19
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
Sura Ya Thelathini Na Mbili: Surat As-Sajda. Ina Aya 30. Mwenye Majmaul-bayan anasema: Imeshuka Makka isipokuwa Aya tatu zimeshuka Madina; kuanzia 18 – 20.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
الم ﴿١﴾
1. Alif Laam Miim.
تَنزِيلُ الْكِتَابِ لَا رَيْبَ فِيهِ مِن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾
2. Ni uteremsho wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kinachotoka kwa Mola wa walimwengu wote.
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ بَلْ هُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أَتَاهُم مِّن نَّذِيرٍ مِّن قَبْلِكَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٣﴾
3. Au wanasema amekizua? Bali hicho ni haki itokayo kwa Mola wako, ili uwaonye watu wasiofikiwa na mwonyaji kabla yako, huenda wakaongoka.
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ مَا لَكُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا شَفِيعٍ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ ﴿٤﴾
4. Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita. Kisha akatawala kwenye Arshi. Hamna walii wala mwombezi isipokuwa Yeye. Basi je hamkumbuki?
يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مِنَ السَّمَاءِ إِلَى الْأَرْضِ ثُمَّ يَعْرُجُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٥﴾
5. Hulipanga jambo kutoka mbinguni hadi ardhini, kisha linapanda kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyohisabu.
ذَٰلِكَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٦﴾
6. Huyo ndiye Mjuzi wa mambo ya ghaibu na ya dhahiri, Mwenye uwezo, Mwenye kurehemu.
الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ ﴿٧﴾
7. Ambaye ametengenza vizuri umbo la kila kitu. Na akaanzisha umbo la mtu kwa udongo.
ثُمَّ جَعَلَ نَسْلَهُ مِن سُلَالَةٍ مِّن مَّاءٍ مَّهِينٍ ﴿٨﴾
8. Kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji hafifu.
ثُمَّ سَوَّاهُ وَنَفَخَ فِيهِ مِن رُّوحِهِ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٩﴾
9. Kisha akamlinganisha sawa na akampulizia roho yake. Na amewajaalia kusikia na kuona na nyoyo. Ni uchache mnavyoshukuru.
AMETENGENEZA VIZURI UMBO LA KILA KITU
Aya 1 – 9
MAANA
Alif Laam Miim.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Ni uteremsho wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kinachotoka kwa Mola wa walimwengu wote.
Ushahidi wa hilo tumeuleza kwenye Aya kadhaa; kama vile Juz. 1 ( 2:23 – 25), Juz. 5 (4:80 – 82) na Juz. 18 (24:55 – 57).
Au wanasema amekizua? Bali hicho ni haki itokayo kwa Mola wako, ili uwaonye watu wasiofikiwa na mwonyaji kabla yako, huenda wakaongoka.
Wapenda anasa wanaojitia kwenye upotevu, katika vigogo wa kikuraishi, walisema: “Qur’an ni utungo wa Muhammad.” Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema, kuwarudi, kuwa hapana bali ni wahyi wa Mwenyezi Mungu na Muhammad amewajia na yale ambayo hajawaletea yeyote kabla yake wala hatawaletea yeyote baada yake.
Amewajia na kheri ya dunia na akhera akawakataza dhulma na ufisadi mlio nao, ili mpate mawaidha na muache kabla hayajawafikia majanga. Ilitakiwa mumshukuru Muhammad kwa fadhila hii badala ya kumpangia njama za kiuadui na kumfanya ni mwongo mzushi.
Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita. Kisha akatawala kwenye arshi. Hamna walii wala mwombezi isipokuwa Yeye. Basi je hamkumbuki?
Siku sita ni kinaya cha mikupuo au mara. Makusdio ya Arshi ni utawala. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:54), Juz. 11 (10:3) na Juz. 19 (25:59). Katika Juz. 8 (54:56) tumeeleza kauli zilizosemwa kuhusu siku sita na rai yetu.
Hulipanga jambo kutoka mbinguni hadi ardhini, kisha linapanda kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyohisabu.
Makusudio ya kupanga jambo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimwengu, kila kiumbe akakipa sifa kwa namna inavyotaka hekima yake. Akamwajibishia kiumbe ambaye amempa uweza na utambuzi kulazimiana na njia aliyomwongoza.
Makusudio ya ‘kupanda kwake katika siku’ ni kuwa matendo ya viumbe yatakwenda kwake Siku ya Kiyama. Miaka elfu ni kinaya cha kurefuka zama.
Maana ni kuwa viumbe wote wamezungukwa na mipangilio ya Mungu na ulinzi wake. Yeye ndiye aliyewaleta na akawapangilia vizuri: “ambaye amekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza” Juz. 16 (20:50). Ni Yeye atakayekimaliza na kukirudisha, na matendo yatapelekwa kwake siku ambayo itakuwa ndefu na nzito kwa waasi na wakosefu.
Huyo ndiye Mjuzi wa mambo ya ghaibu na ya dhahiri, Mwenye uwezo Mwenye kurehemu.
Muumba wa kila kitu na msimamizi wa kila kitu. Ni Mjuzi wa ya lililokuwa na litakalokuwa, liwe dogo au kubwa, la dhahiri au la kujificha. Ni Mwenye nguvu kwa uweza wake na ufalme wake na Mwenye huruma kwa viumbe wake na waja wake.
Ambaye ametengenza vizuri umbo la kila kitu.
Kila kiumbe kilichopatikana kwa nidhamu kamili basi ni kizuri na kimepangika, kikifahamisha uwezo wa mtengenezaji na utukufu wake. Hakuna kitu chochote kilichopo ila utaona nidhamu na uwiano unaofahamisha kuweko mjuzi mwenye hekima:
مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ ﴿٣﴾
“Hutaona tofauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa rehema. Hebu rudisha jicho, je unaona kosa lolote” (67:3).
Na akaanzisha umbo la mtu kwa udongo.
Makusudio ya mtu hapa ni baba wa watu, Adam.
Kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji hafifu ambayo ni manii. Kisha akamlimganisha sawa katika umbile zuri na akampulizia roho yake.
Hiki ni kinaya cha uhai. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:2) na Juz. 18 (23:12 – 14).
Amewajaalia kusikia na kuona na nyoyo. Ni uchache mnavyoshukuru.
Neema ya ubainifu inatokana na neema ya usikizi uoni na utambuzi. Ama matamanio ya chakula ni kwa ajili ya kuishi na matamanio ya jinsia ni kwa ajli ya kubakia. Hakuna matamanio yoyote kwa mtu isipokuwa yana faida na hekima.
وَقَالُوا أَإِذَا ضَلَلْنَا فِي الْأَرْضِ أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ بَلْ هُم بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ كَافِرُونَ ﴿١٠﴾
10. Na husema: Ati tutakapopotea ardhini, kweli tutakuwa kwenye umbo jipya? Bali wao wanakanusha kukutana na Mola wao.
قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ ﴿١١﴾
11. Sema, atawafisha malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu.
وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الْمُجْرِمُونَ نَاكِسُو رُءُوسِهِمْ عِندَ رَبِّهِمْ رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ ﴿١٢﴾
12. Na ungeliwaona wakosefu wanavyoinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao. Mola wetu! Tumeona na tumesikia, turejeshe tutatenda mema, kwani hakika sisi tuna yakini.
وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿١٣﴾
13. Na lau tungelitaka tungeipa kila nafsi muongozo wake. Lakini imehakikika kauli kutoka kwangu: Kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa wote majini na watu.
فَذُوقُوا بِمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا إِنَّا نَسِينَاكُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٤﴾
14. Basi onjeni kwa sababu ya kusahau mkutano wa siku yenu hii, hakika sisi tumewasahau. Na onjeni adhabu yenye kudumu kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
WAKOSEFU WANAINAMISHA VICHWA VYAO.
Aya 10-14
MAANA
Na husema: Ati tutakapopotea ardhini, kweli tutakuwa kwenye umbo jipya?”
Hii ni sawa na kauli yao:
أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ ﴿٥﴾
“Ati tutakapokuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya?” Juz.13(13:5)
Bali wao wanakanusha kukutana na Mola wao.
Unaweza kuuliza
: Washirikina walitangaza waziwazi kufuru yao ya kukutana na Mwenyezi Mungu waziwazi. Sasa kuna haja gani ya kusema wanakanusha kukutana na Mola wao? Si ni sawa na kumwambia aliyetangaza ukafiri kuwa wewe ni kafiri?
Jibu
: makusudio ni kuwa wao hawakuipinga akhera kwa ujuzi, bali ni kwa ujinga na kuiga; sawa na kumwambia aliyetangaza ukafiri: wewe ni mjinga.
Sema, atawafisha malaika wa mauti aliyewakilishwa kwenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu.
Yaani, ewe Muhammad! Waambie waliokufuru kuwa nyinyi mtakufa tu, hilo halina shaka. Baada ya mauti hakika itawafunukia na mtajua kuwa bila shaka saa ya Kiyama itakuja na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua walio katika makaburi.
Na ungeliwaona wakosefu wanavyoinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao.
Walipinga ufufuo na wakawafanyia maskhara waliouamini, waliowapa mwito wake na kuwahadhari na mwisho mbaya. Watapofufuliwa na kusimama mbele ya Mola wao kwa ajili ya hisabu watainamisha vichwa vyao kwa kuona haya na majuto na kusema:
Mola wetu! Tumeona na tumesikia, turejeshe tutatenda mema, kwani hakika sisi tuna yakini.
Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:27) na Juz. 18 (23:99 – 100).
Na lau tungelitaka tungeipa kila nafsi muongozo wake.
Razi anasema: “ Hii ni wazi kuwa madhehebu yetu yako sahihi pale tunaposema: Mwenyezi Mungu hakutaka imani kutoka kwa kafiri na hakutaka kwake isipokuwa kufuru.”
Nasi tunamwambia Razi: Ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyetaka kufuru kwa kafiri, na hakuna anayerudisha matakwa yake, basi kwa nini atamwadhibu. Vipi na Yeye ndiye aliyesema: “Wala hatukuwadhulumu, bali wao ndio waliokuwa madhalimu” (43:76).
Usahihi ni kuwa makusudio ya matakwa ya Mwenyezi Mungu hapa ni matakwa ya kiuumbaji ambayo ni kusema ‘kuwa.’
Yaani lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwalazimisha uongofu wangeliongoka. Na kama angelifanya hivyo, basi kusingekuwa na thawabu wala adhabu. Hayo tumeyaeleza mara kadhaa. Tazama Juz. 6 (5:49 – 50).
Lakini imehakikika kauli kutoka kwangu: Kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa wote majini na watu.
Imehakikika kauli kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba ataijaza Jahannam kwa wafisadi na wale walioasi kwa hiyari na matakwa yao wenyewe. Ama wale ambao walimwitikia Mola wao wana maghufira na malipo makubwa. Kuna Hadith Qudsi inayosema: “Nimeiumba Pepo kwa anayenitii hata kama ni mtumwa Muhabeshi; na moto kwa anayeniasi hata kama ni bwana wa kikuraishi.”
Basi onjeni kwa sababu ya kusahau mkutano wa siku yenu hii, hakika sisi tumewasahau. Na onjeni adhabu yenye kudumu kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
Hakuna yoyote aliyefuata matamanio yake na hawa yake ila atamsahau Mwenyezi Mungu na hisabu na ataikufuru haki na dhamiri. Na kesho malaika wa adhabu watamwambia mkosaji huyu: umelewa utamu wa dunia basi leo onja uchungu wa akhera. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:51) na Juz. 10 (9:67).
إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ﴿١٥﴾
15. Hakika wanaoziamni Aya zetu ni wale tu ambao wanapokumbushwa hizo huanguka kusujudu na humsabihi kwa kumsifu Mola wao, nao hawatakabari.
تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾
16. Mbavu zao zinaachana na vitanda kumwomba Mola wao kwa hofu na tumaini, na hutoa katika yale tuliyowaruzuku.
فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٧﴾
17. Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayofurahisha maisha. Ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
أَفَمَن كَانَ مُؤْمِنًا كَمَن كَانَ فَاسِقًا لَّا يَسْتَوُونَ ﴿١٨﴾
18. Je, aliye mumin ni sawa na aliye fasiki? Hawawi sawa.
أَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ جَنَّاتُ الْمَأْوَىٰ نُزُلًا بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٩﴾
19. Ama wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na bustani za makao. Ndipo pa kufikia kwa waliyokuwa wakiyatenda.
وَأَمَّا الَّذِينَ فَسَقُوا فَمَأْوَاهُمُ النَّارُ كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا أُعِيدُوا فِيهَا وَقِيلَ لَهُمْ ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ ﴿٢٠﴾
20. Na ama wale ambao wamefanya ufuska, basi makazi yao ni motoni; kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya moto ambayo mlikuwa mkiikadhibisha.
وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَىٰ دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢١﴾
21. Na kwa hakika tutawaonjesha adhabu hafifu kabla ya adhabu kubwa, labda watarejea.
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ ثُمَّ أَعْرَضَ عَنْهَا إِنَّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ مُنتَقِمُونَ ﴿٢٢﴾
22. Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa kwa ishara za Mola wake kisha akazikataa. Hakika sisi ni wenye kuwachukulia kisasi wakosefu.
MUUMIN ANAWEZA KUWA SAWA NA FASIKI?
Aya 15 – 22
MAANA
Hakika wanaoziamni Aya zetu ni wale tu ambao wanapokumbushwa hizo huanguka kusujudu na humsabihi kwa kumsifu Mola wao.
Makusudio ya waumini hapa ni wale wanaoijua haki na kuitumia na kujitolea muhanga kwa ajaili yake; wanamwabudu Mwenyezi Mungu usiku na mchana kwa kumtegemea Yeye na kumfanyia ikhlasi peke yake, asiyekuwa na mshirika. Ama tasbihi, rukui na sujudi kwa msukumo wa chumo na kibiashara kwa dini, yote hayo ni unafiki sio ibada na ni uzandiki sio imani.
Nao hawatakabari;
yaani waumini wanaikaribisha haki na kuacha masilahi yao binafsi kwa ajili ya haki; kwa sabu hiyo ndiyo dini yao na masilahi yao.
Ni wajibu kusujudi kwa mwenye kuisoma Aya hii au kuisikiliza na imesemekana hata mwenye kuisikia pia bila ya kukusudia.
Mbavu zao zinaachana na vitanda kumwomba Mola wao kwa hofu na tumaini.
Vitanda ni kinaya cha usingizi. Tukiunganisha Aya hii na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu.” Juz. 18 (24:37), maana yatakuwa: Hakika waumini haiwashughulishi biashara wala usingizi kuacha ibada ya Mwenyezi Mungu, jambo ambalo linaelezea kuhofia kwao adhabu yake na kutumai kwao thawabu zake.
Ibada hiyo ndiyo aliyoikusudia Mwenyezi Mungu aliposema: “Na usi- mamishe Swala, hakika Swala inakataza machafu na maovu.” Kuna Hadith isemayo: Kisimamo cha mja kinamkurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kinamkataza dhambi, kinafuta maovu na kufukuza ugonjwa mwilini.” Ama Swala ya kibiashara huwa inaamrisha uovu na ubaya. Kwa sababu ubaya unaelekeza kwenye mfano wake na vile vile wema.
Na hutoa katika yale tuliyowaruzuku.
Wamemwabudu Mwenyezi Mungu kwa nyoyo, miili na mali.
Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayofurahisha maisha. Ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
Makusudio ya nafsi ni nafsi yoyote, iliyokuwa na itakayokuwa katika ardhi au mbingu. Maana ni kuwa hakuna yeyote anayejua uhakika wa thawabu za kufurahisha ambazo Mwenyezi Mungu amewaandalia waumini, wenye kufanya matendo. Mtume anasema katika Hadith: “Mwenyezi Mungu anasema: “Nimewaandalia waja wangu wema ambayo hakuna jicho liliyaona wala sikio lililoyoyasikia, wala moyo uliyoyawazia.”
Je, aliye mumin ni sawa na aliye fasiki? Hawawi sawa.
Tafsri nyingi; ikiwemo Jamiu ya Tabariy, Bahrul-muhit ya Andalusi, Ruhul-bayan ya Haqi, zimesema kuwa Aya hii ilishuka Madina kuhusiana na Ali bin Abi Twalib na Walid bin U’qba bin Abi Mu’it. Tutanukuu yale ya Tabariy: “Kulipita maneno baina ya Walid na Ali. Walid akasema: “Mimi nina ulimi mpana kuliko wewe, nina meno makali kuliko wewe na ninafaa zaidi kwenye jeshi kuliko wewe.” Ali akamwambia, nyamaza wewe ni fasiki, ndipo ikashuka: ‘Je, aliye mumin ni sawa na aliye fasiki? Hawawi sawa.
Hapana wallah hawawi sawa duniani wala kwenye mauti na akhera pia.
Ama wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na bustani za makao. Ndipo pa kufikia kwa waliyokuwa wakiyatenda.
Hii ni kutofautisha baina ya mumin mwenye takua na kafiri muovu; ni sawa na kutofautisha wema na uovu, heri na shari na Pepo iliyoandaliwa wenye takua na moto ulioandaliwa wakosefu.
Na ama wale ambao wamefanya ufuska, basi makazi yao ni motoni; kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya moto ambayo mlikuwa mkiikadhibisha.
Waumini watapata Pepo zenye neema na mafasiki watapata moto unaowaka. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:22).
Na kwa hakika tutawaonjesha adhabu hafifu kabla ya adhabu kubwa, labda watarejea.
Makusudio ya adhabu hafifu ni adhabu ya duniani; kama vile kahati, balaa n.k. Anawaonya kwayo na kwa nguvu za hoja, wale walioghafilika na wanaojishughulisha na mambo ya batili na kuiacha haki, ili waonyeke na wapate mawaidha.
Vinginevyo watafikiwa na adhabu kubwa: “Moto wa Jahanam hali ya kudumu humo. Ni tosha yao. Na Mwenyezi Mungu amewalaani. Na wana wao adhabu ya kudumu.” Juz. 10 (9:68).
Kwa hakika ilivyo ni kuwa viongozi na watawala ndio chimbuko la kwanza la ufisadi na uovu. Kuna Hadith zinayosema: “Watawala wakiwa waongo huzuiliwa mvua, na mtawala akiwa jeuri dola inakuwa dhalili.”
Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa kwa ishara za Mola wake kisha akazikataa. Hakika sisi ni wenye kuwachukulia kisasi wakosefu.
Mwenye kupata mawaidha kisha asiwaidhike nayo basi huyo ni katika wakosefu wakubwa. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaonya kwa ulimi wa mitume wake na kwa madhara na shida, lakini nyoyo zao zikasusuwaa na wakaendelea na dhulma na ufisadi. Ndio Mwenyezi Mungu akawalipiza kisasi na Yeye ni mwenye nguvu Mwenye kulipiza kisasi.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَلَا تَكُن فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَائِهِ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٢٣﴾
23. Hakika tulimpa Musa Kitabu basi usiwe na shaka ya kukipokea kwake, na tukakifanya ni mwongozo kwa wana wa Israil.
وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ ﴿٢٤﴾
24. Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu waliposubiri, na wakawa na yakini na ishara zetu.
إِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٢٥﴾
25. Hakika Mola wako ndiye atakayefafanua baina yao Siku ya Kiyama katika lile walilohitalifiana.
أَوَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ أَفَلَا يَسْمَعُونَ ﴿٢٦﴾
26. Je, haikuwabainikia, ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao nao wanatembea katika maskani zao. Hakika katika hayo kuna ishara, basi je, hawasikii.
أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَسُوقُ الْمَاءَ إِلَى الْأَرْضِ الْجُرُزِ فَنُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا تَأْكُلُ مِنْهُ أَنْعَامُهُمْ وَأَنفُسُهُمْ أَفَلَا يُبْصِرُونَ ﴿٢٧﴾
27. Je, hawaoni kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kame, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayokula wanyama wao. Je, hawapati busara.
وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْفَتْحُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٨﴾
28. Na wanasema: Ushindi huu utatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
قُلْ يَوْمَ الْفَتْحِ لَا يَنفَعُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِيمَانُهُمْ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ ﴿٢٩﴾
29. Sema: Siku ya ushindi wale ambao wamekufuru haitafaa imani yao, wala hawatapewa muda.
فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَانتَظِرْ إِنَّهُم مُّنتَظِرُونَ ﴿٣٠﴾
30. Basi achana nao na ungoje; hakika wao wanangoja.
USIWE NA SHAKA YA KUIPOKEA KWAKE
Aya 23 – 30
MAANA
Hakika tulimpa Musa Kitabu basi usiwe na shaka ya kukipokea kwake, na tukakifanya ni mwongozo kwa wana wa Israil.
Wafasiri wengi wamesema kuwa ‘Kwake’ inarudi kwa Musa; kwa maana ya kuwa Muhammad atakutana na Musa usiku wa Miraji. Ilivyo hasa ni kuwa dhamiri hiyo inarudia kwenye Qur’an; kwa maana ya kuwa, ewe Muhammad! Tumekutermshia Qur’an kama tulivyomteremshia Musa Tawrat. Wala haitakikani kutia shaka katika hilo wewe wala mwingine.
Kuhusu kukatazwa Mtume kutia shaka tumekuelezea mara nyingi. Tazama Juz. 3 (3:59-63).
Na tukawafanya miongoni mwao maimamu wanaoongoza kwa amri yetu waliposubiri, na wakawa na yakini na ishara zetu.
Makusudio ya maimamu hapa ni mitume wa Kiisrail; kama vile Musa, na Isa ambaye nasaba ya upande wa mama yake inafikia kwa Daud. Kila Mtume wa kiisraili alipata aina kwa aina ya adhabu na mateso; bali waisrail waliwaua manabii wao kadhaa:
وَيَقْتُلُونَ النَّبِيِّينَ بِغَيْرِ الْحَقِّ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ ﴿٦١﴾
“Na wakiwaua Manabii pasipo haki. Basi haya ni kwa sababu ya kuasi kwao na kupituka mipaka.” Juz. 1 (2:61).
Pamoja na yote hayo, waliweza kuvumilia wakawa na subira na wakaendelea kutekeleza risala yao. Kwa hiyo nawe Muhammad vumilia maudhui ya watu wako na uendelee na risala yako.
Hakika Mola wako ndiye atakayefafanua baina yao Siku ya Kiyama katika lile walilohitalifiana.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:113), Juz. 11(10:93) na Juz. 14 (16:124).
Je, haikuwabainikia, ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao nao wanatembea katika maskani zao. Hakika katika hayo kuna Ishara, basi je, hawasikii.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20).
Je, hawaoni kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kame, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayokula wanyama wao.
Je, hawapati busara kwa jinsi Mwenyezi Mungu alivyoipa uhai ardhi baada ya kufa kwake na akaotesha humo kila aina za mimea wanayokula watu na wanyama? Kama hivyo atawafufua wafu baada ya kuwa ni mchanga na mifupa
Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; kama Juz. 17: (22:5).
Na wanasema: ushindi huu utatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
Aya hii ni mfano wa ile isemayo: “Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?” Juz. 17 (21:38). Kwa sababu makusudio ya ushindi hapa ni siku itakayohukumiwa kwa haki. Hilo linatiliwa nguvu na kauli inayofuatia:
Sema: Siku ya ushindi wale ambao wamekufuru,
na wakaifanyia inadi haki katika maisha ya dunia,haitafaa imani yao
huko akhera wakati watakapoiona adhabu. Kwa sababu imani hiyo itakuwa ni kuukimbia moto sio imani ya kweli na yakini.
Wala hawatapewa muda.
Mwenyezi Mungu hawezi kuwapa muda siku ya Kiyama, kwa sababu ali- wapa muda mrefu duniani, lakini hawakuitumia fursa hiyo.
Basi achana nao na ungoje; hakika wao wanangoja.
Wao wanangoja ufikwe na majanga, basi achana nao na ungoje kidogo tu, utaona hukumu ya Mwenyezi Mungu kwako na kwao. Yeye atakunusuru na atawafedhehsha wao:
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾
“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.” Juz. 10 (9:33).