22
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
Sura Ya Thelathini Na Nane: Surat Saad. Imeshuka Makka, Ina aya 88
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
ص وَالْقُرْآنِ ذِي الذِّكْرِ ﴿١﴾
1. Swaad. Naapa kwa Qur’an yenye ukumbusho.
بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي عِزَّةٍ وَشِقَاقٍ ﴿٢﴾
2. Lakini waliokufuru wamo katika majivuno na upinzani.
كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ فَنَادَوا وَّلَاتَ حِينَ مَنَاصٍ ﴿٣﴾
3. Vizazi vingapi tumeviangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwishapita.
وَعَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ وَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا سَاحِرٌ كَذَّابٌ ﴿٤﴾
4. Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anayetokana na wao. Na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo.
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ ﴿٥﴾
5. Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili kweli ni jambo la ajabu.
وَانطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ يُرَادُ ﴿٦﴾
6. Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililopangwa.
مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ ﴿٧﴾
7. Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu.
أَأُنزِلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ مِن بَيْنِنَا بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ مِّن ذِكْرِي بَل لَّمَّا يَذُوقُوا عَذَابِ ﴿٨﴾
8. Ati yeye ndiye aliyeteremshiwa mawaidha kati yetu?” Bali wao wana shaka na mawaidha yangu; bali hawajaionja adhabu yangu.
أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَحْمَةِ رَبِّكَ الْعَزِيزِ الْوَهَّابِ ﴿٩﴾
9. Au wanazo wao hazina za rehema za Mola wako, Mwenye nguvu, Mpaji?
أَمْ لَهُم مُّلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَلْيَرْتَقُوا فِي الْأَسْبَابِ ﴿١٠﴾
10. Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake? Basi na wazipande sababu zote.
جُندٌ مَّا هُنَالِكَ مَهْزُومٌ مِّنَ الْأَحْزَابِ ﴿١١﴾
11. Ni jeshi litakaloshindwa miongoni mwa makundi yatayoshindwa.
NAAPA KWA QUR’AN YENYE MAWAIDHA
Aya 1 – 11
MAANA
Swaad.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Naapa kwa Qur’an yenye ukumbusho, Lakini waliokufuru wamo katika majivuno na upinzani.
Jawabu la kiapo linakadiriwa kuwa ni ‘Hakika hiyo ni haki.’ Makuraishi walikadhibisha Qur’an ambayo ina kheri yao na enzi yao. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaapa kwa Qur’an yenyewe kwamba hiyo ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba hakuna sababu ya kukadhibisha huku isipokuwa kiburi cha wakadhibishaji, kuikimbia kwao haki na uadui wao kwa Muhammad(s.a.w.
w
)
.
Kuapa kwake Mwenyezi Mungu kwa Qur’an kunaashiria kwamba hiyo Qur’an kushinda kwake kunafahamishwa na ufasaha wake na ukweli wake unafahamishwa na mafunzo yake. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawahadharisha makuraishi na kuwakumbusha maangamizi ya waliotangulia pale walipowakadhibisha mitume, kwa kusema:
Vizazi vingapi tumeviangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwishapita.
Wa mwanzo walijizuia na haki na kuwafanya watu wa haki ni mahasimu wao; sawa na mlivyofanya nyinyi. Walipojiwa na adhabu wakaanza kurudi nyuma na kunyenyekea, lakini muda ulikwishapita tena. Kwa hiyo bora muamini sasa kabla ya kupita muda mkajuta ambapo majuto hayatafaa kitu tena.
KUMWIGA MWENYE KUMPWEKESHA MUNGU NA KUMWIGA MSHIRIKINA
Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anayetokana na wao.
Muhammad(s.a.w.
w
)
ni Mkuraishi, hilo halina shaka, lakini si katika vigogo wala mataghuti wao, vipi awe ni miongoni mwao? Lau angelikuwa mion- goni mwao angewafanya watu watumwa wake na akawa na hazina au nyumba ya dhahabu. Tazama Juz. 15 (17: 90) kifungu cha ‘Kupenda mali’ na Juz. 18 (25:7) kifungu cha ‘Mantiki ya watu wa pesa ni benki na ardhi.’
Na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo.
Kwa nini ni muongo?
Jibu
ni:
Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili kweli ni jambo la ajabu.
Ajabu kwa hawa sio kuwa Muhammad(s.a.w.
w
)
anapinga shirki na kuweko waungu wengi, ingawaje hilo wanaliwaza, lakini ajabu hasa ni Muhammad(s.a.w.
w
)
kutoka kwenye maigizo yao na mazowea yao waliyoyarithi tangu jadi na jadi. Wao hasa wanatetea kuiga kwa mababa na mababu zao kuwa ndio dini na msingi; sio kuwa wanatetea masanamu kwa kuwa ni masanamu. Wanatetea masanamu kwa vile ni turathi na urithi kutoka kwa wakale wao:
إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءَنَا عَلَىٰ أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَىٰ آثَارِهِم مُّقْتَدُونَ ﴿٢٣﴾
“Kwa hakika tuliwakuta baba zetu juu ya mila na hakika sisi tunafuata nyayo zao.” (43:23).
Imani ya wajinga hawa ni sawa na imani ya washirikina, kwa sababu chimbuko la imani mbili ni moja nalo ni kuiga. Tofuati ni kuwa kumuiga mwenye kumpwekesha Mungu ni sahihi na kwenye kukubalika kwa sababu kuna msingi wa hali halisi; kama, kwa mfano, nikikuambia:
“Mwenye nadharia ya mvutano ni Newton na mwenye nadhariya ya uwiyano ni Einstein” Lakini kuiga kwa washirikina ni upotevu.
Na mwenye kuiga hivyo atabeba majukumu na atawajibishwa ila akiwa hana ajualo; kama mnyama. Kwa sababu kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakuna msingi wowote kwake.
Kwa maneno mengine ni kuwa fikra itakuwa ni ya kweli ikiwa inatokana na uhalisi wa hali; iwe imetokana na elimu au kuiga. Tazama Juz.2 (2:168-170). Kifungu: ‘Kufuata na msingi wa itikadi.’
Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililopangwa. Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu.
Makusudio ya wakubwa wao ni vigogo wa kikuraishi. Kudumu kwenye miungu ni kudumu kuiabudu. Jambo lililopangwa ni kudumu kwenye ibada ya masanamu. Mila ya mwisho ni itikadi ya utatu ya kimasihi (kikiristo). Washirikina waliita ya mwisho kwa vile ndiyo dini ya mwisho kujitokeza wakati wao.
Kwenye Tafsir Tabariy na nyinginezo imeelezwa kuwa wazee wa kikuraishi walimwendea Abu Twalib na kumwambia: “Mwana wa nduguyo na aachane na miungu yetu nasi tutamwacha na Mungu wake anayemwabudu. Abu Twalib alipomwambia hilo Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.
w
)
alisema:
“Ninawataka neno moja tu waliseme, basi waarabu na waajemi watawafuata.” Wakasema tutakukubalia hilo na mengine kumi, ni lipi hilo? Akasema: “Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu. (Lailaha illa llah)” wakaondoka zao huku wakisema: “Hivi miungu yote ameifanya kuwa mmoja!”
Riwaya hii inaafikiana na dhahiri ya Aya na inasaidiwa na hali halisi ya washirikina na nafasi ya mzee aliyelemewa.
Ati yeye ndiye aliyeteremshiwa mawaidha kati yetu?
Mwenyezi Mungu atamchagua vipi Muhammad na hali hana jaha wala mali?
Bali wao wana shaka na mawaidha yangu,
Wao ni washirikina. Kwa sababu miongoni mwao kuna waliompinga Muhammad(s.a.w.
w
)
kwa hasadi na wengine wakampinga kwa kulinda masilahi yao.
Bali hawajaionja adhabu yangu.
Wakishaionja shaka itawaondokea na “wataficha majuto” Juz. 11 (10:54).
Au wanazo wao hazina za rehema za Mola wako, Mwenye nguvu, Mpaji?
Makusudio ya hazina za rehema hapa ni utume tu, au utume na neema nyinginezo za Mwenyezi Mungu na hisani yake. Maana ni kuwa kwa nini washirikina wanalalamikia na kupinga rehema ya Mwenyezi Mungu ya kumchagua kwake kuwa mjumbe kwa walimwengu? Je ni kwa kuwa wao wanamiliki hiyari hii badala ya Mwenyezi Mungu?
Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake?
Mmliki wa ulimwengu ni yule anayemiliki utume, kuutoa na kumuenzi nao amtakye. Na washirikina hawamiliki chochote kwa Mwenyezi Mungu kuweza kumpa utume mtu mkubwa kati ya miji miwili.
Kuna jambo moja ambalo wanaweza kwalo kumiliki mbingu na ardhi nalo ni Basi nawazipande sababu zote.
Makusudio ya sababu ni njia na nyenzo. Maana ni kuwa utume anauhukumu ambaye anamiliki ulimwengu na viliomo ndani yake. Basi vigogo wa kikuraishi wakitaka kumchagua kwa utume yule wanayemtaka, kabla ya chochote nawamiliki nyenzo za kufikia kwenye umiliki huu ikiwa wanaweza. Changamoto hii ni ubainifu wa kutosha kabisa.
Ni jeshi litakaloshindwa miongoni mwa makundi yatayoshindwa.
Wale waliokupiga vita, ewe Muhammad, si chochote, watashindwa mbele ya mwito pamoja na wingi wa majeshi na vikosi vyao.
كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ ذُو الْأَوْتَادِ ﴿١٢﴾
12. Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh, na kina A’adi na Firauni mwenye vigingi.
وَثَمُودُ وَقَوْمُ لُوطٍ وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ أُولَـٰئِكَ الْأَحْزَابُ ﴿١٣﴾
13. Na Thamud na kaumu ya Lut na watu wa mwituni. Hayo ndiyo makundi.
إِن كُلٌّ إِلَّا كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ عِقَابِ ﴿١٤﴾
14. Wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahili adhabu yangu.
وَمَا يَنظُرُ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً مَّا لَهَا مِن فَوَاقٍ ﴿١٥﴾
15. Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda.
وَقَالُوا رَبَّنَا عَجِّل لَّنَا قِطَّنَا قَبْلَ يَوْمِ الْحِسَابِ ﴿١٦﴾
16. Na wao husema: Mola wetu Tuletee upesi sehemu yetu kabla ya Siku ya Hisabu.
اصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاذْكُرْ عَبْدَنَا دَاوُودَ ذَا الْأَيْدِ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿١٧﴾
17. Subiri kwa wayasemayo, Na umkumbuke mja wetu Daud. Mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia.
إِنَّا سَخَّرْنَا الْجِبَالَ مَعَهُ يُسَبِّحْنَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِشْرَاقِ ﴿١٨﴾
18. Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi
وَالطَّيْرَ مَحْشُورَةً كُلٌّ لَّهُ أَوَّابٌ ﴿١٩﴾
19. Na pia ndege waliokusanywa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
وَشَدَدْنَا مُلْكَهُ وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ ﴿٢٠﴾
20. Na tukautia nguvu ufalme wake. Na tukampa hikima na kukata hukumu.
SUBIRI JUU YA HAYO WANAYOSEMA
Aya 12 – 20
MAANA
Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh, na kina A’adi na Firauni mwenye vigingi Na Thamud na kaumu ya Lut na watu wa mwituni.
Wote hawa waliwakanusha mitume; baadhi yao wakaangamizwa kwa tufani; kama vile watu wa Nuh, wengine kwa kuzama baharini, kama Firauni.
Kuwa na vigingi ni kinaya cha kujikita ufalme wake kama linavyokitwa hema na vigingi kwenye ardhi.
“Basi Thamud waliangamizwa kwa balaa kubwa (la ukelele wa adhabu). Ama A’d waliangamizwa kwa upepo mkali usiozuilika” (69:5-6).
Kaumu ya Lut majumba yao yalipinduliwa juu chini. Tazama Juz. 12 (11:82). Watu wa mwituni Mwenyezi Mungu aliwaadhibu adhabu chungu. Tazama Juz.14 (15:78) na Juz. 19 (26:176).
Hayo ndiyo makundi. Wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahili adhabu yangu.
Mwenyezi Mungu aliviadhibu vikosi vya shetani kwa sababu ya madhambi yao; ikiwa ni malipo ya yale waliyoyafanya. Je, wanaomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w)
hawahofii kuwafika yaliyowafika hao.
Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda.
Hawa ni waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w)
. Maana ni; wanangoja nini kwa Mungu baada ya kukukadhibisha ewe Muhammad na hali Mwenyezi Mungu, kwa neno moja tu anaweza kuwapelekea adhabu itayowafyeka katika muda ambao hawataweza kuusia wala kurudi kwa watu wao.
Na wao husema: Mola wetu! Tuletee upesi sehemu yetu kabla ya Siku ya Hisabu.
Yaani sehemu yetu ya adhabu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwatishia na adhabu ya Jahannam kupitia kwa Mtume wake mtukufu, lakini wao wakasema kwa madharau kuwa ikiwa ni kweli basi anangoja nini mpaka siku ya Kiyama? Basi na iwe duniani sio akhera.
Subiri kwa wayasemayo,
kuwa wewe ni mwongo na mengineyo ya uzushi. Kwani mwisho wa mambo yao ni hasara na kusalimu amri.
Mtume(s.a.w.w)
alisubiri na kuvumilia adha ya washirikina kwa muda wa mika 13 na vitimbi vya wanafiki kwa miaka kadhaa huko Madina. Alivumilia muda huu mrefu akiwa na mategemeo ya mustkabali hata kama utachelewa. Hazikupita siku Muhammad(s.a.w.w)
akashinda kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na akaudhihirisha uislamu kuliko dini zote, wajapochukia washirikina.
Na umkumbuke mja wetu Daud.
Hili ni jina la kiebrania lenye maana ya mpendwa (mahboob). Yeye alikuwa mfalme wa pili wa Kiyahudi, wa kwanza alikuwa Talut:
إِنَّ اللَّـهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا ﴿٢٤٧﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme.” Juz. 2 (2:247).
Tawrat imemwita Talut huyu kwa jina la Shaul (Saulo). Imeelezwa kwenye Kamusi ya Kitabu kitakatifu’ kwamba Shaul ndiye mfalme wa kwanza wa waisrail na kwamba Daud alipigana katika jeshi lake. Razi anasema kuwa Mwenyezi Mungu amemsifu Daud kwa sifa nyingi. Kisha akazifafanua kwenye kurasa nne. Tutazifupiliza kwenye mistari ifuatayo: Mwenyezi Mungu alimwambia Muhammad(s.a.w.w)
:
Subiri kwa wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daud.
Hii ni karama kwa Daud.
Mwenye nguvu;
yaani mwenye nguvu ya kumtii Mwenyezi Mungu.
Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia;
yaani akiyarudisha mambo yote kwa Mwenyezi Mungu.
Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye. Na pia ndege waliokusanywa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْرَ ﴿١٠﴾
“Enyi milima sabihini pamoja naye na ndege” Juz. 22 (34:10).
وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ ﴿٧٩﴾
“Na tuliidhalilisha milima na ndege pamoja na Daud ikisabihi.” Juz. 17: (21:79).
Kwa maelezo zaid kuhusu Daud rejea huko.
Na tukautia nguvu ufalme wake.
Na tukampa hikima.
Ambayo ni kukiweka kitu mahali pake. Kwa ibara ya Razi ni elimu na kuitumia. Imeitwa hivyo kwa sababu hekima ni kupanga mambo na kuyaweka sawa.
Na kukata hukumu.
Razi anasema ni uwezo wa kudhibiti maana na kuyatolea tafsiri ya upeo wa juu. Hivi ni zaidi ya tunavyofahamu kuwa kukata hukumu ni elimu ya kuhukumu, kwa uadilifu, mambo ya wanaoteta.
Hivi ndivyo Qur’an ilivyomsifu Daud kwa sifa bora za ukamilifu, lakini Tawrat imemsifu kwa sifa mbaya mbaya; kama dhulma, ufuska, hadaa na kunyanyag’anya wanawake; kiasi amabacho waliochangia kuweka kamusi ya Kitabu Kitakatifu wakasema katika ukurasa 365, chapa ya mwezi Machi 1967, ninanukuu: “Mara nyingine Daud aliweza kufanya mambo ya kufedhehesha na ya aibu.”