15
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO
وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا ﴿٤٥﴾
45. Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mbinguni yakachanganyika na mimea ya ardhi ikawa majani makavu yaliyokatikakatika yanayopepeprushwa na upepo, Na Mwenyezi Mungu ana uwezo juu ya kila kitu.
الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا ﴿٤٦﴾
46. Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vibakiavyo vizuri ndivyo bora mbele ya Mola wako na kwa malipo na tumaini bora.
PAMBO LA MAISHA YA DUNIA
Aya 45 – 46
MAANA
Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mbinguni yakachanganyika na mimea ya ardhi ikawa majani makavu yaliyokatikakatika yanayopepeprushwa na upepo.
Dunia ni nzuri yenye mandhari ya kijani ya kupendeza, lakini ina ghururi na madhara. Haina kheri katika akiba yake isipokuwa takua; kama alivyosema Imam Ali
.
Haya ndiyo maana ya Aya; ambapo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameifananisha dunia, katika uzuri wake, na mvua iliyonyesha kwenye ardhi ikairutubisha na ikaota miti ya kila aina, lakini mara inageuka na kuwa kame, majani yakawa makavu yanayopukusika yakirushwa na upepo. Hivi ndivyo yalivyo maisha ya dunia, ni mazuri lakini yameficha ubaya.
Na Mwenyezi Mungu ana uwezo juu ya kila kitu.
Anaweza kuuondoa ulimwengu na kuumaliza kabisa; kama alivyoweza kuumba na kuuleta. Anasema Ibnul Arabi katika kitabu Futahitl-Makkiyya “Mwenyezi Mungu ni muweza wa mambo na ana uwezo wa kuumba” Anakusudia kuwa Mwenyezi Mungu anasifika kuwa ni muweza pale anapotaka kitu kuwa kikawa, ni sawa aseme au asieme na anasifika kuwa ana uweza pale anaposema na kitu kikawa vilevile.
MALI NA WATOTO NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA
Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia.
Pambo la maisha liko aina mbili: La umma na la kibinafsi. La umma ni kama vile kujenga njia za mawasiliano; mfano barabara n.k. Au taasisi; mfano kujenga vyuo vikuu, vituo vya malezi ya watoto viwanda n.k.
Na la kibinafsi ni kama nyumba, gari, mtoto mtiifu aliyefaulu, viwanda, umaarufu katika jamii n.k. Vipambo hivi sio haramu. Vitakuwaje haramu na hali Yeye ndiye aliyesema:
قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ ﴿٣٢﴾
“Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki?” Juz. 8 (7:32).
Lakini pambo binafsi halistahili mtu kujitukuza na kujifaharisha nalo. Kwa sababu kipimo cha kutukuzwa pambo ni kwa manufaa ya umma na kubakia vizazi na vizazi. Hili ndilo alilolikusudia Mwenyezi Mungu pale aliposema:
Na vibakiavyo vizuri ndivyo bora mbele ya Mola wako na kwa malipo na tumaini bora.
Kwa sababu mwenye kutekeleza atapata huko Akhera yale aliyoyatumai, mbali ya kupata heshima na kuendelea kutajika katika maisha haya ya dunia.
Kwa ufupi ni kuwa mali ni nyenzo sio lengo. Inapimwa na kukadiriwa kwa natija yake na athari yake. Ikiwa ni kheri itakuwa kheri na ikiwa ni shari basi itakuwa shari. Ikitumika kwa njia ya shari na ufisadi, kama vile mashindano ya silaha, basi itakuwa mali ni shari na ikitumika katika kutekeleza mahitaji, basi mali itkuwa ni kheri.
Na kheri hiyo iko aina mbili: Ikiwa itamletea manufaa mwenye nayo au kumkinga na madhara basi itakuwa ya binafsi na itaisha kwa kuisha. Lakini ikiwa manufaa yake ni kwa umma basi itakuwa ni katika vibakiavyo vizuri.
وَيَوْمَ نُسَيِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا ﴿٤٧﴾
47. Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi iwazi. tutawafufua wala hatuta- muacha yeyote katika wao.
وَعُرِضُوا عَلَىٰ رَبِّكَ صَفًّا لَّقَدْ جِئْتُمُونَا كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ بَلْ زَعَمْتُمْ أَلَّن نَّجْعَلَ لَكُم مَّوْعِدًا ﴿٤٨﴾
48. Na watahudhurishwa mbele ya Mola wako kwa safu. Hakika mmetufikia kama tulivyowaumba mara ya kwanza; bali mlidai kuwa hatutawawekea miadi.
وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا ﴿٤٩﴾
49. Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo. Na watasema: “Ole wetu! Kina nini kitabu hiki hakiachi dogo wala kubwa ila kinalihesabu? Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa, Na Mola wako hadhulumu yoyote.
TUTAWAFUFUA WALA HATUTAMUACHA YEYOTE
Aya 47 -49
MAANA
Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi i wazi.
Ardhi hii tunayoishi leo, Mwenyezi Mungu ameitaja katika Aya nyingi, miongoni mwazo ni hii tuliyo nayo. Hapa Mwenyezi Mungu ameisifu kwa sifa mbili:
Kwanza, kuwa Mwenyezi Mungu ataing’oa milima mahali ilipo na aipeleke kama mawingu, Sifa ya pili, kwamba ardhi yote kuanzia pembe hadi pembe itakuwa wazi bila ya kuweko kizuizi chochote. Hapo ndio itakuwa ufufuo ambao Mungu ameuashiria kwa kusema:
Na tutawafufua wala hatutamuacha yeyote katika wao.
Mwenyezi Mungu atawafufua wote, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, kwa ajili ya hisabu.
Na watahudhurishwa mbele ya Mola wako kwa safu.
Huko nyuma tumetaja kuwa hisabu na malipo ni kweli isiyokuwa na shaka. Tumelithibitisha hilo kwa dalili mkataa, katika kufasiri Aya zinazoonyesha hivyo; miogoni mwazo ni, Juz; 11 (10:4) kifungu cha ‘Hisabu na malipo ni lazima’.
Aya tuliyo nayo inasema kuwa viumbe watahudhurishwa kwa Mungu kesho wakiwa wamepiga safu. Makusudio ya kuhudhurishwa hapa ni kusimama kwa Mungu kwa ajili ya hisabu.
Ama kuhusu neno safu, wafasiri wametofautiana; wengine wameliacha neno na dhahiri yake, wengine wakaleta sarufi na kulichukulia tamko yale yasiyowezekana. Tuonavyo sisi ni kuwa safu ni fumbo la utaratibu na nidhamu, kwamba viumbe watahudhurishwa kwa mola wao kwa mpangilio madhubuti.
Hakika mmetufikia kama tulivyowaumba mara ya kwanza; bali mlidai kuwa hatutawawekea miadi.
Hivi ndivyo atakavyoanza Mwenyezi Mungu kuwahukumu wale waliokuwa wakipinga ufufuo: Tuliwatoa matumboni mwa mama zetu mkiwa uchi hamna chochote; vilevile leo tumewatoa makaburini mwenu. Hakuna tofauti isipokuwa pale mwanzo mlikuwa hamuulizwi chochote na leo mmetolewa ili muulizwe yale mliyokuwa mkiyafanya, kuyaamini na kuyasema. Miongoni mwayo ni kusema kwenu kuwa ufufuo ni uzushi na vigano. Je, mmeona leo?
Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo.
Hii ndiyo Siku ya Ufufuo mliyokuwa mkiikadhibisha, Kila mmoja atapewa daftari la matendo yake na aambiwe:
اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا ﴿١٤﴾
“Soma kitabu chako! Nafsi yako leo inakutosha kukuhisabu” (17:14)
Yaani soma daftari la matendo yako na ujipigie mahisabu wewe mwenyewe. Atasoma huku akitetemeka kwa hofu isiyokuwa na matumini yoyote wala matarajio ya kuokoka. Lau angeliogopa adhabu tangu mwanzo na kajiepusha na njia yake, angelikuwa leo yuko kwenye amani na sala- ma. Lakini alijiaminisha huko na anahofu hapa.
Na watasema: ole wetu! Kina nini kitabu hiki hakiachi dogo wala kubwa ila kinalihesabu?
Hapo mwanzo walikuwa wakisema hakuna kitabu wala hisabu.
Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa,
bila ya kuzidi wala kupungua; Kwanini isiwe hivyona Mola wako hadhulumu yoyote
? Si kwenye thawabu wala adhabu; bali huwa zikaongezwa thawabu kwa mwenye kufanya wema na kusamehewa mwenye kufanya uovu.
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا ﴿٥٠﴾
50. Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsujudia isipokuwa Iblis. Alikuwa miongni mwa majini akatoka kwenye amri ya Mola wake. Je, mnamfanya yeye na dhuria zake kuwa mawalii badala yangu, hali wao ni adui zenu? Ni uovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.
مَّا أَشْهَدتُّهُمْ خَلْقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَا خَلْقَ أَنفُسِهِمْ وَمَا كُنتُ مُتَّخِذَ الْمُضِلِّينَ عَضُدًا ﴿٥١﴾
51. Si kuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi wala kuumbwa kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni mkono.
وَيَوْمَ يَقُولُ نَادُوا شُرَكَائِيَ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُم مَّوْبِقًا ﴿٥٢﴾
52. Na siku atakaposema waiteni hao mliodai kuwa ni washirika wangu, Basi watawaita nao hawatawaitikia. Nasi tutaweka baina yao maangamizi.
وَرَأَى الْمُجْرِمُونَ النَّارَ فَظَنُّوا أَنَّهُم مُّوَاقِعُوهَا وَلَمْ يَجِدُوا عَنْهَا مَصْرِفًا ﴿٥٣﴾
53. Na wahalifu wataona moto na watadhani kuwa wao watauingia wala hawatapata pa kuepukia.
WALISUJUDI ISIPOKUWA IBLISI
Aya 50 – 53
MAANA
Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsujudia isipokuwa Iblis;
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1(2:11), Juz. 8 (7:11) na Juzuu hii ya 15 (17: 61).
Alikuwa miongoni mwa majini akatoka kwenye amri ya Mola wake.
Yaani alitoka kwenye twaa ya mola wake. Mara nyingi tumesema kuwa sisi tunaamini kuweko majini, kwa sababu wahyi unathibitisha hilo na akili haipingi hilo; na kwamba ufafanuzi wake tunamwachia Mjuzi wa ghaibu.
Je, mnamfanya yeye na dhuria zake kuwa mawalii badala yangu?
Qur’an huwa inajifasiri yenyewe na sehemu moja inaitolea ushahidi sehemu nyingine. Katika Aya nyingi imeleta ibara ya kuwa wale wanaoichanganya haki na batili kuwa ni askari wa Iblisi na mawalii wake.
Kwa hiyo hapa inafaa kufasiri kuwa dhuria za Iblisi ni askari wake na wazaidizi wake na kwamba kizazi cha Ibilisi, askari wake na mawalii wake, ni wale wanaoichanganya batili na uongo na kuzulia haki. Sio mbali kwamba ibara ya kuwa hao ni dhuria za Ibilisi, ni kufanana vitendo vyao na vyake.
La kushangaza ni kauli ya asemaye kuwa Ibilisi ana tupu ya kiume katika paja lake la kuume na tupu ya kike katika paja lake la kushoto. Kwa hiyo aniingiza ya kiume kwenye hiyo ya kike na anapata kizazi na dhuria
Hali wao ni adui zenu?
Kila anayekupambapamba na kukudanganya na mambo ya batili au kukusifia mambo usiyokuwa nayo, basi huyo ni adui yako, ujue hilo au usijue.
Ama yule anayezua vigano juu ya Ibilisi na wengineo, basi huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na pia wa ubinadamu.
Ni uovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.
Madhalimu ni wale wanaobadilsha twaa ya Mwenyezi Mungu kuwa twaa ya shetani; miongoni mwao ni wale wanaowachagua wafisadi kwenye vyeo na kuwafidhilisha kuliko watu wema.
Si kuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi wala kuumbwa kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni mkono.
Ambao hawakushuhudishwa ni ibilisi na dhuria zake. Makusudio ya mkono hapa ni usaidizi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) akilitaka jambo ni kuliambia kuwa kisha likawa, hamshauri wala hamtaki msaada yeyote, kwa sababu yeye hawahitajii walimwengu.
Na wakati alipoumba vitu hakumuhudhurisha yeyote katika wao, hata kama ni mwenye takua zaidi ya wote; sikwambii tena akiwa ni mpotezaji; kama vile Ibiisi na askari wake. Madamu mambo yako hivyo, imekuwaje kuasiwa muumbaji na kutiiwa yule ambaye hawezi kujisaidia hata yeye mwenyewe au kujikinga na madhara?
Na siku atakaposema waiteni hao mliodai kuwa ni washirika wangu, Basi watawaita nao hawatawaitikia. Nasi tutaweka baina yao maangamizi.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawaambia wale waliokuwa wakimfanyia washirika katika twaa yake: wako wapi wale ambao mliwatii na mkadai kuwa wao watawapa manufaa siku hii ya lo ngumu? Hebu waiteni tuone kama watawaitikia. Hapana! Wenyewe wana shughuli inayowashughulisha; wako katika adhabu ya moto, Kauli yake Mwenyezi Mungu kuwa watawaita na wasiwasikie ni fumbo la kukata kwao tamaa kwa matarajio waliyokuwa wakiyatarajia.
Na wahalifu wataona moto na watadhani kuwa wao watauingia wala hawatapata pa kuepukia.
Makusudio ya kudhani hapa ni kujua na kuwa na yakini. Pia kuepukia ni kuepuka na moto. Kukimbia kesho ni sawa na kujaribu kuyakimbia mauti leo hapa duniani.
وَلَقَدْ صَرَّفْنَا فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ لِلنَّاسِ مِن كُلِّ مَثَلٍ وَكَانَ الْإِنسَانُ أَكْثَرَ شَيْءٍ جَدَلًا ﴿٥٤﴾
54. Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’an kila aina ya mifano. Lakini mtu amezidi kila kitu kwa ubishi.
وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَن يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ وَيَسْتَغْفِرُوا رَبَّهُمْ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمْ سُنَّةُ الْأَوَّلِينَ أَوْ يَأْتِيَهُمُ الْعَذَابُ قُبُلًا ﴿٥٥﴾
55. Na hapana kilichowazuia watu kuamini ulipowajia uongofu na kuomba maghu- fira kwa Mola wao; isipokuwa yawafikie ya wale wa zamani au iwajie adhabu waziwazi.
وَمَا نُرْسِلُ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَيُجَادِلُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالْبَاطِلِ لِيُدْحِضُوا بِهِ الْحَقَّ وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَمَا أُنذِرُوا هُزُوًا ﴿٥٦﴾
56. Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji. Na waliokufuru wanabishana kwa batili, ili waivunje haki kwayo, na wanazifanya ishara zangu na yale waliyoonywa, kuwa ni mzaha.
MTU NI MBISHI SANA
Aya 54 – 56
MAANA
Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’an kila aina ya mifano, Lakini mtu amezidi kila kitu kwa ubishi.
Makusudio ya mtu hapa sio kila mtu bali ni watu wengi zaidi, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu kwenye Aya kadhaa: “Watu wengi hawana akili” “watu wengi hawajui” watu wengi hawaamini” n.k. Qur’an ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa waja wake, kinachowaongoza kwa dalili zake na mawaidha yake na kuhimiza kushikamana na hukumu zake na mafundisho yake.
Mwenyezi Mungu amefafanua mawaidha na dalilil hizi kwa mifumo mbalimbali na akazipigia mifano mbalimbali; ikiwemo ile ya watu wawili waliotajwa katika Aya ya 32 ya Sura hii na kufananisha maisha na maji katika Aya ya 54. lakini watu hawatii akilini na wanabishana katika mambo yaliyo wazi, wakijaribu kubatishilisha haki kwa mambo ya uongo na ya kupambamba.
Na hapana kilichowazuia watu kuamini ulipowajia uongofu na kuomba maghufira kwa Mola wao; isipokuwa yawafikie ya wale wa zamani au iwajie adhabu waziwazi.
Makusudio ya uongofu ni Qur’an na ubanifu wake ulio wazi. kuomba maghufira ni kutubia na yaliyowafikia wa zamani ni maangamivu; kama yaliyowafikia kaumu ya Nuh, Lut, A’d na Thamud.
Maana ni kuwa washirikina hawajaribu kuamni au kufikiria kuamni mpaka wapatikane na moja wapo ya mambo mawili: Kwanza ni kushukiwa na adhabu ya kuwafyeka; kama ilivyowashukia waliokuwa kabla yao; ndipo wataamni; ambapo imani, wakati huo, haifai kitu; kama Firauni ambaye aliamini alipoona maangamizi na kufa maji kunafika. Jambo la pili ni kuiona adhabu ana kwa ana.
Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipobainisha, katika aya zilizotangulia, kuwa Yeye ameleta dalii zilizo waziwazi na watu wengi wakakataa isipokuwa ubishi, sasa anasema kuwa dalili hizi hazifai kitu kwa watu wasioamini isipokuwa wakati wa kukata roho au wanapotishika na adhabu wanapoiona kwa macho yao au wanapoamini kuwa itawafikia tu.
Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji.
Huu ndio umuhimu wa Mtume kumpa habari njema ya neema yule mwenye kutii na kumuonya na adhabu yule mwenye kuasi, Maana haya yamekaririka mara nyingi. Tazama Juz. 6 (4:165).
Na waliokufuru wanabishana kwa batili, ili waivunje haki kwayo na wanazifanya ishara zangu na yale waliyoonywa, kuwa ni mzaha.
Ameziweka wazi ishara na akazithibitisha kwa ubainifu na dalili, lakini waliokufuru wakabishana na wakajaribu kuzibatilisha kwa uongo na mizaha. Makusudio ya kuzifanyia mizaha ishara za Mwenyezi Mungu hapa sio mizaha ya kusema tu; bali ni kuwa kila mweye kuijua hukumu, miogoni mwa hukumu za Mwenyezi Mungu, na asiitumie, basi yeye ni katika walioifanya Qur’an na dini ya Mwenyezi Mungu kuwa ni mchezo.
Imam Ali
anasema:“Mwenye kuisoma Qur’an, kisha akafa akaingia motoni – kwa kutoitumia Qur’an – basi huyo ni katika waliozifanyia mzaha ishara za Mwenyezi Mungu.
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ فَأَعْرَضَ عَنْهَا وَنَسِيَ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ إِنَّا جَعَلْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ أَكِنَّةً أَن يَفْقَهُوهُ وَفِي آذَانِهِمْ وَقْرًا وَإِن تَدْعُهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ فَلَن يَهْتَدُوا إِذًا أَبَدًا ﴿٥٧﴾
57. Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa ishara za Mola wake na akazipuuza na akasahau yaliyotangulizwa na mikono yake? Hakika tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tumeweka kwenye masikio yao uziwi, Na ukiwaita kwenye uongofu hawataongoka kabisa.
وَرَبُّكَ الْغَفُورُ ذُو الرَّحْمَةِ لَوْ يُؤَاخِذُهُم بِمَا كَسَبُوا لَعَجَّلَ لَهُمُ الْعَذَابَ بَل لَّهُم مَّوْعِدٌ لَّن يَجِدُوا مِن دُونِهِ مَوْئِلًا ﴿٥٨﴾
58. Na Mola wako ni mwenye maghufira na mwenye rehema, lau angeliwachukulia kwa walioyachuma, bila shaka angeliwafanyia haraka kuwaadhibu, Lakini wana miadi ambayo hawatapata kimbilio la kuepukana nayo.
وَتِلْكَ الْقُرَىٰ أَهْلَكْنَاهُمْ لَمَّا ظَلَمُوا وَجَعَلْنَا لِمَهْلِكِهِم مَّوْعِدًا ﴿٥٩﴾
59. Na miji hiyo tuliwaangamiza walipodhulumu na tukawawekea miadi ya maangamizo yao.
ALIYEKUMBUSHWA ISHARA ZA MOLA WAKE AKAZIKATAA
Aya 57 – 59
MAANA
Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa ishara za Mola wake na akazipuuza na akasahau yaliyotangulizwa na mikono yake?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameziweka wazi dalili za kuweko kwake na wajibu wa kumtii Yeye kwa mifumo mbali mbali; kisha akapiga mifano mingi ya hayo. Akamwamrisha mtu kufanya kheri na kutubia dhambi zake zilizopita, akamkataza shari na akamuhadharisha kukhalifu amri na makatazo na kuendelea na dhambi. Lakini mtu ameyapuuza yote hayo na akaitia nafsi yake kwenye maangamivu.
Hakika tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu na tumeweka kwenye masikio yao uziwi.
Umetangula mfano wake pamoja na tafsiri katika Juz. 7 (6:25) na Juz. hii ya 15 (17: 46).
Na ukiwaita kwenye uongofu hawataongoka kabisa.
Wataongoka vipi na hali kwenye nyoyo zao kuna vifuniko na kwenye masikio yao kuna uziwi. Kila asiyenufaika na mawaidha mazuri, basi huyo ni sawa na kipofu wa moyo na macho na ni kiziwi.
Na Mola wako ni mwenye maghufira na mwenye rehema, lau angeliwachukulia kwa walioyachuma, bila shaka angeliwafanyia haraka kuwaadhibu.
Umetangula mfano wake pamoja na tafsiri katika Juz. 14 (16:61).
Lakini wana miadi ambayo hawatapata kimbilio la kuepukana nayo.
Mausudio ya miadi hapa ni wakati wa kufika mbele ya Mwenyezi Mungu, Ni miadi isiyovunjwa wala kukimbiwa.
Imam Ali (a.s) anasema kumwambia Mola wake:“Wewe ni wa milele huna muda na wewe ni mwishilio usioepukwa na wewe ni ahadi isiyokimbiwa. Uko mikononi mwako utosi wa kila mnyama na kwako ni marejeo ya kila nafsi.”
Na miji hiyo tuliwaangamiza walipodhulumu na tukawawekea miadi ya maangamizo yao.
Makusudio ya miji hapa ni ya kina A’d,Thamud na wengineo katika umma zilizopita. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alijaalia wakati maalum wa kuaangamia madhalimu, ukifika hawatachelewa hata saa moja wala hawatatangulizwa.