10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَعْمَالُهُمْ كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا وَوَجَدَ اللَّـهَ عِندَهُ فَوَفَّاهُ حِسَابَهُ وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٣٩﴾
39. Na wale ambao wamekufuru vitendo vyao ni kama sarabi jangwani, mwenye kiu huyadhania ni maji, hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawasawa. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.
أَوْ كَظُلُمَاتٍ فِي بَحْرٍ لُّجِّيٍّ يَغْشَاهُ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ سَحَابٌ ظُلُمَاتٌ بَعْضُهَا فَوْقَ بَعْضٍ إِذَا أَخْرَجَ يَدَهُ لَمْ يَكَدْ يَرَاهَا وَمَن لَّمْ يَجْعَلِ اللَّـهُ لَهُ نُورًا فَمَا لَهُ مِن نُّورٍ ﴿٤٠﴾
40. Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyofunikwa na mawimbi juu ya mawimbi na juu yake yapo mawingu-Giza juu ya giza. Akiutoa mkono wake anakurubia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru, basi hawi na nuru.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٤١﴾
41. Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtaksa vilivyomo mbinguni na ardhini na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Swala yake na tasbihi yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wayatendayo.
وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ ﴿٤٢﴾
42. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo.
VITENDO VYAO NI KAMA SARABI (MANGATI)
Aya 39 – 42
MAANA
Na wale ambao wamekufuru vitendo vyao ni kama sarabi jangwani, mwenye kiu huyadhania ni maji, hata akiyaendea hapati chochote.
Makusudio ya makafiri hapa ni wale wanaokana utume wa Muhammad, kwa sababu ya inadi, ubaguzi, kupuuza au uzembe; yaani hakuutafuta uhakika akiwa ana uwezo wa kufanya utafiti na kuchunguza.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja wale ambao mambo ya dunia hayawafanyi wakaacha akhera na kwamba yeye atawalipa kwa yale mema waliyoyafanya, sasa anawataja hawa wapinzani wakanushaji, kwamba wao wametegemea batili na wakaitakidi kuwa ni haki itakayowafaa mbele ya Mwenyezi Mungu; sawa na mwenye kiu anavyotegemea mazigazi. Akitaka kuyafikia basi anakuta ni jua kali linalomzidishia kiu.
Wala hakuhusika na wasifa huu yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu au utume wa Muhammad(s.a.w.
w
)
tu. Isipokuwa wanahusika wengi katika umma wa Muhammad(s.a.w.
w
)
ambao wanajidhania kuwa ni watu wa heri na takua, huku wakiwafanyia chuki na hasadi waja wa Mwenyezi Mungu na wakiipupia dunia na majanga yake.
Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa-sawa. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.
Kumkuta Mwenyezi Mungu ni kukuta hisabu yake na malipo yake. Maana ni kuwa kafiri anaitakidi akiwa duniani kwamba yeye ataokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu kutokana na amali njema aliyoifanya, lakini atakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu ili aangalie hisabu, hatapata kitu katika vile alivyoviwazia; bali atakuta dhambi, hisabu na adhabu. Matumaini yote yatayeyuka, kama yalivyoyeyuka ya yule aliyetegemea mangati.
Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyofunikwa na mawimbi juu ya mawimbi na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mkono wake anakurubia asiuone.
Bahari kuu ni bahari yenye maji mengi, mawimbi yamepandana na juu yake kuna mawingu mazito. Huu ni mfano fasaha zaidi wa watu wenye matamanio ambao wamezama katika bahari ya maovu na machafu: uongo, riya, mifundo, majisifu, kiburi, tamaa, pupa na mengineyo yasiyokuwa na kikomo. Mwenye kuishi katika giza hili ambalo haoni kitu, ataona vipi hakika na kuielewa.
Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru, basi huyo hana nuru.
Tabrasi amesema: "Makusudio ni ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia wokovu katika akhera, basi hana uokovu." Tuonavyo sisi ni kuwa wale ambao hawaongoki kwenye njia ya haki aliyowapa muongozo Mwenyezi Mungu, basi wao wataishi katika kuzubaa, ujinga na upotevu.
Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtaksa vilivyomo mbinguni na ardhini na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Swala yake na tasbihi yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wayatendayo.
Umepita mfano wake katika Juz. 15 (17:44).
Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, kwa sababu ndiye aliyeziumba na muumba ni mfalme wa kweli.
Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya hisabu na malipo.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُزْجِي سَحَابًا ثُمَّ يُؤَلِّفُ بَيْنَهُ ثُمَّ يَجْعَلُهُ رُكَامًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلَالِهِ وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مِن جِبَالٍ فِيهَا مِن بَرَدٍ فَيُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ وَيَصْرِفُهُ عَن مَّن يَشَاءُ يَكَادُ سَنَا بَرْقِهِ يَذْهَبُ بِالْأَبْصَارِ ﴿٤٣﴾
43. Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatanisha pamoja, kisha huyafanya mrundo? Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka mbinguni, kwenye milima ya mawingu, mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.
يُقَلِّبُ اللَّـهُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّأُولِي الْأَبْصَارِ ﴿٤٤﴾
44. Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hilo kuna mazingatio kwa wenye busara.
وَاللَّـهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِّن مَّاءٍ فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ أَرْبَعٍ يَخْلُقُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤٥﴾
45. Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo, na wengine huenda kwa miguu miwili na wengine huenda kwa minne. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
لَّقَدْ أَنزَلْنَا آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤٦﴾
46. Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha. Na Mwenyezi Mungu humuongoza atakaye kwenye njia iliyonyooka.
MAJI
Aya 43 – 46
MAANA
Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatanisha pamoja, kisha huyafanya mrundo. Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka mbinguni, kwenye milima ya mawingu, mvua ya mawe.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hupeleka upepo unoasukuma mawingu kutoka mji mmoja hadi mwingine, kisha huyakusanya pamoja yakiwa mrundo kwa umbo la mlima. Kwenye mawingu haya kunakuwa na maji yanayomiminika na yanayoganda katika vipande vya theluji ambavyo ndivo vinavyoitwa mvua ya mawe.
Akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye.
Mwenyezi Mungu kutumia mvua ya mawe kwa mujibu wa hekima. Ikiwa hekima imepitisha kuangamia mimea au kitu chochote, basi huipelekea mvua; vinginevyo huiepusha.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13: 12 -13). Huko na sehemu nyingine zinazonasibiana nazo tumeeleza kuwa dhahiri ya ulimwengu inategemea sababu zake za kimaumbile moja kwa moja na zinakomea kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuwa ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.
Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.
Umeme wake ni wa hayo mawingu. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema: "Unakurubia umeme kunyakua macho yao." Juz. 1 (2:20).
Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana, kwa urefu na ufupi.
Hakika katika hilo
la kubadilishakuna mazingatio kwa wenye busara,
ambao hawagandi tu kwenye sababu za maumbile, bali wanamtafuta aliyezifanya na kuzitengeneza na kumtambua.
Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wo huenda kwa matumbo, na wengine huenda kwa miguu miwili na wengine huenda kwa minne.
Hakika uweza wa Mwenyezi Mungu na umoja una ushahidi mwingi usiokuwa na idadi. Miongoni mwao ni ule unajitokeza katika kuumba vitu vilivyoganda, tunayoyashuhudia katika uumbaji mimea, wanyama na wanaotembea ardhini.
Hayo ndiyo yaliyoashiriwa katika Aya hii. Tukiangalia mfungamano wa maji katika kutengenezwa mnyama ni kuwa hakika ya maji ni moja, lakini wanyama walioumbwa kutokana na maji hayo wanatofautiana, wengine wanatembea kwa tumbo, kama wale wanaotambaa, wengine wanatembea kwa miguu miwili, kama binadamu na wengine kwa miguu mine, kama ngamia nyumbu wanyama mwitu na wengineo ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria kwa kauli yake:
Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Wanyama wote, kuanzia aina ndogo hadi kubwa, wako kwenye nidhamu kamili, ambapo kila mmoja anafanya kuliangana na inavyoafikiana na maslahi yake. Hii ni dalili mkataa kwamba nyuma ya yote hayo kuna mpangaji aliye hodari na mwenye hekima.
Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta dalili za kuweko kwake, ukuu wake na umoja wake; kama hizi za kuumba aina mbalimbali za wanyama. Hakuacha udhuru wowote kwa mwenye kutafuta sababu. Imam Ali
anasema:"Amewabunia umbile la ajabu katika vyenye uhai na visivyokuwa na uhai na vilivyotulia na vyenye harakati, akaweka ushahidi na ubainifu katika utovu wa utengenezaji wake na ukuu wa cheo chake, kiasi cha akili kuweza kumfuata na kumkubali na kusalimu amri kwake."
Na Mwenyezi Mungu humuongoza atakaye kwenye njia iliyonyooka.
Hakuna shaka kwamba mwenye kufuata njia iliyonyooka ambayo Mwenyezi Mungu ameiamrisha basi huyo ameongoka mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kuasi amri yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, huyo amepotea kwa Mungu na kwa watu wote, hilo halina shaka.
وَيَقُولُونَ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِّنْهُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَمَا أُولَـٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na wanasema tumeamini Mwenyezi Mungu na Mtume na tumetii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala wao si wenye kuamini.
وَإِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kikundi kimoja kinakataa.
وَإِن يَكُن لَّهُمُ الْحَقُّ يَأْتُوا إِلَيْهِ مُذْعِنِينَ ﴿٤٩﴾
49. Na ikiwa haki ni yao wanamjia kwa kutii.
أَفِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَمِ ارْتَابُوا أَمْ يَخَافُونَ أَن يَحِيفَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَرَسُولُهُ بَلْ أُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٥٠﴾
50. Je, wana maradhi katika nyoyo zao au wanaona shaka au wanahofia kuwa atawadhulumu Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Bali wao ndio madhalimu.
إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥١﴾
51. Haiwi kauli ya waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ila ni kusema: Tumesikia na tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.
وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّـهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٥٢﴾
52. Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.
وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِنْ أَمَرْتَهُمْ لَيَخْرُجُنَّ قُل لَّا تُقْسِمُوا طَاعَةٌ مَّعْرُوفَةٌ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao ya kwamba ukiwaamrisha, hakika watatoka. Sema: msiape! Utiifu unajulikana. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾
54. Sema: mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kama mkikengeuka basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa. Na mkimtii yeye mtaongoka na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi.
WANAFIKI
Aya 47 – 54
MAANA
Na wanasema tumeamini Mwenyezi Mungu na Mtume na tumetii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala wao si wenye kuamini.
Ambao husema tumeamini na tumetii, wako aina tatu: Ya kwanza, ni wale wanaosema kwa ulimi yale wanayoyaamini, kuyakubali moyoni na kufanya kwa mujibu wake. Hawa sio waliokusudiwa kwenye Aya tuliyo nayo.
Aina ya pili, ni wale wanaosema na kuamini, lakini wanaasi wala hawatendi kwa mujibu wake; yaani wanamini kinadharia sio kimatendo.
Aina ya tatu, ni wale wanaosema kwa ndimi zao yale ambayo hayamo nyoyoni mwao kabisa. Hawa ndio wanafiki.
Aya tuliyo nayo inahusu aina ya pili na ya tatu; wala haihusiki na wanafiki tu; kama ilivyosemekana. Kwa sababu imani bila matendo haina faida yoyote, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani au hakuchuma kheri kwa imani yake" Ju. 8 (6:158).
Na wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kikundi kimoja kinakataa.
Wafasiri wengi wanasema kuwa kulitokea ugomvi wa ardhi baina ya mnafiki mmoja na Yahudi. Mnafiki akasema tukaamuliwe kwa Ka'bul-akhbar, Myahudi, kwa kujua kuwa anakubali rushwa. Myahudi akamwambia tukahukumiwe kwa Muhammad kwa kujua kuwa hakubali rushwa. Lakini mnafiki alikataa. Ndio ikashuka Aya hii. Ni sawa iwe riwaya ni sahihi au la, lakini inafafanua zaidi tafisiri ya Aya.
IJARIBU DINI YAKO NA IMANI YAKO
Na ikiwa haki ni yao wanamjia kwa kutii.
Wao hawaijui haki ila ikiafikiana na matamanio yao; kama ikihalifiana nayo basi wanaikana. Huu ndio ubinafsi ambao hauhusiki na wanafiki tu; isipokuwa uko katika maisha ya baadhi ya waumini au wale wanaojiita waumin. Wanadai kuwa wanaidhihirisha haki na wanipinga batili. Lakini ni haki gani hiyo wanayoidhihirisha na batili gani hiyo wanayoipinga?
Katika ufahamu wao na imani yao, haki ni ile inayoafikiana na masilahi yao na batili ni ile inayohalifiana na masilahi yao. Wao wamejisahau.
Wanaamini kuwa hawatendi isipokuwa haki na hawatamki isipokuwa ukweli, lakini hawapati msukumo wa hilo, isipokuwa kwa msukumo wa hawaa na masilahi yao.
Hawa wana hali mbaya zaidi kuliko wanafiki ambao wanawadanganya watu na hawajidanganyi wao wenyewe. Kwa sababu wana uhakika na uongo wao na riya yao.
Lakini hawa wanafanya uovu wenyewe wakijiona wanafanya wema. Sio siri kusema kuwa wao hawana sifa ya imani. Kwa sababu mumin wa kweli hahadaiki na hila za shetani na ubatilifu wake; bali anajituhumu ikiwa kitendo chake kitampambia sifa. Kwani kazi muhimu ya shetani ni kuwapambia watu matendo yao maovu, kuwaonyesha batili kuwa ni haki na upotevu kuwa ni unyoofu.
Inasemekana kuwa mtu mmoja alimwambia Iblisi: "Wewe huwawezi waumini mfano wangu." Ibilisi akacheka na kumwambia maneno yako haya tayari yanaonyesha umekwishaingia kwenye mtego. Ghururi yako hii ni mtekelezaji aliyeingia moyoni mwako, akauharibu na akaupofusha mpaka ukawa hauna hisia.
Baada ya hayo! Mwenye kutaka kuijaribu imani na dini yake, inatakikana aangalie kuwa je, anaituhumu nafsi yake au anaiona ni safi isiyokuwa na kasoro? Je, anaikubali haki hata kama ni dhidi yake? Ikiwa atajituhumu na kuikubali haki kwa namna yoyote itakayokuwa basi yeye ni katika waumini, vinginevyo atakuwa katika walioangamia.
Je, wana maradhi katika nyoyo zao au wanaona shaka au wanahofia kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali wao ndio madhalimu.
Walikataa kuhukumiwa kwa Mtume; wala hakuna lililopelekea hilo ila chuki yao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu au kuutilia shaka utume wake au kuhofia kuwa atawadhulumu. Sababu yoyote itakayokuwa, lakini hakatai hukumu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
isipokuwa kafiri au aliyeidhulumu nafsi yake na ya mwingine.
Haiwi kauli ya waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ila ni kusema: Tumesikia na tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wanafiki na kwamba wao wana- jizuia kuiendea mahakama ya Mtume wanapoitwa huko, sasa anataja waumini, kwamba ni wale wanaomwitikia kila atakayewapa mwito wa kwenda kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wanaitikia mwito wake kwa unyenyekevu na utiifu. Hawa ndio wanachama wa Mwenyezi Mungu"Hakika wanachama wa Mwenyezi Mungu ndio wenye kufanikiwa."
(58:22)
Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu kwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na pepo yake.
Kuunganisha hofu na uchaji kwenye utiifu, ni kwa upande wa kuunganisha kitafsiri. Kwa sababu mwenye kumtii Mwenyezi Mungu atakuwa amemuhofia na kumcha. Lakini wafasiri hawakukubali ila kutafoutisha baina ya matendo haya. Wakasema: kumtii Mwenyezi Mungu kunakuwa katika aliyoyaamrisha na kuyakataza, kumhofia kunakuwa katika maasi na kumcha kunakuwa katika yatakayokuja.
Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao ya kwamba ukiwaamrisha, hakika watatoka.
Walioapa ni wanafiki. Wao waliaapa kwa kiapo cha nguvu kwamba Mtume akiwaamrisha waache majumba yao na mali zao basi watamsikiliza na kumtii, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawakemea na imani yao hiyo ya uongo kwa kusema:
Sema: msiape! Utiifu unajulikana. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
Yaani ewe Muhammad! Waambie wanafiki, msiape kwani Mwenyezi Mungu anajua kuwa utiifu wenu huu ni wa uongo na wa kujionyesha (ria) na kwamba nyinyi ni maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na amewaandalia adhabu chungu mnayostahiki.
Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa dhahiri na batini, sio kwa unafiki na ria. Kama mkikengeuka basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa.
Wanaambiwa wanafiki, na yaliyo juu yake ni juu yake Mtume. Maana ni kuwa Mtume ni mwenye kukalifiwa kufikisha na nyinyi ni wenye kukalifiwa kutii. Atakayepuuza basi hisabu ya kupuuza itakuwa ni yake; ni sawa awe ni Mtume au yule aliyetumiwa Mtume.
Na mkimtii yeye mtaongoka na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi. Mwenye kutekeleza aliyokalifishwa, basi malipo yake yako kwa Mwenyezi Mungu.
Mtume amekwishafikisha na kutekeleza wajibu wake, yaliyobaki, kazi kwenu.