12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾
45. Soma uliyopewa wahyi katika Kitabu. Na usimamishe Swala, hakika Swala inakataza machafu na maovu. Na hakika dhikri (utajo) ya Mwenyezi Mungu ni kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya.
Aya 45
MAANA
Soma uliyopewa wahyi katika Kitabu.
Soma ewe Muhammad, mifano hii tuliyowapigia watu katika Qur’an, huenda wakafahamu na wakawa na takua.
Na usimamishe Swala, hakika swala inakataza machafu na maovu.
Unaweza kuuliza
: Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Swala inamzuia mwenye kuswali kufanya uchafu na mambo mabaya na wala hayafanyi; na lakini inajulikana kuwa wengi wao ni mafasiki; bali baadhi ya wanaoswali wana sera za tabia mbaya kuliko baadhi ya walahidi (wapagani) na washirikina?
Jibu
: Hapana! Hakika dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Swala inamkataza mwenye kuswali asifanye machafu na maovu, inamkataza na kumzuia kwa kauli na mwongozo.
Tofauti ni kubwa baina ya kukataza na kuzuia. Wala hakuna dalili yoyote kuwa mwenye kuswali anakatiza na uchafu na uovu kwa sababu ya Swala.
Hakuna mwenye shaka kuwa kila tamko katika matamko ya Swala na kila harakati katika harakati zake inakataza kumuasi Mwenyezi Mungu na kuamrisha twaa yake.
Kwa maneno mengine ni kuwa swala ni kama Qur’an – inaamrisha na kukataza kisharia sio kimaumbile. Tazama kifungu: ‘Kuumba na kuweka sharia’ katika Juz. 1 (2:26-27).
Ibni Al-arabiy, katika kitabu Futuhatil-makiyya ana maelezo ya ndani na yaliyozama kuhusiana na Aya hii. Ufafanuzi wake ni kuwa mwenye kuswali anakatazwa kusema neno au tendo ambalo linapingana na uhalisi wa Swala na kuivunja, lakini hakatazwi neno au tendo linalooana na Swala; kama kuzidisha tasbih au tahmid katika rukui na sujudi au kutoa sadaqa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu katikati ya Swala; kama alivyofanya Amiru al-mu’minin, Ali
alipotoa sadaka pete yake akiwa amerukui.
Kwa hiyo basi makusudio ya uchafu na uovu ni kila kauli au tendo linalovunja Swala; yaani kila Swala inamwambia mwenye kuswali: ‘chunga!’ Usifanye kitu kitakachonibatilisha na kunitoa kwenye muundo wangu na hakika yangu.
Na hakika dhikri (utajo) ya Mwenyezi Mungu ni kubwa kabisa.
Maana ya dhikri ni kukumbuka. Makusudio sio kuwa dhikri ni kubwa kuliko Swala, kwa sababu hiyo Swala yenyewe ni dhikri; isipokuwa makusudio ni Mwenyezi Mungu anawadhukuru (anawakumbuka) waja wake zaidi kwa upole wake na huruma zake; wakati huo huo naye ni mwenye kukumbukwa sana.
Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkumbukaji kwa kuwa anawakumbuka waja wake kwa rehma zake na upole wake; naye ni Mwenye kukumbukwa, kwa sababu waja wake wanamkumbuka kwa nyoyo zao kiimani na kiikhlasi, kwa ndimi zao kitasbihi na tahlili na kwa vitendo vyao kwa rukui na sujudi. Kwa hiyo Yeye ni mkumbukaji zaidi ya wengine na ni mwenye kumbukwa zaidi ya wengine.
Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya,
ya kheri na shari na kuilipa kila nafsi iliyoyachuma nao hawatadhulumiwa.
وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ وَقُولُوا آمَنَّا بِالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْنَا وَأُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَـٰهُنَا وَإِلَـٰهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ ﴿٤٦﴾
46. Wala usjadiliane na watu wa Kitabu isipokuwa kwa njia iliyo nzuri kabisa. Isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni mmoja na sisi ni wenye kusilimu kwake.
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ فَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَمِنْ هَـٰؤُلَاءِ مَن يُؤْمِنُ بِهِ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا الْكَافِرُونَ ﴿٤٧﴾
47. Na hivyo ndio tumekuteremshia Kitabu. Basi wale ambao tumewapa Kitabu wanakiamini. Na miongoni mwa hao wako wanaokiamini. Na hawazikatai ishara zetu isipokuwa makafiri.
وَمَا كُنتَ تَتْلُو مِن قَبْلِهِ مِن كِتَابٍ وَلَا تَخُطُّهُ بِيَمِينِكَ إِذًا لَّارْتَابَ الْمُبْطِلُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kuume. Ingelikuwa hivyo wangelifanya shaka wabatilifu.
بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا الظَّالِمُونَ ﴿٤٩﴾
49. Bali hicho ni ishara zilizo wazi katika vifua vya waliopewa ilimu; na hawazikatai ishara zetu isipokuwa madhalimu.
MJADALA KWA NJIA NZURI
Aya 46 – 49
MAANA
Njia Ya Mjadala Katika Qur’an
Wala usjadiliane na watu wa Kitabu isipokuwa kwa njia iliyo nzuri kabisa.
Makusudio ya watu wa Kitabu ni mayahudi na manaswara (wakristo). Kujadiliana kwa njia nzuri ni kuwa hoja na dalili ziwe kwa mfumo wa kuvutia sio wa kufukuza, ziwe wazi na sio kufungwa fungwa na kuweko na insafu ya kuusikiliza upande wa pili na kukubaliana nao kwenye lile la haki; ni sawa awe ni katika watu wa Kitabu au wengineo.
Mfano ulio wazi zaidi juu ya hilo ni kauli ya Mwenyezi Mungu kwa washirikina waliosema: “Hakika sisi tuliwakuta baba zetu juu ya desturi; na hakika sisi tunafuata nyayo zao.” Akasema:
أَوَلَوْ جِئْتُكُم بِأَهْدَىٰ مِمَّا وَجَدتُّمْ عَلَيْهِ آبَاءَكُمْ ﴿٢٤﴾
“Hata nikiwaletea yenye muongozo bora kuliko mliyowakuta nayo baba zenu?” (43:24).
Upole huu wa kusema: ‘Hata nikiwaletea yenye muongozo bora’ unavunja hoja na unaingia katika moyo wa mwenye kusikiliza vizuri.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kuwataja watu wa Kitabu, kwa sabubu wao ndio wanaotakiwa kukubali haki haraka kuliko washirikina, kwa vile wao wanamwamini Mungu, malaika wake, vitabu vyake na mitume wake.
Isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao
, ambao ni wale walioifanyia inadi haki na wakang’ang’ania upotevu wala hawajitolei kwa hali yoyote. Basi aina hii ya watu wa kitabu muachane nao wala msijadiliane nao katika dini kabisa.
Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an, yenye hekima, ambazo zinawajadili wapinzani na wabatilifu ataona kuwa njia ya mjadala wa kiqur’ani inakuwa kwenye uhuru wa kiakili katika nyanja zote. Uhuru huu unajitokeza pale Qur’an inapoleta dalili mkataa ya usahihi wa madai yake na wajibu wa kuyaamini:
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ﴿٥٣﴾
“Tutawaonyesha ishara Zetu zilizo katika upeo wa mbali, na katika nafsi zao, mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli.” (41:53).
Vile vile uhuru huu unadhihiri pale Qur’an inapomtaka mpinzani atoe dalili za kuutetea msimamo wake:
قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١١١﴾
“Sema: Leteni dalili zenu, kama nyinyi ni wasema kweli” Juz. 1 (2:111).
ائْتُونِي بِكِتَابٍ مِّن قَبْلِ هَـٰذَا أَوْ أَثَارَةٍ مِّنْ عِلْمٍ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤﴾
“Nileteeni Kitabu kilicho kabla ya hiki au alama yoyote ya ilimu ikiwa mnasema kweli.” (46:4).
وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا ﴿٣٣﴾
“Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo nzuri.”
Juz.21 (25:33).
Huu ndio mjadala wa kiqur’ani ulivyo hasa; kusimamisha hoja kwenye madai yanayohitajia akili, kumtaka hoja anayepinga na kumjibu kwa nguvu ya hoja na fasaha zaidi akiwa ana athari yoyote ya shaka au dalili.
Mtindo huu wa Qur’an umejitokeza kwa mifumo mbali mbali; miongoni mwayo ni hii ifuatayo:
Kutosheka na ubainifu wa jambo na kuchambua maana yake. Qur’an imetumia mfumo huu kuwarudi waabudu masanamu na kuupinga uungu wake; pale ilipoweka wazi kuwa yanashindwa na kitu kidogo:
إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾
“Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu hawatoumba nzi wajapojumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika atakaye na anayetakiwa.” Juz. 17 (22:73).
Yaani vipi mtu anaabudu ambacho hakiwezi kuumba hata nzi?
Vile vile Qur’an imetumia mfumo huu katika kuwarudi wale waliodai kuwa Bwana Masih ni mungu:
مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمُ الْآيَاتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٧٥﴾
“Masih mwana wa Maryam hakuwa ila ni Mtume. Wamepita kabla yake Mitume. Na mama yake ni mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyowabainishia ishara, kisha angalia jinsi wanavyogeuzwa.” Juz. 6 (5:75).
Yaani anayekula chakula ni muhitaji na Mungu huwa hahitaji kitu isipokuwa yeye ndiye anayehitajiwa. Tazama Juz. 6 (5:76 – 81).
Kutoa dalili ya kuweko kitu kwa kuweko msabibashaji: Qur’an imeutumia mfumo huu kufahamisha kuweko Mwenyezi Mungu, katika Aya kadhaa zikiwemo hizi:
أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ ﴿٦﴾
“Je, hawaangalii mbingu zilizo juu yao, vipi tulivyozijenga na tuakazipamba wala hazina nyufa.” (50:6).
Haiwezekani jengo hili lilopangiliwa vizuri na kupambwa na nyota liwe limekuja kwa sadfa. Kwa hiyo imewajibisha kuweko mpangiliaji mwenye hekima. Pia Qur’an imetumia mfumo huu kujulisha umoja wa Mungu pale iliposema:
لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا ﴿٢٢﴾
“Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika.” Juz. 17 (21:22).
Kwamba kuweko wengi kungeleta ufisadi; na kwa kuwa hakuna ufisadi basi sio wengi. Kwa ibara ya watu wa mantiki ni kuwa kutokuweko linalolazimiana, ambalo ni ufisadi, kunafahamisha kutokuweko linalolazimiwa, ambalo ni kuweko na waungu wengi.
Kutoa dalili kwa umwanzo: Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametumia mfumo huu kutoa dalili ya kuweko marejeo ya ufufo katika Aya 27 ya Sura Ar-Rum kwenye Juzuu hii tuliyo nayo: “Naye ndiye ambaye anaanzisha uumbaji kisha ataurudisha na jambo hili ni jepesi zaidi kwake.” Kwamba mwenye kuweza kukifanya kitu bila ya kuweko kitu kingine, basi ana uwezo zaidi kukikusanya tena baada ya kutawanyika.
Mifumo hii yote ni dalili mkataa kwamba mjadala wa kiqur’ani uko kwenye msingi wa kiakili na uhuru wake; na kwamba lengo ni kuidhi- hirisha haki kwa ajili ya kuiamini na kuitumia au kumjibu mwenye kupinga kwa mfumo wa kumkinaisha mwenye kuitafuta haki kwa ajili ya haki.
Na semeni: Tumeamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni mmoja na sisi ni wenye kusilimu kwake.
Maneno yanaelekezwa kwa waislamu. Maana ni kuwa enyi waislamu! Kama ilivyokuwa wajibu kwenu kujadiliana vizuri na yule mnayemtarajia katika watu wa Kitabu, vile vile msiwaonyeshe uadui; bali mchanganyike nao na muwaambie tunayemwabudu sisi ndiye mnayemwabudu nyinyi. Sisi tunamwamini yeye na tunaamini Tawrat iliyoteremshwa kwa Musa na Injil iliyotermshwa kwa Isa; sawa na tunavyoiamini Qur’an iliyoteremshwa kwa Muhammad. Kwa maneno mengine ni: kuweni kwa uislmu ni pambo wala msiwe ni fedheha.
Na hivyo ndio tumekuteremshia Kitabu.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w)
. Makusudio ya Kitabu ni Qur’an. Maana ni kuwa, kama tulivyomteremshia Musa Tawrat na Isa tukamtermshia Injil, kabla yako, vile vile nawe tumekuteremshia Qur’an.
Basi wale ambao tumewapa Kitabu wanakiamini.
Hii ni kuwaishiria wale waliosilimu katika mayahudi na manaswara.
Na miongoni mwa hao wako wanaokiamini.
Ni ishara ya wale waliosilimu katika washirikina wa kiarabu.
Na hawazikatai ishara zetu isipokuwa makafiri.
Unaweza kuuliza kuwa
: kukataa ndio kukufuru; hapo basi maana yatakuwa hawazikatai ila wakataaji; sawa na kusema: Hakai ila mkaaji. Na Qur’an haiko hivi?
Jibu
: Makusudio ni kuwa dalili za ukweli wa Qur’an ziko wazi kiasi ambacho hawezi kuzipinga, isipokuwa aliyeifanya batili ndio dini. Na ukafiri ni itikadi, mwenye nayo haiachi hata kama ubatilifu wake utadhihiri kama jua; sawa na mayahudi walioambiana: “Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu.” Juz. 3 (3:73).
Na hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kuume. Ingelikuwa hivyo wangelifanya shaka wabatilifu.
Wameafikiana wana historia kuwa Muhammad(s.a.w.w)
hakusoma kwa mwalimu yoyote, mkubwa wala mdogo. Lakini pamoja na hivyo ameleta Qur’an iliyo muujiza wa miujiza katika itiakadi yake, sharia yake, mafunzo yake, misingi yake yote, kuwatolea habari mitume waliotangulia na mengineyo.
Hii ni dalili tosha kuwa hiyo ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, haikutengenezwa na mtu.
Lau Mtume(s.a.w.w)
angeliandika na kusoma au akawa amesoma kwa mwalimu, wazushi wangesema kuwa Qur’an imetungwa na Muhammad, si wahyi wa Mwenyezi Mungu.
Kuna mmoja alisema Muhammad(s.a.w.w)
amechukua Qur’an kutoka kwa mtawa wa kinaswara huko Sham. Hatujui ameyatoa wapi haya? Sijui atasemaje kuhusu Aya hizi:
لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ ثَالِثُ ثَلَاثَةٍ ﴿٧٣﴾
“Kwa hakika wamekufuru wale waliosema, Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa utatu.” Juz.6 (5:73).
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣١﴾
“Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam. Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye. Ametakata na wanayomshirikisha nayo.” Juz. 10 (9:31).
Tazama kifungu cha ‘Qur’an na wanaohubiri utatu’ katika Juz. 6 (4:171 – 173).
Bali hicho ni ishara zilizo wazi katika vifua vya waliopewa ilimu; na hawazikatai ishara zetu isipokuwa madhalimu.
Hapana! Qur’an haikutengenezwa na Muhammad(s.a.w.w)
, bali ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanaiamini na kuitegemea wale wanaotafuta ilimu kwa imani ya haki na kuitumia.
Ama wale ambao wameifanya ilimu ni duka la biashara, basi wataipinga, kwa sababu inapiga vita unafiki na ukandamizaji.
وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَاتٌ مِّن رَّبِّهِ قُلْ إِنَّمَا الْآيَاتُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٥٠﴾
50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake? Sema: Hakika ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; na mimi kwa hakika ni muonyaji mwenye kubain- isha tu.
أَوَلَمْ يَكْفِهِمْ أَنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَرَحْمَةً وَذِكْرَىٰ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٥١﴾
51. Je, kwani hayakuwatosha kwamba tumekuteremshia Kitabu wanachosomewa? Hakika katika hiyo kuna rehema na mawaidha kwa watu wanaoamini.
قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ شَهِيدًا يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالَّذِينَ آمَنُوا بِالْبَاطِلِ وَكَفَرُوا بِاللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٥٢﴾
52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yangu na nyinyi, anajua yaliyomo mbinguni na ardhini. Na wale ambao wameamini batili na wakamkufuru, hao ndio waliopata hasara.
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَوْلَا أَجَلٌ مُّسَمًّى لَّجَاءَهُمُ الْعَذَابُ وَلَيَأْتِيَنَّهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na wanakuhimiza adhabu. Na lau si wakati maalum uliowekwa, basi adhabu ingeliwajia na hakika ingeliwatokea ghafla na hali wao hawatambui.
يَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ ﴿٥٤﴾
54. Wanakuhimiza adhabu na hali Jahannam kwa hakika imewazunguka makafiri.
يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٥﴾
55. Siku itakayowafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao na atasema: Onjeni mliyokuwa mkiyatenda.
ISHARA ZIKO KWA MWENYEZI MUNGU
Aya 50 – 55
MAANA
Na walisema: “Mbona hakutermshiwa ishara kutoka kwa Mola wake?” Sema: Hakika ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; na mimi kwa hakika ni muonyaji mwenye kubainisha tu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2: 118-119), Juz. 7 (6:37), Juz. 11 (10:20) na nyinginezo.
Je, kwani hayakuwatosha kwamba tumekuteremshia Kitabu wanachosomewa?
Kila kilichomo ndani ya Kitabu hicho kinashuhudia kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Wao wameshindwa kuleta hata sura mmoja mfano wake. Kimefichua mambo mengi waliyoyadhamiria na kuyaficha; kime- wasimulia visa vya waliopita na wakashuhudia ukweli wake wale wenye insafu katika watu wa Kitabu.
Hayo ni hoja tosha kwa anayeitafuta haki kutoka chimbuko lake. Na washirikina walijikweza na kuifanyia inadi risala ya Muhammad(s.a.w.w)
na hali wana uhakika na hilo. Lililowazuia kufuata haki ni tamaa na manufaa tu.
Hakika katika hiyo kuna rehema na mawaidha kwa watu wanaoamini.
Hiyo ni ishara ya Qur’an nayo ni rehema na neema kwa anayeitumia. Pia ni ukumbusho na mawaidha kwa anayeisadiki na kuamini sharia zake na ishara zake.
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yangu na nyinyi,
anashuhudia na kujua kuwa nimefikisha risala yake na kwamba nyinyi mmeikadhibisha na kuipinga. Vile vileanajua yaliyomo mbinguni na ardhini,
wala hakifichiki kwake chochote.
Na wale ambao wameamini batili na wakamkufuru, hao ndio waliopata hasara.
Kila yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu ni batili na kila mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu huyo ni kafiri aliye fasiki. Yote hayo ni balaa inayostahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na mwisho wake ni Jahannam.
Na wanakuhimiza adhabu. Na lau si wakati maalum uliowekwa, basi adhabu ingeliwajia.
Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
aliwalingania makuraishi kwenye Tawhid na uadilifu, akawahadharisha na mwisho wa shirki na dhulma. Wakasema kwa kung’ang’ania ubatilifu wao: “Haya tuletee adhabu chungu.” Kulikuwako na makuraishi walioona ni bora kuangamia kuliko kumnyenyekea Muhammad kwa kuwa na chuki naye.
Tumewaona watu wengi wakipinga mwito wa haki kwa sababu ya anayetoa mwito huo sio kwa kupinga haki yenyewe.
Basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu wale wanaoihimiza adhabu kwamba Mwenyezi Mungu amekadiria muda maalum wa adhabu yao, lau si hivyo ingeliwajia saa hiyo hiyona hakika ingeliwatokea ghafla na hali wao hawatambui.
Adhabu itawajia tu, lakini ni kwa ghafla bila ya kutambua, ili wazidi machungu juu ya machungu. Uchungu wa kushtukiziwa na uchungu wa adhabu yenyewe.
Wanakuhimiza adhabu na hali Jahannam kwa hakika imewazunguka makafiri.
Wanaharikisha adhabu ya dunia, lakini hawajui kwamba wao wamezungukwa na dhabu kali na kubwa na kwamba itawafikia ghaflasiku itakayowafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao na atasema: Onjeni mliyokuwa mkiyatenda.
Hiyo ni siku ya haki isiyo na shaka; haki itakuwa tu iwe ni sasa au baadaye. Ama moto wa siku hiyo, tunamwomba Mwenyezi Mungu atuepushe nao, utawazunguka pande zote wale walioghadhibikiwa na utaunguza nyama na mifupa na kuwa vumbi; wanarudiwa tena na uhai na moto nao unarudia kazi yake. Hali itaendela kuwa hivyo mpaka pale atakapotaka Mwenyezi Mungu.
Ewe Mola wangu! Najilinda kwako, kwa rehema zako uniepushe na ghadhabu zako na ninkuomba shufaa kwa moyo wangu ulivyojikunja na nasaha na kupenda heri kwa waja wako! Na Wewe ndiwe mjuzi zaidi wa siri zote”.