9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
وَإِن كَادُوا لَيَفْتِنُونَكَ عَنِ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ لِتَفْتَرِيَ عَلَيْنَا غَيْرَهُ وَإِذًا لَّاتَّخَذُوكَ خَلِيلًا ﴿٧٣﴾
73. Na hakika walikaribia kukufitini uache tuliyokupa wahyi ili utuzulie mengine, Na hapo wangelikufanya rafiki.
وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلًا ﴿٧٤﴾
74. Lau sikukuweka imara ungelikurubia kuwaelekea kidogo.
إِذًا لَّأَذَقْنَاكَ ضِعْفَ الْحَيَاةِ وَضِعْفَ الْمَمَاتِ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ عَلَيْنَا نَصِيرًا ﴿٧٥﴾
75. Hapo basi, tungelikuonjesha maradufu ya uhai na maradufu ya mauti; kisha usingelipata wa kukunusuru nasi.
وَإِن كَادُوا لَيَسْتَفِزُّونَكَ مِنَ الْأَرْضِ لِيُخْرِجُوكَ مِنْهَا وَإِذًا لَّا يَلْبَثُونَ خِلَافَكَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٧٦﴾
76. Na kwa hakika walikaribia kukukera katika nchi ili wakutoe humo; na hapo wasingelibakia nyuma yako ila muda mchache.
سُنَّةَ مَن قَدْ أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِن رُّسُلِنَا وَلَا تَجِدُ لِسُنَّتِنَا تَحْوِيلًا ﴿٧٧﴾
77. Ndio desturi ya wale tuliowatuma kabla yako wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.
JE MTUME ANAHADAIKA NA DINI YAKE
Aya 73 -77
MAANA
Na hakika walikaribia kukufitini uache tuliyokupa wahyi ili utuzulie mengine, Na hapo wangelikufanya rafiki.
Waliokaribia ni washirikina. Walijaribu washirikiane na Mtume(s.a.w.w)
kwa kumtaka awakubalie matakwa yao na wamfanye kuwa ni kiongozi na rafiki. Miongoni mwa hayo ni kuigusa miungu yao au angalau aache kuikashifu, lakini Mtume hakuwakubalia matakwa yao washirikina, kwa sababu yeye ni maasum na maasum hawezi kuchangia dini yake na risala yake na mambo mengine.
Unaweza kuuliza
: Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘walikaribia kukufitini’ inafahamisha kuwa yeye Mtume alikaribia kuwakubalia matakwa yao?
Jibu
: Aya hii inafungamana moja kwa moja na Aya inayofuatia.
Lau sikukuweka imara ungelikurubia kuwaelekea kidogo.
Kwa hiyo maana ni kuwa, hakika wewe Muhammad lau si ulinzi wetu kwako kwa kukupa isma (kuhifadhika) ya dhambi, basi ungelikaribia kuwaelekea washirikina na kuwatikia maombi yao, Isma ndiyo iliyokuzuia kuwakubalia. Ni sawa na kusema: ‘Lau si fulani ungeliangamia’ Umetangulia mfano wake katika Juz; 12 (12: 24).
Zaidi ya hayo, kufikiria kufanya kitu ni jambo jingine na kukifanya ni jambo jingine. Kuna Hadith mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba yeye amesema: “Umeondolewa umma wangu yale yanayozungumzwa na nafsi zao madamu hawakufanya au kuzungumza,” yaani kujizungumzia mtu mwenyewe nafsini mwake, hakuna athari, Kuna mapokezi yanayosema, kuwa washirikina walipomwambia Mtume alinyamaza, hakuwajibu.
Hapo basi, tungelikuonjesha maradufu ya uhai na maradufu ya mauti.
Maana ni kuwa, ewe Muhammad! Lau ungeliwaelekea washirikina tungelikuadhibu mara mbili zaidi ya mwengine, duniani na Akhera. Kwa sababu adhabu ya wakuuu inakua kulingana na ukuu wao na cheo chao. Hii ni kiasi cha kukadiria tu, na ‘kukadiria muhali sio muhali.’
Kisha usingelipata wa kukunusuru nasi, kukukinga na adhabu.
Katika Nahju-lbalagha imeelezwa: “Siku ya Kiyama ataletwa kiongozi mkandamizaji, akiwa hana wa kumsaidi wala wa kumtolea udhuru, atatupwa katika Jahannam, azunguke humo kama pia, kisha afungwe kwenye shimo lake.”
Na kwa hakika walikaribia kukukera katika nchi ili wakutoe humo; na hapo wasingelibakia nyuma yako ila muda mchache.
Waliposhindwa washirikina na Mtume walijaribu kumkera kwa kila njia ili atoke Makka, Lau wangelimtoa, basi Mwenyezi Mungu angeliwangamiza muda kidogo baada ya kutoka kwake.
Unaweza kuuliza kuwa
: si walifanya hivyo washirikina pale walipoafikiana kumuua Mtume, mpaka akalazimika kutoka kwenda Makka kwa kuhofia, kama ilivyoelezwa katika Juz. 9 (8:30).
Jibu
: makusudio ni kuwa lau washirikina wangelimtoa wao kwa nguvu na kua ni mkimbizi aliyefukuzwa asiyejua pa kwenda, basi Mwenyezi Mungu angeliwangamiza haraka sana. Lakini Mtume alitoka Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwenda kwa watu ambao walijitolea kwake kwa hali na mali na familia.
Ndio desturi ya wale tuliowatuma kabla yako wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.
Yametangulia maelezo kuhusu hukumu ya Mwenyezi Mungu na kadha yake, kwamba kaumu yoyote itakayomtoa Mtume wao kwa nguvu, Mwenyezi Mungu anaiangamiza haraka. Na hii ndio desturi katika viumbe vyake, haibadiliki wala haigeuki, inaendela wakati wote na mahali kote.
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾
78. Simamisha Swala linapopinduka jua mpaka giza la usiku, na Qur'an ya alfajiri; hakika Qur'an ya alfajiri imekuwa ni yenye kushuhudiwa.
وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩﴾
79. Na katika usiku amka kwayo ni ziada kwa ajili yako; huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.
وَقُل رَّبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَل لِّي مِن لَّدُنكَ سُلْطَانًا نَّصِيرًا ﴿٨٠﴾
80. Na sema: Mola wangu! Niingize muuingizo mwema na nitoe kutoka kwema, na unipe madaraka kutoka kwako ya ushindi.
وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ﴿٨١﴾
81. Na sema, haki imefika na batili imetoweka. Hakika batili ni yenye kutoweka.
SIMAMISHA SWALA LINAPOPINDUKA JUA
Aya 78-81
MAANA
Aya ya kwanza na ya pili ni miongoni mwa Aya za hukumu, zilizoshuka kwa ajili ya kubainisha nyakati za Swala. Wana-Fiqh wana kauli kadhaa, kama zifuatavyo:
1.Simamisha Swala linpopinduka jua mpaka giza la usiku.
Wametofautiana katika makusudio ya kupinduka jua, Imesemekana ni wakati wa kutua jua na ikasemkena ni kupinduka nusu ya mzingo wa mbingu (meridian), na hiyo ndiyo kauli ya wengi.
Imepokewa kutoka kwa Imam Ja’far As-swadiq
kwamba giza la usiku ni nusu ya usiku.
Katika tafsiri za kisunni na kishia imeelezwa kuwa Aya hii imekusanya nyakati zote za Swala tano: Adhuhuri na Alasiri zinaingia katika kupinduka jua. Magharibi na Isha zinaingia katika giza la usiku na Asubuhi katika Qur’an ya alfajiri.
Katika Shia amesema Tabrasi kwenye Majmau-bayan: “Aya hii imeku- sanya Swala tano: Swala ya adhuhuri na alasiri zinaingia katika kupinduka jua, swala ya magharibi na isha zinaingia katika giza la usiku na makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni swala ya alfajiri; Hizi ndizo Swala tano.”
Katika sunni amesema Razi: “Simamisha Swala, yaani idumishe kuanzia wakati wa kupinduka jua mpaka giza la usiku, inaingia swala ya adhuhuri, alasiri magharibi na isha” Kisha akaendela kusema: “wamekongamana kuwa makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni Swala ya asubuhi.”
Ilivyo ni kwamba mafaqihi, katika vitabu vyao, wanaanza maneno kwa Swala ya adhuhuri kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘linapopinduka jua’ ambapo ameanzia Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa kutaja wakati wake.
Kuongezea mapokezi ya Hadith zinazoelezea kuwa adhuhuri ndiyo ya kwanza kufaradhishwa, kisha zikafuatia nyingine kwa utaratibu ulivyo. Hilo lilikuwa Makka usiku wa Israi, mwaka mmoja kabla ya Hijra (kuhamia Madina).
Madhehebu za kiislamu zimeafikiana kuwa haifai Swala kabla ya kuingia wakati wake na kwamba jua likipinduka ndio umeingia wakati wa Adhuhri, lakini wametofautiana kwenye kiwango cha muda huu, unaisha wakati gani?
Shia Imamiya wamesema kuwa mara tu bada ya kupinduka jua unahusika wakati wa Swala ya adhuhuri kwa kiasi cha kuswaliwa kwake na kiasi cha kuweza kuswaliwa swala ya alsiri mwisho wa mchana kinahusika na Swala ya alasiri. Baina ya wakati wa kwanza na wa mwisho ni wa ushirikano wa Swala mbili; yaani inaweza kuswalia adhuhuri na alasiri.
Dhahiri ya Aya iko pamoja nao: ‘linpopinduka jua mpaka giza la usiku’ wala Mwenyezi Mungu hakutenganisha; kama ilivyo kwenye madhehebu nyingine.
Wengineo wamesema kuwa wakati wa adhuhuri unaanza linapopinduka jua mpaka kuwa kivuli cha kila kitu mfano wake, ikizidi hapo wakati wa adhuhuri utakuwa umekwisha na utakuwa wakati wa alasiri umeingia. Ufafanuzi uko katika kitabu chetu: Al-fiqh ala madhahib al-khamsa (Fiqh kwenye madhehebu matano).
2.Na Qur’an ya alfajiri. Hakika Qur’an ya alfajiri imekuwa ni yenye kushuhudiwa.
Wameafikiana kwamba makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni ile inayosomwa katika Swala ya alfajiri, yaani ya asubuhi. Vil vile wameafikiana kwamba wakati wake unaanzia kutokeza alfajiri ya kweli mpaka kutoka jua (mawiyo); isipokuwa Maliki anasema kuwa asubuhi ina nyakati mbili: Ya hiyari, inaanzia alfajiri hadi kujuana nyuso. Na wakati wa dharura unaoanzia kujuana nyuso hadi kutoka jua. Kauli ya kushangaza ni ile ya masufi wanaosema kuwa makusudio ya alfajiri ni kupasuka moyo.
Wamekongamana mafaqihi, kwa ushahidi wa Tabrasi na Razi, kwamba makusudio ya yenye kushuhudiwa, ni kwamba Malaika wa usiku na mchana wanakusanyika ili washuhudie Swala. Wametegemea riwaya aliyoipokea Bukhari kutoka kwa Abu Hurayra, katika Sahih Bukhari Juzuu ya 6 mlango wa sura Bani Israil, Sisi tunaishuku riwaya hii. Na tunafasiri yenye kushuhudiwa, kuwa ni kuhudhuria hisiya. Kwa sababu mtu wakati wa asubuhi hisia zake zinakuwa zipo baada ya kupumzika na usingizi. Ndio maana ikasemwa ‘usingizi unabeba maazimio ya siku’
3.Na katika usiku amka kwayo ni ziada kwa ajili yako.
Kwayo ni hiyo Qur’an. Kwa ajili yako ni kumuhusisha yeye tu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amekufaradhishia wewe Muhammad swala nyingine, zaidi ya zile tano ambazo ni zako na wengine, uiswali usiku. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ ﴿١﴾ قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٢﴾
“Ewe mwenye kujifunika nguo! Simama usiku isipokuwa kidogo” (73:1-2)
وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا ﴿٢٦﴾
“ Na usiku umsujudie Yeye na umtakase usiku mrefu.” (76:26).
Swala hii inaitwa Swala ya usiku (swalatu-llayl); wakati wake ni kuanzia nusu ya usiku hadi alfajiri. Ni wajibu kwa Mtume(s.a.w.w)
, kama tulivyoeleza mwanzo na ni sunna kwa mwenginewe.
Huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.
Huenda ni neno la kutarajia ikiwa linatoka kwa kiumbe na ni la mkato ikiwa linatoka kwa muumbaji, Hapa anaambiwa Muhammad(s.a.w.w)
.
Hakuna kitu zaidi ya Muhammad wala cheo zaidi ya Muhammad na kizazi zaidi ya kizazi cha Muhammad; isipokuwa yule ambaye hakuna mfano wake kitu chochote. Kuna Hadithi isemayo kuwa Mtume(s.a.w.w)
alifasiri cheo chenye kusifika katika Aya hii kuwa ni cheo atakachowaombea umma wake kesho.
Na sema: Mola wangu! Niingize muuingizo mwema na nitoe kutoka kwema.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu kuomba dua hii. Kuingia kwema na kutoka kwema ni fumbo la haki na ikhlsi katika itikadi, makusudio, vitendo, harakati zote na kupumzika. Hakuna shaka kuwa mwenye kuwa na silaha ya haki na akamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake, basi atamuimarisha kwa kauli thabiti, atampa hoja imara na umakini wa moyo ulio mwema na safi.
Na unipe madaraka kutoka kwako ya ushindi.
Kuna ushindi na madaraka yanayozidi kutajwa Mtume mtukufu pamoja na jina la Mwenyezi Mungu mara tano kwa siku, katika adhana na katika swala za wajibu na sunna? Kuna nguvu gani na heshima adhimu kuliko ile aliyompa Muhammad, aliposema:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ﴿٧﴾
“Anachowapa Mtume kichukueni na anachowakataza kiacheni,” (59:7).
Na sema haki imefika na batili imetoweka. Hakika batili ni yenye kutoweka.
Haki ni risala ya Muhammad, itikadi na sharia. Vinginevyo ni batili, kiuhalisi na mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama vitaaminiwa na watu wa ardhini wote. Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya batili hapa ni ushirikina na kwamba Mtume(s.a.w.w)
alipoikomboa Makka aliingia Al- ka’ba na mlikuwa na masanamu 360, akawa anazisukuma huku akisema: “Haki imefika na batili imetoweka, Hakika batili ni yenye kutoweka.”
NGUVU YA HAKI NA NGUVU YA BATILI
Unaweza kuuliza
: Mara nyingi tunaona na kushuhudia watu wa batili wakishinda na watu wa haki wakishindwa. Hii si inapingana na kauli ya Mwenyezi Mungu ‘Hakika batili ni yenye kutoweka’?
Jibu
: Hakika haki ina nguvu za dhati zisizoepukana nazo kwa hali yoyote; nazo zinatenda kazi na kuathiri kwenye nyoyo safi zilizo takatifu. Mara nyingi athari hii inafikia kiwango ambacho hakuna nguvu yote yote inayoweza kuisimamisha; si mapanga ya wachinjaji wala unyongaji wa mataghuti.
Historia inatusimilia jinsi mashahidi wa itikadi walivyojitolea kuwa mashahidi kwa nyuso za kutabasamu na nafsi zilizo radhi; bali hayo yametokea wakati wetu huu huko Vietnam, Korea, Palestina na kwengineko.
Ndio! Ni kweli hawa ni wachache; kama ilivyo kawaida ya kila jambo tukufu lenye thamani. Lakini wangelikuwa wengi kwa idadi au wengi kwa viwango vya asilimia, basi dunia ingelijaa uadilifu, na dhulma na jeuri isengelikuwa na athari yoyote. Sisi hatuna shaka ubinadamu utakwenda na njia hii; hata kama muda utakuwa mrefu.
Ama batili, haina nguvu wala urefu, isipokuwa kuweko kwake kunategema rushwa, dhulma, ukandamizaji, kuwafukuza watu njama n.k.
Haya yote yataondoka kadiri siku zinavyokwenda na hali kubadilika. Ama nguvu ya haki huwa inakwenda na wakati, inabakia hivyo hivyo tu wakati wote. Kwa sababu inategema hiyo haki yenyewe, kama ilivyo. Kwa ajili hii ndio tunasema tena: Sisi tuna imani isiyokuwa na shaka kwamba mwisho ni wa haki na neno la juu litakuwa la haki peke yake.
وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾
82. Na tunateremsha katika Qur’an ambayo ni ponyo na rehema; Wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa hasara.
وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ كَانَ يَئُوسًا ﴿٨٣﴾
83. Na tunapomneemesha mtu hugeuka na kujitenga kando na inapomgusa shari hukata tamaa.
قُلْ كُلٌّ يَعْمَلُ عَلَىٰ شَاكِلَتِهِ فَرَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَنْ هُوَ أَهْدَىٰ سَبِيلًا ﴿٨٤﴾
84. Sema: kila mmoja anafanya kwa namna yake, Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia.
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾
85. Wanakuuliza kuhusu roho, Sema: roho inatokana na amri ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.
QUR’ANI NI PONYO
Aya 82-85
MAANA
Na tunateremsha katika Qur’an ambayo ni ponyo na rehema.
Qur’an ni rehema kwa yule anayeitakia nafsi yake rehema na ni ponyo la ukafiri, ulahidi, ujinga, ufisadi na kila uchafu, kwa yule mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na haki.
Imam Ali
katika kuisifu Qur’an ansema:“Hakika hiyo ni kamba imara, nuru inayobainisha, ni dawa yenye kuleta nafuu, ni kichujio cha takataka, ni hifadhi kwa mwenye kushikamana nayo na ni uokovu kwa mwenye kufungamana nayo.”
Mwenye kuhalifu hukumu miongoni mwa hukumu za Qur’an atakuwa miongoni mwa madhalimu na waliohasirika.
Wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa hasara.
Qur’an ni rehema kwa waumini na nakama kwa madhalimu na wafisadi, kwa sababu kila wanapoasi hukumu miongoni mwa hukumu zake, wanazidi dhambi na adhabu.
Na tunapomneemesha mtu hugeuka na kujitenga kando na inapomgusa shari hukata tamaa.
Maana ya Aya hii yanafupilizwa na kauli ya Imam Ali
katika wasifu wa mtu: “Akijitosheleza huchangamka na kushawishika na anapofukarika hukata tamaa na kubweteka. Umepita mfano wake katika Juz; 11 (10:12) na Juz. 12 (11: 9).
Sema: kila mmoja anafanya kwa namna yake, Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia.
Wafasiri wamesema: “Namna, ni njia. Na maana ya Aya ni kuwa kila mmoja kati ya mumin na kafiri anafanya kwa njia yake na maumbile yake” lakini sisi tutaifafanua, kama tulivyoifahamu, katika hali zifuatazo:
1. Neno kila mmoja linafahamisha kuenea kwa mtu mmoja mmoja; kwa mfano ukisema: kila mtu analifahamu hili, ni kama umesema: Zayd analifahamu na Bakari, Hindu n.k. (yaani kila mmoja ana namna yake ya kulifahamu) Lakini ukisema: watu wote wanalifahamu, itakuwa kadhia ni moja na hukumu itakuwa imewaenea kwa ujumla sio kwa mtu mmoja mmoja. Kwa hiyo maana ya Aya ni kuwa kila mmoja katika watu ana namna yake inayomuhusu yeye peke yake; kama vile alama za vidole, kila mmoja ana zake.
2. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ja’far As-swadiq
kwamba yeye amefasiri namna kwa maana ya nia. Usahihi wa tafsiri hii unafahamika kutoka na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia’ iliyokuja moja kwa moja bila ya kuweko kiunganishi kingine.” Yaani Mwenyezi Mungu anamjua anayetaka kuongoka na kufu- ata njia yake bila ya makusudio mengine yoyote isipokuwa dhati yake Aliye Mtukufu.
Kwa hiyo maana ya Aya yatakuwa: Kila mtu anafanya kulingana na nia yake na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atapambana naye kulingana na nia yake; ikiwa kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi itakuwa ni shari.
Mwenye kudhihirisha kheri mbele ya watu ili awahadae watu na kumbe ana malengo ya shari, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni mshari. Na mwenye kuiba mkate ili ajisitiri njaa baada ya kukosa budi, akiwa hana njia nyingine, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu hastahiki adhabu.
ROHO INATOKANA NA AMRI YA MOLA WANGU
Wanakuuliza kuhusu roho, Sema: roho inatokana na amri ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.
Roho ina maana nyingi. Makusudio yake hapa ni uhai. Mtume(s.a.w.w)
aliulizwa kuhusu roho, Mwenyezi Mungu akamwamrisha amwambie muulizaji kuwa roho ni katika vitu vinavyopatikana kwa amri ya Mungu ambayo ni kusema ‘Kuwa na ikawa.’
Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa vitu viko aina mbili: Aina ya kwanza, Mwenyezi Mungu anavileta kupitia sababu za kimaumbile kutokana na maada; kama mwili wa binadamu.
Aina ya pili ni ile inayopatikana kwa kiasi cha amri tu; ambayo ni neno ‘kuwa’ Na roho ni katika aina hiyo. Aya imeliweka wazi hilo, Kwa sababu neno: ‘roho inatokana na amri ya Mola wangu,’ ni ishara ya neno ‘amri’ lilioko katika kauli yake nyingine Mwenyezi Mungu:
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾
“Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia kuwa! Na kikawa,” (36:82).
Majaribio yamethibitisha hakika hii na wakaiamini wale waliobobea na kumaliza miaka mingi kwenye utafiti wa asili ya uhai. Waliamni hakika hii baada ya kubainika kwamba sababu ya moja kwa moja ya uhai haina muungano wowote wa kuishia kwenye maada. Lau ingelikuwa inaishia kwenye maada, wangeliweza kumtengeneza binadamu kwenye viwanda vyao na maabara yao.
Wamejaribu wakashindwa: “Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” Yaani kadiri viwanda vyenu vinavyotengeneza vitu vya ajabu, lakini si chochote kulingana na chembe hai za nzi, sikwambii nzi mwenyewe: “Enyi watu! Umepigwa mfano, basi usikilizeni, Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawataumba hata nzi, wajapojumuika kwa hilo, Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kutoka kwake.
ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾
Amedhoofika huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa,”(22:73)
Umepita mfano wake katika Juz; 9 ( 6:95).
MWENYEZI MUNGU NA ELIMU YA CHEMBE HAI
Imetokea sadfa, wakati nikifasiri Aya hii, nikasoma makala katika gazeti Ruzil Yusuf la Misri
toleo la April 1969 likiwa na maelzo haya:
“Mwili wa mtu una mamilioni ya chembe hai ambazo haziwezi kuonekana isipokuwa kwa darubini. Katika miaka ya karibuni ilikuwa ni vigumu kuweka elimu ya chembe kwa sababu wataalamu walikuwa hawawezi kuz- ifungua hizo chembe au kuzidunga sindano. Kwa vile kazi ilikuwa inahi- taji chombo kidogo kuliko milimita elfu moja, basi sindano nayo ingelihi- tajika iwe na ncha ndogo kuliko milimita milioni moja.
Hatimae walifanikiwa wataalamu kuzifungua chembe hizo kupitia mwanga, sawa na tunavyowasha sigara kutokana na mwanga wa jua kupitia kioo. Ni njia pekee iliyowawezesha wataalamu kuzifungua chembe hai na kugundua kuwa ni mkusanyiko uliosheheni makumi ya viumbe mbalimbali, kila kimoja kikiwa na sifa yake maalum na kazi yake na mfungamano ulionacho pamoja na wakazi wengine wa chembe hizo.
Kuweza kufahamu kazi hizo na mifungamano hiyo, kutahitajia miaka ya utafiti kama sio vizazi. Ndio ikaanza elimu ya chembe hai na tukawa sasa tunajua kwamba chembe hai zina mwili na viungo, utando, nyuzi na mengineyo ya kushangaza akili.
Imedhihirika kwamba chembe hai za damu ni mkusanyiko wa chembe zinazoelea. Idadi yake ni mara kumi zaidi ya watu wote. Mkusanyiko huo unatengeneza chembe nyingine kila baada ya miezi mine na kuhifadhi idadi ya chembe nyingine, kiasi ambacho zile zinazokuja hazipungui wala kuzidi zile zilizoondoka. Wala hazina matatizo ya makazi kwa sababu ya wingi, kama ilivyo kwa watu.
Hapa ndio kuna maajabu! Ubongo wa mifupa uzalishe mikondo ya damu ya aina na iliyo na kazi tofauti tofauti yenye chembe nyekundu na nyeupe zinazoua na zinazokinga, Vipi basi jinsi moja ilete jinsi nyingi tofauti tofauti? Kwani ngamia anaweza kuzaa ndovu, tena azae mamba, kisha azae kicheche? Lakini kwenye damu linapatikana hilo. Haya ni maajabu kweli! Kwa ufupi kabisa ni kwamba chembe hai hivi sasa zimekuwa ndio gumzo kubwa la utafiti wa kisayansi na njia yake mpya; pengine ni njia pekee ya kufahamu siri za uhai.”
Umeona maajabu haya! Kiumbe kidogo ambacho hakiwezi kuonekana isipokuwa kwa kukuzwa mara elfu, tena hakiwezi kupasuliwa ila kwa mwangaza, unywele kwake ni kama ndovu aliye kwenye chungu chungu.
Pamoja na yote haya, kiumbe hiki kina viungo, mishipa, utando na mengineyo; kama mwanadamu. Kisha viumbe hivi, vya ajabu, vinafanya maskani yake ndani ya mwili wa mtu, vikiwa ni mamilioni, kwa kiasi cha miezi mine kisha vinakuja vingine kwa idadi ile ile ya vile vilivyoondoka bila ya kuzidi wala kupungua; kisha vingine na vingine na kuendelea.
Je, hii yote ni sadfa? Je, sadfa inaweza kukaririka mara bilioni. Je, viungo vyote hivyo, utando na nyuzi zilizofumwa kwa nidhamu na mpangilio ni sadfa?
Je sadfa inaweza kuzalisha vitu vya aina mbali mbali kutoka katika aina moja? Maswali yote haya na mengineyo yanataka jawabu.
Hapana! Tena hapana kabisa! Hakuna tafsiri ila kuweko Mjuzi mwenye uweza wa kuumba ulimwengu na uhai kwa neno ‘Kuwa’ na ikawa.
Baada ya hayo, kila sayansi inavyozidi kupiga hatua, ndio dalili na ushahi- di wa kuweko Muumba mwenye amri, unazidi. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu, aliyesema: “Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu”.