TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE Juzuu 18

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 12080
Pakua: 3030


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12080 / Pakua: 3030
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE Juzuu 18

Mwandishi:
Swahili

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾

55. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale ambao wameamini na wakatenda mema kuwa hakika atawafanya makhalifa katika ardhi, kama alivyowafanya waliokuwa kabla yao. Na kwa yakini atawaimarishia dini yao aliyowapendelea na hakika atawabadilishia amani baada ya hofu yao. Wawe wananiabudu, hawanishirikishi. Na mwenye kukufuru baada ya hayo, basi hao ndio mafasiki.

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na simamisheni Swala na toeni Zaka na mtiini Mtume ili mpate kurehemiwa.

لَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ وَلَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٥٧﴾

57. Usiwadhanie waliokufuru kwamba watashinda na makazi yao ni motoni na hakika ni marejeo maovu.

UKHALIFA WA WAUMINI ARDHINI

Aya 55 – 57

MAANA

Mwenyezi Mungu amewaahidi wale ambao wameamini na wakatenda mema kuwa hakika atawafanya makhalifa katika ardhi, kama alivyowafanya waliokuwa kabla yao.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa umma wowote utakaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ukashikana na sharia yake, basi Mwenyezi Mungu atawafanya makhalifa na kuwaimarisha ardhini. Hilo ni hakika.

Baadhi ya wafasiri wamechukua hakika hii, kisha wakafafanua na kufasiri maana ya imani na matendo mema. Wakayawekea mipaka yake na maelezo yake. Ama sisi tuko pamoja na wale waliosema kuwa makusudio ya Aya ni Mtume na maswahaba. Kwani wao walipata tabu na udhia mwingi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kabla na baada ya Hijra. Washirikina na mayahudi kwa pamoja waliwalenga kwa mishale yao.

Hadi kufikia mwaka wa ushindi, walikuwa huko Madina hawawezi kupambazukiwa au kuchwelewa na jua bila ya kushika silaha. Mpaka mmoja wao akasema, kama ilivyo katika tafsir At-Tabari: Hakuna siku tutakayokuwa na amani na kuweka chini silaha yetu. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) akamwambia: 'Hamtakuwa na wepesi (mpaka ikifika ile siku) atakapokuwa mtu anakaa bila ya silaha. Ahadi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikathibitika.

Hazikupita siku, ikawa wanaishi katika amani ya nafsi zao na mali zao, wakatawala nchi zote za urabuni na kuchukua miji mingi ya Ulaya ya mashariki na magaharibi.

Na kwa yakini atawaimarishia dini yao aliyowapendelea.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaishiria kuenea Uislamu na utawala wake mashariki mwa ardhi na magharibi yake.

Na hakika atawabadilishia amani baada ya hofu yao.

Hii ndio natija ya kuvumila, kuwa na subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Yamepita maelezo yake kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 9 (8:26)

Wawe wananiabudu, hawanishirikishi.

Shirki haihusiki na kuabudu masanamu peke yake. Atakayemtii kiumbe katika kumuasi Mungu basi huyo yuko katika hukumu ya shirki.

Na mwenye kukufuru baada ya hayo ya kuwa khalifa, kuimarishwa kati- ka ardhi na kuwa na amani baada hofu,basi hao ndio mafasiki na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki.

Na simamisheni Swala na toeni Zaka na mtiini Mtume ili mpate kurehemiwa.

Huu ni ubainifu na tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya iliyopita. 'Wale ambao wameamini na wakatenda mema.

Usiwadhanie waliokufuru kwamba watashinda na makazi yao ni motoni na hakika ni marejeo maovu.

Anaambiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) kwa lengo la kumhadharisha anayeuhalifu ujumbe wake na akaupinga. Vile vile yeye ni tishio kwa kila mwenye kubadili neema ya Mwenyezi Mungu kuwa kufuru. Katika Nahjul-balagha imeelezwa: "Uchache wa kulazimiana kwenu na Mwenyezi Mungu ni kutotumia neema zake kwa kumuasi."

NJIA NYINGINE YA MUUJIZA WA QUR'AN

Katika Juz.1 (2:23 - 25) kifungu cha 'Siri ya muujiza wa Qur'an,' tulieleza kauli za maulama kuhusu muujiza wa Qur'an. Katika Juz. 3 (3:61) tulisema kwamba kuwa tayari Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) na maapizano kwa kutegemea ushindi ambao umeelezewa na Qur'an na ukawa, ni dalili kubwa ya ukweli wa Qur'an na yule aliyeletewa.

Katika Juz. 6 (5:53) tulieleza kwamba Qur'an ilivyofichua tabia ya mayahudi kwamba wao lau watakuwa na utawala wangefanya kama wafanyavyo leo huko Palestin, ni dalili mkataa ya muujiza wa Qur'an; ambapo yamethibitika hayo baada ya kuyatolea habari kwa zaidi ya miaka elfu moja na mia tatu iliyopita.

Hivi sasa sisi tunapofasiri Aya hii tuliyo nayo 'Mwenyezi Mungu amewaahidi…' tumegundua njia nyingine ya muujiza wa Qur'an. Nayo ni kuwa matamshi ya Qur'an ni ya kiarabu ambayo wameyatumia waarabu katika mazungumzo na maandishi, kabla ya Qur'an na baada yake, bila ya tofau- ti ya herufi au mfumo wa jumla, lakini pamoja na hayo, jumla kwenye Qur'an inabeba maana nyingi, jambo ambalo halipatikani pengine pasipokuwa kwenye Qur'an; hata Hadith pia.

Ndio maana Imam Ali(a.s ) akamwambia Ibn Abbas:"Usigombane na makhawarij kwa Qur'an, kwa sababu Qur'an inachukua sana njia mbalimbali, utasema na wao watasema, lakini wahoji kwa Hadith, hawatakuwa na njia ya kutokea"

Siri katika hilo inakuwa katika upeo wa mwenye kunena sio wa maneno yenyewe. Vinginevyo mfumo wa Qur'an na isiyokuwa Qur'an ungekuwa mmoja tu. Hakika maneno yameganda hayana uhai. Msemaji ndiye anayeyapa uhai. Ndio maana kukawa na tofauti ya uhai wa maneno kulingana na msemaji mwenyewe.

Atakavyozungumza mataalamu ni tofauti na atakavyozungumza mtu wa kawaida, hata kama maneno na jumla zitakuwa sawa. Hata Qur'an pia ufahamu wake unatofautiana kulingana na anayeisoma. Vile vile maneno yoyote yanatofautiana kulingana na anayesema akiwa mnafiki au mwenye ikhlasi.

Kwa hiyo upeo mkubwa wa Qur'an kwa njia mbalimbali ni dalili mkataa kuwa inatokana na ambaye elimu yake imeenea kwenye kila kitu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنكُمْ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ مِّن قَبْلِ صَلَاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُم مِّنَ الظَّهِيرَةِ وَمِن بَعْدِ صَلَاةِ الْعِشَاءِ ثَلَاثُ عَوْرَاتٍ لَّكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ وَلَا عَلَيْهِمْ جُنَاحٌ بَعْدَهُنَّ طَوَّافُونَ عَلَيْكُم بَعْضُكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٨﴾

58. Enyi ambao mmeamini! Na wawatake ruhusa, wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume na wale ambao hawajafikia baleghe miongoni mwenu, mara tatu kabla ya Swala ya Alfajiri na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Swala ya Isha. Ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

وَإِذَا بَلَغَ الْأَطْفَالُ مِنكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٩﴾

59. Na watoto wanapofikia kubaleghe basi na watake ruhusa, kama walivyotaka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ وَأَن يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَّهُنَّ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٦٠﴾

60. Na wanawake wakongwe ambao hawatarajii kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao bila ya kuonyesha mapambo. Na kama wakistahi ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

KUPIGA HODI MTOTO NA MTUMWA

Aya 58 – 60

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Na wawatake ruhusa, wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume na wale ambao haijafikia baleghe miongoni mwenu, mara tatu.

Iliyowamiliki mikono ni watumwa.

Kwenye Sura hii katika Aya ya 27, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekataza kuingia nyumba za wengine bila ya kubisha hodi. Katika Aya ya 28, akaamrisha kurudi ikiwa mtu hakuitikiwa hodi. Katika Aya 31 akawakataza wanawake kujiweka wazi; isipokuwa kwa baadhi ya ndugu, watumwa, wasiokuwa na matamanio na waototo wadogo wasiopambanua uchi na kitu kingine.

Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema waamrisheni watumwa wenu na watoto wadogo ambao hawajafikia baleghe, wabishe hodi, kabla ya kuingia kwenu, katika nyakati tatu. Kwa sababu ni nyakati za faragha ya mtu kujiweka uchi. Hizo nyakati tatu ni:

1.Kabla ya Swala ya Alfajiri, ambapo mtu anaamka kutoka usingini akiwa na nguo za kulalia.

2.Na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri; yaani wakati wa kulala kidogo mchana (qaylula) na kupumzika kwa sababu mtu anapunguza nguo zake.

3.Na baada ya Swala ya Isha, ambapo watu wanaelekea kwenye mambo yao mahususi.

Ni nyakati tatu za faragha kwenu.

Huu ni ubainfu wa kutofautisha nyakati hizo tatu na nyingine na kubainisha sababu za kupiga hodi, kwamba ni wakati wa faragha wa mtu kuvua nguo.

Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi.

Hakuna dhambi kwenu enyi waumini wala kwa watumwa na watoto baada ya nyakati hizi kuingia bila ya idhini, katika nyakati zisizokuwa hizi.

Kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi.

Yaani kuwazunguikia wao, na wao kuwazungukia nyinyi. Kila mmoja anamuhitajia mwingine.

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

Amewabainishia hukumu hizi na akawaamrisha kulazimiana nazo ili muwe na adabu kwa elimu yake na hekima yake.

Na watoto wanapofikia kubaleghe basi na watake ruhusa, katika nyakati zote, sio katika nyakati tatu. Kwa sababu ruhusa hii ya nyakati tatu ni kwa wale ambao hawajafikia kubaleghe. Ama wale ambao wame- baleghe hawana tofauti na wengine walio wakubwa. Haya ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Kama walivyotaka ruhusa wa kabla yao.

Yaani kama ilivyo wajibu kuomba ruhusa kwa wakubwa wakati wote, vile vile ni wajibu kwa aliyefikia baleghe bila ya kutofautisha. Mvulana anakuwa baleghe kwa kutoa mbegu za uzazi au kufikisha miaka 15. Msichana anakuwa baleghe kwa kutoka hedhi au kushika mimba au kufik- isha miaka 9 kwa uchache. Wengine wanasema ni miaka 15.

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

Sisi hatujui wajihi wa kukaririka huku, kulikokuja moja kwa moja bila ya kuingia kati Aya nyingine, isipokuwa kutilia mkazo na kuhimiza amri ya kupiga hodi.

Na wanawake wakongwe ambao hawatarajii kuolewa.

Hawa ni wanawake waliokoma kutoka hedhi na kuzaa wakawa ni wazee wasiokuwa na matamanio ya wanaume wala wanaume pia hawawatamani.

Si vibaya kwao kupunguza nguo zao bila ya kuonyesha mapambo.

Hakuna ubaya kwa bibi kikongwe kuvua nguo zake za nje ambazo anazi- vaa barabarani na sokoni, lakini asikusudie kwa hilo kujionyesha kwa wanaume ili wamwangalie, hata kama yeye si wa wanaume, lakini huenda akatokea atakayesema: Huyu enzi zake!

Na kama wakistahi ni bora kwao.

Ni bora kwa bibi kikongwe, kutopunguza nguo zake kwa watu kando, hata kama ameruhusiwa kufanya hivyo. Kwa sababu hilo liko mbali na tuhuma. Kuna Hadith isemayo: "Acha lisilo na ubaya kwa kuhadhari lilo na ubaya."

Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

Anasikia kauli na anajua yanayotia wasiwasi katika nyoyo.

لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾

61. Si vibaya kwa kipofu, wala kwa kiguru, wala kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila kwenye nyumba zenu, au nyumba za baba zenu au nyumba za mama zenu au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za khalati zenu, au za mliowashikia funguo zao au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba mjitolee salaam. Ni maamkuzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu yenye baraka yaliyo mema. Hivyo ndivyo anavyowabainishia Mwenyezi Mungu Aya zake mpate kutia akilini.

SI VIBAYA KWA KIPOFU

Aya 61

MAANA

Wanaombiwa katika neno 'Mliowashikia' ni walio na utawala kwenye mali kwa usimamizi, wasiya au wakala. Maana ya dhairi ya Aya ni kuwa hakuna ubaya kwa kipofu, kiguru, mgonjwa na wengineo kula bila ya kuomba ruhusa, kwenye majumba ya ndugu zao waliotajwa, wakiwa pamoja na wenye nyumba au peke yao. Vile vile si vibaya kwa wakili kula kwa wema mali aliyowakilishwa; kama ambavyo si vibaya kwa rafiki kula nyumbani kwa rafiki yake.

Wote hawa wanaweza kula katika majumba haya kwa sharti la kutojua kuwa wenyewe hawataki. Mafakihi wengi wanasema anayoruhusa ya kula matunda, saladi au chakula kilichokwishaandaliwa, lakini sio kile ambacho kimewekwa akiba.

Unaweza kuuliza kuwa : neno 'Wala kwenu nyinyi mkila kwenye nyumba zenu' inafahamisha kuwa mtu anaweza kula nyumbani kwake bila ya kujiomba ruhusa yeye mwenyewe. Maneno hayaendi sawa hapa, itakuwaje?

Jibu : Makusudio yake ni nyumba ya mke na ya mtoto, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ﴿١١﴾

"Na amewajaalia mke na mume kutokana na nyinyi wenyewe." (42:11).

Kuna Hadith isemayo:"Chema zaidi anachokula mtu ni chumo lake." Na mtoto ni chumo lake, kutokana na Hadith nyingine isemayo:"Wewe na mali yako ni wa baba yako."

Swali la pili : Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kuwataja vipofu walemavu na wagonjwa, na wao wanaingia kwenye neno 'nyinyi wenyewe.' Kwa sababu wanambiwa watu wote. Sasa kwani kuna mtu atakayetia wasiwasi kwa walemavu hao waliotajwa na wagonjwa, kuwa hawafai kula kwenye hizo nyumba?

Kuna kauli nyingi za majibu ya swali hili. Wafasiri wengine wametaja tano. Iliyo karibu zaidi ni ile isemayo kuwa maswahaba walikuwa wakiona uzito kula na vipofu kwa kuwa hawatoweza kuona chakula kinachofaa, wasije wakala mapumba. Na kiguru waliona kuwa atapata tabu ya kukaa na wengine kwa vile chakula kilikuwa kinawekwa chini na mgonjwa naye hawezi kushiriki vizuri kula na wengine, ambapo wenzake watamaliza haraka naye ataona haya kubaki peke yake.

Kwa kuwa maswahaba walikuwa hawali katika majumba haya yaliyotajwa kutokana na Aya isemayo: "Wala msile mali zenu baina yenu kwa batili." Juz.1 (2:88). Ndipo Mwenyezi Mungu akawahalalishia kula kwenye majumba hayo, pamoja na kula na walemavu hao na wagonjwa.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَإِذَا كَانُوا مَعَهُ عَلَىٰ أَمْرٍ جَامِعٍ لَّمْ يَذْهَبُوا حَتَّىٰ يَسْتَأْذِنُوهُ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَأْذِنُونَكَ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ فَإِذَا اسْتَأْذَنُوكَ لِبَعْضِ شَأْنِهِمْ فَأْذَن لِّمَن شِئْتَ مِنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمُ اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٢﴾

62. Hakika waumini ni wale tu ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakiwa pamoja naye kwa jambo la wote, hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Hakika wale wanaokuomba ruhusa, hao ndio wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na watakapokuomba ruhusa kwa baadhi ya mambo yao, mruhusu umtakaye miongoni mwao na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.

لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

63. Msifanye kumwita Mtume baina yenu kama mnavyoitana nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale wanoondoka kwa kujificha. Basi na watahadhari wale ambao wanahalifu amri yake, isije ikawapata fitna au ikawapata adhabu chungu.

أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قَدْ يَعْلَمُ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ وَيَوْمَ يُرْجَعُونَ إِلَيْهِ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٦٤﴾

64. Ehee! Hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika yeye anajua mliyo nayo. Na siku watakaporudishwa kwake atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

HAWAONDOKI MPAKA WAKUOMBE RUHUSA

Aya 62 – 64

MAANA

Hakika waumini ni wale tu ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakiwa pamoja naye kwa jambo la wote, hawaondoki mpaka wamtake ruhusa.

Wanafiki walikuwa wakitoroka kwa kujificha kila wanapoitwa kwenye jambo muhimu katika kikao pamoja na Mtume. Ndipo ikashuka Aya hii kubainisha wajibu wa kutiiwa Mtume na umma wake, wajibu wa kusaidiana waislamu ili kuuinua Uislamu na kwamba Mwislamu wa kweli ni yule anayeitikia mwito wa Mtume na kusaidiana kwa pamoja, jambo ambalo lina kheri na masilahi, kwa juhudi zake zote. Wala asikimbie wajibu huu kwa kutafuta visababu.

Akiwa ni mkweli katika udhuru basi auleze kwa Mtume(s.a.w. w ) na amuombe ruhusa. Hali hii ni wajibu kwa kila kiongozi anayetekelea haki za raia kwa ikhlasi.

Hakika wale wanaokuomba ruhusa , wakiwa ni wa kweli katika kauli zao na wana haja ya dharura,hao ndio wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kikwelikweli. Ama wale ambao wanatafuta visababu vya uongo, basi hao ndio wanafiki wanaosema kwa midomo yale ambayo hayako nyoyoni mwao. Muimin ni kama askari, anangojea amri tu ya kiongozi wake wala haiachi ila kama ana udhuru wa kweli, hapo huomba ruhusa.

Na watakapokuomba ruhusa kwa baadhi ya mambo yao, mruhusu umtakaye miongoni mwao na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufia, Mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu amemwachia amri Mtume(s.a.w. w ) akitaka atoe ruhusa au akatae, na akamwamrisha kumuombea Mungu yule mkweli mwenye ikhlasi.

Unaweza kuuliza kuwa : Mwenyezi Mungu mahali pengine amesema: "Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo?" Juz. 10 (9:43) na kwenye Aya hii amemruhusu kutoa ruhusa, zitaungana vipi Aya hizi?

Jibu : Kule Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake kuthibitisha kuweza kumjua mkweli na muongo. Katika sura hii tuliyo nayo, amem- ruhusu kutoa ruhusa baada ya kujua uhakika wa mwenye kutaka ruhusa, malengo yake na natija ya kutaka idhini awe mumin au mnafiki. Kwa hiyo atatoa ruhusa kwa misingi hii.

Inawezekana ni masilahi kumpa ruhusa mnafiki, ikiwa kubakia kwake kundini kunaleta madhara na pia inawezekana kumnyima ruhusa kukawa na manufaa kwa kuhitajika kwake kundini.

Msifanye kumwita Mtume baina yenu kama mnavyoitana nyinyi kwa nyinyi.

Maneno wanelekezewa wale waliokuwa na Mtume, wakifundishwa adabu wakiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) ambapo waliamrishwa wanapotaka ruhusu wasimwite kwa majina yake au lakabu yake; mfano kusema: ewe Muhammad au Ewe Abul-Qasim; kama wanavyoitana wao kwa wao.

Bali wamwite kwa sifa zake tukufu, za unabii au utume; kwa mfano kusema: Ewe Nabii wa Mungu au Ewe Mtume wa Mungu! Kwani kumheshimu yeye ndio kumheshimu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amekutanisha twaa yake na ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) katika Aya kadha zikiwemo hizi:

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٥٧﴾

"Basi wale waliomuamini na wakamheshimu na wakamsaidia na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye. Hao ndio wenye kufaulu. Juz.9 (7:157).

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ ﴿٢﴾

"Enyi ambao mmeamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele, kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi." (49:2).

Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale wanoondoka kwa kujificha.

Yaani kujificha kwa wanafiki wanapotoroka pale wanapoambiwa mambo muhimu, kama jihadi n.k., hakufichiki kwa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa wanafiki walikuwa wakiondoka kwenye vikao vya Mtume(s.a.w. w ) kwa kujiziba na wengine.

Basi na watahadhari wale ambao wanahalifu amri yake isije ikawap- ata fitna au ikawapata adhabu chungu.

Amri yake hapa ni amri ya Mungu na makusudio ya fitna hapa ni balaa duniani. Hii ni hadhari na ahadi ya adhabu duniani na akhera kwa mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Ehee! Hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika yeye anajua mliyo nayo. Na siku watakaporudishwa kwake atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Mwenyezi Mungu hawahitajii walimwengu. Twaa ya mtiifu haimfai chochote, wala uasi wa muasi haumdhuru chochote.

Yeye ni mjuzi wa yanayokuwa nyoyoni na wa siku ambayo watu watakusanyika ndani yake kwa hisabu. Atawapa habari ya matendo yao na makusudio yao na watapata wanayostahiki wala Mola wako hamdhulumu yoyote.