4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَإِنَّكَ لَتَدْعُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٧٣﴾
73. Na hakika wewe unawaita kwenye njia iliyonyooka.
وَإِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ عَنِ الصِّرَاطِ لَنَاكِبُونَ ﴿٧٤﴾
74. Na hakika wale ambao hawaiamini akhera wanajitenga na njia hiyo.
وَلَوْ رَحِمْنَاهُمْ وَكَشَفْنَا مَا بِهِم مِّن ضُرٍّ لَّلَجُّوا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٥﴾
75. Lau tungeliwarehemu tukawaondolea shida waliyo nayo, bila shaka wangeliendelea na upotevu wao wakimangamanga.
وَلَقَدْ أَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ فَمَا اسْتَكَانُوا لِرَبِّهِمْ وَمَا يَتَضَرَّعُونَ ﴿٧٦﴾
76. Na hakika tuliwatia katika adhabu, lakini hawakuelekea kwa Mola wao wala hawakunyenyekea.
حَتَّىٰ إِذَا فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا ذَا عَذَابٍ شَدِيدٍ إِذَا هُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ ﴿٧٧﴾
77. Mpaka tulipowafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa ni wenye kukata tamaa.
وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾
78. Yeye ndiye aliyewaumbia kusikia na kuona na nyoyo. Ni kuchache mno kushukuru kwenu.
وَهُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٧٩﴾
79. Yeye ndiye aliyewaumba katika ardhi na kwake mtakusanywa.
وَهُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ وَلَهُ اخْتِلَافُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٨٠﴾
80. Yeye ndiye anayehuisha na kufisha na Yeye ndiye mwenye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je, hamfahamu?
UNAWAITA K W ENYE NJIA ILIYONYOOKA
Aya 73 – 80
MAANA
Na hakika wewe unawaita kwenye njia iliyonyooka. Na hakika wale ambao hawaiamini akhera wanajitenga na njia hiyo.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuelezea upotevu wa washirikina na kwamba wao hawana udhuru wowote wa kumkanusha kwao Muhammad(s.a.w.w)
, sasa anamwambia Mtume wake Mtukufu kwamba yeye anazo hoja za kutosha kuwa yeye ni mkweli katika mwito wake na kwamba washirikina ambao wamemkanusha yeye na siku ya mwisho wameiacha haki na wakapotea njia ya kheri na uongofu. Nao, katika hilo, wanajidhu- ru wenyewe na hawatakudhuru wewe na chochote.
Lau tungeliwarehemu tukawaondolea shida waliyo nayo, bila shaka wangeliendelea na upotevu wao wakimangamanga.
Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kuhamia Madina kutoka Makka aliwapa dhiki makuraishi kwa kutuma vikosi kuwazuilia njia, mara nyingine alikuwa akiviongoza mwenyewe, na akaamrisha kuwakatia uhu- siano. Basi wakaingia kwenye dhiki, lakini bado waliendelea na upotevu wao na kufuru yao. Lau kama Mwenyezi Mungu (s.w.t) angeliwaondolea shida waliyo nayo, wasingelizingatia kuachana na upotevu wao.
Na hakika tuliwatia katika adhabu, lakini hawakuelekea kwa Mola wao wala hawakunyenyekea.
Ukiwahadharisha wanapinga, ukiwatia adabu hawazingatii na ukiwaondolea wanakuwa jeuri. Watakuwa hivi mpaka siku watakapofufuliwa, watakpoondolewa pazia washuhudie malipo ya mghafala wao na jeuri yao. Hapo watakata tamaa ya kuokoka na kujutia yaliyopita.
Mpaka tulipowafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata
tamaa na hali Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikwishawahadharisha na adhabu hii kali na kuwapa kiaga, lakini wakapuuza nafsi zao wakazipeleka kwenye maangamizi.
Yeye ndiye aliyewaumbia kusikia na kuona na nyoyo
za kufahamu, ili mnufaike kwa mtakyoyasikia na kuyaona muweze kujua ya kheri na masilahi.
Neema za Mwenyezi Mungu kwa mtu hazina idadi, kubwa yake ni akili kisha usikizi na uoni. Ametangulia kutaja usikizi kwa sababu mtoto anayezaliwa huanza kusikia tangu kuzaliwa kwake, wala haoni mpaka siku ya nne; kama wanavyosema. Ama kuchelewa akili hilo liko wazi.
Ni kuchache mno kushukuru kwenu;
yaani kutii kwenu.
Yeye ndiye aliyewaumba katika ardhi na kwake mtakusanywa.
Alituuumba katika ardhi hii kisha atatufufua kwake baada ya mauti. Yeye ndiye anayehuisha na kufisha na Yeye ndiye mwenye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je, hamfahamu? Hakika huu ni utengenezaji wa Mwenye uweza aliye Mjuzi. Tazama Juz. 1 (2:28 -29) na Juz. 3: (3:26-27).
بَلْ قَالُوا مِثْلَ مَا قَالَ الْأَوَّلُونَ ﴿٨١﴾
81. Bali walisema kama walivyosema wa mwanzo.
قَالُوا أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٨٢﴾
82. Je, tukishakufa tukawa mchanga na mifupa ndio tutafufuliwa?
لَقَدْ وُعِدْنَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا هَـٰذَا مِن قَبْلُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٨٣﴾
83. Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni vigano vya wa kale.
قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٤﴾
84. Sema, ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٨٥﴾
85. Watasema, ni vya Mwenyzi Mungu. Basi je, hamkumbuki?
قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿٨٦﴾
86. Sema, ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu?
سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٨٧﴾
87. Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu. Sema, basi je, hamuogopi?
قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٨﴾
88. Sema, ni nani mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu? Na yeye ni mlinzi wala hapalindwi kwake, kama mnajua.
سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ ﴿٨٩﴾
89. Watasema, ni wa Mwenyezi Mungu. Sema, basi vipi mnadanganyika?
بَلْ أَتَيْنَاهُم بِالْحَقِّ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٩٠﴾
90. Bali tumewaletea haki. Na kwa hakika wao ni waongo.
WALISEMA KAMA WALIVYOSEMA WA MWANZO
Aya 81 – 90
MAANA
Bali walisema kama walivyosema wa mwanzo.
Waliosema ni washirikina waliokuwa zama za Mtume(s.a.w.
w
)
. Walikanusha ufufuo, wakatoa sababu mbili:
Kwanza
: ni kustaajabu walikokuleta kwa ibara hii:
Je, tukishakufa tukawa mchanga na mifupa ndio tutafufuliwa?
Pili
: kwamba wao hawajamuona aliyekufa kisha akarudi kuwa hai. Maana haya yamekusudiwa katika kauli yao:
Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni vigano vya wa kale.
Yaani tumeyasikia kabla yako ewe Muhammad, pia tuliyasikia kwa wazee wetu, lakini hakujatokea athari yoyote. Ni nani aliyekufa kisha akarudi kutoa habari?
Lau wangelitaamali uumbaji wa kwanza wasingelipinga uumbaji wa pili. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:5) na Juz. 15 (17:49).
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajadili wapinzani hawa, kwa mfumo wa kielimu wenye hekima, katika Aya tatu zifuatazo:-
1.Sema, ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
Alimwamrisha Mtume wake kuwakabili na swali hili. Kwa sababu wao wanakiri na kukubali kwamba Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu.
Yaani ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu; wala hakuna maana ya kuwa ni vyake ila ni kwakuwa ameviumba na kuvianzisha. Ikiwa Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuumba ardhi basi vilevile Yeye anaweza kufufua wafu.
Basi je, hamkumbuki na kufikiria hakika hii ambayo ni aliyeweza kuanzisha mara ya kwanza pia anaweza kurudisha mara ya pili? Kila anayeweza kitu, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, anashindwa na vingine, anajua vichache na hajui vingi. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ni Muweza na Mjuzi wa kila kitu.
2.Sema, ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu? Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu.
Arshi ni kinaya cha ufalme wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na utawala wake. Ambaye mbingu na ardhi ni yake basi ni wepesi kwake kumrudisha aliyekufa humo.
Sema, basi je, hamuogopi ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake?
Tumezungumzia kuhusu mbingu saba katika Aya 17 ya sura hii
3.Sema, ni nani mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu?
Makusudio ya ufalme wa kila kitu ni kuwa kila kitu kinamnyenyekea na kumhitajia Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba hahitajii chochote.
Na yeye ni mlinzi wala hapalindwi kwake, kama mnajua.
Yeye ni rehema kwa mwenye kutaka rehema na ni uokovu kwa anayetaka kuokoka; wala hapana mwenye kuweza kumrehemu au kumuokoa yule ambaye anastahiki ghadhabu na adhabu yake.
Watasema: ni wa Mwenyezi Mungu.
Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake.
Sema: basi vipi mnadanganyika?
Maadamu mnakubali hayo, basi vipi mnaukana ufufuo na kuhadika na haki?
Bali tumewaletea haki.
Hapana! Hawakudanganyika na haki wala hawakutatizika na batili, baada ya kuwasimamia hoja na dalili zilizo wazi. Na kwa hakika wao ni waongo. Hawakuhadaika isipokuwa wamejitia kuhadaika na kudhihirisha uongo na uzushi. Wao hawakutosheka na ufufuo kwa hoja kwamba dalili zake zimejificha.
Unaweza kuuliza
: Imejulikana vipi kwamba wao walikana ufufuo wakiwa na imani nao, na kuna Aya nyingi zimeonyesha mshangao wao na kutojua kwao kukisia uumbaji wa kwanza na ufufuo?
Jibu
: Ndio ni kweli, lakini kila ambaye amepatiwa hoja za kutosha zilizo wazi na akaendelea kukataa, ni sawa na yule anayekataa makusudi.
مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٩١﴾
91. Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana, wala hanaye mungu mwingine. Ingelikuwa hivyo basi kila Mungu angelichukua alivyoviumba. Na baadhi yao wangeliwashinda wengine. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu.
عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٩٢﴾
92. Mjuzi wa ghaibu na dhahiri. Ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo.
قُل رَّبِّ إِمَّا تُرِيَنِّي مَا يُوعَدُونَ ﴿٩٣﴾
93. Sema, Mola wangu! Ukinionyesha waliyoahidiwa.
رَبِّ فَلَا تَجْعَلْنِي فِي الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٩٤﴾
94. Mola wangu usinijaalie katika watu madhalimu.
وَإِنَّا عَلَىٰ أَن نُّرِيَكَ مَا نَعِدُهُمْ لَقَادِرُونَ ﴿٩٥﴾
95. Na hakika sisi ni wenye kuweza kukuonyesha tuliyowaahidi
ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ ﴿٩٦﴾
96. Kinga maovu kwa yaliyo mema zaidi. Sisi tunayajua wanayoyasifia.
وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾
97. Na sema, Mola wangu! Najikinga kwako na wasiwasi wa shetani.
وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾
98. Na ninajilinda kwako wasinikaribie.
حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾
99. Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu nirudishe.
لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾
100. Ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.
MJUZI WA GHAIBU NA YALIYO WAZI
Aya 91 -100
MAANA
Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana.
Hana mshirika wala mtoto. Lau angelikuwa na mtoto angelifanana naye. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hana mfano na chochote.
Wala hanaye mungu mwingine. Ingelikuwa hivyo basi kila Mungu angelichukua alivyoviumba.
Lau ulimwengu ungelikuwa na waumbaji wawili, basi kila mmoja angelihusika na sehemu fulani ya ulimwengu; angelikuwa na mipaka yake nidhamu yake na mambo yake yasiyoafikiana na sehemu nyingine. Kwa kuwa nidhamu ya ulimwengu ni moja na mambo yake ni mamoja, basi muumba wake ni mmoja.
Na baadhi yao wangeliwashinda wengine.
Vile vile lau waumbaji wangelikuwa wengi, hilo lingesababisha kila mmoja kuwa mshindi juu ya mwingine kwa wakati mmoja. Kwa sababu sifa ya Mungu ni kuwa juu ya kila kitu. Yaani kama waungu wangelikuwa wengi basi kungelikuwa na mashindano; kama inavyokuwa kwa watawala. Na huo ndio ufisadi hasa.
Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu
kuwa ana mwana au washirika. Umetangulia ufafanuzi wake katika Juz. 5 (4:50).
Mjuzi wa ghaibu na dhahiri.
Makusudio ya ghaibu ni yale ambayo viumbe hawawezi kuyajua. Na ya dhahiri ni yale ambayo viumbe wanaweza kuyajua. Kwa hakika ilivyo hasa ni kuwa ugawanyo huu unafaa kwa viumbe, sio kwa muumba. Kwa sababu kwake yeye vitu vyote ni sawa kiujuzi na kiuwezo.
Ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo,
kutokana na kutowatambua hao washirika. Ikiwa kitu hakitambui muumba maana yake ni kuwa hakiko.
Sema, Mola wangu! Ukinionyesha waliyoahidiwa, Mola wangu usinijaalie katika watu madhalimu.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake aombe dua ya kuokoka na ghadhabu na adhabu yake itakayowapata wenye hatia na madhalimu, pamoja na kujua kuwa Mtume(s.a.w.
w
)
yuko katika amani na salama. Lakini lengo la dua hii ni kuhadharisha watu wa shirk na madhalimu. Mara nyingi waongozaji wanatumia mfumo huu kuonyesha kupingana na yule aliyeghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu.
Na hakika sisi ni wenye kuweza kukuonyesha tuliyowaahidi.
Mtume(s.a.w.
w
)
aliwaonya makuraishi kwa adhabu kama watamkadhibisha na kupinga utume wake, wakacheka na wakafanya masikhara; ndio Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake Mtukufu kuwa usihuzunike! Sisi tunaweza kukuonyesha maangamizi, lakini tunaahirisha kwa hekima na maslahi yako na ya Uislamu.
Pengine hekima hiyo ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua kuwa baadhi yao au baadhi ya watoto wao watamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wawe ni nguvu ya kuusaidia Uislamu na waislamu; kama ilivyotokea hivyo hasa.
KUKINGA MAOVU KWA MEMA ZAIDI
Kinga maovu kwa yaliyo mema zaidi. Sisi tunayajua wanyoyasifia.
Ni nini kukinga kwa kutenda yaliyo mema zaidi? Je, ni kuvumilia maudhi na kumnyamazia anayekuudhi, kama wasemavyo wafasiri wengi?
Kinga inatofautiana kulingana na hali. Inaweza ikawa kutumia nguvu dhidi ya adui ndio kukinga kwa yaliyo mema zaidi. Hapo ni ikiwa aliyechokozwa ana uwezo na ikawa kumnyamazia mchokozi kunamtia mori wa kufanya uovu na uadui. Imam Ali
anasema: "Kutekeleza ahadi kwa wasio na ahadi ni kuvunja ahadi na kuvunja ahadi kwa wasio na ahadi ni kutekeleza ahadi"
Na inawezekana kuwa kumnyamzia mchokozi ni kinga ya kufanya mema zaidi, ikiwa huko kumnyamazia kutamfanya ajute na atubie au ikiwa aliyechokozwa hana nguvu za kutosha kumzuia mchokozi. Kwani hapo itakuwa ni kujiingiza katika mambo ambayo hayana mwisho mzuri.
Kwa ajili hii Mtume alivumilia maudhi akiwa Makka kwa kutokuwa na uwezo, lakini aliwatia adabu wachokozi baada ya kuhamia Madina na kupata nguvu.
Na sema, Mola wangu! Najikinga kwako na wasiwasi wa shetani, na ninajilinda kwako wasinikaribie.
Ni wazi kuwa shetani hana uwezo wowote kwa Mitume, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika waja wangu huna mamlaka nao isipokuwa wale wapotofu waliokufuata." Juz. 14 (15:42).
Unaweza kuuliza
: Ikiwa shetani hana uwezo wowote kwa Mitume, basi kwa nini Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kujikinga nao?
Jibu
: Kujikinga na kitu hakumaanishi kutowezekana kutokea kwake. Kwani maasumu wanajikinga na ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu zaidi kuliko wengine, pamoja na kuwa wao wako katika amani na salama. Kwa maneno mengine ni kuwa kumkimbilia Mwenyezi Mungu ni dua, na dua inafaa kuwa ni kinga ya uovu na balaa hata kama haiko. Huko nyuma tumeashiria kwamba wacha Mungu mara nyingi wanaonyesha uovu katika dua zao kwa unyenyekevu.
Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu nirud- ishe ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha.
Wakati alipokuwa na fursa ya kufanya matendo mema aliipoteza na kuipuuza. Baada ya kumfikia mauti ndio anataka kurudia uhai ili afanye amali njema. Hivi ndivyo alivyo kila mzembe, anaipoteza nafasi anapokuwa nayo na inapomtoka huanza kuijutia.
Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu.
Hakuna kurejea kabisa! Hata kama mzembe huyu atakubaliwa kurudi mara ya pili atarudia uasi wake. Ama kusema kwake 'ili nitende mema' ni maneno matupu tu yasiyokuwa na maana wala utekelezaji. Hilo amelifafanua Mwenyezi Mungu aliposema: "Na kama wangelirudishwa bila shaka wangeliyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo" Juz.7 (6:28).
Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.
Nyuma yao ni kinaya cha kila upande. Maana ni kuwa wao wametaka kurejea duniani na baina yao na maisha ya dunia kuna kizuizi kitaka-chobaki mpaka siku ya kiyama. Hapo ndio kitaondoka kizuizi, lakini itakuwa ni wakati wa viumbe kusimama mbele ya Mola wao kwa ajili ya hisabu na malipo.