TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Juzuu 17

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 9007
Pakua: 3502


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9007 / Pakua: 3502
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Juzuu 17

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

Sura Ya Ishirini na Mmoja : Surat Al – Anbiya. Imeshuka Makka Ina Aya 112

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مُّعْرِضُونَ ﴿١﴾

1. Imewakurubia watu hisabu yao nao wamo katika mughafala wanapuuza.

مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ ﴿٢﴾

2. Hawafikii dhikr mpya kutoka kwa Mola wao ila huisikiliza na huku wanaifanyia mchezo.

لَاهِيَةً قُلُوبُهُمْ وَأَسَرُّوا النَّجْوَى الَّذِينَ ظَلَمُوا هَلْ هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ أَفَتَأْتُونَ السِّحْرَ وَأَنتُمْ تُبْصِرُونَ ﴿٣﴾

3. Zimeghafilika nyoyo zao Na wale waliodhulumu hunog’ona kwa siri: Ni nani huyu isipokuwa ni mtu tu kama nyinyi. Mnauendea uchawi hali nanyi mnaona?

قَالَ رَبِّي يَعْلَمُ الْقَوْلَ فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٤﴾

4. Alisema: Mola wangu anajua yasemwayo mbinguni na ardhini na Yeye ni mwenye kusikia, mwenye kujua.

بَلْ قَالُوا أَضْغَاثُ أَحْلَامٍ بَلِ افْتَرَاهُ بَلْ هُوَ شَاعِرٌ فَلْيَأْتِنَا بِآيَةٍ كَمَا أُرْسِلَ الْأَوَّلُونَ ﴿٥﴾

5. Lakina walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua, bali huyo ni mshairi. Basi atuletee ishara kama walivyotumwa wale wa mwanzo.

مَا آمَنَتْ قَبْلَهُم مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَفَهُمْ يُؤْمِنُونَ ﴿٦﴾

6. Hawakuamini kabla yao watu wa mji tuliouangamiza. Je, wataamini hao.

IMEWAKURUBIA WATU HISABU YAO

Aya 1 – 6

MAANA

Imewakurubia watu hisabu yao nao wamo katika mughafala wanapuuza.

Makusudio ya hisabu hapa ni siku ya Kiyama, nayo iko karibu na kila mtu, kwa sababu itakuja tu, hata kama muda utakuwa mrefu. Maana yake yanafupishwa na kauli ya Imam Ali: “Usijisahau kwani wewe hujasahauliwa.” Na akasema tena: “Usighafilke kwani wewe hujasahauliwa.” Akasema tena: “Hatua fupi ilioje ya mtu aliye na siku moja tu ambayo hawezi kuizidisha, na mauti yaliyo na haraka yanamuandama mpaka aitoke”

Hawafikii dhikr mpya kutoka kwa Mola wao ila huisikiliza na huku wanaifanyia mchezo.

Wanaikabili haki kwa kuikadhibisha, nasaha za kejeli na hadhari za dharau. Zimeghafilika nyoyo zao na haki, hawajali kitu wala hawahisi majukumu ya kuulizwa hisabu na malipo; sawa na wanyama na wadudu.

Na wale waliodhulumu hunog’ona kwa siri: Ni nani huyu isipokuwa ni mtu tu kama nyinyi.

Washirikina walinong’onezana kuhusu aliyesilimu na kuongoka, kuwa huyo Muhammad, ni nani hata tumtii na kumfuata? Yeye si mtu tu kama watu wengine, anakula chakula na anatembea sokoni? Ama elimu na fadhila basi ni maneno bila maana na miujiza ni uchawi na kuvunga.

Mnauendea uchawi hali nanyi mnaona?

Mnauendea hapa, ina maana ya kukubali, na mnaona ni kwa maana ya mnajua. Si ajabu wao kuzikadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu na dalili zake ambazo amekuja nazo Mtume mtukufu(s.a.w.w) . Kila mwenye kiburi hutafuta visingizio vya aina hii ikiwa hana hoja.

Alisema: Mola wangu anajua yasemwayo mbinguni na ardhini na Yeye ni mwenye kusikia, mwenye kujua.

Walimwambia Mtume(s.a.w.w) kuwa yeye ni mchawi akawajibu kuwa Mwenyezi Mungu anajua ukweli wake na anajua kauli yao hii, kwa sababu hakifichiki kwake kitu chochote katika ardhi na katika mbingu. Atawahisabu na atawalipa vile mnavyostahiki.

Hakuna jawabu kwa anayeipinga haki isipokuwa kupelekwa kwenye mahakama ya uadilifu.

Lakina walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua, bali huyo ni mshairi.

Waliikataa wanamangamanga haki wakatafuta visingizio vya kutumia, wakabaki tu. Mwenye Majmaul-bayan anasema: “Hivi ndivyo anavyokuwa yule Mwenye kuhemewa. Anasema ni mchawi, mara ni mshairi, mara anaota. Hana moja analolishikilia. Huku ndio kujipinga kwa dhahiri.”

Basi atuletee ishara kama walivyotumwa wale wa mwanzo.

Washirkina walimwambia Muhammad(s.a.w.w) : Ukiwa wewe ni Mtume basi tuletee muujiza, kama vile ngamia wa Swaleh, fimbo ya Musa na miujiza mingineyo ya mitume waliopita. Ndio Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema:

Hawakuamini kabla yao watu wa mji tuliouangamiza.

Maana ya jawabu hili ni kuwa, ni kweli kwamba mitume waliotangulia walikuja na miujiza, kama vile ngamia na fimbo, lakini watu wao hawakuwaamini, bali walikataa na wakamakadhibisha, ingawaje wao wenyewe ndio walioitaka. Kwa ajili hiyo tukawaangamiza.

Kwa hiyo inatakiwa enyi washirikina muangalie natija inayofungamana na miujiza sio muujiza wenyewe. Kwa sababu itawatokea hivyo hivyo, ikiwa Mwenyezi Mungu atawakubalia mapendekezo yenu.

Je, wataamini hao.

Yaani wale waliokuwa kabla yao hawakuamini miujiza waliyoipendekeza, vile vile hawa hawataamini miujiza wanayoipendekeza. Natija itakuwa ni kuangamizwa, kama walivyoangamizwa wa kwanza; ambapo hekima yake Mwenyezi Mungu ilipitisha kuwa waangamizwe kwa miujiza waliyoitaka.

وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧﴾

7. Na hatukuwatuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi. Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.

وَمَا جَعَلْنَاهُمْ جَسَدًا لَّا يَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَمَا كَانُوا خَالِدِينَ ﴿٨﴾

8. Na hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.

ثُمَّ صَدَقْنَاهُمُ الْوَعْدَ فَأَنجَيْنَاهُمْ وَمَن نَّشَاءُ وَأَهْلَكْنَا الْمُسْرِفِينَ ﴿٩﴾

9. Kisha tukawatimizia miadi na tukawaokoa wao na tuliowataka na tukawaangamiza waliopita mipaka.

لَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ كِتَابًا فِيهِ ذِكْرُكُمْ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٠﴾

10. Hakika tumewateremshia Kitabu, ndani yake mna ukumbusho wenu. Je, hamtii akili?

وَكَمْ قَصَمْنَا مِن قَرْيَةٍ كَانَتْ ظَالِمَةً وَأَنشَأْنَا بَعْدَهَا قَوْمًا آخَرِينَ ﴿١١﴾

11. Na miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawaumba baada yao watu wengine.

فَلَمَّا أَحَسُّوا بَأْسَنَا إِذَا هُم مِّنْهَا يَرْكُضُونَ ﴿١٢﴾

12. Basi walipohisi adhabu yetu mara wakaanza kukimbia.

تَرْكُضُوا وَارْجِعُوا إِلَىٰ مَا أُتْرِفْتُمْ فِيهِ وَمَسَاكِنِكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْأَلُونَ ﴿١٣﴾

13. Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu na maskani zenu mpate kusailiwa.

قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿١٤﴾

14. Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.

فَمَا زَالَت تِّلْكَ دَعْوَاهُمْ حَتَّىٰ جَعَلْنَاهُمْ حَصِيدًا خَامِدِينَ ﴿١٥﴾

15. Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya wamefyekwa wamezimika.

WAULIZENI WENYE KUMBUKUMBU

Aya 7 – 15

MAANA

Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi. Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.

Imekwishatangulia kwa herufi zake katika Juz. 14 (16:43).

Na hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.

wao wenyewe.

Manabii sio roho bila ya miili wala wao hawatakaa maisha hapa duniani. Wao ni kama watu wengine, hawana tofauti isipokuwa kwa kufikisha neno la Mungu na kwamba wao ni wakamilifu. Angalia Juz. 16 (20: 35) kifungu ‘Hakika ya Utume’.

Kisha tukawatimizia miadi na tukawaokoa wao na tuliowataka na tukawaangamiza waliopita mipaka.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaishiria kwenye kauli yake hii pale aliposema:

كَتَبَ اللَّـهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢١﴾

“Mwenyezi Mungu amekwishaandika: Hakika nitashinda mimi na Mitume wangu.“Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.” (58:21).

Na akasema tena:

إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ ﴿٥١﴾

“Hakika bila shaka tutawanusuru mitume wetu na walioamini katika maisha ya duniani na siku watakaposimama mashahidi.” (40:51).

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaahidi mitume na wau- mini kuokoka na makafiri kuangamia. Alitekeleza ahadi yake. Ni nani kuliko Mwenyezi Mungu katika utekelezaji ahadi?

MUHAMMAD NA WAARABU

Hakika tumewateremshia Kitabu, ndani yake mna ukumbusho wenu. Je, hamtii akili?

Kabla ya Muhammad(s.a.w.w) na Qur’an waarabu hawakuwa ni chochote. Baada ya vitu viwili hivyo wakawa ni watu mashuhuri, ikatajwa historia namaendeleo yao, wakawa ni watu wa hali ya juu.

Anasema: W.L. Dewarnet katika Ensaiklopidia yake ya Historia ya kisa cha maendeleo katika ulimwengu: “Muhammad ni mkuu miongoni mwa wakuu wa Historia. Aliwainua watu walioishi katika giza la ushenzi, anga ya joto na ukame wa jangwa, kwenye ustawi wa kiroho na kimaadili. Alifaulu kwenye lengo hili kwa namna ambayo hajawahi kuifikia kiongozi yeyote katika historia yote.

Alipoanza mwito wake miji ya waarabu ilikuwa ni jangwa tupu linalokaliwa na makabila ya waabudu mizimu yenye watu wachache wasiokuwa na umoja wowote. Lakini kufikia kufa kwake wakawa ni umma wenye mshikamano, wakiwa wamekiuka ubaguzi na upuuzi.

Wakawa juu ya uyahudi na ukiristo na dini ya nchiyake ikawa wazi na nyepesi. Ikajengeka misingi ya kijasiri, utukufu na uzalendo. Kwenye kizazi kimoja tu ikaweza kushinda vita mia moja na katika karne moja ikaweza kuanzisha dola kuu na kubakia hadi leo kuwa ni nguvu kuu ulimwenguni”

Na miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawaumba baada yao watu wengine.

Haya ni makemeo na kiaga kwa wale wanaomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) kwamba wao yatawapata yaliyowapata waliokuwa kabla yao katika umma zilizowakadhibisha mitume wao. Kisha Mwenyezi Mungu awalete wengine wasiokuwa na uhusiano wowote na walioangamizwa; awarithishe milki zao na majumba yao. Wajenge upya na wastarehe na kheri zake na baraka zake.

Basi walipohisi adhabu yetu mara wakaanza kukimbia.

Hii ni taswira ya hali ya washirikina inapowafikia adhabu kutoka mbinguni, wanajaribu kuikimbia, lakini wapi! Inawezekana vipi kuukimbia utawala wa Mwenyezi Mungu na hukumu yake? Kama hapo mwanzo wangelikimbilia kwa Mwenyezi Mungu wangelikuta amani. Ama kumkimbia yeye Mwenyezi Mungu ni sawa na mtu kukimbia kivuli chake.

Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu na maskani zenu mpate kusailiwa.

Kabla ya kuteremshwa adhabu washirikina walikuwa hawajishughulishi na lolote zaidi ya mali na starehe zao, lakini ilipowashukia adhabu, nyoyo na akili zao zilipofuka na wakatupilia mbali kila kitu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaambia kwa kuwatahayariza: Mnaenda wapi? Rudini kwenye mali zenu na watoto wenu.

Leo mnaziacha na jana mlikuwa mkiziabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Haya ndio malipo ya anayeacha uongofu na asiongoke kwenye uongofu.

Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.

Walitulia na starehe zao, wakaitikia matamanio yao na wakamtuhumu anayewapa nasaha, lakini walipoiona adhabu walijuta na wakaita ole wetu, lakini majuto ni mjuukuu hayarudishi yaliyopita.

Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya wamefyekwa wamezimika.

Wanalia ole wetu na adhabu iko kichwani mwao ikiendelea. Haikufaa mali wala jaha. Huo ndio mwisho wa wakosefu.

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ ﴿١٦﴾

16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.

لَوْ أَرَدْنَا أَن نَّتَّخِذَ لَهْوًا لَّاتَّخَذْنَاهُ مِن لَّدُنَّا إِن كُنَّا فَاعِلِينَ ﴿١٧﴾

17. Kama tungelitaka kufanya mchezo tungelijifanyia sisi wenyewe, kama tungekuwa ni wafanyao mchezo.

بَلْ نَقْذِفُ بِالْحَقِّ عَلَى الْبَاطِلِ فَيَدْمَغُهُ فَإِذَا هُوَ زَاهِقٌ وَلَكُمُ الْوَيْلُ مِمَّا تَصِفُونَ ﴿١٨﴾

18. Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka. Na ole wenu kwa mnayoyasifia

وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ ﴿١٩﴾

19. Ni vyake vilivyoko mbinguni na ardhini na walioko mbele yake hawafanyi kiburi wakaacha kumwabudu wala hawachoki.

يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ ﴿٢٠﴾

20. Wanamsabihi usiku na mchana wala hawanyog’onyei.

أَمِ اتَّخَذُوا آلِهَةً مِّنَ الْأَرْضِ هُمْ يُنشِرُونَ ﴿٢١﴾

21. Au wamepata miungu katika ardhi inayofufua.

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا فَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٢٢﴾

22. Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika. Ametasika Mwenyezi Mungu, Mola wa arshi, na hayo wanayoyasifu.

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ ﴿٢٣﴾

23. Yeye haulizwi kwa ayatendayo na wao ndio waulizwao kwa wayatendayo.

JE, VITENDO VYAKE MWENYEZI MUNGU MTUKUFU VINA MALENGO?

Aya 16 – 23

MAANA

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:191). Huko tumenukuu kauli kuhusiana na kuwa je, vitendo vya Mwenyezi Mungu vinakuwa na sababu ya malengo au kwake Mwenyezi Mungu hakuna ubaya wala hana wajibu wa chochote?

Kama tungelitaka kufanya mchezo tungelijifanyia sisi wenyewe, kama tungekuwa ni wafanyao mchezo.

Mchezo na upuuzi ni muhali kwa yule anayekiambia kitu kuwa na kikawa. Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: ‘Lau tungelitaka kama tungekuwa ni wafanyao mchezo’ yaani hatukataka wala hatufanyi. Lau angelitaka kufanya mchezo – kukadiria muhali sio muhali – angelijifanyia kwa namna yoyote inayolingana na cheo chake; sio katika namna ya waja; kama kucheza na wanawake na watoto.

Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka.

Makusudio ya haki hapa ni ukweli na uhakika kwa mkabala wa mchezo alioukanusha Mwenyezi Mungu Mtukufu na makusudio ya batili hapa ni upuzi na mchezo.

Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kusema hatufanyi mchezo sasa anasema kuwa vitendo vyake kwake ni uhakika na ukweli si mchezo na upuzi; bali ukija upuzi na mchezo kutoka popote anauvunjilia mbali. Vipi ataliridhia lile asiloliridhia kwa mwingine?

Na ole wenu kwa mnayoyasifia nayo Mwenyezi Mungu na kumbandika sifa za kutengeneza. Ni vyake vilivyoko mbinguni na ardhini na walioko mbele yake hawafanyi kiburi wakaacha kumwabudu wala hawachoki.

Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya walioko mbele yake, ni Malaika. Tunavyofahamu sisi ni kuwa makusudio ni kila mwenye cheo na jaha mbele ya Mwenyezi Mungu, awe Malaika au mtu.

Wanamsabihi usiku na mchana wala hawanyonyog’onyei.

Yaani hawachoki, bali wanadumu kwenye twaa katika kauli na vitendo wala hawamtuhumu Mwenyezi Mungu kwa kumsawirisha au kumpa sifa za kutengeneza.

Au wamepata miungu katika ardhi inayofufua.

Yaani kila anayeabudiwa na washirikina, hawezi kuhui wafu wala hawafufui wafu walio makaburini, bali Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayehui na kufisha.

Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika. Ametasika Mwenyezi Mungu, Mola wa arshi, na hayo wanayoyazua.

Tazama tuliyoyaandika kwenye Juz. 5 (4:48) Kifungu ‘Dalili ya umoja na utatu.’

Mwenye kujua ni hoja kwa asiyejua Yeye hahojiwi kwa ayatendayo na wao ndio wanaohojiwa kwa wayatendayo.

Baadhi wametoa dalili kwa Aya hii kwamba hakuna ubaya kwa Mungu wala hawajibikiwi na jambo lolote. Anaweza kumwadhibu mtiifu na kumlipa thawabu muasi. Lakini hii inapingana na uadilifu wake, hekima na rehema yake.

Usahihi hasa ni kuwa maana ya Aya ni Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kuwa ni mwadilifu kwa dhati yake, haijuzu kwa yeyote kumwingilia kwa kauli yake na vitendo vyake. Kwa sababu haijuzu kuambiwa mwadilifu, kwa nini umefanya uadilifu? Na mkweli, kuambiwa kwa nini umesema kweli? Kama ambavyo haifai kwa asiyejua utabibu kumwambia tabibu hodari, kwa nini unatoa dawa hii?

Mfano wa maswali haya unafaa kwa aliye kifani wake. Ama asiyejua kitu, analotakiwa ni kufanya juhudi ya kumtafuta mjuzi na kuhakikisha ujuzi wake kutokana na dalili na alama. Akishapata uhakika basi inakuwa ni wajibu kwake kumfuata kwa yale aliyo na ujuzi nayo; sawa na mgonjwa anavyomfuata tabibu.

Walikwishasema wahenga: “Ajuaye ni hoja kwa asiyejua.” Ikiwa mambo ni hivi kwa kiumbe pamoja na kiumbe mwenzake. Itakuwaje kwa kiumbe pamoja na muumba wa mbingu na ardhi?

Siku moja mwanafunzi alimuuliza mwalimu wake: “Kwa nini tuko na kwa nini tunaishi?”

Mwalimu akamwambia mwanafunzi wake: “Kwa nini ewe mwanangu unajilazimisha na mambo yasiyokuwa na mwanzo wala mwisho? Kwa nini usiamini dini ikastarehe nafsi yako na uawache yale usiyoyaweza, ufuate unayoyaweza? Wewe ni mmoja wa maelfu ya mamilioni ya watu na mji wako uanaoishi ni moja ya maelfu ya miji. Ardhi tunayoishi ni moja ya mamilioni ya sayari na ulimwengu ulio na sayari zote hizo, hatujui kuwa kuna mfano wake unaouzidia. Je, sehemu moja inaweza kudhibiti yote hayo? Je, tone moja linaweza kuihoji bahari?

Mwanangu! Mimi sisemi kuwa usifanye uchunguzi na kupeleleza, kwani kutafuta hakika ni miongoni mwa sababu za kupatikana binadamu, lakini maadamu akili yako ni ndogo kuweza kufahamu hakika hiyo, basi ngoja mpaka uzidi kupata ufahamu na utambuzi. Mwisho ukishindwa, liache jambo kama lilivyo. Kwa sababu udogo wa akili yako kufahamu jambo, haimaanishi kuwa jambo hilo ni mchezo na upuzi; isipokuwa inamaanisha kuwa hujalifahamu; kwa hiyo muachie aliyeumba vyote vilivyoko.”

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ هَـٰذَا ذِكْرُ مَن مَّعِيَ وَذِكْرُ مَن قَبْلِي بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ الْحَقَّ فَهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٢٤﴾

24. Au wamejifanyia miungu mingine badala yake. Sema, leteni dalili yenu. Hii ni ukumbusho wa walio pamoja nami na ukumbusho wa waliokuwa kabla yangu. Lakini wengi wao hawajui haki kwa hiyo wanapuuza.

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

25. Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimpa wahyi kwamba hapana Mungu isipokuwa mimi, basi niabuduni mimi tu.

وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَـٰنُ وَلَدًا سُبْحَانَهُ بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ ﴿٢٦﴾

26. Na wanasema, Mwingi wa rehema ana mwana! Ametakasika na hayo! Bali hao ni waja waliotukuzwa.

لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ ﴿٢٧﴾

27. Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri yake.

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ ﴿٢٨﴾

28. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia. Nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.

وَمَن يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلَـٰهٌ مِّن دُونِهِ فَذَٰلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ ﴿٢٩﴾

29. Na yeyote miongoni mwao atakayesema: mimi ni mungu, badala yake, basi tutamlipa Jahannamu. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.

LETENI DALILI ZENU

Aya 24 – 29

MAANA

Au wamejifanyia miungu mingine badala yake. Sema leteni dalili yenu.

Kila mtu huwa anasema, mwenye kudai ni lazima alete ushahidi; hata kama yule anayeelekezewa madai ni mtu duni; sikwambii akiwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake. Basi iko wapi dalili?

Hii Qur’an ni ukumbusho wa walio pamoja nami na ukumbusho wa waliokuwa kabla yangu.

Vitabu vyote vya mbinguni vinaamrisha Tawhid na kukataza shirki. Ikiwa shirki haina dalili ya kiakili wala ya kinakili, basi chimbuko lake ni ujinga na upofu.

Lakini wengi wao hawajui haki kwa hiyo wanapuuza. Hii ni kukemea ujinga wao na upotevu wao.

Na hatukumtuma kabla yako Mtume yoyote ila tulimpa wahyi kwam- ba hapana Mungu isipokuwa mimi, basi niabuduni mimi tu.

Aya hii ni ubainifu na tafsiri ya Aya iliyo kabla yake. Ya kwanza inasema kuwa hakuna athari yoyote ya shirki katika vitabu vya Mwenyezi Mungu na hii inasema kuwa hakutumwa mtume yeyote isipokuwa kwa ajili ya tawhidi na kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika ibada.

Na wanasema: Mwingi wa rehema ana mwana. Ametakasika na hayo! Bali hao ni waja wa waliotukuzwa.

Mayahudi au kikundi katika wao walisema kuwa Uzayr ni mwana wa Mungu, Wanaswara (wakiristo) wakasema Masih ni mwana wa Mungu; na baadhi ya makabila ya kiarabu yakasema kuwa Malaika ni mabinti wa Mungu.

Ndio Mwenyezi Mungu akawarudi wote hao, kwamba mliowataja ni waja sio watoto, tena wao wana daraja na cheo mbele ya Mola wao.

Ajabu ni yale yaliyoelezwa katika Tafsiri At-Tabari, akiwanukuu waliosema kuwa Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu: “Mwenyezi Mungu alimuoa jini akamzalia Malaika.” Hili ameliashiria Mwenyezi Mungu katika kauli yake:

وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا ﴿١٥٨﴾

“Na wameweka mahusiano ya nasaba baina Yake na majini” (37:158).

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha sababu ya daraja ya Uzayr, Masih na Malaika mbele yake, kwa kusema:

Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri yake.

Yaani wao hawatumii rai wala kiasi.

Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao.

Yaliyo mbele yao ni fumbo la vitendo vyao vya sasa na yaliyo nyuma yao ni vitendo vyao vilivyopita. Maana ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu anayajua vizuri matendo yao ya kheri na makusudio yao mazuri; naye atawalipa ujira wao kwa yale mazuri waliyoyafanya.

Wala hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia Yeye.

Hii ni kumrudi yule anayemwabudu Mtume, walii au Malaika kwa tamaa ya kuombewa kwa Mungu. Kwa maana kwamba waja waliotukuzwa watawaombea wale wenye kuridhiwa na Mwenyezi Mungu sio washirikina walioghadhibikiwa.

Nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea pamoja na kuwa wana ikhlasi na vyeo mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na yeyote miongoni mwao atakayesema: mimi ni mungu, badala yake, basi tutamlipa Jahannamu. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.

Hao waja wema waliotukuzwa, lau mmoja atadai kuwa yeye ni mungu badala ya Mwenyezi Mungu au ni mshirika wake, basi malipo yake yatakuwa ni Jahannamu, kama washirikina wengine, bila ya kuwa na tofauti yoyote.

أَوَلَمْ يَرَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ كَانَتَا رَتْقًا فَفَتَقْنَاهُمَا وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٠﴾

30. Je, hao waliokufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha tukaziambua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai. Je, hawaamini?

وَجَعَلْنَا فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِهِمْ وَجَعَلْنَا فِيهَا فِجَاجًا سُبُلًا لَّعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٣١﴾

31. Na tukaweka katika ardhi milima ili isiwayumbishe. Na tukaweka humo upana wa njia ili wapate kuongoka.

وَجَعَلْنَا السَّمَاءَ سَقْفًا مَّحْفُوظًا وَهُمْ عَنْ آيَاتِهَا مُعْرِضُونَ ﴿٣٢﴾

32. Na tukaifanya mbingu kuwa sakafu iliyohifadhiwa, lakini wanazipuuza ishara.

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na Yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi. Kila kimoja katika anga vinaogoelea.

وَمَا جَعَلْنَا لِبَشَرٍ مِّن قَبْلِكَ الْخُلْدَ أَفَإِن مِّتَّ فَهُمُ الْخَالِدُونَ ﴿٣٤﴾

34. Na hatukumjaalia mtu yeyote wa kabla yako kuishi milele. Je, ukifa wewe wao wataishi milelele?

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ ﴿٣٥﴾

35. Kila nafsi itaonja mauti. Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na kheri na kwetu mtarejeshwa.

وَإِذَا رَآكَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَـٰذَا الَّذِي يَذْكُرُ آلِهَتَكُمْ وَهُم بِذِكْرِ الرَّحْمَـٰنِ هُمْ كَافِرُونَ ﴿٣٦﴾

36. Na wanapokuona wale ambao wamekufuru hawakufanyii ila mzaha: Je, huyu ndiye anayewataja miungu wenu? Na hao ndio wanaokataa dhikri ya Mwingi wa rehema.

MAJI NI UHAI

Aya 30 – 36

MAANA

Je, hao waliokufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha tukazibandua?

Mwanzoni mwa Juzuu ya kwanza tumefafanua maelezo yenye kichwa cha maneno ‘Qur’an na sayansi,’ tukasema kuwa Qur’an ni kitabu cha dini kinachomwongoza mtu kwenye ufanisi wake wa kidunia na akhera; na wala sio kitabu cha nadharia za falsafa, sayansi au falaki n.k.

Na kwamba kila Aya miongoni mwa aya za Qur’an za kilimwengu au za kihistoria, kama vile visa vya mitume, lengo lake ni kutupa mawaidha na mafunzo au kutuongoza kujua kuweko Mwenyezi Mungu, tuweze kumwamini.

Miongoni mwa Aya za kilimwengu ni hii tuliyo nayo. Humo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja mambo mawili: Kwanza, kwamba sayari za Jua, ikiwemo Jua, Ardhi, Mars, Jupita, Zohali, Zebaki n.k. Zote zilikuwa zimeshikana kama kitu kimoja, kisha Mwenyezi Mungu akazipambanua na kila moja akaifanya ni sayari peke yake.

Wataalamu wameikubali nadharia ya kubanduka Jua na Ardhi, lakini wakatofautiana katika namna ya kubanduka kwake. Qur’an nayo haikufafanua kuhusu aina ya kubanduka kwake. Nasi tunayanyamazia yale aliyoyanyamazia Mungu.

Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai.

Hili ni jambo la pili lilotajwa na Aya. Kwamba maji ndio chimbuko la kila kitu kinachokua; awe ni mtu, mnyama au mmea.

Katika Juz. 12 (11:7) Mwenyezi Mungu anasema: “Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita na arshi yake ilikuwa juu ya maji.” Huko tumezungumzia kuwa makusudio ya Arshi ni miliki yake na utawala wake na kwamba maji yalikuwako kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi.

Miongoni mwa kauli za Ahlu bayt(a.s) ni kuwa maji ndio ya kwanza kuumbwa na Mwenyezi Mungu. Ikiwa elimu hivi leo haijaugundua uhakika huu, lakini inawezekana ikaugundua kesho ya karibu au ya mbali.

Amenukuu Abul-hayan Al-andalusi katika Bahrul-muhit, kwamba Hamid amesoma: ‘Tumejalia maji kuwa ni uhai wa kila kitu.’ Kisomo hiki kinatilia nguvu kuwa maji ndiyo yaliyoumbwa mwanzo na ndio chimbuko la kwanza la kila kitu, na kwamba kila kitu kina uhai, kiwe kinakua au hakikui hata kama kwa dhahiri kinaonekana kimeganda.

Je, hawaamini baada ya dalili zote hizi na ubainifu?

Na tukaweka katika ardhi milima ili isiwayumbishe. Na tukaweka humo upana wa njia ili wapate kuongoka.

Mahali pengine imesemwa:

لِّتَسْلُكُوا مِنْهَا سُبُلًا فِجَاجًا ﴿٢٠﴾

“Ili mtembee humo katika njia pana” (71:20)

Imetangulizwa njia ndio ukaja upana. Maana yote nisawa.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameweka njia pana ardhini ili watu wazitumie kwenye makusudio yao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 14: (16:15).

Na tukaifanya mbingu kuwa sakafu iliyohifadhiwa, lakini wanazipuuza ishara.

Kuwa sakafu maana yake ni kama sakafu. Makusudio ya iliyohifadhiwa hapa ni kubakia sayari sehemu yake kwa nguvu ya mvutano. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

وَيُمْسِكُ السَّمَاءَ أَن تَقَعَ عَلَى الْأَرْضِ ﴿٦٥﴾

“Na anazizuia mbingu zisianguke juu ardhi.” (22:65).

Kuzuia kumetegemezwa kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye ndio sababu ya sababu zote. Maana ni kuwa nidhamu hii ya undani katika kuumba mbingu ni dalili mkataa, kwa wenye akili, ya kuweko muumbji, umoja wake, uweza wake, ujuzi na hekima yake. Lakini watu wengi wanazipinga ishara za Mwenyezi Mungu na dalili zake wakipondokea kwenye hawa zao na ladha zao.

Na Yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi.

Kila kimoja kati ya usiku, mchana, jua na mwezi kina uhusiano mkubwa na binadamu. Mchana ni wa kujishughulisha, usiku ni wa kupumzika na kutulia, jua na mwezi ni kwa ajili ya mwanga, hisabu na faida nyinginezo. Hayo yote ni neema kubwa kwa waja Wake na nguvu ya hoja ya ukuu wa usultani Wake.

Kila kimoja katika anga vinaogoelea.

Kila sayari inazunguka kwa vipimo na harakati zinazooana nayo.

Unaweza kuuliza : Ikiwa tutakadiria kusema kila kimoja basi tungesema ‘kinaogelea,’ sasa kuna wajihi gani wa kusema vinaogelea?

Wafasiri wameleta majibu mengi, lenye nguvu zaidi ni lile linalosema: Kila moja kati ya mwezi na jua kina matilai yake na mashukio yake. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akarudisha dhamiri ya wingi kwa kuzingatia hayo.

Na hatukumjaalia mtu yeyote wa kabla yako kuishi milele. Je, ukifa wewe wao wataishi milelele?

Tabrasi amesema: “Washirikina wa kikuraishi waliposhindwa na Muhammad(s.a.w.w) walisema tumngoje afe, ndipo ikashuka Aya hii kuwajibu kuwa hakuna yeyote atakayeokoka na mauti. Je, mtume akifa nyinyi washirikina hamtakufa? Mfumo wa Aya haukatai aliyoyasema Tabrasi.

Kila nafsi itaonja mauti.

Hakuna wa kuyakimbia mauti. Mauti mazuri ni yale ya kufa shahidi kwa ajili ya kuitafuta haki na kuibatilisha batili.

Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na kheri na kwetu mtarejeshwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) huwapa mtihani waja wake kwa wanayoyapenda na wanayoyachukia, ili idhihiri hakika ya kila mtu. Yule atakayeshukuru wakati wa raha, akavumilia wakati wa shida, basi huyo ni katika waumini wenye ikhlasi na atakuwa na malipo ya thawabu. Na yule mwenye kukufuru na akajivuna, basi huyo ni katika wale waliothibitikiwa na adhabu.

Inasemekana kuwa Amirul-mu’minin, Ali, aliugua. Wenzake wakaja kumtazama na wakamuuliza: “Vipi hali yako ewe Amirul-muminin?” Akasema: “Ni shari tu.” Wakasema: “Maneno haya hayasemwi na mtu mfano wako!”

Akasema: “Mwenyezi Mungu anasema: Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na kheri. Kwa hiyo kheri ni afya na kujitosheleza na shari ni ufukara na ugonjwa.”

Pia Amirul-muminin amesema: “Ambaye dunia yake itamnyookea na asijue kuwa anafanyiwa vitimbi, basi imedanganyika akili yake.” Neno mtihani katika Aya ni kutilia mkazo neno tutawajaribu.

Na wanapokuona wale ambao wamekufuru hawakufanyii ila mzaha: “Je, huyu ndiye anayewataja miungu wenu?.” Na hao ndio wanaokataa dhikri ya Mwingi wa rehema.

Wamemkataa Mwenyezi Mungu wakaamini mawe. Mtume akawaita kwenye imani ya Mwenyezi Mungu mmoja aliye peke yake na waachane na mawe.

Lakini wakamfanyia masikhara yeye na mwito wake wa haki iliyo wazi, kwamba masanamu yao na mawe yao hayadhuru wala hayanufaishi.

Baadhi yao wamesema: “Hili ni jambo la ajabu kabisa.” Lakini hakuna ajabu, hii ni kawaida ya kila ambaye amechotwa na manufaa na masilahi ya kibinafsi na akakua katika malezi ya kuiga mazingira, mababa na mababu; ni sawa uigizaji huo uwe ni wa kuabudu mawe au kung’ang’ania rai bila ya elimu wala muongozo. Na nisawa malengo yawe ni mali au jaha. Wote hali moja.