4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَىٰ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١٤﴾
14. Na alipofikilia kukomaa kwake na akastawi, tulimpa hukmu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
وَدَخَلَ الْمَدِينَةَ عَلَىٰ حِينِ غَفْلَةٍ مِّنْ أَهْلِهَا فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ قَالَ هَـٰذَا مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ عَدُوٌّ مُّضِلٌّ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾
15. Na akaingia mjini wakati wenyeji wake wako kwenye mghafala. Akakuta humo watu wawili wanapigana – huyu ni katika kundi lake na huyu ni katika adui zake. Yule aliye katika kundi lake alimtaka msaada dhidi ya yule aliye katika adui zake. Musa akampiga, akammaliza. Akasema: Hiki ni kitendo cha shetani; hakika yeye ni adui mpotezaji dhahiri.
قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿١٦﴾
16. Akasema: Mola wangu! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
قَالَ رَبِّ بِمَا أَنْعَمْتَ عَلَيَّ فَلَنْ أَكُونَ ظَهِيرًا لِّلْمُجْرِمِينَ ﴿١٧﴾
17. Akasema: Mola wangu! Kwa ulivyonineemesha, sitakuwa msaidizi wa wakosefu.
فَأَصْبَحَ فِي الْمَدِينَةِ خَائِفًا يَتَرَقَّبُ فَإِذَا الَّذِي اسْتَنصَرَهُ بِالْأَمْسِ يَسْتَصْرِخُهُ قَالَ لَهُ مُوسَىٰ إِنَّكَ لَغَوِيٌّ مُّبِينٌ ﴿١٨﴾
18. Akapambaukia mjini akiwa na hofu na hadhari, mara yule aliyemtaka msaada jana anampigia kelele. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mpotevu dhahiri.
فَلَمَّا أَنْ أَرَادَ أَن يَبْطِشَ بِالَّذِي هُوَ عَدُوٌّ لَّهُمَا قَالَ يَا مُوسَىٰ أَتُرِيدُ أَن تَقْتُلَنِي كَمَا قَتَلْتَ نَفْسًا بِالْأَمْسِ إِن تُرِيدُ إِلَّا أَن تَكُونَ جَبَّارًا فِي الْأَرْضِ وَمَا تُرِيدُ أَن تَكُونَ مِنَ الْمُصْلِحِينَ ﴿١٩﴾
19. Basi Musa alipotaka kumkamata kwa nguvu, yule aliye adui yao akasema: Ewe Musa! Unataka kuniua, kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki ila kuwa jabari katika ardhi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wema.
ALIPOFIKIA KUKOMAA
Aya 14 – 19
MAANA
Na alipofikilia kukomaa kwake na akastawi, tulimpa hukmu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 12 (12:22). Kule imekuja kwa wasifu wa Yusuf na hapa ni wa Musa.
Na akaingia mjini wakati wenyeji wake wako kwenye mghafala. Akakuta humo watu wawili wanapigana – huyu ni katika kundi lake na huyu ni katika adui zake. Yule aliye katika kundi lake alimtaka msaada dhidi ya yule aliye katika adui zake. Musa akampiga, akam- maliza.
Makusudio ya mji hapa ni mji wa Misri.
Siku moja Musa aliingia mitaani bila ya kujulikana na yeyote. Akawaona watu wawili wanagombana na kupigana – mmoja ni Mkibti katika wafuasi wa Firauni na mwingine ni Mwisrail katika jamaa za Musa. Kwa ujumla Wakibti walikuwa wakiwakandamiza waisrail na wakiwahisabu ni watumishi na watumwa wao.
Basi yule Mwisrail akamtaka msaada Musa. Musa naye akampiga ngumi au fimbo kwa kukusudia kumtia adabu na kukinga dhulma, si kwa kukusudia kuua na yule akaanguka ni maiti. Huku kunaitwa kuua kimakosa.
Akasema: Hiki ni kitendo cha shetani; hakika yeye ni adui mpotezaji dhahiri.
Anakusudia kile kitendo cha kugombana wale wawili sio pigo alilopiga Musa. Maana ni kuwa mapigano baina ya wawili, chanzo chake ni wasi-wasi wa shetani na hadaa yake ya kuingiza kwenye uasi na madhambi.
Akasema: Mola wangu! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Mitume na mawili wanajiona mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wapungufu. Hiyo ni katika aina ya kunyenyekea na dua. Hilo halifahamishi kuweko dhambi wala upungufu.
Kwa sababu anayemjua Mwenyezi Mungu kisawasawa huwa anaituhumu nafsi yake kuwa na upungufu wa kumtii Mwenyezi Mungu na kumwabudu.
Ndio maana humwomba msamaha wa dhambi. Wa kale walisema: “Uovu wa watu wema ni wema wa waovu.” Tazama tuliyoyaeleza kwa anuani ya ‘Toba na maumbile’ katika Juz. 4 (4:17-18).
Akasema: Mola wangu! Kwa ulivyonineemesha, sitakuwa msaidizi wa wakosefu.
Musa alimuomba msamaha Mola wake na akamwahidi kuwa atawapiga vita mataghuti na wakosefu; kama vile Firauni na jeshi lake na kumsaidia kila mumin.
Akapambaukia mjini akiwa na hofu na hadhari.
Musa alihofia kuuawa kwa sababu ya Mkibti na kutarajia shari kutoka kwa Firauni na watu wake.
Wakati akiwa katika hali hiyo, mara yule aliyemtaka msaada jana anampigia kelele. Anampigia kelele za kumtaka msaaada. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mpotevu dhahiri.
Wewe kazi yako ni kugombana na Wakibti na kutusababishia matatizo. Hebu chunga upotevu wako!
Basi Musa alipotaka kumkamata kwa nguvu yule aliye adui yao,
Musa alitaka kumkamata Mkibti, kwa sababu wakibti ndio waliokuwa wakiwachokoza waisrail na kuwachukulia kuwa ni watumwa wao, kama tulivyoashiria mwanzo. Mkibti alidhani kuwa Musa anataka kumuua, kwa hiyo akasema:
Ewe Musa! Unataka kuniua, kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki ila kuwa jabari katika ardhi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wema.
Jana ulimuua mtu na leo unataka kuniua mimi, je wewe ni mbabe au mtu mwema? Hii inaashiria kwamba Musa alikuwa ni katika watu wema mwenye tabia nzuri na kwamba kuua hakuendani na tabia yake.
وَجَاءَ رَجُلٌ مِّنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ يَسْعَىٰ قَالَ يَا مُوسَىٰ إِنَّ الْمَلَأَ يَأْتَمِرُونَ بِكَ لِيَقْتُلُوكَ فَاخْرُجْ إِنِّي لَكَ مِنَ النَّاصِحِينَ ﴿٢٠﴾
20. Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akaipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanapanga kukuua. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanaokupa nasaha.
فَخَرَجَ مِنْهَا خَائِفًا يَتَرَقَّبُ قَالَ رَبِّ نَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢١﴾
21. Basi akatoka mjini akiwa na hofu na hadhari. Akasema: Mola wangu! Niokoe na watu madhalimu.
وَلَمَّا تَوَجَّهَ تِلْقَاءَ مَدْيَنَ قَالَ عَسَىٰ رَبِّي أَن يَهْدِيَنِي سَوَاءَ السَّبِيلِ ﴿٢٢﴾
22. Alipoelekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu akaniongoza njia iliyo sawa.
وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِّنَ النَّاسِ يَسْقُونَ وَوَجَدَ مِن دُونِهِمُ امْرَأَتَيْنِ تَذُودَانِ قَالَ مَا خَطْبُكُمَا قَالَتَا لَا نَسْقِي حَتَّىٰ يُصْدِرَ الرِّعَاءُ وَأَبُونَا شَيْخٌ كَبِيرٌ ﴿٢٣﴾
23. Alipoyafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wakinywesha (wanyama wao), na akakuta nyuma yao wanawake wawili wanazuia (wanyama wao). Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi mpaka wamalize hao wachunga na baba yetu ni mzee sana.
فَسَقَىٰ لَهُمَا ثُمَّ تَوَلَّىٰ إِلَى الظِّلِّ فَقَالَ رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ ﴿٢٤﴾
24. Basi akawanyweshea kisha akarudi kivulini na akasema: Mola wangu! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayoniteremshia.
فَجَاءَتْهُ إِحْدَاهُمَا تَمْشِي عَلَى اسْتِحْيَاءٍ قَالَتْ إِنَّ أَبِي يَدْعُوكَ لِيَجْزِيَكَ أَجْرَ مَا سَقَيْتَ لَنَا فَلَمَّا جَاءَهُ وَقَصَّ عَلَيْهِ الْقَصَصَ قَالَ لَا تَخَفْ نَجَوْتَ مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٥﴾
25. Basi mmoja wa wale wanawake wawili akamjia naye anatembea akiona haya. Akasema: Baba yangu anakuita akulipe ujira wa kutunyweshea.Basi alipomjia na kumsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka na watu madhalimu.
قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ ﴿٢٦﴾
26. Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumwajiri ni mwenye nguvu na mwaminifu.
قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾
27. Akasema: Mimi ninataka kukuoza mmoja wa mabinti zangu hawa wawili kwa kunifanyia ajira ya miaka minane na kama ukitimiza kumi hiyari yako. Mimi sitaki kukutaabisha. Inshaallah utanikuta miongoni mwa watu wema.
قَالَ ذَٰلِكَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ أَيَّمَا الْأَجَلَيْنِ قَضَيْتُ فَلَا عُدْوَانَ عَلَيَّ وَاللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٢٨﴾
28. Akasema: Hayo yamekwishakuwa baina yangu na yako. Muda wowote kati ya miwili nitakoumaliza nisifanyiwe ubaya na Mwenyezi Mungu ni wakili juu ya haya tunayoyasema.
NJAMA
Aya 20 – 28
MAANA
Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akaipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanapanga kukuua. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanaokupa nasaha.
Firauni na wapambe wake walijua yaliyotokea baina ya Musa na Mkibti wa kwanza aliyemuua kimakosa na wa pili aliyemwambia unataka kuniua. Kwa hiyo wakashauriana kuhusu mambo ya Musa na kuazimia kumuua. Mmoja wa waumini alipojua hilo alikimbia kwa Musa kumpa habari na akamshauri awakimbie madhalimu.
Wafasiri wengi wamesema kuwa mumin huyu ni yule aliyeashiriwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
“Na akasema mumin aliyekuwa mmoja katika watu wa Firauni aliyeficha imani yake: Mtamuua mtu kwa kusema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu naye amewajia na hoja zilizo wazi?” (40:28).
Basi akatoka mjini akiwa na hofu na hadhari. Akasema: Mola wangu! Niokoe na watu madhalimu.
Musa alitoka mjini bila ya maandalizi yoyote; hana chakula wala maji, au yeyote wa kuongozana naye. Alitoka kwa hadhari akihofia asionekane na chinjachinja wa Firauni. Zaidi ya hayo alikuwa hajui anakwenda wapi? Basi akamkimbilia Mola wake, akamwachia Yeye mambo yake na akamwomba kuongoka na kuokoka na Firauni na watu wake.
Alipoelekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu akaniongoza njia iliyo sawa.
Musa alitembea bila ya kujua anakwenda wapi, lakini ana yakini kuwa Mola wake atamwongoza njia iliyo sawa ambayo itampelekea kuokoka na kufaulu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamshika mkono na kumwelekeza Madyana, mji wa Shua’yb, ambao baina yake na Misri pana masafa ya mwendo wa siku nane katika jangwa pana sana.
Basi Musa akakata mbuga kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa akila mimea ya ardhini. Jana alikuwa ikulu ya Firauni akistarehe. Mimea ya ardhi na hofu ni bora mara elfu kwa wenye ikhlasi kuliko starehe pamoja na dhulma; kama alivyosema Imam Husein
: “Wallahi! Sioni mauti ila ni wema; na sioni kuishi pamoja na madhalimu ila ni uovu.”
Alipoyafikia maji ya Madayana alikuta umati wa watu wakinywesha (wanyama wao) na akakuta nyuma yao wanawake wawili wanazuia (wanyama wao). Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi mpaka wamalize hao wachunga na baba yetu ni mzee sana.
Mwendo wa Musa uliishia kwenye kisima. Akakuta kundi la watu waki-wanywesha maji wanyama wao na akawaona wanawake wawili pembeni wakiwa na kondoo wao wanataka kunywa maji, lakini wao wanawazuia.
Musa akashtuliwa na hali hii, akawauliza, kwa nini mnawazuia nao wana kiu? Wakasema sisi ni wanawake dhaifu, hatuwezi kusukumana na wanaume. Tunangoja mpaka wamalize ndio nasi tupate nafasi, na baba yetu ni mzee sana, hawezi kuja kuchota maji. Nafsi ya Musa ikataharaki kidini na kiubinadamu, akawasaidia.
Hakuna ajabu kwa Musa kuwasaidia wanawake dhaifu; wala si ajabu kwa Shua’yb na mabinti zake kuishi kwa jasho lao.
Hii ndiyo sera ya mitume na makhalifa wao wenye takua, tangu zamani na baadaye. Bali ajabu ni kuwa roho hii ya Qur’an haina athari yoyote katika nafsi zetu sisi tunaodai kumjua Mwenyezi Mungu, Kitabu chake, na sera ya mitume wake. Ajabu ya maajabu ni kwamba tunashindana katika kuitafuta dunia na mapambo yake.
Basi akawanyweshea, kisha akarudi kivulini na akasema: Mola wangu! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayoniteremshia.
Musa aliwapatia maji wanyama wa wasichana wawili, kisha akaenda chini ya mti kupata kivuli, akiwa na uchovu na njaa. Akamwomba Mwenyezi Mungu fadhila na ukarimu wake. Wala hakung’angania sana au kuomba zaidi, kwa sababu alichokitaka ni kuziba tumbo tu.
Kama angelikuwa anaomba akhera angeling’ang’ania. Katika Nahjul balagha imeelezwa: “Wallahi hakumuomba isipokuwa mkate wa kula tu. Rangi ya kijani ya majani ilikuwa ikionekana kwenye ngozi ya tumbo lake kwa wembamba wake na kutengana na nyama yake.”
Basi mmoja wa wale wanawake wawili akamjia naye anatembea akiona haya. Akasema: Baba yangu anakuita akulipe ujira wa kutunyweshea.
Wale wasichana wawili walirudi kwa baba yao na wakamwelezea yaliyotokea. Basi akamwambia mmoja wao: Nenda kamwite tuje tumlipe hisani yake. Basi akaenda msichana akiwa amegubikwa na haya, ustahi na heshima na kumweleza alivyosema baba yake.
Basi alipomjia na kumsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka na watu madhalimu.
Musa alikubali mwito, na mzee akamkaribisha na kumshukuru kwa kitendo chake. Musa alipotulia na kumwamini yule mzee, alimsimulia yaliyompitia kwa Firauni na watu wake. Yule mzee akamwambia usihofu, umefika. Hapa kwetu ni ngome ya amani, haifikiwi na Firauni wala mfano wake katika madhalimu.
Wafasiri wametofautiana kuhusu mzee huyu ni nani? Wengi wao wamesema ni Shuaib na wengine wakasema siye. Hakuna ya kutegemewa kwa hawa wala wale. Nasi hatuna haja na tofauti hizi madam hazina uhusiano wowote na imani wala maisha.
Sisi tumechagua jina la Shua’yb kiasi cha kumwelezea huyo mzee tu, sio kuwa tumekubaliana na jina hilo na pia kwa kuwa ni jina liloenea kwa wengi; kama lilivoenea baina ya wanafunzi na ulamaa wa Najaf.
Akasema mmoja katika wale wanawake ambaye alimwita kwa baba yake: Ewe baba! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumwajiri ni mwenye nguvu na mwaminifu.
Tunasema aliyesema ni yule aliyemwita kutokana na kauli yake ‘mwenye nguvu’ pale alipowasaidia kuchota maji na ‘mwaminifu’ pale alipokuwa na staha wakati wakielekea kwa baba yake.
Akasema: Mimi ninataka kukuoza mmoja wa mabinti zangu hawa wawili kwa kunifanyia ajira ya miaka minane na kama ukitimiza kumi hiyari yako. Mimi sitaki kukutaabisha. Inshaallah utanikuta miongoni mwa watu wema.
Musa mkimbizi, fukara asiyekuwa na chochote, ambaye kwa siku kadhaa, ameishi kwa kula mimea ya ardhi; mpaka akamuomba Mola wake tonge ya kumwezesha kuishi, leo anahiyarishwa kuchagua mke amtakaye. Bila shaka hapa kuna siri ya utu wa Musa na utukufu wake uliomgusa mzee na mabinti zake. Vile vile katika masimulizi yake na sera yake kwa Firauni na watu wake.
Mzee alitambua, kutokana na akili yake safi, kwamba mtu huyu atakuwa na athari ya mbali. Kwa sababu matendo ya mtu aghlabu yanatoka kwenye chimbuko moja. Kwa hiyo mzee, hapa alifuzu kutokana na ukwe huu. Kuna faida gani kubwa zaidi ya kuwa mkwe wa Mtume na mwenye takua.
SHARIA YA KIISLAMU IMEFUTA SHARIA ZOTE
Mafaqihi wamezungumza mengi kuhusiana na Aya hii, wakaitolea dalili kuwa walii wa mwanamke ndiye atakayetamka tamko la ndoa. Lakini ilivyo ni kuwa inafaa kwa mwanamume au mwanamke mwenyewe kutam- ka. Hilo linafahamika kimsingi bila ya kuhitaji nukuu. Shafii na Imamiya wamesema kuwa ndoa haifungiki isipokuwa kwa tamko la ziwaj na nikah. Hii ni baada ya kuiunganisha Aya hii, yenye tamko la nikah, na ile yenye tamko la ziwaj.
فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا ﴿٣٧﴾
“Basi Zaid alipokwisha haja naye tulikuoza wewe” (33:37).
Malik na Hambal wakasema pia ndoa inafungika kwa neno hiba, kutokana na Aya yenye neno hiba:
وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ ﴿٥٠﴾
“Na mwanamke mumin akijitoa mwenyewe kwa Nabii.” (33:50).
Hanafi naye akasema kuwa ndoa inafungika kwa neno lolote linalofahamisha kutaka kuoana.
Mafaqihi wengi wamesema kuwa muda wa kuchunga wanyama miaka minane au kumi haukuwa mahari au sehemu yake. Bali mahari yalikuwa mbali; na kwamba kauli ya mzee: “kunifanyia ajira” maana yake ni kuwa ukichunga wanyama kwangu kwa ajira, nitakuoza mmoja wa mabinti zangu kwa mahari; sawa na kusema: ‘Ukifanya hivi nami nitafanya hivyo.’
Haya ndio maana sahihi ya Aya. Kwa vyovyote iwavyo, hakuna hoja yoyote, katika Aya hii kwa, waliyoyasema mafaqihi. Kwa sababu hizo ni simulizi za sharia zilizotangulia. Nasi tuna uhakika kwamba sharia ya Kiisalmu imefuta sharia zote zilizotangulia, wala haifai kutumia hukumu yoyote miongoni mwa hukumu hizo zilizotangulia, isipokuwa kwa dalili maalum au ya kiujmla kutoka katika Kitab au Sunna. Na hapo itakuwa ni kukitumia Kitab au Sunna, sio kuitumia sharia hiyo.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ ﴿٣٨﴾
“Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote.” Juz. 7 (6:38).
Na kauli yake:
وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ ﴿٨٩﴾
Na tumekuteremshia Kitabu hiki kubainisha kila kitu.” Juz.14: (16:89),
Yaani kila kitu katika misingi ya kiislamu na sharia yake.
Mtume(s.a.w.w)
naye anasema: “Hakuna kitu kitakachowakurubisha nyinyi Peponi isipokuwa nimewaamrisha, na hakuna kitu kitakachowaweka mbali na moto isipokuwa nimewakataza.”
Akasema: Hayo yamekwishakuwa baina yangu na yako. Muda wowote kati ya miwili nitakoumaliza nisifanyiwe ubaya na Mwenyezi Mungu ni wakili juu ya haya tunayoyasema.
Haya ni maneno ya Musa. Muda wa kwanza ni Hijja nane na wa pili ni Hijja kumi. Maana ni kuwa Musa alimwambia mzee, nimekubali na kuridhia kuoa na kuchunga wanyama.
Mimi nitakuwa na hiyari ya kumaliza nane au kumi. Muda wowote nitakaoumaliza basi usiwe na hoja kwangu na Mwenyezi Mungu ndiye shahidi juu ya haya uliyojiwajibishia na niliyojiwajibishia.
Kuna Hadith isemayo kuwa Musa alichagua muda wa kumi. Wafasiri wengi wanasema kuwa yeye alimchagua mdogo naye ndiye aliyesema, baba yangu anakuita. Na pia kumwambia baba yake, hakika yeye ana nguvu na ni mwaminifu.