2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَقُصُّ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَكْثَرَ الَّذِي هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٧٦﴾
76. Hakika hii Qur’an inawasimulia wana wa Israil mengi wanayohitilafiana.
وَإِنَّهُ لَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾
77. Nayo hakika ni uongofu na rehema kwa waumini.
إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُم بِحُكْمِهِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ ﴿٧٨﴾
78. Hakika Mola wako atakata baina yao hukumu yake naye ni mwenye nguvu, Mjuzi.
فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ إِنَّكَ عَلَى الْحَقِّ الْمُبِينِ ﴿٧٩﴾
79. Basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika wewe uko kwenye haki iliyo wazi.
إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ ﴿٨٠﴾
80. Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma.
وَمَا أَنتَ بِهَادِي الْعُمْيِ عَن ضَلَالَتِهِمْ إِن تُسْمِعُ إِلَّا مَن يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا فَهُم مُّسْلِمُونَ ﴿٨١﴾
81. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao. Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.
وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ ﴿٨٢﴾
82. Na itakapowaangukia, tutawatolea mnyama katika ardhi atakayewasemeza, kwamba watu walikuwa hawana yakini na ishara zetu.
وَيَوْمَ نَحْشُرُ مِن كُلِّ أُمَّةٍ فَوْجًا مِّمَّن يُكَذِّبُ بِآيَاتِنَا فَهُمْ يُوزَعُونَ ﴿٨٣﴾
83. Na siku tutakapowakusanya watu kutoka kila umma, kundi katika wanaokadhibisha ishara zetu. Nao watagawanywa mafungu mafungu.
حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوا قَالَ أَكَذَّبْتُم بِآيَاتِي وَلَمْ تُحِيطُوا بِهَا عِلْمًا أَمَّاذَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨٤﴾
84. Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi si mlizikanusha ishara zangu pasipo kuzijua vyema, au mlikuwa mkifanya nini?
وَوَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِم بِمَا ظَلَمُوا فَهُمْ لَا يَنطِقُونَ ﴿٨٥﴾
85. Na kauli itawaangukia kwa vile walivyodhulumu. Basi wao hawatasema lolote.
QUR’AN INASIMULIA
Aya 76 – 85
MAANA
NEMBO YA ISRAIL NI: ‘TUMESIKIA NA TUMEASI’
Hakika hii Qur’an inawasimulia wana wa Israil mengi wanayohitalifiana.
Qur’an imezungumzia na kuyakariri mambo ya kushangaza ya wana wa Israil. Imezungumzia mambo yanayohusiana nao, nembo yao na yale waliyohitalifiana wakati wa Nabii Musa na baadaye.
Nembo yao wanayoifuata bila ya kuicha ni: ‘Tumesikia na tumekataa,’ kama ilivyoelezwa katika Juz. 1(2:93) na Juz. 5 (4:46). Yaani tumemsikia Mwenyezi Mungu na mtume wake na tumemuasi Mwenyezi Mungu na mitume wote. Waliendelea na nembo hii wakati wa Nabii Musa
mpaka akawashtakia kwa Mola wake na akawapa sifa ya ufuska, akisema kwa masikitiko:
رَبِّ إِنِّي لَا أَمْلِكُ إِلَّا نَفْسِي وَأَخِي فَافْرُقْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ ﴿٢٥﴾
“Ewe Mola wangu! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu; basi tutenge na watu hawa mafasiki.” Juz. 6 (5:25).
Katika Aya nyingine amewapa sifa ya upumbavu:
قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُم مِّن قَبْلُ وَإِيَّايَ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ السُّفَهَاءُ مِنَّا ﴿١٥٥﴾
“Alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeliwaangamiza wao na mimi zamani. Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi?” Juz. 9 (7:155).
Bado wanaendelea na nembo yao hii hadi leo. Mnamo mwaka 1967, Umoja wa Mataifa, unaowakilisha mataifa yote duniani, kuanzia mashariki hadi magharibi, ulipitisha azimio la kuitaka Israil ijiondoe katika ardhi ya Quds.
Jibu
la mjumbe wake lilikuwa ni: “Umoja wa Mataifa ni debe la takataka,” kama ilivyonukuliwa katika magazeti.
Ama yale ambayo walihitilafiana ni walivyoifanyia Tawrat wakati wa Musa mpaka Mwenyezi Mungu akawainulia jabali na kuwatishia kuwaangamiza:
وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ وَرَفَعْنَا فَوْقَكُمُ الطُّورَ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُم بِقُوَّةٍ وَاسْمَعُوا قَالُوا سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا ﴿٩٣﴾
“Na tulipochukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu: Kamateni kwa nguvu haya tuliyowapa na sikilizeni. Wakasema: “Tumesikia na tumekataa” Juz 1(2:93)
.
Walihitalifiana katika mitume waliokuja baada ya Musa
. Miongoni mwao ni Bwana Masih
, kundi moja lilimkadhibisha na kundi moja likataka kumuua; kama ilivyoelezwa katika Juz. 1 (2:87).
Vilevile walihitalifiana kuhusu utume wa Muhammad. Hawakumwamini isipokuwa wachache. Kama wangelikuwa ni watafutaji kweli wa haki wangeliafikiana kuichukua Qur’an ambayo imesimama kwa dalili na hoja juu ya ukweli wake.
Nayo hakika ni uongofu na rehema kwa waumini.
Ni uongofu kwa mwenye kutaka kuongoka na rehema kwa kutumia hukumu zake na mafunzo yake.
Hakika Mola wako atakata baina yao hukumu yake naye ni mwenye nguvu, Mjuzi.
Siku ya Kiyama batili zitaondoka na Mwenyezi Mungu atawahukumu waisrail na wengineo katika yale waliyohitalifiana katika mambo ya dini na dunia.
Basi mtegemee Mwenyezi Mungu.
Mwenye kukimbilia kwake basi yuko katika ngome imara na kizuizi cha nguvu.
Hakika wewe uko kwenye haki iliyo wazi.
Na mwenye haki hajali yanayosemwa juu yake.
Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao.
Jumla hizi zina lengo moja, kwamba kuna sifa zinazoua moyo na kumfanya mtu anga’ang’anie ukafiri, unafiki na upotevu. Zinamfanya yeye na maiti ni sawasawa; hafaidiki na mawaidha wala maonyo. Miongoni mwa sifa kuu hizo ni tamaa na pupa ya chumo na cheo.
Maana haya yamekaririka kwa mifumo mbalimbali; miongoni mwayo ni Aya hizi zifuatazo:-
Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika. Juz. 9 (7:179).
Je, wewe unaweza kuwasikilizisha viziwi ingawa hawafahamu? Je, wewe unaweza kuwaogoza vipofu ingawa hawaoni? Juz.11 (10 42–43).
Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.
Anayekusikiliza na kukutii wewe Muhammad ni yule anayeitafuta haki kwa ajili ya haki, kiasi ambacho akipata dalili na hoja anaiamini na kuifuata. Ama watu wa masilahi na tamaa wanakupa mgongo.
Na itakapowaangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika ardhi atakayewasemeza, kwamba watu walikuwa hawana yakini na ishara zetu.
Kuwaangukia, ni kuwathibitikia. Makusudio ya kauli hapa ni yale aliyoyaahidi Mwenyezi Mungu ya kutokea Kiyama. Makusudio ya watu ni makafiri.
Ama kuhusu mnyama, maneno yamekuwa mengi kumuhusu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutubainishia ni yupi. Pia Hadith kutoka kwa maasum hazikuthibiti; hata kama mapokezi yake yatasihi hatuwezi kuitumia, kwa sababu itakuwa imekuja kwa njia moja (Khabarul-waahid) ambayo inakuwa hoja katika hukumu tanzu, si katika maudhui na misingi ya kiitikadi. Na kusema bila ya elimu ni haramu.
Kwa hiyo hakuna kilichobakia isipokuwa kuchukulia dhahiri ya Aya ambayo inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atakapowafufua watu kwa ajili ya hisabu atamtoa kiumbe kutoka ardhini atakayetangaza kuwa makafiri walizikana dalili wazi wazi na hoja mkataa za kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na mitume wake.
Unaweza kuuliza
: kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubainisha hakika ya mnyama huyu akawaacha watu wameduwaa, mpaka wengine wakasema bila ya elimu na kuwazia tu?
Jibu
: Lengo la kutajwa ni kuwatangaza makafiri na kwamba wao watafufuliwa kesho wakiwa madhalili wamefedheheka mbele ya ushahidi. Lengo hili linapatikana kiasi cha kudokeza tu kuwa kutakuwa na mnyama hata kama jina lake halijulikani wala hakika yake. Aya hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Siku ambayo nyuso zitang’aa na nyuso (nyingine) zitasawijika.” Juz. 4 (3:106).
Na siku tutakapowakusanya watu kutoka kila umma, kundi katika wanaokadhibisha ishara zetu.
Neno ‘katika’ ni la kubainisha sio la baadhi; ni kama mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Jiepusheni na uchafu katika mizimu.” akimaanisha mizimu yote sio baadhi.
Maana ni kuwa katika kila umma kuna wanaosadikisha ishara za Mwenyezi Mungu na wenye kuzikadhibisha. Mwenyezi Mungu (s.w.t) kesho atawakusanya wakadhibishaji wote kwa ajili ya hisabu na malipo. Inajulikana wazi kuwa Mwenyezi Mungu atawakusanya wasadikishaji na wakadhibishaji, lakini lengo la kutajwa wakadhibishaji ni ukemeo na kiaga.
Nao watagawanywa mafungu mafungu.
Malaika watawazuia kuumeni na kushotoni na watawachunga kwenda kwenye kisimamo, kama wanyama wakipelekwa machinjioni.
Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi si mlizikanusha ishara zangu pasipokuzijua vyema, au mlikuwa mkifanya nini?
Watakaposimama wakanushaji mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu atawaambia kwa kuwatahayariza, kwa nini mmewakadhibisha mitume wangu na kuacha kuitikia mwito wao? Ikiwa hamkujua ukweli wao kwanini mlipinga dalili za kuwajulisha na msiziangalie kwa mtazamo wa mwenye kutafuta haki kwa njia ya haki? Ni lipi lilo muhimu zaidi ya hilo?
Maulamaa wameafikiana, kwa kauli moja, kuwa akili inahukumiwa kwa wajibu wa kuangalia muujiza wa mwenye kudai utume. Wakasema: Akili haisamehewi kwa lile ambalo ni wajibu ikiwa inaweza kufanya utafiti na kupata maarifa. Kuna Hadith isemayo: “Mja ataambiwa siku ya Kiyama, je ulijua? Akisema, ndio, Ataulizwa tena, je ulifanya? Akisema sikujua (namna ya kufanya), ataulizwa, je ulijifundisha?
Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyodhulumu.
Ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu itawapata kwa sababu ya kufuru yao na uzembe wao wa kufanya utafiti na kuuliza.
Basi hao hawatasema lolote, kwa sababu ya kukatikiwa na hoja na mshangao wao kutokana na vituko vya siku ya Kiyama.
أَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا اللَّيْلَ لِيَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٨٦﴾
86. Je, hawaoni kwamba tumeufanya usiku ili watulie na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye kuamini.
وَيَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ ﴿٨٧﴾
87. Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni wanyonge.
وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾
88. Na unaiona milima unaidhania imetulia nayo inakwenda mwendo wa mawingu. Ni sanaa ya Mwenyezi Mungu aliyekitengeneza vizuri kila kitu. Hakika yeye ana habari za mnayoyatenda
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ ﴿٨٩﴾
89. Watakaokuja na wema watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mfazaiko wa siku hiyo.
وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَكُبَّتْ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٩٠﴾
90. Na wenye kuja na uovu, basi nyuso zao zitatupwa motoni. Kwani mnalipwa isipokuwa yale mliyoyatenda?
إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَـٰذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٩١﴾
91. Hakika nimeamrishwa kumwabudu tu Mola wa mji huu ambaye ameufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kunyenyekea.
وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴿٩٢﴾
92. Na kwamba nisome Qur’an. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake tu na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji tu.
وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ سَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَتَعْرِفُونَهَا وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾
93. Na Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) Atawaonyesha ishara zake mtazijua. Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.
MILIMA INAKWENDA MWENDO WA MAWINGU
Aya 86 – 93
MAANA
Je, hawaoni kwamba tumeufanya usiku ili watulie na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye kuamini.
Imetangulia pamoja na tafsiri yake katika Juz. 11 (10:67).
Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu.
Parapanda itapuziwa kutangaza Kiyama, nyoyo za viumbe zitashtuka, kutokana na mpuzio huo, kwa hofu kuu; isipokuwa nyoyo za Mitume wasadikishaji, mashahidi na watu wema ambao Mwenyezi Mungu amewavua kwa kusema: ‘Ila amtakaye Mwenyezi Mungu.’ Hao aliowavua amewashiria katika kauli yake:
وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا ﴿٦٩﴾
“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema. Na hao ndio marafiki wema.” Juz. 5 (4:69).
Katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa Parapanda itapulizwa mara tatu; Mpulizo wa fazaa, wa kufa watu wote na ule wa ufufuo. Ufufuo wa kwanza unafahamishwa na Aya tuliyo nayo, wa pili na wa tatu unafahamishwa na Aya isemayo: “Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhini, ila aliyemtaka Mwenyezi Mungu. Kisha itapulizwa mara nyingine. Hapo watainuka wawe wanangojea.”
Na wote watamfikia nao ni wanyonge.
Yaani hao wanaohofia watafufuliwa kwa Mola wao wakiwa dhalili.
MILIMA NA HARAKATI ZA ARDHI
Na unaiona milima unaidhania imetulia nayo inakwenda mwendo wa mawingu.
Maudhui ya Aya hii na iliyo kabla yake ni mamoja, kuzungumzia Kiyama na vishindo vyake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ataing’oa milima kutoka sehemu zake na kuiendesha angani, sawa na yanavyopita mawingu, lakini mtu atafikiria kuwa imetulia.
Hiyo inatokana na kuwa umbo kubwa likitembea kwenye mwelekeo mmoja ulionyooka, basi macho hayaoni harakati zake kutoka na ukubwa wake na umbali wa pembe zake; hasa ikiwa mtazamaji yuko mbalia nalo.
Hapa yanatubainikia makosa ya mwenye kuitumia aya hii katika kuthibitisha harakati ya ardhi. Kuna Aya nyingi zinazofahamisha kuwa makusudio ya kutembea milima, katika Aya hii, kutakuwa siku ya Kiyama; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-
وَيَوْمَ نُسَيِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا ﴿٤٧﴾
“Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi iwazi. Na tutawafufua..” Juz. 15 (18:47).
وَسُيِّرَتِ الْجِبَالُ فَكَانَتْ سَرَابًا ﴿٢٠﴾
“Na ikaendeshwa milima ikawa sarabi.” (78:20).
يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا ﴿٩﴾ وَتَسِيرُ الْجِبَالُ سَيْرًا ﴿١٠﴾
“Siku itakapotikisika mbingu mtikisiko. Na milima iwe inakwenda mwendo.” (52: 9 – 10).
Maneno ya Qur’an ni mamoja, sehemu moja inaifafanulia nyingine.
Ndio! Watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w)
, ambao wana elimu ya Kitabu na Sunna, waliweka wazi kuwa ardhi ina harakati kabla ya Companicus, kwa miaka elfu moja. Imam Ali
anasema katika Nahjul-balagha:Na akaiumba ardhi hewani na akiweka bila ya muhimili na akaiinua bila ya nguzo
(khutba 186). Na mjukuu wake Imam Jafar Sadiq akasema:“Kufahamisha vitu kuzunguka na vilivyomo ndani yake zikiwamo sayari saba, ni kuwa ardhi ina harakati…”
Ni sanaa ya Mwenyezi Mungu aliyekitengeneza vizuri kila kitu
, kuanzia kikubwa sana hadi kidogo sana. Ufundi, mpangilio na nidhamu ni ushahidi mkubwa wa kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na uwezo.
Hakika yeye ana habari za mnayoyatenda.
Ambaye amemuumba mtu kwa ufundi wa hali ya juu, anajua kila akitendacho kiumbe, kiwe cha heri au cha shari na yale yanayompitikia katika nafsi yake:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ ﴿١٦﴾
“Na hakika tumemuumba mtu nasi tunayajua yanayoitia wasiwasi nafsi yake na sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wake wa shingo.” (50:16).
Watakaokuja na wema watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mfazaiko wa siku hiyo. Na wenye kuja na uovu, basi nyuzo zao zitatupwa motoni. Kwani mnalipwa isipokuwa yale mliyoyatenda?
Inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu. Nao hawatadhulumiwa.” Juz. 7 (6:179).
Hakika nimeamrishwa kumwabudu tu Mola wa mji huu ambaye ameufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kunyenyekea.
Makusudio ya mji hapa ni Makka Tukufu. amaeuhusisha kuutaja, pamoja na kuwa yeye ni Mola wa ulimwengu wote, ili kuwabainishia makuraishi neema yake kwao kwa sababu ya mji huo. Walikuwa wakitegemeza ubora wao kuliko waarabu wengine kwa taadhima ya mji huo na utakatifu wake na kuwa na amani, kwa kuharamishwa kuua, kupigana, kuwinda, kukata miti na mengine yanayofahamisha utukufu na cheo chake.
Pamoja na yote haya makuraishi waliabudu masanamu wakaichafua Al-ka’ba kwayo, wakimshirikisha nayo Mola wa mji huu mtukufu ambaye amewalisha kutokana na njaa na akawasalimisha na hofu.
Kauli ya Mtume(s.a.w.w)
: ‘Nimeamrishwa kumwabudu …’ ni kuwapinga makuraishi na kwamba wajibu wao ni kuacha ibada ya ya masanamu ambayo hayamiliki chochote, na wamwabudu Mola wa mji huu ambaye ndiye muumba, mfalme na mwenye amri. Na yeye ni muweza wa kila kitu na akawafadhili makuraishi kwa vitu vingi.
Na kwamba nisome Qur’an.
Makusudio ya kusoma Qur’an hapa ni kutoa mwito wa kuiamini na kwenda na sera yake.
Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake tu na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji tu.
Mtume(s.a.w.
w
)
ametoa mwito wa uongofu. Mwenye kusikia na akatii, basi amejifanyia uzuri mwenyewe na atakuwa amefuata njia ya kheri na uokovu. Na mwenye kupinga basi atakuwa amejifanyia ubaya yeye mwenyewe na kujiingiza kwenye shari na maangamizi. Mtume(s.a.w.w)
hana majukumu ya watu wa upotevu baada ya kuwanasihi na kuwafikishia risala ya Mola wake.
Na Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah)
kwa kuniwafikisha kufikisha risala yake kwa waja wake kama alivyopenda na kutaka.
Atawaonyesha ishara zake mtazijua.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaonyesha dalili za ishara zake kwenye nafsi zao na kwenye pambizo, lakini wakazikana. Ndio akawaambia, leo mnazikana na kesho mtazikubali, ambapo kukubali kwenu hakutawafaa kitu.
Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.
Haya ni makemeo na kiaga cha kupinga kwao na kukana ishara za Mwenyezi Mungu na ubainifu wake.