5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا ﴿٢٦﴾
26. Na mpe jamaa wa karibu haki yake na maskini na mwana njia, wala usifanye ubadhirifu.
إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾
27. Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashetani, na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake.
وَإِمَّا تُعْرِضَنَّ عَنْهُمُ ابْتِغَاءَ رَحْمَةٍ مِّن رَّبِّكَ تَرْجُوهَا فَقُل لَّهُمْ قَوْلًا مَّيْسُورًا ﴿٢٨﴾
28. Na ikiwa unajipurukusha nao kwa kutaraji rehema ya Mola wako, basi sema nao maneno laini.
وَلَا تَجْعَلْ يَدَكَ مَغْلُولَةً إِلَىٰ عُنُقِكَ وَلَا تَبْسُطْهَا كُلَّ الْبَسْطِ فَتَقْعُدَ مَلُومًا مَّحْسُورًا ﴿٢٩﴾
29. Wala usiufanye mkono wako umefungwa shingoni mwako, wala usiunyooshe wote kabisa, utabaki mwenye kulaumiwa, mwenye kuishiwa.
إِنَّ رَبَّكَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٣٠﴾
30. Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni mwenye habari, aonaye.
وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا ﴿٣١﴾
31. Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao Hakika kuwaua ni hatia kubwa.
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾
32. Wala msiikurubie zinaa; Hakika hiyo ni uchafu na njia mbaya.
وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَمَن قُتِلَ مَظْلُومًا فَقَدْ جَعَلْنَا لِوَلِيِّهِ سُلْطَانًا فَلَا يُسْرِف فِّي الْقَتْلِ إِنَّهُ كَانَ مَنصُورًا ﴿٣٣﴾
33. Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki. Na aliyeuliwa kwa kudhulumiwa, basi tumempa madaraka walii wake, lakini asipetuke mpaka katika kuua, kwani hakika yeye anasaidiwa.
وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا ﴿٣٤﴾
34. Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi, mpaka afikie kukomaa kwake; Na tekelezeni ahadi. Hakika ahadi itasailiwa.
وَأَوْفُوا الْكَيْلَ إِذَا كِلْتُمْ وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٣٥﴾
35. Na timizeni kipimo mnapopima, na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni kheri kweni na hatima njema.
وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾
36. Wala usifuatilie ambalo huna ujuzi nalo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitasailiwa.
وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولًا ﴿٣٧﴾
37. Wala usitembee katika Ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.
كُلُّ ذَٰلِكَ كَانَ سَيِّئُهُ عِندَ رَبِّكَ مَكْرُوهًا ﴿٣٨﴾
38. Hayo yote ubaya wake ni wenye kuchukiza mbele ya Mola wako.
ذَٰلِكَ مِمَّا أَوْحَىٰ إِلَيْكَ رَبُّكَ مِنَ الْحِكْمَةِ وَلَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتُلْقَىٰ فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا ﴿٣٩﴾
39. Hayo ni katika hekima alizokupa wahyi Mola wako. Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukalaumiwa, uliyetupwa.
WASIA 10
Aya 26 – 39
MAANA
1.Na mpe jamaa wa karibu haki yake na maskini na mwana njia wala usifanye ubadhirifu.
Amenukuu Tabrasi katika Majmaul-bayan kutoka kwa Assadiy, ambaye ni miongoni mwa wafasiri wakubwa, kwamba makusudio ya jamaa wa karibu ni jamaa wa Mtume(s.a.w.w)
.
Abu Hayan Al-andalusi amenukuu kutoka kwa Imam Ali bin Husein
kwamba yeye amesema: “Hao ni jamaa wa Mtume(s.a.w.w)
, Mwenyezi Mungu ameamrisha kuwapa haki yao kutoka katika hazina.
Amesema Abu Bakar Al-mua’firi Al-maliki katika Ahkamul-qur’an: “Anaingia katika jamaa wa karibu jamaa wa Mtume kuingia kwa kutangulia na kwa njia ya aula tu. Lakini hakika Aya ni ya ndugu wa mtu walio karibu zaidi. Ama jamaa wa karibu wa Mtume Mwenyezi Mungu amebainisha kuwahusu wao na akaeleza kwamba kuwapenda ndio ujira wa Mtume kwa yale aliyotuongoza.”
Imesemekana kuwa makusudio ya jamaa wa karibu ni yule ambaye ana haki ya kumtunza na kurithi, masikini ni muhitajia na mwananjia ni msafiri aliyekatikiwa njiani asiyekuwa na uwezo wa gharama za kurudi kwao. Hawa wawili wana haki ya zaka; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٦٠﴾
“Hakika sadaka ni ya (hawa) tu: Mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao na kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na mwana njia.” Juz.10 (9:60).
Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashetani, na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya wabadhirifu kuwa ni ndugu wa shetani, kwa sababu ubadhirifu ni jambo linalochukiwa na Mwenyezi Mungu na kila linalochukiwa na Mwenyezi Mungu linapendeza kwa shetani.
Hakuna anayetofautiana na wenzake kuwa maana ya ubadhirifu ni kutoa mali kwenye njia isiyokuwa yake na kuiweka mahali pasipokuwa pake, iwe kwa uchache au kwa wingi. Kwa ibara ya watu wa mantiki ni kwamba ubadhirifu ni katika aina si katika idadi.
Unaweza kuuliza kuwa
: kauli ya isiyokuwa njia yake na pasipokuwa mahali pake inafanana na maneno yenye kutatiza ambayo yanahitaji ufafanuzi na maelezo; basi ni ipi hiyo njia yake na mahali pake?
Jibu
: kila mwenye kutumia mali yake katika mambo yanayomletea madhara au yasiyokuwa na manufaa yoyote, basi huyo ni mwenye israfu, mbadhirifu na safihi, kikawaida na kisharia; isipokuwa mali anayoitoa kwa ajili ya kuvuta sigara. Tumedokeza kuhusu matumizi mabaya na kuzuiliwa kutumia matumizi ya kimali kwa mwenye kufanya hivyo, katika Juz. 4 (4:5).
WAKO WAPI WAADILIFU?
Swali la pili
linaweza kuja hivi: Mtu ametumia mali yake kwa kunywa pombe, kula nyama ya nguruwe na mengineyo katika yaliyoharamishwa ambayo yanamletea manufaa ya sasa na madhara ya muda ujao. Mtu huyu watu wengi hawamuoni kuwa ni mbadhirifu wala safihi; sasa je, sharia ya kiislamu inawajibisha kuzuiliwa matumizi ya kimali, kwa vile yeye ni safihi mwenye kufanya israfu?
Jibu
: Mtu mwenye akili anayo ruhusa ya kutumia mali yake bila ya kuiingiliwa; awe mumin au kafiri, fasiki au mwadilifu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Mkiwaona wana uwekevu, basi wapeni mali zao” Juz. 4 (4:6) na wala hakusema mkiwaona wana uwekevu wa dini au uadilifu. Imepokewa Hadith Mutawatur kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
kwamba yeye amesema: “Watu wamesalitiwa na mali zao,” na wala hakusema waumini au waadilifu.
Kwa hiyo sharti pekee la kusihi matumizi haya ni uwekevu katika mali si katika dini. Lau ingelikuwa uadilifu na uongofu ni sharti la kusihi matumizi ya mtu katika mali yake, basi nidhamu ingeliharibika na maisha yangesimama, kwa sababu watu wa duniani wako kama tunavyowajua, tutawatoa wapi watu wa dini na waadilifu?
Hanafi, Malik na Hambali wako katika rai yetu hii. Ama Shafii, wamesema kuwa uongofu ndio unaofaa katika dini na mali, kama ilivyoelezwa katika kitab Al-mughni cha Ibn Abi quddama.
Na ikiwa unajipurukusha nao kwa kutaraji rehema ya Moa wako, basi sema nao maneno laini.
Wakusema nao hapa ni jamaa wa karibu, masikini na msafiri aliyeishiwa njiani. Maana ni kuwa, akikuuliza kitu katika mali na wala usipate cha kumpa na ukamuomba Mwenyezi Mungu amtosheleze yeye na akutosheleze wewe kutokana na fadhila yake na rehema yake, basi sema naye kwa kauli laini kwa kumpa maneno mazuri yatakyompa matumaini na matarajio katika moyo wake. Kuna Hadith isemayo: “ Ikiwa hamna wasaa wa kuwapa watu mali zenu basi mnao wasaa wa kuwapa maadili yenu” Mshairi naye anasema: Kutamka kuwe kwema ikiwa hali si njema.
UISLAMU NA NADHARIA YA MAADILI
2.Wala usiufanye mkono wako umefungwa shingoni mwako, wala usiunyooshe wote kabisa, utabaki mwenye kulaumiwa, mwenye kuishiwa.
Kipimo na uwiano ndio msingi wa kila kitu katika Uislam kiitikadi, kisharia na kimaadili; sio ki ulahidi na kiidadi ya waungu. Na si kwa kuondoa milki ya mtu wala kuweka milki ya utaghuti na wala sio udikteta wa kikundi cha watu au wa mtu mmoja wala si utawala wa kila anayetaka, sio utawa wala sio kuzama kwenye matamanio. Kila kitu kinakuwa na uhalali na uharamu:
وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾
“Na kila kitu kwake, ni kwa kipimo” Juz; 13 (13:8).
Kusema kwake ni kwa kipimo ni kuwa na nidhamu inayoafikiana na hekima na masilahi, hakuna kupetuka mpaka wala kupetusha mipaka; wala hivi hivi au kombokombo. Kila kitu kina mpaka wake mbele ya Mwenyezi Mungu ambayo ni wajibu kwa kila mtu asimame kwenye mipaka hiyo bila ya kuikeuka. Kwa mfano mipaka ya hukumu na utawala ni uadilifu; mipaka ya kumiliki ni kutomdhuru mtu au watu; mipaka ya matumizi ni kutofanya uchoyo wala kufanya ubadhirifu na matendo mengineyo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameuletea ibara uchoyo kwa kufunga mkono shingoni, kwa sababu mchoyo anazuia mkono wake kutoa. Na kauli yake: ‘wala usiunyooshe wote kabisa’ anakusudia mkono ambao hauzuii kitu. Mwisho wa wote hawa wawili ni mmoja – kuishiwa na lawama.
Mwenye israfu atauma mkono wa kuishiwa, kujuta na kulaumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu, watu na yeye mwenyewe, pale atakapokuwa mikono mitupu; wakati ambapo bakhili analaumiwa na kila mtu, na kuishiwa kwake kesho ni zaidi kuliko mbadhirifu. Jambo bora zaidi ni wastani.
Unaweza kuuliza
: Je, hii ina maana Uislamu unakubaliana na nadharia ya Socrates inayosema: Kila ubora ni kati ya mabaya mawili. Kwa hiyo ushujaa ni wastani baina ya kujitutumua na woga, ukarimu ni baina ya israfu na uchoyo, unyenyekvu ni baina ya kutahayari na kukosa haya nk?
Jibu
: Hapana! Kwani Uislam unapanga ubora na kuweka sharia ya hukumu kwa misingi ya masilahi ya mtu mmoja mmoja hadi watu wengi. Kila jambo ambalo linaendeleza maisha basi ni wajibu wa lazima kwa kiongozi na wajibu wa kutosheana (kifaya) kwa raia.
Na kila lenye manufaa kwa upande fulani basi ni bora; bali ni ibada ya wajibu kwa kila mwenye uweza au suna kulingana na kiwango cha manufaa. Mwenyezi Mungu anasema:
وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ﴿١٧﴾
“Ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi” Juz; 13 (13:17).
Mtume(s.a.w.w)
amesema: “Bora ya watu ni yule wanayenufaika naye.” Dalili wazi zaidi ya hakika hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.” Juz.9 (7:157).
Msingi huu wa Qur’an – masilahi - unaweza kulingana na nadharia ya wastani kwenye vitu vyenye wastani; kama vile ukarimu kuwa baina ya uchoyo na israfu. Lakini unatofautiana katika vitu visivyo na wastani; kama vile uaminifu ni dhidi ya hiyana, wala hakuna jingine la kuleta wastani kuwa ni baina ya uaminifu na hiyana; Tumezungumzia kuhusu maadili katika Juz. 6 (5:79).
Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni mwenye habari aonaye.
Makusudio ya kumpimia ni kuifanya finyu. Kila kitu kiko mikononi mwake, riziki na zisizokuwa riziki. Kwa sababu Yeye ni mmliki wa milki zote, lakini hekima yake imetaka na kupitisha kutomruzuku yeyote isipokuwa kwa sababu za kiulimwengu ambazo ameziumba na kuziwekea njia za kuchuma mali n.k. Angalia Juz. 6(5: 66) na Juz; 13 (13: 26).
3.Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao pia. Hakika kuwaua ni hatia kubwa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6: 151).
4.Wala msiikurubie zinaa. Hakika hiyo ni uchafu na njia mbaya.
Imekuwa ni uchafu kwa vile mwishilio wake ni kuvurugika na kuchanganyika nasaba. Inatosha zina kuwa ni uovu kwa vile ni katika sifa mbaya za kushutumiwa.
5.Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki.
Umetangulia mfano wake katika katika Juz. 8 (6: 151).
Na aliyeuliwa kwa kudhulumiwa, basi tumempa madaraka walii wake, lakini asipetuke mpaka katika kuua, kwani hakika yeye anasaidiwa.
Kila aliyeuawa bila ya kufanya kosa linalowajibisha kuuliwa basi ameuawa kwa dhulma. Walii wa aliyeuawa ni ndugu zake kwa upande wa baba. Ikiwa hawako basi ni hakimu wa sharia. Kupetuka mpaka katika kuua ni kuua wawili kwa mmoja; kama walivyokuwa wakifanya wakati wa jahilia.
Maana ni kuwa ndugu wa aliyeuawa kwa dhulma wana haki ya kuua aliyeua au kuchukua fidiya; kama ilivyoelezwa katika Hadith tukufu: “Mwenye kuua basi watu wa aliyeuawa wana hiyari mbili: wakipenda wataua na wakipenda watachukua fidiya.”
Kwa vile ndugu wa aliyeuawa wana haki hiyo, basi ni wajibu wa hakimu na kila mwislamu kusaidia kutimizwa haki hii; Yametangulia maelezo kuhusu haya katika Juz. 2 (2:178).
6.Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi, mpaka afikie kukomaa kwake.
Imekwishapita Aya kama hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (6: 152).
7.Na tekelezi ahadi; Hakika ahadi itasailiwa.
Kila aliloliamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza ni wajibu kutekelezwa; ikiwa ni pamoja na mapatano ya bei, ajira n.k. Kwa maelezo zaidi angalia Juz. 6 (5:1).
Na timizeni kipimo mnapopima na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni kheri kwenu na hatima njema.
Kukamilisha kipimo ni wajibu wa kisharia na kidesturi; wala hauhusiki na dini kuliko dini nyingine au desturi kuliko desturi nyingine. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehimiza kukamilisha kipimo kwa mifumo mbalimbali; kama vile: pimeni kwa mizani zilizo sawa, timizeni kipimo na mizani, wala msipunguze na wala msipetuke mipaka. Siri ya hilo ni kwamba ustawi wa jamii hauwezi kuwa bila ya usawa wa vipimo.
KUSEMA BILA YA UJUZI
9.Wala usifuatilie ambalo huna ujuzi nalo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitasailiwa.
Neno kufuatilia limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu Qafwa lenye maana ya kufatilia athari ya jambo. Miongoni mwa majina ya Mtume(s.a.w.w)
ni Almuqfi (mfuatiliaji) kwa vile yeye ni mtume wa mwisho.
Kusema jambo bila ya ujuzi ni vibaya hata kwa yule asiyemwamini Mungu na siku ya mwisho. Mwenyezi Mungu ametaja masikio, macho na moyo akikusudia mwenye vitu hivyo vitatu.
Na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu ataviuliza na kuviadhibu ikiwa vitawekewa vitu visivyovijua; kama vile lau mtu atasema nimesikia naye hakusikia, nimeona naye hakuona au ni ninaitakidi na kuazimia naye hana itikadi wala maazimio yoyote.
Hakuna tofauti baina ya anayekusudia uongo na anayekurupuka kusema jambo bila ya kulithibitisha. Kwani kusema kwa dhana na shubha ni kusema bila ya ujuzi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:
إِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا ﴿٣٦﴾
“Hakika dhana haifai kitu mbele yake haki” Juz; 11 (10:36)
إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ ﴿١١٦﴾
“Hawafuati ila dhana na hawakuwa ila wenye kuzua tu.” Juz; 8 (6: 116)
Mwenyezi Mungu amelinganisha dhana na kuzua.
Kutokana na Aya hii yanajitokeza mambo yafuatayo:
(i) Kubatilika na uharamu wa Taqlid (kufuata) kwa yule mwenye uwezo wa kuchambua hukumu kutoka kwenye rejea zake. Kwa sababu ameacha elimu yake na akaumia elimu ya mwingine. Hii ni rai ya Shia Imamia. Zaydiya, Muu’tazila, Ibin Hazm, Sheikh Muhammad Abduh, Sheikh Shaltut na wengineo. Tumezungumza kwa ufafanuzi kuhusu taqlid katika Juz. 8 (2:259).
(ii) Uharamu wa kutoa hukumu kwa kutumia qiyas (kukisia) na istihsan (kuchukulia kuwa ni vizuri).
Qiyas ni kulinganisha jambo ambalo halikutajwa katika hukumu na jigine lililotajwa kutokana na kuwa na sababu moja.
Kwa mfano sharia kusema kuwa nyanya wa upande wa mama anarithi na ikanyamazia nyanya wa upande wa baba. Tukasema kuwa huyu pia atarithi kwa kukisia kuwa yeye pia ni nyanya.
Istihsan ilivyosimuliwa kutokana na Abu Hanifa ni kutoa hukumu kwa atavyoonelea mujtahidi kuwa ni vizuri bila ya kuweko dalili yoyote isipokuwa anavyoonelea yeye tu.
Rejea Kitabu Allami’ fi usulilfiqh cha Abu Is-haq, Ibrahim bin Ali bin Yusuf Fayruz Abadiy, uk; 65 chapa ya 1939. Mwenya kitabu hicho ametoa mfano wa mwenye kusema:
‘Nikifanya jambo fulani basi mimi ni Myahudi’ akifanya jambo hilo itabidi atoe kafara kwa kuchukulia kuwa ni kama aliyeapa kwa kusema: ‘Wallahi nikifanya jambo fulani basi mimi ni Myahudi.’
Kila mwenye kujasiri kutoa fatwa na kubainisha halali na haramu na yeye si kufu wa kufanya hivyo, basi atakuwa amesema uongo na kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake na atakuwa ni katika wale waliokusudiwa na ile Aya isemayo:
تَاللَّـهِ لَتُسْأَلُنَّ عَمَّا كُنتُمْ تَفْتَرُونَ ﴿٥٦﴾
“Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua” Juz; 14 (16:56)
Na kauli ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w)
: “Mwenye kunisemea uongo kwa makusudi basi na ajichagulie makazi yake motoni” Kumsemea uongo Mwenyezi Mungu na Mtume ni kutoa riwaya kutokana nao au kunasibisha halali na haramu kwao.
Siku hizi mamufti wazushi wamekuwa wengi walioifanya dini kuwa ni njia ya kutafutia riziki na pazia ya kuwa wahaini na vibaraka. Wengine wameanzisha vyama vya kutumikia uzayuni na ukoloni, lakini vina majina ya kiislamu na waislamu ili kuwahadaa na kuwapoteza watu.
Sheikh mmoja aliniuliza kuhusu wake wa Habil na Qabil kuwa je, hao ni katika hurilaini wa peponi au sio? Nikamjibu kuwa masuala haya yanaju- likana kwa kunakili sio kwa kiakili, na nukuu yake haitumiwi isipokuwa ikiwa ni ya Qur’an au Hadith mutawatir wala hakuna nukuu yoyote ya hilo. Kwa hiyo inatupasa tunyamaze yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu.
Akasema: Itakuwaje? Je, tuseme tumeshindwa tutakapoulizwa? Nikamwambia: Je, tunatakikana tujue kila kitu kwa vile sisi tuna vilemba vya ushekhe?
Wala usitembee katika Ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.
Mjinga anaweza kuwa na kiburi na kujifanya mkubwa anapomiliki ghururi za dunia; kama vile jaha na mali. Lakini likimtokea jambo la ghafla katika mambo yaliyojificha, basi anakuwa mnyonge na kudangana hana la kufanya. Mwenye akili ni yule anayejijua, akafikiri na kuzingatia.
Kauli yake Mwenyezi Mungu‘Wala usitembee katika Ardhi kwa maringo’
ni kukataza kiburi na kuamrisha kunyenyekea. Kauli yake:‘Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima’
ni fumbo la kushindwa mtu na kwamba yeye ni mdhaifu wa kufikia anayoyataka; kama alivyo mdhaifu wa mwili wake kuweza kufikilia jabali kwa urefu na kuweza kuipasua ardhi kwa wayo wake.
Hayo yote ubaya wake ni wenye kuchukiza mbele ya Mola wako.
Hayo ni kuishiria yaliyotangulia kutajwa katika yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu na kuyakataza. Makusudio ya ubaya wake ni yale aliyoyakataza hasa. Maana ni kuwa vitu vyote hivi ambavyo amevikataza Mwenyezi Mungu anavichukia, na mwenye kuvifanya ni mwenye kughadhibikiwa na Mwenyezi Mungu na mwenye kustahili adhabu.
Hayo ni katika hekima alizokupa wahyi Mola wako.
Hayo ni ishara ya maamrisho na makatazo yaliyotanglia kutajwa. Hekima ni kukiweka kitu mahali pake; Hakuna mwenye shaka kwamba hukumu zake zote Mwenyezi Mungu ziko mahali pake. Na kwamba mwenye kuichukua atakuwa ameichukua kwa haki, heri na uadilifu.
Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukalaumiwa uliyetupwa.
Imetangulia Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Sura hii Aya 22. Mwenyezi Mungu ameanzia na kukataza shirki na akamalizia nako, kwa sababu tawhid ndio kianzio na lengo la Uislamu, dini ya Mwenyezi Mungu iliyo ya haki. Kwa kuwa hukumu zote zinatoka kwake, basi hakuna halali ila aliyoiamrisha wala haramu ila aliyoiharamisha.