yamethibitika katika nyanja mbalimbali, Tumetaja baadhi katika juzuu zilizotangulia za tafsiri hii. Tutaonyesha baadhi ya mifano ya misingi hiyo kama ifuatavyo:
1. Uislamu Ni Dini Ya Maumbile
Kila msingi katika misingi ya Uislamu, kila tawi katika sharia yake na kila hukumu katika hukumu zake, imejikita kwenye umbile safi: “Ndilo umbile alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu, Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.”
Aya inaonyesha wazi kwamba Uislamu unaitikia matakwa ya maumbile ya binadamu na kunyoosha mikono yake kwa kila jipya lenye faida; ni sawa liwe limekuja kutoka mashariki au magharibi. Amesema Imam Ali
: “Hekima ni adimu kwa Mumin. Chukua hekima hata kama ni kutoka kwa wanafiki.” Akasema tena: “Angalia kauli usiangalie aliyesema” Kuna hadith nyingi zenye maana haya.
2. Imani Ya Uislamu Kwenye Elimu
Uislamu unaamini elimu na kusimamia kwake maisha katika pande zote. Mwenyezi Mungu anasema katika sura hii tuliyo nayo Aya 36: “Wala usifuatilie ambalo huna ujuzi nalo.” Amesema tena:
قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١١١﴾
Sema: Leteni dalili zenu kama nyinyi ni wasema kweli.” Juz.1 (2:111)
فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٤٣﴾
“Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui” Juz,14(16:43).
Mtume(s.a.w.w)
amesema: “Wino wa mulama utapimwa na damu ya mashahidi siku ya kiyama.” Imam Ali naye amesema: “Elimu ni dini, inafuatwa dini kwayo.”
Maana ya kuamini elimu ni kuamini maendeleo na kufanya mambo kwa ajili ya maisha yaliyo bora na ya ukamilifu.
3. Kuiachia Huru Akili
Uislamu unatoa mwito wa kufikiri, kutaamali na kuchunguza maumbile haya kwa kutafiti kuweza kujua siri zake, faida zake na manufaa yake. Vilevile kujua mafungamano ya mtu na muumba wake. Pia Uislamu unatoa mwito kwa dini, elimu na falsafa, kutilia umuhimu mambo yanayoonekana na maarifa ya hisia; jambo ambalo wamekuwa nalo waislamu tangu mwanzo, kisha likaenda kwa wazungu. Ikawa msingi wa elimu ya majaribio uko kwao:
أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ ﴿١٨٥﴾
Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu. Juz. (7:185).
4. Uhuru Wa Kufikiri
Uislamu unatoa uhuru wa kusema na kufikiri, kiasi ambacho Mwenyezi Mungu aliwaruhusu watumishi wake, Malaika, wamuhoji huku wakisema:
قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ ﴿٣٠﴾
Utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu? Juz; 1 (2:30).
Pia aliruhusu Ibrahim
amjadili kuhusu watu wa Lut:
فَلَمَّا ذَهَبَ عَنْ إِبْرَاهِيمَ الرَّوْعُ وَجَاءَتْهُ الْبُشْرَىٰ يُجَادِلُنَا فِي قَوْمِ لُوطٍ ﴿٧٤﴾
“Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.” Juz; 12 (11:74).
Bali alimruhusu hata Iblis kutoa hoja mbele yake:
قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾
“Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo” Juz, 8 (7:12).
5. Wigo Mpana
Mafunzo yote ya kiislam yanaenea kwa wote; hayahusiki na mtu wala kikundi wala hayabagui:
إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ﴿١٣﴾
“Hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye takua zaidi” (49:13)
Hadith inasema: “Nyote mmetokana na Adam, na Adama ametokana na mchanga”.
6. Jihadi
Uislamu umelazimisha jihadi ya hali na mali dhidi ya dhulma na ufisadi kwa kila mwenye uwezo. Mwenyezi Mungu anasema:
“Nendeni mkiwa wepesi na wazito, na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, Hilo ni kheri kwenu mkiwa mnamjua.” Juz; 10 (9:41).
Imam Ali
anasema:“Wallah! Lau si Mwenyezi Mungu kuchukua ahadi kwa Maulama kwamba wasiafiki kuvimbiwa kwa dhalim wala kufa njaa kwa aliyedhulumiwa, ningelitupilia mbali kamba yake na ningelim- nywesha wa mwisho wake kwa glasi ya wa mwanzo wake na dunia yenu hii kwangu ingelikuwa ya upuzi kuliko kamasi za mbuzi.”
Ustadh Muhammad Sa’d Jalal, katika Jarida la Al-katib la Misr anasema, ninamnukuu: “Makusudio ya Imam (Ali) ni kuwa lau si ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa maulama kutokubali tofauti mbaya baina ya watu katika kula; ambapo wengine wanavimbiwa kwa kula ili wengine wawe na njaa, basi asingeli- fanya juhudi ya kuitaka haki yake ya ukhalifa ambayo ndiyo nyenzo ya kuthibitika uadilifu wa kuzuia tofauti iliyotajwa. Kwa hiyo jihadi yake haikuwa kwa ajili ya kutamani utawala na manufaa ya nafsi yake; isipokuwa ilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza hukumu ya uadilifu wa kijamii katika kugawa utuajiri kwa waislamu wote kwa namna ambayo hatakuweko mwenye kuvimbiwa kwa kula wala mwenye utapia mlo.”
7. Mali Ni Ya Mwenyezi Mungu
Vyote vilivyomo ulimwenguni ni mali ya Mwenyezi Mungu na binadamu ni wakala wa vile vilivyomo mikononi mwake. Kwa hiyo ni juu yake kutotumia ila kwa idhini na amri ya yule mwenyewe anayemuwakilisha: “Ni vyake vilivomo mbinguni na vilivyo katika ardhi na viliomo baina yao na viliyomo chini ya ardhi” (20:6) (57:7) Angalia Juz; 4 (180).
8. Uislamu Na Maisha
Uislamu unalenga binadamu aishi katika uwiano unaokwenda sambamba na nidhamu ya ulimwengu na mahitaji ya maisha:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ﴿٢٤﴾
Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai, juz.9 (8:24).
Angalia maelezo yake huko, Hivi karibuni kimetoka kitabu kipya cha mwandishi Wilfred Smith, Anasema katika kitabu hicho: “Waislamu wana uwezo, kulingana na dini yao, wa kuleta maendeleo pamoja na mahitaji ya sayansi na kuchangia katika kutengeneza jamii itakayoongozwa na maendeleo ya kijamii kwa uadilifu na heshima.”
Na kwamba wale wasioamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu.
Hakuna tofauti baina ya anayemkufuru Mwenyezi Mungu na anayekufuru siku ya mwisho. Kwa sababu kukataa kurudishwa viumbe baada ya kufa, maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu hawezi hilo; na hivyo hasa ni kufuru.
Imam Ali
anasema:“Namstaajabu yule anayemtilia shaka Mwenyezi Mungu naye anaona umbile lake; na namstaajabu yule anayekanusha ufufuo wa Akhera naye anaona ufufuo wa kwanza.”
Na mtu huomba shari kama vile aombavyo kheri.
Katika maisha haya kuna huzuni na furaha, tamu na chungu, Hakuna kimo- jawapo kinachodumu. Ni kuanzia hapa ndio ikasemwa: ‘siku ni mbili: kuna siku yako na siku ya kwako.’ Lakini baadhi ya watu wanapopatwa na jambo baya lolote wanalalamika na mishipa kuwasimama, wakidhani kuwa wako kwenye matatizo makubwa yasiyotatulika. Kwa hiyo wanajiombea shari, kama wanavyojiombea heri. Na hii ni aina ya ujinga na upumbavu. Lau wangelingojea siku kidogo tu, matatizo yangeliondoka pamoja na siku zinavyokwenda
Na mtu amekuwa ni mwenye pupa katika kujiombea shari bila ya kuwa na subira na uvumilivu.
Makusudio ya mtu hapa ni baadhi sio watu wote. Kwenye Nahjul-balagha kuna msemo huu: “Msilifanyie haraka lile linalokuwa kwa kungojewa, Wala msione kuchelewa litakalokuja kesho, Ni mangapi yaliyopatikana yakidhaniwa hayatapatikana?”
Na tumeufanya usiku na mchana kuwa ni ishara mbili.
Ni dalili mbili za kuweko Mwenyezi Mungu; Kwa sababu zinafuatana kulingana na kanuni thabiti na nidhamu ya kudumu kwenye maelfu ya miaka; hakuna hata mwaka mmoja uliotufautiana na mwingine. Yote hayo, na mengine mfano wake, ni dalili mkataa ya kuweko mpangiliaji mzuri na mhandisi mwenye ujuzi wa hali ya juu sana.
Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawapa mwito wataalamu na wenye fikra kumwamini Yeye kupitia kufikiria vizuri na kuzingatia maumbile ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, jinsi vilivyopangiliwa kwa utaalamu wa hali ya juu; kama vile kufuatana usiku na mchana na mengineyo yanayoonekana ulimwenguni.
Ama wale watu wa kawaida anawalingania kwa kukumbuka neema zake:
فَلْيَعْبُدُوا رَبَّ هَـٰذَا الْبَيْتِ ﴿٣﴾ الَّذِي أَطْعَمَهُم مِّن جُوعٍ وَآمَنَهُم مِّنْ خَوْفٍ ﴿٤﴾
Basi na wamwabudu Mola wa nyumba hii, ambaye amewaliwasha kutokana na njaa na akawasalimisha na hofu (106: 3-4).
Tunasema hivi huku tukijua kuwa miito yote miwili (kufikiria maumbile na neema) inaweza kuwa pamoja.
Tena tukaifuta ishara ya usiku.
Kusema ishara ya usiku ni kubainisha; maana yake ni hiyo hiyo ishara ambayo ni usiku.
Unaweza kuuliza kuwa
: dhahiri ya neno kufuta ni kuondoka kabisa na inajulikana usiku upo kwa hisia na kuona?
Makusudio ya kufuta hapa ni kuondoka athari ya kiutendaji. Kwa sababu watu wanatulia kinyume na mchana ambapo watu wanafanya kazi na kuhangaika huku na huko. Kwa hiyo linalofutwa hapa ni ule utulivu. Mwenyezi Mungu anasema:
وَجَعَلَ اللَّيْلَ سَكَنًا ﴿٩٦﴾
Ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, Juz. 6 (6:96)
وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا ﴿١٠﴾ وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾
Na tukaufanya usiku kuwa ni sitara na mchana kuwa ni wakati wa maisha (78:10–11).
Na tukaifanya ishara ya mchana ni ya kuangazia kila kitu kionekane ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu.
Usiku ni wa utulivu na kupumzika na mchana ni wa kutafuta riziki kwa mkono na kutoka jasho, sio kwa kughushi, hila, hiyana na kuwa kibaraka ili mtafute fadhila kutoka kwa ofisi za mabalozi na za upelelezi. Fadhila ya Mwenyezi Mungu inatolewa kwa kila mwenye kuitaka; nayo ni bora na ni yenye kubaki, tena ni safi na twahara.
“Ewe Mola tujaalie tutosheke na halali yako tusiwe na haja na haramu yako na tutosheke na twa yako tusiwe na haja na maasi yako na fadhila yako tusiwe na haja ya kumuomba asiyekuwa Wewe”
Na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu.
Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz; 10 (9:36).
Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametubainishia halali na haramu, akatuwekea hoja, dalili na mawaidha. Mwema ni yule aliyejikomboa na matamanio na akajikwamua na hawa ya nafsi yake.
وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ﴿١٣﴾
13. Na kila mtu tumemfungia ndege wake shingoni mwake, Na siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa.
اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا ﴿١٤﴾
14. Soma kitabu chako! Nafsi yako leo inakutosha kukuhisabu.
مَّنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾
15. Anayeongoka hakika anaongoka kwa faida ya nafsi yake tu, na anayepotea anapotea kwa hasara ya nafsi yake tu. Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine, Wala sisi hatuadhibu mpaka tupeleke Mtume.
NDEGE SHINGONI
Aya 13 – 15
LUGHA
Makusudio ya ndege hapa ni matendo ya mtu ya kheri na shari. Waarabu walikuwa wakiona ni bahati njema ndege anayekuja upande wa kuume kwa sababu mtu anaweza kumpiga na wakiona ni kisirani ndege akitokea upande wa kushoto, kwa sababu hawezi kumpiga.
Ndio likaazimwa neno ndege kwa matendo ya heri na shari [6]
.1 Shingoni mwake ni fumbo la kuwa nayo; kama vile amefunga koja au mkufu.
MAANA
Aya hizi tatu zinatofautiana kimatamshi, lakini zinashabihiana kimaana, Kauli yake Mwenyezi Mungu: Na kila mtu tumemfungia ndege wake shingoni mwake ni fumbo la kuwa mtu peke yake ndiye mwenye jukumu la matendo yake. Na kauli yake:
Na siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa.
Maana yake ni kuwa mtu kesho hataweza kuficha kitu chochote katika mambo aliyoyatenda:
يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُّحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِن سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا ﴿٣٠﴾
“Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa Na iliyoyatenda katika uovu, itapenda lau kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye.” Juz. 3(3:30)
Kwa maelezo zaidi angalia huko.
Pia kauli yake Mwenyezi Mungu: Soma kitabu chako! Nafsi yako leo inakutosha kukuhisabu.
Hakuna haja ya shahidi wala mhasibu kesho; Kwa sababu mtu mwenyewe atajishuhudia na atajihisabu. Twabrasi anasema: “Atakuwa anajihisabu mwenyewe kwa sababu Siku ya Kiyama atakapoyaona matendo yake yote yameandikwa na kuona malipo yake pia yameandikwa kwa uadilifu, hayakupunguwa wala kuzidishiwa adhabu hata kidogo, atakiri na kukubali yeye mwenyewe, wala hatakuwa na hoja wala upinzani, Itawadhihirikia watakaofufuliwa kuwa hakuna dhulma.
Anasema Hasan:“Ewe mwanadamu! Amekufanyia insafu yule aliyekufanya ujihisabu mwenyewe.”
Anayeongoka hakika anaongoka kwa faida ya nafsi yake tu, na anayepotea anapotea kwa hasara ya nafsi yake tu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6: 104) na Juz. 11 (10: 108).
Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:164), Wala sisi hatuadhibu mpaka tupeleke Mtume.
Angalia Juz. 2 (2:159) kifungu cha ‘Ubaya wa adhabu bila ya ubainifu’.