6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
وَمَا كُنتَ بِجَانِبِ الْغَرْبِيِّ إِذْ قَضَيْنَا إِلَىٰ مُوسَى الْأَمْرَ وَمَا كُنتَ مِنَ الشَّاهِدِينَ ﴿٤٤﴾
44. Wala wewe hukuwa upande wa magharibi tulipompa Musa amri wala hukuwa miongoni mwa walioshuhudia.
وَلَـٰكِنَّا أَنشَأْنَا قُرُونًا فَتَطَاوَلَ عَلَيْهِمُ الْعُمُرُ وَمَا كُنتَ ثَاوِيًا فِي أَهْلِ مَدْيَنَ تَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَلَـٰكِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ ﴿٤٥﴾
45. Lakini tuliziumba karne na umri ukawa mrefu juu yao. Wala hukuwa mkaazi wa watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu, lakini ni sisi tuliokuwa tukiwatuma Mitume.
وَمَا كُنتَ بِجَانِبِ الطُّورِ إِذْ نَادَيْنَا وَلَـٰكِن رَّحْمَةً مِّن رَّبِّكَ لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أَتَاهُم مِّن نَّذِيرٍ مِّن قَبْلِكَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٤٦﴾
46. Wala hukuwa kando ya mlima tulipomuita. Lakini ni rehema itokayo kwa Mola wako ili uwaonye watu wasiofikiwa na muonyaji kabla yako, huenda wakakumbuka.
وَلَوْلَا أَن تُصِيبَهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَيَقُولُوا رَبَّنَا لَوْلَا أَرْسَلْتَ إِلَيْنَا رَسُولًا فَنَتَّبِعَ آيَاتِكَ وَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na usije ukawasibu msiba kwa iliyoyatanguliza mikono yao, kisha waseme: Ewe Mola wetu! Mbona hukutuletea Mtume nasi tukafuata ishara zako na tukawa miongoni mwa waumini?
فَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ مِنْ عِندِنَا قَالُوا لَوْلَا أُوتِيَ مِثْلَ مَا أُوتِيَ مُوسَىٰ أَوَلَمْ يَكْفُرُوا بِمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ مِن قَبْلُ قَالُوا سِحْرَانِ تَظَاهَرَا وَقَالُوا إِنَّا بِكُلٍّ كَافِرُونَ ﴿٤٨﴾
48. Ilipowajia haki kutoka kwetu walisema: Mbona hakupewa kama aliyopewa Musa? Je, hawakuyakataa aliyopewa Musa zamani? Walisema: ni wachawi wawili wanaosaidiana. Hakika tunawakataa wote.
قُلْ فَأْتُوا بِكِتَابٍ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ هُوَ أَهْدَىٰ مِنْهُمَا أَتَّبِعْهُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٩﴾
49. Sema: Basi leteni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu chenye mwongozo zaidi kuliko viwili nikifuate, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٠﴾
50. Na ikiwa hawakuitikii basi jua kuwa wamejifuatia tu hawaa zao. Na ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayefuata hawaa yake bila ya mwongozo utokao kwa Mwenyezi Mungu? Hakika Mwenyezi Mungu hawongozi watu madhalimu.
وَلَقَدْ وَصَّلْنَا لَهُمُ الْقَوْلَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٥١﴾
51. Na kwa hakika tuliwafululizia maneno ili wapate kukumbuka.
MUHAMMAD NA HABARI ZA WALIOPITA
Aya 44 -51
MAANA
Wala wewe hukuwa upande wa magharibi tulipompa Musa amri wala hukuwa miongoni mwa walioshuhudia.
Anaambiwa Muhammad(s.a.w.
w
)
. Makusudio ya upande wa magharibi ni upande wa magharibi mwa mlima, kama ilivyolezwa katika Tafsir Attabari, mahali alipozungumza Mwenyezi Mungu na Musa. Ama upande wa kuume ulioashiriwa kwenye Juz. 16 (19:52), ni upande wa kuumeni wa Musa. Makusudio ya amri aliyopewa Musa ni ni kuchaguliwa kwake kwa utume na unabii.
Maana ni kuwa kutoa habari Muhammad(s.a.w.w)
matukio ya Musa upande wa magharibi mwa mlima ni dalili mkataa kuwa habari hizo ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu atakuwa amepata wapi elimu ya kujua hakika hiyo ya undani na wala hajaisoma katika Kitabu, kuisikia kwa yoyote wala kushuhudia yeye mwenyewe?.
Lakini tuliziumba karne na umri ukawa mrefu juu yao.
Makusudio ya karne ni umma zilizotangulia na kuisha kati ya zama za Musa na Muhammad ambapo kuna karibu mika elfu mbili. Tazama tuliyoyafafanua katika Aya ya 7 ya Juzuu na sura hii tuliyo nayo.
Maana ni kuwa hakukubakia yeyote wa kutoa habari za umma alizoziumba Mwenyezi Mungu baina ya zama za Musa na Muhammad. Na hii ni dalili wazi kuwa elimu ya Muhammad inatokana na wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa hiyo basi muda mwingi ulipita na watu wakawa kwenye ujinga wa wajinga, wakawa wanahitajia Nabii atakayewaongoza na kuwaelekeza kwenye njia ya sawa. Ndipo Mwenyezi Mungu akamtuma Muhammad kuwa mbashiri na muonyaji, akawapa habari za watu wa umma zilizotangulia na mitume yao kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuwa ni dalili kwamba yeye ni Mtume kwa upande mmoja na ni mawaidha kwa upande wa pili.
Wala hukuwa mkaazi wa watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu, lakini ni sisi tuliokuwa tukiwatuma Mitume.
Madyana ni mji wa Shua’yb. Muhammad alimtolea habari Shua’yb, watu wake na watu wa mji wa Madyan; kama kwamba yeye ni Shua’yb akiwasomea watu wake Aya za Mwenyezi Mungu. Muhammad(s.a.w.w)
hakuwa Mtume wa watu wa Madyana, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyempa habari hizo kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake na mwenye amana ya wahyi wake.
Wala hukuwa kando ya mlima tulipomuita.
Yaani hukuwako ewe Muhammad wakati Mwenyezi Mungu alipomuita Musa kando ya mlima.
Unaweza kuuliza kuwa
: hakuna tofauti baina ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kando ya mlima’ na ile iliyotangulia ‘upande wa magharibi.’ Sasa je, kuna makusudio gani ya kukaririka huku?
Jibu
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) alizungmza na Musa na kumwita zaidi ya mara moja. Kwa hiyo inawezekana kuwa Aya ya kwanza ni kuashiria mwito wa kwanza na Aya ya pili kuwa ni ya mwito wa pili. Zaidi ya hayo, kukaririka ni mfumo wa Qur’an. Tazama tuliyoyeleza kwa anuani ya
‘kukaririka katika Qur’an’ kwenye Juz. 1 (2:47 – 48) na Juz.5 (4:116 -122).
Lakini ni rehema itokayo kwa Mola wako ili uwaonye watu wasiofikiwa na muonyaji kabla yako, huenda wakakumbuka.
Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad kuwa ni rehema kwa walimwengu akionya na kutoa bishara kwa watu, ili wafuate njia itakayowapelekea kwenye wema wa nyumba mbili (Dunia na Akhera).
Unaweza kuuliza
: Utaiunganisha vipi Aya hii na ile isemayo:
وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ ﴿٢٤﴾
“Hakuna umma wowote ila alipata humo muonyaji.” (35:24).
Jibu
: Tumesema mara nyingi kwamba Aya za Qur’an zinafasiriana, kwa sababu chimbuko lake ni moja. Kuna Aya isemayo:“Enyi watu wa Kitabu! Hakika amewafikia Mtume wetu anayebainishia, katika wakati usio na Mitume.” Juz. 6 (5:19), Yaani ulipokatika utumwaji mitume.
Kwa hiyo basi makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wasiofikiwa na muonyaji kabla yako,” sio kuwa Mwenyezi Mungu hakupeleka mitume kabla ya Muhammad kabisa; bali makusudio ni kuwa hakufika mtume kwa kipindi fulani.
Na usije ukawasibu msiba kwa iliyoyatanguliza mikono yao, kisha waseme: Ewe Mola wetu! Mbona hukutuletea Mtume nasi tukafuata Ishara zako na tukawa miongoni mwa waumini?
Makusudio ya msiba ni adhabu ya Mwenyezi Mungu duniani. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipeleka mitume ili iwe ni hoja kwa watu pale itakapowafikia adhabu kwa sababu ya kufuru yao na utaghuti wao. Umepita mfano wake katika Juz. 6 (4:165) na (5:19).
Ilipowajia haki kutoka kwetu walisema: Mbona hakupewa kama aliyopewa Musa?
Mtume alipokuwa hajawajia walisema, akija tutuamwamini. Alipowajia wanatafuta visababu vya ubatilifu. Usumbufu na uhepaji huu hauhusiki na wale waliomkadhibisha Muhammad tu, waliomwambia Muhammad(s.a.w.w)
: Lau ungekuja na fimbo na mkono mweupe wa Musa, tungelikuamini. Hapana! Haya ni mazowea ya mataghuti na wapenda anasa, kila wakati na kila mahali. Ni mazoweya ya wale ambao hawamini chochote isipokuwa masilahi yao na manufaa yao. Ndio wakawa vigeugeu na kuungana na shetani dhidi ya kila wema.
Je, kwani hao hawakuyakataa aliyopewa Musa zamani?
Walimtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kuwaletea mfano wa miujiza ya Musa; ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu kwamba mwenye kuitafuta haki kwa ajili ya haki anaifuata popote pale itakapom- bainikia. Lakini wale ambao hawaamini isipokuwa hawaa na matamanio yao na kuyafanya kuwa ndio mwongozo wao katika mambo yao yote, basi hawa haiwafai dalili na muujiza, uwe wa Musa au wa Muhammad au wa mitume wote.
Dalili ya hakika hii ni kuwa mataghuti waliyakataa aliyokuja nayo Musa; kama ambavyo mataghuti wa kikuraishi walikataa aliyokuja nayo Muhammad. Lau Musa na miujiza yake angelikuwa nafasi ya Muhammad, wangelisema: Lau Musa angelipewa mfano wa aliyopewa Muhammad. Hivi ndivyo walivyo wabatilifu, kila mhali na kila wakati.
Walisema: ni wachawi wawili wamesaidiana. Hakika sisi tunawakataa wote.
Makusudio ya wachawi wawili hapa ni Qur’an na Tawrat na kusaidiana ni kuwa kila moja inaisadikisha nyingine.
Maana ya kiujumla ni kuwa makuraishi walisema Tawrat ni uchawi na Musa ni mchawi. Vile vile wakasema Qur’an ni uchawi na Muhammad ni mchawi na kwamba wanazipinga zote mbili.
Sema: Basi leteni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu chenye mwongozo zaidi kuliko viwili nikifuate, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
Tawrat ni uchawi na mfano wake Qur’an pia ni uchawi, basi ikiwa mnacho kitabu kilicho na kheri kwa watu kuliko Tawrat na Qur’an basi kileteni na mimi nitakifuata na kukitumia. Huu ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ ﴿٨١﴾
“Sema: Ingelikuwa mwingi wa rehema ana mtoto basi ningelikuwa wa kwanza kumwabudu.” (43:81).
Na ikiwa hawakuitikii basi jua kuwa wamejifuatia tu hawaa zao.
Qur’an, kwa ufasaha na balagha yake, imeshinda fasihi na balagha zote. Na imeshinda misingi na mafunzo yote ya binadamu. Hakika Qur’an kwa itikadi yake na sharia yake, inaongoza kwenye usawa zaidi. Na hii ndiyo iliyo mikononi mwa wahakiki na wasomi. Basi na walete kilicho na mwongozo zaidi kwa watu kuliko hiyo au kilicho mfano wake na waite wanayemtaka na wanachokitaka.
Ikiwa watashindwa na wasiamini, basi watakuwa hawana dalili isipokuwa upofu na upotevu unaowaongoza kwenye uovu. Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayefuata hawaa yake bila ya mwongozo utokao kwa Mwenyezi Mungu? Hakika Mwenyezi Mungu hawongozi watu madhalimu
baada ya kujiingiza wenyewe na kufuata njia ya maangamizi na upotevu.
Na kwa hakika tuliwafululizia maneno ili wapate kukumbuka.
Makusudio ya maneno hapa ni Qur’an ambayo imekwishatoa onyo, haina lawama. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaongoza waja kwenye yale wanayostahiki wao na yale yanayostahiki kwa wengine, ili wawe na utiifu na watende. Atakayetenda na akafanya uzuri, basi huyo yuko katika amani. Na adhabu ni ya mwenye kukadhibisha na akakataa.
الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ مِن قَبْلِهِ هُم بِهِ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٢﴾
52. Wale ambao tuliwapa Kitabu kabla yake wanaiamini.
وَإِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ قَالُوا آمَنَّا بِهِ إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّنَا إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلِهِ مُسْلِمِينَ ﴿٥٣﴾
53. Na wanaposomewa, husema: Tunaiamini. Hakika hiyo ni haki inayotoka kwa Mola wetu. Hakika sisi kabla yake tulikuwa waislamu (wanyenyekevu).
أُولَـٰئِكَ يُؤْتَوْنَ أَجْرَهُم مَّرَّتَيْنِ بِمَا صَبَرُوا وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٥٤﴾
53. Basi hao watapewa ujira wao mara mbili. Na wanaondoa ubaya kwa wema na wakatoa katika tuliyowaruzuku.
وَإِذَا سَمِعُوا اللَّغْوَ أَعْرَضُوا عَنْهُ وَقَالُوا لَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ لَا نَبْتَغِي الْجَاهِلِينَ ﴿٥٥﴾
55. Na wanaposikia upuuzi hujitenga nao na husema: Sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu: Salamun alaykum! Hatuwataki wajinga.
WATAPEWA UJIRA MARA MBILI
Aya 52 – 55
MAANA
Wale ambao tuliwapa Kitabu kabla yake wanaiamini.
Yaani waliopewa Kitabu kabla ya Qur’an wanaiamini hii Qur’an. Zimethibiti Hadith Mutawatir kwamba wanaswara (wakiristo) wengi na baadhi ya mayahudi walimwamini Muhammad(s.a.w.w)
, kwa sababu Tawrat na Injili zimenukuu wasifu wake, kabla hazijapotolewa:
الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ ﴿١٥٧﴾
“Ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili” Juz. 9 (7:157)
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:121) na Juz. 4 (3:199).
Na wanaposomewa, husema: Tunaiamini. Hakika hiyo ni haki inayotoka kwa Mola wetu. Hakika sisi kabla yake tulikuwa waislamu (wanyenyekevu).
Maulama wa watu wa Kitabu walisoma sifa za Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na Qur’an Tukufu katika Tawrat na injil. Walizisoma hizo kabla ya kutumilizwa Muhammad(s.a.w.w)
. Alipotumilizwa aliwasomea Qur’an wakaitambua na wakamtambua Muhammad kwa sifa zake, kama zilivyo katika vitabu viwili; sawa na walivyowajua watoto wao:
الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ ﴿١٤٦﴾
“Wale tuliowapa Kitabu wanamjua kama wanavyowajua watoto wao.” Juz.1 (2:146).
Basi baadhi wakaamini na wengine wakaficha haki na hali wanajua, kwa kupupia vyeo na chumo.
Basi hao watapewa ujira wao mara mbili.
Wa kwanza ni kwa sababu ya ikhlasi yao katika dini yao ambayo imewaamrisha kumfuata Muhammad na Qur’an, na wa pili ni kwa walivyovumilia adha ya makafiri wapumbavu, kwa sababu kusilimu kwao kulikuwa ni hoja kubwa kwa yule anayeng’ang’ania ukafiri kwa inadi.
SUBIRA NI HEKIMA NA USHUJAA
Na wanaondoa ubaya kwa wema.
Waislamu wa mwanzo walipambana na maudhi na mateso, kiasi ambacho Muhammad(s.a.w.w)
alikuwa akizomewa na wapumbavu barabarani: “Huyoo mwenda wazimu... Huyoo mwongo... Huyoo mchawi!”
Wakawa na subira wakavumilia bila ya kulalamika. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameiita subira yao wema na maudhi ya washirikina akayaita ubaya.
Katika ibara hii kuna ishara kuwa silaha pekee ya mnyonge ni subira na kwamba hasira na kusimamisha mishipa ni wenda wazimu na kupigana bila ya silaha ni kujitia kitanzi.
Kwa hiyo subira ya mnyonge ni akili na hekima na ni ushujaa na werevu; kwa sharti ya kuhangaika na kufanya juhudi ya kuondoa huo unyonge na visababishi vyake. Lakini atakayebweteka na kufanya uvivu atakuwa amejitweza mwenyewe na kuridhia udhalili na unyonge.
Kwa maneno mengine ni kuwa unyonge ni kama ugonjwa, ni lazima utafutiwe dawa ya kuuondoa, sio kuvumilia kubaki na ugonjwa isipokuwa baada ya kushindwa kabisa na kukata tamaa.
Na wakatoa katika tuliyowaruzuku.
Wanaondoa shari ya uovu kwa kuvumilia. Pia wanafanya wema kwa kutoa kile wanachoruzukiwa na Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake. Imam Ali
anasema:Muadhibu ndugu yako kwa kumfanyia wema na urudishe uovu wake kwa kumneemesha.
Na wanaposikia upuuzi hujitenga nao.
Makafiri walianzisha matusi na shutuma kwa wale waliosilimu na kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wakavumilia na kujitia hamnazo,na husema: Sisi tuna vitendo vyete na nyinyi mna vitendo vyenu.
Nyinyi mmeridhia batili mliyo nayo na sisi tumeridhia haki tuliyo nayo.
Salamun alaykum!
Wafasiri wamesema: Salamu hii ni ya kuwavumilia majahili sio ya maamkuzi; sawa na kumwambia unayetaka uepukane naye: “Niondokee kwa amani.
Hatuwataki wajinga.
Hatuchanganyiki nao wala hatuwi na hulka zao.