16
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI
ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٤١﴾
41. Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa sababu ya iliyoyafanya mikono ya watu. Ili Mwenyezi Mungu awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda. Huenda wakarejea.
قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلُ كَانَ أَكْثَرُهُم مُّشْرِكِينَ ﴿٤٢﴾
42. Sema: Nendeni katika ardhi na tazameni ulikuwaje mwisho wa wale waliotangulia, wengi wao walikuwa washirikina.
فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ الْقَيِّمِ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّـهِ يَوْمَئِذٍ يَصَّدَّعُونَ ﴿٤٣﴾
43. Basi uelekeze uso wako kwenye dini ya sawasawa, kabla ya kufika siku isiyozuilika, inayotoka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watatengana.
مَن كَفَرَ فَعَلَيْهِ كُفْرُهُ وَمَنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِأَنفُسِهِمْ يَمْهَدُونَ ﴿٤٤﴾
44. Anayekufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake, na anayetenda mema basi wanazitengenezea nafsi zao.
لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِن فَضْلِهِ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ ﴿٤٥﴾
45. Ili awalipe walioamini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hapendi makafiri.
UFISADI UMEDHIHIRI BARA NA BAHARINI
Aya 41 – 45
MAANA
Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa kwa sababu ya iliyoyafanya mikono ya watu.
Kundi la wafasiri limesema makusudio ya baharini hapa ni miji ya pwani na bara ni miji iliyo mbali na pwani. Wengine wamesema makusudio ya bahari ni mji kutokana na wingi wa wakazi wake na bara ni kijiji kutokana na uchache wa wakazi wake.
Tunavyofahamu sisi ni kuwa bara na baharini ni kinaya cha wingi wa ufisadi na kuenea kwake.
Kila aliloliharamisha Mwenyezi Mungu na kulikataza kulifanya ni kosa na ufisadi katika ardhi; kama vile vita dhulma, israfu, uasherati, pombe, kamari, kuzipuuza faradhi za Mwenyezi Mungu na waja wake n.k.
Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesifia zama za ujahili kwa kudhihiri ufisadi bara na baharini; ambapo hakukuwa na silaha za kemikali wala mabomu ya atomiki au mashirika ya ulanguzi na unyonyaji wala makasino na mabaa. Je, itakuwaje kwa hivi sasa ambapo nusu ya ulimwengu inahofiwa kuangamizwa wakati wowote, sio kwa kitendo cha Mwenyezi Mungu wala majanga ya asili, bali ni kwa kitendo cha binadamu wenyewe wanaomiliki silaha za maangamizi?
Hakuna njia ya kusalimika watu na shari hii isipokuwa kuangamizwa sila- ha zote. Ama umoja wa mataifa na shirika linalosimamia nguvu za nyuklia halijamhakikishia binadamu usalama wake wala si ya kutegemewa.
Ili Mwenyezi Mungu awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda. Huenda wakarejea.
Ufisadi katika ardhi ni natija ya kuachana na Mwenyezi Mungu na kutojilazimisha na maamrisho yake na makatazo yake. Neno ‘baadhi’ hapa linaashiria adhabu ya dunia na adhabu ya akhera ni mbaya zaidi na ya kufedhehesha. Katika dua zilizopokewa, kuna dua hii: “Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na dhambi inayobadilisha neema na kuteremsha balaa.” Bwana wa Mitume anasema:“Ogopeni dhambi kwani zinafuta kheri.”
Inatosha kuwa ni ushahidi wa hilo kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَتِلْكَ الْقُرَىٰ أَهْلَكْنَاهُمْ لَمَّا ظَلَمُوا وَجَعَلْنَا لِمَهْلِكِهِم مَّوْعِدًا ﴿٥٩﴾
“Na miji hiyo tuliwaangamiza walipodhulumu na tukawawekea miadi ya maangamizo yao.”
Juz. 15 (18:59).
Sema: Nendeni katika ardhi na tazameni ulikuwaje mwisho wa wale waliotangulia, wengi wao walikuwa washirikina.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:137), Juz.7 (6:11) na Juz. 20 (27:69).
Basi uelekeze uso wako kwenye dini ya sawasawa, kabla ya kufika siku isiyozuilika, inayotoka kwa Mwenyezi Mungu
ambayo ni siku ya hisabu na malipo isiyokimbilika. Mwema ni yule ambaye amemfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika matendo yake na makusudio yake na akaihisabu nafsi yake kabla ya kuhisabiwa.
Siku hiyo watatengana. Watatawayika makundi mawili: kundi moja Peponi na jingine Motoni. Umetangulia mfano wake katika Juzuu na Sura hii Aya 14.
Anayekufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake, na anayetenda mema basi wanazitengenezea nafsi zao.
Neno kutengeneza, limefasiriwa kutokana na neno Yamhadun lenye maana ya kutandika kitanda. Watu wenye matendo mema wanajitandikia makaburi yao na kufanya maandalizi ya mahitaji ya amani na raha kabla ya kuingia huko; sawa na inavyoandaliwa nyumba ya kuishi duniani. Imepokewa Hadith kutoka kwa Imam Ja’far Sadiq
:“Hakika matendo mema yanamtangulia mtendaji ili kumwandalia, sawa na mtumishi amwandaliavyo bwana wake.”
Umetangulia mfano wake katika Juz. Juz. 3(2:286).
Ili awalipe walioamini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hapendi makafiri.
Maneno hapa yanafungamana na ‘siku hiyo watatengana.’ Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama atawafanya watu makundi mawili ili awalipe Pepo waumini kutokana na matendo yao, kwa sababu anawapenda na anapenda matendo yao mema. Mwenyezi Mungu anawachukia makafiri na atalipa wanavyostahili.
Katika Nahjul-balagha imesemwa:“Hakika Mwenyezi Mungu anampemda mja na kuchukia matendo yake na anapenda matendo na kumchukia mtendaji wake.”
yaani anampenda mumin kwa imani yake na anachukia matendo yake mabaya na anamchukia kafiri kwa kufuru yake na anapenda matendo yake mazuri.
وَمِنْ آيَاتِهِ أَن يُرْسِلَ الرِّيَاحَ مُبَشِّرَاتٍ وَلِيُذِيقَكُم مِّن رَّحْمَتِهِ وَلِتَجْرِيَ الْفُلْكُ بِأَمْرِهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٤٦﴾
46. Na katika ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara na ili kuwaonjesha rehema yake na ili majahazi yatembee kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ رُسُلًا إِلَىٰ قَوْمِهِمْ فَجَاءُوهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَانتَقَمْنَا مِنَ الَّذِينَ أَجْرَمُوا وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na hakika tulikwishawatuma mitume kwa kaumu zao na wakawajia na hoja zilizo waziwazi. Tukawaadhibu wale waliofanya makosa na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru waumini.
اللَّـهُ الَّذِي يُرْسِلُ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَيَبْسُطُهُ فِي السَّمَاءِ كَيْفَ يَشَاءُ وَيَجْعَلُهُ كِسَفًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلَالِهِ فَإِذَا أَصَابَ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ ﴿٤٨﴾
48. Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapowafikishia awatakao katika waja wake, mara wanakuwa na furaha.
وَإِن كَانُوا مِن قَبْلِ أَن يُنَزَّلَ عَلَيْهِم مِّن قَبْلِهِ لَمُبْلِسِينَ ﴿٤٩﴾
49. Ingawaje kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa.
فَانظُرْ إِلَىٰ آثَارِ رَحْمَتِ اللَّـهِ كَيْفَ يُحْيِي الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ ذَٰلِكَ لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٥٠﴾
50. Angalia athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyoihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo, bila shaka, ndiye mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu
وَلَئِنْ أَرْسَلْنَا رِيحًا فَرَأَوْهُ مُصْفَرًّا لَّظَلُّوا مِن بَعْدِهِ يَكْفُرُونَ ﴿٥١﴾
51. Na kama tungeutuma upepo wakauona umekuwa rangi ya njano, juu ya hayo wangeku- furu.
KATIKA ISHARA YA KILIMWENGU
Aya 46 – 51
MAANA
Na katika ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara na ili kuwaonjesha rehema yake na ili majahazi yatembee kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake na ili mumshukuru.
Kila kitu kinachofungamana na hekima katika kupatikana kwake, ni dalili mkataa ya kukanusha sadfa na kwamba kuna makusudio na utashi katika kupatikana kwake. Dalili hii ndio makusudio ya ishara za Mwenyezi Mungu zinazofahamisha kuweko kwake.
Upepo- ukiwa ni dalili ya umoja wa Mwenyezi Mungu na uweza wakeuna faida nyingi; miongoni mwa faida hizo ni: Kuleta mawingu ya mvua yanayowashiria watu kheri, kutembea majahazi kwenye maji yakiwa yanachukua chakula kutoka mji mmoja hadi mwingine na mengineyo; kama yale aliyoyaashiria Imam Ja’far Sadiq
kwa kusema:
“Lau upepo utasimama siku tatu, basi kila kitu kitaharibika juu ya uso wa ardhi na kitavunda. Kwa sababu upepo uko kwenye daraja ya kiyoyozi kinachoondosha na kukinga uchafu kwenye kila kitu. Uko kwenye daraja ya roho ikitaka mwilini unaoza na kubadilika... Ametukuka Mwenyezi Mungu mzuri wa waumbaji.”
Na ili mshukuru.
Yaani mpate kuogopa maasi kwa siri na dhahiri. Tumeashiria huko nyuma, zaidi ya mara moja, kwamba Mwenyezi Mungu anapitisha vitu kwa sababu zake na inategemezwa kwake kwa vile yeye ndiye msababishi wa kwanza ambaye sababu zote zinakomea kwake.
Na hakika tulikwishawatuma mitume kwa kaumu zao na wakawajia na hoja zilizo waziwazi. Tukawaadhibu wale waliofanya makosa na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru waumini.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimtuma Muhammad(s.a.w.w)
na hoja za kutosheleza; kama alivyowatuma kabla yake Ibrahim, Musa, Isa na wengineo, na hoja zilizowazi. Basi wengi wakawakadhibisha na wachache wakawaamini. Mwenyezi Mungu atawaadhibu wakadhibishaji siku hiyo kubwa na atawanusuru Mitume na walio pamoja nao.
Nusra hii ni wajibu kwa Mwenyezi Mungu aliyojiwajibishia yeye mwenyewe kama alivyojiwabishia rehema. Tazama Juz. 11 (10:3-4) kifungu cha ‘Hisabu na malipo ni lazima’
Lengo la Aya hii ni onyo kwa wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w)
kuwa yatawasibu mfano wa yaliyowasibu wale waliokadhibisha mitume yake hapo kabla.
Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapowafikishia awatakao katika waja wake, mara wanakuwa na furaha. Ingawaje kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa.
Huu ni ufafanuzi wa Aya ilyotangulia: ‘Na katika ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara.’
Kwa ufupi maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazipeleka pepo kutimua mawingu na kuyatawanya mbinguni, kisha zinayagawa mapande mapande na kulileta kila pande kwenye mji aliooukusudia Mwenyezi Mungu.
Likifika hutoka maji mawinguni na kuanguka kwenye mji uliokusudiwa. Hapo watu wake hufurahi na kupeana habari njema. Na hapo mwanzo walikuwa wamekata tamaa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:57).
AKILI NA FIKRA YA UFUFUO
Angalia athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyoihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo, bila shaka, ndiye mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Makusudio ya rehema ya Mwenyezi Mungu hapa ni mvua na athari yake ni kuwa hai ardhi baada ya kufa. Uhai huu unaonekana kwa macho ni dalili mkataa kuwa fikra ya uhai baada ya mauti na ufufuo ni sahihi isiyokubali shaka yoyote.
Kwa sababu mwenye akili akitilia maanani na kufikiria vizuri uhai wa ardhi baada ya kufa kwake hana budi kusalimu amri na kuamini fikra ya ufufuo; vinginevyo atakuwa miongoni mwa wanaoamini kuweko kitu na kutokuweko kwa wakati mmoja, jambo ambalo haliwezekani.
Hapa ndio kuna siri ya kukaririka Aya zinazotanabahisha akili juu ya ufufuo wa ardhi baada ya kufa kwake, kama dalili ya uwezekano wa ufufuo wa watu; miongoni mwa Aya hizo ni:
وَاللَّـهُ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَسُقْنَاهُ إِلَىٰ بَلَدٍ مَّيِّتٍ فَأَحْيَيْنَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا كَذَٰلِكَ النُّشُورُ ﴿٩﴾
“Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa tukaihuisha ardhi kwayo baada ya kufa kwake. Ndio kama hivyo kutakuwa kufufuliwa” (35:9)
Nyingine ni:
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ﴿٣٩﴾
“Na miongoni mwa ishara zake ni kwamba unaiona ardhi ni nyonge, lakini tunapoiteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Hakika bila shaka aliyeihuisha ardhi ndiye atakayehuisha wafu.” (41:39)
Na nyinginezo nyingi.
Na kama tungeutuma upepo wakauona umekuwa rangi ya njano, juu ya hayo wangekufuru.
Yaani Mwenyezi Mungu akipeleka upepo utakaogeuza mimea yao rangi ya njano baada ya kuwa kijani, watakata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu na wataipinga hekima yake na kumkufuru Yeye na neema yake.
Hii haifahamishi chochote isipokuwa imani yao kwa Mwenyezi Mungu ni njozi tu. Lau ingelikuwa imejikita moyoni wangelikuwa imara nayo katika shida na raha.
Imam Ali
amesema:“Katika imani kuna ile iliyothibiti na kutulia moyoni na kuna ile inayokaa nyoyoni na vifuani kwa muda tu.”
Mumin, kama binadamu, anaumia na kuhuzunika, anapopatwa na masaibu yeye mwenyewe, mtoto wake au mali yake, lakini hilo halimtoi kwenye dini yake. Mtume(s.a.w.w)
alipofiwa na mtoto wake Ibrahim alisema: “Jicho linalia na moyo unahuzunika wala hatusemi yanayomchukiza Mola.”
فَإِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ ﴿٥٢﴾
52. Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma.
وَمَا أَنتَ بِهَادِ الْعُمْيِ عَن ضَلَالَتِهِمْ إِن تُسْمِعُ إِلَّا مَن يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا فَهُم مُّسْلِمُونَ ﴿٥٣﴾
53. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao. Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْقَدِيرُ ﴿٥٤﴾
54. Mwenyezi Mungu ndiye ambaye amewaumba katika udhaifu, kisha akajaalia nguvu baada ya udhaifu, kisha akajaalia udhaifu baada ya nguvu na uzee. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.
وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يُقْسِمُ الْمُجْرِمُونَ مَا لَبِثُوا غَيْرَ سَاعَةٍ كَذَٰلِكَ كَانُوا يُؤْفَكُونَ ﴿٥٥﴾
55. Na siku itakaposimama Saa, wakosefu wataapa kuwa hawakukaa duniani ila saa moja. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakigeuzwa.
وَقَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَالْإِيمَانَ لَقَدْ لَبِثْتُمْ فِي كِتَابِ اللَّـهِ إِلَىٰ يَوْمِ الْبَعْثِ فَهَـٰذَا يَوْمُ الْبَعْثِ وَلَـٰكِنَّكُمْ كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٥٦﴾
56. Na waliopewa ilimu watasema: Hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka siku ya kufufuliwa. Basi hii ndio siku ya kufufuliwa. Lakini nyinyi mlikuwa hamjui.
فَيَوْمَئِذٍ لَّا يَنفَعُ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَعْذِرَتُهُمْ وَلَا هُمْ يُسْتَعْتَبُونَ ﴿٥٧﴾
57. Basi siku hiyo hautawafaa waliodhulumu udhuru wao wala hawatapokelewa toba yao.
وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ وَلَئِن جِئْتَهُم بِآيَةٍ لَّيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ أَنتُمْ إِلَّا مُبْطِلُونَ ﴿٥٨﴾
58. Na hakika tulikwishawapigia watu kila mfano katika hii Qur’an. Na ukiwaletea ishara yoyote bila shaka watasema wale ambao wamekufuru: Nyinyi si chochote ila ni wabatilifu.
كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٩﴾
59. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga muhuri kwenye nyoyo za wasiojua.
فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَا يَسْتَخِفَّنَّكَ الَّذِينَ لَا يُوقِنُونَ ﴿٦٠﴾
60. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki; wala wasikuhafifishe wale wasiokuwa na yakini.
AMEWAUMBA KATIKA UDHAIFU
Aya 52 – 60
MAANA
Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao. Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.
Zimetangulia kwa herufi zake katika Juz. 20 (27: 80 – 81).
Mwenyezi Mungu ndiye ambaye amewaumba katika udhaifu, kisha akajaalia nguvu baada ya udhaifu, kisha akajaalia udhaifu baada ya nguvu na uzee. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.
Mtu hakuwako, kisha akawa na akagura daraja mbali mbali; kuanzia mchanga hadi tone la manii, kijusi hadi kuwa mtoto wa kunyonya, kuachishwa ziwa (kunyonya) hadi kuwa mtoto mdogo na kuanzia ujana hadi uzee na ukongwe.
Udhaifu wa kwanza ulioashiriwa na Aya ni ule wa mwili na utambuzi wa akili kwenye utoto. Imesemekana kuwa ni udhaifu wa kuwa tone la manii. Ama nguvu ni ujana, na udhaifu wa pili ni wa ukongwe; kama walivyoafikiana wafasiri. Ndio maana tukasema udhaifu wa kwanza ni utoto kulinganisha na uzee ambao ndio udhaifu wa pili, kwa maafikiano ya wafasiri.
Kwa vyovyote iwavyo ni kuwa makusudio ya Aya kuashiria mabadiliko ya mtu kutoka hali moja hadi nyingine ni kuwa mtu atambue kuwa yeye yuko mikononi mwa Mwenyezi Mungu akimgeuza vile atakavyo; kumpa uhai, kumfisha, kumpa udhaifu na nguvu. Kisha marejo ni kwake.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (16:70).
Na siku itakaposimama Saa, wakosefu wataapa kuwa hawakukaa duniani ila saa moja.
Makusudio ya Saa ni Siku ya Kiyama. Kusema isipokuwa saa moja ni kukusudia sehemu ya wakati katika maisha ya dunia. Maana ni kuwa wakosefu wakati watakapotolewa makaburini, wataapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakukaa makaburini isipokuwa muda mchache.
Umetangulia mfano wake kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 16 (20:102). Huko tumechanganya Aya tatu: ya kwanza ni ile inayosema:“Watanong’onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu.”
Juz. 16 (20: 103) ya pili inasema:“Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku.”
Juz. 15 (18:19). Ya tatu ni hii tuliyo nayo. Na tumejibu huko swali la je, zinaoana vipi Aya tatu hizo?
Hivyo ndivyo walivyokuwa wakigeuzwa.
Duniani walikuwa wakigeuza ukweli kuwa uongo huku wakiapa kuwa hakuna ufufuo wala hisabu. Na Akhera vilevile wataapa kuwa hawakukaa isipokuwa saa moja.
Na waliopewa ilimu watasema: hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka siku ya kufufuliwa. Basi hii ndio siku ya kufufuliwa.
Wakosefu watasema watakayoyasema kuhusu muda wa kukaa kwao makaburini na watu wanaomwamini Mungu na hisabu yake na thawabu zake watawaambia: Mmekaa kiasi alichotaka Mwenyezi Mungu mkae na muda mliokaa makaburi ni wenye kuthibiti katika ujuzi wake Mwenyezi Mungu Mtukufu; wala hakuna aujuae isipokuwa Yeye.
Kuna faida gani ya kuzungumza kwenu kuapa kuhusu muda wa kukaa makaburini na hali nyinyi mlikuwa mkiikana siku hii ambayo leo mnaona vituko vyake kwa macho yenu?
Lakini nyinyi mlikuwa hamjui.
Yaani nyinyi mko kwenye upofu na upotevu ulio wazi.
Basi siku hiyo hautawafaa waliodhulumu udhuru wao wala hawat- apokelewa toba yao.
Kauli nyingine inayofanana na hii ni:
وَإِن يَسْتَعْتِبُوا فَمَا هُم مِّنَ الْمُعْتَبِينَ ﴿٢٤﴾
“Na wakiomba toba hawakubaliwi.” (41:24).
Yaani siku hiyo hakutakuwa na udhuru wala kukubaliwa toba ya mkosefu, baada ya kuhadharishwa na kuonywa akakataa isipokuwa ukafiri.
Na hakika tulikwishawapigia watu kila mfano katika hii Qur’an.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:54).
Na ukiwaletea ishara yoyote bila shaka watasema wale ambao wamekufuru: Nyinyi si chochote ila ni wabatilifu.
Wanawaambia mitume, viongozi wema na wakombozi kuwa ni wabatilifu na waongo. Na wale wahaini na vibaraka wanaolipwa, kuwa ndio wenye haki. Hili si jambo geni; kwani mataghuti walio wakosefu wanaipima haki na batili kwa manufaa yao na hawaa zao.
Ikiwa inaafikiana nao basi hiyo ni haki hata kama ni shari na ufisadi; na inayohalifiana nao basi hiyo ni batili hata kama ni heri na wema.
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga muhuri kwenye nyoyo za wasiojua.
Mwenyezi Mungu amepiga muhuri kwenye nyoyo zao kwa sababu wao walifuata kwa hiyari yao njia inayopelekea hilo. Kuwa kipofu na haki ni natija ya ujinga; na dhulma na utaghuti ni natija ya kuwa kombo na njia ya uongofu. Ama kunasibishwa hilo kwa Mwenyezi Mungu maana yae ni kuwa sababu za natija yake zinalazimiana naye.
Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki; wala wasikuhafifishe wale wasiokuwa na yakini.
Vumilia ewe Muhammad, uendelee na mwito wako na uvumilie adha katika njia yake. Hazitapita siku nyingi ila ujumbe wako utaenea mashariki ya ardhi na magharibi yake jina lako litatajwa pamoja na jina la Mwenyezi Mungu na litaombewa rehema na taadhima.
Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametuneemesha kwa Muhammad(s.a.w.w)
, Mtume wa rehema na kiongozi wa watu kwenye heri. Basi turuzuku shafaa yake, ewe mwenye kubadili mabaya, pamoja na wingi wake, kwa mazuri.