TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16078
Pakua: 3324


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 19 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16078 / Pakua: 3324
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَقُل لِّعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنزَغُ بَيْنَهُمْ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوًّا مُّبِينًا ﴿٥٣﴾

53. Waambie waja wangu waseme maneno mazuri. Kwani shetani huchochea baina yao. Hakika shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.

رَّبُّكُمْ أَعْلَمُ بِكُمْ إِن يَشَأْ يَرْحَمْكُمْ أَوْ إِن يَشَأْ يُعَذِّبْكُمْ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ وَكِيلًا ﴿٥٤﴾

54. Mola wenu anawajua vilivyo, akipenda atawarehemu na akipenda atawaadhibu. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao.

وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِمَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَقَدْ فَضَّلْنَا بَعْضَ النَّبِيِّينَ عَلَىٰ بَعْضٍ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا ﴿٥٥﴾

55. Na Mola wako anawajua vilivyo waliomo mbinguni na waliomo ardhini. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya manabii kuliko wengine; na Daud tulimpa Zaburi.

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِهِ فَلَا يَمْلِكُونَ كَشْفَ الضُّرِّ عَنكُمْ وَلَا تَحْوِيلًا ﴿٥٦﴾

56. Sema: Waombeni hao mnaodai badala Yake; hawawezi kuwaondolea madhara wala kuyabadilisha.

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ إِنَّ عَذَابَ رَبِّكَ كَانَ مَحْذُورًا ﴿٥٧﴾

57. Hao wanawaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kujikurubisha kwa Mola wao, hata walio karibu miongoni mwao, na wanataraji rehema zake na wanaihofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako ni ya kuhofiwa.

WAAMBIE WAJA WANGU WASEME MANENO MAZURI

Aya 53 – 57

MAANA

Waambie waja wangu waseme maneno mazuri.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake mtukufu awaamrishe waumini au watu wote waseme maneno mazuri, watamke haki na uadilifu kwa thamani yoyote itakayokuwa, Angali Juz; 13 (14: 24–26).

Kwani shetani huchochea baina yao.

Shetani hutafuta makosa ya ulimi ili ayafanye ni kuni za moto wa uadui na chuki baina ya watu. Makosa ya ulimi hayawi tu kwa kutukana bali pia kwa kusifu pasipokuwa mahali pake na kwenye matamshi ya ufuska na uovu.

Hakika shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.

Uadui huu aliubainisha wazi pale aliposema:

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿١٦﴾ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ﴿١٧﴾

“Kwa kuwa umenipoteza, basi hakika nitawakalia katika njia yako iliyonyooka; kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao” Juz; 8 (7:16-17).

Mola wenu anawajua vilivyo, akipenda atawarehemu na akipenda atawaadhibu.

Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwadilifu na Mwenye hekima. Anajua hali za waja wake, yale yaliyo na masilahi nao na yale yenye ufisadi na anawachukulia kwa uadilifu wake na hekima yake.

Atamrehemu anayestahiki rehema naye ni yule anayefuata amri na mtiifu; Na atamwadhibu anayestahiki adhabu; naye ni yule muasi jeuri. Hiyo ni baada ya kuwawekea hoja kwa kuwafikishia yaliyo halali na yaliyo haramu kupitia kwa Mtume mtukufu.

Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao , bali ni mfikishaji:

فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾

“Basi ni juu yako kufikisha na juu yetu hisabu,” Juz.13: (13:40).

Na Mola wako anawajua vilivyo waliomo mbinguni na waliomo ardhini. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya manabii kuliko wengine; na Daud tulimpa Zaburi.

Mwenyezi Mungu anawajua watu wa mbinguni na wa ardhini na anajua uwezo wa kila mmoja wao. Kwa misingi hiyo ndio huwachagua wajumbe kwenda kwa mitume wake; kama vile Jibril(a.s) . Na hupeleka mitume wabashiri na waonyaji kwa watu.

Kama alivyowafadhilisha baadhi ya Malaika kuliko wengine; vilevile Mitume, baadhi amaewafadhilisha kuliko wengine.

Unaweza kuuliza kuwa : Uislamu unasimama kwenye misingi ya usawa ;sasa kuna maana gani ya ubora huu kwa baadhi kuliko wengine? Kisha ubora huu utapatikana vipi kwa Malika na Mitume na hali tunajua kuwa wote ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye kutukuzwa, hawamtangulii kwa jambo lolote na wanafanya kulingana na amri yake?

Jibu : Ndio ni kweli kuwa hakuna tofauti kwa msingi wa utiifu, isma, na utawala kama ulivyo; isipokuwa kwa upande wa sifa; kama vile dhahabu tunajua kuwa yote ina thamani, lakini kuna baadhi inathamani zaidi kuliko nyingine. Vile vile vitu vingine vizuri vinatofautiana kulingana na uzuri wake na daraja yake, sio katika kuwa kwake na hakika yake. Ndio maana ikasemwa: ‘Nuru juu ya nuru’ au ‘kheri juu ya kheri’

Swali la pili : imekuwaje Mwenyezi Mungu kumtaja Daud peke yake kuwa amempa Zaburi na tunajua kuwa Musa alimpa Tawrat, Isa Injil na Muhammad akampa Qur’an?

Amemtaja peke yake kuwarudi washirikina waliosema: vipi Muhammad atakuwa ni mtume na yeye ni yatima fukara. Njia ya kuwarudi ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaujalia ujumbe wake kwa yule anayestahiki - awe yatima aliyefukara, kama Muhammad au tajiri, kama Daud. Katika vitabu vingi vya sera na tarikh, hutajwa Mfalme Daud.

Sema: Waombeni hao mnaodai badala Yake, hawawezi kuwaondolea madhara wala kuyabadilisha.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Aya hii na inayofuatia zilishuka kwa ajili ya wale wanaoabudu malaika, Isa na Uzayr. Na kwamba wanokusudiwa hapa sio waabudu masanamu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewataja hao waabudiwa kwa kusema: ‘wao wenyewe wanatafuta njia ya kujikuru- bisha kwa Mola wao,’ na kutafuta nji hakuelekeani na masanamu.

Kwa hiyo maana ni kuwa ewe Muhammad! Waambie wale wanaoabudu Malaika, Isa na Uzayr: yakiwapata madhara, kama ufukara na maradhi, basi waaombeni wale manowaabudu wawaondolee, kisha muangalie, je wanaweza kuwakinga au kuwabadilishia? Hakuna mwenye shaka ya kushindwa kwao, kwa vile wao wenyewe hawawezi kujikinga itakuwaje kwa mwengine?

Hao wanawaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kujikurubisha kwa Mola wao.

Yaani hao ambao mnawaabudu enyi washirikina wanatafuta kujikuruku- bisha kwa Mwenyezi Mungu kwa twaa, hawajitii kiburi kwa waja wengine, wanamtakasa na kumsujudia Mungu, sasa vipi nyinyi mnawaabudu.

Hata walio karibu miongoni mwao, na wanataraji rehema zake na wanaihofu adhabu yake.

Yaani kila mmoja kati ya Malaika, Isa na Uzayr anajitahidi, kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi ili awe karibu na msamaha wake na rehema zake na awe mbali na machukivu yake.

Hiyo ni kwa vile Hakika adhabu ya Mola wako ni ya kuhofiwa.

Wanaihofia manabii na mawalii, je, wengine? Kila mwenye akili ni lazima ahofie mwisho na kuuandalia maandalizi, kwa hali yoyote atakavyokuwa na cheo na daraja; hasa ikiwa mwenye kuchukua hisabau anajua siri na yaliyofichikana.

وَإِن مِّن قَرْيَةٍ إِلَّا نَحْنُ مُهْلِكُوهَا قَبْلَ يَوْمِ الْقِيَامَةِ أَوْ مُعَذِّبُوهَا عَذَابًا شَدِيدًا كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا ﴿٥٨﴾

58. Hapana mji wowote ila Sisi tutauangamiza kabla ya Siku ya Kiyama au kuupa adhabu kali, Haya yamekwishaandikwa kwenye Kitabu.

وَمَا مَنَعَنَا أَن نُّرْسِلَ بِالْآيَاتِ إِلَّا أَن كَذَّبَ بِهَا الْأَوَّلُونَ وَآتَيْنَا ثَمُودَ النَّاقَةَ مُبْصِرَةً فَظَلَمُوا بِهَا وَمَا نُرْسِلُ بِالْآيَاتِ إِلَّا تَخْوِيفًا ﴿٥٩﴾

59. Na hapana kinachotuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na wathamudi tuliwapa ngamia jike kuwa ni dalili inayoonekana, lakini wakamdhulumu. Nasi hatupeleki ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.

وَإِذْ قُلْنَا لَكَ إِنَّ رَبَّكَ أَحَاطَ بِالنَّاسِ وَمَا جَعَلْنَا الرُّؤْيَا الَّتِي أَرَيْنَاكَ إِلَّا فِتْنَةً لِّلنَّاسِ وَالشَّجَرَةَ الْمَلْعُونَةَ فِي الْقُرْآنِ وَنُخَوِّفُهُمْ فَمَا يَزِيدُهُمْ إِلَّا طُغْيَانًا كَبِيرًا ﴿٦٠﴾

60. Na tulipokwambia: hakika Mola wako amekwishawazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tuliyokuonyesha ila ni fitna (majaribu) kwa watu na mti uliolaaniwa katika Qur’an. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.

MJI WOWOTE

Aya 58 – 60

MAANA

Mahdiy Anayengojewa

Hapana mji wowote ila Sisi tutauangamiza kabla ya siku ya Kiyama au kuupa adhabu kali, Haya yamekwishaandikwa kwenye Kitabu.

Dhahir ya Aya inafahamisha kuwa watu wote watatoweka kabla ya siku ya kiyama, ambapo itafika siku kwenye ardhi kutakuwa hakuna yoyote kabisa; na kwamba jambo hili limekwishaandikwa katika kadha na kadari ambayo haiepukiki. Kuna jamii itatoweka kwa mauti ya kawaida na nyingine kwa adhabu kali, lakini Mwenyezi Mungu hakubainisha wasifa wa hawa wala wale.

Hiyo ndiyo dhahir ya Aya, lakini wafasiri wamesema kuwa jamii njema itatoweka kwa mauti ya kawaida na jamii ya ufisadi itatoweka kwa adhabu kali. Lakini haya hayaafikianai na kauli yao katika kufasiri Aya za mwanzo za sura Hajj:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ ﴿١﴾ يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ ﴿٢﴾

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu, Hakika tetemeko la Saa (ya Kiyama) ni jambo kuu. Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshae na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake na utawaona watu wamelewa kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali,” (22:1-2).

Tuonavyo sisi mji alioukusudia katika kauli yake hii ni mji ambao watu wake ni madhalimu; yaani jamii yenye ufisadi tu; na kwamba Yeye ataiangamiza jamii hii au ataiadhibu kabla ya Siku ya Kiyama, wala hawatabakia ispokua watu wema tu, wote wakiwa wanaishi kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu wakiwa na amani ya nafsi zao na vitu vyao vyote.

Kuna Hadith nyingi zinazozungumzia suala hilo; miongoni mwazo ni hizi:-

Hadith iliyoko kwenye Sunan Abi Daud As-sasjsataniy, kikiwa ni mojawapo ya Sahih sita kwa masunni, Juzuu ya pili chapa ya mwaka 1952, uk. 422:

“Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : Lau haitabaki isipokuwa siku moja ya dunia, basi Mwenyezi Mungu atairefusha siku hiyo mpaka amlete mtu kutokana na watu wa nyumba yangu (Ahli bayti), Jina lake linafanana na jina langu na jina la baba yake ndio jina la baba yangu, ataijaza ardhi usawa na uadilifu; kama ilivyojazwa dhulma baada kujazwa usawa na uadilifu.”

Hadith iliyoko katika Sunan Ibn Maja, Pia nayo ni miongoni mwa sahih sita, juzuu ya pili chapa ya mwaka 1952, Hadith namba: 4083: Amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu: “Atakuwa katika umma wangu Mahdi, utaneemeka uma wangu neema ambayo haujaneemeka mfano wake.”

Mapinduzi na kujitoa mhanga kwa kujilipua (intifada), kila mahali kwa ajili ya kujikomboa na dhulma, ufisadi, ujinga na umasikini, yana fahamisha waziwazi kuwa hilo litakuwa tu karibuni au baadaye.

Na hapana kinachotuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na wathamudi tuliwapa ngamia jike kuwa ni dalili inayoonekana, lakini wakamdhulumu.

Washirikina walipendekeza kwa Mtume awaletee muujiza wanaoutaka wao. Miongoni mwa waliyoyasema ni: Tuchimbulie chemchem kutoka ardhini, tuletee Mungu na Malaika, tuletee kitabu kutoka mbinguni tukisome na mengineyo.

Ndio Mwenyezi Mungu akawajibu katika Aya hii, kwamba yeye amekwishapitisha katika kadha na kadari yake, kuwang’owa kwa adhabu kila kaumu iliyokadhibisha miujiza iliyokuja kwa maombi yao.

Wathamudi walimwomba Mtume wao awapatie ngamia wa muujiza. Alipowajia na sifa zile walizozitaka, walimkanusha na wakamchinja. Ukawanyakua ukelele wakawa ni wenye kuangamia; Yametangulia maelezo ya ngamia katika Juz; 8 (7:73 –79).

Imekwishapitisha kadari yake kutowang’oa Makuraishi, kutokana na mapendekezo waliyoyapendekeza kwa Mtume. Kwa sababu watapatikana watu watakaotubia na kuamini, watazaliwa wengine wapigania jihadi kwa Mwenyezi Mungu. zaidi ya hayo kadari ya Mwenyezi Mungu imepitisha kuwa uma wa Muhammad na sharia yake ubakie mpaka siku ya ufufuo. Kwa sababu hii na nyinginezo, Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuitikia maombi ya makuraishi.

Nasi hatupeleki ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.

Hakuna ishara yoyote inayodhihiri mikononi mwa Mtume ila ina malengo; yakiwemo: mawaidha, makaripio na kuhadharisha adhabu isiyokuwa na kinga wala kafara; sasa vipi wao wanaharakia kutoa maombi ya adhabu?

Na tulipokwambia: hakika Mola wako amekwishawazunguka hao watu.

Imeelezwa hapo juu kuwa makuraishi walimtaka Mtume awalete muujiza na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimpa wahyi Mtume wake kuwa lau atawaitikia maombi yao na wakaasi, wataangamia.

Lakini jawabu hili halikuwakinaisha washirikina na wakamwambia kuwa lau ungelikuwa ni Mtume ungelituletea yale tunayotaka, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia mtume wake kuwa wewe endelea tu, wala usiwajali wale wanaofanya inadi na kiburi. Sisi tunawajua zaidi watu na wanayoy- afanya na tumewadhibiti.

Katika maana ya Aya hii ni ile isemayo:

وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ﴿٦٧﴾

“Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu,” Juz. 6 (5:67).

Na hatukuifanya ndoto tuliyokuonyesha ila ni fitna (majaribu) kwa watu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kuwa alimuonyesha Mtume wake ndoto usingizini na kwamba ndoto yenyewe ni fitna, lakini hakubainisha ilikuwa ya aina gani wala makusudio ya hiyo fitna au majaribu.

Ndio maana wafasiri wakatofautiana katika maana yake, Akataja Razi kati- ka Tafsiri al-kabir, Abu Hayan Al-andalusi katika Al-bahrul-muhit, Muhammad bin Ahmad Al-kalabiy, katika Attas-hil na wengineo, wametaja kauli kadhaa katika tafsiri ya ndoto na fitna.

Miongoni mwazo ni mtume(s.a.w.w) aliota kuwa yeye ataingia Makka pamoja na swahaba, lakini alipotaka kuingia makuraishi walimzuia katika mwaka wa Hudaybiya.

Akaingiwa na shaka mwenye shaka miongoni mwa waislamu kuhusu ndoto ya Mtume, akamwambia: “Si umesema kuwa tutaingia Makka kwa amani?” Akasema: “Ndio, kwani nimesema tutaingia mwaka huu?” Akasema: “Hapana” Mtume(s.a.w.w) akasema: “Inshallah tutaingia” wakaingia mwaka uliofuatia.

Miongoni mwa kauli nyingine zinazotokana na tafsiri ni kuwa Mtume(s.a.w.w) aliona kwenye ndoto bani Umayya wakiiparamia mimbari yake kama anavyoparamia nyani, akahuzunika na akawa hana raha, na hakuonekana akicheka.

Kikundi miongoni mwa swahaba wako kwenye tafsiri hii; miongoni mwao ni Said bin Al-musabbib na Ibn Abbas; kama ilivyo katika Tafsiru-rrazi. Pia Sahal bin Sa’d; kama ilivyo katika Tafsir Al-bahr al-muhit.

Katika Sahih Al-bukhari Juzuu ya tisa Kitabu Al-fitan, imeelezwa kuwa Mtume(s.a.w.w) alisema: “Kuangamia kwa umma wangu kutakua mikononi mwa wafidhuli wa kikuraishi,” Riwaya hii inatia nguvu tafsiri ya ndoto kuhusu Bani Umayya.

Kwa hiyo makusudio yaNa mti uliolaaniwa katika Qur’an ni Bani Umayya. Katika Tafsiru-rrazi imeelezwa kuwa kuna kundi la wafasiri wanasema: “Mti uliolaaniwa katika Qur’an ni mayahudi.” Matukio ya Historia ya kale na ya sasa yamethibitisha kuwa mayahudi ndio mzizi wa fitina.

Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.

Mwenyezi Mungu amewahadharisha wanafiki kwa mifumo mbalimbali, lakini haikufaa kitu; bali hizo hadhari ziliwazidishia upotevu, kwa sababu wao hawataharaki isipokuwa kwa wahyi wa masilahi na manufaa. Ama hoja, maadili na misimamo, kwao ni maneno na njozi tu.

8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ قَالَ أَأَسْجُدُ لِمَنْ خَلَقْتَ طِينًا ﴿٦١﴾

61. Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alisema: Je, nimsujudie uliyemuumba kwa udongo?

قَالَ أَرَأَيْتَكَ هَـٰذَا الَّذِي كَرَّمْتَ عَلَيَّ لَئِنْ أَخَّرْتَنِ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَأَحْتَنِكَنَّ ذُرِّيَّتَهُ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٦٢﴾

62. Akasema: Unaona! Huyu ndiye uliyemtukuza zaidi kuliko mimi? Kama utaniahirisha mpaka Siku ya Kiyama, bila shaka nitakiburuza kizazi chake isipokuwa wachache tu.

قَالَ اذْهَبْ فَمَن تَبِعَكَ مِنْهُمْ فَإِنَّ جَهَنَّمَ جَزَاؤُكُمْ جَزَاءً مَّوْفُورًا ﴿٦٣﴾

63. Akasema: Ondoka! Atakayekufuata katika wao, basi Jahannam itakuwa ndio malipo yenu, malipo yenye kutimia.

وَاسْتَفْزِزْ مَنِ اسْتَطَعْتَ مِنْهُم بِصَوْتِكَ وَأَجْلِبْ عَلَيْهِم بِخَيْلِكَ وَرَجِلِكَ وَشَارِكْهُمْ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ وَعِدْهُمْ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُورًا ﴿٦٤﴾

64. Na uwachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na wendao kwa miguu na shirikiana nao katika mali na watoto na uwaahidi. Na shetani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.

إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ وَكِيلًا ﴿٦٥﴾

65. Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, na Mola wako anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

WAKASUJUDU

Aya 61-65

MAANA

Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alisema: Je, nimsujudie uliyemuumba kwa udongo?

Umepita mfano wake katika Juz. 1 (2:35) na Juz, 8 (7:11).

KUMTANGULIZA ALIYEZIDI JUU YA ALIYEZIDIWA

Akasema: Unaona! Huyu ndiye uliyemtukuza zaidi kuliko mimi?

Iblisi anahoji kwa majisifu na ufedhuli akimwambia, aliyemtukufu na kutukuka, kuwa ni nani huyo ambaye umemfadhilisha kuliko mimi? Na ni kitu gani kimemfanya awe na heshima hiyo na ukamilifu? Naona ni kinyume na hivyo:

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾

“Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.” Juz; 8 (7:12).

Habithi huyu alijitia ubora kwa kutetea mantiki yake, kuwa yeye ni bora na mkamilifu; Kwa hiyo yeye hafai kumsujudia aliyemzidi.

Ibilisi amekosea katika mantiki yake haya; Kwa sabau yeye si bora kabisa kuliko Adam, bali ni kinyume. Kwahiyo Mwenyezi Mungu hakumtanguliza aliyezidiwa juu ya aliyezidi; kama alivyodai Ibilisi. Ni akili gani inayoruhusu kuwa Mwenyezi Mungu amkurubishe aliye baidi na ambaidishe aliye karibu? Lakini hakika hii imefichika kwa Ashaira[8] na Mu’tazila, waliposema kuwa inafaa kutangulizwa aliyezidiwa juu ya aliyemzidi. Tazama kitabu Al-mawqif Juzuu ya nane Uk. 373.

Wanasema Ashaira; Akili inakubali kuwa Mwenyezi Mungu atamwadhibu mtiifu na kumpa thawabu muasi, kwa sababu, kwa Mwenyezi Mungu hakuna uovu wala hana wajibu wowote. Tazama kitabu hicho hicho Uk. 195. Shia Imamiya wanasema akili haikubali kuwa Mwenyezi Mungu amwadhibu aliyefanya wema, lakini inakubali kuwa anaweza kuwasamehe waovu; sawa na mwenye haki yake, anaweza akasamehe yote au baadhi.

Wakaendelea kusema kuwa haikubaliki kiakili kutangulizwa aliyezidiwa juu ya aliyemzidi kwa sababu ni daraja ya juu na ya chini kulingana na utaratibu wa kimaumbile. Kumfanya aliyejuu kuwa yuko chini na aliye chini kuwa yuko juu ni kinyume na mantiki ya kiakili na kimaumbile.

Kama utaniahirisha mpaka siku ya kiyama, bila shaka nitakiburuza kizazi chake isipokuwa wachache tu.

Ibilisi anatishia kuchukua kisasi kwa kizazi cha Adamu; si kwa jambo lolote ila ni kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtukuza Adamu. Anachukua kisasi kwa kuwaburuza kwenye maasi, kama vile anavyokokotwa mnyama; isipokuwa wachache tu ambao ni wale wenye ikhlasi.

Kisha Ibilisi anataka apewe muda katika maisha yake ili apoteze watu na afanye ufisadi; Mwenyezi Mungu akamkubalia maombi yake,akasema: ondoka! Atakayekufuata katika wao, basi Jahannam itakuwa ndio malipo yenu, malipo yenye kutimia.

Ibilisi alipotishia kuwapoteza wanadamu, Mwenyezi Mungu naye akamkemea yeye na wale atakaowapoteza na kumwambia: fanya utakavyo, atakufuata kwenye upotevu yule atakayetaka, kwani mimi si mlazimishi yeyote kwenye twaa na maasi. Wote ninawapa uwezo, akili na utashi na ninawabainishia njia ya kheri na njia ya shari. Ninakataza hili na kuamuru lile. Mwenye kufuata na akatii, basi pepo ni makazi yake na mwenye kuwa jeuri na akaasi basi jahannam ndio makazi ya waasi; watal- ipwa humo malipo wanayostahiki kwa ukamilifu bila ya upungufu.

Na uwachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na wendao kwa miguu.

Hakuna jeshi la hakika hasa la iblisi lililo na farasi au bila ya farasi; isipokuwa ni fumbo la wafisadi, yaani watu wanaofuata hawaa, wahaini na vibaraka.

Amesema Imam Ali katika Nahjul-balagha: “Tahadharini asije aka-chochea -shetani- kwa mwito wake na kuwakusanya kwenye jeshi lake la wapanda farasi na wanaokwenda kwa miguu.” Sheikh Muhammad Abduh naye akaongezea kwa kusema: ”Anawachochea mfanye lile alitakalo, mkichelewa atawakusanyia jeshi lake la wapanda farasi na waendao kwa miguu, yaani wasaidizi wake.”

Umepita mfano wake katika Juz; 8 (7:18). Huko tumejibu maswali matatu: kuwa je, alizungumza moja kwa moja na Mwenyezi Mungu au kwa kupitia kitu kingine? Je, upotevu unatokana na Mwenyezi Mungu au na Ibilisi? Kwanini Mwenyezi Mungu akampa muda Ibilisi ili apoteze watu? Rudia huko.

Na shirikiana nao katika mali na watoto.

Kushirkiana katika mali ni fumbo la kila mali iliyopatikana kwa njia isiyokuwa ya haki; kama vile uporaji, riba, utapeli, hiyana na kuwa kibaraka. Au kuitumia isivyostahiki; kama vile kufanya israfu, kuitumia kwenye pombe, kamari na kwenye mambo ya kujionyesha. Ama kushirikiana katika watoto ni fumbo la zina, kuua watoto kwa kuhofia ufukara na aibu na kuwalea malezi ya ufisadi.

Na uwaahidi na shetani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.

Ahadi ya udanganyifu ni kuivisha batili nguo ya haki na makosa kuyavika nguo ya usawa; kwa mfano shetani kumtia wasiwasi anayeamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, kuwa usihofie kumuasi Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni karimu Mwingi wa maghufira, na wewe bado una umri, utatubia kesho na kuomba maghufira.

Kuna baadhi ya mapokezi yanayosema kuwa Ibilisi alimtia wasiwasi mfanya ibada mmoja katika waisrail, afanye dhambi kisha atubie ili ibada yake iwe na nguvu.

Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, na Mola wako anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

Umepita mfano wake katika Juz. 14 (15: 42).

رَّبُّكُمُ الَّذِي يُزْجِي لَكُمُ الْفُلْكَ فِي الْبَحْرِ لِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ إِنَّهُ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٦٦﴾

66. Mola wenu ndiye anayewaendeshea majahazi, ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kuwarehemu.

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا ﴿٦٧﴾

67. Na inapowagusa dhara katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu, Anapowaokoa mkafika nchi kavu mnageuka. Na Mtu amekuwa mwingi wa kukanusha.

أَفَأَمِنتُمْ أَن يَخْسِفَ بِكُمْ جَانِبَ الْبَرِّ أَوْ يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ثُمَّ لَا تَجِدُوا لَكُمْ وَكِيلًا ﴿٦٨﴾

68. Je, mmeaminisha kuwa hataweza kuwadidimiza upande wa nchi kavu au kuwaletea tufani la kokoto, kisha msipate wa kutegemea?

أَمْ أَمِنتُمْ أَن يُعِيدَكُمْ فِيهِ تَارَةً أُخْرَىٰ فَيُرْسِلَ عَلَيْكُمْ قَاصِفًا مِّنَ الرِّيحِ فَيُغْرِقَكُم بِمَا كَفَرْتُمْ ثُمَّ لَا تَجِدُوا لَكُمْ عَلَيْنَا بِهِ تَبِيعًا ﴿٦٩﴾

69. Au mmeaminisha kuwa hatawarudisha humo mara nyingine awapelekee kimbunga cha upepo awazamishe kwa mlivyokufuru, kisha msipate wa kutufuatilia.

ANAWAENDESHEA MAJAHAZI

Aya 66-69

MAANA

Mola wenu ndiye anayewaendeshea majahazi, ili mtafute katika fad- hila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kuwarehemu.

Jahazi inatembea kwenye uso wa bahari kwa sababu za kimaumbile, hilo halina shaka, lakini sababu hizi zote zinaishia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu yeye ni muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Ni kwa sababu hii ndio ikafaa kutegemeza kuendesha kwake Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hekima ya hilo ni kuwa mtu daima awe katika fikra ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mtendaji mkuu wa vilivyomo ulimwenguni na wala sio maumbile. Ama lengo la jahazi ni kurahisisha mawasiliano.

Na inapowagusa dhara katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu, Anapowaokoa mkafika nchi kavu mnageuka, Na mtu amekuwa mwingi wa kukanusha.

Umepita mfano wake katika Juz. 11 (10:22).

Je, mmeaminisha kuwa hataweza kuwadidimiza upande wa nchi kavu au kuwaletea tufani la kokoto, kisha msipate wa kutegemea?

Watu wote wako mikononi mwa Mungu, popote pale walipo, hata wakiwa kwenye ngome zilizo na nguvu. Wakiwa baharini anaweza kuwangamiza kwa kufa maji, wakiwa nchi kavu anaweza kuwadidimiza ardhini au kunyweshewa na mvua ya mawe na wakiwa kwenye ngome imara anivunjilia mbali. Hawezi kujiaminisha ila mjinga.

Au mmeaminisha kuwa hatawarudisha humo mara nyingine awapelekee kimbunga cha upepo awazamishe kwa mlivyokufuru, kisha msipate wa kutufuatilia.

Humo ni baharini. Maana ni kuwa hakuna njia nyingine ya kuangamia isipokuwa baharini, basi Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuwarudisha humo, awazamishe kwa kimbunga na asipatikane wa kumfuatilia Mungu kwa aliyowafanyia.

Ufupi wa Aya hizo ni kuwa mjinga humhofia Mwenyezi Mungu anapokuwa na shida, lakini shida ikimuondokea anamgeuka; pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni muweza wa kunufaisha na kudhuru. Ama mumin mwenye akili anapata mawaidha kwa shida na raha, anahofia haya na kutaraji msaada kwa yale.

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا ﴿٧٠﴾

70. Hakika tumewatukuza wanaadamu na tumewabeba nchi kavu na baharini na tumewaruzuku vitu vizuri na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ فَمَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَأُولَـٰئِكَ يَقْرَءُونَ كِتَابَهُمْ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴿٧١﴾

71. Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao. Basi atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kuume, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.

وَمَن كَانَ فِي هَـٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٧٢﴾

72. Na aliyekuwa kipofu katika hii, basi Akhera atakuwa kipofu na aliyepotea zaidi njia.

WANAADAMU TUMEWATUKUZA

Aya 70-72

MAANA

Kwanini Mwenyezi Mungu amewatukuza wanaadamu? Kabla ya kujibu swali hili, kwanza tubainishe maana ya matamshi ya Aya.

Hakika tumewatukuza wanaadamu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemtukuza binadamu kwa kumpa uwezo na ujuzi uliomfanya awe ni muheshimiwa mwenye kutukuzwa. Tutataja baad- hi ya ujuzi huu na uweza baada ya kumaliza kufasiri matamshi ya Aya.

Na tumewabeba nchi kavu na baharini.

Kubebwa huku ni baadhi ya mambo aliyomtukuzwa nayo binadamu. Ni wazi kwamba kurahisishiwa mawasiliano ni katika mambo ya kuendeleza maisha watu.

Na tumewaruzuku vitu vizuri.

Kila linalomletea mtu manufaa kwa namna moja au nyingine, basi hilo ni zuri, lenye kheri na jema; liwe la kimaada au la kimaana.

Na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.

Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya wengi katika Aya ni wote. Kwa hiyo wakawaingiza Malaika, Suala hili limechukua kurasa ndefu za tafsiri; pamoja na kujua kuwa halina athari yoyote ya kiutendaji, isipokuwa kurefusha maneno.

Ilivyo hasa ni kuwa Aya iko mbali tena mbali sana na kufadhilisha baina ya binadamu na malaika. Na kwamba neno wengi linabaki kwenye dhahiri yake; kwani hakuna dharura ya kuleta taawili; bali elimu inawajibisha kubakia na dhahiri yake.

Kwani ugunduzi wa elimu umebatilisha nad- hariya isemayo kuwa ardhi ndio kituo kikuu cha ulimwengu na binaadamu ndiye bwana mkubwa wa ulimwengu wote.

Ugunduzi huu umehakikisha upotevu wa binadamu kulingana na ukubwa wa ulimwengu. Ugunduzi unathibitishwa na kukubaliwa na Qur’an, pale iliposema:

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٧﴾

“Umbo la mbingu na ardhi ni kubwa kuliko umbo la watu, lakini watu wengi hawajui (40:57)

Yaani hii sayari ya ardhi ambayo anaishi binadamu ni mojwapo tu ya mamilioni ya sayari ambazo sayansi hazijui idadi yake, pamoja na kuwa imegundua mambo ambayo hayana ukomo. Zaidi ya hayo ni kwamba wataalamu wengi wanasema kuwa kuna sayari zinazokaliwa na viumbe vyenye akili pengine zaidi kuliko binadamu.

Ni kweli kuwa binadamu ni bwana mkubwa aliyetukuzwa, hilo halina shaka, lakini yeye si bwana wa viumbe vyote, bali ni mmoja tu kati ya mabwana. Hakuna jambo linalofahamisha hilo zaidi kuliko ujinga wa binadamu kwenye vitu vingi na kushindwa kwake kuvitumia, Bali hajui vitu vingi vilivyomo ardhini; sikwambii vilivyo katika sayari nyingine. Kimsingi ni kwamba sharti la kwanza la ubwana ni uwezo wa kutumia vitu.

Baada ya kufafanua matamshi ya Aya, sasa tunadokeza mambo ambayo Mwenyezi Mungu amemtukuza nayo binadamu:

1. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuumba mtu akalifanya zuri umbo lake na sura yake. Mwenyezi Mungu anasema:

وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ﴿٦٤﴾

“Na akawatia sura na akazifanya nzuri sura zenu.” (40:64).

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾

“Hakika tumemuumba mtu katika hali nzuri sana,” (95:4).

2. Akili. Lau si hiyo, binadamu asingekuwa chochote, bali lau si akili muumba asingejulikana. Kwayo tunajua utukufu wa Mwenyezi Mungu na ukubwa wa ulimwengu na ukubwa wa akili yenyewe vilevile.

Mmoja wa wenye akili anasema: “Ikiwa ulimwenguni kuna nyota zinazomeremeta, basi ndani ya akili kuna nyota inayomeremeta na kuangaza. Ikiwa vitu vinavyotuzunguka vimepangiliwa kwa ufundi, basi akili ni kuu zaidi. Ikiwa wataalamu wa falaki wanaona kuwa mpangilio wa ndani wa ulimwengu na ukuu wake ni dalili ya ukuu wa Muumbaji, basi kuweko mtu ni dalili kubwa zaidi ya ukuu wa Mwenyezi Mungu. Ikiwa kuangalia mbin- guni kunamfanya mtu ahisi upotevu wake, basi kujifikiria mtu kunamfanya ahisi ubingwa na ukuu wa aliyemuumba na kuumba ulimwengu wote.”

Ulimwengu ni mkuu na akili ni kuu. Kitu pekee cha kujua ukuu wa Mwenyezi Mungu, ulimwengu na mtu ni akili, Lakini usisahau kuwa sio mtu tu, peke yake ndiye aliyepewa akili.

3. Mtu ana sifa na siri nyingi: elimu na ujinga, dini na kufuru, mapenzi na chuki, upole na hasira, ujasiri na hofu, ukarimu na ubakhili, unyenyekevu na kiburi, uaminfu na hiyana, uthabiti na kuwa kigeugeu na mengineyo mengi yasiyokuwa na idadi. Sijui kama ametia chumvi aliyesema: “Binadamu sio kitu kimoja isipokuwa ni mamilioni ya vitu vilivyo na akili na vilivyo na wazimu, vilivyoendelea na visivyo na maendeleo.”

4. Binadamu huwa anatafuta kuishi kwenye maisha, hata kama tayari yuko katika maisha bora, atatafuta bora zaidi. Kuna Hadith isemayo: “Lau mtu angelikuwa na mlima wa dhahabu na mwingine wa fedha, basi atatamani wa tatu.” Ikiwa binadamu yuko hivyo, basi inafaa kwake pia kuwa na hamu kubwa ya kufikia kwenye utukufu zaidi.

5. Mtu ana sharia na misimamo, ambayo ni lazima aifuate na kuitumia. Ataulizwa na kuhisabiwa; na atakuwa mtukufu au mpuuzi.

6. Mtu anaathirika kwa waliopita na yeye anawathiri wajao, wakati huo huo akiathiriana na alio nao; wanamuathiri naye anawaathiri. Ndio maana akawa ana historia, turathi na athari, ambapo viumbe vingi havina.

7. Mtu ana maisha mengine, amabyo ni uwanja wa hukumu na malipo, kutokana aliyoyafanya katika maisha yake ya kwanza, na mengineyo katika neema alizoziashiria Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ﴿٣٤﴾

“Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti,” Juz;13 (14:34).

Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao. Basi atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia , basi hao watasoma kitabu chao.

Imam ni yule anayefuatwa na kufutwa amri zake, Anaweza kuwa mtu, wahyi, akili au hawaa. Kuna Hadith isemayo: “Watu wataitwa Siku ya Kiyama kwa Imam wa zama zao, kitabu cha Mola wao na sunna ya nabiiwao.”

Makusudio ya kitabu katika Aya ni kitabu cha matendo ya mtu, watu wa kuume ni watu watiifu walio wema na watu wa kushoto ni waasi walio waovu.

Maana ni kuwa mnadi atanadi siku ya Kiyama: Wako wapi wafuasi wa Mitume na wa viongozi wema? Wako wapi waliotumia akili na dini? Watakuja na watachukua kitabu cha mambo wema na thawabu zake kwa mikono yao ya kuume, wakiwa na furaha.

Vilevile atanadi mnadi: wako wapi wafuasi wa madhalimu na wasaidizi wao? Wako wapi wahaini na wafisadi? Watakuja na watachukua kitabu cha maovu na adhabu yake kwa mikono yao ya kushoto wakiwa madhalili waliohizika.

Wala hawatadhulumiwa hata chembe.

Yaani Mwenyezi Mungu atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake, hapunguzi thawabu za mwenye kufanya wema wala hazidishi adhabu ya mwenye kufanya uovu.

Na aliyekuwa kipofu katika hii, basi Akhera atakuwa kipofu na aliyepotea zaidi njia.

Katika hii, ni dunia na kipofu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule aliyezama kwenye ujinga. Wasifu wa fasaha zaidi katika hilo ni aliyoyasema Imam Ali(a.s) :

“Amepotelewa na makusudio, mwenye uchu wa maneno ya bid’a, mwenye kulingania upotevu. Yeye ni fitna ya mwenye kufitinika na ni mpotevu wa uongofu uliokuwa kabla yake, mpotezaji wa aliyemfuata katika uhai wake na baada ya kufa kwake”.

Kwa ufupi wa maana ya Aya hii ni kwamba ambaye amali yake imekuwa mbaya katika maisha haya, basi mwisho wake huko Akhera utakuwa mbaya. Vile vile Aya hii inafahamisha wazi kuwa thawabu au adhabu kati- ka Akhera inafungamana moja kwa moja na matendo katika maisha ya dunia.

Ndio maana ikasemwa: ‘Dunia ni shamba la Akhera.” Inatosha kuwa ni dalili kauli yake Mtume: “Watu watafufuliwa na niya zao.” Angalia Juz. 4 (3: 142).