25
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
هَـٰذَا ذِكْرٌ وَإِنَّ لِلْمُتَّقِينَ لَحُسْنَ مَآبٍ ﴿٤٩﴾
49. Huu ni ukumbusho. Na hakika wenye takua wana marudio mazuri.
جَنَّاتِ عَدْنٍ مُّفَتَّحَةً لَّهُمُ الْأَبْوَابُ ﴿٥٠﴾
50. Bustani za milele zitazofunguliwa milango kwa ajili yao.
مُتَّكِئِينَ فِيهَا يَدْعُونَ فِيهَا بِفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ وَشَرَابٍ ﴿٥١﴾
51. Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji.
وَعِندَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ أَتْرَابٌ ﴿٥٢﴾
52. Na pamoja nao wapo wenye kutuliza macho, walio marika.
هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِيَوْمِ الْحِسَابِ ﴿٥٣﴾
53. Haya ndiyo mliyoahidiwa kwa Siku ya Hisabu.
إِنَّ هَـٰذَا لَرِزْقُنَا مَا لَهُ مِن نَّفَادٍ ﴿٥٤﴾
54. Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyomalizika.
هَـٰذَا وَإِنَّ لِلطَّاغِينَ لَشَرَّ مَآبٍ ﴿٥٥﴾
55. Ndio hivi! Na hakika wenye kupituka mipaka bila ya shaka watapata marejeo maovu.
جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿٥٦﴾
56. Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nayo ni malalo movu mno.
هَـٰذَا فَلْيَذُوقُوهُ حَمِيمٌ وَغَسَّاقٌ ﴿٥٧﴾
57. Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha!
وَآخَرُ مِن شَكْلِهِ أَزْوَاجٌ ﴿٥٨﴾
58. Na mengineyo ya namna hii.
هَـٰذَا فَوْجٌ مُّقْتَحِمٌ مَّعَكُمْ لَا مَرْحَبًا بِهِمْ إِنَّهُمْ صَالُو النَّارِ ﴿٥٩﴾
59. Hili ndilo kundi litakaloingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho kwao. Hakika hao wanaingia Motoni.
قَالُوا بَلْ أَنتُمْ لَا مَرْحَبًا بِكُمْ أَنتُمْ قَدَّمْتُمُوهُ لَنَا فَبِئْسَ الْقَرَارُ ﴿٦٠﴾
60. Waseme: Lakini nyinyi! Hamna makaribisho! Nyinyi ndio mliotutangulizia haya, napo ni pahala paovu kabisa!
قَالُوا رَبَّنَا مَن قَدَّمَ لَنَا هَـٰذَا فَزِدْهُ عَذَابًا ضِعْفًا فِي النَّارِ ﴿٦١﴾
61. Waseme: Mola wetu! Aliyetutangulizia haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni.
وَقَالُوا مَا لَنَا لَا نَرَىٰ رِجَالًا كُنَّا نَعُدُّهُم مِّنَ الْأَشْرَارِ ﴿٦٢﴾
62. Watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ni katika waovu?
أَتَّخَذْنَاهُمْ سِخْرِيًّا أَمْ زَاغَتْ عَنْهُمُ الْأَبْصَارُ ﴿٦٣﴾
63. Je, tuliwafanyia maskhara, au macho yamewakosa?
إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّ تَخَاصُمُ أَهْلِ النَّارِ ﴿٦٤﴾
64. Hakika hayo ya kuhasimiana watu wa Motoni ni kweli.
WENYE TAKUA NA WALIOPETUKA MIPAKA
Aya 49 – 64
MAANA
Huu ni ukumbusho.
Yaani huko kutaja Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya zilizotangulia, sifa za manabii, kama Ibrahi, Ismail, Daud, Suleiman na wengineo.
Na hakika wenye takua wana marudio mazuri.
Mwenye takua ana mwanzo mzuri duniani na thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake akhera, nazo niBustani za milele zitazofunguliwa milango kwa ajili yao,
wataingia kwa amani bila ya kuulizwa au kuzuiwa.
Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji. Na pamoja nao wapo wenye kutuliza macho, walio mari- ka.
Starehe za vyakula na vinywaji na zaidi ya hayo kuna mahurulaini, hawamnyooshei jicho mtu yoyote isipokuwa waume zao. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo (37:41).
Haya ndiyo mliyoahidiwa kwa Siku ya Hisabu.
Alioyaahidi Mwenyezi Mungu hayawezi kuachwa.
Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyomalizika.
Ndio hivi! Na hakika wenye kupituka mipaka bila ya shaka watapata marejeo maovu
kabisa; kinyume kabisa na wenye takua. Wale wana makazi ya amani na hawa wana makazi maovu.
Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nayo ni malalo movu mno.
Watakua ni kuni zake nayo itakuwa ni shuka zao.
Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha!
Katika tafsiri Ar-Razi imeelezwa kuwa hapa kuna maneno yaliyotangulizwa na mengine kuja nyuma. Asili yake ni: Haya ni maji ya moto na usaha basi nawauonje.
Na mengineyo ya namna hii.
Adhabu ya watu wa motoni haimalizikii na maji ya moto na usaha tu; bali kuna aina nyinginezo za adhabu zinazofanana kwa ukali na ugumu na zinatofautiana kwa aina; kama vile Zaqqum na nyinginezo ambazo hakuna jicho lililoziona wala sikio lililozisikia.
Hili ndilo kundi litakaloingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho kwao. Hakika hao wanaingia Motoni.
Wakosefu wataingia motoni makundi makundi. Likiingia kundi moja likikutana na waliotangulia watawaambia hakuna makaribisho kwenu! Mmekuja kwetu basi mmepata makazi mabaya.
Waseme: Lakini nyinyi! Hamna makaribisho! Nyinyi ndio mliotutan- gulizia haya, napo ni pahala paovu kabisa! Waseme: Mola wetu! Aliyetutangulizia haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni.
Maneno haya yote ni ya wale waliofika wakiwajibu waliotangulia. Wamewapokea kwa shari nao wakawarudishia zaidi. Kusema kwao: ‘nyinyi ndio mliotutangulizia haya,’ ni ishara ya kuwa viongozi wa upotevu ndio watakaotangulia motoni kisha wafuatiliwe na wafuasi wao. Kusema kwao ‘haya’ ni hayo ya adhabu. Kisha wafuasi watamtaka Mwenyezi Mungu awaongezee adhabu wale waliowahadaa.
Haya yamekaririka kimaana kwenye Aya kadha, zikiwemo. Juz. 2 (2:166), Juz. 8 (7:37) na Juz. 22 (34:31).
Watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ni katika waovu?
Watakaosema ni wale waliopituka mipaka. Makusudioya watu waliohisabiwa kuwa ni katika waovu ni wale wanyonge. Wenye mabavu katika maisha ya dunia walikuwa wakipora mali za wanyonge kisha wakiwaona kama wanyama na vyombo vya kutumia.
Walalahoi ni wanyama na washari. Kwa nini? Kwa vile wao wanakula kutokana jasho lao; wala hawakeshi kwenye makasino, mabaa na madanguro. Ama wale mataghuti, wanaopituka mipaka, basi wao ndio walio bora kwa vile wanastarehe na kufuja mali za wanyonge. Wanyonge ni wapumbavu kwa vile hawaendi mwendo wa kujificha, lakini wapenda anasa hao ndio mabwana kwa vile wanajigeuza kila rangi.
Siku ya hukumu vifuniko vyote vitafunuka na wahaini wataona makazi yao katika moto wa Jahannam, wala hawatumuona yeyote katika wale waliokuwa wakiwaita ni waovu. Watashangaa na kuulizana wako wapi? Hawatachukua muda ila watajua kuwa wako mbele za mfalme muweza. Basi roho zitawatoka kwa majuto na hilo litawazidishia maumivu.
Je, tuliwafanyia maskhara, au macho yamewakosa?
Haya ni maneno ya waliopetuka mipaka watajifanyia masikhara wenyewe Siku ya Kiyama, kwa sababu walikuwa wakiwafanyia masikhara wale walioamini.
Hakika hayo ya kuhasimiana watu wa Motoni ni kweli.
Kuhasimiana kwenyewe ni huko kukaribishana motoni. Na hilo bila shaka litakua tu.
قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنذِرٌ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٦٥﴾
65. Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana Mola ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenza nguvu.
رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ ﴿٦٦﴾
66. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, Mwenye nguvu, Mwingi wa maghufira.
قُلْ هُوَ نَبَأٌ عَظِيمٌ ﴿٦٧﴾
67. Sema: Hii ni habari kubwa kabisa.
أَنتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ ﴿٦٨﴾
68. Nyinyi mnaipuuza.
مَا كَانَ لِيَ مِنْ عِلْمٍ بِالْمَلَإِ الْأَعْلَىٰ إِذْ يَخْتَصِمُونَ ﴿٦٩﴾
69. Sikuwa na ilimu ya wakuu watukufu walipokuwa wakishindana.
إِن يُوحَىٰ إِلَيَّ إِلَّا أَنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٧٠﴾
70. Sikupewa wahyi isipokuwa kwamba mimi ni mwonyaji tu aliye dhahiri.
إِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن طِينٍ ﴿٧١﴾
71. Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo.
فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ ﴿٧٢﴾
72. Na nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi muangukieni kwa kusujudu.
فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ ﴿٧٣﴾
73. Wakasujudu Malaika wote pamoja.
إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿٧٤﴾
74. Isipokuwa Ibilisi alijivuna na akawa katika makafiri.
قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْعَالِينَ ﴿٧٥﴾
75. Akasema: Ewe Iblisi! Kipi kilichokuzuia kumsujudia yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu?
قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿٧٦﴾
76. Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.
قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ ﴿٧٧﴾
77. Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa.
وَإِنَّ عَلَيْكَ لَعْنَتِي إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٧٨﴾
78. Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo.
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿٧٩﴾
79. Akasema: Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴿٨٠﴾
80. Akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda,
إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ ﴿٨١﴾
81. mpaka siku ya wakati maalumu.
قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٢﴾
82. Akasema: Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote.
إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ ﴿٨٣﴾
83. Isipokuwa wale waja wako miongoni mwao waliosafishwa.
قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ ﴿٨٤﴾
84. Akasema: Ni haki! Na ndio haki niisemayo.
لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٥﴾
85. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao.
قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُتَكَلِّفِينَ ﴿٨٦﴾
86. Sema: Siwaombi ujira juu ya haya, wala mimi si katika wanaojifanya.
إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿٨٧﴾
87. Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.
وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُ بَعْدَ حِينٍ ﴿٨٨﴾
88. Na bila ya shaka mtajua habari zake baada ya muda.
MIMI NI MUONYAJI TU
Aya 65 – 88
MAANA
Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana Mola ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenza nguvu. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake, Mwenye nguvu, Mwingi wa maghufira.
Ewe Muhammad! Waambie washirikina kuwa mimi ninawabashiria mumpwekeshe Mwenyezi Mungu na ninawaonya kuwa msimshirikishe na yeyote kwenye ibada.
Yeye peke yake ndiye mwenye ufalme, mwenye nguvu na msamehevu kwa yule mwenye kutubia mwenye kurejea kwa Mola wake.
Sema: Hii ni habari kubwa kabisa. Nyinyi mnaipuuza.
Neno ‘hii’ linarudia kwenye Qur’an na walioipuuza ni washirikina, kwa ujinga au kwa inadi na kupupia masilahi yao. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameisifu Qur’an kuwa ni habari, kubwa kwa sababu imejikita kwenye itikadi, sharia na misingi yote ya asasi za manufaa ya wote na kusaidiana.
UISLAMU NA MSICHANA WA KINGEREZA
Mnamo mwezi January 1970, nilisoma mihadhara miwili ya Roger Garaudy aliyoitoa mjini Cairo, Darul-aharam, mnamo mwezi wa November 1969. Garaudy ni miongoni mwa wataalamu wakubwa wa fikra wa kifaransa. Ni profesa wa falasafa na ni Daktari wa fasihi. Mihadhara yake hiyo iliandikwa kwenye jarida la Attalia namba 1-1970. la Misri.
Miongoni mwa aliyoyasema katika muhadhara wake wa kwanza ni: “Ukombozi wa waarabu haukuwa ni wa kivita wala wa kikoloni; isipokuwa ulikuwa ni wa kuleta fursa katika kila mji kuleta maendeleo kutokana na sanaa ya kiislamu na maendeleo yake. Ukombozi wa waarabu umeleta mwamko wa kiichumi wa ulimwengu, pamoja na kuweko ukabaila katika miaka ya mwanzo ya ukombozi.”
Katika muhadhara wake wa pili alisema: “Sisi tuko kwenye turathi adhimu ya misimamo ya kiislamu ambayo inaweza kutoa mchango mkubwa kati- ka maendeleo ya kiislamu.”
Akaendelea kusema: “Tunamuona mwanafikra mkubwa wa kifaransa, Bacon anasema: “Falsafa yote imechimbuka kutokana na Uislamu.”
Vile vile nilisoma kwenye gazeti la Al-jumhuriya la Misr, la 21/1/ 1970, kwamba msichana mmoja msomi wa kingereza, aitwaye Bridget Honey aliingia kwenye dini ya kiislamu hivi karibuni. Kwa ufupi gazeti linaelezea kuwa msichana huyu alikuwa, kama watu wengine wa kimagharibi, ana chuki na shaka nyingi juu ya Uislamu. Lakini baada ya kusoma, kwa umakini na bila chuki, tarjuma ya Qur’an na vitabu vingine, na akajua mafunzo yake, alijikuta ni mwislamu bila ya kutambua.
Kisha msichana huyu akamwambia mwandishi wa gazeti: “Ni vigumu sana kuubainihsa uhakika wa Uisalmu kwa maneno ya harakaharaka. Kwa sababu huo ni kama aina ya fulani ya kiuhandisi ya ajabu uliokamilika, kila sehemu ikiikamilisha sehemu nyingine. Na siri ya uzuri wake inatokana na kuoana mafungu yake. Sifa hii ya uislmu ndiyo inayoathiri kwa undani ubinadamu.
Hakika mfumo mzuri katika Uislmu wa kutosheleza matakwa ya kimwili naya kiroho una mvuto wa nguvu katika magharibi ya kileo na unaweza kuleta athari kwenye maendeleo ya kisasa. Unawawekea wazi njia ya magharibi kuelekea kwenye usafi na kufaulu kiuhakika.”
Ingelikuwa bora lau vijana wetu, akiwemo yule mwenye kitabu cha fikra ya kupinga dini, wangelifuata njia ya msichana huyu; wakasoma Qur’an na kuyachunguza kwa undani maana yake, wakasoma waliyoandika wataalmu kuhusu Uislamu; kama alivyofanya msichana huyu. Kisha wauhukumu Uisalmu wao wenyewe kulingana na walivyosoma na wakafahamu.
Kwa uchache athari atayoipata mwenye kuisoma Qur’an na kuyazingatia vizuri maana yake ni kujua uadilifu wa mwenye uweza na kwamba Yeye atawalipa wema wanaofanya mema na mabaya wanaofanya mabaya. Atabakia na nini mtu kama atakosa imani hii?
Sikuwa na ilimu ya wakuu watukufu walipokuwa wakishindana. Sikupewa wahyi isipokuwa kwamba mimi ni mwonyaji tu aliye dhahiri.
Makusudio ya wakuu watukufu hapa ni Malaika. Maana ni kuwa sema ewe Muhammad kuwaambia washirikina. Mimi nimewapa habari za Malaika wakati Mwenyezi Mungu alipowambia:
إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ ﴿٣٠﴾
“Mimi nitaweka khalifa katika ardhi” (na wao) wakasema: Utaweka humo watakaofanya uharibifu?” Juz. 1 (2:30).
Nisingeyajua haya lau sikunifahamisha na kunipa wahyi Mwenyezi Mungu; au mnaona mimi ninamzulia Mwenyezi Mungu? Nami sidai lolote kwa ajili yangu, isipokuwa kuwaonya mumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake kwa kutaka thawabu zake na kuhofia adhabu yake.
Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo. Na nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi muangukieni kwa kusujudu.
Makusudio ya roho ya Mwenyezi Mungu hapa ni uhai. Mwanafasihi mmoja wa kisasa anasema: Bali makusudio ni dhamiri ya mtu hasa, na kwamba Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Malaika kumsujudia Adam kwa vile yeye ni elimu. Mara ngapi dhamiri itamwadhibu kiumbe huyo mwenye mwili wa udongo na roho ya Mwenyezi Mungu? “Hakika tumemuumba mtu katika tabu” (90:4). yaani dhiki na mashaka yenye kuendelea.
Wakasujudu Malaika wote pamoja; isipokuwa Ibilisi alijivuna na akawa katika makafiri.
Mwenye kitabu “Kupinga fikra ya dini” anasema katika uk. 90: “Kukataa Iblisi kumsujudia Adam kunaenda sambamba na matakwa ya Mwenyezi Mungu.”
Kauli hii nayo inaenda sambamba na madhehebu ya kisunni, yanayosema kuwa hakuna kulazimiana baina ya anayoyaamuru Mwenyezi Mungu na anayoyataka, wala baina ya anayoyakataza na anayoyachukia. Anaweza kuamuru anayoyachukia na anaweza kukataza anayoyapenda. Tazama Al- mawaqif (8:176).
Miongoni mwa waliyoyatolea dalili ya hilo nikuwa Mwenyezi Mungu alimwamrisha Ibilisi kumsujudia akiwa Yeye Mwenyezi Mungu hataki hivyo, lau angelitaka Mwenyezi, Mungu basi Ibilis angelisujudi tu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hufanya anayoyataka.
Lakini kauli ya mwenye kitabu cha kupinga dini haiendi sambamba na madhehebu ya Shia wanaosema kuwa Mwenyezi Mungu ana matakwa aina mbili: kutaka kwa kuumba ambako kunaelezwa na ibara ya “Kuwa na ikawa” (kun fayakun).
Na kutaka kwingine ni kwa kisharia ambako kunaelezewa na kuamrisha na kukataza. Tazama Juz. 1 (2:26-27). Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) alitaka kusujudiwa Adam kwa matakwa ya kisharia sio matakwa ya kuumba.
Akasema: Ewe Iblisi! Kipi kilichokuzuia kumsududia yule niliye- muumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazielezea sababu za kimaumbile kwa ibara ya mikono yake, kwa sababu zinakomea kwake. Mwenyezi Mungu Mtukufu: anasema kwenye Juzuu hii tuliyo nayo:
أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا ﴿٧١﴾
“…kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyamahowa.” (36:71).
Maana ni, kwa nini umejizuia kumsujudia Adam ewe Ibilisi? Je, umejifanya kuwa na kiburi na ukajiweka kwenye cheo usichokuwa nacho? Au kweli wewe unajiona kuwa ni mkubwa na mtukufu kuliko Adam?
Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.
Alijibu kuwa ana uhakika yeye ni mkubwa na mtukufu zaidi kuliko Adam, kwa vile ametokana na moto unaokuwa viwandani na kutengenezewa sila- ha za maangamizi, lakini Adamu ametokana na udongo kwa hiyo yeye ni mkulima, kwa vile ni maji na mchanga.
Amesahau au amejitia kusahahu, habithi huyu, kuwa maji ndio asili ya uhai na kwamba maendeleo yote ni tanzu.
Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa. Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo. Akasema: Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa. Akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda, mpaka siku ya wakati maalumu. Akasema: Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote, isipokuwa wale waja wako miongoni mwao waliosafishwa. Akasema: Ni haki! Na ndio haki niisemayo. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao.
Yametangulia maelezo ya kisa cha kuumbwa Adam, kusujudu Malaika na kukataa Ibilisi kusujudu katika Juzuu zifuatazo:-
• Juz. 1 (2:30 – 34).
• Juz. 8 (7:11 – 18).
• Juz. 14 (15:26 – 44).
• Juz. 15 (17:61-65).
• Juz. 15 (18:50).
Sema: Siwaombi ujira juu ya haya, wala mimi si katika wanaojifanya.
‘Haya’ ni haya ya tabligh na kukumbusha. Makusudio ya kujifanya hapa ni uwongo. Maana ni ewe Muhammad! Waambie wale wanaokukadhibisha kuwa mimi ninawapa nasaha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, sitaki malipo kutoka kwenu wala shukrani, na wala mimi simzulii Mwenyezi Mungu. Vipi nimzulie na hali ninacho kitabu kinachosema kweli, na kilichoshinda ndimi na akili zote kuweza kuleta mfano wake.
Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote walio na moyo au wanaotega sikio na wenyewe ni mashahidi.
Na bila ya shaka mtajua habari zake baada ya muda.
Itawabainikia baada ya muda kidogo katika maisha ya dunia ambapo watu wataingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi. Vile vile itawabainikia haki huko akhera ambapo uhakika utathibiti na batili itapotea.
MWISHO WA SURA YA THELATHINI NA NANE: SURAT SAAD