1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA
Mwendelezo Wa Sura Ya Ishirini Na Tano: Surat Al-Furqan.
وَقَالَ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْنَا الْمَلَائِكَةُ أَوْ نَرَىٰ رَبَّنَا لَقَدِ اسْتَكْبَرُوا فِي أَنفُسِهِمْ وَعَتَوْا عُتُوًّا كَبِيرًا ﴿٢١﴾
21. Na walisema wale wasiotarajia kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu. Hakika wametakabari katika nafsi zao na wameasi uasi mkubwa.
يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلَائِكَةَ لَا بُشْرَىٰ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ وَيَقُولُونَ حِجْرًا مَّحْجُورًا ﴿٢٢﴾
22. Siku watakayowaona Malaika, haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu, na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho.
وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾
23. Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, kisha tutayafanya mavumbi yaliyotawanyika.
أَصْحَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَئِذٍ خَيْرٌ مُّسْتَقَرًّا وَأَحْسَنُ مَقِيلًا ﴿٢٤﴾
24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi bora na mapumziko mazuri zaidi.
وَيَوْمَ تَشَقَّقُ السَّمَاءُ بِالْغَمَامِ وَنُزِّلَ الْمَلَائِكَةُ تَنزِيلًا ﴿٢٥﴾
25. Siku itakapopasuka mbingu kwa mawingu na watateremshwa malaika kwa wingi.
الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ لِلرَّحْمَـٰنِ وَكَانَ يَوْمًا عَلَى الْكَافِرِينَ عَسِيرًا ﴿٢٦﴾
26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Mwingi wa rehema. Na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا ﴿٢٧﴾
27. Na siku dhalimu atajiuma mikono yake akisema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!
يَا وَيْلَتَىٰ لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا ﴿٢٨﴾
28. Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki.
لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا ﴿٢٩﴾
29. Kwa hakika amenipoteza nikaacha dhikri baada ya kunijia, na shetani ndiye anayemtupa mtu.
HAKUNA FURAHA KWA WAKOSEFU
Aya 21 – 29
MAANA
Na walisema wale wasiotarajia kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu.
Bado maneno yanaendelea kuwahusu washirikina, wasiotarajia kukutana na Mola wao, wala kuhofia adhabu yake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya hii, amewazungumzia kwamba wao wamependekeza washuke Malaika ili wawape habari kuwa Muhammad ni Nabii au aje Yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu atoe habari hiyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:92)
Hakika wametakabari katika nafsi zao na wameasi uasi mkubwa.
Kuna kiburi gani kikubwa zaidi kuliko jeuri yao hii ya kutaka kumuona Mungu na kuzungumza naye ana kwa ana? Hawa hawana tofauti na wale waliosema kuwa hatumwamini Mungu mpaka tumuone, wakati huo wanaamini vitu ambavyo haviingii katika hisia yoyote.
Watu wa kimaada wanadai kuwa hakuna kitu chochote isipokuwa asili pofu ambayo ilijileta yenyewe au ilipatikana kwa sadfa, na ndiyo iliyoupangilia ulimwengu huu wa ajabu na iliyoumba usikizi na uoni. Katika mantiki yao ni kwamba asili ndiyo iliyo na uwezo wa kila kitu, lakini hiyo yenyewe haitambui kitu.
Wao wanajipinga wenyewe, kwa sababu kukubali kwao kupatikana nidhamu, ni kukiri kuweko nguvu yenye uwezo na ujuzi; na kusema kwao kuwa hakuna chochote isipokuwa asili pofu ni kuikana nguvu hiyo. Maana yake ni kuwa asili ina utambuzi na haina utambuzi, inajua na haijui.
Siku watakayowaona Malaika, haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu.
Washirikina walipendekeza washukiwe na malaika, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu kuwa kutakuwa na siku ambayo watawaona malaika, Siku ya Kiyama, lakini hakutakuwa na jambo la kuwafurahisha , bali ni majanga juu ya majanga yatakayowapata:
يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٥﴾
“Siku itakapowafunika adhabu kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyokuwa mkiyatenda” (29:55).
Na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho.
Watakaosema ni malaika. Maana ni kuwa malaika watawaambia wakosefu, leo ni haramu mtazuiwa kuona mnayoyataka.
Imesemekana kuwa watakaosema ni wakosefu kuwaambia malaika kuwa haifai nyinyi leo kutuudhi na kutuadhibu.
Tafsiri zote mbili zinafaa na zinarejea kwenye maana moja ambayo ni kuhofia wakosefu shari ya siku ya Kiyama na vituko vyake.
Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo,
waliyodhani kuwa yatawafaa leo,kisha tutayafanya mavumbi yaliyotawanyika.
Kwa sababu yalikuwa kwenye misingi isiyokuwa ya imani wala ikhalsi: “Mfano wa wale ambao wamemkufuru Mola wao vitendo vyao ni kama majivu yanayopeperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya kimbunga. Hawana uwezo wa chochote juu ya walichokichuma. Huko ndiko kupotelea mbali.” Juz. 13 (14:18).
Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi bora na mapumziko mazuri zaidi.
Makusudio ya bora na zaidi sio uzaidi wa mengine, isipokuwa makusudio ni kuwa makazi na mapumziko hayo yenyewe ni bora na mazuri; ni kama kusema Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, kwa maana ya kuwa ni mkubwa zaidi katika dhati yake na sifa zake.
Siku itakapopasuka mbingu kwa mawingu.
Makusudio ya siku hapa ni Siku ya Kiyama; na mawingu ni sayari ambazo zitakuwa chembechembe zisizoweza kuonekana hata kwa macho, zitaijaza anga, kama vile mawingu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria kuharibika kwa Siku hiyo, kwenye Aya nyingi; kama vile:
إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ﴿١﴾
“Jua litakapokunjwa.” (81:1),
وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انتَثَرَتْ ﴿٢﴾
“Na nyota zitakapotawanyika.” (82:2).
Yaani jua litakapozimika na nyota zitakapoanguka.”
Na watateremshwa malaika kwa wingi,
wakiwa na ya kuwafurahisha wema na kuwachukiza wakosefu.
Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Mwingi wa rehema
Yeye tu peke yake, hakuna atakayekuwa na lolote.
Na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
Hakuna siku ngumu zaidi kwa mkosefu kuliko siku ya kuhukumiwa kwake, kuhisabiwa makosa yake na kutolewa hukumu ya haki na uadilifu? Lau angelihukumiwa kunyongwa ingelikuwa mambo yamekwisha, lakini ni hukumu ya kudumu:
كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ ﴿٥٦﴾
“Kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilishia ngozi nyingine ili waonje adhabu.” Juz.5 (4:56).
Na siku dhalimu atajiuma mikono yake akisema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!
Hiki ni kinaya cha majuto na masikitiko. Hapo ndio ukomo wa kila mwenye kughurika, mzushi na muongo. Miongoni mwa dua zilipokewa kutoka kwa Nabii(s.a.w.w)
ni:“Ewe Mola wangu! Najilinda kwako na madhambi yanayoleta majuto.”
Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki.
Makusudio ya fulani hapa ni kila mwenye kufuatwa aliyempoteza mfuasi wake na kumwongoza kwenye maangamizi. Kuna Hadith isemayo:“Mtu atafufuliwa kwenye dini ya rafiki yake.”
Jamaa katika wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilimshukiwa Uqba bin Mu’it na Ubayya bin Khalaf. Kwamba dhalimu atakayeuma mikono yake ni huyo wa kwanza na fulani ni huyo wa pili. Hata kama tukikadiria usahihi wa riwaya, ni kuwa sababu ya kushuka Aya haizuwii kuenea kwa wengine.
Hakika amenipoteza nikaacha dhikri baada ya kunijia, na shetani ndiye anayemtupa mtu.
Makusudio ya dhikri hapa ni Qur’an, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelitumia neno hili kwa kukusudia Qur’an katika Aya kadhaa; kama vile:
ص وَالْقُرْآنِ ذِي الذِّكْرِ ﴿١﴾
“Naapa kwa Qur’an yenye dhikri.” (38:1).
Aya inafahamisha kuwa wale walioisikiza Qur’an walikinai kwenye nafsi zao, lakini mashetani-watu waliwadanganya na wakawaepusha na haki, ikawa mwisho wao ni kufedheka. Na huu ndio mwisho wa kila mwenye kufanya kwa maelekezo ya watu wa hawa, si kwa maelekezo ya imani yake na dhamiri yake.
وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا ﴿٣٠﴾
30. Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.
وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا ﴿٣١﴾
31. Na hivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu. Na Mola wako anatosha kuwa mwenye kuongoza na mwenye kunusuru.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً كَذَٰلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا ﴿٣٢﴾
32. Na walisema wale ambao wamekufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja? Ndivyo hivyo, ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.
وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا ﴿٣٣﴾
33. Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyonzuri.
الَّذِينَ يُحْشَرُونَ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ إِلَىٰ جَهَنَّمَ أُولَـٰئِكَ شَرٌّ مَّكَانًا وَأَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٣٤﴾
34. Wale watakaokusanywa kifudifudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahali pabaya na ndio wenye kupotea njia sana.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا ﴿٣٥﴾
35. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.
فَقُلْنَا اذْهَبَا إِلَى الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَدَمَّرْنَاهُمْ تَدْمِيرًا ﴿٣٦﴾
36. Tukawaambia nendeni kwa watu waliozikadhibisha Ishara zetu, basi tukawaangamiza kabisa.
وَقَوْمَ نُوحٍ لَّمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ وَجَعَلْنَاهُمْ لِلنَّاسِ آيَةً ۖ وَأَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿٣٧﴾
37. Na watu wa Nuh walipowakadhibisha mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.
وَعَادًا وَثَمُودَ وَأَصْحَابَ الرَّسِّ وَقُرُونًا بَيْنَ ذَٰلِكَ كَثِيرًا ﴿٣٨﴾
38. Na kina Ad na Thamud na watu Rass na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.
وَكُلًّا ضَرَبْنَا لَهُ الْأَمْثَالَ وَكُلًّا تَبَّرْنَا تَتْبِيرًا ﴿٣٩﴾
39. Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.
وَلَقَدْ أَتَوْا عَلَى الْقَرْيَةِ الَّتِي أُمْطِرَتْ مَطَرَ السَّوْءِ أَفَلَمْ يَكُونُوا يَرَوْنَهَا بَلْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ نُشُورًا ﴿٤٠﴾
40. Na kwa hakika wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je hawakua wakiuona? Bali walikuwa hawatarajii kufufuliwa.
WAMEIFANYA QUR’AN NI MAHAME
Aya 30 – 40
MAANA
Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.
Yaani wameachana nayo na wakakataa kuiamini au kuipa mtazamo wa kutafuta haki ili kuwa na yakini nayo. Vigogo wa kikuraishi waliukadhibisha unabii wa Muhammad(s.a.w.w)
na yaliyosemwa na Qur’an kwa kuhofia uchumi wao na kupupia vyeo vyao.
Ndipo Mtume akapeleka mashtaka yake kwa Mola wake ambaye mambo yote yako mikononi mwake. Hivi ndivyo afanyavyo mwenye akili, hashtakii haja yake isipokuwa kwa yule ambaye hukumu ya mashtaka hayo iko mikononi mwake.
Ndio, inawezekana mtu kumshtakia rafiki yake atakayemliwaza na kumpa moyo. Imam Jafar Sadiq
amesema:“Mwenye kumshtakia ndugu yake amemshitakia Mwenyezi Mungu, na mwenye kumshtakia mwingine atakuwa amemshtaki Mungu.”
Anakusudia ndugu wa kiimani, na kwamba muuminii akimshtakia muuminii kama yeye humwombea Mungu ampe faraja na kumwamrisha awe na subira, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutokata tamaa na rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini akimshitakia asiyekuwa muumini humshakizia au kumshauri kuepukana na Mungu.
Na hivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu.
Mkombozi anaweza akamwambia taghuti, ewe mkosefu, na kumlaumu kwa ufisadi, upotevu na kuvunja haki za binadamu na mengineyo, lakini taghuti ametulia tu, wala hajali. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:112).
Huko tumejibu swali la: Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyewajaalia Manabii wawe na maadui, kama inavyoonyesha Aya, kwa nini basi awaadhibu kwa kuwafanyia uadui Mitume?
Na Mola wako anatosha kuwa mwenye kuongoza na mwenye kunusuru.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w)
yakiwa na ahadi kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kumsaidia Mtume wake kutokana na maadui zake; kama alivyomsadia kumuongoza kwenye haki na kuidhihirisha dini yake kuliko dini zote, wajapochukia washirikina.
Na walisema wale ambao wamekufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja?
Qur’an ilishuka kwa vipindi kulingana na haja ya watu. Mwanzo wa kushuka kwake ulikuwa pale Mtume(s.a.w.w)
alipokuwa na miaka arubaini ya umri wake mtukufu. Ukaendelea wahyi kushuka polepole mpaka pale Mtume alipohama kwenda mahali pa hali ya juu akiwa na miaka 63.
Washirikina walijaribu kila mbinu kuwaepusha watu na Qur’an. Wakasema ni vigano vya watu wa kale, lakini hawakuendelea na mbinu hii, kwa sababu ilikuwa ikijipinga yenyewe. Wakatafuta propaganda nyingine, wakasema mbona Qur’an isiteremshwe mara moja, kwani Mungu anahitaji kufikiria, kama wafanyavyo watunzi?
Hata kama ingeliteremka mara moja wasingelikosa la kusema, kama kawaida ya wapinzani, kuwa mbona isingeliteremka kidogo kidogo ili tuweze kuifahamu, kuathirika nayo na kuizowea. Lakini ukweli hujitokeza, hata wakiupinga.
Ndivyo hivyo, ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.
Yaani tumeiteremsha Qur’an kwa mpangilio wa moja baada ya nyingine, ili moyo wake uwe na nguvu ya kuuhifadhi, kufahamu maana yake na kudhibiti hukumu zake.
Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo nzuri, wale watakaokusanywa kifudifudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahali pabaya na ndio wenye kupotea njia sana.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w)
. Watakaoleta mfano na kufufuliwa kifudifudi ni washirikina. Makusudio ya mfano wowote ni kila wanalomtaaradhi nalo Mtume mtukufu.
Katika Aya ya 5, ya Sura hii kwenye Juzuu iliyopita, wanapinga kwa kusema kuwa ni ngano za watu wa kale, katika Aya ya 7, wanasema kwa nini anakula na kutembea sokoni, katika Aya 8, wanasema amerogwa, katika Aya ya 21, iliyo kwenye Juzuu hii, wanasema kwa nini hakuteremshiwa malaika au tumuone Mungu na katika Aya 32 wanasema kwa nini isiteremshwe mara moja.
Baada ya kuyabatilisha madai yao haya ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa anamwambia Mtume wake:‘Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo bora’
Yaani washirikina watakujadili kwa batili na sisi tutakuunga mkono kwa haki iliyo wazi na hoja ambayo itavunja kauli zao na kufedhesha batili zao. Hiyo ni hapa duniani. Ama malipo yao huko akhera, ni kuwa mazabania watawavuta kwenye nyuso zao.
Ambaye atakuwa katika hali hii huyo ndiye muovu wa viumbe vya Mungu na mwenye makazi mabaya zaidi.
Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri. Tukawaambia nendeni kwa watu waliozikadhibisha Ishara zetu, basi tukawaangamiza kabisa.
Kisa cha Musa na Firauni kimekwishatangulia kwenye Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.9 (7:103 – 145). Katika Juz. 16 (20:9), tumezungumzia sababu za kukaririka kisa cha Musa
.
Na watu wa Nuh walipowakadhibisha mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.
Pia kisa cha Nuh kimekwishapita mara kadhaa. Tazama Juz.12 (11:25 – 49).
Na kina Ad na Thamud na watu a Rass.
Rass ni jina la kisima na watu wake ni kaumu ya Shu’ayb. Imetangulia mifano katika Juz. 12 (11:50 – 61 na 84 – 95).
Na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.
Yaani, vile vile tuliangamiza kaumu nyingi zilizokuwa baina ya kina Ad na watu wa Rass, kwa sababu wao waliwakadhibisha manabii na mitume.
Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.
Tuliwaangamiza baada ya ubainifu, onyo, mawaidha ya visa na kupiga mifano, lakini wao waling’ang’ania ukafiri na upotevu. Ikawa malipo yao ni kuangamizwa.
Na kwa hakika wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je hawakua wakiuona? Bali walikuwa hawatarajii kufufuliwa.
Makusudio ya mji hapa ni mji wa kaumu ya Lut kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَلُوطًا آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَت تَّعْمَلُ الْخَبَائِثَ ﴿٧٤﴾
“Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu.” Juz. 17 (21:74).
na pia kauli yake:
فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ ﴿٨٢﴾
“Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini. Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana.” Juz. 12 (11:82).
Maana ni kuwa washirikina walipokuwa kwenye misafara yao wakipitia mji wa Lut na kuona athari ya maangamizi na kubomoka, walitakiwa wapate funzo na waamini utume wa Muhammad, lakini wakapinga na kuwa na inadi, kwa sababu hawana yakini na ufufuo, hisabu na malipo.