1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA
Sura Ya Ishirini na Mmoja : Surat Al – Anbiya. Imeshuka Makka Ina Aya 112
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مُّعْرِضُونَ ﴿١﴾
1. Imewakurubia watu hisabu yao nao wamo katika mughafala wanapuuza.
مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ ﴿٢﴾
2. Hawafikii dhikr mpya kutoka kwa Mola wao ila huisikiliza na huku wanaifanyia mchezo.
لَاهِيَةً قُلُوبُهُمْ وَأَسَرُّوا النَّجْوَى الَّذِينَ ظَلَمُوا هَلْ هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ أَفَتَأْتُونَ السِّحْرَ وَأَنتُمْ تُبْصِرُونَ ﴿٣﴾
3. Zimeghafilika nyoyo zao Na wale waliodhulumu hunog’ona kwa siri: Ni nani huyu isipokuwa ni mtu tu kama nyinyi. Mnauendea uchawi hali nanyi mnaona?
قَالَ رَبِّي يَعْلَمُ الْقَوْلَ فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٤﴾
4. Alisema: Mola wangu anajua yasemwayo mbinguni na ardhini na Yeye ni mwenye kusikia, mwenye kujua.
بَلْ قَالُوا أَضْغَاثُ أَحْلَامٍ بَلِ افْتَرَاهُ بَلْ هُوَ شَاعِرٌ فَلْيَأْتِنَا بِآيَةٍ كَمَا أُرْسِلَ الْأَوَّلُونَ ﴿٥﴾
5. Lakina walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua, bali huyo ni mshairi. Basi atuletee ishara kama walivyotumwa wale wa mwanzo.
مَا آمَنَتْ قَبْلَهُم مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَفَهُمْ يُؤْمِنُونَ ﴿٦﴾
6. Hawakuamini kabla yao watu wa mji tuliouangamiza. Je, wataamini hao.
IMEWAKURUBIA WATU HISABU YAO
Aya 1 – 6
MAANA
Imewakurubia watu hisabu yao nao wamo katika mughafala wanapuuza.
Makusudio ya hisabu hapa ni siku ya Kiyama, nayo iko karibu na kila mtu, kwa sababu itakuja tu, hata kama muda utakuwa mrefu. Maana yake yanafupishwa na kauli ya Imam Ali: “Usijisahau kwani wewe hujasahauliwa.” Na akasema tena: “Usighafilke kwani wewe hujasahauliwa.” Akasema tena: “Hatua fupi ilioje ya mtu aliye na siku moja tu ambayo hawezi kuizidisha, na mauti yaliyo na haraka yanamuandama mpaka aitoke”
Hawafikii dhikr mpya kutoka kwa Mola wao ila huisikiliza na huku wanaifanyia mchezo.
Wanaikabili haki kwa kuikadhibisha, nasaha za kejeli na hadhari za dharau. Zimeghafilika nyoyo zao na haki, hawajali kitu wala hawahisi majukumu ya kuulizwa hisabu na malipo; sawa na wanyama na wadudu.
Na wale waliodhulumu hunog’ona kwa siri: Ni nani huyu isipokuwa ni mtu tu kama nyinyi.
Washirikina walinong’onezana kuhusu aliyesilimu na kuongoka, kuwa huyo Muhammad, ni nani hata tumtii na kumfuata? Yeye si mtu tu kama watu wengine, anakula chakula na anatembea sokoni? Ama elimu na fadhila basi ni maneno bila maana na miujiza ni uchawi na kuvunga.
Mnauendea uchawi hali nanyi mnaona?
Mnauendea hapa, ina maana ya kukubali, na mnaona ni kwa maana ya mnajua. Si ajabu wao kuzikadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu na dalili zake ambazo amekuja nazo Mtume mtukufu(s.a.w.w)
. Kila mwenye kiburi hutafuta visingizio vya aina hii ikiwa hana hoja.
Alisema: Mola wangu anajua yasemwayo mbinguni na ardhini na Yeye ni mwenye kusikia, mwenye kujua.
Walimwambia Mtume(s.a.w.w)
kuwa yeye ni mchawi akawajibu kuwa Mwenyezi Mungu anajua ukweli wake na anajua kauli yao hii, kwa sababu hakifichiki kwake kitu chochote katika ardhi na katika mbingu. Atawahisabu na atawalipa vile mnavyostahiki.
Hakuna jawabu kwa anayeipinga haki isipokuwa kupelekwa kwenye mahakama ya uadilifu.
Lakina walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua, bali huyo ni mshairi.
Waliikataa wanamangamanga haki wakatafuta visingizio vya kutumia, wakabaki tu. Mwenye Majmaul-bayan anasema: “Hivi ndivyo anavyokuwa yule Mwenye kuhemewa. Anasema ni mchawi, mara ni mshairi, mara anaota. Hana moja analolishikilia. Huku ndio kujipinga kwa dhahiri.”
Basi atuletee ishara kama walivyotumwa wale wa mwanzo.
Washirkina walimwambia Muhammad(s.a.w.w)
: Ukiwa wewe ni Mtume basi tuletee muujiza, kama vile ngamia wa Swaleh, fimbo ya Musa na miujiza mingineyo ya mitume waliopita. Ndio Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema:
Hawakuamini kabla yao watu wa mji tuliouangamiza.
Maana ya jawabu hili ni kuwa, ni kweli kwamba mitume waliotangulia walikuja na miujiza, kama vile ngamia na fimbo, lakini watu wao hawakuwaamini, bali walikataa na wakamakadhibisha, ingawaje wao wenyewe ndio walioitaka. Kwa ajili hiyo tukawaangamiza.
Kwa hiyo inatakiwa enyi washirikina muangalie natija inayofungamana na miujiza sio muujiza wenyewe. Kwa sababu itawatokea hivyo hivyo, ikiwa Mwenyezi Mungu atawakubalia mapendekezo yenu.
Je, wataamini hao.
Yaani wale waliokuwa kabla yao hawakuamini miujiza waliyoipendekeza, vile vile hawa hawataamini miujiza wanayoipendekeza. Natija itakuwa ni kuangamizwa, kama walivyoangamizwa wa kwanza; ambapo hekima yake Mwenyezi Mungu ilipitisha kuwa waangamizwe kwa miujiza waliyoitaka.
وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧﴾
7. Na hatukuwatuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi. Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.
وَمَا جَعَلْنَاهُمْ جَسَدًا لَّا يَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَمَا كَانُوا خَالِدِينَ ﴿٨﴾
8. Na hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.
ثُمَّ صَدَقْنَاهُمُ الْوَعْدَ فَأَنجَيْنَاهُمْ وَمَن نَّشَاءُ وَأَهْلَكْنَا الْمُسْرِفِينَ ﴿٩﴾
9. Kisha tukawatimizia miadi na tukawaokoa wao na tuliowataka na tukawaangamiza waliopita mipaka.
لَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ كِتَابًا فِيهِ ذِكْرُكُمْ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٠﴾
10. Hakika tumewateremshia Kitabu, ndani yake mna ukumbusho wenu. Je, hamtii akili?
وَكَمْ قَصَمْنَا مِن قَرْيَةٍ كَانَتْ ظَالِمَةً وَأَنشَأْنَا بَعْدَهَا قَوْمًا آخَرِينَ ﴿١١﴾
11. Na miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawaumba baada yao watu wengine.
فَلَمَّا أَحَسُّوا بَأْسَنَا إِذَا هُم مِّنْهَا يَرْكُضُونَ ﴿١٢﴾
12. Basi walipohisi adhabu yetu mara wakaanza kukimbia.
تَرْكُضُوا وَارْجِعُوا إِلَىٰ مَا أُتْرِفْتُمْ فِيهِ وَمَسَاكِنِكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْأَلُونَ ﴿١٣﴾
13. Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu na maskani zenu mpate kusailiwa.
قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿١٤﴾
14. Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.
فَمَا زَالَت تِّلْكَ دَعْوَاهُمْ حَتَّىٰ جَعَلْنَاهُمْ حَصِيدًا خَامِدِينَ ﴿١٥﴾
15. Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya wamefyekwa wamezimika.
WAULIZENI WENYE KUMBUKUMBU
Aya 7 – 15
MAANA
Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi. Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.
Imekwishatangulia kwa herufi zake katika Juz. 14 (16:43).
Na hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.
wao wenyewe.
Manabii sio roho bila ya miili wala wao hawatakaa maisha hapa duniani. Wao ni kama watu wengine, hawana tofauti isipokuwa kwa kufikisha neno la Mungu na kwamba wao ni wakamilifu. Angalia Juz. 16 (20: 35) kifungu ‘Hakika ya Utume’.
Kisha tukawatimizia miadi na tukawaokoa wao na tuliowataka na tukawaangamiza waliopita mipaka.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaishiria kwenye kauli yake hii pale aliposema:
كَتَبَ اللَّـهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢١﴾
“Mwenyezi Mungu amekwishaandika: Hakika nitashinda mimi na Mitume wangu.“Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.” (58:21).
Na akasema tena:
إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ ﴿٥١﴾
“Hakika bila shaka tutawanusuru mitume wetu na walioamini katika maisha ya duniani na siku watakaposimama mashahidi.” (40:51).
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaahidi mitume na wau- mini kuokoka na makafiri kuangamia. Alitekeleza ahadi yake. Ni nani kuliko Mwenyezi Mungu katika utekelezaji ahadi?
MUHAMMAD NA WAARABU
Hakika tumewateremshia Kitabu, ndani yake mna ukumbusho wenu. Je, hamtii akili?
Kabla ya Muhammad(s.a.w.w)
na Qur’an waarabu hawakuwa ni chochote. Baada ya vitu viwili hivyo wakawa ni watu mashuhuri, ikatajwa historia namaendeleo yao, wakawa ni watu wa hali ya juu.
Anasema: W.L. Dewarnet katika Ensaiklopidia yake ya Historia ya kisa cha maendeleo katika ulimwengu: “Muhammad ni mkuu miongoni mwa wakuu wa Historia. Aliwainua watu walioishi katika giza la ushenzi, anga ya joto na ukame wa jangwa, kwenye ustawi wa kiroho na kimaadili. Alifaulu kwenye lengo hili kwa namna ambayo hajawahi kuifikia kiongozi yeyote katika historia yote.
Alipoanza mwito wake miji ya waarabu ilikuwa ni jangwa tupu linalokaliwa na makabila ya waabudu mizimu yenye watu wachache wasiokuwa na umoja wowote. Lakini kufikia kufa kwake wakawa ni umma wenye mshikamano, wakiwa wamekiuka ubaguzi na upuuzi.
Wakawa juu ya uyahudi na ukiristo na dini ya nchiyake ikawa wazi na nyepesi. Ikajengeka misingi ya kijasiri, utukufu na uzalendo. Kwenye kizazi kimoja tu ikaweza kushinda vita mia moja na katika karne moja ikaweza kuanzisha dola kuu na kubakia hadi leo kuwa ni nguvu kuu ulimwenguni”
Na miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawaumba baada yao watu wengine.
Haya ni makemeo na kiaga kwa wale wanaomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w)
kwamba wao yatawapata yaliyowapata waliokuwa kabla yao katika umma zilizowakadhibisha mitume wao. Kisha Mwenyezi Mungu awalete wengine wasiokuwa na uhusiano wowote na walioangamizwa; awarithishe milki zao na majumba yao. Wajenge upya na wastarehe na kheri zake na baraka zake.
Basi walipohisi adhabu yetu mara wakaanza kukimbia.
Hii ni taswira ya hali ya washirikina inapowafikia adhabu kutoka mbinguni, wanajaribu kuikimbia, lakini wapi! Inawezekana vipi kuukimbia utawala wa Mwenyezi Mungu na hukumu yake? Kama hapo mwanzo wangelikimbilia kwa Mwenyezi Mungu wangelikuta amani. Ama kumkimbia yeye Mwenyezi Mungu ni sawa na mtu kukimbia kivuli chake.
Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu na maskani zenu mpate kusailiwa.
Kabla ya kuteremshwa adhabu washirikina walikuwa hawajishughulishi na lolote zaidi ya mali na starehe zao, lakini ilipowashukia adhabu, nyoyo na akili zao zilipofuka na wakatupilia mbali kila kitu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaambia kwa kuwatahayariza: Mnaenda wapi? Rudini kwenye mali zenu na watoto wenu.
Leo mnaziacha na jana mlikuwa mkiziabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Haya ndio malipo ya anayeacha uongofu na asiongoke kwenye uongofu.
Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.
Walitulia na starehe zao, wakaitikia matamanio yao na wakamtuhumu anayewapa nasaha, lakini walipoiona adhabu walijuta na wakaita ole wetu, lakini majuto ni mjuukuu hayarudishi yaliyopita.
Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya wamefyekwa wamezimika.
Wanalia ole wetu na adhabu iko kichwani mwao ikiendelea. Haikufaa mali wala jaha. Huo ndio mwisho wa wakosefu.
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ ﴿١٦﴾
16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.
لَوْ أَرَدْنَا أَن نَّتَّخِذَ لَهْوًا لَّاتَّخَذْنَاهُ مِن لَّدُنَّا إِن كُنَّا فَاعِلِينَ ﴿١٧﴾
17. Kama tungelitaka kufanya mchezo tungelijifanyia sisi wenyewe, kama tungekuwa ni wafanyao mchezo.
بَلْ نَقْذِفُ بِالْحَقِّ عَلَى الْبَاطِلِ فَيَدْمَغُهُ فَإِذَا هُوَ زَاهِقٌ وَلَكُمُ الْوَيْلُ مِمَّا تَصِفُونَ ﴿١٨﴾
18. Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka. Na ole wenu kwa mnayoyasifia
وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ ﴿١٩﴾
19. Ni vyake vilivyoko mbinguni na ardhini na walioko mbele yake hawafanyi kiburi wakaacha kumwabudu wala hawachoki.
يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ ﴿٢٠﴾
20. Wanamsabihi usiku na mchana wala hawanyog’onyei.
أَمِ اتَّخَذُوا آلِهَةً مِّنَ الْأَرْضِ هُمْ يُنشِرُونَ ﴿٢١﴾
21. Au wamepata miungu katika ardhi inayofufua.
لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا فَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٢٢﴾
22. Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika. Ametasika Mwenyezi Mungu, Mola wa arshi, na hayo wanayoyasifu.
لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ ﴿٢٣﴾
23. Yeye haulizwi kwa ayatendayo na wao ndio waulizwao kwa wayatendayo.
JE, VITENDO VYAKE MWENYEZI MUNGU MTUKUFU VINA MALENGO?
Aya 16 – 23
MAANA
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:191). Huko tumenukuu kauli kuhusiana na kuwa je, vitendo vya Mwenyezi Mungu vinakuwa na sababu ya malengo au kwake Mwenyezi Mungu hakuna ubaya wala hana wajibu wa chochote?
Kama tungelitaka kufanya mchezo tungelijifanyia sisi wenyewe, kama tungekuwa ni wafanyao mchezo.
Mchezo na upuuzi ni muhali kwa yule anayekiambia kitu kuwa na kikawa. Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: ‘Lau tungelitaka kama tungekuwa ni wafanyao mchezo’ yaani hatukataka wala hatufanyi. Lau angelitaka kufanya mchezo – kukadiria muhali sio muhali – angelijifanyia kwa namna yoyote inayolingana na cheo chake; sio katika namna ya waja; kama kucheza na wanawake na watoto.
Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka.
Makusudio ya haki hapa ni ukweli na uhakika kwa mkabala wa mchezo alioukanusha Mwenyezi Mungu Mtukufu na makusudio ya batili hapa ni upuzi na mchezo.
Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kusema hatufanyi mchezo sasa anasema kuwa vitendo vyake kwake ni uhakika na ukweli si mchezo na upuzi; bali ukija upuzi na mchezo kutoka popote anauvunjilia mbali. Vipi ataliridhia lile asiloliridhia kwa mwingine?
Na ole wenu kwa mnayoyasifia nayo Mwenyezi Mungu na kumbandika sifa za kutengeneza. Ni vyake vilivyoko mbinguni na ardhini na walioko mbele yake hawafanyi kiburi wakaacha kumwabudu wala hawachoki.
Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya walioko mbele yake, ni Malaika. Tunavyofahamu sisi ni kuwa makusudio ni kila mwenye cheo na jaha mbele ya Mwenyezi Mungu, awe Malaika au mtu.
Wanamsabihi usiku na mchana wala hawanyonyog’onyei.
Yaani hawachoki, bali wanadumu kwenye twaa katika kauli na vitendo wala hawamtuhumu Mwenyezi Mungu kwa kumsawirisha au kumpa sifa za kutengeneza.
Au wamepata miungu katika ardhi inayofufua.
Yaani kila anayeabudiwa na washirikina, hawezi kuhui wafu wala hawafufui wafu walio makaburini, bali Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayehui na kufisha.
Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika. Ametasika Mwenyezi Mungu, Mola wa arshi, na hayo wanayoyazua.
Tazama tuliyoyaandika kwenye Juz. 5 (4:48) Kifungu ‘Dalili ya umoja na utatu.’
Mwenye kujua ni hoja kwa asiyejua Yeye hahojiwi kwa ayatendayo na wao ndio wanaohojiwa kwa wayatendayo.
Baadhi wametoa dalili kwa Aya hii kwamba hakuna ubaya kwa Mungu wala hawajibikiwi na jambo lolote. Anaweza kumwadhibu mtiifu na kumlipa thawabu muasi. Lakini hii inapingana na uadilifu wake, hekima na rehema yake.
Usahihi hasa ni kuwa maana ya Aya ni Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kuwa ni mwadilifu kwa dhati yake, haijuzu kwa yeyote kumwingilia kwa kauli yake na vitendo vyake. Kwa sababu haijuzu kuambiwa mwadilifu, kwa nini umefanya uadilifu? Na mkweli, kuambiwa kwa nini umesema kweli? Kama ambavyo haifai kwa asiyejua utabibu kumwambia tabibu hodari, kwa nini unatoa dawa hii?
Mfano wa maswali haya unafaa kwa aliye kifani wake. Ama asiyejua kitu, analotakiwa ni kufanya juhudi ya kumtafuta mjuzi na kuhakikisha ujuzi wake kutokana na dalili na alama. Akishapata uhakika basi inakuwa ni wajibu kwake kumfuata kwa yale aliyo na ujuzi nayo; sawa na mgonjwa anavyomfuata tabibu.
Walikwishasema wahenga: “Ajuaye ni hoja kwa asiyejua.” Ikiwa mambo ni hivi kwa kiumbe pamoja na kiumbe mwenzake. Itakuwaje kwa kiumbe pamoja na muumba wa mbingu na ardhi?
Siku moja mwanafunzi alimuuliza mwalimu wake: “Kwa nini tuko na kwa nini tunaishi?”
Mwalimu akamwambia mwanafunzi wake: “Kwa nini ewe mwanangu unajilazimisha na mambo yasiyokuwa na mwanzo wala mwisho? Kwa nini usiamini dini ikastarehe nafsi yako na uawache yale usiyoyaweza, ufuate unayoyaweza? Wewe ni mmoja wa maelfu ya mamilioni ya watu na mji wako uanaoishi ni moja ya maelfu ya miji. Ardhi tunayoishi ni moja ya mamilioni ya sayari na ulimwengu ulio na sayari zote hizo, hatujui kuwa kuna mfano wake unaouzidia. Je, sehemu moja inaweza kudhibiti yote hayo? Je, tone moja linaweza kuihoji bahari?
Mwanangu! Mimi sisemi kuwa usifanye uchunguzi na kupeleleza, kwani kutafuta hakika ni miongoni mwa sababu za kupatikana binadamu, lakini maadamu akili yako ni ndogo kuweza kufahamu hakika hiyo, basi ngoja mpaka uzidi kupata ufahamu na utambuzi. Mwisho ukishindwa, liache jambo kama lilivyo. Kwa sababu udogo wa akili yako kufahamu jambo, haimaanishi kuwa jambo hilo ni mchezo na upuzi; isipokuwa inamaanisha kuwa hujalifahamu; kwa hiyo muachie aliyeumba vyote vilivyoko.”