9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
قَالَ أَجِئْتَنَا لِتُخْرِجَنَا مِنْ أَرْضِنَا بِسِحْرِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٥٧﴾
57. Akasema: Ewe Musa! Hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
فَلَنَأْتِيَنَّكَ بِسِحْرٍ مِّثْلِهِ فَاجْعَلْ بَيْنَنَا وَبَيْنَكَ مَوْعِدًا لَّا نُخْلِفُهُ نَحْنُ وَلَا أَنتَ مَكَانًا سُوًى ﴿٥٨﴾
58. Basi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe ambayo hatutaivunja sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.
قَالَ مَوْعِدُكُمْ يَوْمُ الزِّينَةِ وَأَن يُحْشَرَ النَّاسُ ضُحًى ﴿٥٩﴾
59. Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri
فَتَوَلَّىٰ فِرْعَوْنُ فَجَمَعَ كَيْدَهُ ثُمَّ أَتَىٰ ﴿٦٠﴾
60. Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ وَيْلَكُمْ لَا تَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا فَيُسْحِتَكُم بِعَذَابٍ وَقَدْ خَابَ مَنِ افْتَرَىٰ ﴿٦١﴾
61. Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.
فَتَنَازَعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ وَأَسَرُّوا النَّجْوَىٰ ﴿٦٢﴾
62. Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe na wakanon’gona kwa siri.
قَالُوا إِنْ هَـٰذَانِ لَسَاحِرَانِ يُرِيدَانِ أَن يُخْرِجَاكُم مِّنْ أَرْضِكُم بِسِحْرِهِمَا وَيَذْهَبَا بِطَرِيقَتِكُمُ الْمُثْلَىٰ ﴿٦٣﴾
63. Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao na waondoe njia yenu iliyo bora.
فَأَجْمِعُوا كَيْدَكُمْ ثُمَّ ائْتُوا صَفًّا وَقَدْ أَفْلَحَ الْيَوْمَ مَنِ اسْتَعْلَىٰ ﴿٦٤﴾
64. Kwa hiyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa hakika leo atafuzu atakayeshinda.
FIRAUNI ANAWAKUSANYA WACHAWI
Aya 57 – 64
MAANA
Akasema: Ewe Musa! Hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
Firauni aligongwa na hoja asizoweza kuzijibu alipokabiliana na Musa. Vipi ataweza kuzijibu nazo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu? Firauni alikuwa akijua wazi kuwa Musa na Harun si wachawi na kwamba uchawi hauwezi kumtoa mtu nchini mwake na kwenye ufalme wake.
Kama wachawi wangelikuwa na uwezo huu basi wangelikuwa ndio watawala kila wakati na kila mahali. Lakini Firauni aliposhindwa kujibu mapigo, alikimbila hila, ujanja ujanja, uwongo na uzushi; sawa wanavyofanya leo wakoloni na vibaraka wao, wanapowaita wakombozi kuwa ni waharibifu na wenye nia safi kuwa ni wafanya fujo.
Basi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Weka miadi baina yetu na wewe ambayo hatutaivunja sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.
Firauni alimtaka Musa apange siku ya mapambano baina yake na wachawi, yawe mahali palipo wazi kila mtu aweze kuona mapambano hayo na kuyafuatilia.
Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri.
Musa alichagua siku ya sikukuu ndio iwe mapambano baina yake na wachawi, ambapo watu hawatakuwa na kazi waweze kukusanyika na akachaguwa wakati baina ya asubuhi na mchana, kwa vile ndio wakati mzuri wa kukusanyika watu; huku akiwa anataka kuidhihirisha haki na kuivunja batili.
Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
Aya hii pamoja na ufupi wake ina ubainifu mkubwana na inachukua maana nyingi. ‘Akarudi, akatengeneza, akaja’ Neno akarudi, linaelezea kuondoka Firauni kwenda kwa wasaidizi wake na kushauriana kupanga mipango.
Neno akatengeneza linaelezea kutuma wajumbe katika pembe zote za nchi kutafuta wachawi na kuwaleta. Mshauri wake alimshauri afanye hivyo; kama inavyoashiria Aya katika Juz. 9 (7:112). Na neno akaja, linaelezea kuja kwake na majigambo yake kwenye uwanja wa mapambano.
Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.
Musa alitanguliza nasaha na onyo kwa wachawi kabla ya kuanza kazi yoyote ya uchawi na akawahadharisha na kuondolewa mbali na adhabu kama wataendele kuwadanganya watu na kuwavunga; kisha akawafahamisha kuwa kadiri Firauni alivyo na nguvu ya utawala, lakini ni mdhaifu sana wa kuweza kuwadhuru au kuwanufaisha.
Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe na wakanon’gona kwa siri.
Waliozozana ni wachawi. Aya hii inaashiria kuwa baadhi ya wachawi waliathirika na maneno ya Musa au angalau waliingia shaka. Katika Tafsir Aya hii inaashiria kwamba baadhi ya wachawi waliathirika na maneno ya Musa
, Au angalau yalitia shaka katika nafsi zao. Katika Attabariy imeelezwa kuwa wachawi walisema kutokana na tahadhari ya Musa kuwa maneno haya siyo ya mchawi.
Ni kweli kwamba maneno yakitoka kwenye moyo wa mwenye ikhlasi huchukua mkondo kuelekea kwenye moyo wa mwenye ikhlasi. Waliathirika baadhi ya wachawi kwa mawaidha ya Musa, wakaanza kupingana wenyewe, Kama kawaida yalipita majadiliano kuwa je, waendelee au wasiendelee.
Majadiliano haya yalipita kwa siri asisikie Musa wala Firauni. Lakini mwisho walioshinda ni wale waliong’ang’ania kuendelea na upinzani, kwa dalili ya alivyowasimulia Mwenyezi Mungu:
Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao na waondoe njia yenu iliyo bora. Kwa hiyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa hakika leo atafuzu atakayeshinda.
Maneno yote haya ni ya wachawi na hawa wawili wanawakusudia Musa na Harun. Makusudio ya njia iliyo bora ni dini, kwa dalili ya Aya nyingine isemayo:
“Na Firauni akaema: Niacheni nimuuwe Musa naye amwite Mola wake, mimi nahofia asije kuwabadilishia dini yenu”
(40:26).
Maana ni kuwa baadhi ya wachawi walisema kuwa Musa na Haruna ni mahodari katika fani ya uchawi kwa hiyo wanataka watushinde ili waimalize dini yetu wabakie wao ndio mabwana katika miji na wawatawale watu wawe watumwa wao.
Kwa hiyo basi hatuna budi tuwe na mshikamano dhidi yao na tutoe juhudi zetu zote ili tuwashinde, tuwe na cheo siku hii ya leo inayoshuhudiwa.
قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَن تُلْقِيَ وَإِمَّا أَن نَّكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَلْقَىٰ ﴿٦٥﴾
65. Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?
قَالَ بَلْ أَلْقُوا فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ ﴿٦٦﴾
66. Akasema; bali tupeni nyinyi! Mara kamba zao na fimbo zao zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.
فَأَوْجَسَ فِي نَفْسِهِ خِيفَةً مُّوسَىٰ ﴿٦٧﴾
67. Basi Musa akaingia hofu katika nafsi yake.
قُلْنَا لَا تَخَفْ إِنَّكَ أَنتَ الْأَعْلَىٰ ﴿٦٨﴾
68. Tukasema; usihofu hakika wewe ndiye utakayeshinda.
وَأَلْقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلْقَفْ مَا صَنَعُوا إِنَّمَا صَنَعُوا كَيْدُ سَاحِرٍ وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ ﴿٦٩﴾
69. Na kitupe kilicho kuumeni kwako, kitavimeza walivyovitengeneza, hakika walivyovitengeneza ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote aendapo.
فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سُجَّدًا قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ هَارُونَ وَمُوسَىٰ ﴿٧٠﴾
70. Basi wachawi wakaangushwa kusujudi. Wakasema:tumemwamini Mola wa Haruna na Musa!
قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ فِي جُذُوعِ النَّخْلِ وَلَتَعْلَمُنَّ أَيُّنَا أَشَدُّ عَذَابًا وَأَبْقَىٰ ﴿٧١﴾
71. Akasema: Mumemwamini kabla sijawapa ruhusa! Hakika huyo ni mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasu- lubu kwenye vigogo vya mitende. Na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi ni mkali wa adhabu na kuiendeleza?
قَالُوا لَن نُّؤْثِرَكَ عَلَىٰ مَا جَاءَنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالَّذِي فَطَرَنَا فَاقْضِ مَا أَنتَ قَاضٍ إِنَّمَا تَقْضِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٧٢﴾
72. Wakasema: Hatutaathirika nawe katika ishara waziwazi zilizotujia na yule aliyetuumba. Basi hukumu utakavyohukumu; kwani wewe unahukumu maisha haya ya duniani tu
إِنَّا آمَنَّا بِرَبِّنَا لِيَغْفِرَ لَنَا خَطَايَانَا وَمَا أَكْرَهْتَنَا عَلَيْهِ مِنَ السِّحْرِ وَاللَّـهُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿٧٣﴾
73. Hakika sisi tumemwamini Mola wetu ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na mwenye kudumu zaidi.
إِنَّهُ مَن يَأْتِ رَبَّهُ مُجْرِمًا فَإِنَّ لَهُ جَهَنَّمَ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ ﴿٧٤﴾
74. Hakika atakayemjia Mola wake naye ni mhalifu, basi kwa hakika yake ni Jahannamu, Hafi humo wala haishi.
وَمَن يَأْتِهِ مُؤْمِنًا قَدْ عَمِلَ الصَّالِحَاتِ فَأُولَـٰئِكَ لَهُمُ الدَّرَجَاتُ الْعُلَىٰ ﴿٧٥﴾
75. Na atakayemjia naye ni mumin aliyetenda mema basi hao ndio wenye daraja za juu
جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَذَٰلِكَ جَزَاءُ مَن تَزَكَّىٰ ﴿٧٦﴾
76. Bustani za milele zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa.
BAINA YA MUSA NA WACHAWI
Aya 65 – 76
MAANA
Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa? Akasema; bali tupeni nyinyi! Mara kamba zao na fimbo zao zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:113).
Basi Musa akaingia hofu katika nafsi yake.
Wafasiri wengi wamesema kuwa Musa alihofia nafsi yake, kama ilivyo kawaida ya maumbile, lakini ilivyo hasa hakuhofia nafsi yake. Vipi iwe hivyo naye anajua kuwa wachawi ni wazushi na kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia yeye na nduguye kuwa mimi niko pamoja nanyi! Ispokuwa alihofiwa mambo yasivurugike na watu wakachanganyikiwa wakadanganyika na uchawi.
Tukasema; usihofu hakika wewe ndiye utakayeshinda.
Usihofu kuwa watu watachanganyikiwa, hapana! Macho na akili zitafunukiwa kuwa wewe uko katika haki na wao ni wabatilifu; hata wachawi wenyewe watakiri kuwa wewe ni mkweli mwaminifu na kwamba wao ni wazushi, wenye vitimbi na hadaa; na Firauni ndiye aliyewalazimisha.
Na kitupe kilicho kuumeni kwako, kitavimeza walivyovitengeneza, hakika walivyovitengeneza ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote aendapo, Basi wachawi wakaangushwa kusujudi. Wakasema: tumemwamini Mola wa Haruna na Musa! Akasema: mumemwamini kabla sijawapa ruhusa! Hakika huyo ni mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu kwenye vigogo vya mitende. Na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi ni mkali wa adhabu na kuiendeleza?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:117)
Wakasema: Hatutaathirika nawe katika ishara waziwazi zilizotujia na yule aliyetuumba.
Firauni alitaka wachawi wamwache Mwenyezi Mungu wamfuate yeye baada ya kufunukiwa na upotevu wake. Wakasema ni kitu gani basi kinaweza kutuathiri! Je, ni hiyo dunia yako, ambayo hata wewe mwenyewe utaiacha, au ni vitisho vyako na adhabu yako, na hali adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kubwa na kali?
Basi hukumu utakavyohukumu
: Sisi hatuogopi vitisho vyako na mateso yako maadamu tuna yakini na Mola wetu;kwani wewe unahukumu maisha haya ya duniani tu,
yawe tamu au chungu. Na sisi si watoto wa dunia isipokuwa ni wa Akhera, ambayo itabaki na wala wewe huna mamlaka huko hata ya kujitetea wewe mwenyewe.
Hivi ndivyo anavyokuwa kila mwenye ikhlasi, haogopi upanga wa wachinjaji kwa ajili ya dini yake na misimamo yake. Ni muhali kabisa kuishi dini au misimamo yoyote ikiwa hakuna watu wa aina hii.
Hakika sisi tumemwamini Mola wetu ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na mwenye kudumu zaidi kuliko wewe Firauni.
Mapambano yalikuwa yanaonyesha kuwa ni baina Musa na wachawi, lakini kiuhakika hasa yalikuwa ni baina ya chama cha Mwenyezi Mungu na cha shetani.
Katika raundi ya kwanza tu walishuhudia watazamaji, akiwe- mo Firauni na wachawi, kuwa chama cha Mwenyezi Mungu ndio mshindi. Wachawi wakatangaza kuwa wao wamehakikisha haya kwa ujuzi usio na shaka. Na kwamba wao walikuwa kwenye upotevu kwa kumpinga Musa; na Firauni ndiye aliyewaelekeza hayo na kuwalazimisha, Wakamwomba msamaha Mwenyezi Mungu.
Kuomba msamaha kwa wachawi ni dalili wazi kuwa mchawi hana nguvu yoyote; isipokuwa ni kuvungavunga na upotevu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: ‘zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.’
Hakika atakayemjia Mola wake naye ni mhalifu, basi kwa hakika, yake ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi.
Hili ni fumbo la kudumu na adhabu. Mfano wake ni Aya isemayo: “Hawatamalizwa wakafa wala hawatapunguziwa adhabu yake. (35:36).
Neno mhalifu linatumika kwa kila mwenye kufanya ufisadi na uovu katika kauli au vitendo; awe kafiri au asiwe kafiri. Dalili ya kuwa makusudio ya mhalifu yanaenea ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na atakayemjia naye ni mumin aliyetenda mema basi hao ndio wenye daraja za juu
ambapo amekutanisha imani na matendo mema. Maana yake ni kuwa imani bila ya matendo haimnufaishi mwenye nayo.
Kwa maneno mengine ni kuwa waumini ni wale walio wema katika makusudio yao na matendo yao. Ama wale wanaohangaika katika ardhi kufanya ufisadi wao wako katika kundi la wahalifu; hata kama wataijaza ardhi kwa tahlili na takbir.
Bustani za milele zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa
Bustani (Pepo) na daraja za juu mbele ya Mwenyezi Mungu ni za wale waliozitakasa nafsi zao kwa mapenzi na ikhlasi kwa watu wote na kuzitwaharisha na kila aina ya khiyana tamaa na karaha. Kuna mamia ya Aya zenye maana hii kwa uwazi na kwa ishara.
وَلَقَدْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَسْرِ بِعِبَادِي فَاضْرِبْ لَهُمْ طَرِيقًا فِي الْبَحْرِ يَبَسًا لَّا تَخَافُ دَرَكًا وَلَا تَخْشَىٰ ﴿٧٧﴾
77. Na tulimpa wahyi Musa: Toka usiku na waja wangu na uwapigie njia kavu baharini, usikhofu kukamatwa wala usiogope.
فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ بِجُنُودِهِ فَغَشِيَهُم مِّنَ الْيَمِّ مَا غَشِيَهُمْ ﴿٧٨﴾
78. Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake, Basi kiliwafudikiza baharini kilichowafudikiza.
وَأَضَلَّ فِرْعَوْنُ قَوْمَهُ وَمَا هَدَىٰ ﴿٧٩﴾
79. Na Firauni aliwapoteza watu wake na hakuwaongoza.
يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ قَدْ أَنجَيْنَاكُم مِّنْ عَدُوِّكُمْ وَوَاعَدْنَاكُمْ جَانِبَ الطُّورِ الْأَيْمَنَ وَنَزَّلْنَا عَلَيْكُمُ الْمَنَّ وَالسَّلْوَىٰ ﴿٨٠﴾
80. Enyi wana wa israil! Hakika tuliwaokoa na adui yenu! Na tukawaahidi upande wa kuume wa mlima. Na tukawateremshia Manna na Salwa
كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَلَا تَطْغَوْا فِيهِ فَيَحِلَّ عَلَيْكُمْ غَضَبِي وَمَن يَحْلِلْ عَلَيْهِ غَضَبِي فَقَدْ هَوَىٰ ﴿٨١﴾
81. Kuleni katika vizuri tulivyowaruzuku, wala msipituke mipaka katika hayo isije ikawashukia ghadahabu yangu, Na inayemshukia ghadahabu yangu basi huyo amepotea.
وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ ﴿٨٢﴾
82. Hakika mimi ni mwingi wa maghufira kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema tena akaongoka.
WAPIGIE NJIA
Aya 77 – 82
MAANA
Na tulimpa wahyi Musa: Toka usiku na waja wangu na uwapigie njia kavu baharini, usikhofu kukamatwa wala usiogope.
Firauni aling’ang’ania inadi yake na akataa kila kitu isipokuwa kiburi na ujabari na kumpa sifa Musa kuwa ametoka nje na ni mchawi. Akapata wa kumuunga mkono katika hilo:
وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ أَتَذَرُ مُوسَىٰ وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ ﴿١٢٧﴾
“Na wakasema wakuu wa kaumu ya Fir’aun: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi.” Juz. 9 (7:127)
Firauni alishikilia kutaka kumuua Musa, ndipo Mwenyezi Mungu akampa wahyi atoke Misr usiku pamoja na wana waisrail na apige bahari kwa fimbo yake ipasuke itokee njia waifuate waisrail hadi upande mwengine wasalimike na maangamizi na Firauni na shari yake:
فَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ ﴿٦٣﴾ وَأَزْلَفْنَا ثَمَّ الْآخَرِينَ ﴿٦٤﴾ وَأَنجَيْنَا مُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَجْمَعِينَ ﴿٦٥﴾ ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ ﴿٦٦﴾
“Tulimletea wahyi Musa tukamwambia piga bahari kwa fimbo yako, Basi ikatengana, na kila seemu ikawa kama mlima mkubwa, Na tukawajongeza hapo wale wengine, Na tukamwokoa Musa na waliokuwa pamoja naye, Kisha tukawazamisha hao wengine” (26: 63 – 66).
Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake; Basi kiliwafudikiza baharini kilichowafudikiza.
Kusema kiliwafudikiza kilichowafudikiza ni kulikuza jambo. Hapo kuna maneno mengi ya kukadiriwa; kama ilivyo kawaida ya Qur’an. Kwa sababu mfumo wa maneno unafahamisha hivyo.
Kukadirwa kwake ni: Musa alitoka na watu wake usiku. Alipofika baharini akapiga kwa fimbo yake na bahari ikapasuka kukawa na njia isiyokuwa na maji, wakaifuata waisrail. Firauni na jeshi lake wakawaandama. Walipofika waisrail upande wa pili na mjeshiya Firauni kuingia yote, bahari ilirudi wakafamaji wote na waisraili wakasalimika wote.
Na Firauni aliwapoteza watu wake na hakuwaongoza.
Aliwapoteza na haki na akawapoteza baharini vilevile. Hapo mwanzo alikuwa akiwaambia:
وَمَا أَهْدِيكُمْ إِلَّا سَبِيلَ الرَّشَادِ ﴿٢٩﴾
“Wala siwaongozi ila kwenye njia ya uongofu” (40:29)
Enyi wana wa israil! Hakika tuliwaokoa na adui yenu!
Firauni aliyekuwa akiwapa adhabu mbaya ya kuwachinja watoto wenu wa kiume na kuwaacha wanawake.
Na tukawaahidi upande wa kuume wa mlima.
Anaishiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) ahadi aliyomwahidi Musa baada ya kufa maji Firauni, Ahadi yenyewe ni kwenda Musa upande wa mlimani, ateremshiwe Tawrat, amabayo ndani yake mna ubainifu wa sharia na hukumu.
Na tukawateremshia Manna na Salwa: Kuleni katika vizuri tulivyowaruzuku
Umetangulia mfano wake, kwa herufi zake, katika Juz. 1 (2:57)
Wala msipituke mipaka katika hayo isije ikawashukia ghadahabu yangu. Na inayemshukia ghadahabu yangu basi huyo amepotea.
Katika hayo ni hayo tuliyowaruzuku. Kupetuka mpaka katika hayo, ni kuchukua au kutoa kwa njia isiyokuwa yake ya kisharia.
Maana ni kuwa mwenye kuchuma mali kwa njia isiyokuwa ya halali au kuitumia kwa njia isiyokuwa ya halali, basi malipo yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni maangamizi na adhabu ya kuunguza; sawa na Firauni na wengineo katika waasi walio mataghuti.
Hakika mimi ni mwingi wa maghufira kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema tena akaongoka.
Mwenyezi Mungu husamehe madhambi kwa masharti mane:
1. Kwanza: kutubia nako ni kujuta kwa maasi yaliyokuwa pamoja na kuomba msamaha.
2. Pili: kuiamini haki, popote itakapokuwa na itakavyokuwa; ni sawa iafikiane na malengo yake au yahalifiane.
3. Tatu: kuitumia haki. Kwani imani bila ya matendo ni kama matamshi bila ya maana.
4. Nne: ni kuongoka. Makusudio yake ni kuendelea kuifuata haki mpaka kufa. Na hapa ndio tunapata jibu la mwenye kuuliza kuwa, kuna haja gani ya kuunganisha mwenye kuongoka na mwenye kuamini na akatenda mema.