9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
Sura Ya Ishirini Na Tisa: Surat A’nkabut. Imesemekana kuwa imeshuka Makka, ina Aya 69.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
الم ﴿١﴾
1. Alif Laam Miim.
أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾
2. Je, wanadhani watu wataachwa waseme tumeamini nao wasijaribiwe?
وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾
3. Hakika tuliwajaribu waliokuwa kabla yao. Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wakweli na kwa yakini atawatambulisha waongo.
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ أَن يَسْبِقُونَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿٤﴾
4. Au wanadhani wanaotenda maovu kwamba watatushinda? Ni mabaya wanayohukumu.
مَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ اللَّـهِ فَإِنَّ أَجَلَ اللَّـهِ لَآتٍ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٥﴾
5. Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika. Naye ni mwenye kusikia mwenye kujua.
وَمَن جَاهَدَ فَإِنَّمَا يُجَاهِدُ لِنَفْسِهِ إِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٦﴾
6. Na anayefanya juhudi basi hakika anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَحْسَنَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٧﴾
7. Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaondolea maovu yao, na tutawalipa mazuri ya waliyokuwa wakiyatenda.
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾
8. Na tumemuusia mtu kuwatendea wema wazazi wake wawili. Na wakikushikilia unishirikishe mimi na yale usiyokuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu mimi ndio marejeo yenu, na nitawaambia mnayoyatenda.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُدْخِلَنَّهُمْ فِي الصَّالِحِينَ ﴿٩﴾
9. Na wale ambao wameamini na wakatenda mema kwa hakika tutawaingiza katika wema.
IMANI, JIHADI NA SUBIRA
Aya 1 – 9
MAANA
Alif Laam Miim.
Umepita mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Wasidhani watu wataachwa waseme tumeamini nao wasijaribiwe?
Imani sio tamko la kusemwa, bali hapana budi liamambatane na mitihani na majaribu ya aina ya raha na tabu. Mwenye kuvumilia tabu na asitoke kwenye dini yake na akashukuru raha na kunyenyekea, wala cheo na mali isimfanye jeuri na kupetuka mipaka, huyo ndiye mumin wa kweli. Vinginevyo atakuwa sio mumin chochote.
Hivi ndivyo inavyofahamisha dhahiri ya Aya. Tukiiunganisha na Aya nyingine zinazohusiana na maudhui haya, tunapata muhtasari wa kuwa kuna jambo ambalo haliepukani na imani kwa hali yoyote. Nalo ni kuitikia muumini mwito wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kimatendo sio kimatamshi; yaani afanye bidii yake yote kutii amri ya Mungu na makatazo yake na kuambatana hayo na tabia yake na matendo yake. Anapopata mtihani na msukosuko wowote, basi umzidishe imani na unyenyekevu, kwa sababu anamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu.
Tazama Juz. 2 (2: 153 – 157), kifungu cha ‘Thamani ya Pepo,’ Juz. 2 (2:211 – 212), kifungu cha ‘Hakuna imani bila ya takua’ na Juz. 5 (4: 135 – 136) kifungu cha ‘Baina ya dini na watu wa dini.’
Hakika tuliwajaribu waliokuwa kabla yao.
Wafuasi wa Mitume waliotangulia tuliwajaribu kwa shida, wakavumilia na wakawa na subira ya uungwana na wakazidi kushikamana na dini yao na ikhlasi kwa Mola wao na mitume yao.
Tafsiri inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ni manabii wangapi waliopigana pamoja nao waumin wengi, nao hawakulegea kwa yale yaliyowasibu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika, wala hawakudhalilika. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaosubiri.” Juz. 4 (3:146).
Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na kwa yakini atawatambulisha waongo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamtahini mja wake kwa kumpa mbele ya dunia na nyuma yake, ili vidhihiri vitendo vyake vitakavyomfanya astahiki thawabu na adhabu. Kwa sababu yeye ambaye, imetukuka hekima yake, hamhisabu mtu kutokana na maandalizi yake ya kheri au ya shari; isipokuwa anamhisabu kwa matendo yake ambayo yanadhihirika.
Au wanadhani wanaotenda maovu kwamba watatushinda?
Waovu wanafikiria kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kuwapata? Itakuwaje naye ni muweza wa kila kitu? Ni nani atakayeweza kuwazuia naye na hali yeye hana mpinzani wala mshirika aliye sawa naye?
Ni mabaya wanayohukumu
kwamba wao wataponyoka na utawala wa Mwenyezi Mungu na hukumu yake.
Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wenye kukufuru siku ya mwisho sasa anataja mwenye kumwamini. Akamwambia mumin huyu:
Thibiti kwenye imani yako, kwani saa itafika tu hakuna shaka, basi ifanyie kazi.
Naye ni mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Anasikia unayoyasema na anajua unayoyadhamiria na kuyafanya na atakulipa yaliyopita.
Na anayefanya juhudi basi hakika anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake.
Tafsiri ya Aya hii ni ile Aya isemayo:
فَمَنْ أَبْصَرَ فَلِنَفْسِهِ وَمَنْ عَمِيَ فَعَلَيْهَا ﴿١٠٤﴾
“Basi atakayefungua macho ni faida yake mwenyewe; na atakayeyapofua ni hasara yake mwenyewe.” Juz. 7 (6:104).
Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu
, haumnufaishi utiifu wa mwenye kutii, wala haumdhuru uasi wa mwenye kuasi.
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaondolea maovu yao, na tutawalipa mazuri ya waliyokuwa wakiyatenda.
Mwenye kuamini baada ya kukufuru, akawa mwema baada ya kuwa mfisadi, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe na kumghufiria yaliyopita. Zaidi ya hayo atapata thawabu kutokana na imani yake na wema wake; sawa na ambaye hana dhambi.
Katika msingi huu wa heri kuna heri zote za utu. Kwa sababu unafungua mlango wa matumaini ya wenye dhambi na makosa na kupata msukumo wa kutubia na kujing’oa kwenye uovu. Hakuna njia nzuri kuliko hii ya kuisafisha jamii na dhulma na ufisadi.
TENA KUWATENDEA WEMA WAZAZI WAWILI
Na tumemuusia mtu kuwatendea wema wazazi wake wawili. Na wakikushikilia unishirikishe mimi na yale usiyokuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu mimi ndio marejeo yenu, na nitawaambia mnayoyatenda.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameamrisha kuwatendea wema wazazi wawili na kuwatii katika kila kitu isipokuwa katika lile ambalo haliridhii Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwani hakuna kumtii kiumbe kwa kumuasia muumba.
Tumelizungumzia kwa ufafanuzi hilo katika Juz. 15 (17:23). Na katika vitabu vya Hadith, kuna kisa kinachofahamisha kuwa kuwatendea wema wazazi wawili kunanufaisha wakati wa shida na pia kwamba dua bora ya kumwelekea Mwenyezi Mungu wakati wa shida ni matendo mema.
Imepokewa kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
kwamba watu watatu walingia kwenye pango lililokuwa njiani, wakalala humo. Likaanguka jiwe kubwa kutoka mlimani likawazibia mlango. Baada ya kufikiria sana hawakupata njia isipokuwa kuelekea kwenye dua kumuomba Mwenyezi Mungu peke yake awaokoe na maangamizi haya.
Kisha akakumbuka kila mmoja tendo jema alilolitenda: Wa kwanza, akakumbuka jinsi alivyowatendea wema wazazi wake wawili na kuwapatia raha. Basi jiwe likasogea kidogo. Wa pili akakumbuka kumtekelezea haja mwanamke aliyekuwa na dharura bila ya kufanya naye tendo chafu. Jiwe likasogea tena. Wa tatu akasema kuwa alikuwa na mfanyakazi aliyeondoka bila ya kuchukua mshahara wake. Ule mshahara akauhifadhi na ukazaa, ukawa na wanyama wengi sana, basi akampa mshahara wake na ile ziyada. Hapo jiwe likamalizika kufunguka na wakatoka kwenye pango.
Riwaya hii iwe ni sahihi au la, lakini kisa kinauelezea Uislamu na uhakika wake, kwa sababu unadhibiti njia ya uokovu duniani na akhera kwa matendo mema, sio kwa kauli na kujionyesha.
Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaingiza katika wema.
Unaweza kuuliza
: Kuna tofauti gani kati ya Aya hii na ile iliyotangulia, isemayo: Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, kwa hakika tutawaondolea maovu yao, na tutawalipa mazuri ya waliyokuwa wakiyatenda?
Jibu
: Kuingizwa katika kundi la watu wema; kama vile mashahidi na mawalii, ni daraja ya juu zaidi sana kuliko kusamehewa na kulipwa. Ni sawa na kumwambia aliyefanya uovu kisha akatengenea na kuwa mwenye ikhlasi: Nimekusamehe na nitakufanyia wema fulani. Zaidi ya hayo nitakuweka kwenye idadi ya wateuliwa walio bora.
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّـهِ وَلَئِن جَاءَ نَصْرٌ مِّن رَّبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ أَوَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾
10. Na katika watu kuna wanaosema: Tumemwamini Mwenyezi Mungu, lakini wanapoudhiwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanayafanya maudhi ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na itakapokuja nusra kutoka kwa Mola wako lazima watasema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliyomo vifuani mwa walimwengu?
وَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْمُنَافِقِينَ ﴿١١﴾
11. Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale ambao wameamini na kwa yakini atawatambulisha wanafiki.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا اتَّبِعُوا سَبِيلَنَا وَلْنَحْمِلْ خَطَايَاكُمْ وَمَا هُم بِحَامِلِينَ مِنْ خَطَايَاهُم مِّن شَيْءٍ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿١٢﴾
12. Na wale ambao wamekufuru waliwaambia walioamini: Fuateni njia yetu nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo.
وَلَيَحْمِلُنَّ أَثْقَالَهُمْ وَأَثْقَالًا مَّعَ أَثْقَالِهِمْ وَلَيُسْأَلُنَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَمَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿١٣﴾
13. Na kwa hakika wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao, na kwa hakika wataulizwa siku ya Kiyama juu ya waliyoyazua.
KATIKA WATU KUNA WANAOSEMA, TUMEAMINI
Aya 10 – 13
IMANI AU SARABI?
MAANA
Na katika watu kuna wanaosema: Tumemwamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapoudhiwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanayafanya maudhi ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Aya hii inaleta picha ya uhakika ya baadhi ya watu tunaowajua na kuishi nao. Shetani amewapambia watu hawa kwa hila na wasiwasi wake, mpaka wakamsadiki, wakajiona ni katika watu wa takua na imani; kumbe hawaitakidi wala kuona kitu chochote isipokuwa manufaa na masilahi yao.
Hakuna kitu kinachofahamisha zaidi kuwa imani zao ni njozi na sarabi, kuliko kule kuhofia kwao watu japo kwa kitu kidogo tu. Wanawahofia itakapodhihiri haki na usawa kwa kauli au kwa vitendo; sawa na mawalii na wenye takua wanavyomhofia Mwenyezi Mungu.
Imetangulia ishara ya kundi hili katika Aya isemayo:
فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَخْشَوْنَ النَّاسَ كَخَشْيَةِ اللَّـهِ أَوْ أَشَدَّ خَشْيَةً ﴿٧٧﴾
“Walipolazimishwa kupigana, mara kundi moja katika wao wakawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu au kwa hofu zaidi.” Juz. 5 (4:77).
Huko nyuma tulisema kuwa hakuna yoyote anayeifuata haki ila ataitolea thamani kwa nafsi yake na vitu vyake. Vinginevyo watu wa haki na wanaoinusuru, wasingekuwa na ubora wowote. Tazama Juz. 2 (2: 153 – 157), kifungu cha ‘Thamani ya Pepo.’
Kuna Hadith isemayo: “Mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu huogopewa na kila kitu, na asiyemwogopa Mwenyezi Mungu haogopewi na chochote.”
Na itakapokuja nusra kutoka kwa Mola wako lazima watasema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi.
Wao wako pamoja na dini ikiwa ni biashara yenye masilahi, na wao ni maadui wa dini ikiwa itawataka wajitolee muhanga japo kidogo. Kauli fasaha zaidi katika maana haya ni ile ya Bwana wa mashahidi, Husein bin Ali
pale aliposema:“Watu ni watumwa wa dunia na dini wameilamba kwa ndimi zao tu, inachukulika yanapokuwa mazuri maisha yao. Wapatwapo na misukosuko, wenye dini wanakuwa wachache.”
Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:141).
Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliyomo vifuani mwa walimwengu?
Mnataka kumhadaa Mwenyezi Mungu na kumfanyia hila na yeye ni mjuzi wa mnayoficha na mnayoyadhihirisha?
Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale ambao wameamini na kwa yakini atawatambulisha wanafiki.
Umetangulia mfano wake katika Aya 3 ya sura hii na Juz. 4 (4:154).
Na wale ambao wamekufuru waliwaambia walioamini: Fuateni njia yetu nasi tutayabeba makosa yenu.
Washirikina wa Makka waliwaambia wale walioitikia mwito wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
: Vipi mnamfuata Muhammad na kuvumilia mengi kwa ajili yake? Mwacheni na mrudi kwenye dini yetu. Ikiwa mnahofia adhabu ya Mwenyezi Mungu baada ya mauti, kama anavyowahofisha Muhammad, basi sisi tutawabebea. Walisema hivi wakikusudia kuwa ufufuo baada ya mauti ni porojo.
Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo.
Kwa sababu kila mtu atalipwa kwa matendo yake, hatabeba mzigo wa wengine au kuulizwa kwa niaba yake:
قُل لَّا تُسْأَلُونَ عَمَّا أَجْرَمْنَا وَلَا نُسْأَلُ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٢٥﴾
“Sema: hamtaulizwa kwa makosa tuliyoyafanya, wala sisi hatutaulizwa kwa mnayoyatenda nyinyi.” (34:25).
Na kwa hakika wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao.
Kila anayempoteza mwingine atabeba dhambi zake na dhambi za kupoteza; kwa sababu amesababisha kupatikana upotevu na kuenea. Ama yule anayemfuata mpotevu atabeba dhambi zake bila ya kupungua, kwa sababu aliitikia upotevu kwa hiyari yake.
Kwa maneno mengine ni kuwa mpotezaji ana dhambi mbili: Moja kwa upotevu wake na nyingine ni kwa kupoteza. Na mfuasi ana dhambi moja ya kupotea kwa hiyari yake.
Na kwa hakika wataulizwa siku ya Kiyama juu ya waliyoyazua
ya kudai kwao kuwa Mwenyezi Mungu ana mshirika, kusema kwao kuwa Mtume(s.a.w.w)
ni mchawi, kuwaambia waumini kuwa watawabebea dhambi zao n.k.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَلَبِثَ فِيهِمْ أَلْفَ سَنَةٍ إِلَّا خَمْسِينَ عَامًا فَأَخَذَهُمُ الطُّوفَانُ وَهُمْ ظَالِمُونَ ﴿١٤﴾
14. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa kaumu yake, akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini. Basi tufani iliwachukua hali ya kuwa wao ni madhalimu.
فَأَنجَيْنَاهُ وَأَصْحَابَ السَّفِينَةِ وَجَعَلْنَاهَا آيَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٥﴾
15. Tukamwokoa yeye na watu wa safina na tukaifanya kuwa ni ishara kwa walimwengu wote.
NUH
Aya 14 – 15
MAANA
Na hakika tulimtuma Nuhu kwa kaumu yake, akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini. Basi tufani iliwachukua hali ya kuwa wao ni madhalimu. Tukamwokoa yeye na watu wa safina na tukaifanya kuwa ni ishara kwa walimwengu wote.
Dhahiri ya Aya inafahamisha kwa uwazi kuwa Nuhu aliishi miaka 950 na akili hailikitai hilo. Kwa hiyo ni wajibu kulisadiki. Ama kutafuta visababu kwamba siku hizo watu walikuwa wachache ndio maana umri ukarefushwa, kama walivyosema baadhi ya wafasiri, hilo haifai kulitegemea katika kufasiri wahyi.
Katika Kamusi ya Kitabu Kitakatifu imeelezwa kuwa jina la Nuhu ni Samiy na maana yake ni raha na baba yake ndiye aliyemuita hivyo.
Lakini ni lazima ieleweke kuwa jina Samiy linatokana na Sam bin Nuhu, sasa vipi mzazi anasibishwe kwa mwana? Na katika Uk. 448 wa kamusi hiyo hiyo imeelezwa kuwa Sam ni mtoto wa Nuhu na kwamba alizaliwa akiwa Nuhu ana miaka 500. Kamusi haikuasharia tarehe ya wakati wa Nuhu; pengine ni kwa kukosekana rejea. Yametangulia maneno kuhusu Nuhu
katika Aya kadha; zikiwemo: Juz. 8 (7:59 – 64) na Juz.12 (11:25 – 26).