14
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
وَاتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِن كِتَابِ رَبِّكَ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ وَلَن تَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٧﴾
27. Na soma uliyopewa wahyi katika kitabu cha Mola wako, Hapana wa kubadilisha maneno yake, Wala hutapata makimbilio isipokuwa kwake.
وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾
28. Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni, wakitaka radhi yake; wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia; wala usimtii tuliyemghafishilisha moyo wake asitukumbuke na akafuata matamanio yake na mambo yake yakawa yamepita kiasi.
وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا وَإِن يَسْتَغِيثُوا يُغَاثُوا بِمَاءٍ كَالْمُهْلِ يَشْوِي الْوُجُوهَ بِئْسَ الشَّرَابُ وَسَاءَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٢٩﴾
29. Sema hii ni kweli itokayo kwa Mola wenu, basi atakaye aamini na atakaye akufuru. Hakika sisi tumewaandalia wenye kudhulumu moto ambao hema lake litawazunguka, Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!
SOMA ULIYOPEWA WAHYI
Aya 27 -29
MAANA
Na soma uliyopewa wahyi katika kitabu cha Mola wako, Hapana wa kubadilisha maneno yake.
Anasema Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake mtukufu: Fikisha tuliyokuteremshia yanayohusiana na watu wa pango na wengineo katika yaliyokuja kwenye Qur’an Tukufu. Kuwa na yakini na yale tunayokupa habari. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake.
Siku na matukio yamethibitisha kuwa Muhammad(s.a.w.w)
ni rehema iliyoongozwa kutoka mbinguni kwa ajili ya watu. Kila zama zinavyozidi kuendelea ndio unapatikana ushahidi wa hakika hii.
Wala hutapata makimbilio isipokuwa kwake.
Yaani huna pa kumkimbia Mungu, Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w)
. Maana yake ya dhahiri ni kuwa wewe Muhammad una majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu wala hutapona ukiwa utatia shaka katika haki- ka ya Qur’an au kufanya uzembe katika kuifikisha.
Hasha! Haiwezekani kwa Mtume wa rehema kutia shaka au kufanya uzembe. Vipi iwe hivyo na hali Mwenyezi Mungu anajua zaidi pa kuuweka ujumbe wake! Isipokuwa makusudio ni kumweleza yule anayetia shaka katika utume wa Muhammad(s.a.w.w)
au kuhalifu aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni, wakitaka radhi yake; wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia; wala usimtii tuliyemghafishilisha moyo wake asitukumbuke na akafuata matamanio yake na mambo yake yakawa yamepita kiasi.
Ikisemwa isuburishe nafsi yako pamoja na fulani; yaani kuwa naye. Makusudio ya wanaomuomba Mola wao ni wale waumini wenye ikhlasi. Asubuhi na jioni ni fumbo la kudumu kwenye twaa ya Mungu. macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya dunia; yaani usigeuze umuhimu wako kutoka kwa watu wa dini ukaenda kwa watu wa dunia. Walioghafishilishwa ni makafiri na wenye makosa. Kupita kiasi mambo ni kauli na vitendo kupituka haki na uadilifu.
Imepokewa kuwa Uyayna - mmoja wa viongozi wa washirikina - alikwenda kwa Mtume(s.a.w.w)
akaona mafukara wamekaa naye, akiwemo Salmani Farisi akiwa na kilemba kilichojaa jasho na mkononi akiwa na jani la mtende.
Uyayna akasema: “Huu uvundo wa hawa haukusumbui wewe. Sisi vigogo wa Mudhar tukisilimu watasilimu watu wengi, Hakuna kinachotuzuia isipokuwa wafuasi wako hawa tu, Hebu achana nao tukufuate sisi au uwafanyie kikao chao na sisi tuwe na kikao chetu” Ndipo ikashuka Aya hiyo.
Sisi hatujui usahihi wa mategemezi ya riwaya hii, lakini tunaitilia nguvu kwa sababu inaenda na muktadha wa hali; yaani hali ya wapenda makuu na kujifanya wakubwa wakiwadharau wanyonge. Hilo limenukuliwa na Qur’an:
وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ ﴿٢٧﴾
“Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni” Juz; 12, (11:27).
Kabla ya Mtume(s.a.w.w)
kumjibu Uyayna na mfano wake kuwa ndio au hapana, aliye Mtukufu na kutuka akamwambia: kuwa pamoja na waumini, kwa vile wao wako pamoja nami, nami niko pamoja nao na uvumilie na wanayoyasema wapenda makuu. Kwa sababu subira yako kwao ni subira ya Mwenyezi Mungu na utiifu wake. Kwani huoni imani yao na ikhlasi yao kwangu na kwako katika kila kitu, wakitaka radhi yangu na thawabu zangu?
Ama waovu waliopofushwa na matamanio ya nyoyo zao, wanaofanya mambo kwa masilahi yao tu, wakikataa kuishi na wengine kwa haki na uadilifu, isipokuwa kiburi na kujikweza na kupituka mipaka yote ya Mwenyezi Mungu na ya binadamu, Hawa usiwasikilize. Kwani kauli yao hiyo ni ushenzi, uongo na upotevu; bali ni juu yako kupambana nao na kuwawekea ngumu kwa kauli na vitendo:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قَاتِلُوا الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ وَلْيَجِدُوا فِيكُمْ غِلْظَةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴿١٢٣﴾
“Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri na wakute kwenu ugumu; na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.” Juz, 11 (9:123).
Sema hii ni kweli itokayo kwa Mola wenu.
Anaambiwa Mtume awaambie wale walioghafilishwa nyoyo zao au watu wote. Hii ni usisitizo wa kauli iliyotangulia ya wasomee uliyopewa wahyi
Basi atakaye aamini na atakaye akufuru.
Hii ni sawa na kauli yake Mungu:
إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾
“Hakika sisi tumembainishia njia, Ama ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru” (76:3).
Aya hii inafahamisha kuwa mtu ana hiyari sio mwenye kuendeshwa, Lakini Razi amemrudi mwenye kutoa dalili kwa Aya hii kwamba utashi wa mtu haufanyi yeye mwenyewe, bali unafanywa na Mungu kwa hiyo kwake yeye mtu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari.
Nasi tunamjibu: Hakika utashi wa mtu unatokana na sababu na mazingira yanayomzunguka. Mfano mtu kumuona mwanamke mzuri nafsi yake ikampondokea, na hali dini imewajibisha mtu kuizuiwa nafsi yake, katika hali hii.
Hakuna mwenye shaka kwamba hili liko chini ya uwezo wake mtu (anaweza kulizuia), Mtume wa Mwenyezi Mungu ameliita hilo ‘Jihadi kubwa’ Kuna riwaya isemayo kuwa Mtume alituma kikosi cha wapiganaji.
Kiliporudi, akasema: Karibuni watu waliomaliza jihadi ndogo na kubakiwa na jihadi kubwa.” Akaulizwa ni ipi jihadi kubwa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Jihadi ya nafsi. Hakika jihadi bora ni ya yule mwenye kufanya jihadi ya nafsi yake ambayo iko baina ya mbavu zake.
Hakika sisi tumewaaandalia wenye kudhulumu moto ambao hema lake litawazunguka. Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!
Hili ni onyo na hadhari kwa kwa yule anayeathirika na ukafiri kuliko imani na batili kuliko haki, kwamba adhabu itazunguka pande zote; sawa na hema linavyomzunguka mtu, na watendela kupata kila aina ya dhabu.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿٣٠﴾
30. Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri
أُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِّن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٣١﴾
31. Hao wana bustani za milele zinazopita mito chini yake, watavaa nguo za kijani za hariri na atlasi, Huku wakiegemea juu ya makochi. Ni malipo bora yalioje na mahali pazuri palioje pa kupumzika.
UJIRA WA WATENDAO MEMA HAUPOTEI
Aya 30 – 31
MAANA
Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja madhalimu na adhabu yao, sasa anataja wema na malipo yao. Akabainisha aina hii ya thawabu kwa kauli yake:
Hao wana bustani za milele zinazopita mito chini yake, watavaa nguo za kijani za hariri na atlasi, Huku wakiegemea juu ya makochi. Ni malipo bora yalioje na mahali pazuri palioje pa kupumzika.
Katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anasema:
وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ﴿٧١﴾
“Na humo vitakuwemo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia” (43:71).
Imam Ali
anasema: “Kila neema isiyokuwa Pepo ni ya kudharauliwa na kila balaa isiyokuwa moto ni raha.” Umepita mfano wake katika Aya nyingi ikiwemo Juz. 1 (2: 82), Juz.4 (3:171) na Juz.5 (4:57).
Kauli ya kushangaza ni ile ya badhi ya masufi, kwamba makusudio ya kivazi ni tawhid, nguo za kijani ni sifa zinazoleta furaha, hariri ni vipawa, atlasi ni maadili na makochi ni majina ya Mwenyezi Mungu.
Wala hakuna ujeuri mkubwa kwa Mungu kuliko kutafsiri makusudio yake kwa njozi na mawazo au kwa hawaa na malengo mengine.
وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا رَّجُلَيْنِ جَعَلْنَا لِأَحَدِهِمَا جَنَّتَيْنِ مِنْ أَعْنَابٍ وَحَفَفْنَاهُمَا بِنَخْلٍ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمَا زَرْعًا ﴿٣٢﴾
32. Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimjalia vitalu viwili vya mizabibu na tukavizunguushia mitende na kati yake tukajaalia mimea ya nafaka.
كِلْتَا الْجَنَّتَيْنِ آتَتْ أُكُلَهَا وَلَمْ تَظْلِم مِّنْهُ شَيْئًا وَفَجَّرْنَا خِلَالَهُمَا نَهَرًا ﴿٣٣﴾
33. Hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hivyo kilichotindika. Na ndani yake tukapasua mito.
وَكَانَ لَهُ ثَمَرٌ فَقَالَ لِصَاحِبِهِ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَنَا أَكْثَرُ مِنكَ مَالًا وَأَعَزُّ نَفَرًا ﴿٣٤﴾
34. Naye alikuwa na mazao. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda kwa mali na nguvu za watu.
وَدَخَلَ جَنَّتَهُ وَهُوَ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ قَالَ مَا أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَـٰذِهِ أَبَدًا ﴿٣٥﴾
35. Akaingia kitaluni kwake, naye ameidhulumu nafsi yake, akasema: Sidhani kuwa haya yataharibika milele.
وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا ﴿٣٦﴾
36. Wala sidhani kuwa hiyo saa (ya Kiyama) itatokea, Na kama nitarudishwa kwa Mola wangu bila shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya.
قَالَ لَهُ صَاحِبُهُ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا ﴿٣٧﴾
37. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je, umemkufuru ambaye amekuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya kuwa mtu kamili?
لَّـٰكِنَّا هُوَ اللَّـهُ رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِرَبِّي أَحَدًا ﴿٣٨﴾
38. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, wala si mshirikishi na yeyote.
وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاءَ اللَّـهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّـهِ إِن تَرَنِ أَنَا أَقَلَّ مِنكَ مَالًا وَوَلَدًا ﴿٣٩﴾
39. Na lau ulipoingi kitaluni kwako ungelisema, alitakalo Mwenyezi Mungu huwa (mashaallah!), hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe.
فَعَسَىٰ رَبِّي أَن يُؤْتِيَنِ خَيْرًا مِّن جَنَّتِكَ وَيُرْسِلَ عَلَيْهَا حُسْبَانًا مِّنَ السَّمَاءِ فَتُصْبِحَ صَعِيدًا زَلَقًا ﴿٤٠﴾
40. Basi huenda Mwenyezi Mungu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako na kukipelekea maafa kutoka mbinguni na kugeuka ardhi tupu inayoteleza.
أَوْ يُصْبِحَ مَاؤُهَا غَوْرًا فَلَن تَسْتَطِيعَ لَهُ طَلَبًا ﴿٤١﴾
41. Au maji yake yadidimie usiweze kuyagundua.
وَأُحِيطَ بِثَمَرِهِ فَأَصْبَحَ يُقَلِّبُ كَفَّيْهِ عَلَىٰ مَا أَنفَقَ فِيهَا وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُشْرِكْ بِرَبِّي أَحَدًا ﴿٤٢﴾
42. Yakaangamizwa matunda, akabaki anapinduapindua viganja vyake, kwa vile alivy - oyagharimia, nayo imeanguka juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yoyote.
وَلَمْ تَكُن لَّهُ فِئَةٌ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مُنتَصِرًا ﴿٤٣﴾
43. Wala hakuwa na kundi la kumsadia kinyume na Mwenyezi Mungu wala mwenyewe hakuweza kujisaidia.
هُنَالِكَ الْوَلَايَةُ لِلَّـهِ الْحَقِّ هُوَ خَيْرٌ ثَوَابًا وَخَيْرٌ عُقْبًا ﴿٤٤﴾
44. Huko usaidizi ni wa Mwenyezi Mungu, Mkweli. Yeye ni Mbora kwa malipo na mbora wa matokeo.
BAINA YA KAFIRI TAJIRI NA MUMIN FUKARA
Aya 32 – 44
MUHTASARI WA KISA
Tulipofasiri Aya 27 ya Sura hii tulitaja kuwa vigogo wa kishirikina walitoa sharti la kumwamini kwao Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kuwa awafukuze mafukara au awatengee vikao vyao ili wasichanganyike na mafakura, kwa vile wao ni mabwana na viongozi na watu wengine ni watumwa wao tu.
Aya tulizo nazo sasa zinaleta picha ya matajiri wenye kiburi, kwa mtu mmoja tajiri mwenye mali na mashamba na picha ya mafukara waumini, kwa mtu mmoja fukara asiye na chochote, lakini anajitukuza kwa maadili yake na tajiri anajitukuza kwa mali yake. Yanapita majibizano baina yao yanayowakilisha mvutano baina ya haki na batili. Hatimaye haki inashinda na batili inaanguka. Amesema kweli mwenye hekima aliyesema: “Mwenye kupigana na haki itampiga mweleka”
Kwa ufupi, maana ya Aya hizo ni: Yule anayejitukuza kwa mali yake, anamiliki mashamba mawili makubwa yenye miche ya ngano na nafaka nyinginezo. Pia mna miti mingi ya mitende na mizabibu. Mashamba yote mawili yana chemchem ya maji; mavuno yake ni mazuri na kamili. Ama yule anayejitukuza kwa maadili yake, hana kitu chochote.
Mwenye mashamba akamwambia yule fukara kwa kujisifu na kujinaki: Mimi nimekushinda na kila kitu – mali na jaha. Angalia mimea, miti, matunda na mito ya maji niliyo nayo. Hii ndio milki ya kudumu itakayoku- ja wafaa watoto na wajukuu; sio pepo mnayodai nyinyi masikini. Hivi baada ya mauti kweli kuna pepo na moto? Kama itakuwa ni kweli basi hadhi yangu huko itakuwa kubwa kuliko hapa duniani. Kwa sababu aliye tajiri hapa huko pia atakuwa tajiri .
Yule mumin akamjibu kwa kumjadili na kumlaumu: Hivi unasema haya kwa kumbughudhi na kumkufuru ambaye amekufanya uwe mtu? Umesahau asili yako? Wewe si umetokana na Adamu na Adam akatokana na mchanga? Hukuwa wewe ni tone la manii? Mimi mwenzako ninamwamini Mwenyezi Mungu na ninampwekesha, ninamsifu kwa kuniongoza kwenye njia yake na radhi zake. Kama ungekuwa na busara basi ungelimnyenyekea Mwenyezi Mungu na kumshukuru badala ya kujitia ujuvi kwa dhambi. Ni lipi liliokufanya ujiaminishe na mambo ya kushtukiza ya ghafla? Mungu akiwapa muda waasi kwa huruma zake huwa amewapa muda wa hasira zake na nakama yake.
Kabla ya hata kumaliza maneno yake yule mumin, mara miti ikaanza kuanguka, mito ikakauka, mimea ikateketea na kila kitu shambani kikaharibika. Mwenye shamba akasema: “Sikufikira kabisa itaharibika hii.” Baada ya kuona alivyofanya Mwenyezi Mungu na kukata tamaa ya mimea yake na miti yake alisema kwa masikitiko: “Laitani nisingemshirikisha Mola wangu na yeyote.” Lakini wapi! Hivi sasa na hali hapo mwanzo umemuasi na ukawa katika wafisadi?
Huu ndio muhtasari wa kisa. Na makusudio ya kisa hicho ni kuwa mtu aamini kwa kauli na vitendo kuwa hakuna hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu mmoja mwenye kushinda. Na kwamba Yeye ambaye imetukuka hekima yake saa yoyote anayotaka anaweza kumgeuza mtukufu kuwa dhalili na dhalili kuwa mtukufu. Vilevile tajiri kuwa fukara na fukara kuwa tajiri na afya kuwa ugonjwa na maumivu na kinyume chake. Vile vile mtu aamini kuwa milki ya mwenye kuumbwa si chochote kadiri itakavyokuwa ila akiibadilisha katika kazi za kheri.
Baada ya muhtasari huu sasa tuingilie ufafanuzi wa na tafsiri ya Aya ingawaje nyingi ziko wazi zisizohitaji ufafanuzi.
MAANA
Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimjalia vitalu viwili vya mizabibu na tukavizunguushia mitende na kati yake tukajaalia mimea ya nafaka, Hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hivyo kilichotindika. Na ndani yake tukapasua mito.
Anaambiwa Muhammad(s.a.w.w)
awambie washirikina waliosema kuwa awafukuze mafukara au amwambie kila mpenda makuu mwenye kiburi, Makusudio ya watu wawili ni tajiri na fukara ambao walikuwa na majibizano.
Ni maarufu Qur’an kuwa mara nyingi inaleta mifano ya fikra na misingi ya kiujmla na kufananisha na vitu vyenye kuhisiwa; kama kufananisha imani na nuru na ukafiri na giza. Pia mara nyingine inafananisha chenye kuhisiwa na chenye kuhisiwa kingine kilichowazi zaidi na kilicho na ubainifu zaidi; kama kufananisha mwenye kurtadi na mbwa mwenye kuhema kwa nguvu.
Lengo la yote hayo ni kufafanua na kuweka wazi, kuongezea mazingatio na mawaidha:
وَعَادًا وَثَمُودَ وَأَصْحَابَ الرَّسِّ وَقُرُونًا بَيْنَ ذَٰلِكَ كَثِيرًا ﴿٣٨﴾ وَكُلًّا ضَرَبْنَا لَهُ الْأَمْثَالَ وَكُلًّا تَبَّرْنَا تَتْبِيرًا ﴿٣٩﴾
“Na tuliwaangamiza kina watu A’d na Thamud na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyokuwa kati yao na wote tuliwapigia mifano.” (25:38-39).
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa amefananisha hali ya mataghuti wapenda makuu wenye kiburi na mtu mmoa kafiri mwenye kiburi mjinga aliye na vitalu viwiwili ambavyo ndani yake mna mto, mimea ya nafaka na miti inayobeba matunda bora ya wakati huo, ambayo ni tende na zabibu.
Mimea yote inatoa mazao kwa wakati wake kwa ukamilifu. Na akamfananisha mumin na mtu mmoja mnyeneykevu mwenye maarifa, lakini hana chochote ni fukara. Yakatokea majibizano baina ya wawili hao; kama ifuatavyo:-
Basi akmwambia mwenzake naye akibishana naye.
Aliyesema ni yule tajiri mwenye kiburi kumwambia mwenzake mumin mwenye adabu
Mimi nimekushinda kwa mali na nguvu za watu.
Aliona kuwa mali na jaha ndio kipimo cha utukufu, lakini imani na ikhlasi ni maneno matupu tu yasiyokuwa na maana. Hii ndio mantiki ya mafasiki na wovu, tangu zamani hadi leo. Thamani ya mtu kwao ni kile anachokimiliki, sio matendo mema wala elimu nzuri.
Mali ndiyo inayosababisha matatizo ya binadamu, Ndio kichocheo cha kwanza cha fitina ya silaha za maangamizi na kutumia mamilioni ya walalahoi kutengenezea silaha hizo. Wanyonyaji wanaiba mali ya wananchi na kuigeuza mabomu na maroketi kisha wayatupe kwa hao hao wananchi waliowanyanganya riziki zao na maliasili zao.
Akaingia kitaluni kwake, naye ameidhulumu nafsi yake
kwa sababu aliyaitikia matamanio yake akaitia hatarini nafsi yake; sawa na anayemkubalia mwanawe mambo yatakayomdhuru na kumwangamiza.
Akasema: Sidhani kuwa haya yataharibika milele.
Razi anasema: “Vipi alisema kuwa sidhani kuwa haya yataharibika milele pamoja na kuwa hisia zinafahamisha kuwa dunia si yenye kubakia? Tunasema: alikusudia kuwa havitaharibika katika uhai wake”
Jibu sahihi ni kuwa ujinga na ghururi zilimpofusha mwenye shamba na kila kitu hata na vitu waziwazi na vyenye kuhisiwa. Anasema Mtukufu wa wasemao: “Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi, Hao ndio walioghafilika.” Juz. 9 (7:179).
Wala sidhani kuwa hiyo saa (ya Kiyama) itatokea.
Dhana hii haitegemei chochote isipokuwa majivuno ghururi na mambo ya kuwazia tu, kwamba neema yake ni ya milele haitaisha. Hii ndio tafsiri ya mataghuti wajivuni wanaokana hisabu na ufufuo.
Na kama nikirudishwa kwa Mola wangu bila shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya.
Kwa fikra yake anaona kuwa wapenda makuu huko pia wana nafasi, Anakisia ya ghaibu kwa ya sasa. Hajui kwamba uokovu kesho ni wa wamchao Mungu, sio mataghuti na wajivuni:
مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ﴿٢٨﴾ هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ ﴿٢٩﴾
“Mali yangu hayakunifaa, Madaraka yangu yamenipotea” (69:28-29).
Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je, umemkufuru ambaye amekuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kamili?
Mumini alimwambia kafiri kwa kumlaumu, kuwa unamkana aliyekuumba na dalili zake ziko wazi kwako? Umepata vipi uhai pamoja na akili yake na uoni wake? Si ulikuwa si chochote?
Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, wala si mshirikishi na yoyote.
Anaendelea kusema mumin, ama mimi nimeongoka kwa umbile langu na akili yangu kwa muumba wangu na muumba wa kila kitu na nimeamini kuwa Yeye pekee ndiye muumba mwenye kuruzuku.
Kisha muumin akamkumbusha yule kafiri neema ya Mwenyezi Mungu kwake na wajibu wa kumshukuru na kumsifu kwa kumwambia:
Na lau ulipoingia kitaluni kwako ungelisema alitakalo Mwenyezi Mungu huwa (mashaallah!), hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.
Yaani lau ungelikuwa una busara ungelitambua kuwa kheri na fadhila ni kuongezeka ujuzi wako sio mali yako, ungeshindana na watu kwa maadili yako sio kwa jaha yako na kujua kuwa hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu mmoja mwenye nguvu na kushinda.
Ni Yeye pekee ndiye anayetoa enzi na jahaa na kubadilisha utajiri kwa ufukara na ufukara kwa utajiri; alitakalo huwa na asilolitaka haliwi.
Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, basi huenda Mwenyezi Mungu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako na kukipelekea maafa kutoka mbinguni na kugeuka ardhi tupu inayoteleza; au maji yake yadidimie usiweze kuyagundua.
Mumin aliendelea kumjia juu kafiri kwa mali yake, akamwambia kuwa utajiri na ufukara unatoka kwa Mungu na wewe hujui mimi nina utajiri zaidi wa kukushinda wewe alioniwekea akiba Mwenyezi Mungu kwenye nyumba ya milele kushinda hivi vitalu vyako unavyojifaharisha navyo.
Hujui wewe kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kunifanya tajiri mimi na kukufanya fukara wewe baina ya asubuhi na jioni.
Wewe unajigamba na mali yako, kwa sababu watu wanakusifia. Je sifa hizi ndio zitakukinga na mambo yanayofichwa na nyakati? Je, umejiaminisha na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu? Huogopi wewe na hivyo vitalu vyako kushukiwa na majanga kutoka mbinguni na ukabaki mtupu?
Yakaangamizwa matunda, akabaki anapinduapindua viganja vyake kwa vile alivyoyagharimia nayo imeanguka juu ya chanja zake.
Kupinduapindua viganja ni fumbo la kujuta. Mimea iliangamia, miti ikaanguka kila upande na maji yakauka mpaka tone la mwisho. Ardhi ikawa inateleza; kama kwamba hakukuwa na chochote.
Ufukara ukachukua nafasi ya utajiri, dhiki mahali pa faraja na udhalili na kuvunjikiwa mahali pa kujitukuza na kiburi. Haya ndio matunda ya ukafiri, dhulma na ufisadi – hasara na majuto ya juhudi na mali.
Akawa anasema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yoyote.
Kama kwamba anakusudia, kwa kauli hii, kurudi kitalu chake, lakini wapi?
لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ﴿١٥٨﴾
“Basi nafsi haitaifaa imani yake ambayo haikuiamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake” Juz; 8 (6:158).
Wala hakuwa na kundi la kumsadia kinyume na Mwenyezi Mungu wala mwenyewe hakuweza kujisaidia.
Kabisa! Hakuna ndugu wala rafiki au jaha wala mali, isipokuwa Mwenyezi Mungu.
قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٢﴾
“Sema: Hakika hakuna yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake tu.” (72:22).
Huko usaidizi ni wa Mwenyezi Mungu, Mkweli. Yeye ni Mbora kwa malipo na mbora wa matokeo.
Huko ni ishara ya siku ya kiyama; yaani, ikiwa mtu katika maisha haya anapata wa kumtetea na kumsaidia, basi siku ya kiyama hatapata isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) peke yake.
Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua na amewaandalia ujira mwema na mahali pazuri.