26
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA
أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٩﴾
9. Je, Afanyaye ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake. Sema: Je, wanalingana sawa wale ambao wanajua na wale ambao hawajui? Hakika wanaokumbuka ni wenye akili tu.
قُلْ يَا عِبَادِ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا رَبَّكُمْ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ وَأَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةٌ إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾
10. Sema: Enyi waja wangu ambao mmeamini! Mcheni Mola wenu. Wale ambao wamefanya wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni pana. Hakika si mengineyo, wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ ﴿١١﴾
11. Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia Yeye Dini.
وَأُمِرْتُ لِأَنْ أَكُونَ أَوَّلَ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٢﴾
12. Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.
قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٣﴾
13. Sema: Hakika mimi ninahofia adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu.
قُلِ اللَّـهَ أَعْبُدُ مُخْلِصًا لَّهُ دِينِي ﴿١٤﴾
14. Sema: Mwenyezi Mungu ninamuabudu kwa kumsafia Yeye Dini yangu.
فَاعْبُدُوا مَا شِئْتُم مِّن دُونِهِ قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١٥﴾
15. Basi abuduni mpendacho badala yake. Sema: Hakika waliohasirika ni wale waliojihasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri
لَهُم مِّن فَوْقِهِمْ ظُلَلٌ مِّنَ النَّارِ وَمِن تَحْتِهِمْ ظُلَلٌ ذَٰلِكَ يُخَوِّفُ اللَّـهُ بِهِ عِبَادَهُ يَا عِبَادِ فَاتَّقُونِ ﴿١٦﴾
16. Watakuwa na vivuli vya moto juu yao, na chini yao vivuli. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni.
HADHARI YA AKHERA NA MATARAJIO YA REHEMA YA MOLA
Aya 9 – 16
MAANA
Hata Manabi Wana Shauku Na Hofu
Je, Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja yule anayeamini wakati wa shida na kukufuru wakati wa raha, anafuatishia kumtaja yule anayeamini wakati wa shida na raha. Neema haimzidishii kitu isipokuwa imani, shukrani, kusujudu na kurukui wakati wa giza la usiku, watu wakiwa wamelala. Hafanyi kitu isipokuwa shauku ya thawabu za Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake.
Katika Aya hii kuna ishara kuwa mtu hafanyi ila kwa msukumo shauku na hofu, awe ni mwenye takua au muovu. Tofauti ni kuwa muovu anafanya na kuacha kwa shauku ya starehe za dunia na kuhofia tabu na machungu, lakini mwenye takua anafanya na kuacha kwa sahuku ya shamba la Akhera na neema zake na kuhofia adhabu yake na moto wake.
Hali hii iko hata kwa manabii walio maasumu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasifu kwa kusema: “Wakituomba kwa shauku na hofu.” Juz. 17 (21:90).
Sema: Je, wanalingana sawa wale ambao wanajua na wale ambao hawajui? Hakika wanaokumbuka ni wenye akili tu.
Makusudio ya wanaojua hapa sio wale waliohifadhi sherehe na matini, wala sio wale waliogundua elektroni, mabomu ya masafa marefu na kupanda mwezini au kwenye Mars.
Hapana! Sio hao kabisa; isipokuwa makusudio ni wale wanaofanya kheri kwa binadamu wote na kuwakomboa wanaoadhibiwa ardhini na kuwaondoa watu kwenye tabu na mashaka.
Ama ulama wasiojali au wale ambao wameuza dini yao kwa mshetani na maibilisi kwa ajili ya kuwachapa watu na wakagundua silaha za maangamizi, hawa ni kama wanyama; bali wao wamepotea zaidi ya wanyama.
Hawawezi kuitambua hakika hii isipokuwa wale wenye akili na busara.
Sema: Enyi waja wangu ambao mmeamini! Mcheni Mola wenu,
kwa sababu imani bila takua wala amali njema haina manufaa yoyote. Ndio maana baadhi ya maulama wamesema kuwa matendo mema ni sehemu ya kuamini haki.
Wale ambao wamefanya wema katika dunia hii watapata wema.
Haya ni maneno mapya hayaungani na yaliyotangulia. Maana yake ni kuwa mwenye kufanya hata chembe ya amali ya kheri ataiona.
Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni pana.
Kwa hiyo atayepata dhiki mjini kwake na akashindwa kutekeleza wajibu wake wa kidini au wa kidunia basi ahamie kwengine. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:97).
Hakika si mengineyo, wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Yaani wenye kuvumilia shida kwa subira ya kiungwana na kukataa kusalimu amri kwenye ufukara na udhalili. Ama wale ambao wanawanyeyekea wenye nguvu na kuwa waoga mbele ya mataghuti, hao ndio waliohasirika duniani na akhera na huko ndiko kuhasrika waziwazi.
Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia Yeye Dini.
Hakuna tofauti baina ya Nabii na mwenginewe. Yeye anaamrishwa kum- fanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika kauli na matendo yake yote; kama binadamu mwingine.
Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.
Mtume(s.a.w.
w
)
aliwapa watu mwito wa uislamu baada ya kutangulia yeye mwenyewe kwenye Uislamu, kwa sababu anafanya anayoyasema wala hasemi asiyoyafanya.
Sema: Hakika mimi ninahofia adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu.
Muhammad(s.a.w.
w
)
anamhofia Mwenyezi Mungu kwa sababu Yeye hawezi kumwepuka Mwenyezi Mungu wala hana hoja naye, bali yeye ni hoja ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake wote.
Utukufu zaidi kwa Muhammad(s.a.w.
w
)
ni kwamba yeye ni mtiifu kwa Mola wake, mwenye kumfanayia ikhlasi na mtangulizi wa mambo ya heri, akipata wahyi kutoka kwa Mola wake na akiutekeleza unavyotakikana:
قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِّنَ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلَا بِكُمْ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٩﴾
“Sema: mimi si kioja katika mitume; wala sijui nitakavyofanywa wala nyinyi; sifuati ila niliyopewa wahyi na mimi si lolote ila ni muonyaji, mwenye kubainisha.” (46:9).
Sema: Mwenyezi Mungu ninamuabudu kwa kumsafiia Yeye Dini yangu.
Mara nyingine Muhammad(s.a.w.
w
)
anasisitiza, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kwamba Yeye ni mja mwenye kuamriwa. Mustshriq mmoja wa kingereza, Jeb Hamilton, mwalimu katika chuo kikuu cha Oxford, katika kitabu “Modern trends in Islam” anasema: “Qur’an inakataa fikra ya kuingiliwa kati, baina ya Mwenyezi Mungu na mtu. Unamweka mtu moja kwa moja mbele ya Mola wake bila ya kuweko wa katikati kiroho au kiutu.” Na hii ni tofuati kubwa inayoshindia Uislamu dini nyingine.
Basi abuduni mpendacho badala yake.
Huu ni ufasaha wa hali ya juu kuelezea hasira za Mwenyezi Mungu na makemeo kwa yule anayemfanya muabudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Sema: Hakika waliohasirika ni wale waliojihasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri.
Wamezihasiri nafsi zao kwa sababu wamejiingiza kwenye Jahannam, marejeo mabaya kabisa, na wamewahasiri watu wao kwa sababu atakayekuwa mshirikina katika wao ataangamia. Na mumin ni adui wa mwenye kushirikisha duniani na akhera.
Watakuwa na vivuli vya moto juu yao, na chini yao vivuli.
Yaani adhabu ya kuungua itawazunguka kila mahali.
Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni.
Mwenyezi Mungu amewabainishia adhabu ya akhera ili waweze kujiepusha nayo wakiwa duniani kwa kufanya utiifu na ikhlasi. Vinginevyo wataionja tu.
Msemaji mmoja alisema kuwa Pepo ni ladha za kiroho na moto ni machungu ya kinafsi na kwamba yote yaliyoelezwa kwenye Qur’an katika sifa za kihisia ni aina ya kupiga mfano na kuleta karibu kwenye akili. Kwa vile mabedui wanapenda sana asali, maziwa, pombe na wanawake mahurilaini. Msemaji wa maneno haya ametolea dalili kauli yake, kwa Aya hii tuliyo nayo: “Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake.”
Kwamba inavyofahamika ni kuwa Mwenyezi Mungu ametaja matamshi ya adhabu kwa ajili ya kuhofisha tu, wala hakuna hakika
Tunajibu
: kila tamko lililokuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake ni wajibu kuchukulia dhahiri yake, ila ikiwa halingiliki akilini; na hapo tutalitumia kimajazi yanayokwenda na tamko lenyewe.
Hakuna tamshi katika matamshi ya sifa za Pepo na Moto yaliyotajwa na Qur’an, linalokataliwa na akili. Kwa hiyo ni wajibu kubakia tamko kwenye dhahiri yake, bila ya kuweko haja ya kuleta taawili.
Maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake,” ni kuwa anawabainishia uhakika wa mambo, ili wachukue hadhari na wajiepushe na sababu zitakazopelekea hilo. Aya iliyotaja sifa za Moto ndio inayofahamisha maana haya:
إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّ تَخَاصُمُ أَهْلِ النَّارِ ﴿٦٤﴾
“Hakika hayo ya kuhasimiana watu wa Motoni ni kweli.” (38:64).
Ama kauli ya kuwa huruma ya Mwenyezi Mungu haiafikiani na adhabu ya ya Moto kwa kiumbe huyu masikini aliye dhaifu, tunaijibu hivi:
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewandalia adhabu kali na chungu wale wanofanya ufisadi katika ardhi wakamwaga damu, kuwafanya waja wa Mungu kuwa watumwa wao, wakaangamiza watu kwa silaha za maangamizi na kuwaua kwa maelfu ndani ya dakika. Jahannam, pamoja na sifa zake zote, haitoshi kuwa ni malipo kwa hawa; bali wamehurumiwa pia. Amani imshukie yule aliyesema: “Ghadhabu haimshughulishi (asiwe) na huruma, wala huruma haimshughulishi (asiwe) na mateso.”
Tazama kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi’ katika Juz.13 (14:46-52).
وَالَّذِينَ اجْتَنَبُوا الطَّاغُوتَ أَن يَعْبُدُوهَا وَأَنَابُوا إِلَى اللَّـهِ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ فَبَشِّرْ عِبَادِ ﴿١٧﴾
17. Na wale wanaojiepusha na kuabudu taghut, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu.
الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّـهُ وَأُولَـٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٨﴾
18. Ambao husikiliza maneno, wakafuata mazuri yake zaidi. Hao ndio aliowaongoza Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili.
أَفَمَنْ حَقَّ عَلَيْهِ كَلِمَةُ الْعَذَابِ أَفَأَنتَ تُنقِذُ مَن فِي النَّارِ ﴿١٩﴾
19. Je, Yule mwenye kustahili hukumu ya adhabu, Je, wewe unaweza kumwokoa aliyomo Motoni?.
لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ غُرَفٌ مِّن فَوْقِهَا غُرَفٌ مَّبْنِيَّةٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَعْدَ اللَّـهِ لَا يُخْلِفُ اللَّـهُ الْمِيعَادَ ﴿٢٠﴾
20. Lakini waliomcha Mola wao watapata ghorofa zilizojengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَلَكَهُ يَنَابِيعَ فِي الْأَرْضِ ثُمَّ يُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَجْعَلُهُ حُطَامًا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿٢١﴾
21. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha yakawa chem-chem katika ardhi? Kisha kwa maji hayo akatoa mimea yenye rangi mbali mbali. Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano kisha huifanya imevunjikavunjika. Bila ya shaka katika hayo kuna ukumbusho kwa wenye akili.
WANAOSIKILIZA MANENO WAKAFUATA MAZURI YAKE
Aya 17 – 21
MAANA
Na wale wanaojiepusha na kuabudu taghut, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu.
Makusudio ya Tghut hapa ni masanamu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawabashiria wale walioacha shirki wakatubia na wakamtii Mwenyezi Mungu
Ambao husikiliza maneno, wakafuata mazuri yake zaidi. Hao ndio aliowaongoza Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili.
Makusudio ya maneno mazuri sio uzuri wa matamshi na ufasaha wake; isipokuwa ni yale yanayonufaisha duniani na akhera – yakiwa yana madhara basi ni mabaya. Ama maneno yasiyodhuru wala kunufaisha, basi hayo hayawezi kusifiwa kwa ubaya wala kwa uzuri.
Kauli ya Mwenyezi Mungu ni nzuri zaidi kuliko kauli yoyote, wala hakuna kitu bora kuliko kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, iwe kauli au vitendo. Kwa sababu vitu kutoka kwake ni sawa.
Wale wanaosikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu na wakayafanyia kazi ndio walioongoka, mbele ya Mwenyezi Mungu, kwenye maarifa mazuri zaidi na ndio wanaochukua kiini cha maneno sio maganda.
Imam Ali
anasema:“Kithirisheni kumtaja Mungu kwa kuwa ni utajo mzuri zaidi, na yafanyieni shauku ambayo (s.w.t) amewaahidi wachamungu, kwa kuwa ahadi yake ni ahadi ya kweli mno, na fuateni mwongozo wa Nabii wenu kwa kuwa huo ni mwongozo bora zaidi, na fanyeni kwa mwenendo wake kwa kuwa ni mwenendo mwongofu bora mno, na jifundisheni Qur’an kwa kuwa hiyo ni maongezi mazuri zaidi, na jitahidini kuifahamu kwa kuwa ni chanuo la nyoyo.”
Je, Yule mwenye kustahili hukumu ya adhabu
ni sawa na yule aliyeokolewa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Je, wewe Muhammad unaweza kumwokoa aliyomo Motoni?
Hapana! Hakuna wasila wowote wa kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu ila matendo mema na msamaha wa Mwenyezi Mungu, iliyotukuka hekima yake. Hapana mwenye shaka kwamba mwenye kuzama katika upotevu, Mwenyezi Mungu hatamwangalia: “Hao hawatakuwa na sehemu yoyote akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu iumizayo. Juz. 3 (3:77).
Lakini waliomcha Mola wao watapata ghorofa zilizojengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.
Hii ndio ahadi ya Qur’an – kukutanisha bishara na onyo, ahadi na kiaga, kuwataja wenye takua na thawabu zao na kuwataja mataghuti na adhabu yao. Hawa wana vivuli vya moto na wale wana ghorofa za pepo. Hii ni ahadi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu; na ninani mkweli wa maneno zaidi ya Mwenyezi Mungu?
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha yakawa chemchem katika ardhi?
Mvua inashuka kutoka mbinguni na kutirizika juu aya ardhi, kisha maji yananyonywa ndani ya ardhi, yanakuwa chemchem na kuwanufaisha watu. Je, hii yote ni sadfa au ni mipangilio ya Mjuzi Mwenye hekima?
Kisha kwa maji hayo akatoa mimea yenye rangi mbali mbali.
Je, mimea hii yenye rangi na ladha tofauti imetengenezwa na maumbile asili au ni kwa msaada wa Aliyetengeneza hayo maumbile asili na yaliyo ndani yake?
Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano.
Baadae mimea hunyauka na kuwa manjano inapokomaa; kisha huifanya imevunjikavunjika.
Baada ya kukauka.
Bila ya shaka katika hayo kuna ukumbusho kwa wenye akili.
Katika kuteremshwa mvua, kuoteshwa mimea, kuwa kijani kisha kuwa njano, kisha kuvunjikavunjika kulingana na hekima na masilahi. Yote hayo ni ukumbusho wa muumbaji na mwanzilishaji.
Ikiwa haya yote yametokana na maji na mchanga, basi ni nani aliyeyaleta hayo maji, mchanga na ulimwengu kwa ujumla?
Tazama: Kifungu ‘Uhai umetoka wapi?’ katika Juz. 7 (6:95 – 99) na kifungu ‘Roho inatokana na amri ya Mola wangu’ katika Juz. 15 (17:62 – 85).