11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَىٰ تِسْعَ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ فَاسْأَلْ بَنِي إِسْرَائِيلَ إِذْ جَاءَهُمْ فَقَالَ لَهُ فِرْعَوْنُ إِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا مُوسَىٰ مَسْحُورًا ﴿١٠١﴾
101. Hakika tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize wana wa Israil; alipowajia na firauni akamwambia: Hakika mimi nakuona wewe umerogwa.
قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ بَصَائِرَ وَإِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا فِرْعَوْنُ مَثْبُورًا ﴿١٠٢﴾
102. Akasema: Hakika umekwishajua kuwa hakuziteremsha hizi isipokuwa Mola wa mbingu na Ardhi, kuwa ni dalili. Hakika mimi nakuona, ewe firauni, umeangamia.
فَأَرَادَ أَن يَسْتَفِزَّهُم مِّنَ الْأَرْضِ فَأَغْرَقْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ جَمِيعًا ﴿١٠٣﴾
103. Na akataka kuwahamisha katika ardhi, Tukamzamisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.
وَقُلْنَا مِن بَعْدِهِ لِبَنِي إِسْرَائِيلَ اسْكُنُوا الْأَرْضَ فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ جِئْنَا بِكُمْ لَفِيفًا ﴿١٠٤﴾
104. Na tukawaambia, baada yake, wana wa Israil: kaeni katika ardhi, Na itakapokuja ahadi ya Akhera tutawaleta nyote pamoja.
TULIMPA MUSA ISHARA TISA
Aya 101 – 104
MAANA
Hakika tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi.
Yamewishatangulia maelezo, katika Aya kadhaa, kuhusu Musa
na watu wake na miujiza yake na pia kuhusu Firauni na wakuu wake na utaghuti wake.
Inawezekana kuwa mnasaba wa kutajwa miujiza ya Musa hapa, ni kuwa Mwenyezi Mungu alipotaja mapendekezo ya washirikina kwa Muhammad(s.a.w.w)
, alifuatishia kuonyesha mapendekzo ya Firauni kwa Musa na matokeo yake yakawa ni balaa kwake; kwamba itatokea hivyo hivyo, lau Mwenyezi Mungu atajibu mapendekezo ya washirikina kwa Muhammad(s.a.w.w)
.
Kwa sababu wao watayakataa yatakapowajia; sawa na walivyofanya watu wa Firauni na wangeliangamia kama alivyoangamia Firauni. Kwa hiyo kukosa kujibiwa ni heri kwao na Mwenyezi Mungu anajua yanayowafaa waja na yale ya kuwaharibia.
Musa ana ishara na miujiza mingi, ikiwemo ile ya kuifanya risala yake iwe nyepesi; kama vile kuondoka mifundo ya ulimi wake, kuneemeshwa na kufadhilishwa wana wa Israil kwa kutolewa maji katika jiwe, kuteremshiwa manna na salwa au kuhofishwa kwa kufunikwa na mlima. Mingine ni ya kumpa fundishoFirauni na watu wake ili waweze kuamini au malipo ya inadi yao.
Hiyo ndiyo miujiza tisa iliyoashiriwa na Aya. Iliyo dhahiri zaidi ni kugeuka fimbo kuwa nyoka, mkono kuwa mweupe na kuangamizwa makafiri baharini. Ama sita iliyobakia, mitano yake imeashiriwa na Aya hii:
فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿١٣٣﴾
“Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu” Juz; 9 (7:133)
Na wa sita ni kuangamizwa mali zao: “Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanawapoteza watu na njia yako.
Mola wetu! Ziangamize mali zao na zitie shida nyoyo zao, Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza. Akasema Mwenyezi Mungu, maombi yenu yamekubaliwa. Basi muwe na msimamo wala msifuate njia ya wale wasiojua.” Juz; 11 (10:88-89).
Waulize wana wa Israil
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
. Makusudio ya wana wa israili ni wale walioamini; kama vile Abdullah bin Salam na maswahiba zake. Lengo la swali hili na jawabu ni kuwadhihirishia mayahudi na wasiokuwa mayahudi ukweli wa Mtume mtukufu kwa kila alilowaletea kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Alipowajia na Firauni akamwambia: Hakika mimi nakuona wewe umerogwa.
Yaani umchawi, kwa maana ya kuwa umepewa elimu ya uchawi, kwa dalili ya Aya nyingine isemayo: “Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.” Juz; 9 (7:109). Walisema hivyo baada ya kushuhudia fimbo inageuka kuwa nyoka mkubwa na mkono rangi ya maji ya kunde kuwa mweupe bila ya ubaya.
Akasema; hakika umekwishajua kuwa hakuziteremsha hizi isipokuwa Mola wa mbingu na Ardhi, kuwa ni dalili. Hakika mimi nakuona, ewe firauni, umeangamia.
Makusudio ya ‘hizi’ ni ishara tisa.
Firauni alipomwambia Musa, mimi nakuona u mchawi, Musa alimjibu kuwa unajua kwa hakika ukweli wa ishara na niliyokuletea na kwamba hizo ni dalili wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zinazokuonyesha wewe na watu wote kuwa mimi ni mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini wewe unafanya inadi na kiburi kwa ajili ya kupupia cheo chako.
Ikiwa wewe unaniona kuwa mimi ni mchawi basi mimi ninakuona wewe umeangamia; na hayo ni malipo ya kukadhibisha kwako haki na atakayekuwako ataona. Kila mwenye kuipinga haki na akaona uzito kuambiwa basi huyo ni mwanachama wa Firauni na mila yake.
Na akataka kuwahamisha katika ardhi.
Aliyetaka kuwatoa ni Firauni, na waliotakiwa kutolewa ni Musa na watu wake. Maana ni kuwa Firauni alitaka ardhi ya Misri isikaliwe na Wana wa israil kwa kuwaua, kuwachukua mateka na kuwafukuza. Lakini janga likamgeukia yeye, kama inavyokuwa kwa kila taghuti.
Tukamzamisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.
Mwenyezi Mungu aliwangamiza baada ya kuwapatia hoja na dalili wazi, lakini wakakataa isipokuwa ukafiri na kupetuka mipaka.
Na tukawaambia, baada yake, wana wa Israil: kaeni katika ardhi.
Ardhi iliwakunjukia wana wa Israil, baada ya kupata amani kwa kuangamia Firauni, Mwenyezi Mungu akawapa hiyari ya kukaaa popote katika nchi. Ilitakikana washukuru Mungu kwa neema hii, lakini wao wakapetuka mipaka na wakafanya uovu:
Wakaabudu ndama badala ya Mwenyezi Mungu, wakasema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumbwa na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu ni fukara na wao ni matajiri, wakawaua mitume, wakala haramu na riba, wakaipotoa Tawrat, wakajaribu kumuua Bwana Masih, na kumzulia mama yake uovu na mengineyo aliyoyasajili Mwenyezi Mungu katika Tawrat, Injili na Qur’an na watu wakayasajili katika vitabu vya historia na vya Hadith vya zamani na vya sasa. Uzayuni unatosha kuwa ni ushahidi wa hakika ya kikundi hiki kiovu na kwamba hicho ni shari na balaa kwa ubinadamu.
Na itakapokuja ahadi ya Akhera tutawaleta nyote pamoja.
Maneno hapa wanaambiwa wana wa Israil na akhera ni Siku ya Kiyama, kuletwa pamoja ni mkusanyiko wa wanaotofautiana. Makusudio ni kutoa hadhari na kiaga kwa wale watakokuja katika wana wa Israil kuleteta fitina na ufisadi katika nchi.
Hii ndio dhahiri ya tamko la Aya, Lau ingelikuwa inafaa kufasiri Qur’an kwa maoni yetu, basi tungelisema kuwa neno ‘kuletwa pamoja’ linaashiria kujumuika mayahudi na uzayuni, kutoka huko na huko, katika ardhi ya Palestina na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawasalitia uovu mkali na itakuwa ni ahadi itakayotimizwa. Usawa ni tuliyoyaelezea katika Aya ya 4 ya sura hii, rudia huko.
وَبِالْحَقِّ أَنزَلْنَاهُ وَبِالْحَقِّ نَزَلَ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿١٠٥﴾
105. Na kwa haki tumeiteremsha na kwa haki imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.
وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا ﴿١٠٦﴾
106. Na Qur’an tumeigawanya ili uwasomee watu kwa kituo; na tumeiteremsha kidogo kidogo.
قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا ﴿١٠٧﴾
107. Sema, iaminini au msiiamini. Hakika wale waliopewa ilimu kabla yake, wanaposomewa, huanguka kifudifudi wanasujudu.
وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِن كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولًا ﴿١٠٨﴾
108. Na wanasema: Ametakasika Mola wetu, Hakika ahadi ya Mola wetu lazima itimizwe.
وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ﴿١٠٩﴾
109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidishia unyenyekevu.
قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ وَلَا تَجْهَرْ بِصَلَاتِكَ وَلَا تُخَافِتْ بِهَا وَابْتَغِ بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا ﴿١١٠﴾
110. Sema, mwiteni Mwenyezi Mungu (Allah) au mwiteni Mwingi wa rehema (Rahman), kwa jina lolote mtakalomwita, Yeye ana majina mazuri. Wala usiisome jahara Swala yako wala usiifiche, bali tafuta njia baina ya hizo.
وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾
111. Na sema, sifa njema zote ni za ambaye hakujifanyia mtoto wala hana mshirika katika ufalme, wala hana msaidizi kwa sababu ya udhaifu na mtukuze kwa matukuzo makubwa.
KWA HAKI TUMEITEREMSHA
Aya 105 – 111
MAANA
Na kwa haki tumeiteremsha na kwa haki imeteremka.
Wafasiri wana kauli nyingi katika jumla mbili hizi; Yenye nguvu zaidi ni ile aliyoisema Tabrasi na Razi. Kwa ufupi wa kauli yao ni kuwa makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Na kwa haki tumeitremsha’, ni kwamba Qur’an imedhamini haki na makusudio ya ‘Na kwa haki imeteremka’ ni kwamba Mwenyezi Mungu kwa kuiteremsha Qur’an alitaka watu waiamini na waitumie. Hilo lilipatikana kwa hakika; ambapo waislamu waliiamini na wakaitumia wale wenye ikhlasi.
Sisi tuko pamoja na Razi na Tabrasi katika kufasiri jumla ya kwanza. Ama jumla ya pili, tuonavyo sisi ni kuwa kila walilokuwa nalo watu kabla ya kuteremshwa Qur’an na watakalokuwa nalo baada ya kuetremshwa, basi Qur’an inalikubali ikiwa ni la haki, kheri na masilahi.
Kwa maneno mengine ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kusema katika jumla ya kwanza kuwa ameiteremsha Qur’an kwa haki kheri na masilahi, katika jumla ya pili anasema pia Qur’an inakubaliana na kila lililo haki lenye kheri na masilahi wakati wowote litakapokuwa, kabla au baad aya Qur’an.
Kuna Aya zilizo na maana ya tafsiri hii; kama vile:
وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ ﴿١٧﴾
“Ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi” Juz.13 (13:17)
يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ ﴿١٨٥﴾
“Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi wala hawatakii yaliyo mazito” Juz;2 (2:185).
Imam Ja’far As-swadiq
naye amesema:“Kila lenye masilahi kwa watu kwa namna moja au nyingine, basi linajuzu.”
Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.
Umbashirie Pepo mtiifu na umonye na moto muasi. Baada ya hapo anayetaka aamini na anayetaka na akufuru.
إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ مَن يَضِلُّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿١١٧﴾
“Hakika Mola wako anawajua vyema wanaopotea njia yake na anawajua sana wanaoongoka,” Juz;8 (6:117).
JE, QUR’ANI ILISHUKA KIDOGO KIDOGO?
Na Qur’an tumeigawanya ili uwasomee watu kwa kituo.
Qur’an haikuteremka kwa Muhammad kwa mpigo; bali iliteremka kidogo kidogo, ikifiuatana na mara nyingine ikichelewa kulingana na masilahi na matukio ambayo huzuka mara kwa mara. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾
“Hakika tumeitermsha Qur’an katika laylatul-qadr (usiku wa heshima),” (97:1).
Maana yake ni kuwa ilianza kuteremshwa usiku huo, kisha ikaendelea hadi kufa Mtume(s.a.w.w)
na kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kushuka kwake ilikuwa ni miaka ishirini na tatu.
Mwenyezi Mungu amebainisha lengo la kufanya hivyo kwa kusema: ‘ili uwasomee watu kwa kituo;’ yaani kutoa muda ili iwe rahisi kuifahamu na kuihifadhi.
Aya hii ni dalili wazi ya kumkosoa anayesema kuwa Qur’an imeshuka kwa mara moja yote na mtume akaifikisha kidogo kidogo. Mwenyezi Mungu amemrudi mwenye kusema hivi kwa kauli yake: “Na wakasema wale waliokufuru: kwa nini hakuteremshiwa Qur’an kwa jumla moja?” (25: 32) Yaani moyo wako uweze kuwa na nguvu kuweza kufahamu maana ya Qur’an na siri zake.
Zaidi ya hayo kuna Aya kadhaa zinazosimulia visa na matukio yaliyojitokeza upya au kubainisha hukumu yake; kama vile kisa cha Badr, Uhud, Ahzab na Hunayn. Pia kisa cha Wakiristo wa Najrani na mayahudi wa Madina. Vile vile tukio la wake wa Mtume, mwanamke aliyemjadili Mtume kuhusu mumewe na mengineyo.
Amesema Sheikh Mufid: “Qur’an imeshuka kwa sababu na matukio kwa hali baada ya hali. Hilo linafahmika kutokana na dhahiri ya Qur’an, Hadith mutawatr na kongamano la maulama.”
Na tumeitermsha kidogo kidogo.
Jumla hii ni tafsiri na ubainifu wa yaliyo kabla yake.
Sema: iaminini au msiamini. Hakika wale waliopewa ilimu kabla yake, wanaposomewa, huanguka kifudifudi wanasujudu. Na wanasema: Ametakasika Mola wetu, Hakika ahadi ya Mola wetu lazima itimizwe. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidishia unyenyekevu.
Kabla yake, ni kabla ya Qur’an. Wanaoambiwa ni washirikina ambao walimwekea masharti Muhammad(s.a.w.w)
ya kumwamini; kama ilivyoelezwa katika Aya ya 9 ya Sura hii. Kuanguka kifudifudi ni kusujudu kwa uso. Kumetajwa kusujudu mara mbili, kwa sababu kwa kwanza ni kwa ajili ya kumwadhimisha Mwenyezi Mungu na kwa pili ni kwa kuathrika na Qur’an katika nafsi zao.
Wale ambao wamepewa elimu kabla ya Qur’an ni wale waloiangalia haki katika watu wa Kitabu ambao walimwamini Muhammad(s.a.w.w)
na wenye maumbile safi, kama wale tutakaowadokeza katika kifungu kinachofuatia.
WANYOOFU
Mnyoofu ni yule aliyeacha batili na kufuata haki na njia yenye kunyooka. Wakati wa Jahiliya kulikuwa na watu waliopetuka mazingira yao, na kwa mamubile yao safi waliweza kutambua kwamba kuna muumba mmoja mwenye uwezo wa ulimwengu huu na kwamba baada ya mauti kuna ufu- fuo, hisabu, adhabu na thawabu.
Vile vile kwamba kuabudu masanamu ni ujinga na upotevu. Kuna baadhi ya shairi zao katika kitabu Al-aghani Juzuu ya 3 na Sirat ibn Hisham, Juzuu ya 1. Chapa ya mwak 1936:
• Je, ni Mungu mmoja au elfu miungu?
• Ni dini iliyokioja iliyogawanyika mafungu
• Lakini namuabudi Mola wangu Rahamani
• Anisamehe zangu dhambi Mola ghafuri manani
• Tawaona watu wema makazi yao Peponi
• Na makafiri madhalima kwenye sairi Motoni
Ibn Hisham anasema katika Juzuu ya 1 ya As-siratun-nabawiyya: “Walikusanyika makuraishi katika Idd yao ya masanamu waliyokuwa wakiyaadhimisha, wakajitoa watu wane ambao ni: Waraqa bin Nawfal, Abdallah bin Jahsh, Uthman bin Alhuwayrith na Zayd bin Amr. Wakaambiana: Wallah hawa watu wenu hawana chochote, wameikosea dini ya baba yao Ibrahim! Nini haya mawe tunayozungukia, hayasikii, hayaoni, hayadhuru wala hayanufaishi!
Zayd hakuingia kwenye uyahudi wala unaswara (ukiristo), Aliacha dini ya watu wake kwa kujiepusha na masanamu, mfu, damu na dhabihu zilizokuwa zikitolewa kwa masanamu. Akakataza kuwaua watoto wa kike na akawa anamwambia baba yake: “Usimuue mimi nitamgharimia malezi yake.”
Alikuwa akijasiri kuwaambia watu wake na kuwakosoa huku akiwaambia: “Mimi ninamwabudu Mola wa Ibrahim. Ewe Mola wangu! Lau ningejua namna inayopendeza zaidi ya kukuabudu ningeliifanya; lakini siiju, Kisha anasujudi kwenye kiganja chake.
Zayd aliendela kuwasafihi maquraishi na ibada yao. Walipoona ni hatari walimtaka ami yake Khattwab, baba wa Umar bin, Alkhattab amzuie na amkataze, naye akamkataza. Lakini Zayd bado aliendelea na mwito wake. Al-Khattab akawa anawatuma vijana wahuni wa Kikuraishi, akiwemo mtoto wake Umar, kumzuia asiingie Makka, Zaidi akawa anapenye Kisiri.
Walipofahamu walimwambia al-Khattab na wakawa wanamfukuza na kumwudhi kwa sababu ya kuogopa kwao asije akawavutia watu kwenye dini yake, Baadaye Zaid akatoka kutafuta dini ya Ibrahim
. Akawa anahangaika huku na huko katika nchi mbalimbali. Hata hivyo alipokanyaga nchi ya Lakhm, alishambuliwa na kuuawa. Rafiki yake Waraqa alimlilia na kumtungia mashairi haya:
• Hakika bin Amri meongozwa kwa wema
• Mejiepusha na tanuri ya moto unaochoma
• Me mwabudu adhimu Mola aso mithili
• Ukaiacha mizimu ya matwaghuti jahili
• Rehema za Mola wake kiumbe humfikia
• Hata chini ajizike bonde sabini kungia
Zaidi aliuawa kabla ya kutumwa Mtume Muhammad(s.a.w.w)
, lakini mtoto wake alimwamini Mtume(s.a.w.w)
Yeye pamoja Umar bin al-Khattab, ambaye alikuwa ni binamu yake, walimwendea Mtume na kumwuliza: Tunaweza kumuomba Mwenyezi Mungu amsamehe Zaid bin Amr?” Mtume alijibu: “Ndiyo. Yeye atafufuliwa kama mwakilishi pekee wa jamaa zake.”
Abdallah bin Jahsh, alibakia mpaka ukaja Uislamu, akasilimu na akahama yeye na mkewe, Ummu Habiba bint Abi Sufyan, kwenda Habasha (Ethiopia), akafia huko baada ya kurtadi kwa kuingia kwenye dini ya unaswara (ukiristo) Baadae Mtume akamuo Ummu Habiba.
Uthman bin Huwayrith, alikwenda kwa Kaizari mfalme wa Roma na akawa Mnaswara, huko alipewa cheo kikubwa na akafa Sham. Waraqa aliingia dini ya unaswara (ukristo) na akasoma vitabu vitakatifu vya dini hiyo mpaka akavifahamu barabara. Aliishi Makka, kama mtawa, akiwakataza watu wake kuabudu masanamu.
Warqa alikuwa ni binamu wa Khadija, mke wa Mtume(s.a.w.w)
. Uliposhuka wahyi kwa mtume alikwenda naye kwa binamu yake huyo. Akamuuliza, ewe mwana wa ndugu yangu, unaona nini? Mtume alipomwambia akasema: “Huyo ndiye Malaika Mkuu amabye aliwashukia Musa, Natamani ningekuwa kijana, natamani niwe hai wakati watu wako watakapokutoa. Mtume akasema: Hivi watanitoa? Akasema ndio! Hakuna mtu yeyote kabisa aliyekuja na mfano wa jambo lako ila hufanyiwa uadui. Kama nikiwahi siku hiyo nitakusaidia sana!
Waraqa alitamka kwa wahyi wa umbile lake safi, “Ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu” Kila mtu atakayerejea kwenye umbile lake hili atamwamini Muhammd(s.a.w.w)
na atamsaidia kwa sababu “Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu, Hiyo ndiyo dini iliyo sawasawa, Lakini watu wengi hawajui.” (30:30).
Sema, mwiteni Mwenyezi Mungu (Allah) au mwiteni Mwingi wa rehe- ma (Rahman), kwa jina lolote mtakalomwita, Yeye ana majina mazuri.
Washirikina walikuwa na masanamu mbalimbali, wakiyaita kwa majina ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalii yoyote.
Katika majina hayo hakukuwa na jina la Rahman. Kwa hiyo Mtume alipowalingania kumwabudu Rahman ndio wakasema, ni nani huyo Rahman? “Na wanapoambiwa msujudieni mwingi wa rehema (Rahman) wao husema: Ni nani huyo mwingi wa rehma? Je,tumsujudie unayetuamrisha wewe?” (25:60) Yaani ni wasifu gani huu ambao hauna athari yoyote kwa waungu wetu?
Kauli yake Mwenyezi Mungu: Sema, mwiteni Mwenyezi Mungu (Allah) au mwiteni Mwingi wa rehema (Rahman) ni jawabu tosha la upinzani wao.
Kwa sababu maana yake ni kwamba majina na matamshi ni nyenzo tu ya ibara. La kuzingatia ni yule anayeitwa. Mwiteni mtakavyo katika majina yake, yote ni mazuri; Kwa sababu yanaleta ibara ya maana nzuri nayo yako sawasawa katika uzuri.
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ﴿١٨٠﴾
“Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri,” Juz; 9 (7:180).
Kwenye Juzuu hiyo ya 9, tumefafanua zaidi katika kifungu cha ‘Je, majina ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo au yana kiasi.’
Wala usiisome jahara Swala yako wala usiifiche, bali tafuta njia baina ya hizo.
Makusudio ya jahara kwenye Swala ni kusoma kwa sauti kubwa na kuficha ni kusoma kwa sauti ndogo. Imam Jafar Asswadiq
anasema katika kufasiri Aya hii: “Jahara ni kuinua sauti na kuficha ni kiasi ambacho masikio yako hayasikii. Na soma kisomo kilicho baina yake”
Na sema: sifa njema zote ni za ambaye hakujifanyia mtoto wala hana mshirika katika ufalme, wala hana msaidizi kwa sababu ya udhaifu, na mtukuze kwa matukuzo makubwa.
Tunamuhimidi Mwenyezi Mungu kwa utukufu wa hisani yake na ukuu wa buruhani yake. Tunamuepusha na kuwa na mtoto kwa vile anajitosha na kila kitu, si muhitaji; na kwa kuwa mtoto anafanana na baba yake na kumrithi na Yeye hana wa kufanana naye wala wa kumrithi.
Tunamwepusha na mshirika kwa vile hiyo ni dalili ya kushindwa:
وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا ﴿٤٤﴾
“Hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushindwa na chochote mbinguni wala ardhini; Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uweza.” (35:44).
Kila mwenye nguvu mbele yake ni dhaifu na kila mwenye utukufu kwake ni dhalili; ndio maana inakuwa Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi na Mwenye shani kiasi wasichoweza kusifu wanaosifu na kutekeleza haki yake wenye kushukuru.
MWISHO WA SURA YA KUMI NA SABA