6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA
إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ ﴿٩٢﴾
92. Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu kwa hivyo niabuduni.
وَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ كُلٌّ إِلَيْنَا رَاجِعُونَ ﴿٩٣﴾
Na wakalivunja jambo lao baina yao. Wote watarejea kwetu.
فَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا كُفْرَانَ لِسَعْيِهِ وَإِنَّا لَهُ كَاتِبُونَ ﴿٩٤﴾
94. Na atendaye mema naye ni mumin, basi haitakataliwa bidii yake na hakika sisi tutamwandikia.
وَحَرَامٌ عَلَىٰ قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَنَّهُمْ لَا يَرْجِعُونَ ﴿٩٥﴾
95. Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.
حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍ يَنسِلُونَ ﴿٩٦﴾
96. Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.
وَاقْتَرَبَ الْوَعْدُ الْحَقُّ فَإِذَا هِيَ شَاخِصَةٌ أَبْصَارُ الَّذِينَ كَفَرُوا يَا وَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا بَلْ كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٩٧﴾
97. Na miadi ya haki itakaribia, ndipo yatakapokodoka macho ya wale waliokufuru. Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa ni wenye kudhulumu.
إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ ﴿٩٨﴾
98. Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.
لَوْ كَانَ هَـٰؤُلَاءِ آلِهَةً مَّا وَرَدُوهَا وَكُلٌّ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٩٩﴾
99. Lau haya yangelikuwa ni miungu yasingeliingia na wote watadumu humo.
لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَهُمْ فِيهَا لَا يَسْمَعُونَ ﴿١٠٠﴾
100. Lao humo ni kupiga mayowe na wala hawatasikika.
UMMA MMOJA
Aya 92 – 100:
MAANA
Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu kwa hiyo niabuduni.
LUGHA
Maana ya neno umma ni watu wenye lugha moja na historia moja. Kisha neno hili likawa linatumika zaidi kwa maana ya dini na mila. Maana haya ndiyo yaliyokusudiwa hapa.
Umma wenu huu ni itikadi ya mitume ambayo ni tawhid pamoja na kufuata amri za Mwenyezi Mungu kwa kauli na vitendo. Msemo ‘wenu’ unaelekezwa kwa watu wote.
Maana ni kuwa enyi watu wote! Shikeni dini ya Tawhidi waliyokuwa nayo Mitume na mumwabudu Mungu mmoja aliye peke na mumfanyie ikhlasi katika kauli na vitendo.
Na wakalivunja jambo lao baina yao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamrisha wote wawe kwenye itikadi ya tawhidi, lakini wakagawanyika wakawa makundi ya wakana Mungu na washirikina. Hata wale wafuasi wa Mitume nao wanatukanana na kujitenga na wengine; bali hata wafuasi wa Mtume mmoja nao ni hivyo hivyo.
Wote watarejea kwetu.
Haya ni makemeo na hadhari kwa wale wanaofarikiana wakawa vikundi.
Na atendaye mema naye ni mumin, basi haitakataliwa bidii yake na hakika sisi tutamwandikia.
Imani pamoja na matendo mema ni njia ya Peponi na imani bila ya matendo haifai chochote. Hiyo ni kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ﴿١٥٨﴾
“Basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.” Juz. 8 (6:158).
Ama matendo mema bila ya imani, humnufaisha mtendaji kwa namna moja au nyingine na huenda ikamfaa huko Akhera kwa kupunguziwa adhabu. Tumeyafafanua hayo katika Juz. 4 (3:158) kwenye kifungu ‘kafiri na amali njema’ Pia Umepita mfano wake katika Juz. 14 (16: 97)
Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.
Aya hii ni jawabu la swali la kukadiria, kwamba je, washirikina katika watu wa kijiji kilichoangamizwa na Mwenyezi Mungu kwa kufuru yao, watarudishwa tena kuwa hai na kuadhibiwa huko Akhera, kama walivyoadhibiwa duniani?
Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa watu wote, kesho watarejea kwa Mwenyezi Mungu; hata wale walioangamizwa duniani kwa dhambi zao na ni muhali kukosa kurejea kwa Mwenyezi Mungu baada ya mauti; bali hakuna budi lazima watafufuliwa.
Swali la pili
: je inafaa kuadhibiwa akhera baada ya kuadhibiwa duniani? Huko si ni kuadhibu mara mbili kwa kosa moja?
Jibu
: Hapana! Kuadhibiwa kwao duniani kulikuwa ni kwa ajili ya kuwakadhibisha kwao Mitume waliowajia na miujuza; kama zinavyofahamisha Aya hizi zifuatazo na nyinginginezo mfano wake:
وَقَوْمَ نُوحٍ لَّمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ ﴿٣٧﴾
“Na kaumu ya Nuh walipowakadhibisha Mitume tuliwagharikisha” (25:37)
كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ ﴿١٢﴾ وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ ﴿١٣﴾ وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ ﴿١٤﴾
“Kabla yao walikadhibisha kamu ya Nuh na watu wa Rassi na Thamud na A’d na Firauni na ndugu wa Lut na watu wa vichakani na kaumu ya Tubbai, wote waliwakadhibisha Mitume, kwa hiyo kiaga kikathibitika juu yao.” (50: 12-14).
Ama adhabu ya Akhera ni ya ukafiri wenyewe na madhambi mengineyo; kama dhulma n.k.
Kwa hiyo adhabu zinakuwa nyingi kutokana na dhambi kuwa aina nyingi, sio kwa dhambi moja.
Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.
Katika Juz. 16 (18: 94) tuliwanukuu baadhi ya wafasiri wakisema kuwa Juju ni wa Tatars na Majuju ni Wamongoli. Vile vile tumesema huko kuwa ukuta wa Juju na Majuju hauko tena. Kwa hiyo basi makusudio ya kufunguliwa Juju na Majuju ni kuenea kwao katika mabara.
Vyovyote iwavyo sisi hatujawahi kusoma ya kutegemewa kuhusu Juju na Majuju, si katika tafsiri wala mahali penginepo. Kwa hiyo tutasimama kwenye dhahiri ya nukuu ya Qur’an tu na ufafanuzi tutawachia wengine.
Na miadi ya haki itakaribia, ndipo yatakapokodoka macho ya wale waliokufuru.
Makusudio ya miadi ya haki hapa ni Kiyama, hapo akili za waliokufuru zitapotea na macho yatatoka kutokana na vituko vya siku hiyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14: 42).
Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
Yaani watasema hivyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:5) na katika juzuu na Sura hii tuliyo nayo Aya 14 na 46.
Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.
Hapa wanaambiwa washirikina wa Makka. Makusudio ya mnayoyaabudu ni masanamu yao. Maana ni kuwa, enyi washirikina! Nyinyi na masanamu yenu mtakutana kwenye Jahannamu kesho. Kuna Hadithi isemayo: “Mtu yuko pamoja na anayempenda.”
Unaweza kuuliza
: Kuna faida gani ya kutiwa masanamu kwenye Jahannamu na ni mawe yasiyokuwa na utambuzi wala hisiya?
Wafasiri wamejibu kuwa lengo ni kuwazidishia masikitiko wale wanaoyaabudu, kila watakapoyaona karibu nao. Lakini jawabu hili ni kiasi cha kuchukulia uzuri na hisia tu. Lilio bora ni kuicha Aya nyingine ijibu:
فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ﴿٢٤﴾
“Basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri.” Juz. 1 (2:24).
Kuna riwaya isemayo kuwa Ibn Az-Zab’ariy – mmoja wa washirkina wa kikuraishi na mshairi wao – aliingilia Aya hii kama mayahudi wanamwabudu Uzayr na wanaswara (wakristo) wanamwabudu Masihi na hawa wawili ni watu wa Peponi, kama anavyosema Muhammad, sasa vipi aseme kila kinachoabudiwa ni kuni?
Mtume akamjibu: Ni ujinga ulioje wako wewe kutojua lugha ya watu wako. Kwani huoni herufi ma (ambayo) ni ya visivyo na akili?
Zaidi ya hayo maneno yanawahusu washirikina wa kikurashi, kama tulivyotangulia kusema nao wanaabudu masanamu.
Lau haya yangelikuwa ni miungu yasingeliingia na wote watadumu humo.
Haya ni ishara ya masanamu. Maana ya Aya yako wazi, kwamba lau masanamu yangelikuwa miungu yasingeliiingia motoni. Ni kama kusema: Lau ungelikuwa mwaminifu usingelifanya khiyana, lakini umefanya khiyana kwahiyo wewe si mwaminifu. Mfano huu katika mantiki unaitwa kutoa dalili kwa kipimo cha kuvua (istithnaiyy).
Lao humo ni kupiga mayowe na wala hawatasikika.
Hapa anaambiwa kila mkosaji, awe mwislamu au kafiri. Humo ni humo ndani ya Jahannam. Maana ni kuwa kila mkosaji atakuwa katika Jahannam akilalama kwa machungu; hatasikia neno la upole wala huruma, bali atakayemuona atamtahayariza na kumsema:
وَقِيلَ لِلظَّالِمِينَ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ ﴿٢٤﴾
“Na wenye kudhulumu wataambiwa onjeni yale mliyokuwa mkiyachuma.” (39:24).
إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ ﴿١٠١﴾
101. Hakika wale ambao umewatangulia wema kutoka kwetu, hao watatenganishwa na hayo.
لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ ﴿١٠٢﴾
102. Hawatasikia mvumo wake. Nao watudumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.
لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿١٠٣﴾
103. Hiyo fazaa kubwa haitawahuzunisha. Na Malaika watawapokea: Hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.
يَوْمَ نَطْوِي السَّمَاءَ كَطَيِّ السِّجِلِّ لِلْكُتُبِ كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ وَعْدًا عَلَيْنَا إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ ﴿١٠٤﴾
104. Siku tutakapozikunja mbingu mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni wenye kufanya.
وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِي الزَّبُورِ مِن بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِيَ الصَّالِحُونَ ﴿١٠٥﴾
105. Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa Ardhi watairithi waja wangu walio wema.
إِنَّ فِي هَـٰذَا لَبَلَاغًا لِّقَوْمٍ عَابِدِينَ ﴿١٠٦﴾
106. Hakika katika haya kuna ujumbe kwa wafanyao ibada.
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾
107. Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.
ARDHI WATARITHI WAJA WANGU WALIO WEMA
Aya 101 – 107
MAANA
Hakika wale ambao umewatangulia wema kutoka kwetu, hao watatenganishwa na hayo.
Mwenyezi Mungu aliwaahidi wenye takua kuamiliana nao kwa wema. Miongoni mwa wema huo ni kuokoka na moto.
Hawatasikia mvumo wake.
Hii ni kusisitiza watakavyokuwa mbali nao.
Nao watudumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.
Watasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu wakineemeshwa kwenye Pepo yake.
Hiyo fazaa kubwa haitawahuzunisha, sikwambii ndogo tena.
Kwani fazaa zina daraja, kuanzia machungu ya kukata roho, upweke wa kaburini, kisha kutoka makaburini kwa ajili ya hisabu hadi kuingia Jahannam.
Na Malaika watawapokea: Hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.
Malaika watawapokea kwa takrima na kuwaambia kuwa Mwenyezi Mungu amewakusanya kwenye siku hii aliyowaahidi kwa ufalme wa daima na neema isiyokatika. Aya hizi tatu zinafupilizwa na neno:
هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ ﴿٦٠﴾
“Je, malipo ya hisani si ni hisani tu.” (55:60)
Au neno:
لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ﴿٢٦﴾
“Kwa wafanyao wema ni wema.” Juz.11 (10:26).
Siku tutakapozikunja mbingu mkunjo wa karatasi za vitabu.
Makusudio ya vitabu hapa ni maandishi ya matamko yanayoayaandikwa kwenye karatasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atazikunja sayari, siku ya Kiyama, pamoja na ukubwa na wingi wake; kama inavyokunjwa karatasi yenye maandishi; kiasi ambacho kila sayari itafanana na herufi au neno lilo kwenye karatasi.
Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni wenye kufanya.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amefananisha ufufuo na kuumba kwa kwanza; kwamba, kama kulivyowezekana kwa kwanza, basi kwa pili pia kuunawezekana. Si muhali kwa Mwenyezi Mungu kutekeleza ahadi yake.
Hilo halimshindi Mwenyezi Mungu; kwani mwenye kuumba ulimwengu basi hawezi kushindwa kuurudisha tena baada ya kuharibika na kutawanyika:
وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ﴿٢٧﴾
“Na Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha. Na hilo ni jepesi zaidi kwake” (30:27).
TENA MAHDI ANAYENGOJEWA
Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa Ardhi watairithi waja wangu walio wema.
Zaburi ni kitabu cha Daud na ukumbusho ni vitabu vya mbinguni vilivyotangulia; kama vile vitabu vya Ibrahim na Musa. Maana yake ni kuwa utawala wa dunia, ingawaje hivi sasa uko mikononi mwa mataghuti waovu, lakini Mwenyezi Mungu atauhamisha uende kwa walio wema. Hilo halina budi. Hapo amani na uadilifu utaenea ardhini na watu wote wataneemeka na kheri za Ardhi na baraka zake.
Kuna Hadithi nyingi zenye maana ya Aya hii; miongoni mwazo ni ile aliy- oipokea Abu Daud katika Kitabu cha Sunan, ambacho ni mojawapo ya Sahihi sita: “Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu:
Lau haitabakia katika dunia isipokuwa siku moja tu, basi Mwenyezi Mungu angeliirefusha siku hiyo mpaka amtume mtu kutoka katika watu wa nyumba yangu (Ahlu bayt) jina lake linafanana na jina langu, na jina la baba yake ni kama la baba yangu, ataijaza ardhi uadilifu baada ya kujazwa dhulma na jeuri” [4]
.
Kanuni ya maisha hailikatai hilo, bali inalithibitisha na kulisisitiza. Ikiwa nguvu hivi sasa ziko mikononi mwa unyama wenye kudhuru wa umoja wa mataifa, baraza la usalama n.k. basi hakuna litakalozuia, siku moja kugeuka nguvu hiyo kutoka mikononi mwa madhalimu waovu hadi kwa watu wa haki na uadilifu; bali maumbile yanapenda kujikomboa na dhulma.
Pia kuna misingi isemayo: “Kila kilicho katika ardhi kina harakati, kama ilivyo na harakati ardhi na kwamba kudumu hali ni muhali.” Yote hayo yanapelekea kuwa hatimaye nguvu zitakuwa mikononi mwa wema wanao- faa.
Hakika katika haya kuna ujumbe kwa wafanyao ibada.
Haya ni haya ya kuwa ardhi itarithiwa na waja wema; hata kama ni baada ya muda. Makusudio ya wafanyao ibada hapa ni wale wanaopata mawaidha kwa kuzingatia na kunufaika na maonyo.
Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
. Risala yake ni rehema kwa wa mwanzo na wa mwisho. Huko nyuma tumeeleza mara nyingi kuhusu misingi ya risala hiyo na mafunzo yake.
Inatosha, kuthibitisha hilo, kauli za mwenye risala hiyo; kama vile: “Hakumwamini Mwenyezi Mungu yule ambaye watu hawamwamini. Likikuhuzunisha ovu na likakufurahisha jema, basi wewe ni mumin.”
Ni kwa hisia hizi ndio uadilifu utasimama, amani kuenea na maisha kuwa bora. Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu hilo katika Juz. 7 (6:92).
قُلْ إِنَّمَا يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٨﴾
108. Sema: Hakika umeletwa wahyi kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Je nyinyi mmesilimu?
فَإِن تَوَلَّوْا فَقُلْ آذَنتُكُمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ وَإِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ أَم بَعِيدٌ مَّا تُوعَدُونَ ﴿١٠٩﴾
109. Kama wakikataa, basi sema: Nimewatangazia sawasawa. Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.
إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ مِنَ الْقَوْلِ وَيَعْلَمُ مَا تَكْتُمُونَ ﴿١١٠﴾
110. Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua mnayoyaficha.
وَإِنْ أَدْرِي لَعَلَّهُ فِتْنَةٌ لَّكُمْ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ ﴿١١١﴾
111. Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
قَالَ رَبِّ احْكُم بِالْحَقِّ وَرَبُّنَا الرَّحْمَـٰنُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ ﴿١١٢﴾
Akasema: Mola wangu! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasifia.
HAKIKA MUNGU WENU NI MMOJA TU
Aya 108 – 112
MAANA
Sema: Hakika umeletwa wahyi kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Je nyinyi mmesilimu?
Mwenyezi Mungu alimwarisha Mtume wake awaambie washirikina kuwa Mwenyezi Mungu ameniletea wahyi kwamba Yeye ni mmoja tu hana mshirika katika kuumba kwake na wala katika ujuzi wake.
Ulimwengu huu na maajabu yake na kanuni zake unashuhudia kwa uwazi juu ya umoja, uweza na ukuu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Basi kwa nini hamuamini na kufuata amri yake? Kwanini mnadanganyika kuacha kumwabudu Yeye na kwenda kuabudu mawe yasiyodhuru wala kunufaisha?
Kama wakikataa, basi sema: Nimewatangazia sawasawa.
Baada ya kuwalazimu hoja ya kufikisha na maonyo, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu awaambie kuwa nimekishatekeleza wajibu wangu na nikafikisha risala ya Mola wangu. Kwa hiyo haukubaki udhuru wowote kwenu.
Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.
Mimi nina yakini na adhabu yenu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameiahadi na kuwahadhirisha nayo, na ahadi yake Mwenyezi Mungu ni ya kweli na adhabu yake pia ni kali zaidi, lakini sijui itakuwa lini. Ni sawa iwe karibu au mbali, lakini ina wakati wake. Ngojeni nami niko pamoja nanyi katika wenye kungojea.
Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua mnayoyaficha.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:7).
Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
Sijui kuna hekima gani ya kupewa kwenu muda na kucheleweshewa adhabu. Je Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaka kumdhirisha kila mmoja hakika yake, aweze kutubia mwema na aendelee mouvu au ametaka mustarehe siku zilizobakia kwenye umri wenu? Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye.
Akasema (Muhammad): Mola wangu! Hukumu kwa haki.
Yaani idhihirishe haki na uwanusuru watu wake kwa wale wanaoipinga.
Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasema kuwa masanamu yenu ni miungu na madai yenu kwangu kuwa ni mzushi.
Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wewe ni mtukufu kwa kila anayekuzulia. Wema ni wa yule anayekufuata, akachukua athari yako na akamwambia mzushi, kama vile ulivyosema wewe:
Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasifia.
MWISHO WA SURA YA ISHIRINI NA MMOJA