8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّـهُ عَلَيْكُمُ اللَّيْلَ سَرْمَدًا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِضِيَاءٍ أَفَلَا تَسْمَعُونَ ﴿٧١﴾
71. Sema: Mwaonaje, kama Mwenyezi Mungu angeliufanya usiku uwakalie moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakayewaletea mwangaza basi je, hamsikii.
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّـهُ عَلَيْكُمُ النَّهَارَ سَرْمَدًا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِلَيْلٍ تَسْكُنُونَ فِيهِ أَفَلَا تُبْصِرُونَ ﴿٧٢﴾
72. Sema: Mwaonaje, kama Mwenyezi Mungu angeliufanya mchana uwakalie moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakayewaletea usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?
وَمِن رَّحْمَتِهِ جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٧٣﴾
73. Na katika rehema zake amewafanyia usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake na ili mpate kushukuru.
وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تَزْعُمُونَ ﴿٧٤﴾
74. Na siku atakapowaita na akasema: Wako wapi mliokuwa mkidai kuwa ni washirika wangu.
وَنَزَعْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ شَهِيدًا فَقُلْنَا هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ فَعَلِمُوا أَنَّ الْحَقَّ لِلَّـهِ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٧٥﴾
75. Na tutatoa shahidi katika kila umma na tuseme: Leteni hoja zenu! Hapo watajua kwamba hakika haki ni ya Mwenyezi Mungu na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua.
HEKIMA YA USIKU NA MCHANA
Aya 71 – 75
MAANA
Sema: Mwaonaje, kama Mwenyezi Mungu angeliufanya usiku uwakalie moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakayewaletea mwangaza basi je, hamsikii.
Binadamu hufanya kazi na kupumzika kwa usingizi. Kazi inahitajia mwangaza na usingizi kwenye giza unakuwa mzito na unaleta siha ya mwili.
Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaumba mchana kwa ajili ya kufanya kazi na usiku kwa ajili ya kupumzika. Lau usiku ungeliendelea bila ya asubuhi au mchana ukaendelea bila ya usiku basi maisha yangelikuwa balaa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipotaja usiku amesema: ‘Hamsikii?’ na mchana akasema: ‘Hamuoni?’ kwa sababu usiku unanasibiana na kusikia na mchana kwa kuona.
Huko nyuma tumesema kuwa kufuatana usiku na mchana kunategemezwa moja kwa moja kwenye sababu zake za kimaumbile na kunategemezwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kupitia hizo sababu, kwa vile yeye ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo, na ndiye aliyeupangilia vizuri kwa hekima yake.
Na katika rehema zake amewafanyia usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake na ili mpate kushukuru.
Yaani amewafanyia usiku mpumzike na amewafanyia mchana mtafute. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:67), Juz. 15 (17:12) na Juz. 19 (25:47).
Na siku atakapowaita na akasema: Wako wapi mliokuwa mkidai kuwa ni washirika wangu.
Imetangulia punde tu katika Sura hii tuliyo nayo Aya 62. hatujui wajihi wa kukaririka huku isipokuwa kuthibitisha na kusisitiza.
Na tutatoa shahidi katika kila umma na tuseme: Leteni hoja zenu!
Kesho Mwenyezi Mungu (s.w.t) kila umma atauletea nabii wao atoe ushahidi juu yao kuwa alifikisha ujumbe na aeleze upinzani alioupata na kukadhibishwa baada ya kuwawasilishia hoja na kukata nyudhuru zote. Hapo Mwenyezi Mungu (s.w.t) atasema Mtume amenieleza yake, haya nanyi elezeni yenu na kile kilichowafanya muwakadhibishe; sawa na hakimu anavyofanya–kwanza anamsikiliza mwenye madai kisha mshatikiwa anajibu.
Hapo wataziba mdomo wabatilifu na adhabu itawastahili. Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:143), Juz. 14 (16:89).
Hapo watajua kwamba hakika haki ni ya Mwenyezi Mungu.
Yaani watajua kuwa hoja ya Mungu itawasimamia juu yao na wao hawatakuwa na hoja kwa Mwenyezi Mungu.
Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua,
kuwa Mwenyezi Mungu ana mshirika na uwongo walioueneza juu ya watu wema.
إِنَّ قَارُونَ كَانَ مِن قَوْمِ مُوسَىٰ فَبَغَىٰ عَلَيْهِمْ وَآتَيْنَاهُ مِنَ الْكُنُوزِ مَا إِنَّ مَفَاتِحَهُ لَتَنُوءُ بِالْعُصْبَةِ أُولِي الْقُوَّةِ إِذْ قَالَ لَهُ قَوْمُهُ لَا تَفْرَحْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْفَرِحِينَ ﴿٧٦﴾
76. Hakika Qaruni alikuwa katika kaumu ya Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa hazina ambazo funguo zake ziliwaelemea kundi la watu wenye nguvu. walipomwambia watu wake: Usijigambe, hakika Mwenyezi Mungu hapendi wanaojigamba.
وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّـهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّـهُ إِلَيْكَ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴿٧٧﴾
77. Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya akhera; wala usisahau fungu lako la dunia. Na fanya wema kama alivyokufanyia wema Mwenyezi Mungu, wala usitafute ufisadi katika ardhi; hakika Mwenyezi Mungu hapendi wafisadi.
قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ عِندِي أَوَلَمْ يَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَهْلَكَ مِن قَبْلِهِ مِنَ الْقُرُونِ مَنْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُ قُوَّةً وَأَكْثَرُ جَمْعًا وَلَا يُسْأَلُ عَن ذُنُوبِهِمُ الْمُجْرِمُونَ ﴿٧٨﴾
78. Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya elimu niliyo nayo. Je, hakujua kwamba Mwenyezi Mungu amekwishaangamiza karne zilizokuwa kabla yake waliokuwa na nguvu zaidi kuliko yeye na wenye makundi makubwa zaidi. Na wakosefu hawataulizwa dhambi zao.
فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ فِي زِينَتِهِ قَالَ الَّذِينَ يُرِيدُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا يَا لَيْتَ لَنَا مِثْلَ مَا أُوتِيَ قَارُونُ إِنَّهُ لَذُو حَظٍّ عَظِيمٍ ﴿٧٩﴾
79. Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema wale waliokuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungelikuwa nayo kama aliyopewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.
وَقَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَيْلَكُمْ ثَوَابُ اللَّـهِ خَيْرٌ لِّمَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا وَلَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الصَّابِرُونَ ﴿٨٠﴾
80. Na wakasema wale ambao wamepewa elimu: Ole wenu! Thawabu za Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda. Na wala hawatapewa isipokuwa wenye subira.
فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الْأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِن فِئَةٍ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُنتَصِرِينَ ﴿٨١﴾
81. Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake ardhini; wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu wala hakuwa miongoni mwa wanaojisaidia.
وَأَصْبَحَ الَّذِينَ تَمَنَّوْا مَكَانَهُ بِالْأَمْسِ يَقُولُونَ وَيْكَأَنَّ اللَّـهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَوْلَا أَن مَّنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا لَخَسَفَ بِنَا وَيْكَأَنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٢﴾
82. Na wakawa wanasema wale waliotamani mahala pake jana: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Asingetufanyia hisani Mwenyezi Mungu angelitudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi.
QARUNI NA UKANDAMIZAJI WA KIBEPARI
Aya 76 – 82
MAANA
Hakika Qaruni alikuwa katika kaumu ya Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa hazina ambazo funguo zake ziliwaelemea kundi la watu wenye nguvu.
Qaruni alikuwa katika wana wa Israil, kwa sababu yeye alikuwa katika kaumu ya Musa. Inasemekana alikuwa ni binamu yake. Yeye ndiye aliyeweka jiwe la msingi la ubepari wa ukandamizaji au alikuwa ni mwakilishi wake. Kwa sababu yeye alihodhi na akawatawala watu wake, akilitetea hilo kwa kauli yake: “Nimepewa haya kwa sababu ya elimu niliyo nayo,” kama zinazosema Aya zinazofuatia.
Haya ndio madhehebu ya kiuchumi yasemayo: Mtu binafsi kwanza, kisha ndio jamii. Vile vile yanaashiriwa na Aya hii tuliyo nayo, pale ilipokutanisha dhulma na hazina ya mali. Kuna dhulma gani zaidi kuliko kuwa chakula cha viumbe kimezuiwa na mtu au baadhi ya watu mpaka watake wao?
Watu wa Qaruni walijaribu kumkemea kwa njia nzuri, walipomwambia watu wake: Usijigambe, hakika Mwenyezi Mungu hapendi wanaojigamba.
Vipi unafurahi na mali na kuhadaika nayo na kuifanya ni nyenzo ya dhulma, uadui, anasa na israfu, na karibu yako watu wanakufa njaa? Je unajigamba kwa uweza wako wa kufanya dhambi na uovu?
Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya akhera.
Jitahidi na ufanye kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa kila alichokupa Mwenyezi Mungu katika mali siha na akili. Kwani mtu atakuwa na majukumu na kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na mwili jinsi alivyoutumia, umri wake jinsi alivyoumaliza na mali yake jinsi alivyoichuma na kuitumia.
Wala usisahau fungu lako la dunia.
Usiache mahitaji ya maisha yako na starehe zako. Kula unavyotaka katika vizuri na vya halali na uvae unavyopenda katika nguo nzuri, lakini kutokana na jasho lako sio la wengine. Kwa kufanya hivi utakuwa umepata mafungu mawili: Fungu la dunia na la akhera.
Na fanya wema kama alivyokufanyia wema Mwenyezi Mungu.
Mche Mwenyezi Mungu kwa aliyokuneemesha na umshukuru kwa wema huo kwa waja wake na watu wake; usaidiane nao kwenye yale yaliyo na kheri nawe na wao.
Wala usitafute ufisadi katika ardhi,
kwa kufanya jeuri, hiyana, kiburi, ubabe na kufanya israfu na hali kando yako kuna wanaokufa njaa. Huu ndio ufisadi hasa na hakika Mwenyezi Mungu hapendi wafisadi na amewandalia adhabu chungu.
Akasema kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya elimu niliyo nayo.
Yaani mali aliyo nayo imetokana na elimu yake, kipawa chake na ujanja wake. Kwamba mtu anaweza kuitumia elimu yake na kipawa chake kupora, kuiba, kuua na kuwatoa watu katika miji yao.
Hii sio bid’a ya Qaruni peke yake. Serikali ya U.S.A. imeweka mpango wa kununua akili na vipawa kutoka pembe zote za ulimwengu na kuwafanya wataalamu na wajuzi wahamie huko.
Mpango huu wameuita ‘Brain drain;’ yaani kunyonya akili. Lengo la hilo ni kutumia vipawa vya binadamu kupora mali za nchi na vyakula vya waja mashiriki ya ardhi na magharibi yake.
Je, hakujua kwamba Mwenyezi Mungu amekwishaangamiza karne zilizokuwa kabla yake waliokuwa na nguvu zaidi kuliko yeye na wenye makundi makubwa zaidi.
Vipi atajua naye mali na jaha zimemfurisha kichwa, ikampofusha na mwisho wa dhulma na ikamsahaulisha na aliyoyasikia kuhusu karne zilizopita–kwamba zilikuwa na mali na watu wengi zaidi kuliko yeye, lakini walipokiuka mipaka na kufanya dhulma, Mwenyezi Mungu aliwaonjesha adhabu ya kufedheheka duniani na adhabu ya akhera ni kali na ya kufedhehesha zaidi.
Wafasiri wametolea mfano wa kaumu ya Nuh, A’d na Thamud. Kama ningelikuwa wakati wao nigekubaliana nao, nao kama wangelikuwa wakati wangu wangelitosheka na yaliyotokea Libya mwezi huu ninapoandika maneno haya, Septemba1969, ambapo kuna kundi la vijana limempindua mfalme aliyekuwa na nguvu na utajiri kuliko Qaruni, akiwa anasaidiwa na uzayuni na ukoloni. Wamemng’oa na wakachukua madaraka. Vijana hawa waliteswa na mfalme, wakafungwa na kufukuzwa.
Na wakosefu hawataulizwa dhambi zao.
Yaani Mwenyezi Mungu atawaadhibu bila ya hisabu.
Unaweza kuuliza
: Aya hii tutaiunganisha vipi na Aya isemayo:
فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾
“Naapa kwa Mola wako, tutawauliza wote yale waliyokuwa wakiyatenda.” Juz. 14 (15:92-93).
Pamoja na Aya nyingine kadhaa zenye maana hiyo?
Jibu
: Makusudio ya wakosefu hapa, kulingana na mfumo wa maneno ulivyo, ni wale waliozikosea haki za watu na uhuru, wakazusha fitna na vita kwa ajili ya masilahi yao na manufaa yao. Hawa ndio ambao wataingia motoni bila ya hisabu.
Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Hawataulizwa dhambi zao’ inawavua kutoka wale watakoulizwa wote. Yaani kama tutaziunganisha kauli mbili, maana yatakuwa: Tutawauliza wote isipokuwa waliozikosea haki za watu; wao wataingia motoni bila yamaswali.
Basi akawatokea watu wake katika pambo lake.
Watu wake walimpa hadhari ya mwisho mbaya, lakini shetani akampuzia kwenye pua yake, kiburi kikampanda, akawakusanya watumishi wake na wapambe wake. Akapanda kipando cha fahari, kuwaonyesha watu utajiri wake na kiburi chake, kuwaonyesha wale waliomuhadharisha na kumpa mawaidha kutokana na ulevi wa starehe na dhulma.
Wakasema wale waliokuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungelikuwa nayo kama aliyopewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.
Wadhaifu wa akili walitazama mali na vipambo, wakasahau mwisho wa uovu na kiburi, na wakatamani kuwa na starehe kama za Qaruni ili waangamie kwenye starehe na anasa. Lau wangeliangalia kwa mtazamo wa busara wangelisema kama walivyosema wenye elimu:
Na wakasema wale ambao wamepewa elimu: Ole wenu! Thawabu za Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda. Wala hawatapewa isipokuwa wenye subira.
Yaani watu wa elimu waliwaambia wale madhaifu wa akili, hayo mnayoyatamka ni ushetani na kwamba vilivyo kwa Mwenyezi Mungu ni bora na vyenye kubaki.
Yeyote anayemtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi hudhalilika na kuhizika. Amesema Imam Aliy
: “Ni mara ngapi aliyepungukiwa akapata faida na aliyezidishiwa akapata hasara” Nahjul Balagha Khutba na 114.
Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake ardhini; wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu wala hakuwa miongoni mwa wanaojisaidia.
Dhalimu hawezi kuokoka na kudidimia duniani kabla ya Akhera. Si lazima kudidimia kuwe ni kuzama ardhini, inaweza kuwa ni kwa kufedheheka na kulaaniwa na viumbe wenye kudhulumiwa na kunyimwa haki zao.
Uzoefu unatufahamisha kuwa dhalimu akipatikana na wenye kulipiza kisasi na kutaka haki zao, basi watu wote hujitenga naye; hata wale wasaidizi wake na ndugu zake na kujiona kuwa amedimimia.
Na wakawa wanasema wale waliotamani mahala pake jana: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Asingetufanyia hisani Mwenyezi Mungu angelitudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi.
Jana wale wadhaifu wa akili walikuwa wakisema tunatamani kuwa na aliyo nayo Qaruni, kwa vile walikuwa na mtazamo wa dunia na starehe zake; wakasahau hatima ya dhulma na kiburi. Leo wameshuhudia matokeo ya uovu yakimtokea Qaruni.
Wametambua uhakika na wakamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hakuwapa kama walivyopewa mataghuti.
Katika Nahjul Balagha, imesemwa: “Ni upungufu mngapi umekuwa faida na ziada ngapi zimekuwa ni hasara?” Kuanzia hapa ndio ikasemwa: ‘Mambo ni mwisho wake.’
تِلْكَ الدَّارُ الْآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لَا يُرِيدُونَ عُلُوًّا فِي الْأَرْضِ وَلَا فَسَادًا وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٨٣﴾
83. Hayo ndiyo makazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasiotaka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho ni wa wenye takua.
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَى الَّذِينَ عَمِلُوا السَّيِّئَاتِ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٨٤﴾
84. Atakayetenda mema atapata malipo bora kuliko hayo. Na atakayetenda uovu, hawalipwi watendao uovu ila waliyokuwa wakiyatenda.
إِنَّ الَّذِي فَرَضَ عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لَرَادُّكَ إِلَىٰ مَعَادٍ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ مَن جَاءَ بِالْهُدَىٰ وَمَنْ هُوَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٨٥﴾
85. Hakika aliyekulazimisha Qur’an, bila shaka atakurudisha mahali pa marejeo. Sema: Mola wangu ndiye anayemjua zaidi mwenye kuja na uongofu na aliyemo katika upotofu ulio dhahiri.
وَمَا كُنتَ تَرْجُو أَن يُلْقَىٰ إِلَيْكَ الْكِتَابُ إِلَّا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ ظَهِيرًا لِّلْكَافِرِينَ ﴿٨٦﴾
86. Nawe hukuwa unatarajia kuletewa Kitabu lakini ni rehema ya Mola wako. Basi usiwe kabisa msaidizi wa makafiri
وَلَا يَصُدُّنَّكَ عَنْ آيَاتِ اللَّـهِ بَعْدَ إِذْ أُنزِلَتْ إِلَيْكَ وَادْعُ إِلَىٰ رَبِّكَ وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٨٧﴾
87. Wala wasikuzuie na Aya za Mwenyezi Mungu baada ya kuteremshiwa, na lingania kwa Mola wako, wala usiwe kabisa miongoni mwa washirikina.
وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٨﴾
88. Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwingine. Hapana Mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipokuwa dhati yake, hukumu ni yake na kwake Yeye mtarejeshwa.
ATAKURUDISHA MAHALI PA KUREJEA
Aya 83 – 88
MAANA
Hayo ndiyo makazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasiotaka kuji- tukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho ni wa wenye takua.
Kujitukuza katika ardhi ni kujiweka juu na kuwatawala watu bila ya haki. Ufisadi ni dhulma, uadui, ufuska na uovu.
Maana ni kuwa mwenye kujikweza na kujitukuza kwa watu au kutumia vibaya haki zao, basi Mwenyezi Mungu amemharamishia Pepo na makazi yake ni Jahannam ni makazi mabaya.
Atakayetenda mema atapata malipo bora kuliko huo. Na atakayeten- da uovu, hawalipwi watendao uovu ila waliyokuwa wakiyatenda.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6160).
Hakika aliyekulazimisha Qur’an, bila shaka atakurudisha mahali pa marejeo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake kuwa aliyekuwajibishia kuitumia Qur’an ndiye atakayekurudisha Makka walikokutoa watu wako.
Inasemekana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alipohama Makka kuelekea Madina, akiwa njiani aliutamani, mji wake. Ndipo ikashuka Aya hii kumbashiria kurudi.
Sema: Mola wangu ndiye anayemjua zaidi mwenye kuja na uongofu na aliyemo katika upotofu ulio dhahiri.
Yaani sema ewe Muhammad kumwambia yule usiyemtarajia kuongoka na kung’ang’ania kuwa yeye ni muongofu na wewe ni mpotevu kuwa ni Mwenyezi Mungu peke yake anayeweza kumpambanua muongofu na mpotevu na mwema na muovu. Na atamlipa kila mmoja stahiki yake.
Nawe hukuwa unatarajia kuletewa Kitabu lakini ni rehema ya Mola wako.
Hii ni kumrudi yule aliyemwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu: Wewe si Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bali unamzulia.
Ubainfu ni kuwa, vipi wanakwambia kuwa wewe ni mzushi na hali hukuwahi hata kuwazia hilo hata siku moja; isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyekuneemesha na akakuteua wewe badala ya wengine?
KUFICHUA HABARI ZA VIBARAKA NA WAHAINI
Basi usiwe msaidizi wa makafiri. Wala wasikuzuie na Aya za Mwenyezi Mungu baada ya kuteremshiwa, na lingania kwa Mola wako, wala usiwe miongoni mwa washirikina. Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwingine. Hapana Mungu ila Yeye.
Mwenyezi Mungu amekuteua wewe ewe Muhammad ili uwapige vita wala usiwasaidie. Vile vile amekuchagua kufikisha ujumbe wake kwa waja wake, wala usilaumiwe kwa kuufikisha ujumbe; na umfanyie ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake kwenye kauli zako na vitendo vyako.
Huko nyuma wakati tukifasiri aina ya Aya kama hii inayomwambia maasum kuwa asifanye dhambi tulisema kuwa aliye juu anaweza kumkataza aliye chini kwa aina yoyote ya makatazo anayotaka; kuongezea kuwa jambo linalokatazwa sio lazima anayekatazwa awe anaweza kulifanya.
Hivi sasa tukifasiri Aya hizi, tumepata maana nyingine zaidi. Nayo ni kuwa aina hii ya Aya ni kufichua habari za wenye vilemba na kofia wanaojionyesha kuwa ni watu wa dini kumbe ni askari na wasaidizi wa makafiri waovu na kuelezea hali yao leo na kabla ya leo.
Tumehusisha kutaja baadhi yao hasa, pamoja na kuwa vibaraka wanatokana na kila aina ya watu, kwa vile Aya zinazungumza na anayemlinga- nia Mwenyezi Mungu na sharia yake.
Kila kitu kitaangamia isipokuwa dhati yake, hukumu ni yake na kwake Yeye mtarejeshwa.
Haya ni makemeo na kiaga kwa kila mhaini na kibaraka anayeipangia njama dini yake na nchi yake pamoja na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa utu. Na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu atamhukumu mshirikina ambaye amesimamiwa na hoja, lakini akafanya inadi. Kwani hakuna tofauti kabisa baina ya anayemuomba Mungu mwingine na yule anayewasaidia madhalimu mataghuti, akiwatetea na kutoa mwito waungwe mkono.
Unaweza kuuliza
: Je, hii inamaanisha kuwa ni wajibu kuwachukulia wahaini na vibaraka kama washirikina katika unajisi, kuacha kurithi, kutooana nao na kutozikwa kwenye makaburi ya waislamu?
Jibu
: Ni wajibu wetu kumchukulia kila aliyesema: Ash-hadu alla ilaha illallah wa anna Muhammadarasulullah: (‘Nashudia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu,’ kama tunavyomchukulia mwislamu; kwa namna yoyote vitakavyokuwa vitendo vyake au kwa vyovyote moyo wake utakavyokunjika.
Hiyo ni kwa sababu shahada ina athari yake ya kimaudhui haiepukani nayo kwa hali yoyote, ambayo ni utwahara, kurithiana, kuozana na kuzikwa kwenye makaburi ya waislamu. Ama akhera hiyo ni ya Mwenyezi Mungu peke yake wala hahusiki nayo yeyote asiyekuwa Yeye.
Dhahiri za Aya nyingi zimefahamisha kuwa mshirikina na dhalimu, siku ya Kiyama, watakuwa sawa. Tazama tuliyoyasema katika Juz. 19 (55–62).