11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
كَذَٰلِكَ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَاءِ مَا قَدْ سَبَقَ وَقَدْ آتَيْنَاكَ مِن لَّدُنَّا ذِكْرًا ﴿٩٩﴾
99. Namna hivi tunakuhadithia katika habari za yaliotangulia, Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha.
مَّنْ أَعْرَضَ عَنْهُ فَإِنَّهُ يَحْمِلُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وِزْرًا ﴿١٠٠﴾
100. Atakayejitenga nayo basi hakika siku ya Kiyama atabeba mzigo.
خَالِدِينَ فِيهِ وَسَاءَ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حِمْلًا ﴿١٠١﴾
101. Watadumu humo. Ni mzigo muovu kwao kuubeba siku ya Kiyama!
يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ وَنَحْشُرُ الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ زُرْقًا ﴿١٠٢﴾
102. Siku itakayopulizwa parapanda na tutawakusanya wahalifu siku hiyo wakiwa buluu.
يَتَخَافَتُونَ بَيْنَهُمْ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا عَشْرًا ﴿١٠٣﴾
103. Watanong’onezana wao kwa wao: ‘Hamkukaa ila siku kumi tu.
نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ إِذْ يَقُولُ أَمْثَلُهُمْ طَرِيقَةً إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا يَوْمًا ﴿١٠٤﴾
104. Sisi tunayajua zaidi watakayoyasema, atakaposema mbora wao kwa mwendo: ‘Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.’
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْجِبَالِ فَقُلْ يَنسِفُهَا رَبِّي نَسْفًا ﴿١٠٥﴾
105. Wanakuuliza kuhusu milima. Sema: Mola wangu ataivurugavuruga.
فَيَذَرُهَا قَاعًا صَفْصَفًا ﴿١٠٦﴾
106. Ataiwacha tambarare iliyo sawa sawa.
لَّا تَرَىٰ فِيهَا عِوَجًا وَلَا أَمْتًا ﴿١٠٧﴾
107. Hutaona humo mabonde wala miinuko.
يَوْمَئِذٍ يَتَّبِعُونَ الدَّاعِيَ لَا عِوَجَ لَهُ وَخَشَعَتِ الْأَصْوَاتُ لِلرَّحْمَـٰنِ فَلَا تَسْمَعُ إِلَّا هَمْسًا ﴿١٠٨﴾
108. Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu, na sauti zote zitamnyenyekea Mwingi wa rehma. Basi hutasikia ila mnong’ono.
يَوْمَئِذٍ لَّا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَرَضِيَ لَهُ قَوْلًا ﴿١٠٩﴾
109. Siku hiyo uombezi hautafaa ila wa aliyemruhusu Mwingi wa rehema na akamridhia kusema.
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا ﴿١١٠﴾
110. Anayajua yalio mbele yao na yalio nyuma yao, wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَيِّ الْقَيُّومِ وَقَدْ خَابَ مَنْ حَمَلَ ظُلْمًا ﴿١١١﴾
111. Zitanyenyenyekea nyuso kwa Aliye hai, Mwangalizi Mkuu, Na hakika ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
وَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا يَخَافُ ظُلْمًا وَلَا هَضْمًا ﴿١١٢﴾
112. Na mwenye kutenda mema naye ni mumin, hatahofu dhulma wala kupunjwa.
KAMA HIVYO TUNAKUSIMULIA
Aya 99 – 112
MAANA
Namna hivi tunakuhadithia katika habari za yaliotangulia.
Mwenyezi Mungu anaashiria kisa cha Musa
na habari zake, Maneno hayo anaambiwa Muhammad(s.a.w.w)
. Neno ‘katika’ ni kuelezea baadhi; yaani tunakusimulia baadhi ya habari za umma uliotangulia, kama ulivyosikia. Nazo ni mazingatio na mawaidha kwa watu. Wakati huo huo zinafahamisha ukweli wako na utume wako. Kwa sababu ni habari za ghaibu.
Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha.
Makusudio ya mawaidha hapa ni Qur’an. Imeitwa hivyo kwa sababu ndani yake kuna utajo wa Mwenyezi Mungu na sifa zake, mitume na habari zao, akhera na mambo yake, imani na ukafiri, kheri na shari, halali na haramu, kuumbwa mbingu na ardhi na mengineyo.
Atakayejitenga nayo basi hakika siku ya Kiyama atabeba mzigo.
Kila mwenye kuipinga Qur’an kwa kauli na vitendo au kwa vitendo bila ya kauli, basi atakuwa amejitenga nayo na atakuwa ameibebesha nafsi yake mzigo mzito. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema: “Hakuiamini Qur’an yule anayehalalisha yaliyo haramu” Yatakuja maelezo zaidi kwenye Aya ya 124 ya Sura hii, inshaallah.
Watadumu humo.
Yaani humo mwenye mizigo, Adhabu kuiita mizigo ni katika kutumia sababu kwa msabibishi.
Ni mzigo muovu kwao kuubeba siku ya Kiyama!
Yaani mzigo wa madhambi walioubebesha nafsi zao kwa sababu ya kujtenga kwao na Qur’an.
Siku itakayopulizwa parapanda.
Hiki ni kinaya cha kufufuliwa walioko makaburini.
Na tutawakusanya wahalifu siku hiyo wakiwa buluu.
Hii pia ni kinaya cha kufazaika kwao na hali mbaya watakayokuwa nayo. Ya kushangaza ni yale niliyoyasoma katika Tafsir Al-Bahru-Muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi, akisema: “Makusudio ya ubuluu ni ubuluu wa macho, na macho ya buluu yanachukiza sana kwa waarabu kwa sababu maadui zao waroma wana macho ya buluu.” Mfasiri huyu alikuwa karibu na wakati wa vita vya msalaba (Crusade).
Watanong’onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu.
Miongoni mwa sifa za wahalifu siku ya Kiyama nikuwa wao kutokana na vituko watakavyopambana navyo, watasahau muda wa kukaa kwao katika maisha ya dunia.
Kwa hiyo wataambiana kwa lugha ya maneno au kwa lugha ya hali kwa sauti ya chini: Hatukukaa ispokuwa siku kumi au masaa kadhaa au kitambo kidogo tu.
Unaweza kuuliza
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya hii, amewazungumzia kuwa watasema tumekaa siku kumi, katika Sura Kahf, Aya 19 amesema, siku moja au sehemu ya siku; na katika Sura Rum, Aya 55, watasema kuwa hawakukaa ispokuwa saa moja. Je, kuna wajihi gani wa kuchanganya Aya zote hizo?
Razi amejibu kuwa baadhi ya wahalifu wataona ni siku moja wengine kumi. Tuonavyo sisi ni kuwa neno kumi, siku au saa katika Aya sio kuzungumzia kauli halisi ya wahalifu; ispokuwa ni kinaya cha vile watakavyowazia uchache wa muda na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hayo ameyaletea ibara ya kumi, mara nyingine siku na hata saa. Mwenyezi Mungu ameyaashiria haya kwa kauli yake: “Siku atakayowaita nanyi mkamwitikia kwa kumsifu. Na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mchache tu.” Juz.15 (17:52).
Sisi tunayajua zaidi watakayoyasema, atakaposema mbora wao kwa mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.
Mbora wao kwa mwendo ni yule mwenye sera nzuri na mwenye kujua hakika ya mambo. Maana ni kuwa wakati wanapoambiana kuwa tumekaa siku kumi tu, huyo mbora wao atawaambia: Maisha mliyokuwa nayo mkishindana, si chochote ispokuwa ni kama ndoto tu, hayawezi kuhisabiwa kwa wakati wala kwa siku. Maisha ya uhakika hasa ni haya tuliyo nayo hivi sasa, ambayo hayana muda wala mwisho.
Wanakuuliza kuhusu milima, Sema: Mola wangu ataivurugavuruga. Ataiwacha tambarare iliyo sawasawa, Hutaona humo mabonde wala miinuko.
Muulizaji alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kuwa vipi milima itakavyokuwa siku ya kiyama? Mwenyezi Mungu akamwambia mtume wake Mtukufu: mjibu Aliyeuliza sawali hili kuwa Mwenyezi Mungu ataing’oa na ataigeuza kuwa ni mavumbi yatakayotawanyika angani na pale ilipokuwa patakuwa tambarare bila ya mabonde wala miinuko.
Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu.
Siku hiyo ni siku ya Kiyama, watakofuata ni viumbe na muitaji ni yule atakayewaita viumbe kwenye mkusanyiko, hisabu na malipo. Maana ni kuwa mwito utakuwa wa haki na utaitikiwa na wote, hakuna atakayeweza kuuhalifu: “Siku atakapoita muitaji kuliendea jambo linalochusha; macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika; wanamkimbilia muitaji na makafiri watasema: Hii ni siku ngumu. (54:6-9).
Na sauti zote zitamnyenyekea Mwingi wa rehma. Basi hutasikia ila mnong’ono.
Makusudio ya sauti ni wenye sauti hizo, Na mnong’ono unafahamisha unyenyekevu.
Siku hiyo uombezi hautafaa ila wa aliyemruhusu Mwingi wa rehema na akamridhia kusema.
Hii iko katika maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala hawaombei ila yule Aliemridhia” (21:28). Tumeazungumzia shafaa kwa urefu katika Juz; 1 (2:97).
Anayajua yalio mbele yao na yalio nyuma yao wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:255).
Zitanyenyenyekea nyuso kwa Aliye hai, Mwangalizi Mkuu.
Makusudio ya nyuso ni walio na nyuso hizo. Maana ni kuwa viumbe wote kesho watasalimu amri mbele ya Aliye hai, asiyekufa na Msimamizi wa kila jambo wala hakuna kinachosimamiwa ila kwa ajili yake.
Na hakika ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
Mwenye hasara zaidi katika watu kesho ni yule mwenye kuwadhulumu watu na akaingilia heshima na uhuru wao. Na mwenye faida mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye kufanya kwa ajili ya kheri ya binadamu na masilahi kwa njia ya kheri na ya ubinadamu.
Na mwenye kutenda mema naye ni mumin, hatahofu dhulma wala kupunjwa.
Hii ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni mumin tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.” Juz; 14 (16: 97).
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا وَصَرَّفْنَا فِيهِ مِنَ الْوَعِيدِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ أَوْ يُحْدِثُ لَهُمْ ذِكْرًا ﴿١١٣﴾
113. Namna hiyo tumeiteremsha Qur’an kwa lugha ya kiarabu na tumekariri humo maonyo ili wawe na takua au iwaletee makumbusho.
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾
114. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki, Wala usiifanyie haraka hii Qur’an kabla haujamalizika wahyi wake, Na sema: Mola wangu! Nizidishie elimu.
وَلَقَدْ عَهِدْنَا إِلَىٰ آدَمَ مِن قَبْلُ فَنَسِيَ وَلَمْ نَجِدْ لَهُ عَزْمًا ﴿١١٥﴾
115. Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau wala hatukuona kwake azma.
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ ﴿١١٦﴾
116. Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu wote ispokuwa Iblisi alikataa.
فَقُلْنَا يَا آدَمُ إِنَّ هَـٰذَا عَدُوٌّ لَّكَ وَلِزَوْجِكَ فَلَا يُخْرِجَنَّكُمَا مِنَ الْجَنَّةِ فَتَشْقَىٰ ﴿١١٧﴾
117. Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo, Basi asiwatoe katika Bustani (Pepo) hii, mkaingia mashakani.
إِنَّ لَكَ أَلَّا تَجُوعَ فِيهَا وَلَا تَعْرَىٰ ﴿١١٨﴾
118. Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi.
وَأَنَّكَ لَا تَظْمَأُ فِيهَا وَلَا تَضْحَىٰ ﴿١١٩﴾
Na kwamba wewe hutapata kiu humo wala hutapata joto.
فَوَسْوَسَ إِلَيْهِ الشَّيْطَانُ قَالَ يَا آدَمُ هَلْ أَدُلُّكَ عَلَىٰ شَجَرَةِ الْخُلْدِ وَمُلْكٍ لَّا يَبْلَىٰ ﴿١٢٠﴾
120. Lakini shetani alimtia wasi- wasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujulishe mti wa kuishi milele na ufalme usiokoma?
فَأَكَلَا مِنْهَا فَبَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ وَعَصَىٰ آدَمُ رَبَّهُ فَغَوَىٰ ﴿١٢١﴾
121. Basi wakaula wote na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake na akapotea njia.
ثُمَّ اجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَتَابَ عَلَيْهِ وَهَدَىٰ ﴿١٢٢﴾
122. Kisha Mola wake akamteua na akamkubalia toba yake naakamwongoa.
TUMEITERMSHA QUR’AN KWA LUGHA YA KIARABU
Aya 113 – 122
MAANA
Namna hiyo tumeiteremsha Qur’an kwa lugha ya kiarabu na tumekariri humo maonyo ili wawe na takua au iwaletee makumbusho.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameteremsha Qur’an kwa mja wake Muhammad(s.a.w.w)
kwa lugha ya kiarabu na akawahadharisha waja na hisabu yake na adhabu yake, kwa mifumo mbalimbali, ili wapate kumcha na kumtii kwenye hukumu zake zote au awamkumbuke yeye wanapofanya madhambi ili watubu na wamwombe msamaha. Au hapa, ni kwa maana ya na; kama mfano ukisema: “Kuwa mwana wa chuoni au mwenye zuhudi.” Kwa sababu kukumbuka kuko pamoja na takua; kama ambavyo zuhudi iko pamoja na elimu.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 12 (12:2). Huko tumejibu kwa ufafanuzi swali la mwenye kuuliza, kwa nini Qur’an imeteremshwa kwa lugha ya kiarabu pamoja na kuwa Muhammad (s.a.w.) ametumwa kwa watu wote?
WASIFU WA QUR’AN
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameitaja Qur’an, katika kitabu chake kitukufu, kwa sifa nyingi, zikiwemo hizi zifuatazo:
1. Ya kiarabu; kama ilivyo katika Aya hii na ile ya Juz. 12 (12:2).
2. Ukumbusho:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ ﴿٩﴾
“Na hakika sisi tumeuteremsha ukumbusho huu” Juz; 14 : (15:9).
3. Nuru:
قَدْ جَاءَكُم مِّنَ اللَّـهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾
“Hakika imekwishawafikia nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu” Juz. 6: (5:15).
4. Upambanuzi:
إِنَّهُ لَقَوْلٌ فَصْلٌ ﴿١٣﴾
“Hakika hiyo ni kauli ya upambanuzi” (86:13).
5. Uongofu: “Hicho ni kitabu, hakina shaka ndani yake, ni uongofu kwa wenye takua.” Juz; 1 (2:2).
6. Hekima:
وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
“Naapa kwa Qur’an yenye hekima” (36:2).
وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ ﴿١﴾
“Naapa kwa Qur’an Tukufu” (50:1).
7. Roho:
رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ يُلْقِي الرُّوحَ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ لِيُنذِرَ يَوْمَ التَّلَاقِ ﴿١٥﴾
“Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa siku ya makutano” (40:15).
8. Haki:
إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٧﴾
Hakika hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako, Lakini watu wengi hawaamini, Juz; 12 (11:17).
9. Habari kubwa:
قُلْ هُوَ نَبَأٌ عَظِيمٌ ﴿٦٧﴾ أَنتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ ﴿٦٨﴾
“Sema: Hiyo ni habari kubwa ambayo nyinyi mnaipuuza.” (38:67–68).
10. Ponyo:
قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ﴿٤٤﴾
“Sema: hiyo ni uongofu na ponyo kwa wenye kuamini” (41:44).
11. Rehema:
وَإِنَّهُ لَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾
Na hakika hiyo ni uwongofu na rehema kwa waumini, (27:77).
12. Uteremsho:
تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨٠﴾
Ni uteremsho utokao kwa Mola wa walimwengu wote (56:80).
13. Bishara na onyo:
قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٣﴾ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ﴿٤﴾
Ni Kitabu kilichopambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa kiarabu kwa watu wanaojua, kinachotoa bishara na kuonya (41:3 – 4).
14. Nguvu na utukufu:
وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ ﴿٤١﴾
“Na hakika ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.” (41:41).
15. Adhimu:
وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ ﴿٨٧﴾
Na hakika tumekupa Aya saba zinazorudiwa rudiwa na Qur’an Adhimu, Juz; 14 (15:87).
16. Ubainifu:
وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾
Naapa kwa Kitabu kinachobainisha (43:2).
Hakika bora zaidi inayofahamisha sifa hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameteremsha Qur’an kwa Mtume wake, kwa ajili tu ya kuwaongoza watu kwenye wema, amani na utulivu wao.
Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki.
Imam Ali
anasema, akilingania Mola wake:“Kutakata ni kwako! Ni utukufu ulioje wa tunayoyaona katika uumbaji wako! Na udogo ulioje wa hayo katika uweza wako! Na ni vituko vilioje wa tuvionavyo katika ufalme wako! Na ni uduni ulioje wa tusivyoviona katika ufalme wako! Na ueneaji ulioje wa neema zako katika dunia! Na ni udogo ulioje wa neema hizo kulinganisha na neema za Akhera!”
Wala usiifanyie haraka hii Qur’an kabla haujamalizika wahyi wake
Kuna Hadith isemayo kuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alikuwa anapoletewa Qur’an na Jibril hufuatilia kuisoma kwa kuhofia kisimpite kitu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha asikilize tu wala asifuatishe na kwamba atulie tu wala asiogope kusahau. Usahihi wa Hadith hii unafahamishwa na ile Aya isemayo:
“Usiutikisie, huu wahyi, ulimi wako kwa kuufanyia haraka, Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha, kisha ni juu yetu kuubainisha” (75: 16 – 19).
NIZIDISHE ELIMU
Na sema: Mola wangu! Nizidishie elimu
Elimu aliyomwamrisha Mwenyezi Mungu Mtume wake, kuomba kuzidishiwa ni ile inayomnufaisha mwenye nayo na mwenginewe. Hakuna itikadi wala misimamo, falsafa wala sharia au fasihi na sanaa, zote hizi si lolote mbele ya Mwenyezi Mungu ispokuwa kama zitakuwa ni nyenzo za maisha bora yasiyokuwa na matatizo wala vikwazo vyovyote.
Hata maisha ya Akhera yanafungamana moja kwa moja na kazi itakayon- ufaisha katika maisha ya duniani. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
anasema: “Mbora zaidi wa watu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayewafaa zaidi watu.” Hakuna mwenye shaka kwamba anayewafaa zaidi watu ni yule anayefanya kwa ajili ya maisha bora na jamii.
Kila kitu, wakati huu, kinafahamisha waziwazi kuwa hakuna maisha bora ispokuwa kwa elimu; bila ya kutofautisha baina ya maisha ya kimaada, kijamii na kiutamaduni.
Kama ambavyo jamii yoyote haiwezi kuishi maisha bora bila ya mitambo ya kuchapisha, viwanda vya nguo, nyenzo za mawasiliano, vifaa vya nyumbani na maengineyo ya lazima; basi vile vile haiwezekani kuishi huru na heshima bila ya elimu ya siasa, uchumi, ya kijamii na elimu nyinginezo zinazofanya kazi ya kumtumikia mtu kwa ajili ya utu.
Hii ndiyo elimu sahihi na ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na sema: Mola wangu! Nizidishie elimu’ na kauli ya Mtume: “Mwenye kufuata njia ya kutafuta elimu, amefuata njia ya kwenda peponi.”
Yeyote mwenye kufasiri neno elimu kwa maana ya kuhifadhi maandishi na maelezo, basi huyo ni katika wale wanaoamini kuwa elimu ni matamshi na maandishi tu; na dini ni kupiga takbira na kusoma tasbih tu.
Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau wala hatukuona kwake azma.
Maagano Alioagana Mwenyezi Mungu na Adam ni kutoukurubuia mti na kwamba asisikilize mwito wa Iblis. Makusudio ya kusahau ni kuacha na azma ni uthabiti.
Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu wote ispokuwa Iblisi alikataa.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz; 1 (2:34), Juz; 8 (7:11), Juz. 14 (15: 30 – 31), na katika Juz. 15 ( 17: 61) na (18:50).
Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo, Basi asiwatoe katika Bustani (Pepo) hii, mkaingia mashakani. Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi, Na kwamba wewe hutapata kiu humo wala hutapata joto.
Yaani hutatabika kwenye joto la jua, Neno joto tumelifasiri kutoka neno Dhuha lenye maana ya mchana, Umetumika mchana kwa maana ya joto kwa vile mchana kunakuwa na joto kali.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimuhadharisha Adam kutokana na wasiwasi wa Ibilisi na akamwambia, wewe una hiyari ya mambo mawili; ama unitii mimi na umuasi Ibilisi upate hii Pepo (Bustani) – kama uinavyo – safi na nzuri. Humo hamna njaa, kiu, kukaa uchi wala maradhi, Hamna maumivu wala huzuni, hamna mauti, damu wala machozi, hamna kuhangaika kwenye joto wala baridi, Hamna chochote ispokuwa amani, utulivu na raha.
Au uniasi mimi na kumtii Ibilisi, utoke Peponi uende duniani kwenye taabu, balaa zote, magonjwa na majanga.
Lakini Adam alisahau hadhari hizi; akaandamwa na misukosuko yeye na kizazi chake, kuanzia na kuuliwa Habil hadi uhalifu wa Israil na mengineyo yasiyokuwa na kikomo.
Sio mbali kuwa kutolewa Adam Peponi ni somo na fundisho kwa yule anayefuata matamanio na kwamba malipo yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni adhabu, Angalia kifungu ‘Mtaka yote hukosa yote’ Juz; 1 (2: 35–39).
Lakini shetani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujulishe mti wa kuishi milele na ufalme usiokoma? Basi wakaula wote na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz; 8 (7:19 – 22).
Na Adam akamuasi Mola wake na akapotea njia.
Unaweza kuuliza
: Adam ni nabii na nabii ni maasumu wa makosa, imekuwaje Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumnasibishia uasi na upotevu?
Wamelijibu hilo kwa majibu kadhaa; miongoni mwayo ni kuwa makusudio ya kuasi ni kuacha mapendekezo sio wajibu, jambo ambalo halipingani na isma.
Jibu jingine ni kuwa Adam alipokuwa Peponi alikuwa Akhera ambako hakuna tabligh wala taklifa yoyote ya kuhitajia mitume, na kwamba utume wa Adam ulikuwa wa duniani sio wa Akhera.
Kwa hali yoyote iwayo ni kwamba Adam alitubia na akamuomba msamaha Mola wake;kisha Mola wake akamteua na akamkubalia toba yake na akamwongoa.
Tumeuazungumzia hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz; 1 (2:35–39) kifungu cha ‘isma ya mitume.