TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 15829
Pakua: 3361


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 25 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 15829 / Pakua: 3361
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

Mwandishi:
Swahili

17

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Sura Ya Thelathini na Mmoja: Surat Luqman. Imeshuka Makka isipokuwa baadhi ya Aya. Ina Aya 34.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

الم ﴿١﴾

1. Alif Laam Miim.

تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾

2. Hizo ni Aya za Kitabu chenye hekima.

هُدًى وَرَحْمَةً لِّلْمُحْسِنِينَ ﴿٣﴾

3. Ni uongofu na rehema kwa wafanyao wema.

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ ﴿٤﴾

4. Ambao wanasimamisha Swala; na wanatoa Zaka na wana yakini na akhera.

أُولَـٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥﴾

5. Hao ndio walio na uongofu utokao kwa Mola wao na hao ndio wenye kufanikiwa.

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

6. Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipokujua na wanaichukulia ni mzaha. Hao watapata adhabu ya kufedhehesha.

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا وَلَّىٰ مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا كَأَنَّ فِي أُذُنَيْهِ وَقْرًا فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٧﴾

7. Na anaposomewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni kwake mna uziwi. Basi mbashirie adhabu chungu.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتُ النَّعِيمِ ﴿٨﴾

8. Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na bustani zenye neema.

خَالِدِينَ فِيهَا وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٩﴾

9. Watadumu humo. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye ndiye Mwenye uwezo, Mwenye hekima.

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿١٠﴾

10. Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona na ameweka katika ardhi mlima ili ardhi isiwayumbishe na amewatawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.

هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾

11. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheniwameumba nini hao wasiokuwa Yeye! Lakini madhalimu wamo katika upotevu ulio dhahiri.

HUU NI UUMBAJI WA MWENYEZI MUNGU

Aya 1 – 11

MAANA

Alif Laam Miam.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).

‘Hizo’ ni Aya za Kitabu chenye hekima.

Hizo ni ishara ya Aya za Sura hii, na kwamba hizo zinatokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amekisifu kuwa kina hekima kwa sababu ndani yake mna hekima ya hali ya juu.

Ni uongofu na rehema kwa wafanyao wema ambao wanaitafuta haki na kuitumia kwa sababu ni haki; wala hawana shaka kwamba Qur’an ni uongofu na rehema kwa kila mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na haki. Ama wale ambao tamaa zimepofusha nyoyo zao, basi hao ni ugonjwa usiokuwa na dawa isipokuwa kun’golewa.

Ambao wanasimamisha Swala; yaani wanadumu nayona wanatoa Zaka kwa anayestahikina wana yakini na akhera, wala hawana shaka kwamba wao wataulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusu kauli zao na vitendo vyao.

Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao na hao ndio wenye kufanikiwa.

Kipimo cha uongofu na kufanikiwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuifanyia ikhlasi haki kwa kauli na vitendo na kutomwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu wala usifanyie ubakhili fadhila alizokupa Mwenyezi Mungu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 mwanzo wa sura ya pili.

KUIFANYIA BIASHARA DINI NA DHAMIRI

Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipokujua na wanaichukulia ni mzaha.

Mwenye Majmaul-bayan anasema: “Wafasiri wengi wamesema kuwa makusdio ya maneno ya upuuzi ni nyimbo. Na kutoka kwa Imam Ja’far Sadiq(a.s) imepokewa kuwa ni kuitusi haki na kuifanyia mzaha.”

Tafsiri hii ya Imam ndiyo iliyo karibu zaidi na hali halisi ya mamabo na inaenda na mfumo wa maneno. Kwani Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kutaja waumini waliofaulu, sasa anawataja wakosefu ambao wananunua shutuma kutoka kwa wale wanoifanyia biashara dini na dhamiri, ili wawapoteze watu na haki na kuwavungavunga na mambo ya batili.

Mfano ulio wazi wa hayo ni vile, siku hizi, nguvu ya shari inavyokimbilia kueneza propaganda zake kwa kutoa mamilioni ya pesa kwenye vyombo vya habari ili yaeneze uwongo na uzushi na kuwapa mapesa wahaini na vibaraka ili wawatie shaka wenye wema wenye ikhlasi.

Zaidi ya hayo vyombo hivyo vya kishari vimewavisha vibaraka wake nguo ya dini ili wapandikize bid’a na waifasiri vile watakavyo; kuweza kueneza fitna na mipasuko baina ya mataifa na watu wa dini.

Baada ya vita vya mashariki ya kati vya mwaka 1967, tumeshuhudia aina kwa aina ya propaganda za uwongo na vita vya maneno katika magazeti ya kulipwa. Ama harakati za vibaraka zimefikia kiwango cha kumfanyia ujeuri Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Lakini kila siku zinavyopita zinafichuka njama zao na kufedheheka vibaraka. Wakati wa kuwang’oa utafika tu.

Hao watapata adhabu ya kufedhehesha kwa asababu wameiuza dini yao kwa shetani na wakala njama naye dhidi ya haki na watu wake.

Na anaposomewa Aya zetu huzipa mgongo wa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni kwake mna uziwi. Basi mbashirie adhabu chungu.

Mumin mwenye ikhlasi anaisikliliza haki na anaizibia masikio batili, lakini habithi mkosefu mwenye malengo ya tamaa anaisikiliza batili na kuiiz- ibia masiko haki. Hana malipo huyu isipokuwa adhabu chungu.

Razi amesema: “Mwenye akili anaitafuta hekima kwa thamani yoyote, lakini wao hawakuitafuta na ilipowajia bure hawakuisikiza.”

Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema watakuwa na bustani zenye neema.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipobainisha malipo ya mwenye kuzipinga Aya zake kuwa ni adhabu chungu, sasa anabainisha malipo ya mwenye kuamini kuwa ni Pepo yenye neema.

Watadumu humo na watapata kila wanachokitamani.Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli kwa sababu itatokea tu.

Na Yeye ndiye mwenye uwezo mwenye hekima.

Ni mwenye nguvu kwa uweza wake, usioshindwa, ni mwenye hekima kwa mipangilio yake ambayo haipingi ila jahili au mwenye kiburi.

Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isiwayumbishe na amewatawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:2).

Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye!

Kila kilichomo mbinguni ni ushahidi wa kuweko Mwenyezi Mungu na uweza na umoja wake. Basi mna dalili gani nyinyi washirikiana kuwa mnaowaabudu ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenye sifa moja tu katika sifa zake.

Lakini madhalimu wamo katika upotevu ulio dhahiri.

Kila anayeipinga haki yoyote, baada ya kumdhihirikia dalili yake, basi huyo ni dhalimu mwenye dhambi.

Unaweza kuuliza : Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an tukufu ataona kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) mara nyingi anapobatilisha ushirikina huwa anasisitiza kwa kueleza vitu vilivyo dhahiri na vinavyoonekana; mfano kauli yake hii: ‘Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye!’ au ‘Hawawezi kuumba hata nzi,’ Je, kuna siri gani katika hilo?

Siri ya hilo ni kufichua kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa kikundi kiovu hakiamini hakika yoyote hata kama iko wazi kama mwangaza wa jua, isipokuwa masilahi yake tu. Sifa hii ni mbaya zaidi ya nyingine na ni hatari zaidi; haina dawa isipokuwa nguvu kuu ya upinzani.

وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ أَنِ اشْكُرْ لِلَّـهِ وَمَن يَشْكُرْ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿١٢﴾

12. Na hakika tulimpa Luqman hekima tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliyekufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

13. Na Luqman alipomwambia mwanawe akiwa anampa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu na chochote. Hakika shirki ndio dhulma kubwa.

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿١٤﴾

14. Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake, mama yake amebeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhifu na kumwachisha ziwa (kunyonya) kwa miaka miwili, kwamba unishukuru mimi na wazazi wako. Marudio ni kwangu.

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾

15. Na kama wakikushikilia kunishirikisha mimi na yale ambayo huna ilimu nayo basi usiwatii, na kaa nao kwa wema duniani Na fuata njia ya yule anayerejea kwangu. Kisha hakika marejeo yenu ni kwangu mimi, nami nitawaambia mliyokuwa mkiyatenda.

يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿١٦﴾

16. Ewe mwanangu! Ikiwa kuna jambo la uzito wa hardali likawa ndani ya mwamba au mbinguni au ardhini, basi Mwenyezi Mungu atalileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi, Mwenye habari.

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾

17. Ewe mwangu! Simamisha Swala na uamrishe mema na ukataze mabaya na subiri kwa yanayokusibu, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.

وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾

18. Wala usiwapindie watu uso wako kuwabeua. Wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna anayejifaharisha.

وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ ﴿١٩﴾

19. Na ushike mwendo wa katikati. na uinamishe sauti yako. Hakika sauti mbaya zaidi ni sauti ya punda.

LUQMAN

Aya 12 – 19

MAANA

Na hakika tulimpa hekima tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu.

Neno ‘hekima’ hutumiwa kwa maana nyingi; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo: Kumjua Mwenyezi Mungu na sifa zake, kukiweka kitu mahali pake, maneno yenye mawaidha na kumtii Mwenyezi Mungu. Kuna Hadith isemayo: “Msingi wa hekima ni kumhofia Mwenyezi Mungu”

Luqman alikuwa ni katika wanomjua Mwenyezi Mungu na kumtii, mwenye kulingania kwa Mwenyezi Mungu kwa mfumo mzuri wa utulivu na alikuwa muwazi mwenye kukinaisha.

Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliyekufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 19 (27:40).

Wametofautiana kuhusu Luqman kuwa je, alikuwa Mtume au mja mwema tu. Tofauti hizi hazihusiani chochote na itikadi au maisha. Lililo wajibu kuliamini ni lile lililonukuliwa na Qur’an - kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimneemesha Luqman kwa hekima ambayo ni elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu, kumtii na kutoa mwito kwenye njia yake Mwenyezi Mungu kwa mawaidha mazuri.

Wafasiri na wanahistoria wametaja akili na hekima nyingi za Luqman; miongoni mwazo ni kuwa yeye alikuwa ni mtumwa. Siku moja alitumwa kwenye bustani pamoja na watumwa wengine ili wakalete matunda. Walipofika kwenye bustani wote wakala matunda isipokuwa Luqman. Wakala njama dhidi yake kwa vile hakushiriki kwenye kosa lao.

Wakamfikisha kwa bwana wao na kusema kuwa Luqman amekula matunda yote. Alipoulizwa Luqman akasema: Tunyweshe dawa sote, hapo utadhihiri uhakika. Basi ikawa hivyo. Wote wakatapika matunda isipokuwa Luqman. Vitimbi vikawarudia wao wenyewe.

Tukio jingine ni kuwa siku moja bwana wake alilewa na akaweka rehani ya mali nyingi kuwa anywe maji kwenye ziwa moja huko.

Alipotokwa na ulevi akajuta na akaona amewezwa bila ya kujitambua. Akakimbilia kwa Luqman na kumwambia hii ni siku yako. Luqman akawaambia watu. Hili ziwa lina mito inayomimina maji ndani yake, basi izuwiyeni ili huyu bwana anywe maji ya ziwa. Wakasema hatuwezi kufanya hivyo.

Akawaambia: “Yeye ameweka rehani kunywa maji ya ziwa sio yanyoingia au kutoka ziwani.”

Iwe ni sawa riwaya hii au la, lakini ni mfano wazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimpa Luqman hekima na maarifa. Kutokana na kauli za wafasri na wana historia, inaonyesha kuwa Luqman alikuwa zama za Nabii Daud(a.s) Tazama Juz. 17 (21:80).

Na Luqman alimwambia mwanawe akiwa anampa mawaidha:

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa alimneemesha Luqman kwa hekima, sasa anataja baadhi ya mawaidha yake kwa mwanawe yenye upole na huruma.

Imam Ali(a.s) alimuusia mwanawe Imam Hasan(a.s) wasia mrefu, mwanzo ulikuwa hivi:“Nakuona wewe ni sehemu yangu bali ni mwili wangu wote, kiasi ambacho likikusibu jambo ni kama limenisibu mimi. Na kama kwamba lau mauti yanakujia basi ni kama yamenijia mimi. Jambo lako linanihusu kama linavyonihusu jambo langu.”

Luqman alimuusia mwanawe mambo haya yafuatayo:

Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu na chochote. Hakika shirki ndio dhulma kubwa.

Badhi ya wafasiri wanaona kuwa kauli hii inaonyesha kuwa mwanawe Luqman alikuwa mshirikina. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa kukataza jambo hakufahamishi kuwa anayekatazwa analo. Mwenyezi Mungu alimwambia kipenzi chake: Ibrahim(a.s) :

أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا ﴿٢٦﴾

“…kwamba usinishirikishe na chochote” Juz. 17 (22:26).

Pia alimwambia kipenzi chake Muhammad(s.a.w.w) : “Basi usiwatii makafiri” Juz. 19 (25:52). Imam Ali(a.s ) alimwambia Hasan(a.s ) :“Shikamana na Mwenyezi Mungu… awe ndiye unayemwabudu… Lau angelikuwa na mshirika wangelikujia mitume wake.”

Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake. Amebeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu.

Aya hii na iliyo baada yake ni muendelezo wa wasia wa Luqman kwa mwanawe. Neno udhaifu limefasirwa kutokana na neno wahan lenye maana ya udhaifu na mashaka. Kila mtoto anavyokuwa tumboni mwa mama yake humzidisha udhaifu na tabu.

Na kumwachisha ziwa (kunyonya) kwa miaka miwili.

Mama humnyonyesha mwanawe miaka miwili kisha anamwachisha kunyonya Katika muda huo anapata shida kuongezea shida alizozipata wakati wa mimba na uchungu wa kuzaa. Yametangulia maelezo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 2(2:233).

Kwamba unishukuru mimi na wazazi wako. Marudio ni kwangu.

Yaani siku hiyo nitakuuliza; je ulikuwa ni katika wenye shukrani na twaa au ulikuwa mwenye kuwaudhi wazazi na kuniasi mimi na wazazi wako?Na kama wakikushikila kunishirikisha mimi na yale ambayo huna ilimu nayo basi usiwatii, kwa vile hakuna kumtii kimbe kwa kumuuasi muumba.

Na kaa nao kwa wema duniani kwa kutowakemea na uzungumze nao vizuri na kuwafanyia yale wanayoyapendelea. Yametangulia maelezo ya kuwatendea wema wazazi kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:23) na Juz. 20 (29:8).

Na fuata njia ya yule anayerejea kwangu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kushukuriwa Yeye na wazazi, sasa anaamrisha kutiiwa Yeye katika kila jambo, sio kuwatendea wema wazazi tu. Hilo ameliletea ibara kuwafuata watu wema ambao wamemtii Mwenyezi Mungu katika maarisho na makatazo yake.

Imam Zaynul’abidin(a.s) anasema:“Ewe Mola wangu! Niunganishe na watu wema waliopita na unijaalie katika wema waliobakia na unielekeze njia ya watu wema.”

Kisha hakika marejeo yenu ni kwangu mimi, nami nitawaambia mliyokuwa mkiyatenda.

Huu ni ukemeo na kiaga kwa yule anayemuasi Mwenyezi Mungu na wazazi wawili.

MWAMBA NA KARNE YA ISHIRINI

Ewe mwanangu! Ikiwa kuna jambo la uzito wa hardali likawa ndani ya mwamba au mbinguni au ardhini, basi Mwenyezi Mungu atalileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi, Mwenye habari.

Neno jambo halikutajwa katika Aya, lakini linafahamika kutokana na mfumo wa maneno. Neno ‘uzito wa hardali’ ni kinaya cha udogo na neno ‘ndani ya mwamba au mbinguni au ardhini,’ ni kinaya cha siri na uficho.

Maana ya kiujumla ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua makusudio ya mtu, kauli yake na vitendo vyake vilivyofichika na vilivyo dhahiri, haachi dogo wala kubwa, isipokuwa analidhibiti na kulihisabu.

Makusudio ya maneno haya ni kuwaonya wapotevu wanaopoteza ambao wanaishi na watu kwa ndimi zao na wanaishi na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu kwa nyoyo zao, kwamba wajue mwisho ni kufedheheka na balaa.

Baadhi ya wafasiri wamejiuliza na wakasema: Vipi Mwenyezi Mungu ametaja mbingu na ardhi baada ya kutaja mwamba na inajulikana kuwa mwamba lazima uwe ardhini na sio mbinguni?

Mmoja akajibu kuwa mwamba huu hauko mbinguni wala ardhini isipokuwa uko chini ya ardhi saba na ndio mwamba ambao ng’ombe anayeibeba ardhi kwa pembe yake ndio amesimamia hapo. Mwingine akasema mwamba huu uko hewani. Wa tatu naye akasema una rangi ya kijani. Tazama tafsiri ya Razi na Tabariy.

Qur’an, ambayo Mwenyezi Mungu ameisifu kuwa ni nuru na upambanuzi, imeepekuna na tafsiri zote hizi ambazo adui amezifanya ni nyenzo ya kushutumu na kuifanyia stihzai dini. Tafsiri hii na mfano wake inafa- hamisha kuwa walioifasiri hawajui hekima ya Mwenyezi Mungu ya kupeleka mitume yake na kuteremsha Kitabu chake.

Pia hawajui kwamba dini ya kiislamu ni dini ya maumbile na ya maisha na kwamba msingi wa mwito wake ni imani na ikhlasi. Mwangaza wake ni elimu na uadilifu, njia yake ni bidii na utendaji na lengo lake ni wema na raha.

Ewe mwangu! Simamisha Swala, kwa sababu inakukumbusha Mwenyezi Mungu na kukataza kiburi.Na uamrishe mema na ukataze mabaya . Miongoni mwa mema ni kushikamana na waumini na kuwakaba koo wanafiki.

Na subiri kwa yanayokusibu, hakika hayo ni katika mambo ya kuaz- imiwa.

Makusudio ya mambo ya kuazimiwa ni nguvu ya utashi na uthabiti wa haki. Amri ya kuwa na subira baada ya kuamrisha mema inaonyesha kuwa mwenye kutoa mwito wa haki atapata yale anayopambana nayo kila mwenye kufanya jihadi aliye na ikhlasi kutoka kwa wabatilifu.

Wala usiwapindie watu uso wako kuwabeua.

Yaani usiwageuzie uso wako kwa kiburi, bali wakabili na uwanyenyekee. Katika Nahjulbalagha imeelezwa: “Hakuna upweke kama kujiona na hakuna ufahari kama kunyenyekea.”

Wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna anayejifaharisha.

Baada ya kukataza kutembea kwa maringo anabainisha maana yake kuwa ni kujivuna na kujifaharisha; wala hakuna kitu kinachofahamisha ujinga na upunguani kuliko sifa hizi.

Na ushike mwendo wa katikati. Usiende polepole wala haraka na uinamishe sauti yako. Hakika sauti mbaya zaidi ni sauti ya punda.

Hapa kuna ishara ya kuwa kuinua sauti zaidi ya haja kunafahamisha ujinga na pia kunyamaza kabisa. Mwenye kufanya wastani ndio amejua njia.

Pia ieleweke kuwa mazungumzo yatakuwa mazuri, kwa sauti ya wastani, ikiwa kuna haja ya kuzungumza; vinginevyo itakuwa kunyamaza ni bora na ukamilifu zaidi.

Katika maelezo ya wasifu wa Luqman ni kwamba alikuwa akisikiliza sana na kuzungumza kidogo. Anapozungumza basi neno lake linakuwa kama punje ya mtama kwenye changarawe.

Kuna baadhi ya Hadith zisemazo kuwa kunyamaza ni katika milango ya hekima; yaani ni hekima kunyamaza na kusikiliza kwa makini ni hekima.

Ama kauli ya anayesema: “Ikiwa maneno ni fedha basi kunyamaza ni dhahabu,” maana yake ni kunyamaza kwa kuacha batili na ufedhuli; vinginevyo tamko la haki ni nuru na jihadi, hasa likiwa ni dhidi ya dhulma na jeuri. Kuna Hadith isemayo:“Mwenye kuinyamazia haki ni shetani bubu.”