4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA
وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾
51. Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uongofu wake zamani na tulikuwa tunamjua.
إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَـٰذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ ﴿٥٢﴾
52. Alipomwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayoyanga’ng’ania?
قَالُوا وَجَدْنَا آبَاءَنَا لَهَا عَابِدِينَ ﴿٥٣﴾
53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
قَالَ لَقَدْ كُنتُمْ أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٥٤﴾
54. Akasema: Hakika nyinyi na baba zenu mmekuwa kwenye upotofu ulio dhahiri.
قَالُوا أَجِئْتَنَا بِالْحَقِّ أَمْ أَنتَ مِنَ اللَّاعِبِينَ ﴿٥٥﴾
55. Wakasema: Je, umetujia kwa haki au wewe ni katika wafanyao mchezo?
قَالَ بَل رَّبُّكُمْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الَّذِي فَطَرَهُنَّ وَأَنَا عَلَىٰ ذَٰلِكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ ﴿٥٦﴾
56. Akasema: Bali Mola wenu ni Mola wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliyeziumba, na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
وَتَاللَّـهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَامَكُم بَعْدَ أَن تُوَلُّوا مُدْبِرِينَ ﴿٥٧﴾
57. Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu baada ya kunipa mgogo.
فَجَعَلَهُمْ جُذَاذًا إِلَّا كَبِيرًا لَّهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُونَ ﴿٥٨﴾
58. Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa kubwa lao ili wao walirudie.
قَالُوا مَن فَعَلَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا إِنَّهُ لَمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٩﴾
59. Wakasema: Ni nani aliyeyafanyia haya miungu wetu? Hakika huyu ni katika madhalimu.
قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٠﴾
60. Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.
IBRAHIM
Aya 51-60
MAANA
Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uongofu wake zamani na tulikuwa tunamjua.
Wametofautiana wafasiri kuhusu maana ya uongofu. Ikasemekana kuwa ni kuongoka kwenye utengenefu wa dini na dunia. Pia ikasemekana kuwa ni utume.
Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi kwa dalili ya kauli ‘zamani’ maana yake ni kabla ya mitume waliokuja baada ya Ibrahim
; kama vile Musa
, Isa
na Muhammad(s.a.w.w)
. Pia kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Na tulikuwa tunamjua’ ambayo maana yake ni kauli yake:
اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ﴿١٢٤﴾
“Mwenyezi Mungu diye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake.” Juz. (6:124).
Utume unatoka kwa Mungu, anamuhusisha nao mwenye kuustahiki, wala haupatikanai kwa bidii ya mtu; kama vile imani na takua. Ndio maana husemwa kuwa mumin, kuwa mcha Mungu, lakini haisemwi kuwa Mtume.
Alipomwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayoyanga’ng’ania?
Swali hili linaelekezwa kwa kila mwenye majukumu ya matendo yake na matumizi yake. Vipi mnavitukuza na kuviabudu visivyodhuru wala kunufaisha; na nyinyi mna akili na utambuzi?
Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
Mantiki hii anaikimbilia kila mwenye kushindwa na hoja na dalili. Ukimuuliza kwa nini umefanya hivi, atasema: Fulani amefanya.
Hakuna la kuwaambia watu wa aina hii, isipokuwa kauli ya Nabii Ibrahim:
Akasema: Hakika nyinyi na baba zenu mmekuwa kwenye upotofu ulio dhahiri.
Na upotofu hauwezi kubadilika kuwa uongofu hata ukifuatwa na wengi.
Wakasema: Je, umetujia kwa haki au wewe ni katika wafanyao mchezo?
Walijitia mshangao kutokana na kauli ya Ibrahim, kwa vile wanawaona baba zao wametakaswa na makosa; si kwa lolote ila ni kwa kuwa ni baba zao tu.
Mantiki haya hawahusiki nao kaumu ya Ibrahim tu, wala washirikina wengine; bali kila mwenye kuigiza wengine kwa upofu, yuko sawa na waabudu masanamu.
Akasema: Bali Mola wenu ni Mola wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliyeziumba,
Mimi sifanyi mchezo wala sitii shaka. Vipi nifanye mchezo na kutia shakashaka na hali Yeye ndiye muumba wa mbingu na ardhi namimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo?
Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu baada ya kunipa mgogo.
Ilivyo ni kwamba masanamu hayawezi kufanyiwa vitimbi, kwa sabau hayana hisia; isipokuwa wanaofanyiwa vitimbi ni waabudu masanamu, kwa hiyo kuyafanyia vitimbi ni majazi, sio hakika; isipokuwa yamefanywa ni nyenzo ya kufanyiwa vitimbi wanaoyaabudu.
Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa kubwa lao ili wao walirudie.
Ibrahim aliyavunja masanamu yote na akaliacha lile kubwa lao, ili wale wanaoyaabudu waliulize, kwa nini halikuweza kuwatetea wenzake wadogo nalo lina nguvu? Makusudio yako wazi; nayo ni kuwa washirikina wazingatie kuwa masanamu haya ikiwa hayo yenyewe hayawezi kujitetea, basi ndio hayawezi kumtetea mwengine.
Wakasema: Ni nani aliyeyafanyia haya miungu wetu? Hakika huyu ni katika madhalimu.
Usawa ni kuwa waulize miungu yao imemfanyia nini aliyeyavunja? Lakini haya ndiyo mantiki ya kijinga na kuiga.
Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.
Hii inaashiria kauli ya Ibrahim
: “Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu.”
Baada ya kuandika Juzuu ya sita, nilisoma kwenye mojawapo ya magazeti, kwamba wafukuaji, wamegundua mji wa kwanza wa Ibrahim, Uru. Ikabainika kwamba watu wake walikuwa wakiabudu nyota tatu: ndogo, wastani na kubwa.
Kwa hiyo mpangilio huu uliokuja katika Qur’an kupitia ulimi wa Ibrahim ndio mpangilio wa kimantiki ambao unafuatana na maisha ya wakati huo. Hivi ndivyo elimu inavyoleta dalili kila siku juu ya ukweli wa Muhammad(s.a.w.w)
katika kila aliyoyaeleza.
قَالُوا فَأْتُوا بِهِ عَلَىٰ أَعْيُنِ النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَشْهَدُونَ ﴿٦١﴾
61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia.
قَالُوا أَأَنتَ فَعَلْتَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٢﴾
62. Wakasema: Je, wewe ndiwe uliyeifanyia haya mingu yetu ewe Ibrahim?
قَالَ بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَـٰذَا فَاسْأَلُوهُمْ إِن كَانُوا يَنطِقُونَ ﴿٦٣﴾
63. Akasema: Bali ameyafanya hayo mkubwa wao huyu. Basi waulizeni ikiwa wanatamka.
فَرَجَعُوا إِلَىٰ أَنفُسِهِمْ فَقَالُوا إِنَّكُمْ أَنتُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٦٤﴾
64. Basi wakajirudi nafsi zao. Wakasema: Hakika nyinyi ndio madhalimu.
ثُمَّ نُكِسُوا عَلَىٰ رُءُوسِهِمْ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا هَـٰؤُلَاءِ يَنطِقُونَ ﴿٦٥﴾
65. Kisha wakasimamia vichwa vyao. Wewe unajua kwamba hawa hawasemi.
قَالَ أَفَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكُمْ شَيْئًا وَلَا يَضُرُّكُمْ ﴿٦٦﴾
66. Akasema: Basi nyinyi mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu visivyo wanufaisha kitu wala kuwadhuru?
أُفٍّ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾
67. Kefule yenu na mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Basi hamtii akili?
قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿٦٨﴾
68. Wakasema: Mchomeni na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo.
قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾
69. Tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
وَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَخْسَرِينَ ﴿٧٠﴾
70. Na wakamtakia ubaya, lakini tukawafanya wao ndio wenye kupata hasara.
WAKASEMA: MLETENI
Aya 61 – 70
MAANA
Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia.
Walitaka wamsaili na kumhukumu mbele ya watu wamshuhudie; kisha waone adhabu itakayompata.
Wakasema: Je, wewe ndiwe uliyeifanyia haya mingu yetu ewe Ibrahim?
Walimleta na wakaanza kumhoji. Akasema:
Bali ameyafanya hayo mkubwa wao huyu. Basi waulizeni ikiwa wanatamka.
Kutamka ni katika hali ya kukadiria; ikiwa hawa wana hisia basi aliyefanya ni mkubwa wao. Mfano kusema: ikiwa Mwenyezi Mungu ana mtoto, basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kumwabudu.
Kwa ujumla ni kwamba makusudio ni kuwanyamazisha kwa hoja, na kwamba masanamu haya, kama yangekuwa ni Mungu yangelikuwa na utambuzi, kusema na kumvunajilia mbali anayetaka kuyafanyia ubaya.
Basi wakajirudi nafsi zao.
Baada ya kusikia aliyoyasema Ibrahim
waliulizana: Vipi tuabudu mawe na kutarajia kheri na kuhofia shari yake na hayo yenyewe hayawezi kujikinga na madhara.
Wakasema: Hakika nyinyi ndio madhalimu.
Waliishia kukiri kuwa wao wako katika ujinga, lakini mara tu wakarudia kwenye hali yao ya mwanzo.
Kisha wakasimamia vichwa vyao.
Makusudio ya kusimamia vichwa hapa ni kurudi kwenye uovu wao. Neno lililotumika ni nukisu lenye maana ya kuweka kichwa chini miguu juu. Yaani kumpa silaha adui yako akuue nayo, au kumpa hoja mtu kutokana na vitendo vyako au kauli yako; kama walivyofanya kaumu ya Ibrahim, waliposema:
Wewe unajua kwamba hawa hawasemi.
Ikiwa hawasemi, basi vipi mnawaabudu. At-Tabariy anasema: “Kupindua jambo ni kulifanya kichwa chini miguu juu na kupindua hoja ni kuifanya hoja ya hasimu wako ndio hoja yako; kama walivyofanya kaumu ya Ibrahim.”
Akasema: Basi nyinyi mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu visivyo wanufaisha kitu wala kuwadhuru?
Nyinyi mnajua kuwa haya masanamu hayana utambuzi wala matamshi, hayadhuru wala hayanufaishi, basi vipi mnayaabudu?
Kefule yenu na na mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Basi hamtii akili?
Utafanya nini na watu wanaong’ang’ania upotevu na wao wanajua kuwa huo ni upotevu. Hakuna cha kuwafanya isipokuwa kuwaaambia: poteleeni mbali, enyi mnaofanana na watu na wala sio watu.
Wakasema: Mchomeni na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo.
Wanusuruni miungu, lakini miungu yenyewe haiwezi kujinusuru, na bado ni miungu tu! Ni sawa na yule aliyesema: ‘Huyo ni paa hata kama ameruka angani.’ Huko ndiko kuweka kichwa chini miguu juu.
Tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
Walisema na Mwenyezi Mungu naye akasema. Wala hakuna mwenye kurudisha kauli yake.
Unaweza kuuliza
: Kwa kawaida moto unaunguza, vipi uwe baridi.
Jibu
: Mwenye kuleta athari wa kwanza kwa kila kilichpo ni Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka ukuu wake. Yote hutokana na Yeye, na kwake zinaishia nyenzo zote, ziwe ni sharti, sababu au chochote. Kuunguza kunatokana na moto, moto unatokana na kuni, kuni ni maumbile yaliyotokana na neno lake.
Yeye ndiye aliyeumba moto ambao unaunguza, lakini kwa sharti ya kutouambia ‘kuwa baridi.’ Kwa hiyo kama atauambia hivyo utakuwa kama alivyosema. Kwa maneno mengine ni kuwa kuunguza kwake na kuwa baridi kwake kunafuta matakwa ya Mungu kutokana na kuumba kwake na kuufanya uweko.
Na wakamtakia ubaya, lakini tukawafanya wao ndio wenye kupata hasara.
Waliwasha moto ili umchome Ibrahim, lakini ukawa ni muujiza mkubwa na dalili ya kuthibitisha ukweli wake na utume wake:
وَمَكَرُوا وَمَكَرَ اللَّـهُ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ ﴿٥٤﴾
“Na wakapanga hila; na Mwenyezi Mungu akapanga hila; na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga hila” Juz. 3 (3:54).
Katika baadhi ya tafsiri za zamani, imeelezwa kuwa Namrud alipoona moto haumuathiri Ibrahim, aliamuru mali zake zichukuliwe na yeye mwenyewe atolewe nchini.
Ibrahim akasema: Mkichukua mali zangu basi nirudishieni umri wangu nilioumaliza kwenye nchi yenu. Wakaenda mahakamani, hakimu akatoa hukumu ya kunyang’anyawa mali Ibrahim na Namrud amrudishie umri wake. Hapo akasalimu amri na akamwacha Ibrahim na mali zake. Hekaya hii hatukuinukuu kwa kuamini kuwa ni kwali hivyo; isipokuwa inaonyesha kuwa kila mtu ana haki ya umri wake alioumaliza kwa sharti ya kuwa ameutumia kwenye halali.
وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ ﴿٧١﴾
71. Na tukamwokoa yeye na Lut tukawapeleka kwenye ardhi tuliyoibariki, kwa ajili ya walimwengu wote.
وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ نَافِلَةً وَكُلًّا جَعَلْنَا صَالِحِينَ ﴿٧٢﴾
72. Naye tukampa Is-haq na Yakub kuwa ni zawadi. Na wote tukawajaalia wawe watu wema.
وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِمْ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ وَإِقَامَ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءَ الزَّكَاةِ وَكَانُوا لَنَا عَابِدِينَ ﴿٧٣﴾
73. Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri na wasimamishe Swala na watoe Zaka na walikuwa wanatuabudu sisi.
وَلُوطًا آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَت تَّعْمَلُ الْخَبَائِثَ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمَ سَوْءٍ فَاسِقِينَ ﴿٧٤﴾
74. Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa wabaya, mafasiki.
وَأَدْخَلْنَاهُ فِي رَحْمَتِنَا إِنَّهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٧٥﴾
75. Na tukamwingiza katika rehema zetu. Hakika yeye ni miongoni mwa walio wema.
وَنُوحًا إِذْ نَادَىٰ مِن قَبْلُ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ ﴿٧٦﴾
76. Na Nuh alipoita zamani, nasi tukamwitikia na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
وَنَصَرْنَاهُ مِنَ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمَ سَوْءٍ فَأَغْرَقْنَاهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٧٧﴾
77. Na tukamnusuru na watu waliozikadhibisha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawagharikisha wote.
TUKAMWOKOA YEYE NA LUT
Aya 71 – 77
MAANA
Na tukamwokoa yeye na Lut tukawapeleka kwenye ardhi tuliyoibariki, kwa ajili ya walimwengu wote.
Makusudio ya aliyeokolewa hapa ni Ibrahim
. Lut ni mtoto wa kaka yake. Katika Tafsiri imelezwa kuwa Ibrahim aliondoka akaelekea nchi ya Sham, ambayo ndani ilikuwako Palestina.
Vyovyote iwavyo ni kwamba makusudio ni kumfananisha Muhammad(s.a.w.w)
na kaumu yake pamoja na Ibrahim
na kaumu yake.
Kaumu zote mbili ziliabudu masanamu, zikakataa mwito wa nabii wao na kujaribu kumuua. Manabii wote wawili Mungu aliwaokoa na kuwatengenezea njia ya hijra na kuwaneemesha kwa hijra hiyo.
Naye tukampa Is-haq na Yakub kuwa ni zawadi.
Is-haq ni mtoto wa Ibrahim wa kumzaa, na Yakub ni mjukuu naye ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na wote tukawajaalia wawe watu wema.
Ibrahim, Is-haq , wote walikuwa wema.
Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri na wasimamishe Swala na watoe Zaka na walikuwa wanatuabudu sisi.
Maimamu ndio viongozi wa dini ambao amewateua Mwenyezi Mungu, kuwaongoza waja. Sifa yao kuu ni kwamba wao wanaongoza watu kama alivyoamrisha Mungu, si kama wanavyoamrisha wake zao, watoto wao au wakwe zao; wanahimiza kufanya kheri sio chuki za utaifa; na kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake sio mwenginewe.
Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa wabaya, mafasiki. Na tukamwingiza katika rehema zetu. Hakika yeye ni miongoni mwa walio wema.
Tazama tafsiri yake katika Juz. 8 (7: 80) na Juz 12 (11:77).
Na Nuh alipoita zamani, nasi tukamwitikia na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa. Na tukamnusuru na watu waliozikadhibisha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawagharikisha wote.
Kisa cha Nuh kimetangulia katika Juz. 12 (11:25).