9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ وَأُحِلَّتْ لَكُمُ الْأَنْعَامُ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ ﴿٣٠﴾
30. Ndivyo hivyo! Na anayeitukuza miiko ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake. Na mmehalalishiwa wanyama howa ila wale mliosomewa. Basi jiepusheni na uchafu wa mizimu na mjiepushe na kauli ya uzushi.
حُنَفَاءَ لِلَّـهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ السَّمَاءِ فَتَخْطَفُهُ الطَّيْرُ أَوْ تَهْوِي بِهِ الرِّيحُ فِي مَكَانٍ سَحِيقٍ ﴿٣١﴾
31. Kwa kumtakasia imani Mwenyezi Mungu bila ya kumshirikisha. Na anayemshrikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukampeleka mahala mbali.
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾
32. Ndivyo hivyo! Na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu. Basi hiyo ni katika takua ya nyoyo.
لَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ مَحِلُّهَا إِلَى الْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٣٣﴾
33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda uliowekwa kisha mahali pake ni nyumba ya kale.
وَلِكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنسَكًا لِّيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ ﴿٣٤﴾
34. Kila umma tumeujaalia mihanga ya ibada, ili wamtaje Mwenyezi Mungu katika vile alivyowaruzuku katika wanyama howa. Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, Kwa hiyo jisalimisheni kwake. Na wabashirie wanyenyekevu.
الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَالصَّابِرِينَ عَلَىٰ مَا أَصَابَهُمْ وَالْمُقِيمِي الصَّلَاةِ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣٥﴾
35. Ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka na walio na subira kwa yale yaliyowasibu, na wanao-simamisha Swala, na wanatoa katika tulivyowaruzuku.
MIIKO YA MUNGU NA NEMBO ZAKE
Aya 30 -35
MAANA
Ndivyo hivyo! Na anayeitukuza miiko ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake.
Kutukuza kuko aina nyingi kutegemea na anayetukuzwa na namna ya kutukuzwa inayokubaliana naye.
Hakuna kitu kinachokubaliana na kumtukuza muumba isipokuwa kumtii na kufuata amri yake katika kila jambo. Atakayemtii Mwenyezi Mungu na akafuata amri zake na kuacha makatazo yake, basi atakuwa ametukuza na kuadhimisha miiko yake na nembo zake. Taadhima hii au utiifu huu unamwinua aliyeutenda kwa muumba wake, sio kuwa unamwinua muumbaji, kwa sababu Yeye hawahitajii walimwengu.
Ndio maana akasema:‘Hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake’ yaani kutukuza hukumu za Mwenyezi Mungu kwa kumtii ni kheri ya huyo mtiifu.
Na mmehalalishiwa wanyama howa ila wale mliosomewa.
Mwenyezi Mungu amemharamishia anayehiji kuwinda akiwa katika Ihram yake, pengine anaweza akadhania kuwa ameharamishiwa kula nyama ya wanyama wa kufugwa. Ndio akabainisha kuwa hakuna uhusiano baina ya mawili hayo; na kwamba walioharamishwa ni mfu na waliochinjiwa mizimu. Angalia Juz. 6 (5:3).
Basi jiepusheni na uchafu wa mizimu.
Jiepusheni nayo na msiiabudu, kama mnavyojiepusha na uchafu, kwa sababu yote ni uchafu, ndio maana ikafasiriwa uchafu wa mizimu, ingawaje kuna herufi min, ambayo hapa imekuwa ya kueena na sio ya baadhi, kama inavyokuwa mara kwa mara.
Na mjiepushe na kauli ya uzushi.
Kauli ya uzushi inachanganya kila lilioharamishwa; iwe ni uongo, kusengenya, shutuma na ufyosi. Uzushi mbaya zaidi ni kuleta ushahidi wa uongo, kwa sababu unanyima haki ya Mungu na ya watu. Mtume(s.a.w.w)
anasema: “Uzushi umelinganishwa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu,” kisha akasoma Aya hii.
Kwa kumtakasia imani Mwenyezi Mungu bila ya kumshirikisha.
Yaani kushikamana na dini ya haki na kuachana na dini potofu. Bila ya kumshirikisha ni msisitizo wa hayo. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:107).
Na anayemshrikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukampeleka mahala mbali.
Hiki ni kinaya cha dhambi ya shirki kwamba haifanani na dhambi yoyote, na kwamba adhabu ya mshirikina haishindwi na adhabu yoyote. Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an na Sunna za Mtume ataona kuwa mshirikina ana dhambi kubwa zaidi kuliko mlahidi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Inawezekana siri ya hilo ni kuwa mlahidi hathibitishi upungufu wa muumba, kwa sababu yeye hakubali kabisa kuwa yuko. Hii pia ni dhambi kubwa, hilo halina shaka, lakini dhambi ya mshirikina ni kubwa zaidi, kwa sababu ni kumshirikisha muumba kwa upande mmoja na ni kuthibitisha upungufu kwa muumba kwa upande wa pili.
Ndivyo hivyo! Na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu. Basi hiyo ni katika takua ya nyoyo.
Nembo za Mwenyezi Mungu na miiko yake zina maana moja. Tumezungumzia kuhusu miiko katika Aya iliyotangulia. Hakuna mwenye shaka kwamba hawatii amri za Mwenyezi Mungu isipokuwa wenye takua na ikhlasi.
Miongoni mwa kutukuza nembo za Mwenyezi Mungu na kutii hukumu yake ni kuchinja mnyama aliyenona asiye na kasoro yoyote siku za Hijja. Mtume(s.a.w.w)
anasema: “Hafai aliye kiguru, wala aliyekonda, wala aliyetobolewa sikio wala aliyekatwa sikio wala aliyevunjika pembe.”
Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda uliowekwa.
Katika hao ni hao wa kuchinjwa kwenye Hijja. Muda uliowekwa ni wakati wa kuchinjwa. Maana ni kuwa mwenye kuhiji anaruhusiwa kunufaika na maziwa na mgongo wa mnyama wa kuchinja mpaka wakati wa kuchinja.
Katika Tafsiru-Razi imeelezwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpitia mtu akimkokokota mnyama na yeye mwenyewe amechoka. Mtume akamwambia: “Mpande.” Yule mtu akasema: “Huyu ni wa kuchinja kwa ajili ya Hijja ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!” Akasema Mtume: “Ole wako, mpande!”
Anaendelea kusema Razi: “Abu Hanifa hajuzishi hilo, akatoa hoja kuwa haijuzu kumkodisha kwa hiyo haijuzu kumpanda.” Razi akamjibu Abu Hanifa kwamba hoja hii ni dhaifu, kwa sababu, mjakazi aliyezaa na mmiliki wake hauzwi, lakini inajuzu kunufaika naye.
Kisha mahali pake ni nyumba ya kale.
Yaani mahali pake pa kuchinjwa ni nyumba ya Mwenyezi Mungu takatifu na makusudio yake ni haram yote ikiwemo Mina. Katika Hadith imeelezwa. Mina yote ni machinjioni.
Kila umma tumeujaalia mihanga ya ibada.
Makusudio ya mihanga ya ibada hapa ni kuchinja wanyama kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu,Ili wamtaje Mwenyezi Mungu katika vile alivyowaruzuku katika wanyama howa,
iliyokuja moja kwa moja. Maana ni kuwa hakuna bid’a (uzushi) katika kuchinja mnyama, ilikuweko katika dini zilizotangulia.
Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu.
Kwa hiyo msimtaje mwengine katika dhabihu zenu.
Kwa hiyo jisalimisheni kwake
.Yaani fuateni amri yake na mumfanyie ikhlasi katika kauli na vitendo.
Na wabashirie wanyenyekevu, ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na walio na subira kwa yale yaliyowasibu, na wanaosimamisha Swala na wanatoa katika tulivyowaruzuku.
Mpe habari njema ya Pepo, ewe Muhammad, yule anayemnyenyekea Mwenyezi Mungu, akamwogopa akawa na uthabiti kwenye dini wakati wa raha na dhiki, akamwabudu bila ya unafiki wala ria na akatoa mali yake katika kumtii Mungu na kutaka radhi yake. Hakuna shaka kwamba mwenye kukusanya sifa hizi atakuwa na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu na ya watu.
وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ كَذَٰلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٣٦﴾
36. Na ngamia wa kunona tumewafanyia kuwa ni miongoni mwa nembo za Mwenyezi Mungu, kwao mna kheri. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama safu. Na wanapoanguka ubavu, basi kuleni na mlisheni aliyekinai na aombaye. Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٧﴾
37. Nyama zao hazimfikii wala damu zao, lakini inamfikia takua kutoka kwenu. Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyowaongoa. Na wabashirie wenye kufanya mema.
NGAMIA WANONO
Aya 36 -37
MAANA
Na ngamia wa kunona tumewafanyia kuwa ni miongoni mwa nembo za Mwenyezi Mungu, kwao mna kheri.
Neno ‘Budna’ ni ngamia hasa; kama ilivyoelezwa katika Tafsiri Razi, na Baydhawi. Hufananishwa naye ng’ombe katika hukumu si katika jina.
Hali yoyote iwayo, mtu ni natija ya mambo mengi, yakiwemo mazingira anayoishi. Waarabu, kwa karne nyingi, wakati wa jahiliya na baadaye, wameishi pamoja na ngamia na alikuwa ni sehemu ya maisha yao; wakila nyama yake, kunywa maziwa yake , kuvaa manyoya yake, kubebea mizigo kutoka mji mmoja hadi mwingine n.k. Tazama Juz. 14 (16: 6).
Kwa ajili hii ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamtaja kwenye Aya kadha, kwa tamko la kiujumla; kama vile wanyama howa, au kwa tamko mahususi; kama ilivyo katika Sura 88 na hii Aya tuliyo nayo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaneemesha waja wake kwa ngamia na akamfanya ana manufaa mengi; yakiwemo kujikurubisha mja kwa Mwenyezi Mungu kwa kumchinja katika nyumba yake takatifu. Kuleta ibara ya nembo kwa dhabihu hii ni kufahamaisha kuwa hiyo ni twaa na ibada bora zaidi.
Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama safu.
Katika masharti ya kuchinja ni kusoma Bismillah na kuelekezwa chinjo upande wa Qibla, na ngamia kuwa na aina yake ya kuchinjwa (nahr) ambayo ni maalum kwa ngamia:
Anachomwa kisu au kitu chochote chenye ncha kwenye maungio ya shingo na kifua, akiwa ngamia amesimama au kupiga magoti au amelala ubavu, kwa sharti ya kuwa sehemu zote za mbele ya mwili wake zielekee Qibla.
Njia bora ni kumchinja ngamia kwa namna ilivyoelezwa katika Riwaya ambayo ni kusimamishwa ngamia na kufungwa mmoja wa miguu yake ya mbele na asimame mchinjaji kuelekea Qibla vile vile kisha amchome kwenye maungio ya shingo na kifua. Riwaya hii inaweza kufaa kuwa ni tafsiri ya neno ‘wanaposimama safu.’
Na wanapoanguka ubavu,
yaani wanapoanguka chini na kukata roho,basi kuleni na mlisheni aliyekinai na aombaye.
Aliyekinai ni yule anayeridhia unachompa bila ya kuomba.Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewafanya wanyama tuwatumie, hata kuwachinja pia. Kwa hiyo ni wajibu wetu kushukuru.
Nyama zao hazimfikii wala damu zao.
Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha na walimwengu, hawahitajii, sikwambii nyama zilizochinjwa na damu; bali haihitajii chochote. Imesemekana hii ni kuwarudi washirikina ambao walikuwa wakitapakaza damu ya dhabihu kwenye masanamu yao na kuta za Al-Kaaba.
Lakini inamfikia takua kutoka kwenu.
Unaweza kuuliza kuwa
: maana ya takua ni kumcha Mungu katika yale aliyoyaharamisha; ambapo thawabu yake na manufaa yake yanarudi na kumfikia mtendaji tu. Sasa nini maana ya kuwa inafika kwa Mungu?
Jibu
: Makusudio ya takua hapa ni kumridhisha Mwenyezi Mungu, na radhi ya Mwenyezi Mungu haiepukani na mwenye takua, zinakwenda sambamba. Kwa hiyo maana ni kinachomfikia Mwenyezi Mungu katika dhabihu zenu ni kule kuridhiwa na Mungu sio kukasirikiwa. Inafanana na kumwambia mwanao: kufaulu kwako darasani kunanifanya ni kupende na kukuridhia, na haya ndiyo ninayoyapata kutokana na masomo na kufaulu kwako.
Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyowaongoa.
Amewadhalilisha wanyama kwa waja wake na akawaongoza kujikurubisha kwake kwa kuwachinja ili wamsifu kwa sifa zake njema, wamuad- himishe kwa ujuzi wake na uweza wake, wahofie adhabu yake na kutumai thawabu zake.
Wabashirie wenye kufanya mema
wote; wawe wamefanya mema kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuchinja au kwa jambo jinginelo. Kwani aina za wema hazina idadi. Bora zaidi ni kupigana jihadi na madhalimu na wapotevu japokuwa kwa tamko la haki na uadilifu.
إِنَّ اللَّـهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ خَوَّانٍ كَفُورٍ ﴿٣٨﴾
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini, mwenye kukufuru sana.
أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا وَإِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ ﴿٣٩﴾
39. Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.
الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّـهُ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّـهِ كَثِيرًا وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٤٠﴾
40. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila tu kwa kuwa wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu. Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na (sehemu) za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.
الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ وَلِلَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ ﴿٤١﴾
41. Wale ambao tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka na wakaamrisha mema na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.
MWENYEZI MUNGU HUWAKINGA WALIOAMINI
Aya 38 – 41
MAANA
Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini mwenye kukufuru sana.
Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazuia ukafiri na utaghuti kwa waumini katika maisha haya na siku ya mwisho. Aya iliyo wazi zaidi katika hilo ni: “Hakika bila shaka tutawanusuru Mitume wetu na walioamini katika uhai wa duniani na siku watakaposimama mashahidi.” (40:51).
Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu ameashiria kwenye Aya kadhaa, kwamba mayahudi walikuwa wakiwaua manabii bila ya haki. Miongoni mwazo ni: Juz.3 (3: 21), Juz. 4 (3:112, 181) na Juz 6 (4:154). Kuongezea Historia ya mwanadamu, tangu zamani na sasa, imejaa dhulma na kufanyiwa uadui wale wenye takua na ikhlasi.
Sasa je, kuna wajihi wa kukusanya baina ya zinazofahamisha kuuliwa watu wema na zile zinazofahamisha kunusuriwa watu wa haki?
Jibu
:Kwanza
: Aya za nusra zinawahusu baadhi ya mitume; kama vile: Nuh, Hud, Swaleh, Lut na Muhammad. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono kwa nusra yake amtakaye.” Juz.3 (3:13).
Na Aya hii tuliyo nayo inafahamisha kuwa Muhammad (s.a.w.) na maswahaba ndio wanokusudiwa kwenye kauli yake ‘Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamni.’ Kwa sababu wao ndio waliotolewa majumbani mwao si kwa lolote ila ni kwa kuwa wamesema: ‘Mola wetu ni Mwenyezi Mungu.”
Katika vitabu vya Hadith (As-sihah) imeelezwa kwamba Aya hizi zilishuka wakati Mtume alipofanya hijra (kuhama) kutoka Makka kwenda Madina.
Pili
: Mwenye haki na ikhlasi hawezi kukosa wa kumuunga mkono na kumsaidia kwa mkono wake, mali yake au ulimi wake. Wala hatujawahi kusikia jamii ambayo kwa pamoja imekuwa dhidi ya mwenye kutamka tamko la haki na uadilifu.
Ndio, ni kweli kwamba watetezi wa haki wengi wameuawa, wakatekwa na wakafukuzwa, lakini Mwenyezi Mungu anawapa wasaidizi wanotangaza misimamo yao na kuwatukuza na wakiwakabili maadui zao kwa hoja na dalii mkataa. Hii ni aina ya nusra. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini’ ni sababu ya kauli yake: ‘Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamni.’
Sababu hii inafahamisha kuwa ni wajibu kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu kumsaidia mumin kwa kila alichonacho kinachoweza kumsaidia, angalau kumtetea anapotajwa kwa ubaya; vinginevyo atakuwa ni mhaini mwingi wa kukanusha. Kuna Hadith sahih isemayo: “ Mwenye kuinyamazia haki ni shetani bubu.
Tatu
: Lau ingekuwa mtu akiamini tu, basi anaondokewa na muadui na matatizo, basi wangeliamini watu wote imani ya kibiashara; kama vile anayeiuza dhamiri yake kwa kila mwenye kutoa thamani.
Nne
: Imani ya haki ni kumtii Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na hukumu zake zote. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuamrisha, tukitaka kufanya jambo, tufuate sababu za kimaumbile ambazo amezifanya zitekeleze matakwa yetu. Ameziweka sababu za ushindi kuwa ni umoja na kuandaa nguvu, akasema: “Wala msizozane, msije mkavunjika moyo na zikapotea nguvu zenu.” Na akasema: “Na waandalieni nguvu vile muwezavyo.” Juz. 10 (8: 46, 60).
Katika Futuhatul-Mkkiya, Ibnul A’arabiy ameziletea sababu hizi ibara ya mkono wa Mungu. Ameichukua ibara hii katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Je, hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyama wa mifugo wakawa wenye kuwamiliki.” (36:71). Tazama maelezo kwa anuani ya ‘Dini haioteshi ngano’ katika Juz.3 (8: 1-4).
Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.
Waislamu kule Makka walikuwa ni wanyonge, wakipata kila aina ya maudhi na ukandamizwaji kutoka kwa washirikina; na walikuwa hawawezi kujitetetea. Walikuwa wakimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na wakimshitakia dhulma, naye akiwa hana lolote la kuwaambia isipokuwa kuwausia subra. Miongoni mwa aliyokuwa akiwaambia ni: “Mimi sijaamriwa kupigana.”
Mtume alikatazwa kupigana na washirikina katika zaidi ya Aya 70, alipokuwa Makka. kwa sababu kupigana wakati huo ilikuwa ni sawa na kujimaliza. Tazama Juz.5 (4:77).
Baada ya Mtume na Waislamu kuhamia Madina, wakawa na nguvu, ndipo ikashuka Aya hii. Inasemekana kuwa ndio Aya ya kwanza kushuka kuhu- siana na vita.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha sababu ya kutoa ruhusa hii; kwamba washirikina wamewachokoza waislamu, wakawatoa kwenye miji yao kwa dhulma na kwa uadui na akawaahidi waislamu ushindi kwa maadui zao, pale aliposema: “Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.”
Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu.
Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa kosa pekee la Mtume na swahaba zake kwa washirikina ni kule kusema: “Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu.” Dhahiri hii ndio walioichukua wafasiri wote; bali mmoja wa wafasiri wapya alisema, ninamnukuu: “Hakuna upinzani kuliko kupinga maisha haya yaliyojikita kwenye tamaa, kupingana masilahi, kutofautiana mielekeo na kugongana matamanio.”
Mara nyingi tumeashiria huko nyuma kwamba utaghuti wa kishirikina uli- upiga vita ujumbe wa Muhammad na neno la Tawhid si kwa lolote isipokuwa linataka kuondoa manufaa, matamanio, masilahi yao na kuwe- ka usawa baina ya watu. Angalia tuliyoyaandika kwa anuani ya ‘Masilahi ndio sababu’ katika Juz. 1 (2: 92-96).
Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na (sehemu) za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwaruhusu waumini, wanaochokozwa, kupigana na washirikina, sasa anabainisha sababu ya ruhusa hiyo; kwamba lau si kuweko na nguvu ya upinzani, basi ingeenea vurugu na ufisadi katika ardhi kwa sababu ya unyang’nyi, uporaji na kumwagika damu; hasa baina ya vikundi na watu wa dini.
Mwenyezi Mungu ameielezea fitna baina ya mataifa kwa ibara ya kuvunjwa sehemu zake za kuabudu. Kwa sababu ndio sehemu muhimu kwa mataifa; na zina alama maalum zinazotofautiana na nyingine. Mahekalu ni ya mayahudi, makanisa ni ya wanaswara (wakiristo), na sehemu za kuswalia ni zamataifa mengineyo. Msikiti unatofautiana na sehemu nyingine kwa kuwa Swala humo ni mara tano, usiku na mchana.
Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu anawazuwiya waumini na makafiri. Kama itakuwa ni sawa tafsiri hiyo, haiwezi kufaa kila wakati. Usahihi hasa ni tuliouelezea, kuwa ili kuhifadhika amani na nidhamu ni lazima kuweko na nguvu ya upinzani; ni sawa nguvu hiyo iwe mikononi mwa waumini au makafiri.
Imam Ali (a.s.) anasema: “Hapana budi watu wawe na kiongozi mwema au muovu, atatumiwa na mumin na kafiri, Mwenyezi Mungu atafikisha kwaye muda. Watu watajikusanya kwake waweze kumpiga adui, nia zitakuwa na amani kwaye, mwenye nguvu atakamatwa kwa ajili ya kumuonea mnyonge ili astarehe na kila muovu.”
Kauli hii ya Imam Ali, ilikuwa ni kuwarudi Khawariji waliposema: “Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu.” Angalia tuliyoyaandika kwa anuani hii, kwenye Juz. 12 (12:40).
Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.
Hiki ni kichocheo cha kupigana jihadi ya kuinusuru haki na watu wake.
Wale ambao tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka na wakaamrisha mema na wakakataza mabaya.
Makusudio ya kumakinishwa hapa ni utawala. Mwenyezi Mungu ameapa kwa msisitizo kwamba Yeye atawasaidia watawala, kwa sharti ya kuweko mambo mawili:
Kwanza
: wao wenyewe watekeleze haki ya ibada kwa ukamilifu; kama vile Swala, Saumu na kuamrisha mema na kukataza maovu. Ibada ya kimwili ameileta kwa ibara ya Swala na ibada ya kimali kwa Zaka.
Jambo la pili
: ni kufanya uadilifu baina ya watu, kuisimamisha haki na kuibatilisha batili. Hayo ndio makusudio ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Akivunja moja tu ya mawili haya, Mwenyezi Mungu humpuuza na humwacha.
Unaweza kuuliza
: Tumewaona watawala wengi wasiomwamini Mungu kabisa, sikwambii kumwabudu kwa kuswali na kutoa Zaka, lakini pamoja na hayo utawala wao umestawi na kufuatwa na raia kwa vile wametimiza malengo ya raia na kuwatumikia, wala raia hawaangalii imani yao. Kwa hiyo, inaonyesha, suala la imani sio sharti la kudumu utawala na ustawi wake?
Jibu
: Makusudio ya nusra ya Mwenyezi Mungu, katika Aya, ni kuustawisha utawala katika dunia na thawabu za akhera; bali hii ndio nusra ya kiuhakika. Kwa sababu ufalme wa dunia unaondoka, lakini neema za akhera ni za kudumu bila ya kuwa na ukomo na ni msafi na wa raha kwa pande zake zote.
Mtawala wa dunia anaweza kuustawisha utawala wake duniani akiwa mwadilifu, lakini Akhera akapata adhabu ya kuungua kwa kukufuru kwake dalili za kilimwengu ambazo zinaonyesha kuweko mtengenezaji.
Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.
Yeye peke yake ndio Mfalme wa wafalme, huumpa ufalme amtakaye na humnyima ufalme amtakaye, na yeye ni Muweza wa kila kitu.