2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٢٣﴾
23. Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?
فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً مَّا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾
24. Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu. Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.
إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٢٥﴾
25. Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi ngojeni kwa muda.
قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٢٦﴾
26. Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.
فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ فَاسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ ﴿٢٧﴾
27. Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu. Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao. Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.
فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنتَ وَمَن مَّعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٨﴾
28. Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.
وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٢٩﴾
29. Na sema, Mola wangu! niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiwe mbora wa wateremshaji.
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ وَإِن كُنَّا لَمُبْتَلِينَ ﴿٣٠﴾
30. Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.
NUH
Aya 23-30
MAANA
Kila yaliyokuja kwenye Aya hizi yametangulia kutajwa katika Juz. 12 (11: 25-49) yamemaliza zaidi ya kurasa 22, kwa hiyo hapa tutazipitia juu juu tu.
Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?
Aliwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake na kuwahadharisha na shirki. Wale wapenda anasa wakahofia vyeo vyao na chumo lao. Wakaanzisha kampeni za uongo na kuwatatiza watu kwa shubha za ubatilifu. Mwenyezi Mungu amezitaja tatu miongoni mwazo:
1.Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu.
Walisema, vipi Nuh awe ni nabii naye ni mtu kama nyinyi. Yeye hana lengo la utume katika mwito wake isipokuwa anataka kuwa raisi na nyinyi muwe raia wake. Hii ndio lugha ya wafanyi biashara, wanafasiri faida katika kila kitu.
2.Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.
Hawakusikia kuwa Mwenyezi Mungu alituma mitume, vilevile hawakusikia kuwa Mungu wa ulimwengu wote ni mmoja. Kwa hiyo Nuh si Mtume na miungu ni mingi, yakiwemo masanamu yao. Hakuna tofauti baina ya mantiki haya na mantiki ya anayesema: mimi siamini kuweko kwa sayari ya Mars kwa sababu sijafika huko.
3.Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu.
Walileta uongo huu wakijua fika kuwa ni uongo; kama walivyokuwa maquraishi na uhakika wa wa uzushi wao pale waliposema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amerogwa na ni mwendawazimu.
Basi ngojeni kwa muda.
Yaani mngojeni Nuh afe au awache mwito wake.
Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.
Alikimbilia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu na akamtaka msaada baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.
Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu.
Ni kinaya cha kuichunga kwake Mwenyezi Mungu safina. Na wahyi wetu yaani na amri yetu.
Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri;
yaani maji yatakapochimbuka kutoka ardhini.
Hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao.
Yaani isipokuwa mke wake Nuh na mwanawe ambaye inasemekana jina lake ni Kanani.
Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.
Yaani usiniombe kuokoka wale ambao neno la adhabu limekwishahakika kwao; hata mkeo na mwanao pia.
Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.
Katika Aya hii kuna somo muhimu sana, nalo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapomwangamiza taghuti haitakikani kunyamaza yule aliyedhulumiwa; bali amuhimidi Mwenyezi Mungu kwa kuokoka kwake na kuangalia kuangamia kwake kuwa ni nyenzo tu sio lengo.
Na sema: Mola wangu! Niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiye mbora wa wateremshaji.
Niteremshe kutoka jahazini kwa namna ambayo utanihifadhi na uovu mimi na watu wangu na aliyeamini, kwani wewe ni mtermshaji na muhifadhi bora.
Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.
Yaani sisi tumewafanyia mtihani waja kwa kuwapelekea mitume na kuteremsha vitabu, ili kupambanua muovu na mwema na aonekane wazi wazi kila mmoja wao alipwe thawabu au adhabu, kiasi anachostahiki.
ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ ﴿٣١﴾
31. Kisha baada yao tukaanzisha karne nyingine.
فَأَرْسَلْنَا فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣٢﴾
32. Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kwamba mumwabudu Mwenyezi Mungu! Hamna Mungu asiyekuwa Yeye, je hamuogopi?
وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِلِقَاءِ الْآخِرَةِ وَأَتْرَفْنَاهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يَأْكُلُ مِمَّا تَأْكُلُونَ مِنْهُ وَيَشْرَبُ مِمَّا تَشْرَبُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na wakuu katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binadamu kama nyinyi, anakula mlacho na anakunywa mnywacho.
وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِّثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٣٤﴾
34. Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.
أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ ﴿٣٥﴾
35. Je, anawaahidi ati mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa kwamba mtatolewa?
هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ ﴿٣٦﴾
36. Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa.
إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ ﴿٣٧﴾
37. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tu, tunakufa na tunaishi. Wala sisi si wenye kufufuliwa.
إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا وَمَا نَحْنُ لَهُ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٣٨﴾
38. Huyo si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kumwamini.
قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٣٩﴾
39. Akasema: Mola wangu, ninusuru kwa wanavyonikanusha.
قَالَ عَمَّا قَلِيلٍ لَّيُصْبِحُنَّ نَادِمِينَ ﴿٤٠﴾
40. Akasema: Baada ya muda mchache hakika watakuwa ni wenye kujuta.
فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ بِالْحَقِّ فَجَعَلْنَاهُمْ غُثَاءً فَبُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤١﴾
41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki. Tukawafanya takataka zinazoelea juu ya maji, ikapotelea mbali kaumu ya madhalimu.
HUD
AYA 31-41
KISHA BAADA YAO TUKAANZISHA KARNE NYINGINE
Makusudio ya karne hapa ni watu. Mwenyezi Mungu hakuweka wazi ni akina nani hao. Wafasiri wamesema hao ni A'd, kaumu ya Hud. Na hii ni sawa kwa dalili ya yaliyokuja katika Juz.8 (7:65). Yametangulia maelezo katika Juz. 12 (11: 50 - 65). Kwa hiyo tutapita juu juu, kwenye Aya hizi, kama tulivyopita kwenye Aya zilizotangulia hizi.
Tukawapelekea Mtume mingoni mwao.
Mwenyezi Mungu alimtuma Hud kwa A'd naye ni miongoni mwao.
Kwamba mumwabudu Mwenyezi Mungu! Hamna Mungu asiyekuwa Yeye, je hamuogopi?
Aliwapa watu wake mwito wa tawhid na kuacha shirk kwa kutoa bishara ya radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake na kutoa onyo la hasira za Mweyezi Mungu na adhabu yake.
Na wakuu katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binadamu kama nyinyi, anakula mlacho na anakunywa mnywacho.
Maadamu yuko hivyo hivyo basi hana tofauti wala ubora, basi vipi mnamtii.
Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.
Wao ndio wako hasarani kiiudhahiri na kiuhalisi kutokana na kumuasi kwao Nabii. Lakini wamepindua na wakaufinika uhakika. Haya ndiyo mazoweya ya matwaghuti na wanaodeka kila mahali na kila wakati.
Je, anawaahidi ati mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa kwamba mtatolewa?
Makaburini kuwa hai kama mlivyo sasa. Hiki ni kitu cha ajabu.
Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa kuwa kuna ufufuo baada ya mauti. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tu, tunakufa na tunaishi. Wala sisi si wenye kufufuliwa.
Kwa sababu aliyekufa na yake yamekwisha. Huu ni ubainifu wa yaliyotangulia, ya kuona kwao muhali kufufuliwa baada ya mauti, wakiwa wameghafilika kwamba aliyewaumba kwanza ndiye huyo huyo atakayewarudisha; na kwamba hilo ni rahisi zaidi kuliko kuanzisha, kama ni sawa ibara yao.
Huyo si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kumwamini.
Hawamwamini Hud kwa sababu anasema uongo juu ya Mwenyezi Mungu, lakini kuabudu kwao masanmu ndio ikhlasi ya kweli kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na takua!! Aliye mtupu zaidi katika watu ni yule anayefanya uovu kisha akajiona amefanya wema.
Akasema: Mola wangu, ninusuru kwa wanavyonikanusha.
Alisema hivi baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.
Akasema
- Mwenyezi Mungu -baada ya muda mchache hakika watakuwa ni wenye kujuta,
kutokana na shirki yao na uasi wao ambapo Mwenyezi Mungu atawapatiliza kwa mpatilizo wa mwenye nguvu mwenye uwezo.
Basi ukawanyakua ukelele kwa haki.
Makusudio ya ukelele ni adhabu. Kusema kwake kwa haki ni ishara ya kuwa wanastahili adhabu kutokana na waliyoyafanya.
Tukawafanya takataka zinazoelea juu ya maji.
Yaani wako sawasawa na vitu duni vinavyoelea kwenye maji.
Ikapotelea mbali kaumu ya madhalimu.
Wamepotelea mbali na Mwenyezi Mungu na twaa yake naye akawaweka mbali na fadhila zake na rehema zake.
ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قُرُونًا آخَرِينَ ﴿٤٢﴾
42. Kisha baada yao tukaanzisha karne niyingine.
مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٤٣﴾
43. Hapana umma unaoweza kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
ثُمَّ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا تَتْرَىٰ كُلَّ مَا جَاءَ أُمَّةً رَّسُولُهَا كَذَّبُوهُ فَأَتْبَعْنَا بَعْضَهُم بَعْضًا وَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ فَبُعْدًا لِّقَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٤٤﴾
44. Kisha tukawapeleka mitume wetu mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatishia baadhi yao wengine, ikapotelea mbali kaumu isiyoamini.
ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٤٥﴾
45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye Harun pamoja na ishara zetu, na hoja zilizo wazi.
إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا عَالِينَ ﴿٤٦﴾
46. Kwenda kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivu- na na walikuwa ni kaumu waliojikweza.
فَقَالُوا أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ ﴿٤٧﴾
47. Wakasema: Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?
فَكَذَّبُوهُمَا فَكَانُوا مِنَ الْمُهْلَكِينَ ﴿٤٨﴾
48. Basi wakawakadhibisha wakawa miongoni mwa walioangamizwa.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَىٰ رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ ﴿٥٠﴾
50. Tukamfanya mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara. Na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka, penye utulivu na chemchem za maji.
KILA UMMA ULIKANUSHA MTUME WAKE ALIPOWAFIKIA
Aya 42-50
MAANA
Kisha baada yao tukaanzisha karne niyingine.
Baada yao ni baada ya A'd na karne ni watu. Watu wa kwanza kuja baada ya A'd ni Thamud, kwa dalili ya yaliyoelezwa katika Juz. 8 (7:74)
Hapana umma unaoweza kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
Kila kitu isipokuwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t), kina muda wake hauchelewi wala kuja haraka. Miongoni mwa hayo ni kuangamia wale waliokadhibisha mitume yao. Adhabu ilikuwa ikawajia ghafla bila ya kutambua wala kuhisi.
Kisha tukawapeleka mitume wetu mmoja baada ya mmoja.
Mitume walikuwa wakija mmoja baada ya mwingine. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) alijaalia kila umma uwe na mtume.
Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha au kumuua. Si kwa lolote ila ni kwa kuwa amekuja na ambayo matamanio yao yanayakataa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Kila alipowajia Mtume kwa yale yasiyoyapenda nafsi zenu, mlijivuna, kundi moja mkalikadhibisha na kundi jingine mkaliua." Juz. 1 (2:87)
Tukawafuatishia baadhi yao wengine.
Yaani Mwenyezi Mungu aliangamiza umma uliomkadhibisha Mtume wake mmoja baada ya mwingine na akajaalia ni mazingatio kwa mwenye kuzingatia na habari watayoinukuu kizazi baada ya kizazi kingine.
Ikapotelea mbali kaumu isiyoamini haki wala kuitumia.
Kisha tukamtuma Musa na nduguye Harun pamoja na ishara zetu, kama vile fimbo kugeuka nyoka na kumeremeta mkono, na hoja zilizo wazi za kunyamazisha.
Kwenda kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivuna na walikuwa ni kaumu waliojikweza.
Kuna kujikweza gani na majivuno makubwa zaidi ya kauli ya Firaun:
فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
"Mimi ni Mola wenu mkuu." (79:24)
Au pale aliposema:
مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾
"Simjui kwa ajili yenu mungu asiyekuwa mimi." (28:38).
Watu wengi wana moyo kama wa Firaun, wanaweza kudai uungu kama watakuwa na nyenzo na kupata watakaomwitikia kama alivyopata Firaun.
Wakasema: "Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?"
Firauni alidai uungu na akawaadhibu waisrail kwa kuwachinja watoto wao wa kiume na kuwaacha wa kike. Na Musa na Harun ni katika waisrail; vipi watawafuata?
Basi wakawakadhibisha wakawa miongoni mwa walioangamizwa. Kila anayepituka mipaka mwisho wake ni maangamizi tu. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat na wanaotakiwa kuongoka ni wana wa Israil, lakini hawakuongoka na wala hawataongoka kamwe baada ya kuipotoa Tawrat, wakafuata matamanio yao na wakaijaza dunia ufisadi na upotevu.
Kisa cha Musa kimekaririka mara nyingi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Tumebainisha sababu ya kukaririka kisa katika Juz. 16 (20:9) Kifungu cha 'Kukaririka kisa cha Musa.'
Tukamfanya mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara.
Yaani muujiza. Isa ni muujiza kwa sababu amezaliwa bila ya Baba na Mama yake ni mujiza kwa vile amezaa bila ya mume. Tazama Juz. 3 (3:45-51).
Na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka. Makusudio ni Palestina, kwa sababu Bwana Masih alizaliwa hapo, napo ni penye utulivu na chemchem za maji.