6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا أَيُّ الْفَرِيقَيْنِ خَيْرٌ مَّقَامًا وَأَحْسَنُ نَدِيًّا ﴿٧٣﴾
73. Na wanaposomewa Aya zetu zilizowazi, waliokufuru huwaambia walioamini: lipi katika makundi mawili lenye cheo kizuri na lililo bora barazani
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَحْسَنُ أَثَاثًا وَرِئْيًا ﴿٧٤﴾
74. Na karne ngapi tuliziangamiza zilizokuwa na mapambo mazuri zaidi na wazuri zaidi kwa mandhari?
قُلْ مَن كَانَ فِي الضَّلَالَةِ فَلْيَمْدُدْ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ مَدًّا حَتَّىٰ إِذَا رَأَوْا مَا يُوعَدُونَ إِمَّا الْعَذَابَ وَإِمَّا السَّاعَةَ فَسَيَعْلَمُونَ مَنْ هُوَ شَرٌّ مَّكَانًا وَأَضْعَفُ جُندًا ﴿٧٥﴾
75. Sema: aliye katika upotofu basi Mwingi wa rehema atampa muda mpaka ayaone aliyoahidiwa –Ama ni adhabu au ni saa. Hapo ndipo watajua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu
وَيَزِيدُ اللَّـهُ الَّذِينَ اهْتَدَوْا هُدًى وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ مَّرَدًّا ﴿٧٦﴾
76. Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wale walioongoka, Na mema yenye kubaki ni bora katika malipo mbele ya Mola wako na yana mwisho mwema.
LIPI KATI YA MAKUNDI MAWILI
Aya 73-76
MAANA
Na wanaposomewa Aya zetu zilizowazi, waliokufuru huwaambia walioamini: lipi katika makundi mawili lenye cheo kizuri na lililo bora barazani?
Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi ni dalili, makundi mawili ni waumi- ni na washirikina. Maana ni kuwa Mtume na maswahaba wanawapa washirikina hoja ya mantiki, kiakili na kimaumbile na wao wanajibu kwa mantiki ya tumbo na falsafa yake.
FALSAFA YA TUMBO
Epikouros alikuwa ni mwanafalsafa wa kiyunani (ugiriki) katika wanafunzi wa Aristatle, alikuwa na madhehebu yake peke yake yaliyotofautiana na wenzake na pia wale waliomtangulia.
Kwa ufupi anasema ladha ndio kheri kuu na machungu ndio shari kuu na kwamba thamani ya fadhila inategemea ladha za kimaana; kama ukweli, maisha ya utulivu na raha na pia ladha za kihisia; kama chakula na kinywaji...
Katika mwongozo wa falsafa hii anasema: Mtu asisukumwe na hawa yake na upendeleo wake kwenye ladha fupi itakayofuatiwa na machungu marefu.
Kwa maneno mengine ni kuwa, kwake yeye Epikouros – akiwa haamini ufufuo- ni kwamba kheri yote inakuwa kwenye ladha ya kidunia; ni sawa iwe kwenye tumbo au kwengineko. Kama itakutana na machungu basi linalozingatiwa ni wingi, lile lenye ladha nyingi litakuwa ni kheri na lenye machungu mengi basi ni shari.
Kuna falsafa ya kale inayoaifikiana na Epikouros kwamba kheri yote iko kwenye ladha ya dunia. Yeye anasema kheri iko kwenye ladha ya kimaana na kihisia pamoja nayo anasema kheri iko kwenye ladha ya tumbo na mengineyo ya hisia.
Miongoni mwa wenye falsafa hii ni Firauni na washirikina wa kiquraysh. Firauni alipinga utume wa Musa
, akaleta sababu ya kupinga kwake kwa kusema:
“Au mimi si bora kulio huyu aliye mnyonge wala hawezi kusema wazi. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu...” (43: 52 – 53)
Akasema tena:
فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
“Mimi Ndiye Mola wenu Mkubwa” (79:24).
Kisha akaendela:
أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾
“Kwani ufalme wa Misri si wangu na hii mito inapita chini yangu?” (43:51).
Makurishi nao, kama Firauni, walikanusha utume wa Muhmmad (s.a.w.) na wakatoa hoja kwa kusema:
لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ ﴿١٢﴾
“Mbona hakuteremshiwa hazina?” Juz;12 (11:12)
Falsafa hii haihusiki na Firauni na washirikina wa Makka tu, wala na watanuzi na wenye utajiri; isipokuwa inahusika na kila anayemuheshimu mtu na akampima kwa mali yake, basi yeye ni katika walioamini falsafa ya tumbo.
Miongoni mwa niliyoyasoma ni maneno ya kibaraka mmoja aliyesema: “Hawa wanaoilaumu Marekani na majeshi yake na wanavyowapiga wakombozi kila mahali na vile wanavyopora mali za wanyonge kila mahali, wamesahau au wanajitia kusahahu kuwa Marekani ina nguvu za kielimu na mali; na kwamba mwenye nguvu mpishe.”
Nilikuwa nikidhania kuwa falsafa ya tumbo ilikwisha kwenye zama za dhulma, lakini makala haya nilyoyasoma yamenifanya nitambue kuwa falsafa hii imekita mizizi kwenye nafsi za wapiga debe wa ukoloni na vibaraka wake.
Na karne ngapi tuliziangamiza zilizokuwa na mapambo mazuri zaidi na wazuri zaidi kwa mandhari?
Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:6)
Sema: aliye katika upotofu basi Mwingi wa rehema atampa muda mpaka ayaone aliyoahidiwa – ama ni adhabu au ni saa. Hapo ndipo watajua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake awaambie wale wanaoona kheri iko kwenye tumbo tu, kwamba hayo wanayojifaharisha nayo katika nafasi ya maisha waliyo nayo, kuwa ni mtihani wa Mwenyezi Mungu anowajaribu nao waja wake na anawapa muda mwingi.
Wakishukuru Mwenyezi Mungu atawapa thawabu na marejeo mazuri na wakizidi ukafiri na uasi basi atawasalitia ambaye atawatesa katika maisha haya ya duniani au atawaadhibu Mwenyezi Mungu huko Akhera. Huko watajua ni nani wenye hali mbaya, waumini walio mafukara au makafiri walio matajiri?
Lau mtu atamiliki kila kinacho chomozewa na jua, miliki hiyo si chochote kulinganisha na adhabu ya chini ya Jahannam. Amesema Amirul-mu’min, Aliy
: “Heri siyo kheri ikiwa baada yake ni moto; na shari si shari ikiwa baada yake ni Pepo, Na kila neema isiyokuwa Pepo ni kazi bure na kila balaa isiyokuwa moto ni nafuu.”
Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wale walioongoka
Hilo ni kwa kuwafahamisha hakika yao na sehemu za makosa na za sawa. Hii ni hidaya na neema kubwa.
Na mema yenye kubaki ni bora katika malipo mbele ya Mola wako na yana mwisho mwema.
Mema yanayobakia ni elimu na mambo ya manufaa. Hayo mawili ni bora kuliko mali na jaha. Kwa sababu yanadumu na kubakia manufaa yake na thawabu zake hazikatiki, lakini jaha na mali zinaisha na kuangamia.
أَفَرَأَيْتَ الَّذِي كَفَرَ بِآيَاتِنَا وَقَالَ لَأُوتَيَنَّ مَالًا وَوَلَدًا ﴿٧٧﴾
77. Je, umemuona aliyezikana ishara zetu na akasema: Hakika mimi nitapewa mali na watoto.
أَطَّلَعَ الْغَيْبَ أَمِ اتَّخَذَ عِندَ الرَّحْمَـٰنِ عَهْدًا ﴿٧٨﴾
78. Kwani yeye amepata habari za ghaibu au amechukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
كَلَّا سَنَكْتُبُ مَا يَقُولُ وَنَمُدُّ لَهُ مِنَ الْعَذَابِ مَدًّا ﴿٧٩﴾
79. Hapana! Tutaandika anayoyo asema na tutamkunjulia muda wa adhabu.
وَنَرِثُهُ مَا يَقُولُ وَيَأْتِينَا فَرْدًا ﴿٨٠﴾
80. Na tutamrithi hayo anayoyasema na atatufikia akiwa peke yake.
وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لِّيَكُونُوا لَهُمْ عِزًّا ﴿٨١﴾
81. Na wamechukua miungu mingine ili iwape nguvu.
كَلَّا سَيَكْفُرُونَ بِعِبَادَتِهِمْ وَيَكُونُونَ عَلَيْهِمْ ضِدًّا ﴿٨٢﴾
82. Sivyo kabisa! Wataikataa ibada yao na watakuwa ndio dhidiyao.
أَلَمْ تَرَ أَنَّا أَرْسَلْنَا الشَّيَاطِينَ عَلَى الْكَافِرِينَ تَؤُزُّهُمْ أَزًّا ﴿٨٣﴾
83. Kwani huoni kwamba tume-watuma mashetani kwa makafiri wawachochee kwa uchochezi.
فَلَا تَعْجَلْ عَلَيْهِمْ إِنَّمَا نَعُدُّ لَهُمْ عَدًّا ﴿٨٤﴾
84. Basi usiwafanyie haraka, Sisi tunawahisabia siku.
يَوْمَ نَحْشُرُ الْمُتَّقِينَ إِلَى الرَّحْمَـٰنِ وَفْدًا ﴿٨٥﴾
85. Siku tutakayowakusanya wenye takua kuwa ni wageni wa Mwingi wa rehema.
وَنَسُوقُ الْمُجْرِمِينَ إِلَىٰ جَهَنَّمَ وِرْدًا ﴿٨٦﴾
86. Na tutawachunga wahalifu kuwapeleka Jahannam hali ya kuwa na kiu
لَّا يَمْلِكُونَ الشَّفَاعَةَ إِلَّا مَنِ اتَّخَذَ عِندَ الرَّحْمَـٰنِ عَهْدًا ﴿٨٧﴾
87. Hawatakuwa na mamlaka ya uombezi ila wale waliochukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
JE, UMEMUONA ALIYEZIKANA ISHARA ZETU
Aya 77 – 87
MAANA
Je, umemuona aliyezikana ishara zetu na akasema: Hakika mimi nitapewa mali na watoto.
Imeelezwa katika Hadith na tafsiri kwamaba A’si bin Wail, mzazi wa Amru bin Al’as, aliposikia kuhusu utume, alisema kwa stihzai: Bila shaka mimi huko akhera nitapewa mali na watoto.
Lakini dhahiri ya tamko la Aya linaonyesha kuwa kuna mzandiki fulani aliyesema hivi; ama kuwataja watu majina, hiyo si katika njia ya Qur’an. Mfano wa Aya hii ni kauli ya yule mwenye kitalu aliyesema:
وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا ﴿٣٦﴾
“Na kama nitarudishwa kwa Mola wangu bila shaka nitapata marejeo bora zaidi Kuliko haya”Juz;15 (18:36).
Ameirudi Mwenyezi Mungu kauli hii kwa kusema:
Kwani yeye amepata habari za ghaibu au amechukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
Amepata wapi habari hizi? Au yeye ana funguo za siri au amechukua ahadi na Mwenyezi Mungu katika hilo?
Hapana
! si hivi wala hivyo; isipokuwa yeye ni kafiri muovu.Tutaandika anayoyasema na tutamkunjulia muda wa adhabu
Tumezihifadhi kauli zake na tutamzidishia adhabu zaidi ya kufuru yake na uzushi wake.
Na tutamrithi hayo anayoyasema na atatufikia akiwa peke yake,
akiwa mtupu na pia tutamnyng’anya mali na watoto alio nao, pale anapokufa na kuangamia na tutamfufua siku ya kiyama akiwa peke yake mtupu; sawa na tulivyomuumba mara ya kwanza.
Na wamechukua miungu mingine ili iwape nguvu. Sivyo kabisa!
Kwa sababu mwenye kutaka nguvu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi Mungu humvisha vazi la udhalili.
Wataikataa ibada yao na watakuwa ndio dhidi yao
Yaani hao wanawaabudu wataikataa ibada yao na watakuwa dhidi yao. Tafsiri inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli ya Imam Ali
katika Nahjulbalagha: Sio mbali anayefuatwa atajitenga na mfuasi na kiongozi na anayeongozwa watafarikiana kwa chuki na watalaaniana watakapokutana.
Mwenyezi Mungu naye amesema:
تَبَرَّأْنَا إِلَيْكَ مَا كَانُوا إِيَّانَا يَعْبُدُونَ ﴿٦٣﴾
“Tunajitenga nao mbele yako, Hawakuwa wakituabudu sisi” (28:63);bali walikuwa wakiabudu hawa zao na malengo yao.
Kwani huoni kwamba tumewatuma mashetani kwa makafiri wawa- chochee kwa uchochezi.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) haingilii kati baina yao na mashetani wanowapa wasiwasi na kuwahadaa na maasi, wala hajiingizi, kwa uweza wake wa kufanya, kumzuia shetani; isipokuwa amewabainishia njia ya kheri na shari na kuwapa uwezo kamili wa kutenda na kuwaacha; anawakataza hili na kuwaamrisha lile; kisha anawaachia hiyari katika watakayoyatenda na kuyaacha.
Kama angeliwanyanyag’anya utashi, basi wangelikuwa wao na miti ni sawa.
Basi usiwafanyie haraka. Sisi tunawahisabia siku.
Yaani, ewe Muhammad, usiwe na haraka ya kuangamia makafiri, kwani maangamizi yao yatakuja tu, lakini Mwenyezi Mungu anawangoja mpaka muda uliotajwa, ili avidhibiti vitendo vyao, kisha aje awalipe, wanayostahili. Kwani hakuna kheri ya kurefuka maisha isipokuwa kwa yule anayeamini na akatenda amali njema, lakini mwenye kukufuru na akafanya maovu, basi maisha yake ni balaa:
وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ خَيْرٌ لِّأَنفُسِهِمْ إِنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ لِيَزْدَادُوا إِثْمًا وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٧٨﴾
“Wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa ni kheri kwa nafsi zao, Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika dhambi na wana adhabu idhalilishayo.”Juz.4 (3:178).
Siku tutakyowakusanya wenye takua kuwa ni wageni wa Mwingi wa rehema.
Neno lililotumika katika kufasiri wageni limetokana na neno la kiarabu wafd lenye maana ya wageni wa heshima. Maana ni kuwa wale wanaomtii Mwenyezi Mungu, kesho watakuwa ni wageni wenye kutukuzwa.
Na tutawachunga wahalifu kuwapeleka Jahannam halia ya kuwa na kiu
Waumini watapata makaribisho ya heshima na wahalifu watapata makaribisho ya dharau, kuchungwa kama wanyama wanavyochungwa kwenda kunywa maji; ndivyo wahalifu nao watachungwa kupelekwa kwenye Jahannam.
Hawatakuwa na mamlaka ya uombezi ila wale waliochukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
Kila mwenye kutekeleza ahadi ya Mwenyeezi Mungu na wala asimfanyie hiyana kwenye dogo wala kubwa, basi Mwenyezi Mungu amempa ahadi ya kufuzu na kuokoka na uombezi:
وَأَوْفُوا بِعَهْدِي أُوفِ بِعَهْدِكُمْ وَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ ﴿٤٠﴾
“Na tekelezeni ahadi yangu nitatekeleza ahadi yenu”Juz;1(2:40)
وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَـٰنُ وَلَدًا ﴿٨٨﴾
88. Na wanasema Mwingi wa rehema anamwana.
لَّقَدْ جِئْتُمْ شَيْئًا إِدًّا ﴿٨٩﴾
89. Hakika mmeleta Jambo la kuchusha.
تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِنْهُ وَتَنشَقُّ الْأَرْضُ وَتَخِرُّ الْجِبَالُ هَدًّا ﴿٩٠﴾
90. Zinakurubia mbingu kutatuka kwa hilo na ardhi kupasuka na milima kuanguka vipande vipande
أَن دَعَوْا لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدًا ﴿٩١﴾
91. Kwa kudai kwao kuwa Mwingi wa rehema ana mwana.
وَمَا يَنبَغِي لِلرَّحْمَـٰنِ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا ﴿٩٢﴾
92. Hahitajii Mwingi wa rehema kuwa na mwana.
إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا ﴿٩٣﴾
93. Hakuna yeyote aliyemo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Mwingi wa rehema kuwa ni mtumwa.
لَّقَدْ أَحْصَاهُمْ وَعَدَّهُمْ عَدًّا ﴿٩٤﴾
94. Hakika amewadhibiti na amewahisabu sawa sawa.
وَكُلُّهُمْ آتِيهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَرْدًا ﴿٩٥﴾
95. Na kila mmoja kati yao atam fikia siku ya Kiyama peke yake
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَيَجْعَلُ لَهُمُ الرَّحْمَـٰنُ وُدًّا ﴿٩٦﴾
96. Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema Mwingi wa rehema atawajaalia mapenzi.
فَإِنَّمَا يَسَّرْنَاهُ بِلِسَانِكَ لِتُبَشِّرَ بِهِ الْمُتَّقِينَ وَتُنذِرَ بِهِ قَوْمًا لُّدًّا ﴿٩٧﴾
97. Hakika tumeifanya nyepesi, kwa ulimi wako ili uwabashirie kwayo wenye takua na uwaonye kwayo wabishi
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هَلْ تُحِسُّ مِنْهُم مِّنْ أَحَدٍ أَوْ تَسْمَعُ لَهُمْ رِكْزًا ﴿٩٨﴾
98. Na karne ngapi tumeziangamiza kabla yao, Je, unawaona hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao?
WANASEMA MWINGI WA REHEMA AMEJIFANYIA MWANA
Aya 88 – 98
MAANA
Na wao wanasema Mwingi wa rehema ana mwana. Hakika mmeleta jambo la kuchusha, Zinakurubia mbingu kutatuka kwa hilo na ardhi kupasuka na milima kuanguka vipande vipande kwa kudai kwao kuwa Mwingi wa rehema ana mwana.
Mwenyezi Mungu amewakemea sana wale waliomfanya Mwenyezi Mungu kuwa ana watoto wa kiume na mabinti na akawapa kiaga kwenye Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.1 (2:116), Juz.5 (4:48), Juz. 6 (4:171) na Juz. 7 (6:101).
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akataja hapa kauli yao hii kwa mfumo huu wa kutisha. Nao unafahamisha kuwa mtu anamchezea ambaye hachezewi na yeyote aliye mbinguni wala ardhini.
Binadamu anamchezea Muumba wake naye anaishi kwenye himaya yake, na anamnasibisha mambo ambayo kuyasikia tu yanaweza yakaipasua mbingu na ardhi na kuangusha milima.
Unaweza kuuliza
: kwanini hasira yote hii ya kilimwengu kwa sababu tu ya maneno ya kijinga na ya udhaifu wa akili?
Jibu
: Hasira yote hii, haiko kwa mtu au kikundi cha watu maalum; isipokuwa imetokana na shirki hii ambayo sasa imekuwa ni dini na itikadi wanayoifuata mamilioni, kizazi baada ya kizazi na mifano hii ya mungu mwan na mungu mama.
مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ ﴿٧٥﴾
“Masih mwana wa Maryam hakuwa ila ni Mtume, Wamepita kabla yake Mitume, Na mama yake ni mkweli, Wote wawili walikuwa wakila chaku- la”Juz; 6 (5:75).
Hahitajii Mwingi wa rehema kuwa na mwana.
Kwa sababu mwana anafanana na mzazi wake, na Mwenyezi Mungu hana aliyefanana naye. Na kwa sababu kuwa na mtoto ni kumuhitajia, na Mwenyezi Mungu amejitosheleza na walimwengu wote
Hakuna yeyote aliyomo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Mwingi wa rehema kuwa ni mtumwa.
Hakuna yeyote aliyeko chini au juu ila huwa ni mja wa Mwenyezi Mungu anayemilikiwa. Kimsingi ni kwamba mwenye kumilikiwa sio mtoto na mmliki sio baba.
Hakika amewadhibiti na amewahisabu sawa sawa na kila mmoja kati yao atamfikia siku ya Kiyama peke yake.
Waliodhibitiwa ni walio mbinguni na ardhini na atakyefikiwa ni Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu hapotewi na kujua kitu chochote katika ardhi wala katika mbingu na kwamba kila mmoja atakwenda kwa Mwenyezi Mungu siku ya kiyama akiwa peke yake, hana wa kumnusuru wala kumsaidia au kujisaidia yeye mwenyewe kwa wingi au uchache, sikwambii tena kumsadia mwenginewe. Ambaye atamjia Mwenyezi Mungu katika hali kama hiyo, anawezaje kuwa mtoto wake?
Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema Mwingi wa rehema atawajaalia mapenzi.
Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
anatia mapenzi katika nyoyo za waja wake kwa watu wenye imani na ikhlasi, si kwa chochote ila kwa kuthamini fadhila na hulka njema.
Muhammad bin Ahmad Alkalabiy, mwenye kitabu Attas-hil anasema: Inasemekana kuwa Aya hii ilishukwa kwa Aliy bin Abi Twalib. Sheikh Almaraghi, mmoja wapo wa masheikh wa Al-Azhar, anasema: ‘Ibin Mardaywyh na Dilamiy wamepokea kutoka kwa Baraa, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alimwambia Aliy: Sema ewe Mola wangu nijalie ahadi kwako na unijaalie mapenzi katika nyoyo za waumini’ ndipo ikashuka Aya hii”.
WANASWARA NA BANI HASHIM
Amesema Abu Hayani Al-andalusi katika tafsir yake Albahrul-Muhit: “Aya hii ilishuka kwa Aliy bin Abi Twalib na amesema Muhammad Alhanafiya: huwezi kumpata mumin ila anampenda Aliy. Maajabu ni yale aliyotueleza Imam wa lugha Ridhad Din, Abu Abdillah Muhammad bin Aliy bin Yusuf Al-Answariy Ashatibiy kuhusu aliyosema, ibn Is-haq Mnaswara:
• Uday na Taym kwa ubaya kamwe sitothubutu kuwataja
• Lakini naona ni vibaya Ali kulaumiwa na waja
• Mimi ni mpenzi wa dhuriya ya Hashimu na wanawe pamoja
• Naswira watukufu kupambiya kwa nini imekuwa ni kioja
• Tawaambiya huku kiusiya moyo wangu umekwisha wachuja
• Kupenda nifuraha nawambiya hata wanyama pia wangoja.
Hakika tumeifanya nyepesi, kwa ulimi wako ili uwabashirie kwayo wenye takua na uwaonye kwayo wabishi.
Yaani Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur’an kwa lugha ya kiarabu ili iwe wepesi kuijua na kufahamu maana yake na iwe ni habari njema kwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na onyo kwa mwenye kukufuru na akafanya uovu. Umepita mfano wake katika Juz. 12 (12:2)
Na karne ngapi tumeziangamiza kabla yao, Je, unawaona hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao?
Yaani Mwenyezi Mungu amewaangamiza mpaka wa mwisho wao. Umetangulia mfano wake katika Aya ya 84 ya sura hii; na Juz, 15 (17:17).
MWISHO WA SURA YA KUMI NA TISA