TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 15831
Pakua: 3361


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 25 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 15831 / Pakua: 3361
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

Mwandishi:
Swahili

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

56. Enyi waja wangu mlioamini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa, basi niabuduni mimi tu.

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ثُمَّ إِلَيْنَا تُرْجَعُونَ ﴿٥٧﴾

57. Kila nafsi itaonja mauti, kisha mtarudishwa kwetu.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿٥٨﴾

58. Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, bila shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yapitiwayo na mito chini yake, wadumu humo. Ni neema iliyoje kwa malipo ya watendaji.

الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٥٩﴾

59. Ambao walisubiri na kwa Mola wao wanategemea.

وَكَأَيِّن مِّن دَابَّةٍ لَّا تَحْمِلُ رِزْقَهَا اللَّـهُ يَرْزُقُهَا وَإِيَّاكُمْ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٦٠﴾

60. Wanyama wangapi hawabebi riziki zao. Mwenyezi Mungu anawaruzuku wao na nyinyi. Na Yeye ni Msikizi, Mjuzi.

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٦١﴾

61. Na ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu. Basi wanageuzwa wapi?

اللَّـهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٦٢﴾

62. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake na humdhikisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّن نَّزَّلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ مِن بَعْدِ مَوْتِهَا لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ ﴿٦٣﴾

63. Na ukiwauliza ni nani aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdulillah (sifa njema ni za Mwenyezi Mungu), Bali wengi wao hawafahamu.

WANYAMA WANGAPI HAWABEBI RIZIKI ZAO

Aya 56 – 63

MAANA

Enyi waja wangu mlioamini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa, basi niabuduni mimi tu.

Wameafikiana mafaqihi kuwa haijuzu kwa Mwislamu kukaa katika mji ambao itakuwa uzito kwake kutekeleza wajibu wa kidini; kama vile Swala na mfano wake; hata kama mji huo ndio nyumbani kwake; na kwamba ni lazima ahame kwenda mahali pengine atakapoweza kutekeleza hayo. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi maudhui haya katika Juz. 5 (4:97) kifungu ‘Mafaqihi na wajibu wa hijra’.

Kila nafsi itaonja mauti, kisha mtarudishwa kwetu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwajibisha kuhama mji uliotajwa, alisema kuwa anayehofia kufa uhamishoni, basi hawezi kuokoka na mauti popote pale alipo, nyumbani au ugenini. Na baada ya kufa ataulizwa wajibu aliouacha na mambo ya haramu aliyoyafanya; yakiwemo kukaa kwenye mji anaolazimika kuacha ibada na kunywa pombe.

Na wale ambao wameamini na wakatenda mema, bila shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yapitiwayo na mito chini yake wadumu humo.

Atakayetoka nyumbani kwake kwa kufanya Hijra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Mungu atampa badali bora zaidi yake – ghorofa, miti, na mito katika nyumba na makazi ya amani.

Ni neema iliyoje kwa malipo ya watendaji. Ambao walisubiri na kwa Mola wao wanategemea.

Kuna malipo gani zaidi ya Pepo? Kwa vile ni adhimu basi nayo thamani yake iko ghali na adhimu. Thamani yenyewe ni: kukataa kujisalimisha kwa maadui wa Mwenyezi Mungu, kutomhofia yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake na kuwa na subira kwa ajili yake katika matukio yote, vyovyote yatakavyokuwa.

RIZIKI NA KUMTEGEMEA MUUMBA NA SI KIUMBE

Wanyama wangapi hawabebi riziki zao. Mwenyezi Mungu anawaruzuku wao na nyinyi. Na Yeye ni Msikizi, Mjuzi.

Watu wengi wanamwamini Mwenyezi Mungu kinadharia; kwamba riziki za viumbe ziko mikononi mwake Yeye peke yake, kwamba hazina yake haishi wala haina ukomo na kwamba Yeye ni mkarimu, hakosi kitu anayemwamini na kumtegemea Yeye.

Wanaamini haya yote kinadharia, lakini wanamkana Mungu kimatendo; wanamtegea kumbe badala ya Muumba na wanajikurubisha kwa kimbe kwa mambo yanayoiondoa dini yao na dhamiri yao kwa kuwa na tamaa ya vilivyo mikononi mwake na wanajiweka mbali na Mwenyezi Mungu wakikata tamaa naye na hazina yake.

Aya hii inamkemea mumin huyu aliye kafiri.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni Muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake, aina zote za sababu za riziki zinakomea kwake; nazo ziko tayari kwa kila mwenye kuzitaka na kuzihangaikia. Ikiwa zitakuwa nzito basi zinajiandaa kwa mhitaji kwa ubora zaidi bila ya kutambua; bali viumbe hai vingi haviifanyii kazi riziki wala kuibeba, lakini inawajia pale wanapoihitajia.

Hapa kuna mazingatio kwa vibaraka wahaini na kila mwenye kuiuza dini yake kwa shetani na akayafanya maasi ndio nyenzo ya kupata tonge.

Hasha! Haiwezekeni kwa Mwenyezi Mungu kukataza kitu na azuie sababu za riziki. Vipi iwe hivyo na hali dini yake ni dini ya maisha? Imam Ali(a.s) anasema:“Hakika lile mliloamrishwa lina wasaa zaidi kuliko lile mlilokatazwa na mliyohalalishiwa ni mengi zaidi ya mliyoharamishiwa. Basi acheni yaliyo machache kwa ajili ya yaliyo mengi. Na yaliyo dhiki kwa ajili ya yaliyo na wasaa.”

Akasema tena: “Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni maumbile mawili katika viumbe vya Mwenyezi Mungu na kwamba hayo hayakarubishi ajali wala hayapunguzi riziki.”

Huko nyuma tumeweka wazi tofauti baina ya imani ya kweli na imani ya mawazo. Kwamba imani ya kweli ni ile iliyothibiti kwenye moyo na ikaleta kumhofia Mwenyezi Mungu na kujihimu na twaa yake na radhi yake kwa kauli na vitendo.

Lakini imani ya kuwazia haithibiti moyoni; isipokuwa imerambwa na ulimi, na inakuwa ni ya kuwazia tu, sawa na njozi. Ushahidi mkubwa wa imani hii ya kombokombo ni kuwa mtu anamwamini Mwenyezi Mungu kwa kauli na huku anamtarajia kiumbe na kumhofia badala ya Mwenyezi Mungu.

Na ukiwauliza ni nani aliyemba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu.

Wanaoulizwa ni wapenda anasa waliokaidi risala ya Muhammad(s.a.w.w) .

Unaweza kuuliza : ikiwa wanakubali waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye muumba wa ulimwengu, basi iko wapi sababu ya kupin- gana kwao na mitume?

Jibu : Kimsingi wao wanamkubali Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyewahusu wao kwa mali na utawala na akawachagulia wengine ufukara na utumwa.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu na akaamini kuwa watu wana anayostahiki juu yake na yeye ana anayostahiki juu ya watu, basi huyu ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko huyo anayeamini bila ya matendo

Dalili ya kuwa wao wanamkubali Mwenyezi Mungu kwenye msingi huu ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na wanapoambiwa: Toeni katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu, wale waliokufuru huwambia walioamini: Je, tumlishe ambaye Mwenyezi Mungu akipenda atamlisha? Nyinyi hammo ila katika upotevu dhahiri” (36:47).

Basi wanageuzwa wapi?

Wanaigeuka haki kwa kuzua kuwa Mwenyezi Mungu amewahusu wao tu kuwa na mali kuliko wengine wote.

Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake na humdhikisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:26).

Na ukiwauliza ni nani aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake, bila shaka watasema ni Mwenyezi Mungu.

Wakiulizwa kuhusu mumbaji wa ulimwengu wanajibu kwa kukabali kuwa ni Mwenyezi Mungu lakini kwa masharti yao. Na wakiulizwa aliyeteremsha maji na akahuisha ardhi, ambayo ndiyo sababu ya moja kwa moja ya riziki na utajiri ulio mikononi mwao, pia wanasema na kukubali kuwa ni Mwenyezi Mungu peke yake.

Hapo wanajipinga wao wenyewe. Ikiwa sababu za riziki ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na si mikononi mwao, itakuwaje iwe yao tu peke yao na wengine wasipate? Ikiwa Mwenyezi Mungu ni wa wote, vipi heri zake na baraka zake?

Sema: Alhamdulillah (sifa njema ni za Mwenyezi Mungu), ambaye ameidhihirisha haki hata kupitia mdomoni mwa maadui zake wazushi.

Bali wengi wao hawafahamu kwamba wao ni waongo na wazushi wakijipinga wao wenyewe kwa wenyewe.

وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾

64. Na maisha haya ya dunia si chochote ila ni upuuzi na mchezo. Na nyumba ya akhera ndiyo maisha hasa, lau wangelikuwa wanajua.

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ ﴿٦٥﴾

65. Na wanapopanda katika jahazi, humwomba kwa kumsafia utiifu, lakini anapowavua wakafika nchi kavu mara wanamshirikisha.

لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ وَلِيَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٦٦﴾

66. Ili wapate kuyakana tuliyowapa na wapate kustarehe, punde watajua.

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَةِ اللَّـهِ يَكْفُرُونَ ﴿٦٧﴾

67. Je, hawaoni kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani na hali watu wa pambizoni mwake wananyakuliwa. Je, wataamini batili na kuzikataa neema za Mwenyezi Mungu?

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ ﴿٦٨﴾

68. Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo. Au akadhibishaye haki inapomjia? Je, si katika Jahannam ndio yatakuwa makazi ya makafiri?

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا وَإِنَّ اللَّـهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٦٩﴾

69. Na wale wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, hakika tutawaongoza kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wema.

DUNIA NI UPUUZI NA MCHEZO

Aya 64 – 69

MAANA

Na maisha haya ya dunia si chochote ila ni upuuzi na mchezo.

Makusudio ya dunia hapa ni dunia ya uzembe, uovu, kujifaharisha na israfu kwa hisabu ya wanyonge. Vile vile dunia ya wakoloni na wazayuni waundaji wa mauti, njama za kiuadui na mapinduzi ya kijinga. Dunia ya mashirika ya ulanguzi, unyonyaji, na kuifanyia biashara dini.

Dunia ya vyombo vya habari vya kulipwa ili kutia sumu kwenye fikra na kuvungavunga kuuficha ukweli na propaganda za uwongo.

Hii ndio dunia ya mchezo, ufisadi shari na upotevu, inayomchukiza Mwenyezi Mungu na kuwaandalia wakazi wake adhabu ya kuunguza. Ama dunia ya watu wema, walio huru, waungwana ambao wanaleta masilahi katika nchi na sio ufisadi. Hii ndio dunia ya haki, heri, uongofu na kufaulu ambayo wakazi wake watapata radhi za Mwenyezi Mungu na kufuzu kwa neema yake na Pepo yake.

Na nyumba ya akhera ndiyo maisha hasa, lau wangelikuwa wanajua.

Tunaifasiri kwa kauli yake Imam Ali(a.s) :“Kila neema isiyokuwa Pepo ni upuzi na kila balaa isiyokuwa moto ni faraja.” Na kauli yake katika wasifa wa Pepo “Haikatiki neema yake, haondoki mkazi wake, hazeeki anayedumu humo, wala kukata tamaa anayekaa humo.”

Na wanapopanda katika jahazi, humwomba kwa kumsafia utiifu, lakini anapowavua wakafika nchi kavu mara wanamshirikisha.

Inasemekana kuwa watu wa wakati wa jahiliya walikuwa wanaposafiri baharini huchukua masanamu yao. Dhoruba ikawakumba wanayatupa masanamu na kusema: Yarabi yarabi! (Ewe Mola ewe Mola!). Hili si ajabu. Wengine walikuwa wakitengeneza sanamu ya tende, wakishikwa na njaa wanaila.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:22). Ni vizuri kurudia tuliyoyaandika huko kwenye kifungu ‘Mwenyezi Mungu na maumbile.’

Ili wapate kuyakana tuliyowapa na wapate kustarehe, punde watajua.

Yaani wapate kuacha kushukuru kwa neema ya kuokoka aliyoaneemesha Mwenyezi Mungu kwa ukarimu wake na upole. Basi wataona hizaya ya adhabu itakayowapata kesho.

Je, hawaoni kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani na hali watu wa pambizoni mwake wananyakuliwa.

Wanaambiwa washirikina wa Makka ambao wamempiga vita Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Hiyo ni kutokana na neno ‘Nchi takatifu ina amani.’ Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakumbusha yale aliyowahusu nayo kuliko watu wengine; kwa kukaa katika mji wenye amani ya nafsi na mali; na jirani zao wanaishi na hofu na wasiwasi wa maisha yao na vitu vyao.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:125), Juz. 4 (3:97) na Juz. 20 (28:57).

Je, wataamini batili na kuzikataa neema za Mwenyezi Mungu?

Kila anayenyenyekea batili na akaridhia yasiyokuwa haki kwa tamaa ya dunia, basi yeye ni katika anayeamini batili na kuzikana fadhila za Mwenyezi Mungu na hisani yake.

Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo. Au akadhibishaye haki inapomjia? Je, si katika Jahannam ndio yatakuwa makazi ya makafiri?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:21).

Na wale wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, hakika tutawongoza kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wema.

Juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni mambo mengi; miongoni mwayo ni: kutafuta ilimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kutafuta maisha kwa jasho, kuamrisha mema na kukataza maovu. Ilivyeo bora kabisa kuliko yote ni kuisafisha ardhi na madhalimu na wafisadi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwongoza kwenye haki kila Mwenye kum- fanyia ikhlasi katika nia yake na akafanya uzuri katika matendo yake, wala hamuongozi Mwenye kufanya israfu aliye muongo.

14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Sura Ya Thelathini: Surat Ar-Rum. Imeshuka Makka ina Aya 60

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.

الم ﴿١﴾

1. Alif Laam Miim.

غُلِبَتِ الرُّومُ ﴿٢﴾

2. Warumi wameshindwa.

فِي أَدْنَى الْأَرْضِ وَهُم مِّن بَعْدِ غَلَبِهِمْ سَيَغْلِبُونَ ﴿٣﴾

3. Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda.

فِي بِضْعِ سِنِينَ لِلَّـهِ الْأَمْرُ مِن قَبْلُ وَمِن بَعْدُ وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ ﴿٤﴾

4. Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo waumini watafurahi.

بِنَصْرِ اللَّـهِ يَنصُرُ مَن يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٥﴾

5. Kwa nusra ya Mwenyezi Mungu. Humnusuru amatakaye; na Yeye ndiye Mwenye uwezo, Mwenye kurehemu.

وَعْدَ اللَّـهِ لَا يُخْلِفُ اللَّـهُ وَعْدَهُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٦﴾

6. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake, lakini watu wengi hawajui.

يَعْلَمُونَ ظَاهِرًا مِّنَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ عَنِ الْآخِرَةِ هُمْ غَافِلُونَ ﴿٧﴾

7. Wanajua dhahiri ya maisha ya dunia na wameghafilika na Akhera.

WAROMA WAMESHINDWA

Aya 1 – 7

MAANA

Alif Laam Miim.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).

Warumi wameshindwa katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda katika miaka michache.

Huko nyuma tumetaja aina za miujiza ya Qur’an; miongoni mwazo ni:

• Kushindwa washirikina kuleta mfano wake japo Sura moja tu.

• Itikadi yake ya kumwamini Mungu na mongozo wake unaoleta maendeleo ya mtu na sharia yake inayotekeleza mahitaji yote ya watu, mahali popote na wakati wowote. Pia kukubaliana na sharia za kutungwa zenye masilahi ya watu kwa namna fulani. Na inajulikana kuwa aliyezifikisha sharia hizo hakukaa kwa mwalimu.

• Maneno ya Mwenyezi Mungu yanachukua njia nyingi, kinyume na maneno ya binadamu. Tumegundua wakati tukitafsiri Aya zake, kuwa siri ya hilo ni ukuu wa mwenye kusema na elimu yake isiyolinganishwa na chochote. Tazama Juz. 18 (24:55), kifungu cha: ‘Njia nyingine ya muujiza wa Qur’an.’

Muujiza mwingine wa Qur’an unaojitokeza ni kutoa habari za mambo yaliyofichikana ambayo hayajui isipokuwa mjuzi wa ghaibu; kama kufichua wanayoyadhamiria wanafiki katika nyoyo zao, ushindi wa Mtume kwa maadui zake, kujitokeza Uislamu juu ya dini zote, kurudi Mtume Makka akiwa ni mshindi baada ya kufukuzwa.

Pia kutolea habari yatakayowatokea maswahaba zake baada yake, kuhusu mayahudi na tabia yao na ushindi wa manaswara wa Roma juu wafursi baada ya miaka kadhaa ya ushindi wa Fursi juu ya Roma. Aya tuliyo nayo inazungumzia tukio hili; kama walivyokubaliana wapokezi na wafasiri wote.

Muhtasari wa tukio hilo ni: Wafursi walikuwa kwenye dini ya kimajusi, hawana Kitabu kama washirikina. Warumi walikuwa kwenye dini ya kinaswara (wakiristo) na walikuwa na Kitabu kama waislamu.

Katika zama za Mtume Muhammad(s.a.w.w) kulitokea vita baina ya Fursi na Rumi katika nchi ya Sham. Washirikina walikuwa wanapendelea upande wa Fursi kwa vile walikuwa washirikina kama wao; na waislamu walipendelea upande wa Rumi kwa sababu wana Kitabu.

Basi zikaja habari za ushindi wa Fursi, waislamu wakaona tabu na washirikina wakaona raha, wakiwaambia waislamu: Wafursi wasio na kitabu wamewashinda warumi watu wa Kitabu. Nyinyi mnadai kuwa mtashinda kwa Kitabu alichoteremshiwa Mtume wenu! Basi sisi tusio na kitabu ndio tutakaowashinda; kama ilivyotokea kwa wafursi na warumi.

Ndio ikashuka Aya hii. Haukupita muda wa miaka tisa ndipo Mwenyezi Mungu akadhihirisha ushindi wa warumi juu ya wafursi. Basi wakafurahi waislamu na wakahuzunika washirikina.

Hapa ndio inakuwa siri ya muujiza wa Qur’an, ambapo ilitolea habari za uhakika sio kubahatisha, kuwa vita vitaanza tena baina ya Fursi na Roma na vitamalizika kwa ushindi wa Roma. Na ikaelezea hata wakati. Neno ‘miaka michache’ limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu ‘Bidh’i’ lenye maana ya idadi baina ya tatu na kumi.

Basi ikawa kama ilivyosema Qur’an. Ghaibu hii iliyofichika, haijui ila Mwenyezi Mungu peke yake.

Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake.

Yaani kabla ya ushindi na baada ya ushindi na ni kwake pekee yanarejeshwa mambo yote.

Na siku hiyo waumini watafurahi kwa nusra ya Mwenyezi Mungu.

Watafurahi waislamu siku warumi watakapowashinda wafursi.

Humnusuru amatakaye.

Wawili wakipigana, yule mwenye sababu za kushinda ndiye mshindi, awe na haki au ubatilifu. Mwenyezi Mungu ametegemeza kwake ushindi kwa kuangalia kuwa sababu zote za kilimwengu zinakomea kwake, kwa vile Yeye ndiye Muumba wa ulimwengu na yaliyomo ndani yake.

Na Yeye ndiye Mwenye uwezo, Mwenye kurehemu.

Anamwadhibu dhalimu na kumhurumia mdhulumiwa.

Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake, lakini watu wengi hawajui.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutoa habari za ghaibu, za ushindi wa warumi kwa wafursi, alisisitiza kuwa hilo litatokea tu. Lakini asiyemwamini Mwenyezi Mungu ataamini vipi ahadi yake?

Msisitizo wa uhakika ni ushahidi mkubwa kuwa Qur’an ni wahyi kutoka kwa ambaye kwake ulimwengu wa ghaibu na wa dhahiri ni sawa tu. Lau ingelitokea kinyume, basi maadui wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) wangeliifanya hiyo ni nyenzo ya kuutuhumu ukweli na ujumbe wake.

Wanajua dhahiri ya maisha ya dunia na wameghafilika na Akhera.

Dunia na hali zake ni ulimwengu wa dhahiri unajulikana kwa hisia tano; na Akhera na vituko vyake ni ulimwengu wa ghaibu, haujulikani ila kwa njia ya wahyi na wao hawauamini, basi watajuaje mambo ya Akhera.

أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِم مَّا خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُّسَمًّى وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ لَكَافِرُونَ ﴿٨﴾

8. Je, hawafikiri katika nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake ila kwa haki. Na kwa hakika watu wengi ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao.

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَأَثَارُوا الْأَرْضَ وَعَمَرُوهَا أَكْثَرَ مِمَّا عَمَرُوهَا وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٩﴾

9. Je hawatembei katika ardhi wakaona ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakiilima ardhi na kuistawisha zaidi kuliko walivyoistawisha wao. Na mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu wenyewe.

ثُمَّ كَانَ عَاقِبَةَ الَّذِينَ أَسَاءُوا السُّوأَىٰ أَن كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ وَكَانُوا بِهَا يَسْتَهْزِئُونَ ﴿١٠﴾

10. Kisha ukawa mwisho wa waliofanya ubaya ni kuzikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na wakawa wanazifanyia stihzai.

اللَّـهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿١١﴾

11. Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji na kisha akaurudisha. Na kisha mtarejeshwa kwake.

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يُبْلِسُ الْمُجْرِمُونَ ﴿١٢﴾

12. Na siku itakaposimama Saa wakosefu watakata tamaa.

وَلَمْ يَكُن لَّهُم مِّن شُرَكَائِهِمْ شُفَعَاءُ وَكَانُوا بِشُرَكَائِهِمْ كَافِرِينَ ﴿١٣﴾

13. Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa waliokuwa wakiwashirikisha nao watawakana washirika wao.

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَتَفَرَّقُونَ ﴿١٤﴾

14. Na siku itakaposimama Saa, siku hiyo watagawanyika.

فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَهُمْ فِي رَوْضَةٍ يُحْبَرُونَ ﴿١٥﴾

15. Ama wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani wakifurahishwa.

وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَلِقَاءِ الْآخِرَةِ فَأُولَـٰئِكَ فِي الْعَذَابِ مُحْضَرُونَ ﴿١٦﴾

16. Na ama wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu na mkutano wa Akhera, basi hao watahudhurishwa katika adhabu.

HAWAFIKIRII NAFSI ZAO

Aya 8 – 16

MAANA

Je, hawafikiri katika nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake ila kwa haki.

Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima haumbi kitu chochote isipokuwa kwa haki, na upuuzi kwake ni muhali. Yeye ni Muweza wa kuwarudishia watu uhai baada ya kwisha muda wake uliopangwa.

Mwenye kuangalia vizuri ukuu wa ulimwengu atatambua hekima ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wake na atatambua uweza wake wa kufufua wafu. Kwa sababu kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa kuliko kumrudishia uhai mtu baada ya mauti.

“Je! hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi na hakuchoka kwa kuziumba, ana uwezo wa kuwafufua wafu? Ndio! Hakika yeye ni muweza wa kil kitu” (46:33).

Na kwa hakika watu wengi ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao.

Wanakataa kuwa ana uweza wa kurudisha uhai na hawajui kwamba anayeweza kuuanzisha anaweza pia kuurudisha? Kwa vile sababu ni moja tu.

Je hawatembei katika ardhi wakaona ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:137).

Na wakiilima ardhi na kuistawisha zaidi kuliko walivyoistawisha wao. Na mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu wenyewe.

Watu wa umma zilizopita walikuwa na maendeleo zaidi ya kilimo na majumba kuliko waarabu, lakini walipodhulumu nafsi zao kwa kufuru yao na kuwakadhibisha kwao mitume, Mwenyezi Mungu aliwapatiliza kwa adhabu na maangamizi. Je, hawaogopi wanaomkadhibisha Muhammad kuwapata yaliyowapata waliokuwa na nguvu zaidi.

Kisha ukawa mwisho wa waliofanya ubaya ni kuzikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na wakawa wanazifanyia stihzai.

Mitume wao waliwajia kwa ubainifu ili wawaokoe na upotevu na kuangamia. Wakawafanyia uovu kwa kuwakadhibisha na kuwafanyia stihizai. Ikawa malipo yao ni adhabu na marejeo mabaya.

Mwenyezi Mungu huaanzisha uumbaji na kisha akaurudisha. Na kisha mtarejeshwa kwake.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 20 (29:19).

Na siku itakaposimama Saa wakosefu watakata tamaa.

Siku hiyo ya Kiyama watajua wenye makosa kwamba hakuna mategemeo wala ujanja kwa aliyetanguliza maasi na kuipa muda toba. Wataonja uchungu wa kukata tamaa kwa sababu walizama kwenye upotevu na wakaung’ang’ania.

Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa waliokuwa wakiwashirikisha nao watawakana washirika wao.

Walikuwa na wale wanaowashirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu duni- ani, wakiwafuata kwenye upotevu na ufisadi kwa ujinga na uigizaji. Walikuwa wakiwatarajia kuwanufaisha na kuwaombea siku ya Kiyama. Lakini watakapokusanyika kwa Mwenyezi Mungu wote na kuiona adhabu na kuhakikisha kuwa hakuna utetezi, basi hapo mfuaswa atajitenga na mfuasi na kiongozi na anayeongozwa.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:166 – 167).

Na siku itakaposimama Saa, siku hiyo watagawanyika.

Yaani watagawanyika, wengine ni wa Peponi na wengine ni wa motoni. Yaani wao duniani walikuwa wakikutana sokoni kwenye vyama, masomoni, sehemu za ibada n.k. Lakini siku ya Kiyama hakuna tena makutano.

Ama wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani wakifurahishwa. Na ama wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu na mkutano wa Akhera, basi hao watahudhurishwa katika adhabu.

Mwenyezi Mungu kesho atawafufua viumbe, awakusanye kwa maswali anayotaka kuwauliza, kisha atawafanya makundi mawili: Kundi la watu wa shirki na la watu wa heri. Hawa atawaneemesha kwa makazi mazuri na Pepo zenye neema; na wale atawaadhibu kwa kuwatia katika moto wa Jahannam.

فَسُبْحَانَ اللَّـهِ حِينَ تُمْسُونَ وَحِينَ تُصْبِحُونَ ﴿١٧﴾

17. Basi mtakaseni Mwenyezi Mungu mnapofikia jioni na mnapofikia asubuhi.

وَلَهُ الْحَمْدُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَعَشِيًّا وَحِينَ تُظْهِرُونَ ﴿١٨﴾

18. Na sifa njema zote ni zake katika mbingu na ardhi na jioni na mnapofikia mchana.

يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَيُحْيِي الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَكَذَٰلِكَ تُخْرَجُونَ ﴿١٩﴾

19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilichokufa, na hukitoa kilichokufa kutokana na kilicho hai. Na huhuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtakavyotolewa.

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ إِذَا أَنتُم بَشَرٌ تَنتَشِرُونَ ﴿٢٠﴾

20. Na katika ishara zake ni kuwa amewaumba kwa udongo; kisha mmekuwa watu mnaoenea.

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١﴾

21. Na katika ishara zake ni kuwaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu. Ili mpate utulivu kwao. Na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri.

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافُ أَلْسِنَتِكُمْ وَأَلْوَانِكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْعَالِمِينَ ﴿٢٢﴾

22. Na katika ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi. Na kutofautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa wenye elimu.

وَمِنْ آيَاتِهِ مَنَامُكُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَابْتِغَاؤُكُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ ﴿٢٣﴾

23. Na katika ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia.

وَمِنْ آيَاتِهِ يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَيُحْيِي بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٢٤﴾

24. Na katika Ishara zake ni kuwaonyesha umeme kwa hofu na tamaa, na kuwateremshia maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye akili.

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ ثُمَّ إِذَا دَعَاكُمْ دَعْوَةً مِّنَ الْأَرْضِ إِذَا أَنتُمْ تَخْرُجُونَ ﴿٢٥﴾

25. Na katika Ishara zake ni kusimama mbingu kwa amri yake. Kisha atakapowaita mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.

USHAHIDI WA ULIMWENGU NA KUUMBWA MTU

Aya 17 – 25

MAANA

Basi mtakaseni Mwenyezi Mungu mnapofikia jioni na mnapofikia asubuhi. Na sifa njema zote ni zake katika mbingu na ardhi na jioni na na mnapofikia mchana.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja watu wa Peponi na watu wa Motoni, anatoa amri ya kutukuzwa kwake asubuhi, jioni, mchana na usiku pia. Kwani Hakika Yeye Mwenyezi Mungu ni msifiwa mbinguni na ardhini.

Kuna riwaya moja inayosema kuwa Suleiman Bin Daud, siku moja alimpi- tia mkulima akasema: “Hakika Bin Daud amepewa ufalme mkubwa.”

Suleiman akamwambia: “Tasbih moja tu anayoikubali Mwenyezi Mungu ni bora kuliko waliyopewa ukoo wa Daud.”

Kwenye Nahjul-balagha, imeelezwa: “Mwenyezi Mungu Amejaalia Alhamdu (kusifiwa na sifa njema) ni ufunguo wa utajo wake na ni sababu ya kuzidi fadhila zake na ni dalili ya uungu wake na utukufu wake.

Hukitoa kilicho hai kutokana na kilichokufa, na hukitoa kilichokufa kutokana na kilicho hai. Na huhuisha ardhi baada ya kufa kwake.

Wanaoamini mada wanasema kuwa mada ndiyo iliyoleta uhai, usikikizi, nyoyo n.k. Kama yangekuwa sahihi haya, basi ingelikuwa kila mada inaona, kusikia na kuwa na akili. Kwa sababu vinavyohusiana na kitu ni lazima viwe navyo wakati wowote. Na kwa kuwa tunaona mada nyingine zina uhai na nyingine hazina, basi tumejua kwamba kuna nguvu nyuma ya mada inayompa uhai amtakaye na kutompa amtakaye.

Na kama hivyo ndivyo mtakavyotolewa.

Yaani kufufuliwa. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu ameitoa mimea hai kutokana na ardhi iliyokufa, atamtoa mtu hai kutoka kaburini kwake. Kwa maneno mengine ni kuwa; kama ambavyo alimpa uhai baada ya kuwa si chochote, vilevile atampa uhai mara nyingine baada ya kuwa ni mchanga na mifupa. Basi je, kuna ajabu gani?

Tazama Juz. 7 (6:95 – 99) na Juz. 13 (13:5 – 7) kifungu cha ‘Waanaoamini mada na maisha baada ya mauti.’

Na katika ishara zake ni kuwa amewaumba kwa udongo; kisha mmekuwa watu mnaoenea.

Mwenyezi Mungu amemuumba mtu wa kwanza kutokana na udongo na watu wote wametokana na yeye. Vile vile chakula chao kinachowafanya waishi kinatokana na udongo.

Kwa hiyo, udongo ndio sababu ya kupatikana mtu na kubakia kwake na kuendelea kwake. Vipi mchanga umekuwa mtu mwenye usikizi, uoni, akili, ubainifu, utashi na nguvu zinazofanya maajabu mengi na kuleta maendeleo?

Je, haya ni matengenezo ya sadfa au mada? Na waseme wapinzani watakavyo, lakini akili haiamini isipokuwa kuweko ambaye hana mfano na kitu chochote na ni Mjuzi, Mwenye hekima.

NDOA YA KI-QUR’AN

Na katika ishara zake ni kuwaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu. Ili mpate utulivu kwao. Na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu.

Maana ya ‘Kutokana na nafsi zenu’ ni jinsi yenu na maumbo yenu; mkibadilishana upendo kwa upendo na utulivu kwa utulivu. Wakale walisema: “Kila shepu inazoena na shepu inayofanana nayo.” Lau mke angelikuwa wa jinsi nyingine inayotofautiana na jinsi ya mume, ingelikuwa vigumu kufahamiana na kushirikiana. Kila mmoja angejiona ni mgeni kwa mwenzake na yuko mbali na tabia yake na hulka yake. Tazama Juz. 4 (4:19 – 21) kifungu cha ‘Ndoa ni kubadilishana roho kwa roho.’

Ya kushangaza ni kauli ya baadhi ya wafasiri waliosema kuwa makusudio ya mapenzi ni kujamiiana; na huruma ni mtoto. Hii inafahamisha tu kuwa wafasiri hao wameelemea zaidi upande wa mambo ya kijinsiya na kumuona mwanamke kuwa ni chombo cha kuzaa watoto tu.

Qur’an Tukufu imeabainisha lengo la ndoa kuwa ni kuzoeana, kuhurumiana, uadilifu na usawa; sio baina ya mume na mke tu, bali familia nzima kwa ujumla. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Enyi watu! Mcheni Mwenyezi Mungu ambaye amewaumba kutokana na nafsi moja.

Na akamuumba mkewe katika nafsi hiyo na akaeneza, kutokana na hao wawili, wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana na ndugu wa damu; hakika Mwenyezi Mungu anawachunga.” Juz. 4 (4:1).

Lengo la kumcha Mwenyezi Mungu katika Aya hii ni kila mmoja katika familia atekeleze haki ya mwenzake, ili familia iwe na maisha mazuri yasiyokuwa na misukosuko wala vikwazo. Inajulikana wazi kuwa familia njema ndio msingi wa jamii njema.

Si vibaya kudokeza kuwa ni Sunna kusoma khutuba ya ndoa wakati wa kutaka kuoa, na wakati wa kusomwa tamko la ndoa kwa kumwiga Mtume(s.a.w.w) na kizazi chake. Khutba yenyewe inakuwa ni kumhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu, shahada mbili, kumswalia Mtume na kizazi chake, kuwausia watu takua na kuwaombea Mungu wana ndoa. Imepokewa Hadith kutoka kwa Imam Zainul-abidin: “Mwenye kumhimidi Mwenyezi Mungu amehutubia.”

Vile vile ni Sunna kutabaruku kwa kusoma Aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume wake Mtukufu. Hii imekuwa ni desturi ya wahenga na wa sasa.

Huwa kabla ya kufungisha ndoa wanasoma Aya hii tuliyo nayo. Na katika Hadith wanasoma “Owaneni mtapata kizazi na kuwa wengi. Kwani mimi nitajifaharisha kwa umma nyingine siku ya Kiyama hata kwa mimba iliyoharibika.”

Tumesema kuwa Aya na Hadith hizi zinasomwa kwa kutabaruku tu. Ni makosa kudhaniwa kuwa tabia njema na adabu za Qur’an zitapatikana kwa kusoma Hadith na Aya. Hapana! Tabia njema na adabu zitakuwa kwa malezi tu ya kumlea mtoto ki-qur’ani tangu udogoni; jambo ambalo litampelekea kufahamu lengo alilolikusudia Mwenyezi Mungu katika ndoa.

Ama kuwalea watoto juu ya kupenda mali na kujifharisha na mambo ya kujionyesha ya upuuzi; kama mama kumwambia binti yake: Mungu akujalie upate mume tajiri au baba kumpa nasaha mwanawe kuoa binti wa waziri au wa mfanya biashara mkubwa, malezi haya hayafaidiwi chochote na kusoma Qur’an wala Hadithi.

Hadithi ya owaneni mtapata kizazi, haina shaka yoyote katika usahihi wake, lakini Bwana wa Mitume(s.a.w.w) atajifaharisha kwa waumini wenye takua na wapigania jihadi waungwana na vile vile kwa mimba iliyoharibika. Na atajitenga na waovu wenye ufuska katika vijana wa kike na wa kiume, ambao dini haiwakanyi na lolote.

Vile vile atajitenga na wahaini na vibaraka walio maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu. Kuna Hadith isemayo: “Kwa hakika watu watafikiwa na wakati ambao mtu hatasalimika na dini ila kwa kukimbia kutoka kilele kimoja hadi kingine.” Wakasema: “Yatakuwa lini hayo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: ”Itakapokuwa mtu hapati maisha ila kwa kumuasi Mwenyezi Mungu, basi wakati huo itakuwa halali useja.”

Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri.

Lengo la ndoa ni utulivu, mapenzi na kuhurumiana; na kwamba ndoa za kibiashara na kisiasa mara nyingi zinaishia kwenye maisha mabaya ya kifamilia na hatimaye kuvunjika na watoto kutangatanga.

Na katika ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi.

Mwenyezi Mungu anakariri ishara ya kuumbwa ulimwengu, kwa sababu huo pamoja na maajabu na siri zilizomo ndani yake ni katika dalili zilizo dhahiri zaidi za kuweko Mwenyezi Mungu. Vile vile kukumbusha fadhila zake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na kutofautiana ndimi zenu na rangi zenu.

Yaani kutofautiana lugha na rangi za watu. Pia kuna watu wanatofautiana kwa sura, sauti, alama za vidole n.k. Hekima ya hilo ni kujuana watu na kuwatofautisha. Mzazi amjue mwanawe, mume amjue mkewe, mdai amjue anayemdai n.k. Haiwezekani kabisa kuwa hekima hii ya hali ya juu iwe imepatikana kwa sadfa.

Hakika katika hayo kuna ishara kwa wenye elimu.

Yaani kuna dalili wazi za kuweko mkadiriaji na mpangiliaji mambo.

Na katika ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake.

Mtu anaweza kulala mchana wakati wa adhuhuri (qaylula) na pia anaweza kutafuta riziki usiku. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا ﴿١٠﴾ وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾

“Na tukaufanya usiku ni vazi na tuakaufanya mchana ni maisha,” (78:10 – 11) inachukuliwa kiaghlabu.

Vyovyote iwavyo, lengo ni kukumbusha hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kuyagawanya maisha ya mtu kwenye mateso na raha, ambapo maisha hayawezi kupangika bila ya mawili hayo.

Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia mwito wa Mwenyezi Mungu wakauitikia na mawaidha wakawaidhika nayo.

Na katika Ishara zake ni kuwaonyesha umeme kwa hofu na tamaa na kuwateremshia maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye akili.

Umepita mfano wake katika Juz. 13 (13:12).

Na katika Ishara zake ni kusimama mbingu kwa amri yake.

Kila kitu kinamhitajia Mwenyezi Mungu katika kubaki kwake na kuendelea kwake; sawa na kilivyomuhitajia katika kuumbwa kwake. Kikikosa ulinzi wake, basi kitakuwa ni bure tu kisicho na maana yoyote.

Kisha atakapowaita mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.

Wito wa Mwenyezi Mungu duniani ni wito wa nasaha na mwongozo, wanauitikia wenye takua na kuupinga wakosefu. Ama mwito wake huko akhera ni wakiutekelezaji, asioweza kuukimbia yoyote. Umetukuka uweza wake.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:52).